Padri aliyetaka kanda za kifuska atimuliwa

ROMA, Italia

MKURUGENZI wa zamani wa moja ya majarida ya kikatoliki yanayouzwa kwa wingi nchini Italia, Padri Leonardo Zega ametimuliwa moja kwa moja katika jarida hilo kwa kuandika hoja ya wenye ndoa kuruhusiwa kuangalia picha za kifuska ili kuimarisha uwezo wao wa kufanya tendo la ndoa.

Habari zilizoandikwa na shirika la Habari la Kikatoliki (CNS) zinaripoti kuwa kuondolewa jumla katika utendaji wa gazeti hilo umefanywa na mkurugenzi wa sasa ambaye aliwekwa hapo na Papa katika harakati zake za kuongeza nidhamu na uwajibikaji wa kimaandishi kwa taratibu za kanisa.

Msemaji wa jarida hilo linatolewa mjini Milan, Mauro Broggi akielezea alisema kwamba kuondolewa kwa padri huyo kumekuwa ni lazima kutokana na kuandika mambo ambayo hayaendani na maagizo.

Padri Zega aliondolewa katika nafasi yake Agosti mwaka huu lakini akaruhusiwa kuendelea na kolamu yake ya majadiliano na mapadri, ambapo imedaiwa mara kadha amekuwa akivuka mstari uliowekwa kwa mafundisho ya dini.

Jarida hilo linatoka kwa wiki mara moja likizungumzia maisha ya kikatoliki, Famiglia cristiana, limekuwa likionekana kuchukua msimamo mkali kuhusu maisha na mafundisho ya kanisa kiasi cha kumfanya Papa ambaye pia ni Askofu wa Roma kubadili watendaji wa gazeti hilo linalotolewa na jumuiya matakatifu Paul.

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani hakufanya mabadiliko katika gazeti tu bali alibadili uongozi wa juu wa jumuiya hiyo kwa kumweka mtu mwingine, Padri Franco Pierini, Februari mwaka jana.

Padri huyo ametakiwa kushughulikia zaidi vyombo vya habari vya jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa habari za CNS, jumuiya hiyo imekuwa ikisaka uhuru wa habari kwa kukabiliana vilivyo na utawala wa Vatican hasa Kardinali Joseph Ratzinger.

Kardinali Ratzinger ni Waziri wa Mambo ya Dini na Imani. Jarida la Famiglia Cristiana na machapisho mengine kutoka katika jumuiya hiyo yamekuwa yakishutumiwa kwa kuandika habari zenye mwelekeo mkali kuhusu imani, ngono, utoaji wa mimba na talaka.

Kabla ya papa kuamua kuwaadhibu watu wa jumuiya hiyo kwa kuwapelekea mtu mwingine, jarida la Famiglia lilitoa taarifa ya haja ya watu waliotalikiana kupokea mkate wa Bwana.

Gazeti hilo pia lilishawahi kuandika kuhusu upigaji punyeto na kutaka kanisa liache kulishupalia na kuacha wanamume kwa wake (vijana) kuendelea na punyeto.

 

Walemavu Uganda kuagiza Viagra

Na Amour S. Khamisi,PST,KAMPALA

OFISA wa maendeleo ya biashara wa chama cha watu wenye ulemavu cha Uganda (NUDIPU) Bw. David Mulya amesema kwamba chama chake kitafanya kampeni ya kuingiza dawa ya kuongeza nguvu za kiume (VIAGRA), nchini humo ili kutatua tatizo la wanaume wasio na nguvu za kiume.

Hii itakuwa ni nafasi kwa wanaume ambao uwezo wao wa kukutana kimwili ni ndogo sana kuweza kurudishiwa hadhi yao . Alisema katika mahojiano na PST.

Viagra ni dawa ya kuongeza nguvu za kiume inayotengenezwa na kampuni ya Kimarekani ya madawa ijulikanayo kwa jina la PFIZER Laboratories.

Kwa mujibu wa Taarifa ya chama cha Madaktari wa Uganda nchi hiyo inakadiriwa kuwa wanaume 500,000 hawana nguvu za kiume (mahanisi) .

Mulya alisema kwamba chama chake kinatafuta taarifa juu ya Viagra kama vile gharama na nguvu yake.

Alisema kwamba uhanithi ni hatari zaidi kuliko ukimwi ambapo aliongeza kuwa uhanithi ni ulemavu kwa sababu unaathiri hali ya maumbile ya kawaida ya binadamu kwa muda mfupi na pia unaweza kuwa ulemavu wa kudumu.

 

Zimbabwe yatakiwa kuondoa askari Congo

HARARE,Zimbabwe

MSUKUMO wa kumtaka rais Robert Mugabe kuyaondoa majeshi ya nchi hiyo yaliyopo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya watu wa Congo yanayomsaidia rais wa nchi hiyo Bw.Laurent Kabila umeongezeka ..

Shirika la habari la AANA limerpoti kuwa watu mbalimbali nchini humo wamemtaka Rais Mugabe kuyaondoa majeshi ya nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Congo .

Watu hao wamedai kuwa hakuna chochote cha maana na kwamba vita hiyo inakuwa mzigo mzito kwa Zimbabwe.

Aidha walisema kwamba wakati huu uchumi wa nchi hiyo unalemewa hivyo ni vyema Rais akaondoa majeshi ya nchi hiyo kutoka Congo.

Majeshi ya Zimbabwe yalijiingiza katika mapigano ya Congo kwa lengo la kumsaidia Rais Laurent Kabila dhidi ya waasi wa Banyamulenge miezi miwili iliyopita kufuatia waasi hao kuanza mapambano ya kumng'oa madarakani Rais kabila ambaye walimsaidia kumuweka madarakani mwaka mmoja uliopita baada ya kuyashinda majeshi ya hayati Mobutu Sese Seko.

Pamoja na majeshi ya Zimbabwe yapo majeshi ya nchi ya Angola na Namibia ambayo yamejiunga na majeshi ya Serikali ya Rais Kabila ambayo yamefanikiwa kuwasimamisha waasi upande wa Magharibi na kufanikiwa kuudhibiti mji wa Kinshasa.

Hata hivyo majeshi hayo yameshindwa kuwaondoa waasi upande wa mashariki ya Congo ambako waasi hao wanamiliki eneo hili na hivi karibuni walizifukuza ndege za serikali katika eeo hilo.

Hadi kufikia sasa jumla ya askari 50 wa majeshi ya serikali ya Zimbabwe wamepoteza maisha katika mapigano hayo jambo linalosababisha vyama vya upinzani nchini humo kutaka majeshi ya nchi hiyo yarudi nyumbani na kujitoa katika mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe.

 

Viongozi wa kimila Uganda wataka wanawake wabadili uvaaji

KAMPALA ,Uganda

VIONGOZI wa mila na dini katika jimbo la Buganda nchini Uganda wamewataka wanawake nchini humo kurejea katika mavazi ya asili badala ya yale ya kisasa yasiyo na heshima.

Kwa mujibu wa jarida la All Africa News Agency la mwezi Oktoba mwaka huu limesema kuwa viongozi hao wamepinga vikali uvaaji wa vimini na gauni ndefu zinazobana mwili mavazi ambayo yamekuwa maarufu miongoni mwa wanawake wa nchi hiyo hasa katika mji mkuu wa Kampala.

Jarida hilo linasema kuwa wanawake katika himaya ya Kifalme ya Baganda eneo la kati la nchi hiyo wana mavazi ya asili ya busuti au gomesi ambayo ni ambayo kwa kawaida huwa marefu yakiwa na mikunjo mingi ambayo hayabani mwili wa mvaaji.

Uvaaji wa vazi la busuti ni wa lazima kwa wanawake wote wakati wa sherehe za kijadi lakini wasichana wengi siku hizi wanadhani kwamba vazi hilo si zuri kwa kwenda ofisini na kwenye madisko

Hivi karibuni msimamizi wa kanisa la Mtakatifu Agnes John Kiwanuka aliwakataza wanawake kuvaa vimini na magauni marefu yanayowabana maungo yao.

Katika hatua nyingine inayoonyesha mvutano juu ya mavazi ya vimini kwa wanawake nchini humo mhubiri wa Kanisa Katoliki wa Nsambya ambaye aliwataka wanawake wote waliofukuzwa katika Kanisa la Mtakatifu Agnes wapo huru kujiunga na kanisa lake ambapo alisema wamewafukuza watu wa Mungu.

Padri Paul Gigri alisema haoni kitu chochote kibaya katika mavazi yote ya mitindo ikiwa wanawake hao wanasali na kumuomba Mungu.Katika mitaa ya jiji la Kampala ni hatari kwa wanawake kuvaa nguo fupi na zinazobana maungo yao.