Make your own free website on Tripod.com

Papa asisitiza mazungumzo kufanikisha amani Mashariki ya Kati

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amesema kuwa mazungumzo ndiyo kitu pekee kitakacholeta amani Mashariki ya kati.

Wito huo aliutoa Vatican Jumapili iliyopita wakati wa sala ya Malaika wa Bwana.

Alisema kuwa mawazo mengi hivi sasa yameelekezwa Mashariki ya Kati na hasa Iraq na wiki iliyopita yalivuta hisia ya mataifa mengi duniani.

"Natumaini kwa moyo wangu wote," alisema na kuongeza, "kuwa ufumbuzi wa haki na amani utafikiwa. Zaidi ya yote, natumaini kwamba watu wote ambao wameka-matwa watapunguziwa mateso na maumivu. Ninamwomba kila mmoja kuomba kwa Bwana ili aweze kuiangazia mioyo ya viongozi ili waendelee kutumia vyombo vya kidiplomasia na mazungumzo kutatua mgogoro huu mkubwa."

Papa Yohane Paulo alitaja kuwa Italia siku hiyo ilikuwa ikiadhimisha siku ya kitaifa ya uhamisho, ikiwa na dhamira wa 'Uhamisho kutoka Babeli kwenda kwenye Pentekoste, Umoja katika Roho' ... Ukumbusho huo uwe na matunda mazuri kwa hali ya wanaohama.

Aliendelea kusema kuwa leo hii, nchi nyingi za Ulaya zinaaadhimisha siku ya kukumbuka waliopatwa na ajali za barabarani.

Alisema siku hiyo itachangia kuwafanya madreva kuwajibika na kuheshimu maisha ya watu na sheria za usalama barabarani.

Akihitimisha hotuba yake, Papa alisema Siku ya kutolewa Maria Hekaluni inayofanyika leo kunapoadhimishwa 'Pro orantibus Day', kwa ajili ya msaada wa kiroho na kimwili kwa ajili ya monasteri zilizo na hali ngumu na matatizo.

 

Jumuiya ya kimataifa yatakiwa kuimarisha utetezi wa familia halali za kidini

Kanisa Katoliki limeitaka Jumuiya ya Kimataifa kuimarisha na kutetea haki za familia zinazotokana na ndoa kati ya mme na mke, ikiwa ni pamoja na wajibu wa wazazi kutoa elimu kwa watoto wao.

Wito huo umo kwenye waraka uliotolewa na Halmashauri ya Kipapa ya familia mwishoni mwa mkutano wao uliofanyika Vatican Oktoba 22-24 ambapo viongozi wa kisiasa na serikali wa Ulaya walijadili juu ya haki za binadamu na zile za familia.

Taarifa hiyo iliyokuwa kwenye lugha ya kifaransa inasema wametafakari juu ya uhusiano baina tangazo la Kimataifa la haki za binadamu la mwaka 1948 na lililopigwa chapa na Vatican mwaka 1983.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa tangazo hilo linaupa Umoja wa Mataifa mamlaka ya kimaadili kushughulika kwa ajili ya amani, maendeleo na kulinda haki za kila mtu.

"Mtu lazima alindwe, siyo kama mtu binafsi bali kama mtu, aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu," inasema taarifa hiyo.

Baada ya utangulizi, waraka huo unaangalia maeneo matatu ambapo sehemu ya kwanza inayoitwa ‚dharau kwa haki za familia na maisha', inatoa mifano kadhaa ambapo haki za binadamu hazitambuliwi na kuheshimiwa.

Maeneo hayo ni haki ya mtu kuishi, haki ya kuheshimu mambo na heshima ya mtu binafsi, haki ya kuoa na kuwa na familia inayopelekea kuondoa hadhi ya ndoa na haki ya wazazi kuchagua aina ya elimu kwa watoto wao.

Sehemu ya pili inajadili juu ya ‚jitihada za kutaka kuteka haki za binadamu'. Sehemu hii inaonyesha juhudi zinazo-fanywa kupata mwafaka wa kimataifa kwa kile kinacoitwa haki mpya moja wapo ile ya kutoa mimba.

Sehemu ya tatu inaitwa ‚Kutambua na Kuisaidia Familia,' inajaribu kuonyesha namna gani familia zitambuliwe na kuzisadidia kwa kila hali.

 Jean-Marie Lustiger kuongoza ujumbe wa Papa Burundi

Baba Mtakatifu amemteua Kardinali Jean-Marie Lustiger , Askofu Mkuu wa Paris kuongoza ujumbe wa Vatican kwenye kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 100 ya Ukristu nchini Burundi.

Katika barua hiyo iliyoandikwa Oktoba 10 kwa lugha ya kilatini inasema kuwa sherehe hizo zitafanyika kesho Novemba 22 huko Gitega nchini Burundi.

Kardinali huyo atasaidiwa na Msgr. Gabriel Baregensabe, vicar general wa Bujumbura na Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu la Burundi; Fr. Leo W. Cushley, Katibu wa Balozi wa Vatican nchini Burundi; na Fr. Jacques Ollier Jimbo Kuu la Paris.

Papa ahimiza ushirikiano na walei

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amewataka wenye daraja kuwa ushirikiano wa kila Mara na Walei.

Wito huo aliutoa alipokutana na Wajumbe 15 wa kamati ya Utendaji wa Shirikisho la Makleri wa Italia, ambalo linasimamia masuala ya kiroho, kichungaji, kijamii, kisheria na kifedha ya maisha ya Mapadre na Mashemasi.

Akizungumzia huduma zinazotolewa na Makleri, Baba Mtakatifu alizitaja sababu tatu za lazima wanazopaswa kukabiliana nazo.

Sababu hizo alisema nim kuwa na mazungumzo na ndugu zao na Maaskofu wao, ushirikiano na walei, na kuimarisha ishara katika nyakati hizi za maneno mengi.

Hali hiyo alisema kuwa inahitaji kwa uvumilivu kujenga misingi ya urafiki na kujihusisha.

Papa kufungua sinodi ya Oceania

Papa Yohane Paulo wa Pili ataongoza Misa katika Basilika ya Mt. Petro pamoja na Mababa wa Sinodi, katika tukio la ufunguzi wa Sinodi Maalum ya Maaskofu wa Oceania.

Sinodi hiyo itazungumzia dhamira ya "Yesu Kristu: Kufuata njia yake, Kutangaza ukweli wake, Kuishi maisha yake: Wito kwa watu wa Oceania".

Misa hiyo itafanyika kesho Jumapili Novemba 22 saa tatu asubuhi.

Kardinali kukabidhiwa parokia

Kardinali Christoph Schonborn, O.P., Askofu Mkuu wa Vienna, Austria, kesho Jumapili Novemba 22, atakabidhiwa rasmi Parokia mjini Roma ikiwa ni kawaida kwa Makardinali wote ulimwenguni kuwa na Parokia mjini Roma.

Parokia hiyo ina jina la Yesu Mfanyakazi wa Kimungu iliyoko huko Via Oderisi da Gubbio 16, Rome saa tano asubuhi.

Tamasha la filamu ya Tertio Millenio'kufanyika

Kardinali Paul Poupard Rais wa Halmashauri ya Kipapa ya Utamaduni na Askofu Mkuu John Foley Rais wa Halmashauri ya Kipapa ya Mawasiliano ya Jamii walizungumza kwenye ufunguzi wa kikao kilichoandaliwa na Halmashauri hizo zikishirikiana na Bodi ya Burudani ya Italia yenye dhamira ya Sinema na thamani ya maisha'.

Mkutano huo wa siku tatu unatangulia tamasha la pili la sinema ya kidini Tertio Millenio' iliyoanza jana hadi Novemba 30 mwaka huu.