Make your own free website on Tripod.com

KAULI YETU

 

Vitisho Zanzibar ni utaahira wa demokrasia

 

WIKI iliyopita, zilisikika habari za kushangaza kuwa, zoezi la kuandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu, linazidi kutawaliwa na vitisho vinavyoongezeka kila kukicha.

Taarifa hizi zilibainisha kuwa, miongoni mwa vitisho hivyo vya kipumbavu, ni pamoja na vile vinavyodai baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa, wakatwe vichwa.

Vitisha hivyo, vinadaiwa kutokea katika eneo la Ole, Wete.

Inadaiwa kuwa vitisho hivyo vilitokea katika siku ya mwisho ya uandikishaji wa watu katika dafrari la kudumu la wapiga kura katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Hatua hiyo ilifuatia kuzuiwa kwa baadhi ya watu waliodaiwa kutokuwa na sifa za kujiandikisha.

Kuna taarifa kuwa, polisi wamemtia mbaroni mmoja wa watu wanaodaiwa kuhusika na vitisho vya kumkata kichwa kiongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kiuyu, Bw. Yahaya Salimu.

Vitisho vya mtuhumiwa huyo kwa kiongozi wa Serikiali ya Mtaa, vilitokana na yeye kuzuiwa kujiandikisha akidaiwa kuishi mkoani Tanga kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi mfululilizo, hali inayodaiwa kumuondolea sifa ya kujiandikisha.

Si huyo tu anayeshikiliwa kwa madai ya kufanya vitisho katika zoezi hilo, bali pia Hassan Kombo (29) anayetuhumiwa kupuliza baragumu kwa lengo la kuwaita watu ili wavamie kituo cha Mjini Ole na kumdhuru kiongozi wa Serikali ya Mtaa.

Kama kwamba hiyo haitoshi, vitisho kama hivyo pia vimetolewa kwa kiongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kangagani, Bw. Fakihi Omar Yusuf ambaye nyumba yake iliteketezwa kwa moto katikati ya juma.

Bado wapo baadhi ya watu ambao tuseme hawafamiki sawasawa kama wana matatizo ya akili, ambao kwa akili zao waliamua kuwakata miguu ng’ombe wanne wa Bw. Mshindo Bakari. Watu hao hawajafahamika hadi tunapoandika KAULI YETU.

Sisi tunasema, kitendo cha kutoa vitisho kwa watu kwa sababu ambazo mtu mwenye akili timamu anaweza kuzipatia ufumbuzi tena kwa gharama nafuu kabisa, ni utaahira wa demokrasia na kubwa zaidi, utaahira wa akili.

Ni jambo la ajabu kujichukulia sheria miokononi katika nchi ya kistaarabu inayosisitiza utawala bora wa sheria, eti kumtishia Mtanzania mwenzako kumkata kichwa na kuweka alama za X katika nyumba za baadhi ya watu wakiwamo viongozi wa serikali za mtaa.

Tunasema, mtu kama huyo na yule anayepiga baragumu kuita watu kufanya machafuko kwa hoja za kipumbavu, ni ukichaa na ni vichaa pekee wanaoweza kuitikia mbiu hiyo lakini, si watu wenye akili tikamu.

Tunasema ni utaahira kwa sababu mtu mwenye akili timamu hawezi kuamua kuchoma nyumba ya mtu kwa ajili ya uandikishaji wapiga kura.

Linalothibitisha ukichaa huo ni swali kuwa, ukiwateketeza watu, utamchagua kiongozi ili akuongoze wewe na nani kama sio kubaki peke yako ambae sasa unabadilika na kuwa mtumwa?

Sisi tunaamini kuwa wanaoshiriki kudai haki kwa kutumia upumbavu, wao wenyewe ni wakukwaji wakubwa wa haki za binadamu ikiwamo hii kubwa ya KUISHI na kuwa katika hali ya AMANI na USALAMA.

Bado tunasema vitisho vya namna hiyo ni vya wendawazimu kwa sababu hata kitendo cha kuwakata miguu ng’ombe wasiojua siasa ni nini au kiongozi anachaguliwaje, kinaonesha kuwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa, ni wendawazimu wanaojificha katika kivuli cha siasa ili waishawishi jamii kukubaliana na wendawazimu wao.

Sisi tunasisitiza kuwa, watu au wanasiasa wenye mwelekeo wa siasa na demokrasia za kitaahira kama hizo, hawana budi kujua kuwa Watanzania si vichaa kiasi cha kuburuzwa na siasa za vichaa kama hizo eti kwa kisingizio cha kudai haki na demokrasia.

Kwa mantiki hiyo, tunawasihi watumishi wote wa dola na jamiii kwa jumla, kutowaruhusu vichaa hao wa siasa, kutuchafulia jina na kutuingiza katika mkumbo huo wa demokrasia ya kitaahira.

Tuwakemee kwa nguzu zetu za pamoja kwa matendo na hivyo, kuwachukulia hatua kali za kisheria wote wanaobanika kutaka kuibadili Tanzania kuwa machinjio ya watu.

Umefika wakati sasa Jeshi la Polisi likaacha kusubiri madhara kwanza, bali litumie vijana wake hususan askari kanzu, kuwachunguza na kuwavuta mmoja mmoja, wote wanaoandaa mipango michafu kama hiyo hata kama hawajafanikisha au kuanza maana, ni heri kinga kuliko tiba.

Tunaamini hili likifanyika kwa misingi ya haki pasipo uonevu au kutafuta maslahi binafsi, kuna uwezekano mkubwa wa kuondoa chuya katika mchele mzuri tulio nao ili wakati wa karamu ya uchaguzi, basi uwe ni uchaguzi huru na wa haki.

Sisi tunasema, Watanzania wote wakitambua umuhimu wa kustarabika katika mchakato mzima wa uchaguzi, basi wajue itakuwa ni njia nzuri ya kuwabaini wajanja waliopo madarakani wanaoweza kufanya jaribio la kupindisha mazingira sahihi ya uchaguzi ili wakae madarakani maana wataonekana wazi hata kwa vipofu.

Ndiyo maana tunasema, VITISHO ZANZIBAR NI UTAAHIRA WA DEMOKRASIA NA TUKIUCHEKEA, TUTAVUNA MABUA.

 

 

BARUA

Mkapa mlete Makamba mkoani Mara

Ndugu Mhariri,

 

SISI wakazi wa Mkoa wa Mara hususan wilaya ya Tarime, tunamwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, atuletee Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Luten Yusufu R. Makamba ili aje kutusafishia mkoa huu.

Tunasema hivyo tukiwa hatuna maana kuwa hatuna Mkuu wa Mkoa au aliyepo hafai, la hasha; anafaa sana lakini, tunaamini kwa kazi ambayo tumekuwa tukimsikia Makamba akiifanya katika mikoa aliyopata kufanya kazi ukiwamo huo anaotumikia sasa wa Dar es Salaam, tunaamini kuwa akija huku, Mkoa huu UTATULIA.

Tunasema hivyo kwa kuwa hadi sasa mkoa huu unayo matukio ya ajabu, ya kutisha na ya kushangaza.

Mfano hai wa matukio hayo, ni mapigano ya mara kwa mara ya kikabila baina ya koo za Wanchari na Walenchoka. Hatujui ni kwanini hadi sasa dawa ya kudumu haijapatikana.

Lingine, mkoa huu inaonekana umekaa katika viganja vya baadhi ya watu wachache wenye nguvu za kiuchumi.

Matajiri wana sauti kuliko Serikali na ndiyo maana wanaamua kufanya mambo mengi ya ajabu, wanaogopwa na kutukuzwa kama miungu.

Hii yote ni dalili kuwa, kuna mapungufu fulani katika umakini wa kushughulikia mambo miongoni mwa serikali ya mkoa na wilaya zake sambamba na vyombo vya dola.

Tunamuomba Makamba kwa sababu kwanza Makamba haogopi mtu, bali anachosimamia ni ukweli na haki.

Tunaamini Rais Mkapa akisilikiliza kilio chetu, matatizo yasiyo na kichwa wala miguu, lakini yanayotikisa Mkoa wa Mara ukiwamo ujambazi, mapigano na uonevu hususan hapa wilayani Tarime, yatapungua.

Tunasema yatapungua kwani kama sisi wananchi wenyewe hatutaona umuhimu wa kutoa ushirikiano wetu wa dhati kwa kiongozi, sio rahisi yeye mwenye kwa kuitwa KIONGOZI, akamaliza matatizo; lazima apate ushirikiano wa dhati.

Tunamuomba Mheshimiwa Rais Mkapa asikilize kilio chetu na kukipa maanani.

 

WAPENDA AMANI NA MAENDELEO,

WILAYA YA TARIME.

MARA

Sauti ya kondomu inanuka

 

Ndugu Mhariri,

 

NAOMBA unipe nafasi kidogo kando ya gazeti lako la KIONGOZI ili nitoe dukuduku langu juu ya namna vijana wetu wanavyopotoshwa na mafundisho potofu kuhusu kondomu.

Ukifungua radio nyingi au vituo vya television zetu nyingi nchini, hutashangaa kusikia wingi wa matangazo yanayosisitiza matumizi ya kondomu eti ili kujikinga na maambukizi ya UKIMWI yakiwamo yale matangazo yanayosema, USIONE SOO; TUMIA KONDOMU”.

Sasa mimi nimekuwa nikijiuliza kuwa, Je, hizi kondomu ndizo leseni ya UZINIFU yaani, ni nini? Wapo vijana wengi katika jamii wanaopewa leseni za kuendesha magari na baada ya kuziweka mifukoni wakishapata magari ya kuendesha, tazama yanatokea huko barabarani namna ilivyo fujo na hata wanavyoangamia na kuangamiza maisha ya wengine.

Hata hivyo, inashangaza kuona baadhi ya watu wamekifanya kitu hicho kuwa cha kutamkatamka ovyovyo tu, ingawa kinatia kichefuchefu.

Inashangaza baadhi ya watu na asasi badala ya kuwafundisha vijana kujiheshimu na kujizuia dhidi ya vitendo vya uasherati kwa kufuata maadili ya Kimungu, wanaamua kufanya biashara kwa kusisitiza matumizi ya kondomu huku wakijua zinaangamiza watu kiroho na kimwili.

Viongozi wa baadhi ya dini wakiwamo wa Kanisa Katoliki wamepigana sana vita kukabiliana na utumiaji wa kondomu ambazo siku hizi hata vijana wenyewe, wameamua kuziita majina ya kejeli kama vile matumbo ya kuku kwa kuwa hayaliwi, bali hutupwa.

Ni wazi kuwa kama viongozi hawa wasingekuwa imara, wangehalalisha dhambi ya uzinzi ambayo ni hatari zaidi kuliko hata UKIMWI wenyewe kwani inaathiri si tu mwili, bali hata roho.

Mungu wakati wa uumbaji, aliwaagiza binadamu wazae wakaongezeke na kuijaza dunia. Mwanaume alizawadiwa mbegu za  yai la kizazi ili iungane na yai la kike na kutunga mimba ambayo kwayo, binadamu anazaliwa na kuishi kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu.

 Sasa je, ni mbegu kiasi gani zinajazwa kwenye hayo makondomu na kutupwa nje jalalani? Huo ndio ulikuwa mpango wa Mungu?

Inashangaza kuona hata baadhi ya akina baba ndani ya ndoa zao takatifu, wanaambatana na kondomu; hii ni hatari na aibu kubwa. Ahadi ya uaminifu katika ndoa iko wapi ?

Naomba jamii nzima iepukane na mitazamo duni ya kuthamini kondomu na badala yake, watu watii Amri za Mungu ikiwamo ile inayozuia KUZINI. Hii ndiyo njia pekee ya kuzinusuru roho pamoja na miili ya watu ili vitu hivyo, visipatwe na UKIMWI.

 

Peter Nolasco,

Parokia ya Kilema,

S.L.P. 3041,

MOSHI.

 

 

 

 

TAFAKARI YA WIKI

 

Hakuna njia ya mkato

 

MFANYABIASHARA mashuhuri aliyempeleka mwanae kuanza masomo katika Chuo Kikuu maarufu jijini Washington alitikisa kichwa chake kwa masikitiko makubwa alipopitia muhtasari wa masomo ambayo mwanae anapaswa kujifunza na muda anaopaswa kukaa chuoni.

"Je ni lazima achukue masomo yote haya?  akamuliza Mkuu wa Idara ya kuandikisha na kupokea wanafunzi.

"Je huwezi kumpunguzia masomo ili kozi yake ichukue muda mfupi zaidi? Maana mwanangu anataka amalize masomo mapema"."Ni kweli anaweza kuchukua kozi fupi" akajibu Mkuu wa Idara hiyo ya Kupokea Wanafunzi wapya na kuongeza, "Inategemea kuwa kijana wako anataka kuwa nani baadaye. Mungu anapotaka kuwa na mbuyu anaupatia hata miaka mia mbili ili ukue katika mazingira yake magumu lakini, akitaka kuumba mchicha huchukua majuma matatu nao unakuwa tayari kwa matumizi ya binadamu".

Hakuna asiyependa kupitia njia ya mkato ili kufikia lengo. Tena tuko huru kupitia njia ya mkato tukitaka; lakini kama vile mbuyu usivyoweza kumea na kukua kama mti mkubwa  kwa mwezi mmoja ndivyo na akili pamoja na tabia ya mtu yeyote ilivyo.

Kuurithi ufalme wa Mungu  na kumwona Mungu badala ya ibilisi na shetani  kwa upande mwingine kutategemea jinsi sisi tulivyojitoa bila kujibakiza kwa muda mrefu wa mazoezi ya kiroho bila kukatishwa tamaa na mabadiliko ya nyakati hizi.