Tusikose nidhamu ya muda

JAMBO kubwa sana linalokaziwa na kila mlezi na hata mzazi ni lile la kushika na kutunza muda. Ukweli huo tunaushuhudia hasa tunapoona katika taasisi mbalimbali kama vile shule, vyuo, katika mikutano, kitu chochote chenye kuwahusisha watu wengi ambacho kinachoweza kufanyika kwa ufanisi kama hakuna ratiba au utaratibu wa namna hiyo. Katika ratiba hizo wahusika hufahamisha jambo gani litafanyika muda gani kwa muda gani. Ratiba hutueleza ni lini jambo fulani lianze na lini lifikie mwisho wake..

Licha ya ratiba za kishule na mikutano, kuna pia ratiba za utendaji wa kila siku. Hapo kunakuwa na muda wa kuamka, muda wa kupata kifungua kinywa, muda wa kuanza kazi, muda wa kupata chakula cha mchana, muda wa kufunga kazi, muda wa kula chakula cha jioni na muda wa mapumziko ya jioni. Kisha kunakuwa na muda wa kula chakula cha jioni na muda wa kwenda kulala. Ratiba kama hizo huwa ni za mtu binafsi, lakini pia ni kwa ajili ya watu wanaoishi pamoja, ili mradi wote hao hujitafutia ufanisi wa shughuli zao na pia ili kuweza kuwa na utendaji mzuri wakazi zao.

Ili kuweza kufanikisha shughuli hata zile za usafiri, basi mtu hujipangia muda wa kuanza safari yake akitegemea ni wapi anakokwenda, na huko atatumia muda gani. Hivyo pia kuna ratiba za safari kwa vyombo vya usafiri, kama vile mabasi, ndege, meli, na magari moshi. Kwa kawaida kila msafiri hupenda kufika kule anakotaka kwenda kwa wakati wake na kuzifanya zile shughuli anazoziendea kwa muda unaotakiwa.. Ni jambo la kusikitisha sana kuona mtu anachelewa kuondoka mahali na pia anachelewa kufika mahali anapotakiwa kufika.

Tatizo la uchelewaji linaleta madhara makubwa sana katika utendaji na pia husababisha majanga mengi sana katika jamii yetu. Kumekuwa na matatizo mengi katika jamii yetu kutokana na watu kutokushika ratiba zao.Imewahi kutokea kwamba mhusika fulani akaahidi kwamba atawasili mahali fulani kwa ajili ya shughuli fulani. Kwa bahati mbaya anachelewa kushika muda huo na baadaye anajitetea kwa kusema "kwa sababu zisizozuilika" tumechelewa. Kusema kweli hapo kunakuwa tayari ni ukosefu wa utendaji. kwani tuunasema kuwa muda ni mali.

Mara nyingi sana ikiwa mtu amechelewa kuanza shughuli kwa muda wake basi jambo litakalotokea ni kwamba au shughuli hiyo itafanyika haraka haraka, au pengine haitafanyika kabisa na kusababisha hasara kubwa sana. Mambo yanakuwa mabaya hasa ikiwa mtu amechelewa kuanza safari yake. Kuna madreva wengi ambao huchelewa kuanza safari zao na hivyo badala ya kwenda kwa mwendo mzuri, hapo wanakimbiza sana vyombo ili kulipizia muda waliochelewa. Mapato yake ni kwamba safari inakuwa ni ya wasiwasi na husababisha ajali.

Tungependa kutamka wazi kuwa ajali nyingi sana hutokea kwa sababu watu wahusika hasa madreva hawataki kushika ratiba zao. Ingawaje, hasa kwa siku hizi mabasi yamepangiwa ratiba ya kuondoka mahali na kufika wanapotakiwa wafike, jambo la kushangaza ni kule kuona mabasi mengi yanawahi au yanachelewa, na yakichelewa madreva huwa katika mwendo mkali sana na hivyo kusababisha ajali. Kuna ukosefu mkubwa sana wa nidhamu za ratiba katika utendaji. Jambo hilo siyo kwa madreva wa mabasi tu, bali hata kwa madreva wa magari ya watu binafsi. Mara nyingi wanapenda kufika mahali kwa wakati fulani, lakini huwa wanachelewa kuondoka, na hivyo huwa na mwendo mkali sana na hapo kusababisha ajali zenye kupoteza maisha ya watu na mali zao.

Tabia ya kuchelewa au kutoshika ratiba nbi mbaya sana katika maisha ya jamii na hasa pale ambapo watu wengi wanafanya kazi pamoja. Mtu mstaarabu kwa kawaida hutunza muda. Lakini inasikitisha sana kuona jinsi watu wengi walivyo wazembe katika kushika muda au ratiba zao za utendaji. Tumekuwa hatuna maendeleo katika taifa letu kutokana na kutokuwa na nidhamu katika utendaji wetu. Kama ilivyo katika kuchelewa tuanzapo safari zetu, hivyo pia kuna uchelewaji katika utendaji wetu. Wengi wa wananchi hawatekelezi majukumu yao iwe ni katika maofisi au katika viwanda na taasisi mbalimbali katika jamii kwa wakati wake kwa kuwa ratiba hazishikwi. Kuna kuchelewa sana kwa utekelezaji wa shughuli kwa vile hakuna ratiba zinazofuatwa.

Ukosefu wa kufuata ratiba siyo tu katika shughuli za kiofisi bali pia hata kwa wenzetu wakulima. Mkulima kama mkulima hana budi kufuata ratiba katika utendaji wake ili kuwza kuleta mafanikio katika kazi yake. Wako wakulima wengi ambao hawana ratiba kabisa katika utendaji wao wa shughuli hizo za kilimo. Mapato yake ni kwamba kunakuwa na uzalishaji hafifu. Kwa mfano hawaandai mashamba yao kwa wakati wake, na hivyo mvua zinapofika hufanya mambo kwa haraka na hivyo kuwa na ufanisi mdogo sana katika kazi hiyo ya kilimo.

Kama tulivyosema hapo juu, ni kwamba desturi ya kutokuwa na ratiba, au kuwa na ratiba ambayo haifuatwi, husababisha ufanisi duni na kurudisha maendeleo ya jamii. Kutokufuata ratiba huleta fujo katika utendaji na pia kusababisha hasara kubwa sana katika jamii. Kwa hiyo tukitaka kupunguza ajali katika nchi yetu, hatuna budi kuwa na madreva wanaoshika ratiba. Tukitaka kufanikiwa katika mikutano na malezi yetu, ni lazima katenda kwa kufuata ratiba za utendaji

Daima tunapaswa kutenda kila kitu kwa wakati wake. Ikiwa tutafanya kazi zetu bila kuwa na nidhamu ya kushika ratiba na saa za utendaji, basi mambo yetu yatazidi kuwa mabaya na yasiyo na mafanikio halisi. Hapo tunapaswa kabisa kuwaiga hao wenzetu waliostaarabika kwani daima wanashika muda na ratiba. Kutokushika muda na ratiba kunaleta wasiwasi wa ustaarabu wetu.kwani hali hiyo hurudisha nyuma mafanikio ya utendaji wetu. Tuwe na nidhamu ya kushika ratiba pia tuwe na mipango ya utendaji wetu ili kuweza kufanikiwa katika huduma na utendaji wa kila siku.

 

Wakatoliki tujirudi kiimani

Mhariri,

(KATIKA toleO lililopita kichwa cha habari cha barua hii kilikosewa na kusomeka "Wakatoliki turudi nyuma kiimani" badala ya usahihi wake kama inavyosomeka hapo juu. Kwa sababu hiyo tunairudia barua hii ili kuondoa utata uliojitokeza na tunaomba radhi kwa usumbufu wowote kwa yeyote).

Naomba tena nafasi ndogo katika gazeti hili letu tukufu la KIONGOZI linaloongoza na hali mengine yananyemelea nyuma .

Kutamka ukweli mtupu na kujaribu kujiweka wazi ni kwamba sisi Wakristo wapendwa Wakatoliki kwa njia moja au nyingine tumelegea katika kuitangaza imani yetu.

Kwa mafikira yangu binafsi na pia kwa maono yangu binafsi, naona hii imesababishwa na wingu kubwa linalotukumba la kuibuka kwa makanisa mengi ulimwenguni hususani ya Kilokole.

Makanisa au madhehebu haya yanatofautiana katika imani zao na taratibu zao za ibada na hii ndugu Mkristo isikuchanganye, kwa vile hii ni hesabu rahisi kwani baada ya kujumlisha makanisa haya mengi na imani zao, kule mbele jibu litakuwa "Tunamwabudu Mungu Mmoja bali kwa njia tofauti" . Wakatoliki nawasihi tuwe na msimamo mmoja na madhubuti tuitangaze imani yetu bila kuogopeshwa na madhehebu haya mengine.

Mahudhurio katika makanisa yetu ni ya kiwango cha juu sana, lakini Je, imani yetu ipo juu vile vile ?

Kama jibu ni "ndio" sawa, maana kila mmoja wetu atapiga goti mbele ya Kristo na kujikitetea mwenyewe .

Acha niwe muwazi, moja ya mabo yanayoturudisha nyuma tushindwe kuisukuma imani yetu mbele ni kutojali.

Tukiwa kanisani kuna Neno la Mungu kwa hiyo basi linaposomwa inabidi tuwe makini sana katika kusikiliza Neno hili Takatifu, tuwe watulivu na adabu iwe inatawala mioyo na akili zetu. Lakini utaona wengi wetu tumekaa wengine wanasinzia kanisani, watoto wanalia na kucheza ovyo wengine wanawaza mbali kana kwamba wanasikiliza tu.

Sana sana wanakumbuka kunena "TUMSHUKURU MUNGU" au "SIFA KWAKO EE BWANA" maana haya ni maneno tuliyozoea na hayahitaji kufikiria chochote .

Baada ya misa tukijaribu kuulizana maswali kwa ajili ya kutafakari Neno la Mungu kwa siku ya hiyo, wengi hawakumbuki hata neno moja, lakini sote tumekuja kanisani na tunatoa sadaka na kuipokea Sakramenti Takatifu.

Jamani wenzangu Wakatoliki tujirudi tena tuitetee imani yetu na tuiangalie tumetoka wapi na tunakwenda wapi Kikristo na tutembee pamoja Kiimani kama vile Sinodi yetu inavyotuelekeza katika Ukombozi wa Kiroho.

Upande wa sadaka nao kuna vichekesho.

Sadaka ni zawadi unayoipeleka Altareni ili kumshukuru Bwana Mungu aliyetupa sisi tulicho nacho na bila sadaka hii hatungesali katika nyumba na wala hatungeweza kupata huduma tuzipatazo kutoka kwa viongozi wetu mapadre maaskofu ,masista, na kadhaalika.

Kwa hiyo tusiangalie wingi wa watu na wingi wa sadaka zetu, tujichuinguze wenyewe na tujue tutatoa kiwango gani. Kitendo cha kutoa sh 10/= au 20/= hata 50/= mtu mzima ni aibu. Kumbuka kuwa Kristo anakuona mpaka moyoni mwako.

Jamani hata sh. 100 ni kidogo, afadhali tutoe kwa moyo na Mungu atatuzidishia. Nawatakieni au tutakiane kheri na baraka za Mungu na tusiwe waoga katika kuikiri na kuungama IMANI yetu siku zote, mahali popote na muda wowote! Barikiweni sana Ndugu zangu.

Ni mimi mwenzenu,

Valery A. Mrema.

Box 3622

Dar es Salaam.