Moto waanza kumuwakia rais Clinton

WASHINGTON, Marekani

BARAZA la wawakilishi la Marekani jana likitupilia mbali madai ya chama cha democrats ya kuacha kuzungumzia suala la kushitakiwa kwa Rais Bill Clinton, kwa kashifa yake ya ufuska kutokana na taifa hilo kuwa vitani dhidi ya Irak, lilianza kusikiliza shauri la Rais huyo, shauri ambalo lilitarajiwa kupigiwa kura jana jioni, leo au Jumatatu asubuhi .

Ingawa uwezekano wa kusalimika katika shauri hilo ni sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano, wawakilishi wa Democrat wamelitaka bunge hilo kutofikiria kabisa kumshitaki Amiri Jeshi mkuu wakati majeshi ya nchi hiyo yako vitani.

Shauri hilo lilianza kuzungumzwa licha ya taarifa kwamba majeshi ya nchi hiyo yanajiandaa kufanya shambulio la tatu dhidi ya Irak usiku wa kuamkia leo.

" Suala zima la kwenda kumshitaki Rais ambaye ni Amiri Jeshi mkuu wakati wanawake kwa waume katika jeshi la nchi hiyo wanahatarisha maisha yao kunaonyesha kasoro kubwa katika shauri zima" alisema mjumbe mmoja wa Democratic Bw. David Bonior wa Michigan .

Mwakilishi mwingine wa Democrat Bw.Maxine Waters, wa California amesema kwamba ilikuwa ni uzandiki mtupu kwa spika huyo kuanza taratibu za kumshitaki Rais baada ya yeye mwenyewe kukiri udhaifu wake.

Ingawa mambo yamezidi kuwa mazito kwa Rais Bill watumishi wengi wa Ikulu ya Marekani wanaamini kwamba rais huyo hataondolewa madarakani hata kama shauri hilo litafikishwa katika baraza la Seneti kwa kuwa haitawezekana kwa Baraza hilo kufanikisha theluthi mbili za kura zinazotakiwa kumuondoa Rais Madarakani.

Kama Bunge hilo lenye wajumbe 435 litapitisha hoja ya kushitakiwa kwa Rais, Shauri hilo litapelekwa katika baraza la Seneti na kuamuliwa mapema mwakani.

Rais Bill Clinton anahitaji wajumbe 15 kutoka chama cha Republican kumuunga mkono kama itabidi apone katika jaribio hilo lililong'ang'aniwa na chama cha Republican.

 

Mabomu ya Marekani dhidi ya Irak kumuokoa Bill Clinton?

WASHINGTON, Marekani

MAAFISA wa Ikulu ya Marekani jana waliendelea na juhudi za mwisho za kumuokoa Rais Bill Clinton kutoka katika aibu kubwa ya kushitakiwa katika kashifa yake ya ufuska .

Juhudi hizo zilisitishwa Alhamisi iliyopita baada ya Marekani kuishambulia Irak kwa makombora katika kile kinachodaiwa kuihimiza kutekeleza makubaliano yake na Umoja wa Mataifa.

Jana makombora ya Marekani yaliendelea kuvuma dhidi ya Irak na wataalamu wa masuala ya kijeshi wa Marekani wamesema mashambulio hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Huku kukiwa na mashaka makubwa ya Urais wa Bw.Bill Clinton baada ya kung'ang'aniwa kooni na wajumbe wa chama cha Republican maafisa wa Ikulu ya Marekani wamesema kwamba ndege za kivita za Uingereza na Marekani zilikiruka kutoka katika manowari zilizoko kwenye Ghuba ya Uajemi na kushambulia Irak.

Ingawa majeshi ya Irak yalijibu mashambulio hayo kwa kujaribu kutungua ndege hizo, taarifa za awali zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 50 wa Irak wameuawa na majengo mengi kuharibiwa vibaya.

Aidha inadaiwa watu zaidi ya 100 pia wamejeruhiwa.

Mashambulio hayo yenye lengo la kupunguza uwezo wa kijeshi wa Irak yaliyoanza Jumatano yanadaiwa yataendelea kwa muda mrefu ujao.

Mataifa kadha yaliyomo katika baraza la usalama yameshutumu mashambulio hayo huku Russia ikiwaita mabalozi wake wa Uingereza na Marekani nyumbani kwa mashauriano.

Japan na Ujerumani wanaunga mkono mashambulio hayo.

Russia pia imemtaka Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya kuharibu silaha za Irak Bw. Richard Butler, kujiuzulu. Ripoti ya Mkaguzi huyo wa silaha kwa Umoja wa Mataifa ikidai kukosekana kwa ushirikiano na serikali ya Irak ndiyo iliyotoa sababu ya kushambuliwa kwa taifa hilo. China nayo imeungana mataifa mengine kulaani mashambulio hayo iliyodai ni ya aibu na ya kukatisha tamaa.

Ingawa ndege hazikuonekana waziwazi katika mashambulio hayo, Marekani inasema inatarajia kufanya mashambulio zaidi kwa kutumia madege makubwa ya kivita aina ya B-52 bombers, ambayo yameshehenezwa makombora aina ya cruise.

Katika shambulio hilo nyumba ya mtoto mmoja wa Saddam Hussein ilipigwa mabomu, mtoto huyo hakuwepo nyumbani.

Zaidi ya makombora 200 yalitupwa kwa siku ya kwanza pekee yakilenga kambi kadha za kijeshi na kikosi cha mizinga ya kutungulia ndege.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Bw. William Cohen amesema kuwa hakuna hasra yoyote kwa upande wa taifa hilo.

Juzi Marekani ilitangaza kufunga ofisi zake za ubalozi 40 katika bara la Afrika kwa kuhofia usalama wake kutokana na mashambulio hayo dhidi ya Irak.

Wajumbe wa Baraza la wawakilishi wapatao 435 jana walikuwa wanajadili hoja mbalimbali zinazokusudia kumwondoa madarakani Rais Bill Clinton kutokana na ripoti ya Kenneth Starr.

Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba huenda shauri la Rais huyo likapitishwa kwa kura chache na hivyo kushitakiwa katika baraza la Seneti kwa kutumia vibaya madaraka yake kuficha uhusiani wake wa kimapenzi na mtumishi wa zamani wa Ikulu ya Marekani Bi.Monica Lewinsky.

Katika hali inayoonyesha mkutano wa jana kuwa mgumu zaidi spika mteuliwa wa chama cha Republican Bob Livingston naye alikiri kuwa na vimada na hivyo kuongopa katika ndoa yake kwa miaka 33.

Aidha amesema kwamba kutokana na hali hiyo amesaidiwa kwa ushauri nasaha.

Kukiri huko kulifanyw amuda mfupi kabla ya kuanza kwa kikao cha jana kuzungumzia shauri la Rais Bill Clinton la ufuska katika ikulu ya Marekani na Mwanamke Monica Lewinsky.

"Ninachotaka kuwahakikishia kwamba mambo haya sikuyafanya na wafanyakazi wangu na wala sijatakiwa kueleza mambo hayo chini ya kiapo," Livingston alisema katika taarifa ambayo aliitoa kwa waandishi wa habari.

 

Biashara ya viungo vya mwili yashamiri Chad

l Watoto wanyofolewa sehemu za siri na macho kufanyiwa kafara la kupata utajiri

l Watafuta macho ili wakiiba wasionekane

TANGU Januari mwaka huu mji mkuu wa Chad, Nd'jamena umekuwa ukikabiliwa na wimbi kubwa la wizi wa viungo vya binadamu, wizi wa watoto, kupotea kwa watu katika mazingira ya kutatanisha, watu wanaogushi nyaraka na kutengeneza noti za bandia na pia kuelezwa kwamba kuna nyanya ambayo inatoa machozi.Katika makala haya ya ANB BIA Mwandishi Misse Nanando anaeleza zaidi.

Januari 30, 1998 taarifa ya serikali ilionyesha kwamba Yaya Batit Ali, Rais wa chama ha National Unity, Dialogue and Democracy (PUNDD), moja ya vyama 67 vya kisiasa nchini amepotea katika mazingira ya kutatanisha.

Maswali yaliulizwa yakakosekana majibu. Lakini wenyewe PUNDD walidai kutekwa na serikali, askari waliotumika ni wale wa ANS, Idara inayoshughulikia usalama wa nchi hiyo. Vyombo vya habari vya ndani na nje ya Chad vilisema hivyo, lakini serikali iling'ang'ania kwamba haina habari na wala haihusiki. Ni dhahiri ilikuwa habari mbaya na ya chukizo lakini vyama vya siasa na vingine vikajikuta vinashindwa kabisa kujua au hata kung'amua ukweli wa mambo.

Baadaye zikaanza hisia kwamba lipo kundi linalojishughulisha na utekaji nyara, shughuli ambayo wakati mwingine wanaipakazia serikali.

Hata hivyo kundi hilo linaaminika ndilo lile ambalo huteka watu na wakapeleka Nigeria kwa ajili ya kuwatumikisha katika mashamba ya kahawa wakiwa kama watumwa.

Leo licha ya taarifa mbali mbali za serikali kiongozi huyo yupo gerezani akisubiri kusomewa mashitaka. Kisa, serikali inamtuhumu kusambaza maneno yenye kuikorofisha serikali na kuleta fitina na wananchi wake.

Unaweza kuamini au usiamini. Hayo ya juu si mambo machache yanayotokea kwa kasi katika mji wa Nd'jamena.

Mwezi Aprili mwaka huu kwa wiki nzima wananchi walikuwa wakikusanyika kandoni mwa televisheni zao kuona nyanya inayolia. Nyanya hiyo ilikuwa katika studio za televisheni hiyo ya serikali. Watu wengine hawakuamini hilo, walijua ni kasoro katika makuzi ama kwa kukosa nafasi au basi imekuwa haina vichembe vinavyostahili kuonekana vyema kama nyanya. Hata hivyo watu wengi ambao huamini mambo ya kichawi walisema kwa imani kabisa kwamba wajihi wa nyanya hiyo ni wa kitu kinachotoa machozi na si suala la kukosekana kwa nafasi ya makuzi, wamesema nyanya hiyo inalia kwa kuwa taifa la Chad linapitia katika kipindi kigumu cha mateso.

Uchawi wa jinai

Kuna mambo mengine ambayo yamekuwa yakiendelea katika nchi ya Chad na kuwafanya wazazi hasa akina mama kuhamanika na kuamua kuwadhibiti watoto wao wasitoke nje wakiwa peke yao.

Wengi wa watoto hao wamefichwa nyumbani bila ya kuwepo kwa maelezo muafaka kwa nini wanafichwa ndani. Lakini hata hivyo maneno yalishaenea kwamba wako watu wanaowakamata watoto wadogo wakawachinja na kutwaa sehemu zao za siri kuwapelekea waganga wa kienyeji kwa ajili ya kuwapatia utajiri.

Watoto wanaokwenda shule walielekezwa kabisa kwamba ni marufuku kuongea na mtu wasiyemfahamu wala wasikubali zawadi kutoka kwa awaye yote. Pamoja na kukataliwa kutwaa zawadi wanazopewa na wageni watoto wamezuiwa kumsa-limia mtu wasiyemjua. Hao ni watoto ambao imekuwa lazima waende shuleni lakini wale ambao si lazima walifungiwa ndani.

Jambo la kutisha ni mwanamke mmoja ambaye alimnyonga mdogo wake ili apate macho ya kumfikishia mganga amtengenezee awe tajiri. Pamoja na macho alitakiwa amfikishie mganga ubongo wake. Mwanamke huyu alikamatwa na polisi na kuungama kuwa alikuwa ameagizwa na guru mmoja (mganga) ili aweze kupatiwa utajiri mkubwa.

Katika tukio jingine mwili wa mwanamme kichaa na watoto wawili ulikutwa bila viungo vyao vya siri. Polisi wa upelelezi wameshindwa kumpata muhusika ingawa miili hiyo iliokotwa karibu kabisa na jengo la Halma-shauri ya Jiji la Nd'jamena, kwenye pondo moja.

Tishio jingine kubwa ni lile ambalo lilifika mahakamani na wahusika wakakiri kwamba walimuua Abdelkader ili wapate macho yake na kuyafikisha kwa mganga wapatiwe dawa ya kuiba na wasionekane. Vijana hao waliouawa wana miaka 18 na mmoja alijulikana kwa jina la Ahmat Abdelkaerim na mwenzake Idriss.

Kugushi na Noti bandia

Mambo ya kichawi si tu ndio mambo ya kutisha pekee yaliyokumba mji wa Nd'jamena bali pia yapo mambo ya kuuzi yanayosumbua maisha ya binadamu kama suala la kugushi na utengenezaji wa noti za bandia.

Watu wanaotengeneza noti za bandia nao wanawachezea wananchi wa Nd'jamena kama mchezaji staa wa soka anavyomiliki vyama mpira akiwa uwanjani. Watu hawa wajanja na majahiri wamefanikiwa kuwaibia hata maafisa waandamizi wa serikali. Si mzaha, waziri mmoja alipoteza mshahara wake wote baada ya kuletewa fedha nyumbani kutoka benki zikiwa ni za bandia.

Mtu mmoja alikamatwa nchini Ujerumani akiwa na madawa ya kulevya kokeini na hati ya kusafiria yenye heshima ya kibalozi na alipoulizwa alisema yeye ni msaidizi katika Ikulu ya nchi hiyo, lakini alipopelelezwa vyema ilikuja kubainika kwamba yeye si kitu wala mtu katika serikali ya Chad.Lakini swali linabakia lipataje hati ile ya kusafiria? Imebainika kwamba pasi nyingi za kusafi-ria za Chadi zenye hadhi ya kibalozi ni za kugushi lakini zimetolewa na mamlaka husika.

Nd'jamena sasa imekuwa maarufu kwa hati za bandia, noti za bandia na biashara haramu ya kubadilisha noti, biashara ambayo tayari imeondoa uaminifu wa fedha ya hapa. Unaponunua fedha uwezekano wa wewe kupata ya bandia ni mkubwa wakati vile vile unapotaka chenji unaweza kupata noti bandia.

Inadaiwa umaskini ndio umefanya kufumuka kwa vitendo hivi vya aibu ambavyo vinachangia kuzidi kudidi-miza uchumi wa Chad na kuuweka katika hali mbaya.

Katika hali ya kawaida kuharibika kwa utamaduni wa heshima, ukosefu wa chakula kutokuwepo na bashasha ya maisha kunafanya watu kukurupuka na kufanya vitu ambavyo huwezi kuamini ama vinafanywa na mtu mwenye akili.