KAULI YA KIONGOZI

Kula na kulipa

Kwa kawaida kila mahali ambapo binadamu hupita ni sherti aache nyayo au alama fulani zenye kumtambulisha hapo kama alikuwepo mahali fulani. Alama hizo hujionyesha hasa kutokana na vitu vile alivyovifanya kila mahali alipoweza kuwepo na kuishi. Mambo hayo tunayashuhudia kwa wenzetu wale ambao waliishi kabla yetu. Tumerithi mambo mengi sana kwa wale wenzetu ambao walitutangulia kuishi hapa ulimwenguni. Hakuna mtu ambaye hajarithi kutoka kwa wale waliomtangulia, wawe ni wazazi au walezi, wawe ni majirani, wageni na wale wote ambao wamefanya mambo mbalimbali kwa ajili ya ulimwengu huu na hivyo yamekuwa kama ni vitu vya urithi kwa vizazi vingine.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa kila mmoja wetu ana deni la namna fulani kwa wale waliomtangulia. Kwa hiyo basi tunakiri kuwa tumekuta vitu vingi, na linalotakiwa kwetu sisi nasi yatupasa kuacha vitu vingi kwa vizazi vijavyo au kwa wale wenzetu wanaokuja nyuma yetu. Hivyo vitu ambavyo tunapaswa kuviacha ni sawa kama alama za kukumbusha uwepo wetu hapa duniani. Kwanza kabisa tungependa sana kuwapongeza wale wote ambao wamefanya kila jitihada ya kuacha alama fulani mahali pale ambapo wameishi na kushughulika.

Tukipitapita hapa na pale tunaona kuna majengo mengi mazuri ya zamani. Tukiuliza au tukisoma tunafahamu ni kwa juhudi ya mtu fulani jengo hilo limekuweko. Pia tunashuhudia mashamba makubwa sana ya miti hapa na pale. Hapo tunatambua kuwa kulikuwa na mtu ambaye alipanda miti hiyo na wengine wanaokuja nyuma yake basi tunakula matunda ya huyo jamaa. Kuna wanasayansi na wataalam ambao nao wametuletea mambo mengi mazuri katika ugunduzi wa vitu mbalimbali tunavyovitumia hivi leo kama vile vyombo vya usafiri, vyombo vya sayansi na tekinolojia kama vile compyuta na vinginevyo.

Kwa kifupi ni kwamba kuna mambo mengi sana yaliyofanywa na wenzetu ambayo sisi siku ya leo tunayafaidi. Hivyo hata hao waliotufanyia mambo tunayofaidika nayo siku ya leo, nao walikuwa wamefaidika kwa namna moja au nyingine na mambo yale ambayo wale waliotangulia walikuwa wameyafanya. Huo unakuwa kama mnyororo mrefu wa vitendo katika jamii. Kwa kuwa hakuna mmoja ambaye hajafaidika na cho chote kile kilichokuweko tunajikuta tunalo deni kubwa sana kwa hao wenzetu waliotutangulia na tunapaswa kulilipa hilo deni kwa njia mbalimbali.

Njia kubwa ambayo tunapaswa kuitumia katika kulipa deni hilo la urithi, ni ile ya kuwa tayari nasi kuwaachie wenzetu urithi fulani. Tunajua kuwa binadamu kama binadamu ni kiumbe mwenye akili, utashi, nguvu na karama nyinginezo ambazo sherti azitumie katika kutenda vitendo ambalimbali ambavyo vitamfanya akumbukwe na pia yeye mwenyewe awe kama vile amelipia deni kwa ajili ya kufaidika na yale ambayo alikuwa ameyakuta na kuyatumia bila kuyatolea jasho. Kwa hiyo kila mmoja anapaswa kujiuliza daima: Je, ni mambo gani nimeyakuta mbele yangu na nimefaidika nayo? Na swali la pili la kujiuliza ni Je, mimi ninaacha kitu gani kama urithi kwa wenzangu watakaonifuata? Tunazo nafasi nyingi sana za kuweza kufanya vitu ambavyo vitakuwa kama urithi kwa wenzetu wanaotufuata.

Tunapaswa pia kufanya mabadiliko fulani mahali pale ambapo tuaishi au kushughulika.Ni jambo la aibu kuona mtu ameishi au kufanya kazi mahali fulani kwa muda mrefu sana, lakini hakuna kitu anachokiacha wakati akiondoka mahali hapo. Kwa mfano mtu anashindwa hata kupanda mti mmoja ili wale watakaokuja nyuma yake waweze kumkumbuka. Mara moja nilisikia ndugu zangu wakizungumza kuwa hata kama huwezi kufanya cho chote cha pekee, basi walao badilisha tu ule mpango wa vitu katika nyumba ambayo unaishi au kushughulika.Tunao watu ambao hawana habari ya kufanya chochote kile cha mabadiliko, ingawaje nafasi ya kufanya hivyo wanayo.

Jambo ambalo tungependa sana kuwahimiza katika Kauli Yetu ya leo ni kwamba kila mmoja wetu analazimika kufanya kitu fulani kizuri na cha kuleta faida kwa wengine. Lakini ni jambo la kusikitisha mno kuona kuwa badala ya kuacha urithi kwa wenzetu, hatufanyi hivyo tu bali tunakuwa hata waharibifu wa yale ambayo tumeyakuta na hata tukafaidika nayo.Je, kama hao wenzetu waliotutangulia wasingekuwa watunzaji na wazalishaji na vitu ambalimbali tungekuwa navyo hivyo tulivyo navyo siku ya leo? Kwa hakika kabisa sivyo.

Tatizo kubwa sana tulilo nalo hasa sisi Watanzania kwa ujumla ni lile la kutotilia maanani vitendo vya kujenga "majina" katika jamii yetu. Wengi wetu hutafuta tu faida binafsi na tena ya hivi sasa tu. Lakini kumbe tunapaswa kuacha alama za utendaji katika jamii yetu na hivyo watu waweze kuona na kutambua kuwa na sisi tulikuwepo hapa ulimwenguni. Kuna vitu vingi sana na ambavyo ni rahisi mno kuvitenda, lakini vitadumu katika kumbukumbu za watu. Ni vema basi tukaanza kufanya vitu ambavyo vitatuletea ukumbusho hapo baadaye, lakini pia vikiwa ni kama malipo kwa urithi ule tulioupata kutoka kwa wenzetu. Tunaweza kwa mfano kupanda miti, kujenga cho chote kile, kuwasomesha watoto, au kutoa misaada ya kujenga shule, zahanati, makanisa na mahali penginepo pa ibada.

Tuwaige wale wenzetu wa Ulaya na Marekani au mahali penginepo ambao hutoa michango ya hali na mali katika kujenga majina yao kwa njia hiyo na papo hapo wakiweka ukumbusho wao katika vitu hivi.

Tusiwe watu wa kula tu mali iliyozalishwa na wengine bila sisi wenyewe kuzalisha chochote kwa ajili ya vizazi vijavyo. Hapo tunapaswa kweli kuona aibu kama tumekula bila kuzalisha. Lazima tukumbuke daima ule msemo usemao kwamba ni "kula na kulipa", vinginevyo si vizuri katika maisha yetu sisi binadamu wenye roho na mwili na wenye akili na utashi pamoja na nguvu nyingi za kutendea kazi.

 'Waamini wapunguze jazba sehemu za ibada'

Ndugu Mhariri,

NAOMBA unipe nafasi ya kutosha ili walau leo nipate kuzungumzia mawili matatu ambayo ninaona yamewachanganya akili waamini wenzangu.

Nimejaribu kusoma kwa makini maoni ya Gazeti la Mtanzania toleo Na. 1165. Maoni hayo yalikuwa na kichwa hicho hapo juu. Maelezo ya maoni hayo na hitimisho lake ni vitu vinavyopingana na hivyo kuleta upotofu kwa wasomaji wengi wasiojua undani wa tatizo lililozungumziwa. Naomba nitoe dukuduku langu nikiwa mwamini mkatoliki.

Si kweli kwamba tofauti ya waamini Wakatoliki na waamini wanamaombi, ni NAMNA YAO YA KUFANYA IBADA KAMA ILIVYOANDIKWA. Tofauti yao ni imani zao. Hapa ndipo tatizo linapoanza. Sehemu moja mwadhimisha wa ibada moja anaongoza watu wenye imani tofauti. Ni wazi tokeo lisiloepukika ni fujo. Kama ulisoma waraka wa Baraza la Maaskofu Tanzania ulioitwa "Tahadhali Juu ya Udini Mkali na Upotofu Katika Kanisa Katoliki Tanzania",unaeleza tofauti hii ya imani. Wakati sisi wakatoliki msingi wetu wa imani ni Ekaristi Takatifu na Neno la Mungu, wanamaombi wanaamini katika Ekaristi na Mama Maria .

Tofauti ya msingi wa imani si kitu kidogo . Imani isiyo na msingi yaweza kupeperushwa na upepo wa nyakati, kipaji cha mtu au hata na misukumo ya siasa na uchumi tu.

Kwetu wakatoliki tuna kila sababu ya kulinda imani yetu bila, hivyo tusingekuwepo leo hii. Historia ya Kanisa inaonesha hili.

Kutofautiana kwa namna ya kufanya ibada kunakotangazwa sana ni ishara ndogo kabisa ya nje ya tofauti kuu ya ndani. Mfano halisi ni kupiga magoti wakati wa kupokea Ekaristi Takatifu. Maongozi ya Kanisa yanatoa uhuru kwa viongozi wa mahali kuamua namna ya kupokea; iwe kusimama, kulala (mfano mtu akiwa mgonjwa), kukaa au kupiga magoti .

Jimbo kuu la Dar Es Salaam limekataza kupiga magoti si kwa sababu tendo hilo ni dhambi, lakini kwa kuwa ndicho kitambulisho rahisi cha wale waliokengeuka kiimani.

Wanamaombi wao wanachukulia tendo la kupiga magoti kuwa ndicho kitendo pekee cha utakatifu na kuabudu , kiasi kwamba kinyume chake ni kukufuru .

Huu ndio udini mkali. Wenyewe kwa mtazamo wa kikatoliki, ishara au tendo la nje linapokuwa ndilo lengo la ibada na si njia au kichocheo. Tendo la nje halisi ni ishara tu ya hali ya ndani ya mwamini.

Mimi naamini kuwa watu wengi wanaishia hapa katika kupiga magoti. Wale wanaojitambulisha kuwa Wanamaombi, lakini kumbe ni wafuata mkumbo tu. Hata wale wanaojipachika nafasi ya kuwa wasemaji wao, naogopa nisimhusishe mhariri, japo maandishi yake hayapo mbali na ukweli huu.

Kama kumpokea Yesu Kristo hakutenganishwi na kupiga magoti, ingefaa hata pale tunapompokea katika Neno lake, wakati wa Injili wangelazimisha kupiga magoti. kwani Yesu ni yule yule katika Ekaristi Takatifu na katika Injili Takatifu.

Maoni yake yamejaribu kutusadikisha kuwa chanzo cha sakata ya Magomeni ni mwadhimisha ibada kugundua kuwepo kwa watu waliotengwa na Kanisa Ugunduzi huu ulifuatia amri ya kuondelewa kwao kanisani. Kitu kilichokifumbiwa macho ni ushupavu na ukaidi wa watolewa nje. Wao wanafahamu fika kuwa hawapaswi kuhudhuria ibada Katoliki . Aidha walitumia ujanja kukwepa kizingiti kilichopo nje kilichokuwa kinahakikisha kuwa hawaingii ndani ya Kanisa . Yote haya yanaonyesha kuwa lengo lao halikuwa ibada bali kuleta fujo na inaonekana wamejiandaa kwa hilo.

Mimi nakubaliana na mhariri kuwa dini zote zapaswa kuwa na uvumilivu. Tatizo ni aina gani na kwa sababu gani uvumlivu uwepo . Nikiwa ni mkatoliki , Bwana na Mungu wangu aliyeniambia kuwa"Mimi ni Njia,Ukweli na uzima"alifanya tukio moja siku moja alipokwenda hekaluni Yerusalem: "Basi, akawakuta mle hekaluni watu wakiuza ng’ombe kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa katika meza zao

Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya hekalu pamoja na kondoo na ng’ombe wao, akazitawanya sarafu za wenye kuvunja fedha na kuzipindua meza zao.

Akawaambia wale waliokuwa wanauza"Ondoeni vitu hivi hapa. Msifanye nyumba ya baba yangu kuwa soko!’Wanafunzi wake wanakumbuka kwamba Maandiko yasema :"Upendo wangu kwa nyumba yako waniua"(Yoh.2:13-17). Uvumilivu hata siku moja usiwe sababu ya kuachia mambo msingi ya imani ya mtu kuenda mrama. Kuna nguzo msingi wa imani ambazo hazipaswi kuchezewa. Nguzo hizi zinapaswa kulindwa kwa kila hali na hasa na viongozi wa dini ili kudumisha utakatifu wa imani husika.

Kanisa Katoliki lina kanuni zake zinazoliongoza, moja ya kanuni hizo inazungumzia juu ya mtu aliyetengwa , tuone kanuni 1331 na vipengele vyake vichache, tafsiri ni yangu:Kan1331&1 Mtu aliyetengwa anazuiwa:

1. Kuwa na ushiriki wowote wa kihudumu katika adhimisho la sadaka ya Ekaristi au katika adhimisho lolote rasmi.

2.Kuadhimisha sakramenti na visakramenti na kupokea sakaramenti.

3.Kushika ofisi, huduma au kazi yoyote au kutenda tendo la utawala.&2 kama kutengwa kumewekwa au kutangazwa, aliyetengwa:

1.Anayetaka kwenda kinyume na &1,1 hazuiwi kufanya hivyo au la; tendo la kiliturjia lisimame kama hakuna sababu nzito ya kuingilia.

Bila shaka waamini wa Magomeni hawakuwa na sababu yoyote ya kutaka ibada yao isimamishwe kutokana na ukaidi wa wapenda fujo.

Mimi sitetei hali yoyote ambayo inasababisha watu kuvaa maungoni . hata kiongozi mhusika ukimuuliza hatakujibu hivi. Lakini kuzuia hili, pande mbili zinazohusuika zinabidi zote zijiheshimu zipende amani ukimfukuza akafika ukingoni atakugeukia na kujitetea, japo hapendi na hana uwezo.

Mtu anaweza kujiuliza mbona wakatoliki mnawaruhusu Wakristo wa madhehebu mengine, Waislamu na wasio na dini inayofahamika rasmi na hata wakana Mungu, iweje leo hawa ndugu zetu wanamaombi mnataka kuwaweka mbali nanyi? Kutengwa ni adhabu maalum katika Kanisa Naomba nirudie maneno ya ufafanuzi wa Waraka wa Maaskofu nilioutaja hapo mwanzoni ufafanuzi huu ulitolewa na Halmashauri ya Parokia ya Mt.Yosefu. "Adhabu ya kutengwa ni adhabu maalum katika Kanisa ambayo imewekwa si kwa madhumuni ya kumkomoa mtu, bali kumrekebisha mhusika , ni adhabu inayolenga kumdhihirisha mjitenga na Kanisa uzio wa uovu wake hivyo kumsukuma aweze kujirudi , kujuta na kutubu.

Kama mtengwa ataendelea tu kubaki katika ibada kuna hali ya kujiona kuwa ni mmoja wetu. Hali hii ni potovu kwani yeye amekengeuka kiimani na kimaadili, kutokana na uzushi wake wa kiimani, kukashifu viongozi wa kanisa , kuleta fujo wakati wa ibada na hasa kukosa utii.

Mwenye mapungufu haya anakuwa tayari ameshajiweka mbali na Kanisa Katoliki"

Mhariri alisema kuwa hamshutumu Padre wa Parokia ya Mashahidi wa Uganda Magomeni, alikuwa anajaribu ‘kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa’ toka mwanzo wa maoni yake ndicho kitu alichokuwa akikionesha.

Amedhihirisha tuhuma yake kwa kusema kuwa amekosa uvumilivu, uadilifu wa kichungaji, moyo wa kusameheana na kujisahau kuliko mpelekea kutoa maamuzi ya jazba. Kanisa limeonesha uvumulivu mkubwa toka mwaka 1985 mpaka mwaka huu lilipoamua kutoa uamuzi rasmi. Kama njia ya kistaarabu Magomeni wamezichukua, walichokiita ujanja wa wahusika ndicho kilichopelekea hali iliyotokea. Mhariri nilitegemea pia ukumbushe kwa wahusika kama ni Wakatoliki wafuate maagizo na kanuni za kikatoliki kama hawawezi basi ni vyema kuendelea na makanisa yao kule Ubungo River Side.

Katika ukurasa wa mbele wa Gazeti husika kichwa cha habari kilisema; "Pamoja na Kupigwa, Wanamaombi kuendelea na ibada makanisa Katoliki" uzito na ushupavu wa kauli hii, mhariri hakuiona makusudi ndio maana hakugusa neno lolote juu yake.

Viongozi wa dini wanaitwa wachungaji na huu ni kweli. Kuwa mchungaji hakumaanishi kuacha mifugo yako ipotee au iharibu mazao ya watu. Mchungaji anayeipenda mifugo yake hutembea na fimbo mzaburi anasemaje juu ya hili:’

"Nijapopita katika bonde la giza kuu sitaogopa hatari yoyote, maana wewe ee Mwenyezi Mungu u pamoja nami gongo lako na fimbo yako yanilinda"(23:4).

Ninaamini kuwa vyombo vya habari mna nafasi ya pekee katika kuitunza amani ya jamii yetu, Lengo hili mtalitekeleza vyema mkizingatia ukweli wa pande zote zinazowajibika kuitunza amani nchini.

Padre Stephano Kaombe,

Dar es Salaam