Zoezi la kukamata wenye leseni bandia lisiishie kwa madereva

KUANZIA wiki iliyopita,Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam limekuwa likiendesha operesheni maalum ya kukagua leseni za madereva wa magari ya abiria.

Katika zoezi hilo ambalo linapaswa kupongezwa zaidi ya madereva mia moja wamepatikana na leseni bandia. Kupatikana kwa madereva hao wenye leseni bandia ambao tunaamini idadi yao inaweza kuwa kubwa zaidi ni jambo la kutisha.

Tunasema ni jambo la kutisha kwa vile madereva hao wana dhamana kubwa ya kulinda uhai wa wananchi kulingana na hatari kubwa ya watu wengi kupoteza maisha endapo kanuni za usalama barabarani hazizingatiwi.

Hatuhitajiki kutoa mlolongo wa mifano ya ajali za barabarani nyingi zikiwa za hivi karibuni na zilizosababishwa na uzembe wa madereva,kwani hilo liko wazi kwa kila Mtanzania.

Lakini jambo muhimu ambalo tungependa kulipongeza kiujumla ni hatua ya Jeshi la Polisi kuona umuhimu wa kuendesha operesheni hii ya ukaguzi wa leseni.

Sambamba na pongezi hizo tengependa kutoa changamoto kidogo kuhusiana na zoezi hilo.

Kwanza uzoefu unaonyesha kuwa operesheni nyingi zinazofanywa hapa nchini zimekuwa katika mtindo wa hamaki.

Tunasema mtindo wa hamaki kwa vile zimekuwa zikiibuka mara baada ya tukio kubwa na hivyo inakuwa kana kwamba tukio hilo limewakurupusha wahusika kutoka usingizini.Kwa mfano zoezi hili la sasa limekuja baada ya ajali za mfululizo za hivi karibuni zilizopoteza maisha ya zaidi ya Watanzania 30.

Pili,zoezi lenyewe linaonekana kuwa ni la kutaka kuungusha mti kwa kukata matawi badala ya kukata mizizi na kun’goa shina lake.

Tunasema hivyo kwa vile kimsingi ukaguzi wa leseni kamwe halipaswi kuwa jambo la operesheni maalum bali operesheni ya kudumu au sehemu ya kazi za kila siku za askari wa usalama barabarani.

Kadhalika inaeleweka wazi kwamba wenye jukumu la kutoa leseni ni Jeshi la Polisi,na hivyo inapotokea kupatikana kwa wingi kwa leseni bandia Polisi hawawezi kukwepa kuwa watuhumiwa wa kwanza pia wa "dhambi"ya utoaji leseni bandia.

Sisi tunashauri kuwa ni vema madereva waliokwishapatikana na leseni hizo bandia wakabanwa zaidi ili waeleze walizipata wapi, kwa njia gani na kwa nani,jambo ambalo tunaamini litawaweka askari Polisi wengi matatani au wengi watagundulika kuwa wao ndio hasa watoaji wa leseni bandia.tu.

 

Tunaielekeza wapi jamii yetu kimaadili?

Ndugu Mhariri,

Naomba nami uniweke katika gazeti lako la KIONGOZI, kuelezea machache tu kuhusu jamii yetu kutokuwa na maadili mema kwa mwenyezi Mungu hasa kuanzia miaka ya sabini na kuendelea.

Nimejaribu sana kulinganisha maisha tuliyokuwa tunaishi na wazazi wetu nikiwa mdogo wa umri kati ya miaka mitano hadi miaka ishirini na tano (sasa nimevuka) na maisha ya vijana wa hivi sasa. Ukweli ni kwamba tabia na mienendo ni tofauti kabisa . kwa asilimia kubwa na ninaweza kusema kwamba wanaochangia sana uporomokaji wa maadili mema ni wazazi.

Wazazi wanachangia, walimu wa fani zote kuanzia shule za msingi hadi Chuo Kikuu nao wanachangia, bila kuwasahau walimu wa taasisi zingine na wageni kutoka nchi za nje.

Hapa ninajaribu kuelekeza kidogo jinsi watajwa wanavyochangia kuharibika kwa vijana wetu kitabia.

Wazazi: Mtoto anapozaliwa huishi na wazazi wake hadi utu uzima, yule mtoto kadri anavyokua anaiga matendo ya baba na mama yake na wale wanaomzunguka. Kadri ya uelewa wake, mtoto huamini kuwa wazazi na wale wote wanaomzunguka watendalo lolote ni jema na hivyo linafaa kuigwa. Hapa siwezi kuelezea zaidi, ila naomba sisi wazazi tufanye mambo mema na ndipo tutakapopata kizazi kijacho kizuri chenye tabia njema na kumfurahisha Mungu.

Serikali: Serikali inachangia kidogo katika kuharibika kwa tabia za watoto na hata za watu wazima kwa kuruhusu utamaduni wa nchi za nje, hasa nchi za magharibi kuingia na kutukuzwa bila kudhibitiwa, kama vile wanawake kuvaa nguo za ajabu ajabu kuonyesha sehemu zao za mwili na kadhalika.

Walimu: Ingawa sio wote, utakuta baadhi ya walimu wanadiriki kufanya mapenzi na wanafunzi wao (wake kwa waume). Mtoto hutoka nyumbani na kwenda shuleni na kurudi nyumbani kwa hiyo wazazi na walimu wanapaswa kuwa waangalifu sana katika malezi, kwa kuwa wote wana nafasi kubwa katika malezi ya watoto..

Taasisi zingine zinazoharibu tabia za watoto ni vyombo vya habari hasa magazeti na televisheni. Kwa kutangaza au kuonyesha habari za ajabu ajabu kwa nia tu ya kujipatia pesa, wamiliki wa vyombo vya habari wamekuwa wakichangia au kuchochea kuwa kiasi kikubwa mno upotofu wa maadili. Tunaomba wote kwa pamoja tumheshimu Mungu na kuomba toba tulee kizazi kijacho vizuri.Tujiulize hivi wazazi wetu wangetulea vibaya jinsi tunavyowalewa hawa watoto wetu wakati huu tungekuaje?

 

Ukatili wa Waganga, Wauguzi Tarime umetoa fundisho

Ndugu Mhariri,

Ninaomba nafasi katika gazeti lako la Kiongozi, ili nami niweze kueleza yangu mawazo.

Awali ya yote ningependa kuanza kwa kunukuu maneno ya marehemu Mariamu

( mliyeandika habari za kifo chake kwa sababu ya ukatili wa waganga hivi karibuni) ambayo aliyaacha wakati wake wa mwisho kabla hajaaga dunia. Habari ambayo niliisoma katika gazeti hili la Kiongozi toleo la Agosti 26 Septemba 3. Marehemu Mariamu alisema hivi:-'Manesi njooni mnisaidie jamani, nisaidinei ndugu zangu mie ni mwanamke wenzenu. Hata kama maishani sitawasaidia, basi mtasaidiwa na wengine jamani ...nawaombeni hata uji, njaa nayo inaniuma, aaa-aaa jamani. Basi kama mmeshindwa kabisa kunisaidia, kwa herini; tutaonana Mbinguni'.

Nimeona ninukuu maneno haya ya mwisho ya marehemu Mariamu ni kwa sababu yamenichoma sana moyo wakati ninasoma. Mateso na maneno ya Mariamu ninayafananisha na mateso na maneno ya Bwana Wetu Yesu Kristo msalabani, ambaye aliteseka na kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu.

Lakini Marehemu Mariamu aliteseka na kufa kutokana na jinsi wanadamu tulivyo wadhambi.

Hii inadhihirisha jinsi watu walivyo wadhambi kiasi kwamba upendo umehama kabisa na hata kufikia mahali ambapo mtu anaweza kumwacha binadamu mwenzake akiwa anakufa kama 'LIDUDU' huku akiwa na uwezo wa kumsaidia.

Hata wanyama hupendana na kusaidiana, lakini wanadamu tulioumbwa kwa mfano na sura ya Mungu tunaondoa sura hiyo na kuvaa sura ya madudu, ambayo hata majina yake bado hayajagunduliwa.Ndugu zangu, sipendi niseme sana hususan, jambo hili; maana ni suala ambalo liko wazi kwa kila mtu mwenye busara.

Ila ninalotaka kusema kwa ndugu zangu wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, kuanzia Mganga Mkuu mpaka mhudumu, wafanyakazi wote wa hospitali na zahanati kote nchini na watu wote kwa ujumla.

Maneno ya mwisho ya Marehemu Mariamu tuyachukue kama maneno ya maana na ni fundisho kwetu, kwa misingi hii;

Kwanza wajibu wa kila mtu ni kumpenda wenzake, na haki ya kila mtu ni kupendwa na wenzake. Pili unapaswa kuyaona makali ya mtu mwingine kuwa ni yako. Tatu; tuone njaa ya kutamani kuwaonyesha wenzetu upendo wa kweli, kutoka kwa binadamu wenzetu ambao tumeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Mwisho Marehemu Mariam ametutakia kheri wote tujitahidi kutenda haya yote kiukamilifu na kumpendeza Mungu ili tuweze kukutana naye mbinguni.

Tumsifu Yesu Kristu,

Eberhard A. Haule,

Jumuiya ya Mtakatifu Agnes,

Makete-Songea