KAMA MAANDALIZI YA TIMU ZETU YATAENDELEA KUWA YA KUSUASUA...

Daima Tanzania itaboronga katika michezo ya Kimataifa

Na Said Mmanga,MSJ

KATIKA kipindi cha miaka ya hivi karibuni Watanzania wameshuhudia wawakilishi wao katika michezo mbalimbali ya Kimataifa wakishindwa kufanya vizuri kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, ambapo Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi zilizokuwa zikisifika katika medani ya michezo.

Sio siri katika miaka ya Sabini hadimwanzoni mwa miaka ya Themanini asilimia tisini ya Watanzania walikuwa na matumaini na wawakilishi kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya Kimataifa kama si kurudi na kikombe basi watarudi na medali za kutosha tofauti na sasa ambapo kupata medali kwetu kimekuwa ni kitu cha kushtukiza.

Ni nani asiyejua kama Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi ambazo zilikuwa zikisifika kwa mchezo wa riadha, ngumi,pamoja na mpira wa miguu ingawa hatujawahi kuchukua ubingwa wowote wa Afrika lakini timu ya Tanzania ilikuwa ikitoa upinzani mkali wakati inapokutana na timu ya nchi nyingine.

Hakuna atakayemsahau Filbert Bayi ambaye amewahi kuwa bingwa wa mbio Ulimwenguni katika mita 1500 rekodi aliyoivunja katika michezo yajumuiya ya madola nchini New Zealand mnamo mwaka 1974 mbali na huyo wanamichezo wengine ambao wameiletea sifa Tanzania katika uwanja huo wa riadha ni Suleiman Nyambui, Mwinga Mwamjala ,Nzael Kyomo, Zakarie Barie bila Kumsahau bingwa wa medali ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 Giddamis Shahanga, aliyoitwaa katika michuano ya Jumuiya ya Madola Mnamo mwaka 1982 Mjini Brisbane nchini Australia.

Mbali na mchezo huo pia Tanzania ilikuwa iking'ara katika michezo mingine kama ngumi ni nani asiyemkumbuka bondia wa uzito wa kati Titus Simba ambaye aliwahi kutwaa medali ya fedha katika michuano ya jumuiya ya madola mnamo mwaka 1970 michezo ilifofanyika mjini Edinburg ,Scotland.

Mbali na mwanamasumbi huyo pia walikuwepo mabondia wengine ambao wakati walipokuwa wakiingia ulingoni kila Mtanzania aliamini ni lazima atapata ushindi baadhi yao ni Nassoro Michael, Willy Isangula na wengineo ambao sikuwataja.

Aidha, Tanzania pia ilikuwa ni nchi ambayo ilikuwa ni miongoni mwa zile ambazo zilikuwa zikitoa upinzani mkali wakati timu zake zilipokuwa zikipambana na timu za nje mfano halisi ni mnamo mwaka 1980 wakati timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ilipopambana na timu ya Taifa ya Nigeria Green Eagles, ambapo katika mchezo uliofanyika uwanja wa taifa Taifa Stars walilala kwa mabao 2 - 0, lakini kiwango cha mchezo kilichokuwa kimeonyeshwa ni cha hali ya juu.

Hata kwa upande wa vilabu timu za Tanzania zilikuwa zikiogopewa ni nani asiyejua kuwa katika miaka ya sabini hadi mwanzoni mwa miaka ya themanini timu zetu zilikuwa zikizitetemesha timu kutoka Afrika Magharibi kutokana na kutandaza kandanda safi mfano halisi ni Simba walipoiendesha mchakamchaka timu ya Union Douala mnamo mwaka 1974 mchezo ambao Simba walishinda mabao 2 - 0.

Lakini ni lazima tujiulize kwa nini wanamichezo wetu walikuwa wakifanya vizuri katika kipindi hicho tofauti na sasa ambapo wanamichezo wetu kufanya vizuri imekuwa ni jambo si la kutegemewa ni wazi kuwa katika kipindi hicho timu zetu zilikuwa zikipata maandalizi mazuri na ya kutosha tofauti na hivi sasa ambapo maandalizi yamekuwa n ya ubabaishaji.

Kutokana na kutokuwa na maandalizi mazuri ya timu zetu katika michezo ya Kimataifa ndiyo maana hata katika ile michezo ambayo tulikuwa tukishiriki lazima tufanye vizuri sasa imeanza kututupa mkono na matokeosua timu zetu zinakuwa jamvi la wageni kama sio kichwa cha mwendawazimu zinaposhiriki katika michuano ya Kimataifa.

Lakini sina maana kwamba hivi sasa hakuna wanamichezo wanaofanya vizuri la hasha wanamichezo wanaofanya vizuri wapo mfano ni Hassani Matumla ambaye alitwaa medali ya shaba katika michezo ya Jumuiya ya madola iliyofanyika Mjini Edmonton nchini Canada, bila kuwasahau mashujaa wetu waliotuletea medali katika michezo ya Olimpiki iliyomalizika hivi karibuni nchini Malaysia hao si wengine bali ni Simon Mrashani, Michael Yombayomba na Geway Suja.

Pamoja na kwamba wanamichezo wetu baadhi wameendelea kufanya vizuri lakini idadi hiyo hailingani na wanamichezo ambao wanakwenda katika michuano hiyo mfano ni mwaka huu ambapo timu ya Tanzania katika michezo ya Olimpiki ilikuwa na jumla ya wachezaji 21 wa michezo mbalimbali na matokeo yake tumeambulia medali tatu ambazo tunaziona nyingi kwa kuwa tumezoea kurudi na medali moja au mikono mitupu hii ni dhahiri kwamba maandalizi yetu si mazuri.

Kitu kikubwa kinachochangia kuwa na maandalizi duni kwa timu zetu ni kutokuwepo na utaratibu mzuri katika nyanja ya michezo hapa nchini kuanzia serikalini hadi katika vilabu na vyama vinavyoongoza michezo hapa nchini ni hili lisipoangaliwa kwa makini daima tutakuwa wasindikizaji katika michuano ya kimataifa.

Serikali imekuwa haiki mkazo katika nyanja ya michezo nandiyo maana imekuwa haifuatilii kwa karibu maendeleo ya michezo hapa nchini na wahusika wamekuwa wahubiri wazuri katika kupanga mikakati ambayo haitekelezeki.

Jambo lingine linalosababisha timu zetu kutofanya vizuri katika michaunoya Kimataifa ni uongozi mbovu katika vyama vya michezo pamoja na vilabu vyetu ambapo viongozi wengi katika vyama hivyo au vilabu wamekuwa ni wababaishaji na kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakitaka kujinufaisha wao badala ya Taifa na hii ndiyo maana inapotokea timu kwenda nje iwe kwa mazoezi au kushiriki katika michezo ya Kimataifa utakuta msururu mrefu wa viongozi na wakati mwingine hufikia hatua hata ya kuwakata wachezaji ali mradi waende wakatembee.

Kama kweli Watanzania tunataka tuwe tukiwashangilia wanamichezo wetu kwa kufanya vizuri katika michezo ya Kimataifa hatuna budi kuwa na maandalizi mazuri kwa timu zetu kwani maandalizi ndiyo siri ya timu kufanya vizuri na wala si ubabaishaji unaofanywa hivi sasa na wanaoongoza michezo hapa nchini.

Hivi kweli timu inawekwa kambini kwa muda wa mwezi mmoja halafu inakwenda kupambana na timu ambazo zimekuwa katika maandalizi kwa muda miezi tisa au hata mwaka mzima halafu tuwe na matumaini ya timu kufanya vizuri hio ni ndoto za mchana tena ukiwa umefumba macho na kujianya umelala na kisha unaota.

Pia Serikali nayo iweke mkakati madhubuti wa kuhakikisha timu zetu za Taifa zinaaandaliwa vizuri na ikiwezekana hata zijitoe katika kushiriki michuano mbalimbali ili zifanyiwe maandalizi ya kutosha na ndipo ziingie katika mashindano ya Kimataifa kwani hapo haina ujanja wa kukwepa kwa kuwa timu ya taifa ni lazima serikali kama taifa ionyeshe juhudi zake katika kuziandaa.

Aidha, wakati umefika sasa kwa Tanzania kuwa na sera madhubuti za michezo badala ya kuwa tunababaisha kamwe hatuwezi kufika nadaima tutaendelea kuboronga katika michuano ya kimataifa hakuna haja ya kumyafuta mchswi dawa ni kufanya maandalizi ya kutosha.