Je ujamaa wetu umekufa kabisa?

 

MARA baada ya nchi yetu kujipatia Uhuru, tulijitangazia kuwa mtindo wa siasa yetu ya kila siku utakuwa ni wa "Ujamaa na Kujitegemea". Msingi wa siasa hiyo ulikuwa ni kutokana hasa na utamaduni wetu wa siku nyingi.

Utamaduni wetu wa kiafirika ulikuwa ni katika kuishi pamoja, kusaidiana katika shughuli ambalimbali za maisha ya kila siku. Wazee wetu wanatuambia kuwa maisha ya pamoja yalikuwa ni katika kufanya kazi kwa pamoja na pia katika kusaidiana ikiwa kulitokea shida au tatizo lo lote lile.

Kwa hiyo kila mmoja katika jamii alionekana kuwa na maana na pia kutoa mchango wake popote pale alipotakiwa kufanya hivyo. Mtindo huo wa maisha ulikuwa na faida zake na ndiyo maana ukawa umezingatiwa kabisa na kila mwana jamii..

Lakini kutokana na mabaadilikko katika jamii yetu , kama vile mabadiliko ya kisiasa, mabadiliko ya kiuchumi, na hata mabadiliko ya kimaendeleo, imeonekana kuwa haiwezekani kabisa watu wakaishi kwa mtindo huo.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa ujamaa kama ulivyokuwa hapo awali hauwezi ukadumu katika zama zetu hizi. Lakini pia hatuwezi tukaaacha zile tunu za msingi zilizokuwemo ndani ya ule ujamaa wa wazee wetu.Kulikuwa na mambo mengi sana mazuri ambayo tunapaswa kuyafuata.

Moja ya tunu ambayo ilikuwa ni ya msingi kabisa katika utamaduni wetu wa Kiafrika ni ule moyo wa kusaidiana katika shida na matatizo mbalimbali. Hapo tunaweza kusema kuwa hiyo ni kweli tunu ambayo hata sisi siku ya leo tunaihitaji sana kuienzi.

Tunavyofahamu hakuna mtu asiyepatikana na shida yo yote ile na wakati wo wote ule. Kwanza tukumbuke kuwa hakuna binadamu ambaye anajitosheleza katika maisha yake ya kila siku. Na pili binadamu anao maadui wengi, iwe ni wanyama, hali mbaya ya hewa na hata binadamu mwenzake.

Hapo kusema kweli huhitaji msaada kutoka kwa binadamu mwenzake , na hasa kwa yule ambaye yuko karibu yake, yaani jirani. Kila siku hatukosi kusikia juu ya watu wanaopatwa na matatizo ya hapa na pale. Daima tunasikia kuhusu uombaji wa misaada, iwe ni kwa upande wa serikali, au kutoka mashirika ya dini na yale ya hiari.Mara nyingi uwezo wa binadamu huwa mdogo sana ukilinganishwa na mahitaji yake.

Lakini jambo la kushangaza pengine ni kule kushuhudia jinsi watu wanavyokaa kimya wakati mwenzao anapokabiliwa na shida fulani. Kwa mfano hivi majuzi nilishuhudia jinsi watu waliokuwa ndani ya Daladala wakimwangalia mama mmoja ambaye alikuwa akiporwa mkufu wake na vibaka. Wote katika gari walikuwa wameinamisha vichwa vyao na wala hawakutaka kumsaidia yule mama.

Hapo tunaweza kusema kuwa ule moyo wa asili na wa jadi yetu wa kusaidiana katika shida umekufa. Lakini pia huwa inaleta faraja kama nilivyoshuhudia siku moja jinsi jamaa walivyoweza kumsaidia na kumwokoa na majambazi waliokuwa wanataka kupora mali yake. Hao tunasema kuwa wana ule moyo wa kijamaa.moyo wa kizalendo.

Tunu yetu hii ya kusaidiana hujionyesha kwanza kabisa tunapokuwa tayari kusalimiana na wenzetu mara tukutanapo nao. Watu ambao wamesalimiana na kutakiana hali hawawezi kamwe kuacha kusaidiana shida inapotokea. Tendo la kusalimiana hujenga ule msingi wa udugu na hivyo kuwa tayari kukabili matatizo kwa pamoja.

Tunapenda kutamka katika Kauli Yetu hii kuwa tudumishe ule utamaduni wetu wa asili wa kusaidiana katika shiida na matatizo, licha ya ugumu wa maisha kiuchumi, kisiasa, kidini, kiitikadi na kadhalika.Tukumbuke kuwa binadamu ni kiumbe mwenye kupenda kumsaidia mwenzake ikiwa hakuingiliwa na roho mbaya..

 

Ugombea binafsi hautaumba Mungu Mtu

Mheshimiwa Mhariri

KAULI ya Waziri Mkuu Mhe. Fredrick Sumaye katika ziara yake kutembelea Mkoa wa Dar es Salaam hivi karibuni kuwa Serikali haitaruhusu ugombea binafsi kwa sababu eti utazaa Mungu Mtu! Mimi sikubaliani nayo.

Kauli na mawazo kama haya kwa kweli ni kikwazo cha maendeleo Tanzania. Maendeleo yatapatikana tu iwapo viongozi watakuwa wawazi na wa kweli, wajikane wenyewe, waondoe ubinafi na ushabiki wa kichama na waweke mbele maslahi ya wananchi kwa kujali ushindani wa haki.

Ushindani wa haki utazaa viongozi wawajibikaji kwani wataelewa fika kwamba fagio la uchaguzi ni la haki. Kama hiyo ndiyo filosofia iliyo mbele ya serikali na ndiyo iliyotoa "White paper" basi hakutatokea mabadiliko ya kisiasa nchini wala ya kiuchumi wala ya kiteknolojia.

Bado tuko katika minyororo ya utumwa wa kisiasa na mizengwe ya kulindana na kupanga matokeo ya uchaguzi. Hakika maendeleo ya uchumi wetu na kila kitu aslani vimefungwa na siasa za woga na hila.

Ushindani wa kweli utaleta maendeleo haraka, hakuna kuleana; wananchi wanachotaka ndicho kinakuwa kwa sasa sivyo!

Kauli hiyo ya Mh. Waziri Mkuu ina maana kubwa Mbili:

Kwanza ni kwamba katiba ya sasa inampa madaraka makubwa sana Rais kiasi kuwa anaweza kujigeuza Mungu mtu na uungu huo hautakiwi aupate mtu mwingine yeyote asiye CCM. Aidha watu wa CCM ni warahimu sana wanaojali wanyonge kiasi kwamba hawawezi kujigeuza Miungu watu!

Hofu kwamba huo uungu unaweza kutumiwa vibaya na watu wa kuja katika madaraka ya Tanzania ni dhana potofu! Kwa haraka haraka ni kwamba hapa demokrasia hakuna ila kudanganyana tu. CCM mradi walitangulia na wameshika mpini kwa hiyo wananchi, maendeleo pamoja na wapinzani hawana chao nchini. Na pengine hata Tume ya Uchaguzi inaelekea ipo kwa maslahi ya CCM, ni kichaka wanachojificha CCM kwa faida yao binafsi.

Ieleweke wazi kwamba mchezo huo ni mbaya sana na hauwapi wananchi uwezo wa kuchagua viongozi wawapendao. Siku wengi wakielewa hila za uchaguzi ndiyo mwanzo wa machafuko. Basi ili asipatikane Mungu mtu bora iandikwe katiba mpya itakayoweka wazi madaraka ya Rais yasiyo ya kimungu mtu. nani anastahili kuiandika katiba mpya?

Ni wasomi wetu, wawakilishi wa jumuiya za wananchi kama TFTU, Washirika, Tughe nk. Na katiba mpya ipitishwe na wananchi. Bunge kazi yake ni kutunga sheria kutumia hiyo katiba wala si kubadilisha chochote.

Wananchi si wajinga kwamba hawawezi kutambua pumba na mchele. Kwamba eti wanaweza kudanganywa na mgombea binafsi wakamchagua!

Ieleweke wazi kwamba mgombea binafsi ni mtu wetu, anajua tulipokwama, ana sera zake lakini hatafanya kazi peke yake. Ieleweke pia kwamba hata hiyo katiba ya sasa ya nchi si ajabu ukute ni ya ubunifu wa mtu mmoja tu na wengine wameipitisha tu au pengine wameongeza marekebisho madogo sana.

Mambo ya uongozi bwana lazima kuna kinara wa mawazo kwa hiyo tusiogope mgombea binafsi cha kujali ni kutunga katiba na sheria za kutulinda dhidi ya Umungu mtu kuliko kumzuia mwenye uwezo asiende mbele za watu kujinadi.

Tuwaamini wananchi wetu, wao si wajinga au vipi! Au tuseme CCM inanufaika na ujinga wao? Kwa kweli lihalali katiba ni ya wananchi wa Bunge linaitumia tu kutunga sheria na siyo kubadilisha chochote. Pia wanaoweza kubadilisha katiba ni wananchi kwa kutumia jumuiya zao kama nilivyosema awali. Sasa hivi CCM inajivunia bunge kwa vile wengi ni wake na wanapiga kura kwa ushabiki tu si kwa hoja. Viongozi tafadhalini fanyeni kitu ili hata miaka mia ijayo watu waje waone uongozi wenu haukuwa wa ghilba kwa wananchi wetu bali ulilenga haki.

Wanaonufaika na utawala huu sasa wanakimbiza watoto wao kusoma nje, wanatibiwa nje nk. badala ya kuendeleza nyumbani kwao. Viongozi wamekuwa kama wakimbizi katika nchi yao wenyewe. Nionavyo "white paper" ni mlolongo ule ule wa ghilba za kale ambazo si kwa manufaa ya wananchi bali ni kwa manufaa ya wachache walioshika hatamu.

Himili Chibwana

Box 796,

Dar es salaam.

 

Ujumbe wangu kwa Mapadre

Mheshimiwa Mhariri

MAPADRE wangu na watumishi wa Mungu katika watu, tambueni huruma ya Mungu na upendo wake kwenu.

Tazama Mungu amewachague ninyi kutoka kwa watu ili mmtumikie yeye na mwatumikie watu wake na mwisho muwafikishe kwake katika makao ya milele.

Ingawa mwaenda kinyume, yeye anabaki kuwatunza na kuwahurumia. Jueni kwamba Mungu amewachagua ninyi si ninyi mlio mchagua. Basi kwa kutambua hilo endeleeni katika utumishi wenu. Endeleeni kuwa na motomoto wa utumishi na utoaji wa huduma.

Kuweni wazi mpate kuwa huru katika utumishi wenu. Muombeni Mungu neema zake awaongoze katika safari yenu ya ukombozi.

Useja wenu uwasaidie kuwa wahudumu safi na wapenzi wa Mama kanisa na jumuiya ya wakristo wake. Msiwe watumwa wa malimwengu bali yatumieni kwa ajili ya kujiandalia ufalme wa mbinguni.

Kumbukeni kuwa ni vigumu kutambuliwa na watu bali ni kazi yenu kujitambulisha kwao kwa matendo na huduma zenu.Waombeni kwa Mungu watu wote wanaowazushia uongo. Kesheni katika sala ili mpate nguvu mpya katika imani. Waombeni wenzenu waliojitenga na kulegea ili warudi tena katika jamii yenu.

Mwisho fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu.Baada ya hayo semeni sisi ni watumishi tusio na faida.

WATAWA:

Ninyi ni chumvi na nuru ya dunia. Kolezeni kwa chumvi yenu, pia angazeni kwa mwanga wenu ili dunia ipate kumjua Mungu.

Jiepusheni na yale yote yawezayo kurudisha nyuma au kuvuruga wito wenu. Kumbukeni kuwa ninyi ni viumbe viteule kwa ajili ya kazi ya ukombozi. Kwa hilo basi jitahidini kuwa safi rohoni na mwilini.

Maisha yenu yatawaliwe na Kristo. Mkaribisheni Kristo mioyoni mwenu. Waombeeni wote wanao wadhulumu pia watakieni amani adui zenu. Lisafishe na kulipamba kanisa kwa matendo yenu safi.

Ombeni ili dunia ipate amani na watu wote wamjue Mungu na Injili ienee duniani kote. Kuweni huru na wazi mbele ya Mungu ili mpate kuwa safi na huru katika utumishi wenu.

Tambueni kuwa maisha mliyoyachagua yanapingana na maisha ya hapa duniani. Basi ishini kama wageni na wasafiri. Fikirini zaidi zaidi juu ya maisha ya milele mpate kuwapeleka watu kwenye maisha ya milele. Nanyi pia jiandaeni kwa maisha ya milele.

Fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu na mwisho semeni sisi ni watumishi tusio na faida.

Hayo ndiyo ninayowatakie katika uchungaji. Jipeni moyo Mungu yupo pamoja nanyi.

WALEI

Enyi ndugu zangu walei popote pale mlipo katika maisha yenu ya kila siku. Salaam katika upendo wa Bwana.

Nawaleteeni ujumbe huu nikisema: Tazameni kanisa la Mungu kwa upendo na unyenyekevu, tafakarini huruma ya Mungu juu yetu wanadamu.

Kuweni watu waaminifu katika maisha yenu, timizeni nyajibu zenu kwa manufaa ya jamii nzima na kanisa kwa ujumla. Walio na vyeo wateteeni wanyonge. Kuweni viongozi msiwe watawala, mtangulize Kristo katika yote na popote katika shughuli zenu.

Wapendeni na waombeeni watumishi na viongozi wa kanisa. Msitangaze mapungufu na matatizo yao bali watakieni uvumilivu katika mahangaiko yao.Wapeni moyo pale wanapolegea. Mshirikiane nao katika uchungaji wao ili kanisa la Mungu lipate kusitawi na kuendelea katika kumjua na kumpenda Mungu.

Zaidi ya hayo nawatakieni moyo wa unyenyekevu na utumishi mwema katika shamba la Bwana. Hayo ndiyo maneno yangu kwenu ninyi taifa la Mungu.

Silvia S. Bukombe

Songea,

Ruvuma