Tudumishe umoja wetu

SisiWatanzania kila mwaka tarehe 26 ya Mwezi Aprili huwa tunafanya sherehe za kumbukumbu la Muungano wetu uliofanyika miaka zaidi ya thelathini liyopita. Kutokana na Muungano huo nchi mbili ambazo zilikuwa zikijulikana kama Tanganyika na Zanzibar zilifanya Muungano na ikazaliwa nchi moja inayoitwa Tanzania. Watanzania wengi wametambua umuhimu wa Muungano huo.

Licha ya Muungano wa nchi hizo mbili, tulikuwa pia na ule Muungano wa nchi za Mashariki ya Afrika, zikiwemo nchi ya Kenya, Uganda na Tanzania. Pia tunao Muungano wa nchi huru za Afrika, unaojulikana kama Umoja wa nchi huru za Kiafrika. Kuna pia ule Muungano mkubwa wenye kuzishirikisha nchi nyingi hapa ulimwenguni, nao unaitwa ni Umoja wa Mataifa. Siyo miungano hiyo tu, bali iko mingi sana hapa ulimwenguni. Hiyo yote ina lengo hasa la kujenga ushirikiano na kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo kwa usfanisi zaidi.

Tunaambiwa na wenye hekima kuwa Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Daima watu wanapofanya kazi kwa ushirikiano mapato yake huwa ni bora zaidi na hivyo kunakuwa na ufanisi mkubwa sana. Watu wafanyapo kazi fulani katika kushirikishana huwa na ufasi kwa sababu kila binadamu ana karama zake zilizo tofauti na binadamu mwingine. Kwa hiyo wanaposhirikiana, huchangiana mawazo, maarifa na hata mbinu katika utendaji wao.Tunasema kuwa akili za binadamu ni kama nywele, yaani kila mmoja ana akili zake na hivyo hata utendaji huwa ni tofauti. Lakini ikiwa watu watafanya kazi kwa pamoja, kwa kushirikishana hizo akili kutakuwa na mafanikio makubwa sana. Hivyo ndivyo tunavyoshuhudia katika ulimwengu wa leo. Hayo mafanikio katika mambo ya sayansi na tekinolojia ni mapato ya watu walioshirikisha akili na karama zao kwa pamoja na hivyo kuweza kuleta uvumbuzi wa vitu mbalimbali katika fani hizo tofauti.

Tunasema kuwa watu wakitaka kufanikiwa ni vizuri zaidi ikiwa watafanya kazi kwa kushirikiana. Maisha ya kushirikiana siyo mageni kwa binadamu, kwani binadamu kama binadamu ni kiumbe chenye kuishi katika ushrika na kiumbe kinginge. Hivyo pia hata sisi Waafrika, maisha yetu kwa asili ni maisha ya kushirikiana, yaani maisha ya pamoja, maisha ya ujamaa. Utamaduni wetu ni hasa wa kuishi na kushirikiana katika mambo mbalimbali, iwe ni katika kazi, iwe ni katika furaha na pia hata katika misiba. Mtu yule ambaye alikuwa akijitenga na wenzake alionekana kuwa ni kama vile mchawi. Hivyo ndivyo inavyoweza kuonekana hata siku ya leo kuwa nchi ile isiyotaka ushirikiano na nchi nyingine huwa katika hali mbaya na hivyo kukosa misaada kutoka nchi nyingine hasa wakati inapokuwa katika matatizo.

Kanisa nalo limetambua kuwa likitaka kufanikiwa katika kuihubiri Injili kwa undani kabisa halina budi kujenga ule umoja kutoka kwenye mizizi yaani katika familia. Umoja wenye kujengwa kutoka familia na kisha katika jamii kubwa zaidi tunauita ni Jumuia Ndogondogo za Kikristu. Jumuiya hizo hujengwa kwa familia jirani kuunganika pamoja chini ya uongozi wa jumuiya na kufanya shughuli za kidini na hata za huduma. Wanajumuiya hushirikiana katika ibada, katika shughuli za ujenzi wa kanisa na pia katika kuhudumiana. Umoja huo siyo tofauti sana na ule ambapo ni wa kisiasa ambapo wanakijiji huwa chini ya Mwenyekiti wa kijiji wakishirikiana katika shughuli mbalimbaliza ujenzi wa taifa katika ngazi ya shina na baadaye huzidi kukua hadi kufikia ile ngazi ya kitaifa na kimataifa. Kwa hiyo umoja wetu uwe ni wa kidini au wa kisiasa hauwezi kuwa imara na kukamilika ikiwa haujengeki kutoka katika ngazi ya chini kabisa yaani kuunganika kwa familia mbalimbali zilizo katika ujirani.

Ni jambo la kusikitisha kuona kuna watu ambao hawako tayari kuishi katika umoja fulani. Hali hiyo hudhoofisha kabisa maendeleo ya mahali. Familia isiyoshirikiana na familia nyingine huwa ni kikwazo kwa maendeleo ya familia nyingine. Hivyo pia na hata jamii au taifa ambalo linaishi peke yake kama kisiwa huweza kuwa ni kikwazo kikubwa sana katika shughuli za kimaendeleo. Pia tungependa kuwaonya wale wote ambao huwa na tabia ya kuharibu umoja katika jamii. Ni dhahiri kuwa katika kila muungano au umoja wale wanaoungana hawana budi kupoteza kitu fulani chao cha pekee ili kuweza kufanya muungano uwe ni kitu cha wote.

Kwa maneno mengine katika kila umoja au muungano wale wanaoungana hawana budi kuondokana na ubinafsi. Lakini ikiwa kuna ubinafsi katika wanamuungano, basi hapo muungano hudhoofika, na mwisho wake ni hatari ya kufa huo muungano.

Tunashuhudia hivi leo miungano mingi ikiwa katika hali ya kuyumbayumba iwe ni katika mambo ya siasa na hata katika mambo ya kidini.

Sababu kubwa yenye kusababisha kuvunja au kutetereka kwa umoja na miungano hiyo ni ile tabia ya ubinafsi, yaani kunakuwa na watu ambao wanatafuta faida yao katika umoja huo na hiyvo kuleta matatizo ndani ya muungano na umoja. Tumesema kuwa wale ambao wanaamua kuishi katika muungano au umoja ni sherti wawe tayari kutoa sadaka kwa namna fulani, yaani wawe tayari kuachana na hali ya ubinafsi kwa faida ya umoja. Ulimwengu umeshashuhudia kuanguka kwa miungano mingi sana, pia kuna umoja wa nchi nyingi na hata watu binafsi ukivunjika kwa sababu ya ubinafsi.

Kwa hiyo tukitaka kulinda umoja na miungano yetu yatupasa kila mmoja aondokane na kuogopa kabisa ubinafsi na ule moyo wa uchoyo.

Serikali idhibiti madawa holela mitaani

Ndugu Mhariri,

Ninaomba unipe nafasi katika gazeti lako hili ambalo sasa linaonekana kuibuka kwa kishindo katika ulimwengu huu wa kuhabarishana ili niweze kutoa dukuduku langu kuhusu suala zima linalohusu afya za wanachi na jamii kwa ujumla.

Kinachonisikitisha hapa ni kuwa japo serikali inazo hospitali zake nyingi pamoja na zahanati mbalimbali ambazo tangu miaka ya hivi karibuni wananchi wamekuwa wakitakiwa kuchangia ili kupata huduma za afya ikiwemo hii ya matibabu, bado inaogopesha kuona kuwa kadri siku zinavyosonga na kusisitiza uchangiaji huo, ndivyo hali inavyozidi kutisha katika utoaji wa huduma hiyo.

Bado sisiti kusema kuwa ingawa ni kweli ulio wazi kuwa hospitali mtu huenda ili kulipia, huambulia kupanga foleni ili aonane uso kwa uso na daktari kisha arudi nyumbani bila dawa na kuishia kulipia pesa nyingine katika hospitali za binafsi na maduka ya madawa kwa kuambiwa kuwa HAKUNA DAWA kisha kuelekezwa maduka ambayo madawa hayo yanapatikana hali ambayo inatia shaka na kuzua maswali mengi ikiwa na pamoja na mshangao kwamba fedha za mchango wa huduma ya afya zinafanya kazi gani ?

Au basi hayo maduka na hospitali za kibinafsi wanapata wapi madawa hayo. Hali ya kukosekana madawa katika hospitali za serikali na kupatikana kwa wingi katika maduka ya watu binafsi ambayo mengi ni ya watumishi wa Idara au Wizara ya Afya inaashiria na kutoa funzo gani?

Lakini si hivyo tu, mbona mitaani watu wengi wanauza madawa mithili ya Wamachinga, hao wanatoa wapi dawa hizo?

Mbona serikali imekaa kimya hali kuna tetesi kuwa madawa mengi yanayouzwa na watu hata katika maduka mengi ni yale ambayo yamepita muda wake ila kinachofanyika ni kubandika lebo zinazoonyesha muda wa kuisha tofauti na hali halisi ilivyo?

Tunaomba serikali ifanye uchunguzi wa kina na wa makini ili kuzinusuru afya zetu.

Marwa Mashauri,

S.L.P.66,

Tarime

 HONGERA: Ni wakati muafaka

Ndugu Mhariri,

Napenda nisiwe nyuma kati ya waumini ambao kwa namna ya pekee wangependa kutoa pongezi za dhati kwako katika kuitikia wito wa kanisa ili kuondoa utupu wa kiroho ndani ya mioyo yao kwa kuijaza lishe ya roho kwa Neno la Mungu.

Huu ni wakati na mahali (time and place) ambapo gazeti hili inabidi lisiwe nyuma kutimiza makusudio yaliyomo katika Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II "UJIO WA MILENIA YA TATU (Tertio Millenio Adveniente), juu ya maandalizi kwa Jubilee ya Mwaka 2000, ukurasa 73 ambapo anasema, " Mwaka 1999 ambao ni mwaka wa tatu na wa mwisho wa maandalizi, utakuwa na lengo la kupanulia waumini upeo wa kuona kwa macho ya kiroho ili waweze kuona vitu kwa kina na kimo, urefu na upana kama Kristo;...."

Ni katika mtazamo huo, Kanisa Katoliki kwa kutumia hazina yake ya mafundisho ya imani yatokayo katika Biblia Takatifu na kwa kufuata tafsiri yenye hekima ya Mungu.

Na pia kutoka kwenye mapokeo ya kanisa, maswali yote yajibiwe ili kuelimisha jumuiya ya watu wa Mungu katika nchi yetu.

Wakati huu ni vema pia waumini turejee angalizo ili kuepuka upotoshaji wa maandiko, (2Petro 3:14-18).

Ndugu Mhairi, nazidi kusema hongera, ni wakati na pahala, pia kutimiza mafundisho ya Mtume Petro kumjibu kila mtu aulizaye habari ya tumaini kwa upole na hofu kwa dhamiri njema ili watahayarishwe wale watukanao mwenendo wetu mwema katika Kristo (1Petro 3:15-16).

Ni kweli kwamba waumini wengi wana matatizo kama aliyo nayo Ndugu Sikitiko Amosi, wa Dar es Salaam kama alivyojieleza katika toleo la Jumapili 11-17, 1999, hivyo wawe tayari kupokea msaada huo wa kiroho.

Namalizia kwa kutoa wito kwa waumini wote Wakatoliki, Wakristo wote pamoja na wote wenye mapenzi mema popote walipo kuona uzuri na umuhimu wa kununua gazeti hili la Kiongozi kwa ajili ya ustawi wao na familia zao kimwili na kiroho.

Habari ndani ya gazeti hili zinaleta muunganiko wa Imani moja Katoliki ya Mitume katika kumwamini na kumfuata Yesu Kristo ili tuwe na amani ya Roho katika Mungu mmoja.

Tumsifu Yesu Kristo.

Chrisostom M. Agapiti

S.L.P 31096,

Dar es Salaam.

 Kanisa la Tanzania liige mfano wa Malawi

Ndugu Mhariri,

JAMII yoyote duniani hutambiliwa kwa mila na desturi zake au niseme kwa utamaduni wake.

Waafrika ni jamii mojawapo na Tanzania pia ni jamii miongoni mwa zile za Kiafrika.

Nakumbuka miaka ya sabini wakati Mwalimu Julius Nyerere alipoamrisha polisi kuwachania nguo wanawake ambao walikuwa wakivaa nguo fupi na zilizobana ambazo zinapingana na utamaduni na desturi zetu. Laiti zama zile zingerudi leo!

Siku hizi utamaduni wa watu hususan wanawake kutembea nusu uchi kama sio uchi kabisa limekuwa jambo la kawaida. Ukiuliza utaambiwa ni demokrasia na watajitetea kwamba hatuwezi kusema kwamba kutembea uchi sio utamaduni wa Watanzania kwa vile yapo makabila kama vile Wabarbeig na kadhalika ambapo wanawake hawavai nguo za kusitiri maungo ya siri hadi leo. Lakini hatujiulizi kwamba kama hata Mwenyezi Mungu aliamua kuwavisha nguo Adamu na Hawa pale bustanini, leo tuna nini hata tuanze tena kutembea uchi. Tusijifunze kufanya jambo ovu eti kwa sababu yupo mtu mwingine anayelifanya.

Ukipita kwenye mitaa ya miji hapa Tanzania siku hizi hususan jijini Dar es Salaam utashangaa kuona vijitabu na majarida ya ajabu ajabu ambapo wanawake walio uchi wamepigwa picha, huku majarida na vitabu hivyo vikiongoza kwa mauzo.

Nilisoma katika gazeti hili hivi karibuni kwamba Kanisa nchini Malawi limeanzisha kampeni kabambe ya kukagua filamu, vitabu na majarida yanayovunja kanuni za maadili ya Kiafrika au kiutu.

Kinachoshangaza ni kwamba Kanisa nchini Tanzania halijafanya chochote kukomesha upotofu huu wa maadili unaoongezeka kwa kasi ya kutisha hapa nchini. Ni wakati muafaka kwa Kanisa hapa kwetu kuungana na wenzetu wa Malawi kupinga upuuzi huu.

Richard Abdul-kadr

S.L.P. 21000

Dar es Salaam.