Kuongeza kipato cha ufugaji mjini

MIAKA michache ya hivi karibuni, Serikali baada ya kuona hali ya Mtanzania inazidi kuwa ngumu kiuchumi, basi ikawa imependekeza mbinu mbalimbali za kujiongezea kipato ili mradi kuweza kukabiliana na hali hiyo. Kwanza kabisa Serikali ikatangaza kuwa siku ya Jumamosi iwe ni siku ya mapumziko ambapo wafanyakazi wataweza kupata nafasi ya kujifanyia shughuli zao binafsi kama vile kwenda mashambani, kufanya shughuli za ufundi na nyinginezo.

Licha ya kufanya shughuli hizo za mashambani na za ufundi,lakini pia zikawa zimekubaliwa shughuli nyingine kama vile ufugaji. Hvyo kukaanzishwa miradi mbalimbali ya kufuga kuku, kufuga ng,ombe, nguruwe, mbuzi, bata nk. Watu wakaanza kufuga ng’ombe wa maziwa , wakawa wanafuga kuku wa mayai na wa nyama. Ni kweli kuwa miradi hiyo ikawa imeshamiri sana na hivyo watu wakaweza kujikusuru kwa namna fulani.Ikatokea hata wafanya kazi wengine wakaamua kuacha kazi na kujiingiza katika mambo ya miradi hiyo ya ufugaji hasa wa kuku.

Jambo la kusikitisha na kwamba mahali pa kufanyia shughuli hizo za ufugaji hapakuwa pameandaliwa. Hivyo wale waliokuwa wameamua kufanya shughuli hizo wakatafuta kila mahali palipowezekana. Ikawa imetokea kuwa watu wakawa na mabanda na hata vizizi karibu na nyumba za kuishi. Kumekuwa na vizizi vya kufugia ng’ombe karibu kila kona ya miji yetu na hasa katika jiji la Dar Es Salaa. Ufugaji huo ni kweli unaleta kero kubwa sana kwa wakazi wengine wa mjini. Ni jambo la kuudhi sana kushuhudia harufu mbaya sana katika sehemu mbalimbali za miji. Kuna sehemu ukipita unakumbana na harufu ya mavi ya ng’ombe, kuna sehemu nyingine mtu anakumbana na mavi ya kuku, sehemu nyingine unasikia harufu ya mbuzi. Ukizunguka huko unatishwa na harufu ya nguruwe. Hivyo uzuri wa mji hauko kabisa kwani harufu chachu zimeenea licha ya harufu za uchafu wa kawaida kutoka majumbani mwao.

Licha ya huo uchafu, hao wanyama kama vile mbuzi hata ng’ombe wanaleta kero kubwa sana hasa wanapoachwa kuzagaa mitaani. Imekuwa ni kawaida ya wafugaji wengi kuwacha hao wanyama wao wazagae mitaani na hivyo kuleta usumbufu mkubwa sana kwa watu wapitao hasa madreva.Inaonekana kuwa pengine hao wafugaji au wenye wanyama hao hujiamini kiasi kwamba wanaona hao wanyama hawawezi kutendewa cho chote kile na hivyo mwenye kuwa na tahadhari siyo mfugaji, bali mpitaji.

Ni kweli kuwa ufugaji, kma ulivyokusudiwa ni zoezi na kazi nzuri na yenye faida kwa mwananchi. Lakini inapofikia kiwango cha kuleta kero na hata kuhatarisha maisha ya binadamu wengine, hapo sharti njia nyingine zichukuliwe ili mambo yaende vizuri. Tunapenda kumpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Jiji, Ndugu Charles Keenja kwa hatua ambazo atazichukua ili kuliweka Jiji letu katika hali nzuri, na njia mojawapo ni kuwaondoa hao wanyama wanaozangaa mitaani. Tunatumaini kuwa hao wafugaji watamwelewa vizuri na hivyo kuweza kukubaliana na uamuzi wake huo.

Ni kweli kuwa hakuna mfugaji anayependa kuwa mbali na mifugo yake. Lakini tena kwa upande mwingine haiwezekani kabisa kuruhusu faida ya mtu binafsi iwadhuru na kuwakosesha raha majirani. Mtu anapoamuwa kuishi pamoja na wenzake anapaswa daima kujitahidi kuondoa mambo yale ambayo huleta kero na usumbufu kwa majirani. Kuleta mifugo ndani ya miji, au kuishi karibu na mifugo ni kinyume kabisa cha afya. Hao wanyama kwa ujumla ndio wenye kuleta mainzi mengi katika miji yetu na hivyo kusababisha magonjwa kama vile kipindupindu. Ni nani asiyetambua kuwa kinyesi cha kuku au cha ng’ombe huleta mainzi ambayo huhatarisha afya za watu?

Nawakumbuka sana wale Wamisionari wetu waliotuletea Dini ya Kikristo pamoja na ustaarabu, jinsi walivyokuwa wanaitunza mifugo yao. Popote pale walijenga vizizi vya ng’ombe, vya nguruwe na kuku mbali na nyumba za kuishi watu. Tunasema kuwa huo ndio ustaarabu halisi. Lakini inapofikia kuwa mtu anakuwa na zizi la ng’ombe au nguruwe katika sehemu anayoishi na wenzake, hapo tunatambua kuwa kuna kasoro katika ustaarabu wetu. Kuna watuwengi wanaanzisha miradi ya ufugaji bila kufanya utafiti kuhusu sehemu anayotaka kufanyia huo ufugaji, hasa kuhusu afya na usumbufu kwa majirani. Jambo linalotawala mara nyingi ni ule ubinafsi, yaani kutafuta tu faida ya binafsi bila kuangalia kama wengine wanaathirika na mradi huo au sivyo.

Katika Kauli Yetu hii kwanza tunapenda kuwapongeza hao wenzetu wafugaji kwa jitihada hizo za ufugaji wa wanyama mbalimbali. Tunawapongeza sana kwa juhudi wanazozifanya katika kuwatunza wanyama hao kama vile kutafuta chakula, majani, madawa na mambo mengineyo ambayo hutakiwa kwa ajili ya mifugo yao hio. Linakuwa ni jambo la kutia moyo sana tuonapo magari madogo yakipita barabarani huku yamebeba majani kwa ajili ya ng’ombe. Tunasema hongera sana.Lakini pia tunawasihi kama inawezekana, shughuli hizo zingefanyika huko mashambani na hivyo kupunguza kero za wakazi wa miji .

Ikiwa tumeamuwa kuishi mijini, basi tunapaswa kweli kushika taratibu za mijini. Hapo tunapoambiwa kuwa tuache ufugaji wa wanyama mijjini, tunapaswa kuwa watii. Miji yetu inapaswa kuwa kama vioo vya nchi yetu hasa Jiji letu la Dar Es Salaam. Sisi hatuelewi ni kwa jinsi gani wageni hutuona wanapotutembelea na kufika kushuhudia sehemu mbalimbali za Jiji zimejaa ng’ombe, nguruwe, kuku nk. Na sehemu hizo zinajulikana kama ni sehemu za watu wakubwa hapa nchini. Tunasema tabia hiyo ni ya aibu kabisa na tunapaswa kuondokana nayo kabisa tukitaka kweli jiji letu na miji yetu kwa ujumla ilinganelingane na miji mingine hapa ulimwenguni.

Tunapenda pia kuimalizia Kauli Ysetu hii kwa kumpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Jiji katika hatua anazozichukua ili kulifanya jiji letu lipendeze.Hivyo pia tunatoa rai na kuwaomba Wakurugenzi wote wa miji yetu hapa nchini wasilionee aibu jambo hili la kuiweka miji yetu katika hali nzuri ya kupendeza. Hao Wakurugenzi watambue kuwa ni wajibu wao wa kuyafanya mazingira ya miji yetu yawe mazuri na ya kupendeza kwa wakazi wake na pia kwa wale wote wanao ishi humo.

Wakatoliki tujirudi kiimani

Mhariri,

Naomba tena nafasi ndogo katika gazeti hili letu tukufu la KIONGOZI linaloongoza na hali mengine yananyemelea nyuma .

Kutamka ukweli mtupu na kujaribu kujiweka wazi ni kwamba sisi Wakristo wapendwa Wakatoliki kwa njia moja au nyingine tumelegea katika kuitangaza imani yetu.

Kwa mafikira yangu binafsi na pia kwa maono yangu binafsi, naona hii imesababishwa na wingu kubwa linalotukumba la kuibuka kwa makanisa mengi ulimwenguni hususani ya Kilokole.

Makanisa au madhehebu haya yanatofautiana katika imani zao na taratibu zao za ibada na hii ndugu Mkristo isikuchanganye, kwa vile hii ni hesabu rahisi kwani baada ya kujumlisha makanisa haya mengi na imani zao, kule mbele jibu litakuwa "Tunamwabudu Mungu Mmoja bali kwa njia tofauti" . Wakatoliki nawasihi tuwe na msimamo mmoja na madhubuti tuitangaze imani yetu bila kuogopeshwa na madhehebu haya mengine.

Mahudhurio katika makanisa yetu ni ya kiwango cha juu sana, lakini Je, imani yetu ipo juu vile vile ?

Kama jibu ni "ndio" sawa, maana kila mmoja wetu atapiga goti mbele ya Kristo na kujikitetea mwenyewe .

Acha niwe muwazi, moja ya mabo yanayoturudisha nyuma tushindwe kuisukuma imani yetu mbele ni kutojali.

Tukiwa kanisani kuna Neno la Mungu kwa hiyo basi linaposomwa inabidi tuwe makini sana katika kusikiliza Neno hili Takatifu, tuwe watulivu na adabu iwe inatawala mioyo na akili zetu. Lakini utaona wengi wetu tumekaa wengine wanasinzia kanisani, watoto wanalia na kucheza ovyo wengine wanawaza mbali kana kwamba wanasikiliza tu.

Sana sana wanakumbuka kunena "TUMSHUKURU MUNGU" au "SIFA KWAKO EE BWANA" maana haya ni maneno tuliyozoea na hayahitaji kufikiria chochote .

Baada ya misa tukijaribu kuulizana maswali kwa ajili ya kutafakari Neno la Mungu kwa siku ya hiyo, wengi hawakumbuki hata neno moja, lakini sote tumekuja kanisani na tunatoa sadaka na kuipokea Sakramenti Takatifu.

Jamani wenzangu Wakatoliki tujirudi tena tuitetee imani yetu na tuiangalie tumetoka wapi na tunakwenda wapi Kikristo na tutembee pamoja Kiimani kama vile Sinodi yetu inavyotuelekeza katika Ukombozi wa Kiroho.

Upande wa sadaka nao kuna vichekesho.

Sadaka ni zawadi unayoipeleka Altareni ili kumshukuru Bwana Mungu aliyetupa sisi tulicho nacho na bila sadaka hii hatungesali katika nyumba na wala hatungeweza kupata huduma tuzipatazo kutoka kwa viongozi wetu mapadre maaskofu ,masista, na kadhaalika.

Kwa hiyo tusiangalie wingi wa watu na wingi wa sadaka zetu, tujichuinguze wenyewe na tujue tutatoa kiwango gani. Kitendo cha kutoa sh 10/= au 20/= hata 50/= mtu mzima ni aibu. Kumbuka kuwa Kristo anakuona mpaka moyoni mwako.

Jamani hata sh. 100 ni kidogo, afadhali tutoe kwa moyo na Mungu atatuzidishia. Nawatakieni au tutakiane kheri na baraka za Mungu na tusiwe waoga katika kuikiri na kuungama IMANI yetu siku zote, mahali popote na muda wowote! Barikiweni sana Ndugu zangu.

Ni mimi mwenzenu,

Valery A. Mrema.

Box 3622

Dar es Salaam.

 

Jambo jema ukitaka litendeke, anza mwenyewe

Ndugu Mhariri,

Nimeshitushwa sana na vitisho vya matarajio ya kuua yaliyoandikwa katika gazeti la "Msema Kweli." Kwa miaka mingi Waislamu wamekuwa uwakiukashifu Ukristo hali Wakristu wakiwa kimya tu wasijibu lolote. Baada ya kuvumilia kwa muda mrefu nao wameona vema watoe majibu ya ukweli namna ulivyo lakini ndugu zetu Waislamu wanaonesha dhahiri kuchukizwa na ukweli huo .Je, Kulikoni?

Dini yoyote ni fumbo au siri ya Mungu kwani hakuna awezae kufafanua undani wa Mungu. Duniani zipo dini au madhehebu zaidi ya elfu mbili zote zinamkiri Mungu huyo huyo. Ajabu ni kwamba:

(I) Kila dini wapo wenye elimu ya juu kuhusu dini hiyo na ya dunia pia.

(Ii) Wapo viongozi mahususi kwa kila dini.

(Iii) Hakuna dhehebu ambalo limeshukiwa na mtu au malaika kutoka mbinguni na wala aliyekufa na kisha kurudi tena duniani. Yote mema tutendapo ni imani zetu tu juu ya kumwendea Mungu na kuishi kiungwana hapa duniani.

Dini au dhehebu pekee bila matendo mema kufuatia mapenzi ya Mungu, haimfikishi mtu kwa Mungu bali matendo yote mema yanayoongozwa na dini hiyo na waamini wake. Mimi nikiwa Mkristu au Islamu na ni mwizi; au mchawi na kadhalika kamwe kuitwa Mkristo au Muislamu hakutanifikisha kwa Mungu. Hata mpagani akizitii dhamiri zake njema na kutenda hivyo, Mungu ni mwenye haki na huruma atamfikisha tu kwake.

Kama ni kweli kuwa mnarotarajia na kutumainia ni agizona Neno la Mungu, kwa nini mnaogopa serikali kwa kutotaja majina yenu? Je, serikali na Mungu, mkubwa ni nani? Sio Mungu? Ukweli wa kila uamuzi wa dini yeyote ni lazima upitie kwa viongozi wa dini hiyo;nao wajue vipi kuamua na wala sio bungeni au kufanya mauaji.

Ikiwa kiongozi wa serikali kama mbunge au Waziri anaingilia maswala ya dini bila kuombwa na viongozi wa dini hiyo (ingawa yeye pia ni miongoni ma waamini wa dhehebu hilo) basi huyo kiongozi ni wa hatari katika jumuiya na hivyo haifai jamii kabisa.

Namshukuru Mungu kwa kunipa ufahamu kuwa kuua kwa namna yeyote ile ni dhambi.

Tumsifu Yesu Kristu

Wenu Mzee S.M. Nganga

Box 7472.

Dar

 

Tuwajibike makazini

Ndugu mhariri,

Naomba nieleze machache kuhusiana na watu kushindwa kuwajibika katika kazi zao.

Utakubaliana nami kuwa kwamba japokuwa watu wameajiriwa na wanayo majukumu mbalimbali kutegemeana na nafasi zao lakini wanashindwa kujua kwanini wapo hapo na wanafanya nini.

Hata kama tutachukulia mifano rahisi katika baadhi ya maofisi hususani ofisi za Serikali tukiachilia mbali zile za watu binafsi utakuta mtu yupo ofisini nashindwa kujua kwa nini yupo hapo unapouuliza jambo fulani linalihisi ofisi yake atakwambia njoo kesho au kesho kutwa hata kama sala lenyewe halihitaji kupewa muda wa kutosha kiasi kile.

Ndugu Mhariri kutokana na kushindwa kuwajibika kikweli katik maofisi sisi watu ambao tupo nje ya ofisi tunaathirika na tunaumizwa sana na tabia hizi.

Pia turudi nyuma tujiulize hivi mfanyakazi amepewa cheo kwa ajili ya kuidumia ofisi yake atashindwa kujua mambo yanayoihusu ofisi yake.

ukweli uliopo ni kwamba kila mtu anatakiwa wajibike kikweli katika nafasi yake na hakuna haja ya kumsumbua mtu anayehitaji huduma kwake kwa vile watu wapo kwa ajili ya kutoa huduma hakuna haja ya kumueleza mtu njoo kesho wakati jambo lenyewe linawezekana kwa wakati huo au ni kutafuta rushwa?

Mpenda haki,

Willbroad Bandihai

Dar es Salaam