Jamii iadabishe watoto

MARA nyingi katika matoleo ya gazeti letu hili yaliyopita tumekuwa tukiandika kuhusu maadili na hasa nidhamu kwa vijana wetu. Tumekuwa tukiandika na kushauri kuhusu kuporomoka kwa maadili na nidhamu kwa vijana, hasa wale wanaosoma suhle za sekondari.

Kumekuwa na matukio kadhaa ya aibu kama vile wanafunzi kuwapiga walimu wao na hata kuharibu mali za shule na hata za watu binafsi.

Hivi karibujni huko Bagamoyo kumetokea tena jambo la aibu. Kama ilivyoripotiwa katika Gazeti la Alasiri la Ijumaa, Oktoba 30, 1998, wanafunzi 120 wametimuliwa kutoka shule ya sekondari ya Wavulana.

Alasiri lilieleza kuwa kwa kadiri ya maelezo yaliyotolewa na Mkuu wa Shule hiyo ya sekondari ya wavulana huko Bagamoyo Ndugu Peter Naali, wanafunzi hao walianza kugoma kuingia madarasani kwa madai kuwa hawakuridhika na uamuzi wa uongozi wa shule, uamuzi huo ulihusu kumpa cheo cha Ukaka wa shule mwenzao wasiyemtaka anayejulikana kwa jina la Yohana Mkindo.

Mkuu huyo wa shule aliendelea kueleza kuwa wanafunzi hao ambao ni wa kidato cha pili na cha tatu walivamia majengo na kuyavunja vunja , walivunja nyumba za walimu, maabara ya shule, wakatupa tupa vitabu na kusambaratisha maduka kadhaa ya watu binafsi yaliyo jirani na shule.

Bwana Naali aliendelea kusema kuwa wengine walikuwa wakiendelea kuwafurumusha wenzao waliokuwa madarasani kwa mawe na bakora ili watoke nje na kuwunga mkono.

Tunasema tukio hilo ni la aibu sana. Ni kitendo cha ukosefu wa malezi bora.

Kijana anayeamua kuharibu mali ya shule, mali ya umma na hata ya watu wengine tunamwita ni mharibifu.

Lakini uharibifu wa namna hiyo ni mtu mwenye kichaa. tunajiuliza ni kwa nini vijana wetu wanaamua kufanya vitendo vichafu hivyo? Tunatarajia kuwa kijana ambaye yuko katika kidato cha pili au cha tatu ni mwenye akili na busara ya kutosha.

Kwa kawaida katika shule kuna mabaraza ya wanafunzi na pia walimu wanapaswa kuwa karibu kabisa na wanafunzi. Tulisema hapo awali katika maoni yetu kuwa walimu wetu wawe ni kweli walezi na si wagawaji wa maarifa tu. Inatakiwa kuweko na ukaribu kati ya wanafunzi na walimu katika tukio hilo na pia matukio mengine ya namna hiyo tunaweza kuhisi kuwa vijana wanakosa ushauri wa walimu wao kama walezi wao.

Kwa upande wa wanafunzi tunasikitika kusema kuwa tabia zao zilivyo zinatukatisha tamaa mno. Hao vijana ambao tunaambiwa ni tegemeo la taifa kwa sasa hivi na hapo baadaye. Ikiwa wanakuwa na hasira za uharibifu, watakuwa kweli tegemeo katika taifa.

Vijana wetu wanaosoma katika shule za sekondari siku ya leo ni wale ambao wamepata malezi kutoka shule za chekechea. shule za msingi na katika hizo sekondari.

Tunaamini kuwa katika malezi hao walijifunza na kuzoeshwa kutunza vitu na vifaa mbali mbali. Na siyo huko shuleni tu bali hata kule nyumbani kwao kwa wazazi walifundishwa kutunza mali ya nyumbani. Mambo ya uharibifu yanapotokea huko mashuleni tunayashangaa kwani yanatukatisha tamaa.

Wenzetu walioendelea wanajivunia vitu vilivyodumu muda mrefu. Ukienda huko Ulaya utashuhudia zile meza, vitabu, majumba ya shule na vitu vingine vya zamani, vilivyotumiwa na watu maarufu,. Kuna mambo mengi ya zamani yanayotunzwa vizuri vikiwa na ukumbusho mzuri.

Lakini hali iliyo kwetu sisi ni vigumu kuamini kama tutakuwa na mambo mazuri ya ukombozi katika nchi yetu ikiwa vijana wetu wana tabia ya uharibifu. Wataalamu hutuambia "Old is Gold", maana yake "Kitu cha zamani ni kama vile dhahabu".

Tunapenda kutoa rai yetu tena kuwa tujenge na kudumisha ule utamaduni wa kutunza vitu. Ni jukumu la walezi wote na pia walelewa wote kuzingatia utunzaji wa vitu tulivyo navyo kwani uchumi wetu ni dhaifu mno. Tuone fahari juu ya vitu tulivyovirithi kutoka kwa wale waliotutangulia.