Tuwahudumie wazee wetu

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mwaka huu wa 1999 ni mwaka wa Wazee. Kwa maneno mengine ni kwamba tunapaswa kuwaangalia wazee mwaka huu kwa namna ya pekee hasa kuhusu mahitaji yao na pia huduma zao mbalimbali. Ili tuweze kufanya hivyo hatuna budi kuwafahamu hawa wazee ni watu wa aina gani.

Sote tunajua kuwa wazee kama wazee ni watu ambao wameendelea sana katika umri wao na pia nguvu zao na utendaji vimepungua mno. Hao ni watu ambao wanahitaji sana kupewa huduma ya namna ya pekee ama kutoka kwa ndugu, jamaa, marafiki na hasa kutoka jamii au taifa. Kwa vile hakuna mtu ambaye anaweza kusema kuwa hahusiki na wazee kwa namna moja au nyingine, hapo ni kwamba kila mmoja wetu anahusika na suala hilo la wazee kwa namna moja au nyingine.

Sote tunajua kuwa waliotufanya tuwe hivi tulivyo na wale waliotutangulia kuzaliwa au wazee wetu. Kwa hiyo tunadaiwa shukrani kubwa sana kwao. Shukrani hiyo tunaweza kuionyesha kwa namna mbalimbali, na hasa kwa kuwa tayari kuwahudumia katika siku zao hizo za uzee. Wengi wao wanakuwa katika hali mbaya sana kimaisha na hivyo wanahitaji sana msaada kutoka kwa watoto wao na pia kutoka kwa jamii.

Kwa kadiri ya utamaduni wetu wa kiaafrika, wazee walikuwa wanatunzwa vizuri sana na hivyo wakawaachia baraka zao watoto na wajukuu baada ya kufa kwao. Lakini ni jambo la kusikitisha sana siku hizi tunaposhuhudia wazee wengi wakiishi katika hali mbaya ya mahangaiko licha ya kuwa na watoto au wajukuu wao wenye uwezo wa kuwatunza. Kuna wazee wengi hasa huko vijijini ambao wanaishi maisha duni sana, na kumbe kuna watoto wao ambao wana maisha mazuri huko mijini. Ni jambo la fedheha sana kushuhudia wazee wetu wakiwa ombaomba katika nchi yetu ambayo kwa asili ni yenye kuheshimu sana wazee wake. Siyo utamaduni wetu wa kuwapeleka wazee wetu kwenye vituo vya wazee ili waweze kutunzwa huko.

Katika Kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira tunasoma hivi: "Mwanangu umsaidie baba yako katika uzee wake; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana.." {Yoshua bin Sira 3:12}. Mawaidha hayo hayahusu tu baba zetu wazazi bali ni kwa ajili ya wazee wetu wote. Hapo tunaangizwa kuwasaidia wazee wetu wote katika uzee wao; tunakumbusha kuwa tusiwahuzunishe wazee wetu hasa kwa maneno yetu ya dharau.Tunapaswa kuwatendea kwa upole na uvumilivu kwani wengi wao huwa akili zao pia zimepungua na hivyo kufikiri kwao ni tofauti sana.

Tukichunguza sana tunaona kuwa wazee wetu wengi wanaishi katika hali ya dhiki sana.Wengine wanakosa chakula, wanakosa nguo na hata mahali pakulala. Kuna wazee wengine kwa sababu ya kukosa matunzo hushambuliwa na magonjwa mengi ambayo huwapeka haraka kifoni. Jumuiya ambayo haiwajali wazee hukosa baraka kubwa sana. Tunaambiwa kuwa wazee wengi ni wenye maneno ya hekima na hivyo tunapoweza kuwatunza hapo ndipo tunaweza kushiriki hizo hekima zao na hata ujuzi wao. Tunasoma tena katika Kitabu cha Heikma ya Yoshua bin Sira "Ni nzuri kama nini hekima ya wazee, na mawazo yenye shauri ya wale walioheshimiwa." {Yoshua bin Sira 25:5}

Kuna wazee wengi katika jamii ambao wamekufa bila kuwashirikisha watoto na wajukuu wao maarifa kama vile ya uganga na mang’amuzi mengine kwa sababu tu hawakutunzwa vizuri na hao watoto na wajukuu wao.

Tunapenda kulaani vitendo vibaya vinavyofanyika katika nchi yetu vya kuwaua wazee, eti kwa sababu hufikiriwa kuwa ni wachawi. Katika mwaka huu wa wazee tunatumaini kuwa kutakuwa na mikakati mbalimbali ya kuwasalimisha hao wazee wanaofikiriwa kuwa ni wachawi katika jamii zetu. Tunapaswa kuwatetea hao wazee wetu kwani kuna wengi ambao huuawa kwa sababu tu ya chuki katika jamii. Imani zote za kidini hutufundisha kwamba hakuna mmoja mwenye haki ya kuondoa maisha ya binadamu mwenzake kwa makusudi au kwa sababu zake binafsi. Tunaombwa katika mwaka huu kujitahidi kuwaelewa wazee wetu na hivyo kuwasaidia katika mambo mbalimbali. Ikiwa kweli kuna vitendo vibaya kutoka kwa wazee wetu hao tunapaswa kuviangalia kwa makini na tusitoe hukumu za haraka na hata kuwaua na kuyaafupisha maisha yao.

Vile vile tunapaswa kukumbuka kwamba jinsi tunavyowatendea hao wazee wetu wa leo ni pia jinsi hiyo hiyo tunakavyotendewa nasi tutakapokuwa katika hali hiyo ya uzee. Wengi wetu tukumbuke kuwa siyo siku nyingi tutakuwa nasi wazee kama hao wazee tunaowatesa na kuwadhulumu siku ya leo. Kwa hiyo tujiwekee akiba ya baraka kwa uzee wetu tukiwa tayari kuwahudumia hao wazee tulio nao. Ingawaje kuna hali ngumu ya uchumi siku ya leo katika taifa letu na mahali pengine, hatuna budi bado kudumisha ule utamaduni wetu wa kuwahudumia wazee wetu kwa hali na mali. Tusiige mitindo ya kigeni ya kuwadharau na kuwanyanyasa wazee. Hapo tutakuwa tunajitafutia laana kubwa sana kwa maisha yetu ya hapo baadaye.

 

Barua ya wazi kwa wajumbe wote wa Baraza la Walei Jimbo Kuu la Dar es Salaam

Ndugu wajumbe,

Bila shaka mtakuwa mmepata na kusoma barua kutoka kwa Ndugu. A.J. Kaoma yenye kichwa cha habari: JE KUPIGA MAGOTI WAKATI WA KUPOKEA EKARISTI TAKATIFU NI DHAMBI?

Baada ya kusoma na kutafakari, naomba kutoa mawazo yangu katika kuijibu barua hiyo. Hoja kubwa ya Ndugu huyo ni kuwa kupokea Ekaristi Takatifu tukiwa tumesimama ni dhambi kwani anadai imethibitishwa na Maandiko Matakatifu na amri za Kanisa.

Kila anayesoma barua hiyo atashangaa kama kweli Ndugu Kaoma amekomaa kiimani, kwani baadhi ya hoja anazozitoa zaonyesha uchanga wake. Kwa mfano, Isaya, 45:22-23 haina uhusiano kabisa na kupokea Ekaristi Takatifu tukiwa tumesimama au tumelala au vinginevyo. Ingawaje Kaoma anadai kuwa si mmoja wa kundi la wana-Maombi, kwa hakika maandishi yake yaonyesha wazi kuwa yeye ni mwana- maombi.

Hebu tuangalie kwa undani kiini cha suala analolizungumza Kaoma; Kupokea Ekaristi Takatifu tukiwa tumepiga magoti.

Tujiulize hiyo ni imani yetu au ni taratibu zetu za kiliturujia? Kwa hakika hizo ni taratibu zilizowekwa na Kanisa. Imani yetu ni ipi basi? "Tunasaidi kwa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, kisha tunasadiki kuwa lipo Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume" Taratibu zinawekwa kulingana wa wakati na mazingira, na hivyo zinaweza kubadilishwa.

Imani haibadilishwi kwani kuwepo kwake hakutegemei mazingira. Mtakumbuka kabla ya Mtaguso Mkuu wa II Vatikani, tulikuwa tunatumia lugha ya Kilatini katika adhimisho la Ekaristi Takatifu, hali hiyo ilibadilika baada ya Mtaguso.

Tena wakati wa adhimisho hilo hilo la Ekaristi Takatifu, Mapadre walikuwa wanawaonyesha mgongo waumini na kuwageukia mara chache sana katika baadhi ya matukio. Mtaguso Mkuu wa II wa Vatikani uliondoa taratibu hizo na sasa mapadre wanawaangalia waumini. Hali hizo mbili hazijaondoa ukweli juu ya imani yetu.

Sasa tufuatilie suala la kupokea Ekaristi Takatifu. Katika Agano la Kale tunaweza kulinganisha na tukio hilo na ile Pasaka ya Wayahudi, (Kut.12:11).

Katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu hatusomi kuwa Wayahudi waliamriwa kupiga magoti wakati wanamla |Mwana-kondoo wa Pasaka. Tumesema hapo awali kuwa Isaya 45:22-23 haituonyeshi kuwa waumini wapige magoti wakati wa kupokea Ekaristi Takatifu, badala yake Mungu anaelekeza uhusiano wa unyenyekevu ambao binadamu anapaswa kuwa nao mbele yake. Mungu anatudai pia unyenyekevu wa aina hii tunapojenga mahusiano ya Yesu Kristu, mwana wake wa Pekee na Mkombozi wetu, (Filipi, 2:10-11). Ni unyenyekevu unaodai tuwe nao kila siku na mahali pote, sio mbele ya Ekaristi Takatifu peke yake. Tunapomhusisha Mungu na ibada zisizo za kweli tunaonyesha kutokuwa na unyenyekevu mbele yake.

Katika karamu ya Mwisho, Yesu alikaa kula chakula pamoja na Mitume wake (Luk.22:14). Tukio hili la kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ndio kiini cha imani yetu. Lakini tunasoma kuwa wakati wa kuweka Sakramenti hii ya Ekaristi Takatifu Yesu alikaa, maana yake aliila karamu hii pamoja na wafuasi wake akiwa amekaa. Katika ile Pasaka ya Wayahudi, (Kut. 12:11), Mungu aliwaamuru kuila kwa haraka. Hii ina maana kuwa inawezekana walikula wakiwa wamekaa au wamesimama. Ni vigumu kuila huku wamepiga magoti, kwani hali hiyo ingewaletea usumbufu.

Mtume Paulo anapowaandikia Wakorintho, anatueleza kuwa jambo la kiimani ni kuwa kila tunapokula mkate na kuinywa damu ya Bwana tunatangaza kifo chake mpaka atakapokuja. Tunaona hapa kuwa Mtume Paulo hasisitizi tendo la kupiga magoti. Kumbe kupokea Ekaristi kutazamwe kama tendo la kiimani lenye matarajio ya ufufuko katika Kristo Yesu. Tumpokee Bwana Yesu Kristu katika fumbo la mkate na divai kwa mastahili na kwa imani thabiti, la sivyo tutakula na kunywa hukumu yetu sisi wenyewe, (1Kor.12:26-29).

Sehemu hizo za Maandiko Matakatifu zinaonyesha wazi kuwa kupiga magoti sio msingi wa imani yetu.

Sasa tumwulize Kaoma, amepata wapi msimamo mkali kuwa, kwa kusimama wakati wa kupokea Ekaristi Takatifu tunatenda dhambi mbili; ya kwanza ya kusimama na ya pili ya kukufuru? Kwa kadiri ya maelezo niliyosoma na kusimuliwa amri hiyo imetokana na Shetani/Ibilisi ambaye Kaoma na wenzake wanaamini anahusiana na huyo Bikira Maria wao.

Mahusiano hayo yako hivi, Shetani aitwaye Makata anajifanya kuwa ameagizwa na Bikira Maria awaeleze wanadamu masuala fulani ya kiimani.

Suala mojawapo ni hilo, kuwa "Mama" hapendi wanadamu wampokee Mwanae wakiwa wamesimama au mikononi.

Pia "Shetani" huyo anasemekana anaamriwa na Mungu kufanya matendo ya wokovu kwa wanadamu.

Shetani huyu huwasilisha ujumbe huu kupitia mmoja wa wahudumu wa wana-maombi aitwaye Mtendakazi.

Naye huipata habari hii akiwa katika hali isiyokuwa ya kawaida. Kwa hiyo mtendakazi husikia na kuwaeleza washiriki katika mikesha na ibada mbalimbali.

Tazama ilivyo vibaya kuhusisha Shetani na Utakatifu, yaani kuhusisha Giza na mwanga/Nuru. Hapa unaona wazi ukengeushaji wa teolojia, ambayo Kaoma anasema baadhi ya washiriki wamebobea.

Kama wamebobea katika teolojia hii ya uzushi, basi ni hatari katika imani yetu. Kwa vyovyote vile Bikira Maria hawezi kuwa shirika na Shetani. Kumhusisha na Shetani ni kuvuka mipaka ya uzushi katika imani. Hebu tuangalie kwa undani kwa nini wana-maombi ni wazushi. Tuanze kwa kuangalia uhusiano kati ya Mama Bikira Maria na Shetani. Tangu kuumbwa ulimwengu, Mungu ameweka uadui kati ya Shetani na Mama Bikira Maria, (Mwa 3:15). Kutokana na uadui huu hatutegemei hata mara moja kwamba siku moja Shetani awe mshiriki wa ukombozi pamoja na Mama Bikira Maria, kwani uhusiano kati yao ni wa uhasama. Tena uhasama mkali zaidi unaonekana kati ya uzao wa mwanamke na nyoka, (Ufu.12:1-4). Uadui kati ya mwanamke na nyoka ulianza katika Agano la Kale unapofikia upeo wake katika Agano Jipya. Huu ni uadui kati ya uhai na kifo. Mwanamke analeta uhai, Nyoka analeta kifo.Kwa hiyo tangu mwanzo wa dunia Shetani/Nyoka anasimamia mauti. Mungu alimkomboa binadamu kutoka mauti hayo kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo aliyezaliwa na Mwanamke. Kwa jina la Yesu Kristu Wakristo wanaweza kutoa pepo na kufukuza mashetani. Hii ni kusema kuwa Mungu na shetani hawawezi kujenga ushirika. La sivyo, tendo la ukombozi lingekuwa kazi bure. Kama Mungu anaweza kumwamuru shetani atende matendo ya wokovu wetu, basi hapangekuwa tena haja ya kukombolewa kutoka utumwa wa Shetani maana Shetani angelikwua rafiki yetu.

Kwa kuhitimisha barua yangu kwenu, napenda kusisitiza kuwa suala linaloongelewa na Kaoma halina msingi wa kiimani, bali lina msingi wake katika uzushi.

Tendo la kupiga magoti au kusimama wakati wa kupokea Ekaristi Takatifu linahusu taratibu katika ibada, kamwe sio la kiimani. Na kuhusu jambo hilo, Mtaguso Mkuu wa II wa Vatikani unasema bayana kuwa Papa peke yake, kwa Kanisa zima, na Askofu peke yake kwa jimbo lake, ana mamlaka ya kubadili liturujia, hakuna mtu mwingine anayeweza kubadili.

Liturujia ni ibada ya Kanisa, taifa la Mungu, ni ibada ya wote pamoja wakiongozwa na Mchungaji wao kwa kumsifu Mungu kwa pamoja. Hakuna anayefuata matashi yake. Kwa hiyo, tunamshangaa Kaoma, iwapo Mchungaji Mkuu kwa mamlaka yake akitekeleza jambo la kichungaji kwa ajili ya watu wa Mungu, inakuwaje yeye asikubaliane naye?

Kwa hiyo kumlaumu Askofu wa Jimbo kwa kutenda kwa kadiri ya mahitaji ya Kanisa, ni kwenda kinyume na mamlaka ya Kanisa iliyosimikwa kihalali katika msingi imara wa Yesu Kristo. Kwa maneno mengine mtu wa namna hii sio Mkristu.

Na wala Kaoma asidhani ataashawishi wajumbe wa Baraza la Wakei katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam waache imani ya kweli na kufuata uzushi. Yeye na wenzake wenye imani sawa naye watabaki daima wazushi.

Ndimi wenu,

MWENYEKITI WA BARAZA LA WALEI

PAROKIA YA MBAGALA.