KAULI

Je Tutafika kwa kutumia njia za mkato

Wakati nchi yetu ilipojipatia Uhuru kulikuwa na misemo mbalimbali ambayo ilikuwa ikitukumbusha kuhusu wajibu wetu baada ya kujitawala. Kulikuwa na misemo kama vile:"Uhuru na Kazi, au Uhuru ni Kazi , au tukaambiwa Kazi ni uhai au pia Nguvu Kazi na kadhalika."

Misemo hiyo yote ilikuwa na maana ya kutuhimiza ili tuweze kwenda mbele katika maendeleo ya nchi yetu hii baada ya kujipatia Uhuru wetu.

Neno kubwa hasa ni kwamba hatuwezi kamwe kuendelea bila kufanya kazi kwa bidii. Tunapaswa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Na ndiyo maana katika maisha ya kawaida tunasema kuwa "Kazi ni Uhai", kwani bila kufanya kazi binadamu hawezi akajipatia riziki yake yenye kumfanya aweze kuishi na raha na pia yenye uadilifu na uaminifu katika jamii iwayo yote ile.

Tunasoma katika Kitabu Kitakatifu kuwa Mwenyezi Mungu kumwumba mtu na alimwamuru afanye kazi ya kuutunza ulimwengu wote. Tunasoma hivi: "Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwuumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba akawambia zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi."(Mwanzo 1:28) .

Mungu anaposema kuwa binadamu awe mtawala maana yake yake ni kwamba anatakiwa kufanya kazi . Binadamu hawezi kuwa mtawala ikiwa hafanyi kazi.Mtawala kama mtawala sharti afanye kazi, tena kwa bidii.

Mtume Paulo anapowaandikia Ndugu Watesalonike anawaambia waziwazi kuhusu amri ya kufanya kazi. Anasema hivi ":......ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile." (2Watesalonike 3:10) .W ako wananchi ambao wanaishi kwa kuwategemea ndugu zao tu bila kufanya kazi. Watu wa namna hiyo tuliwaita hapo zamani ni "wanyonyaji wa jasho la watu wengine".

Vitendo vinavyotokea siku ya leo hapa na pale kama vile kuvuja na kuibiwa mitihani hutokana hasa na ile tabia na hali ya uvivu kwa wanafunzi wetu na watu wengine ambao wanahusika katika vitendo hivyo viovu.

Hivyo pia hutokea mahali mbalimbali ambapo watu hawataki kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu. Vijana wetu wengi wanataka kuwa na mambo mawili kwa wakati mmoja, yaani starehe na masomo.

Kwa kuwa wanataka kufaulu katika masomo yao na papo hapo hawakuweza kusoma ipasavyo basi huchukua njia ya mkato ya kununua mitihani . Na wako wafanya kazi wengine, kwa kuwa hawafanyi kazi kwa bidii, hawawezi kuzalisha kiasi cha kutosha na hivyo mishahara yao hubakia ya chini.

Tunapenda kutamka tena katika Kauli Yetu hii kwamba Watanzania hatutaweza kufika huko tunakotaka kwenda kama hatupendi kufanya kazi. Tunapaswa kufanya kazi kwa bidii na pia kwa uadilifu ili tuweze kuleta maendeleo ya kweli katika nchi yetu hii. Pia tunapaswa kuacha tabia na mtindo wa kuwaegemea ndugu, jamaa na hata marafiki.

TUNAONA inatupasa kuyarudia tena yale maneno ambayo yalikuwa yanatamkwa na wale katika kuwafanya wale wavivu wafanye kazi ya kuzalisha na kujitegemea katika maisha yao viongozi wetu wa siasa wakati ule:"USIWE KUPE, UJITEGEMEE" Ni maneno ya kuudhi, lakini papo hapo tunaona kuwa yatasaisdia sana.