Make your own free website on Tripod.com

KAULI YETU

 

Suala la wanasheria kuhusu takrima lizingatiwe

 

VYAMA  vitatu  vya wanasheria  nchini, vimewakilisha ombi Mahakama Kuu ya Tanzania vikitaka kufungua kesi ya Katiba ili Kifungu cha Sheria ya Uchaguzi kinachoruhusu takrima kifutwe.

Sambamba na ombi hilo lililowasilishwa mahakamani hapo Januari 6 mwaka huu kwa hati ya dharura, wanasheria hao pia wanaomba kutolewa kwa amri ya muda ya zuio, kuzuia matumizi ya takrima hadi hapo kesi itakayofunguliwa itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Vyama hivyo kama vilivyobainishwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini ni Kituo cha Sheria za Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Wanasheria  wa Mazingira (LEAT) na Chama cha Msaada wa Sheria (NOLA).

Katika hati yao ya kiapo cha pamoja, wakurugenzi watendaji wa vyama hivyo wanadai kuwa Kifungu cha 98 (2) na  (3) cha Sheria ya Uchaguzi Namba 4 ya 2000, kinakiuka Katiba  na hivyo kinapaswa kufutwa.

Sisi tunatoa pongezi zetu kwa vyama hivi kwa hatua hiyo, ambayo hakika lengo lake ni kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mtu anayetaka kugombea nafasi yoyote iwe wanaochagua au wanaochaguliwa.

Tunasema hivyo kwa sababu, kuzuia rushwa lakini takrima ikaendelea kuruhusiwa, ni sawa na kuudanyanya umma wa Watanzania, kwani hakuna cha maana kinachokuwa kimezuiwa kwa kuwa, hiyo ni sawa na kufanya mapinduzi ya kuondoa sultani, huku unaendeleza usultani wa aina nyingine.

Kwa maana nyingine, wagombea hao wanakuwa wamepewa ufunguo wa kuendeleza rushwa inayokuwa kwa jina jipya; eti badala ya rushwa, sasa inaitwa ni takrima inayotafsiriwa kuwa ni UKARIMU.

Tunaunga mkono hoja ya wanasheria kwa sababu, kwa kawaida ukarimu hautangazwi, tena eti nyakati za kampeni; kwanini isiwe nyakati nyingine?

Kutokana na hali hiyo, bado taifa litakuwa linaendelea kupata viongozi wasio na sifa zinazotakiwa kwani, watakaochaguliwa ni wale wenye uwezo mkubwa kiuchumi; wenye uwezo wa kutoa rushwa na kuificha ndani badala ya kuwa na uwezo na sifa za kutosha katika kuongoza wananchi waliowachagua.

Tunasema hivyo kwa vile hiyo takrima haitaji mazingira gani itolewe, vitu gani vitolewe kwa wapiga kura na kwa kiwango gani. Kinachoshangaza mintarafu hoja ya takrima ni kwamba, kwa nini wapiga kura wakirimiwe kutimiza wajibu na haki yao ya kidemokrasia?

Takrima haiwezi kutofautishwa na rushwa, mgombea atajinadi kwa wapiga kura wake kwa kuwapa vitu mbalimbali ikiwemo pesa taslimu, vyakula, mavazi na vitu vingine vya namna hiyo na vyombo vya dola vitashindwa kumchukulia hatua kwa kile atakachosingizia kuwa hiyo ni takrima kwa wapiga kura wake na si rushwa.

Ieleweke kuwa neno takrima, linatokana na ukarimu ambao mtu anaweza kumtendea mwingine, kutokana na ukarimu huo, mtendwa anaweza kutoa takrima kwa mtenda kama shukrani yake kwa mema aliyomtendea. Hiyo inaruhusiwa kabisa na inakubalika, lakini linapokuja hili suala la mgombea kutoa takrima kwa wapiga kura wake kabla ya uchaguzi, hii ni hongo.

Tunasema ni hongo kwa vile mgombea huyu takrima yake inakuwa haina maana kwa vile wapiga kura wake wanakuwa hawajampigia kura kumchagua, sasa kama hajachaguliwa anatoa takrima kama shukurani ya nini? Kwa mema yapi waliyomtendea kama siyo kujigonga kwao.

Tunasema kama takrima itaendelea kuruhusiwa, basi iwe ni baada ya uchaguzi   kwani hapo italeta maana kwamba mgombea huyo ambaye sasa atakuwa tayari ni kiongozi kutokana na ushindi aliyoupata baada ya kuchaguliwa, atakuwa anatoa takrima kwa wapigakura wake kama shukrani ya kumchagua kuwa kiongozi wao.

Kuendelea kuruhusu takrima wakati wa kampeni za uchaguzi, ni kuwakandamiza wagombea wasiokuwa na uwezo kifedha, ambao licha ya kujinadi kwa sera zao nzuri, lakini wapo katika hatari ya kushindwa kufuatia wenzao kuwa na fedha kwani huko wapigakura wao watawaambia “MKONO MTUPI HAULAMBWI”.

Tunasema, takrima ikiendelea kukumbatiwa, itatufanya tuamini kuwa ni sababu kama hizo za kutotaka kutenda haki kwa watu wa hali ya chini, ndiyo maana pia kukawekwa sheria kwamba, mgombea yeyote atakayetaka kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi, awe na kiasi cha shilingi milioni tano kwa ajili ya kufungua kesi hiyo.

Tunaunga mkono kwa kuwa tunajua mazingira ya Takrima kuruhusiwa, yana hatari ya kuzua manung’uniko au kesi zisizo za lazima za kupinga matokeo ya uchaguzi.

Ugumu wa hali hii utajitokeza katika masharti ya kufungua kesi hizo ambazo sio siri, yanaiyumbisha jamii na kulipotezea taifa mamilioni ya fedha ambazo zingetumika kuboresha huduma za kijamii.

Katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, vyombo husika havina budi kuhakikisha wanapatikana viongozi wenye sifa zinazotakiwa na hii itafanikiwa endapo suala la takrima kwa wagombea, litafutwa.

Ndiyo maana tunasema, tunaiomba Mahakama Kuu na vyombo vingine vya kisheria vizingatie suala hili lililoombwa na wanasheria nchini

 

BARUA

 

Barua ya wazi kwa Serikali

Mikoa ya kusini imesusiwa Kimaendeleo?

Ninaomba Serikali itazame kwa makini neno hilo.Kwa upande mmoja ni kweli “Mjenga nchi ni mwananchi, mjenga wilaya na mkoa ni mwananchi wa wilaya na mkoa ule.”Lakini kuna mambo au hoja leo Mkapa anaita miundo mbinu inayoharakisha maendeleo ambayo Mikoa ya Kusini imepunjwa.

Hoja zinazoonesha kususiwa kimaendeleo kwa mikoa ya Kusini ni pamoja na ukweli kwamba hadi sasa Mikoa ya Mtwara na Lindi pamoja na Wilaya ya Songea Ruvuma ina umeme wa jenereta tu wakati Wilayani Mbinga hakuna hata umeme wa genereta

 Umeme umetoka Kidatu mkoani Iringa jirani na mkoa wa Ruvuma, umeenda Dar es salaam na Zanzibar na mikoa mingine. Aheri ungekomea Dar es Salaam kama ni kwa hoja ya viwanda na maendeleo.

 Gesi ya Songosongo imechukuliwa Kilwa mkoani Lindi, ambapo hakuna umeme na kupelekwa Dar es Salaam!

 Watu wanazo nyumba nzuri zenye mastahili ya kupewa umeme, na siyo  vibatali vya magenereta vinavyozimwa ovyoovyo na TANESCO huku wakidaiwa hela bila usahihi wa matumizi ya umeme.

Mikoa ya Kaskazini kuna umeme hadi vijijini hata katika vijumba visiyo na mastahili. Lakini basi labda wajenga nchi ambao ni wananchi wapo Kaskazini tu.

Mikoa ya Lindi na Mtwara inalima na kuzalisha kwa wingi mazao ya Korosho, mpunga, mtama, nazi na ufuta. Wilaya za Songea na Mbinga mkoani Ruvuma zinazalisha kwa wingi mazao ya Tumbaku, Mahindi, Maharage, Ufuta, Karanga, ngano na Mpunga. Aidha, kuna  bandari muhimu ya Mbambabay

Songea kwenda Mbinga ni pafupi  lakini hakuna barabara ya lami wakati maendeleo ni makubwa sana.

Namshukuru na kumpongeza Rais Mkapa ambaye ameamua sasa kujenga barabara ya lami Mtwara “Corridor” ijengwe hadi Mbambabay mkoani Ruvuma, ambayo imefunikwa kwenye mafaili kwa miaka mingi. Wapo wachache ambao wamekuwa wakipinga jambo hilo la maendeleo.

   Kama huko mlikojenga barabara za lami na kupeleka umeme eti mlifanya    Hivyo kwa vile kuna viwanda, tazameni mali ghafi za watu hawa mnaowakosea haki.Wajengeeni nao viwanda ili wajengewe pia barabara za lami na wapate umeme wa kweli. Hatutaki sasa maneno ya “Serikali imeliona; tupo mbioni”.

Asilimia 90 ya NG’O na misaada yake inaelekezwa Dar es Salaam na mikoa ya Kaskazini. Kama lengo ni kusaidia maendeleo, ilibidi msaidie kulikobaki nyuma kimaendeleo. Wajengeeni kusini barabara za lami na umeme hao wapate matunda hayo kwa maendeleo ya watu na mikoa hiyo.

Kutotazama hayo na kutelekeza ni kama kusema mikoa ya Mtwara na Lindi iwe Msumbiji na wilaya ya Mbinga iwe Malawi.

Hata kama kwenye maamuzi ya mambo mengi nyeti, wapo watu wa Kaskazini amueni kwa busara mambo bila ubinafsi wala upendeleo na kuigawa nchi katika matabaka ya kimaendeleo.

 

    Padri Alois Nchimbi

 S L P 1002 Lindi

 

 

TAFAKARI YA WIKI

Upendo Haubagui

Na Pd. Ubaldus Kidavuri

 

Baba Mmoja na Mkewe ambao japo walikuwa familia changa sana, walikuwa pia na utajiri mkubwa.

Asubuhi moja waliamua kutembelea kituo kimoja cha kulelea watoto yatima kwa lengo la kupata watoto wawili.

Wakajaza fomu na kukamilisha taratibu zote kadiri ya matakwa ya ofisa usajili wa vizazi na vifo. wakati huo huo wakuu wa kituo hiki walikuwa wanajitahidi katika kuwafanya wafadhili hawa wajisikie wako nyumbani.

Mwishowe Mkurugenzi wa Kituo hicho akionyesha kuridhishwa kwake na ombi lao akasema;  "Sasa tutawaonyesha watoto wawili ambao ni wazuri kupita wote hapa katika kituo chetu".

Yule mama akageuka haraka sana na kusema; "Hapana tafadhali! sisi hatutaki watoto walio wazuri kupita wote bali tunataka wawili ambao hawatakiwi wala hawapendwi kabisa".

Mama huyu alijibu vyema kabisa , kikawaida huwa tunachagua kuhusiana na watu wale wanaopendwa karibu na kila mtu.

Lakini kwa kufanya hivyo tunajiwekea mipaka na hivyo kushindwa kuivuka na kuwafikia hasa wahitaji na wale wenye shida zaidi.

Familia hii tajiri inatufundisha kuwa kila mfuasi wa Kristo amekabidhiwa sehemu ya upendo wake ambao anatarajiwa kuushirikisha kwa wengine, na hasa kwa wale ambao wamepewa kidogo sana na hivyo wanaouhitaji zaidi kuliko wengine.

Hata Maandiko Matakatifu yanatufundisha kwamba; "Je, mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda ninyi? Hakuna! Kwa maana, hata watoza ushuru walifanya hivyo! (Mt 5:46).