Mafanikio hutegemea mazoezi

BINADAMU huwa tunatofautiana sana katika utendaji wetu. Mafanikio yetu katika utendaji hutegemea sana uzoefu katika jambo hilo tunalolitenda.

Ili tuweze kuwa na uzoefu katika utendaji wa jambo lolote lile tunapaswa kufanya mazoezi mengi na ya muda mrefu.

Kinyume chake lakini, wengi wetu hatuna uzoefu katika mambo yale tunayotenda na hivyo hakuna mafanikio mazuri.

Kuna mambo mengi yanayohitaji mazoezi. Tukitaka kuimba kwa ufanisi na kwa ufundi tunahitaji kufanya mazoezi. Mambo ndivyo yalivyo katika taaluma zote na hata michezo mbali mbali.

Kwa mfano sisi Watanzania tumekuwa tukishindwa sana katika mashindano ya michezo. Sababu kubwa ni ile ya kutokuwa na uzoefu katika michezo. Uzoefu huo unakosekana kwa sababu hatuna mazoezi ya kutosha na ya muda mrefu. Mazoezi kama mazoezi yanapaswa kuwa ya muda mrefu. Wenzetu walioendelea husema kuwa "mazoezi hufanya kitu kiwe kikamilifu"

Mwenye kufanya mazoezi baadaye huwa na mazoea katika jambo hilo alilolifanyia mazoezi. Hapo huitenda hata bila kufikiri kwa kuwa vionjo, akili na mwili mzima vimekwishazoea vina uzoefu.

Kwa kawaida mazoezi ni matendo yanayofanyika kwa kurudiarudia na mpaka huwa ni sehemu ya mwili. Hapo tunasema kuwa tendo fulani limo damuni. Mazoezi kama mazoezi hufanywa kwa mfululizo bila kukatiza katiza.

Mambo ndivyo yalivyo hata huko mashuleni. Watoto wanaojifunza kusoma na kuandika hufanya mazoezi ya kusoma na kuandika siyo kwa siku moja tu, bali kwa siku nyingi na hata miaka mingi. Pia wale wanaojifunza mambo ya fani katika madarasa ya jua, nao hufanya mazoezi mengi. Kila mwalimu kwa kawaida huwa makini sana katika kuwapa wanafunzi wake mazoezi mbalimbali ili wapate uzoefu katika somo hilo.

Ufanisi katika masomo na taaluma mbali mbali hutegemea sana jinsi wanafunzi wanavyozingatia mazoezi ili kujipatia uzoefu. Wakufunzi mara kwa mara hutoa mazoezi yanayojulikana kama "Home work" yaani kazi za kufanya nyumbani muda baada ya masomo.

Yule anayetaka kufahamu lugha ya kigeni hana budi pia kufanya mazoezi ya kusoma, kuandika na hasa kuzungumza lugha hiyo. Anapaswa kufanya jitihada ya kufanya mazoezi.

Wataalamu hutuambia kuwa haitoshi kufahamu kanuni na mbinu za kuogelea. Ili kufahamu namna ya kuogelea, licha ya kuzifahamu kanuni hizo, mwanafunzi anapaswa kuingia ndani ya maji na kufanya zoezi la kuogelea.

Ndivyo pia tunavyoshuhudia kwa wanaotaka kujifunza kuendesha magari. Licha ya kujifunza sheria za barabarani pamoja na kanuni za kuendesha ni sherti mwanafunzi akae mbele ya usukani na kuuzungusha huku gari likienda mbele au nyuma.

Kwa kadiri mwanafunzi anavyofanya mazoezi mengi, ndivyo anavyoweza kufahamu kendesha gari. Vinginevyo itachukua muda mrefu kufahamu.

Kuna shughuli nyingi baada ya kufanya mazoezi ya muda mrefu huweza kufanyika hata bila kufikiri. Baada ya uzoefu tunaweza kufanya mambo kwa ufanisi zaidi na pengine bila kutambua.

Mazoezi siyo tu katika mambo ya mwili na kiakili bali pia hata katika mambo ya kiroho na kitabia.

Mtume Paulo analithibitisha jambo hilo pale anapowaandikia ndugu Wakorintho akisema: "Wanariadha hujipa mazoezi na nidhamu kali; hufanya hivyo ili wajipatie taji iharibikayo! Lakini sisi twafanya hivyo tupate taji ya kudumu daima" (1 Wakorintho 9:25)

Mazoezi huenda pamoja na nidhamu. Wanamichezo wetu wengi na hata wanafunzi hujidai kufanya mazoezi lakini pengine hawana nidhamu. Kumbe licha ya kufanya mazoezi, nidhamu ni ya muhimu sana. Kama hakuna nidhamu au utaratibu huwa ni vigumu sana kufanikiwa katika mashindano yawayo yote yale.

Tunaposema kuwa tunajiandaa kuingia katika karne mpya ya Sayansi na Tekinolojia ni kwamba imetupasa tuwe na uzoefu katika mambo mbali mbali ya kisanyansi.

Ili tuweze kufanikiwa yatupasa tujikanie mambo yasiyo ya lazima na tutumie muda wetu mwingi katika kujizoeza katika mambo hayo.Tunapaswa kujijengea mazoea ya kusoma sana. Tunaambiwa kuwa ili tujipatie elimu na maarifa kuna njia tatu: Kusoma mambo yale yaliyokwishaandikwa na wataalamu, pili kuwasikiliza wale wenye utaalamu na tatu ni kufungua macho na kuona mambo yale yaliyokwishatendwa au yanayotendwa na wataalamu. Tuwe na uzoefu wa mambo hayo ili tuweze kufanikiwa. Daima tuzoee kusoma, kuwasilikiza wengine na pia kuangalia yale yaliyofanywa na wengine. Tujifunze kutoka kwa yoyote, wakati wowote na chochote kile kizuri.

Wototo wetu si wapumbavu

Ni lazima watanzania tufahamu kuwa maamuzi ya watoto yanategemea yale wanayoyapokea kutoka kwa wazazi , mazingira , shule na marafiki . Kudhani kwamba watoto hawatatilia maanani yale wanayoyaona kwenye jumuia yetu iliyotawaliwa na matangazo ya anasa (Consumerism) ni kuwachukulia kuwa watotto wetu ni wapumbavu.

Tunapaswa kuwaelewa watoto wetu kikamilifu . Tuelewe ni binadamu waliojaa hisia . wanauwezo wa kufikiri na kujiunza .

Kiakili wanakua kulingana na wanayoyapokea katika mazingira wanyoishi .

Mazingira anayokulia mtoto ndio yanayomtofautisha na wengine. Sisi waswahili tunasema "Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo".

Tuwaimarishe watoto wetu kwa nguvu ya hoja tunapowalea ili washawishike kujifunza mema.

Hata hivyo kama hatutawapenda na kuwafurahia wakati wote hawataweza kujifunza yale tunayo wapa. Kuwapigapiga na kuwatishia acheni! Acheni!

Bila kuwajengea mazingira yanayofaa kwa malezi hakutatufikisha mbali. Kupiga watoto kila mara ni kuwafundisha woga, chuki na kulipiza kisasi.

Je mazingira ya Tanzania ya leo yanafaa kwa malezi ya watoto?

Kama tulivyoona mazingira yetu yanatawaliwa na anasa za matumizi .

Vyombo vya habari hujali biashara na sio malezi ya kufaa watoto.

Ulaya wanakabiliwa na mmomonyoko wa maadili kwa sababu ya ‘uhuru wa habari’.

Hatuna budi kujiuliza hivi tunakwenda wapi?

Inatia hofu ingawa hili halionekani kuwa tatizo la kitaifa kama tunapoangalia jamii yetu itamezwa na mila na desturi bomu zinazoletwa na vyombo vya habari bila uthibiti yakinifu. Kuthibiti habari kwa manufaa ya watoto sio kuingilia haki ya kupata taarifa tunaangalia zaidi zile habari zinazoweza kuwapa watoto hisia za ukatili, ngono au kudumisha tamaduni za nje.

Lengo la kuthibiti habari ni kulinda malezi ya watoto ambayo kwa kiasi kikubwa hutegemea mazingira, Nyumbani inatakiwa vyombo vya habari vithibitiwe na wazazi kwa manufaa ya watoto. Mtoto anahitaji kupata muda wa kujifunza, kucheza na kupumzika, sio halali kuwaacha watoto waangalie Televison masaa ishirini na nne.

Ephraim J. Mkenda

Daar es Salaam.

 UMATI ni wapinzani wa amri ya Mungu

Ndugu Mhariri,

Shetani ana sifa mbaya zote . Yeye (Shetani) humnyemelea mwanadamu kwa njia nyingi aliyoruhusiwa ili waangamize. Sisi wanadamu tujihadhari sana tunapojadili mambo yetu. Tusijikweze na kujiona tuna akili au elimu ya kuamua mambo sawa

Tunapotaja sifa za shetani wengi wetu hawaelewi kuwa sifa hizo zinamlenga yeye yule (shetani). Twaita Ibilisi, pepo mbaya, jini, na mengine mengi na ya kikabila kama "Chimlungu" na kadhalika kwa maarifa ya dunia hii kutokana na elimu yetu finyu yeye hujipenyeza na kutupotosha.

Uzazi wa majira ni mbaya . Njia pekee na ni halali kujinyima au kuvumiliana kwa kitambo lakini kutumia dawa kwa ajili hiyo moja kwa moja ni uuaji , kazi ya Mungu haisahihishwi kwani yeye (Mungu) kufanya yote kwa ustadi . Kazi ya Mungu haiongezwi wala kupunguzwa au kupotoshwa , na kujifanya wataalamu hakika tutajikuta tunajenga mnara wa Babeli.

S.M. Ngunga

Box 7472 Dar

(Mtoto wa Marehemu)

Barua ya wazi kwa

Fr. Felician Nkwera

Baba Nkwera "Tumsifu Yesu Kristu".

Napenda kutoa shukrani zangu nyingi kwako, kwa kazi nzuri uliyoifanya katika kitabu "Ukombozi wa Wanadamu", kitabu cha tatu "Zaeni matunda Mema" cha kidato cha 4-6.

Pia natoa shukrani kwa namna ya pekee kwa wale wote ambao kwa maombi (sala) zao uliweza kuikamilisha kazi hiyo.

Nimesoma kitabu chako kiitwacho "Barua ya wazi kwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II" na kukielewa kwa kadri ya upeo wangu nimeridhika kwa kiasi fulani. Sina ugomvi na wewe wala sina hata chembe ya tatizo na Askofu Mkuu, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Tatizo langu kubwa ni hawa watoto wadogo ambao wazazi au walezi wao ni wanamaombi. Je,baada ya watoto hawa kupata mafundisho ya Ubatizo, Ekaristi Takatifu na Kipaimara ndani ya Kanisa Katoliki, watalazimishwa kutotii maanuzi ya Jimbo Kuu Katoliki la - DSM? Endapo watafuata nyayo za wazazi au walezi wao, Baba Mtakatifu Yohane Paulo - II ategemee nini kutoka kizazi kitakachozaliwa ndani ya Wanamaombi ?

Shukrani zangu nyingi ninazitoa kwa Moyo wa Dhati, kwa sala mnazozitoa kwa mama Bikira Maria, aksanteni sana. Kumpokea Yesu Kristu katika fumbo la Ekaristi Takatifu, ni kipimo pekee cha upendo uso na mwisho, wala mipaka kwa "Mungu baba Mwenyezi", kutoa ulimi nje tu pasipo kumpokea Kristu, huku ukiwa umepiga magoti huo sio Ukombozi wa Mwandamu. Kibaya zaidi kwa watoto wadogo "Heri wenye Moyo safi".

Baba Felician Nkwera, kutunga kitabu si sidhani sana, lakini kitabu kinapomtuhumu binadamu mwenzako, ambaye amepewa dhamana na Yesu Kristu ili aongoze Roho za Binadamu, kuufikia na hatimaye kuuishi Ufalme wa Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu; nimefika kikomo cha kufikiri, kuwaza na wala kutoelewa Kanisa litapata mwanga gani juu ya kitabu kile ambacho kitasomwa na maelfu ya binadamu. Ninahakika wewe binafsi jibu unalo.

Wanamaombi wote kumbukeni ya kuwa huu ni mwaka wa Mungu Baba Kikanisa. Kusali sana rozari pasipo kumpokea Kristu huku ni sawa na kujuta dhambi na wala sio kuacha dhambi. Ndugu zangu yawapasa kujuta kutotii kwenu kwa Baba Askofu Mkuu tangu 1990 hadi dakika hii. Pia kuacha kutotii kwenu kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Fr. Nkwera kumbuka kwa upeo kila sekunde, siku ile ambayo ulipata upadrisho ulitamka kwa kinywa chako na kukiri mbele ya wakristu waliokuwepo "Imani ya Kanisa Katoliki" utalifanyia nini hadi kufa kwako? Kimsingi Kanisa Katoliki lina historia yake, mimi nina Imani, Matumaini na Mapendo ya kuwa saa ikifika itakulazimu utoe hesabu ya kondoo kwa kuwa wewe ni Mchungaji.

Kutolea mifano mbali mbali ya watakatifu walipita, eti walipata misukosuko mingi na hata kuthubutu kumtolea mfano Padre Pio ambaye ametangazwa "Mwenye Heri". Si sababu ya kuhalalisha Kutotii kwa - wanamaombi. Kuendelea kuwataja tena na tena Padre Pio na baadhi ya Watakatifu ambao ni marehemu, ili kuhalalisha usaliti ndani ya Kanisa Katoliki Mitume ni Kufuru kubwa kwa Roho Mtakatifu. Hao wote hawawezi kulinganishwa na Mungu Mwenyezi.

Majimbo mengi tu hapa Tanzania Wakatoliki wanampokea Kristu kwa kupiga magoti. Mpendwa Fr. Nkwera naomba utumie akili ya kuzaliwa tu ni kwa nini iwe Dar es Salaam na baadhi ya matawi ya wanamaombi, Kristo anadhihakiwa? Kisa "Kusimama au Kupiga Magoti". Wakatoliki wote wa Dar es Salaam na kutoka sehemu yoyote ile ulimwenguni Tukisimama na Kumpokea Kristu huo sio ubinafsi - wa Polycarp Pengo hata kidogo.

Maamuzi yoyote yale ya Kiroho yatakayotolewa na Mwadhama Polycarp Kardinal Pengo, juu ya Kanisa Katoliki hapa Tanzania yaheshimike na kutekelezwa ipasavyo na kila binadamu mwenye mapenzi mema hapa ulimwenguni. Ukiwaamuru Wanamaombi wasimame wakati wa kukomunika Ekaristi Takatifu, hakutamaanisha kuwa wewe, si Fr. Nkwera, wala hakutakuondolea utambuzi wa karama uliyonayo "Infuluence", na zaidi ya hayo umahiri ulionao katika uandishi wa vitabu hautakoma.

Uhusiano kati ya dola (serikali) na Kanisa Katoliki upo na utaendelea kuwepo daima katika suala la ustawi wa jamii - kimwili. Lakini Kimsingi Kanisa Katoliki lipo ili kuongoza Roho za Waumini kufika mbinguni. Dola (serikali) kazi hiyo hawaiwezi kabisa. Ni kwa nini barua yako ya wazi uliielekeza moja kwa moja si kwa Baba mtakatifu, isipokuwa kwa kiongozi wa dola Mheshimiwa Raisi B. W. Mkapa? Fr. Nkwera ilikupasa kumpa MUNGU YALIYO YAKE na si vinginevyo.

Pole sana tena Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo nina imani, ROHO yako iradhi na mwili pia uradhi kuubeba msalaba.

"BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHO YANGU". Yoh:23:44-46 Tuwasifu milele

YESU, MARIA NA YOSEPH

Ndimi, Mwana VIRAFRA

Gadan. R. M