Make your own free website on Tripod.com

Watanzania tusisubiri jangwa ndipo tupande miti

Hapo jana ilizinduliwa ile kampeni ya upandaji miti popote katika nchi yetu. Tunapenda kuwapongeza viongozi wetu wa serikali kwa kuanzisha kampeni hiyo ya upandaji miti kila mahali. Hakuna mwananchi asiyetambua umuhimu wa miti katika nchi ingawaje kuna wengi ambao hawajishughulishi na upandaji wa miti hiyo .

Nawakumbuka wale ndugu Wamisionari, waliotuletea imani ya Kikristo jinsi walivyokuwa wanajitahidi kupanda miti katika vituo vyao mbalimbali walivyokuwa wanavianzisha. Vituo hivyo vilijulikana kama misheni au misioni.

Kila eneo la misioni lilizungukwa na miti iliyokuwa imepandwa na hawa wamisionari. Hivyo mtu uliweza kutambua misheni iko wapi kutokana na miti iliyokuwa imeizunguka.

Upandaji wa miti haukuwa tu kwa upande wa wazungu wamisionari, bali hata wale wa serikali ya kikoloni, nao walikuwa wakihimiza upandaji wa miti sehemu za ofisi zilizokuwa zinajulikana kama bomani.

Tunaweza kusema kuwa upandaji wa miti ulikuwa ni utamaduni wa hao ndugu zetu wageni iwe ni wa kidini au wa kiserikali. Hapo ni kama walituonyesha mfano wa kupanda miti iwe ni kuzunguka nyumba zetu, iwe ni mashambani au mahali popote pale.

Tunaweza kusema kuna wachache ambao walikuwa tayari kuwaiga hao wageni katika desturi hiyo ya kupanda miti. Lakini watu wenye tabia hiyo ya upandaji miti wamekuwa wachache.

Tukitembea katika nchi yetu kutoka kule Kaskazini hadi Kusini, na kutoka Mashariki hadi Magharibi tunaona jinsi nchi yetu inavyogeuka kuwa jangwa.

Wananchi wengi sana wanao ule utamaduni wa siku nyingi wa kukata miti na wala sio ule wa panda miti. Miti mingi katika nchi yetu imekatwa hovyo sana na haikupandwa mingine badala yake. Mwenyekiti wa taifa Baraza la Mazingira, Ndugu Reginald Mengi aliwaambia wananchi wakati fulani kuwa inatakiwa ukikata mti mmoja kupanda mingine mitatu, akiipa changamoto ile kampeni ya "kata mti, panda mti" Kama utaratibu huo ungefuatwa basi tungekuwa na misitu bado katika taifa letu. Lakini kumbe kwa bahati mbaya tumekuwa na wakataji wa miti wengi mno na tumekosa wapandaji.

Hiyo ni kasoro kubwa sana na tungeweza kusema kuwa tumetenda dhambi ya kuharibu maumbile ya dunia aliyoyaweka Mungu. Tunapaswa kuitubu na kuifanyia malipizi ya kupanda miti zaidi.

Tumesema kuwa kumekuweko jitihada fulani ya upandaji miti katika taifa letu. Ni jambo la kusikitisha sana kuona hiyo miti mara kwa mara imekuwa ikiunguzwa na moto na hivyo hasara kubwa sana imetokea.Tunao watu wengi ambao ni waharibifu na wazembe kabisa katika taifa

letu. Wao wana tabia ya kufurahia uharibifu wa kitu kizuri. Hapo tungependa kusema wazi kuwa hizo kampeni za upandaji miti zaweza kukwamishwa kutokana na ule uzembe wa kuchoma na kuunguza miti hiyo iliyopandwa. Kwa hiyo tunapenda kutoa rai kwa wananchi wote kwamba inawapaswa kushirikiana katika utunzaji wa hiyo miti tunayoipanda katika kampeni iliyoanza hapo jana na ambayo tumeambiwa kwamba itaendelea hadi mwakani mwezi wa sita.

Licha ya hatari ya moto, kuna pia hatari nyingine za wanyama kula matawi ya miti hiyo. Kuna wanyama waharibifu sana wa miti kama vile mbuzi, kondoo, ng'ombe na wengineo. Tungependa pia kutoa ushauri kuhusu utunzaji wa miti kwa kutoruhusu hao wanyama wawe wanatembea ovyo ovyo na kuharibu miti ambayo ni pato la jasho la wananchi wetu.

Kwa maneno mengi tungependa kuwaomba hao wakubwa wenye kusimamia hizo kampeni za upandaji miti waweke sheria zenye adhabu kwa wale wahalifu wanaoleta uharibifu kwa miti ambayo wananchi wameipanda.

Kwa ndugu zetu wananchi tungependa kuwaambia kwamba upandaji miti na utunzaji wa mazingira ni alama ya ustaarabu.

Hivyo ndivyo tunavyoshuhudia katika nchi za wenzetu ambao tunasema wameendelea kama vile huko Ulaya, Marekani, na penginepo.

Lakini kama tunapita na kushuhudia majangwa katika nchi yetu hapo tena tunakuwa na mashaka juu ya ustaarabu wetu.

Kila mmoja wetu hupenda kukaa chini ya kivuli na wala si kwenye uwazi ambao ukiangalia hadi upeo wa macho hakuna mti. Tunapaswa kuondokana kabisa na tabia au desturi ya kukata miti ovyo, na badala yake tujenge mazoea ya kupanda miti na kuitunza. Sote tunatambua kabisa umuhimu wa miti katika nchi. Kwanza kabisa nchi yenye miti au misitu hupendeza sana na kuvutia. Lakini sehemu ambayo haina miti inachukiza sana. Hivyo tunaweza kushuhudia kuwa nyumba ambazo zimezungukwa na miti hupendeza, lakini zile ambazo hazina miti kuzizunguka hazipendezi.

Basi kwa pamoja tuunge mkono kampeni hiyo ya upandaji miti, na hivyo kila mmoja aone kuwa anawajibika katika kampeni hiyo. Viongozi wetu wametuelekeza vizuri sana, linalobakia ni utendaji wetu wa kupanda miti.

Ni matumaini yetu kuwa ikiwa kila mwananchi atachukua hatua ya dhati katika kuitikia mwito huo wa serikali wa kupanda miti, nchi yetu itakuwa imepiga hatua kubwa sana ya kimaandeleo katika utunzaji wa mazingira na tutakuwa tumejiongezea rasilimali kubwa sana katika taifa letu. Haya shime wananchi tupande miti na tuitunze.

 

Jihadharini na mtu huyu

Ndugu Mhariri

Mtu mmoja anayejiita A.J. Kaoma anajitahidi kusambaza makala isemayo"BIBLIA NDIYO TAA YANGU, KUTANGUA AU KUKAMILISHA". Makala hizo zimejaa ufarisayo, kiburi na uasi.

Anajitahidi sana kumtukana kipuuzi Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo kwa lugha ya kifedhuli.

Anataka kutuaminisha kuwa Mwadhama Kardinali hamchi Mungu kwa kuwataka Wakristu wa Dar es Salaam wasimame wanapopokea Kommunio.

Kaoma anataka kutuaminisha kwa nguvu kuwa yeye na wanamaombi ndio wanaoifahamu vizuri Biblia na sheria za Mungu; ndio wanaomtii na wanaomheshimu Mungu tu; na bila kupiga magoti na kupokea Kommunio kwa ulimi basi hakuna kwenda Mbinguni. Wakristu wengine wote ni wapinga Mungu au wao ni Ibilisi.

Kaoma na wenzake wafahamu kuwa wao ndio waasi na wenye dharau na wasiomtii Mungu na kanisa lake. Kwa vitendo vyao,. kwanza wao hawakumchagua kiongozi yeyote wa kanisa kusimamia imani na maadili ya jimbo lolote.

Pili Kaoma na wanamaombi hawana mamlaka halali ya kutafsiri Biblia na kufundisha imani na kuongoza Kanisa la Mungu la mahali. Tatu, wajue wanamfuata Padre Nkwera- mwasi na mwenye shida kubwa ya utii kama wao. Nne, wapo wataalamu wa Biblia wenye kuwaza tofauti na Kaoma.

Hakika Biblia haielezeki na kueleweka kwa kukariri au kunukuu tu mistari ya maandiko Matakatifu.

Hata wasio Wakristu wananukuu Biblia kijinga tu ili kupinga imani au dini ya Kikristu.

Hata hayo maneno anayonukuu Kaoma, wenzake wameyatumia vile vile kumpinga Kristu.

Shida siyo kupiga magoti kwa kupokea Kommunio. Kwanza hatuelezwi katika Biblia kuwa siku ya Alhamisi Kuu wakati wa karamu kuu ya Bwana, chimbuko la Misa Takatifu, kuwa ilifika saa Kristu akawaamuru mitume wake wapige magoti ili awalishe mwili wake. Hatusomi hilo katika Agano jipya. Kaoma analazimisha kuwa maana ya maneno ya nabii Isaya 45:22-23 na ya mtume Paulo (Efe. 5:6) maana yake ni kupiga magoti na kupokea Ekaristi kwa ulimi tu. Na akifanya hivyo imetosha hata akitoka hapo akaenda kula rushwa, kuiba, kusengenya watu na lolote ovu.

Hakuna Askofu Mkatoliki yoyote atakubaliana na Kaoma au Nkwera kwa jambo hilo. Wala hakuna Askofu anayesema kupiga magoti kupokea ni dhambi au jambo baya.

Askofu Severine Niwemugizi

Jimbo la Rulenge, S.L.P. 50,

Ngara,

Bukoba.

 

 Je, sawa kumuita Kiongozi Baba?

Ndugu Mhariri,

Mimi ninayo machache ambayo kwa muda mrefu yananisumbua kwani hoja yangu kubwa kwako ndugu mhariri ni kwamba yapo mambo ambayo kwa kweli ningependa kwa ule upendo wa dhati kupata msaada wa kufafanuliwa mambo machache ambayo sisi waumini wa Kanisa Katoliki wengi wetu yanatushinda kuelewa na mambo hayo tunayafanya pasipo kuyaelewa vilivyo.

Kwa mfano kuhusu kuwepo kwa jina la PAPA (Baba) wa hapa duniani na wakati Bwana Yesu Kristo aliwambia mitume wake kuwa hawatakuwa na mtu aitwaye Baba hapa duniani isipokuwa Baba tuliye naye ni mmoja tu ambaye yuko juu mbinguni, ndiye Mungu.

Sasa cha kushangaza tunapata kusikia hapa duniani yupo mtu tumwitaye Baba na siyo Baba tu tunadiriki kumwongezea neno Mtakatifu yaani "BABA MTAKATIFU".

Hapo kwa kweli inatuchanganya kweli na kujiuliza kwa nini tunakuwa na hali ya kumwita mtu hivyo hapa duniani? hatuoni kama tunampinga Kristo?

Tunaomba viongozi wa Kanisa letu Katoliki wawe wazi kutufafanulia kuhusu jambo hilo. Mimi ningeona aitwe ASKOFU MKUU WA KANISA KATOLIKI DUNIANI, badala ya Kumwita BABA MTAKATIFU kwa maana maneno hayo mimi naona kama kufuru kabisa.

La sivyo mtufafanulie vilivyo tuelewe. Maana tunaambiwa na wenzetu kuwa sisi Wakatoliki tumefichwa baadhi ya mambo kwenye Biblia na kuambiwa tuendee na kitabu kiitwacho "Misale ya Waumini".

Wanadai eti tumefichwa kwa sababu tukisoma Biblia tutakimbia kutoka katika Kanisa hilo ambalo ndilo lenye waumini wengi kuliko mengine yote duniani.

Kwa kweli kwa upande wangu ningependa tufahamishwe maana halisi ya mambo hayo na tufundishwe Bibilia vya kutosha ili tuwe watu ambao tunaifahamu Biblia vizuri ili ieleweke kuwa Kanisa Katoliki lina uelimisho mzuri kwa waamini wake kwa maana "Wachungaji wake huwalisha vizuri kondoo wa Bwana pasipo kuwapoteza".

Jambo la pili, ndugu Mhariri ningependa kuelewa nini maana ya maandishi yaliyoko katika kofia ya PAPA yaliyoandikwa pale kwa maandishi nafikiri ya Kirumi au Kilatini tufahamu maana yake hasa nini iwe kwa kifupi au kwa kirefu na kutufafanulia kwa kila baada ya herufi na namba yake kisha wajumlishe halafu tuweze kuona ili tufahamu sisi waamini wa kanisa Katoliki kwani tutafurahi sana.

Sisi waamini tunaliamini sana Kanisa letu.. Ushauri ambao nitapenda viongozi waelewe ni kwamba tungependa tuandaliwe vyuo vya kufundisha Elimu ya Biblia kwa anayetaka kuelewa basi aende aelimke hapo kwani ni wengi tunahitaji kuifahamu Biblia ambacho ndicho kitabu chenye uhai ndani yake na viongozi wake tunawaamini sana kuliko wengine wengi wa madhehebu mengine. Mwisho ndugu Mhariri ningependa kukupongeza kwa juhudi zako. . "Bwana awe Nanyi".

Mr. Sikitiko Amosi,

S.L.P. 66620,

Dar Es Salaam

 Hongera gazeti la Kiongozi

Ndugu Mhariri,

Napenda upokee hongera zangu za dhati kabisa kwa gazeti letu la kiongozi kuanza kuandika habari sawa na lengo na makusudio yake.

Kwa muda mrefu gazeti la Kiongozi lilikuwa kwa kiasi fulani linaandika habari kinyume na tulivyo kuwa tunatarajia sisi wasomaji.

Habari zilizobeba uzito katika gazeti hili zilihusu masuala ya siasa.

Kwa mfano kunatoleo moja liliandika mbele ya ukurasa wa kwanza "Mrema anywea". habari hii ilinikera sana.

Zilinikera kwa sababu nilikuwa najua mambo ya siasa na dini ni vitu viwli tofauti. habari za kidini zilikuwa chache sana ndani ya gazeti.

Kwa mtazamo wangu hali hii ndio iliyosababisha gazeti la Kionozi likose wasomaji.

Hivi karibuni nimesoma matoleo matatu mfululizo; tangu toleo la mahojiano kati ya mwandishi Beda Msimbe na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo hadi toleo la tarehe 28/03/99.

Nilichogundua ni kwamba uandishi wa gazeti umekuwa mzuri na nadhani ndio uliokuwa mweleko wa gazeti tangu kuanzishwa.

Kwamfano nichukue makala ya Padre Aidan Msafiri katika toleo la 28/3/99 kuhusu namba 666.

Makala hii imetoa elimu kwa watu ambao walikuwa na utata wa namba hizi ndani ya kitabu cha ufunuo sura ya 13:15-18 kwa hilo nakupongezeni sana.

Hii ndiyo kiu ya sisi wasomaji siku zote kwa gazeti la kiongozi.

Ningependa kutoa rai ya kwamba tuongezeeni makala zaidi ya kumjua Mungu wa kweli. yehova ndani ya gazeti hasa kipindi hiki cha Ushindani waki - imani. Makala za siasa achia magazeti mengine.

Tumsifu Yesu kristo.

Augustino F. Mwinuka

Mburahati, Dar es Salaam.