Madhehebu ya dini yasiwe ni kwa sababu za ubinafsi

Wakati akihutubia kwenye ibada ya pamoja ya madhehebu mbalimbali ya Kikristo, siku ya Jumatatu ya Pasaka, tarehe 5,4,1999, katika Kanisa la Mt.Yosef mjini Dar Es Salaam, Askofu mtaafu wa KKKT, Elinazar Sendoro, alisema kuwa kuna watu ambao wanaanzisha makanisa kwa sababu za ubinafsi, na siyo hasa kwa kutokana na ule wito wa kuhubiri Injili. Maneno hayo ya Askofu Sendoro yana ukweli mkubwa sana na tena ni yenye uzito mkubwa mno hasa tunaposhuhudia siku ya leo kuibuka kwa vikanisa vingi hapa nchini. Hapo ni sherti tujiulize ni kwa nini mambo yako hivyo, licha ya ule utajiri wa Roho Mtakatifu alio nao wa kuvuvia popote apendapo na kwa ye yote ampendaye.

Tungeweza kusema kuwa huo ni utajiri wa Roho wa Bwana. Lakini tunajiuliza, licha ya huo utajiri wa Roho, mapato yake yanatutia mashaka. Ni kweli kuwa kila binadamu anao uhuru wa kufuata ile imani inayomwingia ndani ya roho yake. Wengi wetu tumepata imani wetu. kwa njia ya wazazi na walezi wetu, yaani wazazi wetu wametuingiza katika imani ya kikristo kwa kuwa wao waliona hicho ni kitu kizuri na cha kutufaa. Linakuwa ni jambo lisilo sawasawa ikiwa tunaiasi ile imani ambayo tuliipokea kwa njia ya wazazi na walezi wetu. Tuliikubali hiyo imani na tukaishikilia kama walivyotuelekeza hao wazazi na walezi Tunaweza kusema kuwa huo ni kama urithi wetu kutoka kwa wazazi na walezi wetu.

Ni jambo la kusikitisha sana kushuhudia jinsi watu mbalimbali wanavyoiasi tunaamini kuwa hufanya maamuzi hayo kwa kutumia akili kwa namna fulani. Tunazidi kujiuliza ikiwa kweli kuna mambo ambayo hayawaridhishi katika dhehebu hilo waliomo kwa nini wasiyatoe manung'uniko yao hayo kwa wahusika na hivyo kuyasahihisha mambo kwa njia ya mazungumzo. Tunaambiwa na wataalam kuwa ni vizuri zaidi kusahihisha na kurekebisha mambo kutoka ndani kuliko kutoka nje. Yule mtu ambaye anaondoka katika ushirika fulani na kutoa lawama kwa ushirika huo akiwa nje tunaweza kumwona kama ni mtu ambaye hajakomaa bado kiimani. Hivyo tunaweza kuungana na Baba Askofu Sendoro tukisema kuwa ana sababu zake binafsi za kufanya hivyo na wala si kwa sababu ya kuwa na uchungu na imani yake.Tunasema tena huo ni uasi wa kidini.

Jambo jingine ambalo huwa linakera sana ni ile tabia ya wale wenye kuhama madhehebu yao ya awali wakiwa na chuki kwa madhehebu hayo ya awali. Inashangaza sana kushuhudia jinsi Neno la Mungu linvyotumika vibaya katika kudharauliana.Kwa kawaida kwa asili Neno la Mungu hufanya kazi ya kuwaunganisha wafuasi, na siyo kinyume chake.

Hapo yafaa tujifunze yale maneno ya Mtume Paulo kwa Wakorintho akisema: "Nimearifiwa kwmba kila mtu husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo,na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je, Kristo amegawanyika?"{1Wakor. 1:12}.

Ni kweli kuwa kila mmoja anao uhuru wa kushika imani au kuwa katika dhehebu analolipenda, lakini akifanya hivyo hana budi kuwaheshimu wenzake na imani zao. Hatuwezi kuitangaza imani yetu kwa kuwadharau wengine. Ingawaje mambo ya imani licha ya kuwa ni ya mtu binafsi, hujionyesha pia nje kwa jinsi tunavyoiungama hiyo imani. Maisha yetu huwa ni uthibitisho wa nje wa imani zetu. Hakuna imani au dini yo yote ile inayoruhusu madharau kwa watu walio nje ya imani hiyo. Mtu anapoamua kumsema vibaya au kumdharau mwenzake kiimani hapo huonyesha hali ya kutofahamu maana ya dini au imani. Siyo tabia nzuri kutafuta wafuasi wa dini kwa njia ya kudharau wengine wenye imani tofauti .

Tungependa kusema tena katika Kauli Yetu hii kwamba hii mitindo iliyozuka sana hivi ya kuwa na mihadhara na hapo kutolea kashfa kuhusu imani zetu. Tunasema ni jambo la aibu sana kukashfiana hadharani katika mambo ya imani. Sote tutambue kuwa imani kama imani ni kitu nyeti kabisa kwani chamhusu binadamu na Muumba wake. Kwa hiyo inapaswa kuheshimiwa, kulindwa na hata kuogopwa kwa kuwa ni kitu kitakatifu.Ni ajmbo lisilo zuri kujenga kwa njia ya kubomoa au kulaumiana.

Kwa hiyo tunapenda kumalizia Kauli Yetu kwa kuyarudia tena mambo hayo mawili tuliyoyazungumzia. Kwanza ni jambo lisilo sawasawa kwa mtu kuiacha imani yake, na hasa kuanzisha kanisa lake kwa sababu za binafsi. Pili ni jambo lisilopendeza kwa mtu kujenga dhehebu lake kwa kutumia dharau kwa madhehebu mengine. Na jambo la tatu ambalo limeshamiri siku hizi ni kutolea matusi na madharau katika mihadhara ya kidini. Tungependa kuona kuwa katika midhara hiyo waumini wanaelimishwa zaidi kuhusu maandiko matakatifu na pia kwa njia hiyo watu wanafunzwa zaidi jinsi ya kuishi vizuri, kimaandili kwa kufuata hayo maandiko matakatifu. Tuishi imani zetu kwa njia ya kuvumiliana na siyo kwa njia ya kudharauliana na hata kutukanana hadharani.

Udumu umoja wa Makanisa

Ndugu Mhariri,

Katika toleo lililopita la gazeti lako ukurasa wa kwanza kulikuwa na habari inayosema kuwa madhehebu mbalimbali ya Kikristo yamefanya ibada ya pamoja jijini Dar, ninaomba unipe nafasi katika gazeti lako hili la Kiongozi ili nikapate kuzimimina pongezi zangu kwa kamati iliyokaa na kujadili na hatimaye kuamua kuanzisha Umoja huu wa makanisa.

Hali hii inadhihirisha wazi uimara na pia ni ushuhuda tosha kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu aliyekufa na Kufufuka katika wafu kwa nia ya kuwaokoa Wanadamu.

Ninafikia hatua ya kiupongeza hatua hii kwa kuwa inafagia na kuondoa kabisa takataka zote za ubinafsi ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa baadhi ya waumini wa baadhi ya madhehebu wanaojidhania kuwa wao ni tofauti na madhehebu mengine na hata kudhani kwamba wao ni bora kuliko Wakristo wengine

Watambue kuwa mbele ya Mungu ubora wa mtu unatokana na imani na matendo yake kuanzia ngazi ya yeye mwenyewe, jirani yake na hata mbele ya Mwenyezi Mungu; tena siyo kwa kuogopa sheria ya duniani, au kutaka sifa mbele ya macho ya wanadamu, bali kwa lengo kubwa la kutimiza mapenzi ya Mungu.

Umoja huu unadhihirisha kuwa Wakristo wote ni wamoja na kwa kuwa wote ni wafuasi waYesu Kristo, ambaye ni Mwana wa Mungu na Mwokozi wa Ulimwengu wote, hatua hii ni ushuhuda tosha kwa wanaodhani kuwa Yesu si Mwana wa Mungu na wala hakufufuka, sasa waamini kwa inajidhihirisha wazi yenyewe.

Makanisa hayo yaliyojiunga na umoja huo yafanye kila wajualo na kuweza kuona kuwa wanauimarisha na wito wangu kwa madhehebu ambayo hayajajiunga, yatambue umuhimu kwa kujiunga na kuwa wamoja katika Kristu kwani Mungu wetu ni mmoja.

Ushahidi tosha katika hatua yangu ya kuipongeza hatua hii ni Ibada za pamoja za makanisa zilizofanyika katika majimbo mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka yakiwemo yale ya Jimbo Kuu la Arusha, Moshi na Jimbo Kuu la Dar Es Salaam iliyofanyika katika kanisa Kuu la Mtakatifi Yosefu.

Alexandre Mashauri,

c/o RC Church

S.L.P.62,

Tarime.

Wachungaji msitawanye kondoo wa Mungu

Ndugu Mhariri,

Naomba nipate nafasi katika gazeti lako la Kiongozi ili niweze kusema machache kuhusiana na mwenendo wa kanisa la Mungu.

Kwa kweli imekuwa ni aibu kwa kanisa, inapotokea mtumishi ya ngazi yeyote kanisani kuhusishwa na tuhuma mbaya ambazo ni kinyume na maandiko matakatifu ambayo kimsingi ingempasa kuyasimamia ili wengine waweze kuiga mfano kutoka kwake.

Hali hii inapelekea sisi WAKRISTO kushindwa ni njia ipi tupite na ni nani tumshuhudie habari za Yesu ili amkubali kwani wengi wamekata tamaa kutokana na maovu yaliyozagaa miongoni mwetu.

Leo hii limekuwa ni jambo la kawaida watumishi wenye nyadhifa kubwa katika makanisa na madhehebu kuhusishwa na tuhuma nzito kama vile ubakaji, ulevi wa kupindukia, kushikwa ugoni au kufumaniwa, wizi wa sadaka na maovu mengine ambayo ni matope katika kanisa la Mungu.

Vyombo vingi vya habari vimegubikwa na habari nyingi za makanisa zinazoeleza uovu na uchafu uliokithiri katikati ya makanisa hayo ambayo ndiyo tegemeo la wengi (ikwemo serikali) kwamba yangesaidia kukemea maovu katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Siku zilizotangulia, (ijapokuwa mimi si mkubwa sana) historia inaonyesha kutokuwepo kwa maovu ya kama yaliyopo sasa, hasa katika kundi linalowahusisha viongozi wa makanisa na madhehebu ya dini kama ilivyo sasa.

Leo hii majina ya watumishi wa mungu ni kwa ajili ya magazeti mara ooo askofu kabaka waumini...!, mchungaji ashikwa ugoni....!, padri atuhumiwa kula pesa za kanisa na mambo mengi yanayochefua kuhusiana na tabia mbaya za viongozi hawa wa herufi ndogo.

Jamii inashindwa kuelewa ni nini msingi wa tabia hizi na hiki ni chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili katika kanisa na Taifa kwa ujumla. Ni kwa njia hii kanisa la Mungu linameguka na kutawanyika na maneno ya Mungu yanasema 'ole wao wanaolitawanya kundi langu'.

Kwa kuwa dalili zinaonyesha kuwa kurudi kwa Yesu kumekaribia basi ni wajibu wa kila mmoja (anayependa kwenda Mbinguni) kujiweka tayari kwa ajili hiyo.

Ishambo Mremi

SLP 7545

Mwanga -Kilimanjaro.

Wakazi wa Temeke- Yombo walilia usafiri salama

Ndugu Mhariri

Wakati matatizo ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam yamekuwa sugu kufuatia uhaba wa magari ya kubeba abiria hali hii imekithiri katika Wilaya ya Temeke hususani maeneo ya Yombo.

Tatizo la usafiri kutoka sokoni Tandika kwenda maeneo ya Buza , Yombo Makangarawe na Yombo-machimbo. Pia kutoka kituo cha daladala cha shule ya msingi ya Uhuru hadi Lumo Kata ya Yombo Vituka tatizo limefikia hatua ya kuwakera wakazi wa maeneo hayo kiasi cha kukatisha tamaa na kuhoji sababu zilizowafanya wajenge na kuhamia sehemu hizo za tarafa ya Vituka.

Kadri ya hali ilivyo ya barabara ya Tandika hadi Buza na Machimbo inayo sura ya eneo la mafunzo ya madereva wa vita kwani mashimo yaliyotuama maji mengi wakati wa mvua na ambayo magari yakipita maji hayo husaidia kuchimba barabara zaidi kwa kuondoa mchanga yanafanya usafiri uwe mgumu zaidi kwa magari hasa ya abiria mengi yakiwa aina ya Hiace, maarufu kwa jina la Vipanya .

Madereva wa magari haya ya vipanya ambayo kwa kawaida hujaza watu kama dagaa kwa ''kushonana'' wamekua wakilalamikia ukatikaji wa Spring za magari wa mara kwa mara kufuatia kuchimbika barabara ovyo ovyotu kila sehemu.

Pia abiria wanalalamikia uumiaji wa ama mbavu au migongo kutokana na kurushwarushwa kwa nguvu na magari ( vipanya ) yanapokuwa katika mwendo wa kasi katika harakati za kugombea na kuwahi abiria mwisho au mwanzo wa vituo vya safari

Tunaomba viongozi wa Serikali watupie macho suala hilo.

Deo Mbogo

Tandika

Dar es Salaam.