Tunautakia heri mkutano wa viongozi wa dini na siasa

KATIKA ukurasa wa kwanza wa toleo hili, kuna habari juu ya uamuzi wa viongozi wa kidini wa kuwakutanisha viongozi wa kisiasa nchini Juni 22, mwaka huu lengo kuu likiwa kujadili suala zima la amani katika taifa letu.

Viongozi hao wa kidini, wanataka kukaa pamoja na wenzao wa kisiasa ili kuangalia kwa pamoja ni hatua zipi madhubuti zinazostahili kuchukuliwa, hasa wakati wa kusimamia na kuendesha zoezi zito na nyeti la Uchaguzi Mkuu unaotazamiwa kufanyika mwakani, kwa amani, haki na utulivu.

Tungependa bila kukawia, kuwapongeza kwa dhati kabisa viongozi hao wa kiroho kwa uamuzi wao wa busara waliouchukua. Viongozi hao, bila kujali tofauti za kiimani, wamechukua uamuzi sahihi na kwa wakati unaostahili.

Tunasema hivyo, kwa kuzingatia kwamba katika vipindi vyote viwili vya Uchaguzi Mkuu, ule wa mwaka 1995 na mwaka 2000, taifa lilishuhudia vitendo vya uvunjaji mkubwa wa amani na malalamiko makubwa yasiyokwisha, juu ya ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi.

Vyama vya upinzani, vimesikika mara zote mbili vikilalamika kuibiwa kura na Chama Tawala, CCM.

Ingawa sio vizuri kukumbusha machungu yaliyowahi kulikumba Taifa hili, lakini hakuna Mtanzania asiyejua yaliyotokea Januari 27, 2001, huko Visiwani.

Tunasema hakuna asiyejua kwani Watanzania takriban 30, waliuawa katika vurugu kubwa za kisiasa zilizotokea kutokana na kupinga kile kilichoitwa “wizi wa kura” uliodaiwa kufanywa na Chama Cha Mapinduzi, (CCM).

Baadhi ya walionusurika katika vurugu hizo, walilazimika kukimbilia nchi jirani, na hivyo, kwa mara ya kwanza katika historia ya Taifa hili, Tanzania ikawa na rekodi ya kuwa na wakimbizi nje ya nchi.

Kwa mtazamo wetu, pamoja na juhudi za makusudi zilizofanywa na baadhi ya viongozi wa nchi hii na hatimaye kuanzishwa kwa Tume ya muafaka, bado hali ya amani na maelewano ya kweli haijapatikana baina ya CUF na CCM.

Tunasema hivyo kwani kila chama kimekuwa kikitoa matamshi mazito yanayoelekeza kwenye uvunjaji wa amani.

Baadhi ya viongozi wamesikika, tena bila aibu wakitishia kumwaga damu, ikiwa mpinzani wao ataiba kura! Yapo madai kwamba, chama kimoja kimeamua kutoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wake ili wawe tayari kulinda kura zake katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Sisi tunasema, kwa mtu yeyote mwenye akili ya kawaida, anaweza kutabiri kitakachotokea iwapo kila kimoja kitaweka “makomandoo” wake 20 katika kila kituo cha kupigia kura.

Tujiulize katika mazingira kama hayo, hali itakuwaje ?

Taifa limeshuhudia kwa namna ya mshangao mkubwa, vitendo vya uharibifu wa mali za mashirika ya kidini, watu binafsi, na za Serikali kwa sababu ambazo kamwe haziwezi kuwa za kidini, bali siasa zilizojificha katika mgongo wa dini.

Baadhi ya watu wanawatisha wenzao na kuwaamuru kuhama toka sehemu moja ya nchi kwenda sehemu nyingine kwa madai ya kutokuwa wazawa wa eneo hilo. Hii ni hatari sana na huenda, mkutano huo ukawa wa manufaa makubwa kwa Watanzania.

Sisi tunasema, ni kweli na dhahiri kuwa licha ya juhudi za kutafuta na kuimarisha muafaka, bado uadui kati ya CCM na vyama vya upinzani unaongezeka kila siku.

Viongozi wa kisiasa wanatoleana maneno ya kashfa na kejeli katika mikutano ya hadhara ama hata katika vyombo vya habari.

Ungetegemea kuwa uhasama huu ungeishia hapo tu, lakini siyo hivyo. Ndani ya vyama vyenyewe mambo sio shwari. Viongozi kwa viongozi wanagombana na wanafukuzana bila mpangilio.

Madai ya ukiukaji wa katiba za vyama husika ni makubwa. Ndani ya vyama hivyo, malalamiko ya udikteta dhidi ya viongozi waandamizi wa vyama hivyo, ni mengi. Ukabila ambao zamani haukusikika, sasa sio jambo la siri tena.

Tunasema, nenda, CCM, TLP, CHADEMA, CUF, UDP na vyama karibu vyote vya siasa, hakuna hata kimoja kilichopona katika shutuma za vitendo vya rushwa, udini, ukabila, ukanda na udikteta! Hii ni aibu na ishara mbaya ya huko tuendako.

Ni katika hali kama hii, tunapolazimika kuunga mkono hatua ya viongozi wa kidini ya kukaa pamoja na viongozi wa siasa kila mwaka, ili kuangalia namna ya kuinusuru nchi yetu isitumbukie katika janga la kutotawalika.

Tunaomba kila kiongozi wa siasa atakayealikwa, ashiriki kikamilifu na kwa nia thabiti ya kujenga, kuimarisha na kudumisha umoja wa kitaifa na kubwa zaidi, ahakikishe chama chake kinashiriki Uchaguzi Mkuu ujao kikiwa tayari kushinda au kushindwa kwani asiyekubali si mshindani.

Tunasema, viongozi hao wenye dhamana kubwa katika jamii, wote waondokane na dhana mbovu za kwamba, ili uchaguzi uwe huru na haki, lazima vyama vya upinzani vishinde katika uchaguzi, kinyume na hapo, mlolongo wa kesi mahakamani kupinga matokeo; ni aibu na uchanga wa kisisasa.

Kwa upande mwingine tunasema, ni aibu kwa Chama kilichokaa madarakani kujijengea dhana kwamba kikiondolewa madarakani ni fedheha na kwamba, lazima kitumie mbinu zozote kuhakikisha kuwa, kinashinda.

Kwa kawaida, matokeo ya dhana hiyo iliyopitwa na wakati, ni mizengwe ya kila mtindo kujitokeza wakati wa upigaji na kuhesabu kura.

Tunasema, hekima za viongozi wa dini zituongoze na pia, Uchaguzi Mkuu uliofanyika Kenya na kukipa chama cha NARC ushindi, uwe mfano kuwa penye mashindano, lazima mshindi apatikane.

MAKOVU

Na Sr. Karoline Pasel OSB Mtwara

 

MIAKA kadha katika kipindi cha joto katika Kusini mwa Florida, kijana mmoja akaamua kwenda kuogelea katika Bwawa la zamani nyuma ya nyumba yao. Kutokana na haraka ya kwenda kuoga katika maji, kijana huyo alitoka kwa mlango wa nyuma na kuacha viatu, soksi na shati.

Alijirusha majini, hakutambua kwamba kadiri alivyokuwa anaogelea kuelekea kati kati ya bwawa na mamba alikuwa anaelekea ukingoni mwa bwawa hilo. Mama yake akiwa ndani ya nyumba alikuwa anachungulia dirishani na kumwona mwanaye  na mamba wakikaribiana. Kwa huzuni alikimbilia kwenye maji, akiwa anamgumilia mwanaye kwa sauti sana.

Aliposikia sauti ya mama yake, akatambua na kuona na kuogelea kuelekea kwa mama yake, lakini alichelewa. Alipomfikia mama yake tu, mamba alimfikia na kumkamata miguu yake, mama alimkamata mtoto wake kwa mikono, wakaanza mvutano kama vita kati ya mamba na mama. Mamba alikuwa na nguvu zaidi ya mama lakini mama hakukubali kumwacha mtoto wake.

Mkulima alikuwa anapita akasikia makelele akakimbilia na akachukua silaha yake na kumpiga risasi mamba yule.

Baada ya majuma hospitalini, yule kijana alipona. Miguu yake ilikuwa imejeruhiwa vibaya na mamba huyo. Na mikononi mwake kulikuwa na makovu (mikwaruzo) ambayo kucha za mama yake zilizama katika juhudi za kukaza mikono ili kumwokoa mwanae mpendwa.

Mwandishi wa habari ambaye alimuhoji kijana huyo baada ya kupona alimwomba kama angeweza kumwonyesha makovu (michubuko) yake. Yule kijana akakunja suruali yake. Na kisha kwa furaha akasema ‘Lakini angalia mikononi mwangu pia, nina makovu mengine makubwa pia. Nimeyapata hayo kwa sababu mama yangu hakutaka kuniacha nichukuliwe na mamba.

Mimi na wewe tunaweza kujifananisha na mtoto huyu tuna makovu pia. Hapana sio kwa ajili ya mamba, lakini makovu kutokana na maumivu yaliyopita. Baadhi hayaonekani na yametusababisha huzuni kubwa, lakini majeraha mengine ni kwa sababu Mungu amekataa kutuacha tupotee.

Wakati wa mahangaiko yako yupo akikusaidia.

Mpenzi msomaji tafakari yetu hii ya leo inatufundisha kuwa Mungu anatupenda wewe na mimi, wewe ni mtoto wa Mungu, anataka kukulinda na kukuhudumia, lakini wakati mwingine tunajiingiza katika matatizo bila ya kujua kilichopo mbele.

Bwawa la kuogelea la maisha limejazwa mambo mbalimbali na tunasahau kwamba adui wetu anatungojea kutuvamia. Hapo ndipo shida inapoanza na kama una makovu mikononi mwako ya upendo wake Mungu furahi sana. Hakukuacha na wala hatakuacha.

Mungu amekubariki wewe ili uwe baraka kwa wengine. Hauwezi kujua kama mtu yupo kwenye maisha yake na yanaelekea wapi. Usihukumu makovu ya mwengine kwa sababu haujui ameyapataje (vipi) na kwa nini?

Sasa hivi watu wanahitaji kujua kwamba Mungu unawapenda. usiwaache.