Umuhimu wa upasahanaji habari

Tunatambua kuwa binadamu anayo mahitaji mengi sana ya lazima ili aweze kuishi vizuri. Ni wazi kuwa anahitaji chakula, anahitaji maji, anahitaji hewa safi, anahitaji mahali pazuri pa kulala,pia anahitaji nguo za kujihifadhi nk. Lakini licha ya mahitaji hayo yaliyotajwa, bidamu huhitaji kupata habari kutaaka kwa binadamu mwenzake, na pia kumpa habari binadamu mwenzake. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa binadamu anahitaji kuwasiliana na binadamu mwenzake ili aweze kuwa salama, mwenye furaha na pia aweze kuendelea katika mambo mbalimbali.

Tunavyofahamu kuna upashanaji mbalimbali, yaani binaadamu hutumia vyombo mbalimbali vya kupashana habari. Ni wazi kuwa njia ya kwanza ya binadamu kuwasiliana na binadamu mwenzake ni kwa kutumia viungo vya mwili wake kama vile mdomo, macho, mikono, kichwa na kadhahali. Licha ya kutumia viungo alivyo navyo, binadamu hutumia pia vitu vinavyomzunguka kama vyombo ya kupashana habari. Tunasema wazee wetu licha ya kutumia viungo vyao katika kupashana habari waliweza kutumia pia vifaa kama vile ngoma, moto, michoro ardhini na kadhalika. Njia hizo za upashanaji habari zilikuwa ni hasa za kale.

Kwa kadiri binadamu alivyozidi kuendelea katika maarifa ya sayansi na tekinologia kumekuwa na ugunduzi wa njia mbalimbali za kupashana habari. Binadamu anaweza kutumia njia ya maandishi, yaani vitabu na magazeti, yaani njia ya uchapaji. Pia binadamu sasa hivi anaweza kutumia njia ya picha kama katika sinema na televisheni, na anaweza kutumia radio. Isitoshe, binadamu siku ya leo anaweza kutumia njia ya internet na hivyo kuweza kupeleka na kupokea habari kutoka pando zote za dunia kwa haraka sana. Tunasema hayo ni maendeleo ya kisayansi na kitekinolojia katika fani hii ya upashana habari. Njia hizi za upashanaji habari huzidi kukamilika siku kwa siku.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vaticano katika ile Hati inayohusu Vyombo vya Upashanaji Habari inasema kuwa katika macho ya Kanisa njia hizo za upashanaji habari ni vipaji vya Mungu. Kadiri ya maongozi na mpango wa Mungu njia hizo huwaunganisha wanadamu katika undugu. Pia huwasaidia kutekeleza azimio la Mungu kwa ajili ya wokovu wao. Mtaguso unaendelea kueleza kuwa yatupasa kuzidi kufahamu maana ya njia za upashanaji habari na manufaa yake katika jumuiya ya siku hizi.

Tunaweza kusema kuwa Kanisa, hasa hapa petu Tanzania limetambua umuhimu wa njia hizo za Upashanaji habari. Kwanza kuna Idara maalum ya Habari yenye vitengo vitatu. Kitengo cha kwanza hushughulika na mambo ya Uchapaji, yaani maandishi. Humo tunakuta lile Gazeti maarufu la KIONGOZI ambalo limekuweko kwa miaka mingi. Pia kwa upande huo wa maandishi Kanisa limejishughulisha sana na uandishi na utoaji wa vitabu. Tunayo maduka mengi sana ya vitabu yanayoendeshwa na Kanisa licha ya kila Jimbo na hata maparokia kuwa na sehemu ya huduma hiyo ya maandiko.

Kuna kitengo cha Radio ambacho hushughulikia uandaaji na utoaji wa vipindi vya dini vinavyotangazwa na RTD, radio ya taifa. Licha ya matangazo yanayotoka katika RTD kuna vile vile radio za Majimbo, kama vile Radio Tumaini ya Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, na Radio Mariae ya Jimbo Kuu la Songea. Waumini wengi wameshafaidika kutokana na huduma hiyo ya vipindi vya radio.

Katika Idara ya Mawasiliano, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuna kile kitengo cha Upashanaji Habari kwa njia ya vielelezo na michoro. Katika nafasi mbalimbali za maadhimisho ya kitaifa, ya kikanisa, kitengo hicho huwaa kinatayarisha mabango na vitu vingine vya aina hiyo na kusambazwa huko Majimboni ili waumini waweze kupata habari na ujumbe unaotakia.

Katika jitihada ya kufanikisha Upashanaji Habari katika kanisa zima la Tanzania, kumekuwa na Waratibu au Wakurugenzi wa Upashanaji Habari katika Majimbo yote. Kazi yao kubwa ni hasa kuwa viungo vya Idara hiyo, kati ya ofisi ya kitaifa na ile ya kijimbo. Wapashanaji Habari hao ndio wenye kuleta mwako zaidi huko majimboni katika shughuli zinazohusu upashanaji habari. Ili kuweza kuwa waratibu sawasawa katika Majimbo yao, kila mwaka {inapowezekana] hukutana pamoja wote ili kutoleana ripoti ya shughuli zao hizo za upashanaji habari. Pia hujiwekea mikakati mbalimbali ya uboreshaji wa shughuli hizo za upashanaji habari kijimbo na kitaifa.

Hapo jana Wapashanaji Habari hao wamemaliza kikao chao cha mwaka. Kuna mengi waliyoambiana katika ripoti zao. Wamepeana mikakati mbalimbali ya kwenda kutekeleza katika kipindi hicho kijacho, hasa tukikumbuka kuwa tunaelekea kwenye milenia ya tatu ya sayansi na tekinolojia. Tunatumaini hao wapashanaji habari watarudi huko majimboni kwao na kuwa kweli chumvi na mwanga katika fani hii ya upashanaji habari. Tunatambua kuwa kanisa la leo liko katika changamoto kubwa sana kutokana na uhuru na wingi wa vyombo vya habari. Kwa hiyo nao wapashanaji habari wa kanisa hawana budi kwenda na wakati.

Ni kweli kuwa shughuli ya upashanaji habari ina matatizo chungu nzima, lakini kwa kuwa tunaamini hao wanaoingia katika fani hiyo wana wito, hivyo watafanya kazi hiyo kutokana hasa na wito walio nao wa kulihudumia kanisa kwa moyo wa hiari na upendo.

Kwa hiyo tunazidi kuwapa moyo hao wapashanaji habari kutoka Majimbo ya Kanisa letu la Tanzania wazidishe bidii na kujitoa zaidi katika kazi hii ya upashanaji habari.

 

Naomba nijibiwe maswali haya yanayonitatanisha

Ndugu Mhariri,

Napenda upokee hongera zangu za dhati kupitia gazeti lako la KIONGOZI kwa kuweza kutilia maanani barua za Wasomaji katika gazeti hili ambalo ni tegemeo kubwa kwa Wakristo wengi wenye mapenzi mema katika Kristo Yesu Mfufuka.

Ndugu Mhariri baada ya kukupongeza kwa hilo, napenda kumpongeza Ndugu Sikitiko Amosi wa S.L.P. 66620, Dar Es Salaam kwa barua yake iliyouliza mswali ya msingi ambayo nina hakika yamewagusa wengi walio Wakristo na mimi mwenyewe yalinifurahisha sana. Napenda kusema kwamba Mungu awe pamoja na yule atakayeyajibu.

Napenda kusema kuwa ninayo mengi ambayo nahitaji kuyafahamu kama Mkristo Mkatoliki na ninaamini kuwa tuko wengi sana wenye kiu hiyo lakini hatuna majibu yake kwa vile mambo hayo hayafundishwi kwa undani makanisani kama alivyosema ndugu Sikitiko.

Baadhi ya mambo ambayo sijayaelewa vizuri ni kama vile;

1. Kuhusu sala ya Mama wa Yesu (bikira Maria). Sala hiyo ukisali utafika mahali panaposema kuwa "UTUOMBEE SISI WAKOSEFU, SASA NA SAA YA KUFA KWETU". Ndugu Mhariri kwa upande wangu nifikapo hapo nakuta kitendawili, yaani niko katikati. Swali hapo ni kwamba, Je, ni kwanini tuseme usemi huo wakati Bikira Maria alishakufa na wakati huo huo Mungu wetu ni Mungu wa walio hai na wala si Mungu wa waliokufa? Hapo ndugu Mhariri napenda kujifunza mambo kadhaa. Kwanza; Bikira Maria ana nafasi gani sasa hivi hapo alipo? Pili; Nini historia ya Bikira Maria baada ya Yesu kupaa mbinguni? Tatu; Bikira Maria alipata kuzaa watoto wengine baada ya Yesu, na kama alizaa kwanini basi tuendelee kumwita bikira? na Mwiho; tuna hakika gani kwamba kwa kumwomba Bikira Maria sala zetu zinapokelewa na Mungu? Naomba kufahamu fumbo hilo.

Jambo jingine ni kwamba Je, ile picha ya Yesu ilipatikanaje wakti zama zake hapakuwa na kamera? Pia ningependa kujua neno "Biblia" lina asili ya lugha gani?. Nitashukuru kama nitajibiwa maswali yangu hayo ambayo naamini ni maswali ya wengi.

Mwisho nakupongeza kwa kulibadilisha gazeti lako la KIONGOZI kwa kuliwekea mambo ambayo ndiyo kiini chake hasa, yaani ya kidini tofauti na hapo zamani. Naomba mzidi kuliboresha gazeti hilo kwa kuliongezea mafundisho mengi zaidi ya dini.

Michael Khasan,

c/o Silvano Malaika

S.L.P 72020

Dar es Salaam

 

Matatizo ya Greenland Bank na BoT yanatuumiza wanyonge

Ndugu Mhariri,

Hatua ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kuifunga Greenland Bank (T) Ltd, bila kutoa maelezo yanayotosheleza ni hujuma kubwa inayolenga bila huruma kuwatesa wateja wadogowadogo wa Greenland Bank . Aama kweli tembo wakipigana, sisi nyasi ndio tunaoumia.

Tuliamini sana kwamba Greenland Bank ni benki ya wazawa na inasaidia sana watu wadogo. Sasa wateja tunaoteseka hapa Tanzania tunahusika vipi na matatizo ya Greenlad Bank huko Uganda?.

BoT haijatueleza kwa kina matatizo ya Greenland Bank (T) Ltd. Tunasikia ni matatizo ya kisiasa, mara kidini mara kiuchumi, tena kwa upande wa Uganda na wala sio Tanzania. Sasa matatizo haya sisi wateja yanatuhusu nini?

Fedha zetu chache tulizoweka katika benki hiyo sasa hatuwezi kuzichukua. Angalia sisi wanyonge, watu wadogo tunapata matatizo wakati hatuna kosa lolote.

Tunamuomba Mheshimiwa Gavana wa BoT amalize kazi yake haraka ili benki hii ifunguliwe na sisi wanyonge tupate pesa zetu.

Wakati BoT ilipotoa idhini ya kuziruhusu benki za kigeni tuliamini kabisa kuwa ilikuwa na uwezo wa usimamizi na nia njema kabisa, lakini matatizo haya ya kufungwa benki hizi za kigeni yanatuhuzunisha sana.

Ni matumaini yetu kwamba wanaohusika watafanya kila wawezalo ili sisi wanyonge tusiendelee kuteseka zaidi.

Labda nitoe ushauri wangu kama ifutavyo;

Moja; kwa vile Greenland Bank ilisajiliwa hapa nchini kwa sheria zetu zinazosimamiwa na BoT sioni ni kwanini sasa sheria zetu zisitumike na badala yake tusikie na kufuata amri za nje zisizotuhusu kama vile siasa, uchumi, ukabila na majungu yao mengine.

Pili; baada ya kupata taarifa za kutatanisha kutoka Uganda, BoT kama msimamizi wa mabenki ilitakiwa kuchukua hatua za usimamizi wa shughuli za Greenlanda Bank pasipo kufunga au kuathiri uchumi wa wateja wake kwa ujuma. Sambamba na usimamizi huo BoT ilitakiwa kuweka "Task Force" ya wakaguzi wa mahesabu ili kutathmini hali halisi ya benki hiyo. Ilitakiwa kutoa taarifa ya awali kwa wateja na wananchi kwa ujumla. Kuwatoa wateja wasiwasi kwamba matatizo yanayoikumba Greenland Bank ya Uganda hayataathiri utendaji wa benki ya hapa Dar es Salaam, kwani shughuli zote ziko salama mikononi mwa BoT.

Greenland Bank Tanzania inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za BoT na sio BoU.

Usimamizi huo ni muhimu sana kwani uwezekano wa kuhamisha pesa kwa ajili ya kumaliza matatizo kwa ajili ya kumaliza matatizo kwa upande wa Uganda waweza kuwapo.

Kwa hiyo usimamizi huu unalenga kulinda fedha za Watanzania.

Tatu; Gavana wa BoT anatakiwa kuwa mwangalifu sana inapotokea hali kama hii siku zijazo akifahamu kwamba analo jukumu kubwa katika kulinda maslahi ya wananchi wa nchi hii, ikiwa ni pamoja na uchumi wa nchi yao. Hali hii ya Greenland inatuonyesha kutokujali matatizo ya wateja waathirika.Kwani hakuna taarifa yoyote INAYOELEWEKA ilikwisha kutolewa kuhusiana na ufungaji wa benki hii hapa nchini. Tunaomba Waandishi wa habari hasa wa fani ya fedha na uchumi kuitisha "Press Conference" ili Gavana aeleze Umma juu ya hatua zilizochuikuliwa hivi sasa na athari zilizopatikana.

Elizabeth Mkumbo,

c/o Leila Abood

S.L.P 2316

Dar es Salaam