Huduma katika vyombo vya habari iwe katika uwiano

VYOMBO vya habari na upashanaji habari kwa ujumla una malengo makuu matatu. Lengo la kwanza ni kuelimisha wasomaji, wasikilizaji na watazamaji.Lengo la pili ni kuwahabarisha wasomaji, wasikilizaji na watazamaji. Na lengo la tatu ni kuwaburudisha au kuwastarehesha wasomaji, wasikilizaji na au watazamaji. Hivyo tunaposoma kitabu au gazeti tunatarajia kuona malengo hayo ya chombo hicho cha maandishi, yaani wasomaji wapate elimu, wapate habari na pia waburudishwe au kustareheshwa na chombo hicho.Vile vile tunaposikiliza radio, tunatarajia kuwa kutakuwa na kuelimishwa, kupashwa habari na pia kuburudishwa au kustareheshwa. Mambo ndivyo yalivyo pia au yanavyopaswa kuwa tunapoangalia televisheni.

Siku hizi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika nchi yetu kuna vyombo vingi vya mawasiliano vya umma na pia vya watu binafsi, Tuna mitambo ya kuchapisha vitabu ya serikali na mashirika ya umma na pia kuna mitambo ya uchapaji ya watu binafsi. Tuna magazeti yanayotolewa na serikali na pia tunayo magazeti yale ambayo hutolewa na watu binafsi au mashirika binafsi. Tunavyo vituo vya radio vya umma na pia radio za watu binafsi.Na zaidi ya hapo kuna vituo vya televisheni vya watu binafsi na pia "ile ya taifa". Lakini vyombo vyote hivyo vinapaswa kufanya kazi kwa malengo hayo yote matatu, yaani kuelimisha, kuhabarisha na pia kuburudisha.

Jambo la kusikitisha ni kwamba katika vyombo hivyo mbalimbali pengine hakuna ule uwiano wa malengo ya vyombo vya habari. Kuna baadhi ya vyombo vyetu vya habari kama vile redio au televisheni, ambavyo havikidhi malengo yote ya vyombo vya habari. Mara nyingi tunashuhudia kwamba chombo fulani kinakuwa na sehemu kubwa sana ya burudani na ile sehemu ya kuelimisha huwa ni kidogo sana. Kwa mfano kuna vituo vya redio ambavyo hupiga tu muziki kwa masaa mengi, bila kuwaelimisha au kuwahabarisha wasikilizaji. Ni kweli kuwa kuna miziki ambayo ina mafundisho ndani yake, lakini ni kidogo mno. Kuna vituo vya redio ambavyo toka kufunguliwa kwake (pengine zaidi ya mwaka mmoja) hupiga muziki tu kwa masaa mfululizo. Hapo tunaona ni kukiuka malengo hasa ya vyombo vya habari kwa vile hakuna uwiano katika malengo hayo ya vyombo vya habari. Ni muhimu kuwa na mchanganyiko wa vipindi katika redio au televisheni. Tunatambua kuwa kuandaa vipindi mchanganyiko huhitaji watayarishaji wengi, tena wenye ujuzi katika fani hiyo ya uandishi na upashanaji habari. Ndiyo maana kuna vyuo vya kuwasomesha waandishi wa habari, watangazaji na wale wote wanaotaka kufanya kazi katika uwanja huu wa upashanaji habari, lakini jambo linalotakiwa ni kwamba kila mmoja anatakiwa kupata kile anachokihitaji katika chombo cho chote cha habari. Mwenye kutafuta taarifa ya habari, aipate wakati wake; mwenye kutaka elimu katika jambo fulani aipate kwa njia ya chombo hicho anachokitaka. Na yule mwenye kutaka burudani au kustarehe na chombo fulani cha habari astarehe na kuburudika kwa wakati wake.

Ni jambo la kuwakosea wengine haki ikiwa chombo kitazingatia lengo moja tu kati ya hayo matatu.Kuna wengine hata wa mgazeti ambao hutumia muda mwingi au sehemu kubwa sana katika porojo, na hata tunaweza kusema katika mambo ya upuuzi, yasiyojenga, yasiyoelimisha na wala kutoa habari za maana. Kwa kadiri tunavyofahamu, muda wa kuwa hewani, au nafasi katika karatasi una gharama kubwa sana.

Jambo linalotakiwa tufanye, sharti tuzingatie kanuni za upashanaji habari ambazo ni za kimataifa. Kuna miongozo rasmi ya utangazaji ambayo kila mtangazaji na mwenye kituo cha utangazaji yatakiwa afuate. Wale wanaoandika katika magazeti au vitabu, sharti wafuate kanuni za uandishi wake; watangazaji katika redio wanapaswa kufuata kanuni za redio, na hivyo hivyo watangazaji wa televisheni wanapaswa kufuata kanuni za kimataifa za televisheni. Tunapenda kuona vyombo hivyo vinatenda kazi kulingana na maadili, nidhamu na utaratibu wake.

 

Polisi ijifunze kutokana na ajali Mlandizi

Ndugu Mhariri,

Napenda kwa mara nyingine kutoa yangu machache niliyo nayo moyoni kuhusiana na ajali mbaya ya kusikitisha iliyotokea hivi majuzi nchini mwetu huko Mlandizi, ninayo majonzi makubwa moyoni mwangu binafsi na pia mioyo ya watanzania wengine Wakristo, Waislamu na wengineo;tumesikitishwa sana na tukio hilo la kihistoria na la kushtua sio tu Watanzania bali ulimwengu mzima.

Nashangaa sana kusoma na kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa sasa serikali ikishirikiana na Jeshi la polisi wa usalama barabarani ndio inakumbuka kuwa huu ndio wakati muafaka wa kuyadhibiti magari na madereva wanaokiuka sheria za barabarani baada ya ajali ya Mlandizi kutokea! Kwanini udhibiti hii usingelifanywa miaka 20 iliyopita?

Serikali kwanini mnakumbuka wajibu wenu baada ya tukio hatari kama hilo kutokea? Mimi naamini kama askari wetu wangefanya kazi yao vizuri kila wakati bila kusubiri washituliwe na maafa, ajali hazingetokea hivi ama kama zingetokea (maana sote ni binadamu) haingesababisha maafa makubwa kama ya Mlandizi. Roho za watu wasio na hatia zimeondoshwa duniani kwa sababu ya uzembe, ulevi, kutojali ama kukosa ujuzi wa madereva wa magari yetu barabarani. Hatuwezi kusema ati barabara pale Mlandizi ni mbovu !!

Cha ajabu ni kwamba hata magari ya kisasa yanakuonya wewe dereva kuwa punguza mwendo baada ya kupitiliza speed kufikia kasi ya hatari kwa

kengele iliayo kwa maana kwamba dereva mwenye akili timamu angesikia

lakini wapi!

Mwisho nawaombea pumziko la milele wote wale waliopoteza maisha yao sio pale tu Mlandizi bali duniani kote barabarani au angani na pia baharini.

Ni mwenzenu

Vallery A. Mrema

Box 3622

Dar es Salaam.

 

Kiongozi tuokoeni jamani

Ndugu Mhariri,

Kwa niaba ya wananchi wenzetu walala hoi wa wilaya hii, tunaomba utupe nafasi kulipongeza gazeti hili la Kikristo:la KIONGOZI ambalo kwa siku za karibuni ndipo limeanza kuonekana hapa wilayani kwetu Tarime.

Siyo kwamba tunalipongeza kwa kuwa sasa linafika na kuuzwa hapa, bali tunalipongeza kwa kuwa ndilo gazeti la kwanza "kufukua na kuanika" hadharani kero kubwa ambayo imekuwa ikitukabili sisi wakazi wa wilaya hii na vitongoji vyake.

Hatuna shaka kuwa hata Serikali imeona namna walala hoi tunavyokufa bila hata dalili za kuhudumiwa katika hospitali, zahanati na vituo vyetu vya afya.

Eti kigezo na mwamvuli unatumika kutukadamiza walala hoi, ni dhana hii ya uchangiaji matibatu. Hii imetoa mwanya kwa watumishi wa Idara ya afya wenye tamaa ya kujilimbikizia mali, wawachume wananchi wenye chochote na kuwaacha wasio na pesa ya kununua walau dagaa wasiokatwa vichwa wabaki wakifa kama kuku.

Kwa asili na labda basi tuseme kwa kadiri ya upeo mdogo tulionao sisi binafsi ni kwamba tunajua madaktari, manesi na wauguzi wa ngazi mbalimbali ni watu ambao si tu kwamba wanafanyakazi kujali wenzao, bali ni watu ambao wanatakiwa kutumia taaluma zao kuchochea utendaji na ufanisi wa WITO wao ambao ndio kitu muhimu kwanza kuwahudumia watu kwa upendo.

Kama wasomaji wengine watakubaliana na hoja hii, basi tunasimama kidete kusema kuwa Wauguzi wengi katika wilaya hii tangu manesi hadi madaktari ni watu wasio na WITO katika fani hiyo bali ni wanyanganyi wa pesa na uhai wa wanadamu wenzao kwa kutumia taaluma yao; wanajali mno pesa kuliko utu.

Ninasema hivyo maana karibu kila hospitali, zahanati au kituo cha afya chochote cha serikali katika mkoa huu hususani hapa Tarime, ukifika na mgojwa wako huduma ya msingi unayopewa ni "kunyang’anywa" visenti kidogo ulivyo navyo ambavyo pengine ungevitumia kununulia mgojwa ndizi, badala yake zinaanza kuchukuliwa toka mapokezi, nesi anayesukuma kitanda.

Sio hapo tu bali sasa hufika "wenyewe" wanaamua kukuandikia na kukuambia kuwa dawa au vifaa vinavyohitajika havipo; ;hospitali haina dawa; labda utoe pesa wakufatie mjini.

Hivi kweli manesi wa siku hizi wana roho ya kiungwana kiasi hicho? Lakini mbona ukitoa pesa hata nusu dakika haiishi dawa hazijapatikana? Au kila wadi ina duka lake la madawa?

Au basi tazama unaposema hauna chochote au unataka ukanunue mwenyewe wenzetu hao; wauguzi wetu, wanaolipwa kwa ajili yetu wanavyojenga chuki dhidi yako na hata hivyo ndio hao hao wanaokueleza ni duka gani ukanunue.

Maskini unafika duka, zahanati au hospitali hiyo unakuta kwamba ni mali ya nesi, au daktari mliyekuwa naye.

Anayedhani sisi wangapi wilayani hapa wasio na duka la madawa au hospitali hata wengine wasio na sifa za kuwa na vitu hivyo. Tunapenda kuiambia serikali kuwa hospitali za waganga hao binafsi na sio vinginevyo.

Kupitia gazeti hili ambalo sasa hapa Tarime tumeanza kuliita "MKOMBOZI WA WANYONGE" tunaishauri serikali walau badala ya kuchangia matibabu, basi iongeze kodi na ushuru mbalimbali utakaosaidia kuboresha huduma za afya kuliko kutumia njia hii ya sasa ambayo huwanufaisha wachache na kuwaua wengi.

Hata hivyo HONGERA, KIONGOZI TUOKOENI.

Wananchi wapenda haki.

Nyamisangura na Saba saba

S.L.P. 54

Tarime,

 

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere asipuuzwe

Ndugu Mhariri,

Kutokana na kichwa hapo juu ninaomba nafasi katika gazeti letu nitoe haya machache yanayonikereketa.

Mwalimu Nyerere ni Baba yetu hata tusipende. Jambo linalonisikitisha ni kupuuzwa na kumkashifu kuwa amepitwa na wakati. Huku wengine wakimwita kibaka. Jambo hili linadhihirisha kuondoa heshima ya nchi hii.

Baba wa Taifa ametutoa mbali na kulinda heshima ya nchi hii mpaka sasa Tanzania inaheshimika duniani.

Tunaomba waliokabidhiwa madaraka kulinda heshima ya nchi hii wakiongea maneno machafu yanayompuuzia Baba wa Taifa kama wao wamechoka kumheshimu sisi Watanzania tuli wengi bado tunamhitaji. Nafikiri hata hawa wanaopenda madaraka wakimpuuza hawatafanikiwa. Mtu yeyote asiyetaka ushauri na wasia wa wazazi hatafanikiwa; hata Mungu hapendi.

Tunaomba Mungu amsaidie na kumuongezea maisha ili atushauri.

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ni zawadi tuliyopewa kutoka kwa Mungu, tukiikosa tusitengemee kupata mtu wa namna hii.

Kwa hiyo hii ni bahati yetu Watanzania waitunze. Tutajuta baadaye kama hatukuitumia vizuri.

Napendekeza katika nyongeza nchi hii itungwe sheria ya kudumu ya kumheshimu rasmi kama Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ili iwe kumbukumbu kwa vizazi vijavyo waelewe hekima na busara ya baba huyu na waweze kujifunza busara zake.

Mzee Wilson Mhando,

Umba Liver Tours,

S.L.P. 16286

Dar es Salaam.