Biashara huria inapozidi

NCHI YETU inafurahia siku hizi kitu kinachoitwa Biashara huria au soko huria la bidhaa mbalimbali. Watu wale wenye uwezo wa kuwa na mali wanakuwa nayo kwa kutumia njia mbalimbali wanazoweza na wanazozijua. Ni kitu cha kawaida kuwa na vitu vingi sana katika maduka na sehemu mbalimbali za biashara. Tunasema kuwa jambo hilo ni zuri sana kwani kuna ule unafuu wa kupata bidhaa tukilinganisha na jinsi mambo yalivyokuwa hapo siku za nyuma.

Wingi wa vitu umekuwa hata katika vyombo vya usafiri. Kwa hivi sasa kuna magari mengi sana ya abiria. Kuna mabasi mengi yanayofanya kazi ya kubeba wasafiri katika miji, na yako yale yanayokwenda kule mikoani. Mtu akifika kwenye kituo cha mabasi anahangaikiwa sana na pengine jambo hilo huleta kero kwa msafiri kwani badala ya kumsaidia huonekana huyo msafiri ananyanyaswa kwa namna fulani. Karibu kwa kila basi kuna wale wapiga debe ambao kazi yao ni kuita na hata kutafuta abiria. Kwa njia hiyo kumekuwa na ajira kwa vijana wengi. Lakini tunajiuliza jambo hilo ni kweli lina faida au sivyo?

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Tume ya Jiji, Mheshimiwa Charles Keenja, amesema kuwa kuna haja ya kukomesha zile Daladala zinazojulikana kama Vipanya au Hiace. Alisema kuwa hayo magari hayana uhalali wa kubeba watu kwa kadiri ya muundo wake. Pia alitamka kuwa magari hayo yanaleta kero kwa wasafiri na hivyo iko haja ya kuingiza magari yaliyoundwa kwa ajiri ya shughuli hizo za kubeba abaria. Kwa uungwana kabisa amewatahadhalisha wenye mabasi hayo wajaribu kufanya juu chini kurekebisha jambo hilo wakitaka kuendelea na biashara yao hiyo.

Watanzania tulio wengi tunatambua kuwa siku ya leo kuna unafuu kabisa wa usafiri katika nchi yetu, lakini kama tulivyosema hapo juu, biashara hii huria ina madhara yake. Katika kuzungumza na watu mbalimbali nikaambiwa kuwa kuna Watanzania wachache ambao ndio wenye mabasi hayo mengi. Ni jambo la kushangaza kusikia kuwa kuna watu binafsi ambao wana hivyo Vidaladala zaidi ya 15 na wengine hata ishirini. Ni kweli kuwa tumekubaliana na ile biashara huria na pia tumeikataa ile siasa ya ujamaa na tukaikubali ile siasa ya kipepari. Hata hivyo tunapofikia hali ya mtu kuwa na magari mengi sana ya biashara na watu wengine wakiwa katika hali duni mno, tunaweza kujiuliza, je, tunakwenda wapi?

Kwa kuwa hiyo ni biashara huria basi kila mwenye magari huwa anajipangia anavyotaka. Nasikia kuwa wale wahudumu wa hayo magari wanaambiwa kiasi cha kumletea huyo tajiri kila siku. Kwa vile magari hayo ni mengi, na hela wanazodaiwa ni kiasi kikubwa, basi wanalofanya ni kukimbiakimbia na hata kuvunja sheria za barabarani ili mradi wamefanikiwa kupata hela zinazotakiwa kwa ajili ya kumpa tajiri na pia kwa ajili yao wenyewe. Kwa hiyo si jambo la ajabu kuona hao madreva na wahudumu wa madaladala wanakuwa kama wendawazimu katika shughuli hiyo ya uendeshaji magari. Je, nani ambaye hajakumbana na kero za madreva wa Daladala?

Vituo vyetu vilivyo vingi katika miji yetu havikuwa vimeandaliwa kwa ajili ya magari mengi kama ilivyo siku hizi. Hivyo kuna ule msongamano mkubwa sana wa magari hayo madogo. Hivyo tunaona jinsi uegeshaji wa magari hayo unavyokuwa mgumu sana hasa katika Jiji la Dar Es Salaam. Tunatumaini kuwa kwa njia ya kupunguza wingi wa magari na kuingiza magari makubwa nafasi ya kuegesha magari ya abiria itakuwa ya unafuu sana. Hatusemi kuwa tatizo hilo litakwisha, la hasha, bali tunatumaini kuwa mambo yatakuwa na unafuu katika Jiji letu.

Hapo tunapenda kuungana kabisa na Mwenyekiti wa Tume ya Jiji katika kuleta mabadiliko ya magari ya abiria katika Jiji na miji mingine. Ni kweli kuwa katika miji mingi hapa ulimwenguni, magari makubwa hutumika katika kubeba abiria na hivyo vituo vyake ni kwa ajili ya shughuli hiyo.Kwa wale wenzetu ambao wamebahatika kusafiri katika nchi za wenzetu na kuona jinsi mambo ya usafiri yalivyo, natumaini watakubaliana na mapendekezo hayo ya Tume la Jiji. Hatuelewi ni nani ambaye alianzisha mradi huu wa ‘VIPANYA’ katika miji yetu. Na pia tunajiuliza ni nani aliyefanikiwa kuua ile huduma ya UDA na KAMATA katika nchi yetu hii. Hilo ni jambo la kusikitisha sana ambalo limekuwa ni kama vile ugonjwa katika taifa letu. Tumekuwa na tabia ya kuua vitu vya umma na kuingiza vya binafsi, lakini vyenye faida binafsi na hasara kwa umma.

Kwa upande mwingine tunatambua kuwa hao wenzetu wenye magari watapata "hasara" kwa namna fulani, lakini madhara ambayo wanatuletea ni makubwa zaidi na hivyo yafaa kabisa tuepukane nayo. Tunajua kuwa wengi wa wenye mabasi hayo baada ya mabdiliko watakuwa hawana biashara kama wafanyavyo sasa hivi. Hakuna asiyetambua kuwa Daladala zilizo nyingi ni mali ya "wakubwa" na hivyo kama ni kuchuma, basi wamechuma kiasi cha kutosha kwani mali kama mali haishibishi kamwe.Tunaloliomba ni kwamba mabadiliko hayo yafanyike bila kuwa ni upendeleo au woga. Ni dhahiri kuwa Tume ya Jiji haina lengo la kumkomoa mfanyabiashara yo yote yule, lakini hasa ni kwa ajili ya ufanisi na haduma nzuri kwa wananchi.

Kwa upande mwingine tena tunajua kuwa kukomesha magari hayo ya Daladala au Vipanya kutapunguza ajira ya vijana wengi. Jambo hilo ni la kweli kabisa, lakini tunapaswa kujiuliza tena kama ni kweli kuwa hakuna ajira nyingine ya mtu binafsi kama vile kilimo, ufundi nk. Ni kweli kuwa shughuli ya kijana kutembea kwenye gari ni rahisi zaidi kuliko ile ya kushinda shambani na kupigana na jembe. Vijana wengi sana wamo kwenye magari wakipoteza nguvu kazi yao bure katika kupigapiga kelele siku nzima kwenye magari. Watanzania tunao ule utajiri wa nguvu kazi katika vijana wetu, lakini kumbe haitumiki kabisa. Tunaingiliwa na njaa kwa sababu vijana wengi wanapenda kuning’inia kwenye magari, na hawataki kufanya kazi ya kuzalisha.

Tunapenda kumalizi Kauli Yetu hii kwa kuitakia mafanikio hiyo Tume ya Jiji, pamoja na Idara nzima ya Uchukuzi katika zoezi hilo wanalotaka kulifanya kwa ajili ya ufanisi wa huduma kwa wananchi. Pia tunawaomba wahusika wawe na ushirikiano katika zoezi hilo, kwani bila kuwa na ushirikiano pamoja na uelewano si rahisi kufanikiwa.

 

Hospitali binafsi zisijali pesa kuliko uhai wa mtu

Ndugu Mhariri,

NAOMBA nafasi katika gazeti lako ili nitoe maoni yangu machache kuhusiana na hospitali za watu binafsi.

Kwa upande mwingine tunaweza kusema tumeendelea upande wa matibabu kutokana na ongezeko la hospitali binafsi ambazo sasa ni nyingi hasa tukichukulia jiji la Dar es Saalam. Lakini tukirudi nyuma na kuangalia kwa makini tunaweza kujikuta tunaumia vibaya mno na tukaziona hospitali hizo hazina manufaa kwetu.

Ndugu mhariri sina maana ya kuzipinga hospitali za watu binafsi, ninachotaka kusema ni jinsi gani hospitali hizi zinaweza kuwasaidia watu au kuwaua kabisa bila wao kujua.

Nayasema haya kwa mifano ambayo ipo hata ukienda leo katika baadhi ya hospitali.

Chukulia mfano unaumwa ugonjwa wa Typhoid; unaweza kuandikiwa dawa za Malaria, wakati mwingine utalazimishwa kumuona daktari hata kama si lazima au kupima vipimo vya gharama kubwa hata kama unaumwa kichwa na wakati mwingine unaweza kuambiwa umeishiwa maji na ukaambiwa uwekewe chupa tatu hata kama muhimu ni moja.

Kwa vile watu wengi hawakusoma na hata kama wamesoma hawana utaalamu wa kidaktari kwa mtazamo wa kawaida watakubaliana na watakavyoambiwa.

Ndugu mhariri hapa si kuuana?

Napenda kutoa maoni yangu kwa hao watu wenye hospitali pamoja na madaktari wao wawe waaminifu kwa kazi wanazozifanya, wasijali kupokea hela bila kujali uhai wa watu.

Pia watu wote wanaohusika kutoa huduma wasiwe wakali wakati wa kuwapokea wagonjwa. Wawe wanyenyekevu kwa vile mtu anayeumwa anahitaji kubembelezwa na si kufokewa.

Naishauri pia serikali iagalie upya suala hili, kwani wapo watu wengi wanaoumia na pengine wengi wanapoteza maisha yao.

Mpenda haki

Wilbroad Bandihai

S.L.P 413

Dar Es Salaam,

Tanzania.