KAULI YETU

Tunapaswa kutii mamlaka

Kati ya mambo ambayo hutiliwa mkazo sana katika maisha ya kila jamii ni tabia ile ya wanajamii kuwa watii kwa wakubwa wao ambao wamewekwa kihalali kwa ridhaa yao. Hivyo raia hudaiwa utii kwa viongozi wao wa serikali, nao wanachama pia wa kila chama hudaiwa utii kwa viongozi wao wa hivyo vyama. Waumini katika kila dhehebu la dini nao hudaiwa utii kwa hao viongozi na wachungaji wao. Wakati kijana wa kikatoliki anapopewa upadre hutoa ahadi mbele ya Askofu wake. Huulizwa hivi: "Unaniahidi mimi utii na pia kwa waandamizi wangu?" Kijana hujibu kwa nguvu kabisa:"Naahidi’.

<GFIRST 11.35>Huko mashuleni, wanafunzi nao hudaiwa kwa vikubwa kabisa utii kwa walimu na walezi wao. Nako huko jeshini na mahala pote pa mafunzo ya kijeshi hudaiwa utii. Kwa kifupi binadamu mwenye kuishi chini ya uongozi uwao wo wote ule anadaiwa utii. Kwa kawaida kila ukaidi huwa na adhabu yake. Mahali pale ambapo hakuna utii huwa ni mahali penye fujo na machafuko. Kwa hiyo kila mwenye kumkaidi mkubwa ambaye ni halali anapaswa kuadhibiwa kisheria na huyo mkubwa au jamii iliyomweka huyo mkubwa.

Kwa muda hadi sasa kumekuwa na tatizo la waumini wanaojiita ni kikundi cha "Wanamaombi". Kikundi hicho kinaongozwa na Padre Felician Nkwera kikifanya ibada na mikesha ambayo mara nyingi huongozwa na Padre huyo. Padre Felician Nkwera ni Padre wa Jimbo la Njombe. Kwa sababu za kinidhamu, Padre Nkwera alikuwa amesimamishwa kutoa huduma za kipadre na Askofu wake wa Jimbo la Njombe. Ilitegemewa kuwa Padre Nkwera angemtii Askofu wake na hivyo kubakia mtulivu katika Jimbo la Njombe. Lakini kwa bahati mbaya Padre Nkwera hakutaka kubakia katika Jimbo lake, akaondoka na kufika Dar Es Salaam ambako amekuwa akitoa huduma mbalimbali kwa waumini kama vile kuongoza ibada hizo za wanamaombi na shughuli nyingine za kidini ambazo huzifanya bila kuwa chini ya mamlaka ya Askofu. Hilo likiwa ni jambo la kukosa utii kwa mamlaka ya Kanisa Katoliki.Pia ni tendo linalopingana na ahadi ile ya upadrisho wake.

Kwa kifupi tunasema kuwa Padre Nkwera amekuwa ni mkaidi kwa Askofu wake ambaye alimwahidia utii siku ile alipowekewa mikono kama padre. Jambo linalofuata ni kukosa utii pia kwa wale wanaomfuata hasa hao wanaojiita wanamaombi. Kwa hiyo tunasema kuwa kosa la Padre Nkwera ni kutomtii Askofu wake, na pia kosa la hao wanamaombi ni kwenda kupokea huduma kwa padre ambaye ni mkaidi kwa Askofu wake. Tunasema kuwa tatizo siyo katika kupiga magoti au kusimama wakati wa kupokea Ekaristi takatifu, bali hao wanamaombi hutambulikana kwa ukaidi wao wa kupiga magoti wakati wa kupokea Komunyo takatifu.Kwa hiyo ni tendo la kupiga magoti ni moja kati ya ishara zenye kuwatambulisha hao wafuasi wa Padre Nkwera, ambao ni wanamaombi.

Wafuasi wa Padre Nkwera au wanamaombi wanajulikana sana na pia hawapendi kujificha kwani wanaona kuwa huo ni ufiadini ingawaje ni ukaidi. Tunapenda kuungana na uongozi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam kuwaona hao wenzetu ni wakaidi kwa viongozi wa kidini. Tungependa kuwaambia kwamba ni jambo baya sana kushupaa katika udaidi wao. Pia kwa mtindo huo wanawaingiza katika matatizo watoto wao kwani hawawezi kupata huduma kama vile ubatizo, maungamo, na huduma nyingine ambazo waumini wakatoliki huzipata kutoka kwa mapadre na jumuiya za kikristu. Ni jambo linalosikitisha kumwona mwumini akienda mbele kanisni kupokea Ekaristi takatifu na kurudi bila kupokea naye akijisadikisha kuwa Kristu ameingia moyoni mwake. Hayo kusema kweli ni mafundisho na imani potofu kabisa.Ni vema kabisa yakasahihishwa mara moja.

Tungependa kabisa Padre Nkwera awe mnyenyekevu na hivyo awe tayari kwenda kwa Askofu wake na kumwomba radhi. Ni matumaini yetu kuwa Askofu wa Jimbo la Njombe atakuwa tayari kumpokea huyu Padre wake na kumrudisha katika kundi la Mapadre wake wapenzi. Pia tukijua kuwa tunakaribia ile Jubilei Kuu ya Ukristo wetu, tunawasihi hao wanamaombi wafanye utafiti nao wageuza mwenendo wao wakarudi katika kundi lao ili waweze kujiandaa vema kwa hiyo Jubilei Kuu na wasiendelee kuonekana kama viroja katika Kanisa wanaponyimwa huduma zilizo haki yao katika Kanisa. Pia kwa wale waumini ambao wako katika kundi bado ni wajibu wao kuwarudisha hao ndugu wanamaombi ingawaje tunavyowafahamu wamebobea katika ukaidi. Hata hivyo tunaamini kwamba neema ya Mungu hushinda ukaidi. Tuzidi kuwashauri na hasa kuwaombea ili wageuke na kuona kuwa utii ni wa lazima katika kumfuata Kristu, kwani yeye mwenyewe alionyesha mfano wa utii kwa Baba yake na tunasoma kuwa "alikuwa mtii hadi kifo, kifo cha Msalabani’.

 

Bei za dawa zidhibitiwe

Mhariri Kiongozi,

Ni jambo lakusikitisha jinsi bei za dawa zinavyohitilafiana kwa kiwango kikubwa mno.

Ninaye mgonjwa wangu Muhimbili. Dawa nilizoandikiwa nilionyeshwa duka la dawa hapo hapo Muhimbili. Bei ya hapo ni shs. 12,000/- kwa Dozi aliyoandikiwa. sikuwa na hela. Hivyo nilikwenda nyumbani. Baada ya kupata fedha nikapitia duka la dawa lililopo mtaani na kupata kwa bei ya shs. 750/- tu. Naomba serikali ichunguze bei za dawa ama kwa vinginevyo tunaumia.

Wenu,

S.M. Ngunga (Baba Bure)

S.L.P. 7472, DSM

 

ITV Kulikoni?

Mhariri Kiongozi;

NAPENDA kutumia nafasi kidogo katika gazeti lako la kiongozi ili nitoe machache yahusuyo chombo chetu cha I T V , chombo hiki ni kizuri mno hasa ukizingatia habari tunazozipata na kuziona ( live) moja kwa moja.

Lakini jambo linalonikera na kunisisikitisha mimi, na pengine si mimi peke yangu ni pale mnapoonyesha vipindi vya burudani vyenye picha za mapenzi. Kwakweli jambo hili linatuachia sisi watazamaji tulivyoukubali utamaduni wa mtu mweupe na kusahau kabisa utamaduni wa mtu mweusi . Cha kusikitisha zaidi ni kwamba picha hizo zinaonyesha waziwazi mno hata wakati mwingine inakuwa vigumu kuangalia I T V mbele ya wazazi nk, Je, tunapozungumzia kumomonyoka kwa maadili ya jamii tunaliangalia jambo hilo? Je huu ndio wakati wa sayansi na teknolojia ?. Mwisho ninaomba waandaaji wa vipindi hivyo vya burudani kulitupia macho jambo hili. Kwa kufanya hivyio tutakua tumeliokoa Taifa kwa ujmla.

Scholar Mawalla ( mpenda Watoto)

kanisa Katoliki Moshi.