Jasusi hadi ndani ya Vatican

Rome, Italia

MKUU wa Shirika la kipelelezi la zamani la ujerumani ya Mashariki amesema kwamba alifanikiwa kumpata mtawa wa shirika la Wabenediktini na kumtumia kama jasusi wake ndani ya Vatican.

Markus Wolf ambaye alikuwa Mkuu wa shirika hilo maarufu kama Stasi amesema kwamba jasusi lake huyo alikuwa anaitwa Brammer au Brammert kama jina la utambulisho na alikuwa akifanya kazi katika ofisi ya sayansi ya Vatican.

Kwa muda mrefu Wolf amekuwa akisema kwamba anajasusi ndani ya Vatican ambaye hakufanikiwa kukumbuka jina lake vyema.

Alikuwa akizungumza katika televisheni kuadhimisha miaka 20 ya upapa wa John Paul wa Pili ulioadhimishwa mwaka huu mwezi wa Oktoba 13.

Wakatioliki wengi wanaamini kwamba Wolf alikuwa akimzungumzia Padri wa Kibediktini aitwaye Eugen Brammertz ambaye alikuwa akifanyakazi katika gazeti la Vatican linalotolewa kwa Kijerumani hadi kifo chake mwaka 1987.

Padri huyo ambaye alikufa akiwa na umri wa miaka 71 inadaiwa alikuwa mtu wa Stasi, alisema kiongozi wa Wabediktini, Pius Englebert ambaye pia alisema hakuwa anazisadiki kwa kuwa zilivuja baada ya padri huyo kufa na baada ya Muungano wa Ujerumani Mashariki na Magharibi.

Serikali ya Vatican hata hivyo haikuweza kusema chochote kuhusiana na suala hilo.

 

Rais ataka wanasheria Kenya wasiendelee kufundishwa

lKisa wamejijengea hoja ya fedha zaidi kuliko ukweli

lKardinali naye ataka wanasheria na watekelezaji kujali ukweli

NAIROBI, Kenya

UGOMVI wa Rais Daniel Arap Moi na wanasheria wa Kenya umefikia hatua nyingine baada ya rais huyo kusema kwamba nchi hiyo ina mawakili na wanasheria wengi kwa hivyo vyuo vya nchi hiyo visiendelee kufundishwa wengine.

Kauli ya kiongozi huyo mkuu wa Kenya imekuja wakati katika siku za hivi karibuni amekuwa na uhusiano finyu, uhusiano ambao umepelekea kuwaona mawakili na wanasheria wapo pale kwa kutaka maangamizi yake.

Katika miaka 20 ya utawala Rais Moi amekuwa akipambana mara kwa mara na wanasheria.

Kenya ambayo ina watu takribani milioni 30 ina mawakili wasipopungua 2000 wengi wao wakiwa na ofisi zao wenyewe.

Aidha idadi ya wanasheria nchini Kenya inazidi kuongezeka kila mwaka huku vyuo vya Kenya vikiwa na idadi kubwa na wengine wakitokea nchi za Ughaibuni hasa Uingereza na India.

Pamoja na uwingi wa wanasheria hao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Kenya huajiri wageni wengi zaidi kuliko wenyeji na bado sababu haijulikani.

Wachambuzi wa mambo wanahisi kuwa labda ni hali ya wakenya wengi kuamini kwamba wageni ndio pekee wanaoweza kuitenda haki.

Habari zinasema kwamba wengi wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya sheria kwa sababu ya kutaka tu kutengeneza fedha, kwao Unasheria ni kazi yenye fedha za kutosha.

Kutokana na tatizo hilo la fedha makampuni mengi yamekuwa katika matatizo makubwa yakiwemo ya kuwa na kesi ambazo zina walakini kiutaalamu na utata katika mipangilio.

Pamoja na hali hiyo wanasheria wengi zaidi wamejikuta wakisimamishwa kizimbani na wateja wao kutokana na kula fedha za wateja au kuzitumia vibaya.

Katika jarida la African News Bulletin (ANB-BIA) imeelezwa kuwa tatizo kubwa la watu wa Kenya ambalo pengine ndilo limemfanya rais Moi kusema wasiendelee kufundishwa ni ujinga wa wengi wa wakazi wa hapa.

Imeelezwa kuwa wakazi hao mara nyingi huwa tayari kulipa fedha hata kwa kesi ambayo kwao hawawezi kuipatia ushindi kwa kuwa tu wanasheria wameshauri.

Hata hivyo wanasheria hao hawajali kuwa wakweli na waaminifu wanachotaka ni fedha na kisha kuingia mitini wakiona humalzii fedha hizo na wala hawezi kujishindia kesi hiyo.

Katika moja ya mafunzo ya vyombo vya habari imeelezwa kinagaubaga kuwa wanasheria wa Kenya ni wakorofi ambao huweza kuingia katika hali yoyote na kufanyakazi yao hata kama wanajua ni kinyume na ukweli wa mambo.

Wakati huo huo habari kutoka washington zinasema kwamba Kardinali George amezungumzia haja ya wanasheria kuukumbatia ukweli kama unavyoelezwa katika Biblia.

Kardinali George wa Chicago alikuwa kihutubia katika misa huko Washington kwa wanasheria na mawakili na watengenezaji wa sheria.

Kardinali amesema katika misa hiyo ya kuwaombea uangavu wa roho mtakatifu watekelezaji na waundaji wa sheria kuwa inawastahili wao kama watekeleza wa majukumu ambayo mwenyezi Mungu ameyalenga katika historia ya uumbaji wake.

Amesema utekelezaji wa sheria uzizozingatia ukweli na ukweli wa Kibiblia utakuwa hauna maana kama kila kitu kitakuwa kinyume.

Kuna zaidi ya watu 1500 waliohudhuria misa hiyo ambayo hufanywa kila Oktoba ya Jumapili ya kwanza kuwaombe watunzi na watekelezaji wa sheria.

Wahamiaji Afrika Kusini wakipata cha moto

CAPE TOWN, Afrika Kusini

SHIRIKA la habari la Kikatoliki CNS rimeripoti kwamba ugaidi dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini unazidi kuongezeka na kutishia amani kwa wahamiaji hao.

Taarifa zinasema kwamba ongezeko hilo linatokana na madai kuwa wageni wanatwaa nafasi za kazi za wazalendo wa nchi hiyo.

Wageni wakazi walipo nchini Afrika kusini wamesema kwamba wamekuwa wakisikia mara kwa mara mashambulio dhidi ya wahamiaji.

Wahamiaji hao mara nyingi hupata kazi za vibarua na kila walipokuwa wakitoka katika kazi hizo walikuwa wakishambuliwa.

Wahamiaji wenyewe wamekiri kwamba kushambuliwa kwao kunatokana na kudidimia kwa nafasi za kazi na hivyo kazi za kudharaulika kama za uaskari na uuzaji vitu kimachinga ambazo wageni ndio waliokuwa wakizifanya sasa zinavamiwa na wenyeji.