HEADLINES

Mwandishi wa televisheni apoteza kazi kwa kumuuliza swali linaloudhi Waziri Tusisahau maandalizi ya Vijana Stars hata iweje!

Mwandishi wa televisheni apoteza kazi kwa kumuuliza swali linaloudhi Waziri

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

 

MWANDISHI wa kutegemwa katika kituo cha televisheni cha Zanzibar Malini hassan Malini amesi-mamishwa kazi baada ya kumuuliza Waziri wa Habari na Utamaduni Issa Mohamed Issa ambalo linamhusisha na mgogoro wa vilabu vya Zanzibar.

Habari za kusimamishwa kazi mwandishi huyo zimepatikana katika kituo cha televisheni Zanzibar na makao makuu ya wizara ya habari na utamaduni katika eneo la Shangani nje kidogo ya katikati ya mji mkongwe wa Zanzibar.

Uamuzi huo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wa kumsi-mamisha kazi ghafla mwandishi huyo wa habari za michezo umetokea siku moja tangu kufanyika mkutano kati ya waandishi wa habari na waziri wa habari na utamaduni na vijana Issa Mohamed Issa kufuatia migogoro miwili iliyozuka kati ya viongozi wa ZFA na ule kati ya mshauri wa Rais mambo ya michezo Mohemd Raza na klabu ya Small Simba.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari Malini alimuuliza waziri wa habari kwamba misamaha anayoitoa kwa vilkabu vinavyotumikia adhabu vyombo vya michezo haoni kama ndio chanzo cha kukuza migogoro na utomvu wa nidhamu kwa vilabu vya zanzibar?.

Akihojiwa na gazeti hili mwandishi huyo Malini Hassan alikiri kukumbwa na mkasa huo lakini alikataa kuzungumzia kwa undani zaidi kwa madai hana nguvu za kushindana na serikali.

Habari zilizopatikana kutoka katika kituo cha televisheni Zanzibar-Tvz-zimeeleza kwamba mbali na sababu ya kusimamishwa kazi kutokana na kumuuliza waziri swali ambalo halikumridhisha pia sababu nyingine imetajwa kuwa ni shinikizo la makamu mwenyekiti wa ZFA Ibrahim Raza ambalo ameliweka kwa waziri wa habari Issa Mohamed Issa baada ya mwandishi huyo kuripoti katika kipindi cha michezo kuwa makamu mwenyekiti .Ibrahim Raza sio msemaji tena wa ZFA taifa.

Baadhi ya wanamichezo wa Zanzibar wamesema kwamba wamesikitishwa na uamuzi wa waziri Issa kwa sababau umeingilia uhuru wa mwandishi wa kuuliza swali ambalo anahitaji ufafanuzi kujua kwa niaba ya wananchi ,.

Wanamichezo wamesema kwamba wanaangalia uwezekano wa kupeleka ujumbe wao kuonanana na rais wa Zanzibar Dk.Salmin Amour kwa kile wanachodai kwamba hawaamini iwapo suala hilo kulipeleka wizarani kwa sababu aliyemsimamisha na ndiye mwajiri wake mkuu a wa wizara inayoshughulika na vyombo hivyo.

Waziri huyo aliitisha mkutano huo na waandishi kutoa ufafanuzi juu ya mgogoro wa ZFA kati ya makamu mwenyekiti Ibrahim Raza na viongozi wengine wa chombo hicho ambao Raza aliwatuhumu kwamba wana ajenda ya siri dhidi yake.

Aidha waziri Issa alitumia mkutano huo kuzungumzia sokomoko kati ya mshauari wa rais michezo Mohamed Raza na rais wa klabu wa Small Simba Mabruki Ali Lee ambaye alikataa vifaa vya msaada wa mshauri huyo kwa madai kuwa ni vibovu.

Hata hivyo katika mkutano huo Waziri Issa alionekana dhahiri kutetea upande wa kambi ya bwana Mohamed Raza kwamba Small Simba ilifanya makosa kukataa kupokea vifaa hivyo na kusisitiza kwamba TVZ kutokuonyesha sehemu ya kiongozi huyo wa Small Simba alipokuwa akikataa kupokea vifaa hivyo kutoka kwa Bw. Raza.

Wakati huo huo mahojiano kati ya waandishi wa habari na waziri wa utamaduni inasemekana yamezuiwa kuonyeshwa kwa wananchi kupotia tvz.

Habari zilizopatikana zinasema kuwa maafisa wa habari wa kitengo cha TVZ wamelazimika kuzuia mahojiano hayo yasionyeshwe kutokana na mambo muhimu yaliyokuwa yakiulizwa kuwakera watu waliokuwa wakiguswa nayo.

 

 

Tusisahau maandalizi ya Vijana Stars hata iweje!

Na Mwandishi Wetu

HIVI karibuni Watanzania wame-endelea kuzishuhudia timu zao zikifanya vibaya katika michuano ya Kimataifa ambapo wawakilishi wao katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika Yanga waliwakatisha tamaa pale walipochapwa mabao 6 - 0 na Raja Casablanca ya Morocco wakati timu ya Taifa ya vijana ilikufa kiume kwa kuchapwa mabao 3 - 1na timu ya Taifa ya Nigeria.

Ukiondoa Yanga ambayo ili iweze kusonga mbele katika michuano hiyo inahitaji kazi ya ziada ambapo inahitaji kushinda michezo yote mitatu iliyosalia na wakati huo huo ikiwa inaomba dua timu za Manning Rangers ya Afrika Kusini ,Raja Casablanca ya Morocco na Asec Mimosas ya Ivory Coast zifanye vibaya katika michezo yao, lakini timu ya vijana inachohitaji ni kuwafunga Wanigeria katika mchezo wa marudiano utakaofanyika hapo baadaye Jijini.

Kutokana na ari ya wachezaji chipukizi wanaounda timu hiyo ambao hujituma kwa nguvu zao zote wanapokuwa uwanjani kuna uwezekano mkubwa kwa timu hiyo kucheza katika fainali za michuano hiyo zitakazofanyika nchini Ghana.

Kinachotakiwa kwa kocha wa timu hiyo Mansour Magram pamoja na viongozi wengine wanaoisimamia timu hiyo wakiwemo viongozi wa FAT ni kuhakikisha timu hiyo inafanya mazoezi ya kutosha kwa ajili ya kuwakabili wapinzani wao kwa kutoka uwanjani wakiwa na ushindi mkubwa ili kuwaliza watanzania na kuifanya timu hiyo isonge mbele.

Ni dhahiri kuwa timu ya vijana ya Nigeria haikutarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa vijana hao wa kitanzania na ndio maana mara baada ya mchezo huo wameamua kkuifanyia mabadiliko timu yao hii ni wazi kuwa Watanzania tuna nafasi ya kusonga mbele katika michuano kwani pamoja na kwamba tumefungwa lakini kiwango kilichoonyeshwa na vijana hao ni cha hali ya juu.

Mbali na mazoezi ya nguvu kingine kinachotakiwa kwa kocha wa timu hiyo ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji hao ili waone kuwa mabao matatu waliyofungwa si mengi na wana uwezo wa kuyarudisha na kuongeza mengine ikizingatiwa mchezo wa marudiano unafanyika nyumbani.

Kitu cha msingi kinachotakiwa ni kujenga ari na moyo na kucheza kufa na kupona kwa nia ya kuitetea bendera ya Taifa hasa ikizingatiwa kuwa watakuwa wakiingia uwanjani kuwawakilisha watanzania zaidi ya milioni thelathini.

Aidha, minong'ong'ono ya kujitoa kwa timu ya Burkinafaso isiwe sababu ya Vijana Stars kucheza kwa lelemama maana mpira ni vita hivyo kila mmoja ana mbinu zake za kutafuta ushindi huenda tetesi hizo zinaweza kuwa mbinu za Wanigeria hao kutaka timu ya Tanzania ilemae ikijua kuwa hata ikifungwa itasonga mbele.

Aidha, hata kama ni kweli Nchi hiyoimejitoa katika kinyang'anyiro hicho ikumbukwe kuwa Nigeria wametufunga kama wao wametufunga nasi pia tuna wajibu wa kulipa kisasi wa kipigo hicho kwa hiyo kujitoa au kutojitoa kwa Burkinafaso hakuwezi kutufanya watanzania tusiwe na haja ya ushindi katika mchezo wa marudiano na kila Mtanzania ana wajibu wa hali na mali kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri na kusonga mbele katika michuano hiyo.