KAULI YETU

Tufanye utafiti na tupange sio kukurupuka

MARA kwa mara watu huulizana: 'Je, una mpango gani?"

NI jambo jema na la msingi kwa mtu yeyote mwenye kutaka mafanikio yawayo yoyote yale kuwa na mipango.

TUNAWEZA kusema kuwa watu wale ambao tunawaona katika hali bora imetokana na kuwa na mipango. Mtu anapofanya mipango ni kwama anajiwekea malengo fulani ya kufika akitumia mbinu fulani na misaada fulani.

INAONEKANA kuwa wananchi wengi hukosa kuwa na mipango katika utendaji wao. Mapato yake ni kwamba hushindwa kuendelea yaani kufikia malengo wanayotarajia.

WATAALAMU hutuambia kuwa kila anayesafiri inampasa kufahamu ni wapi anaelekea. Ikiwa msafiri hajui anakoelekea itakuwa vigumu kwake kufahamu kama ameshafika kule alikotarajia kwenda ama sivyo.

HIVYO ndivyo mambo yalivyo pia katika shughuli zetu za maendeleo. Tunapaswa kufahamu ni wapi tunakoelekea. Tunapaswa tufahamu pia ni mbinu gani tutazitumia ili kufikia upeo huo.

WANASIASA wetu wamekuwa wakituambia kuwa "kupanga ni kuchagua" Hatuwezi tukafanya kila kitu kwa wakati mmoja. Kwa hiyo inatupasa tuchague ni jambo lipi tuanze kulifanya. Tunapaswa kuona mbele. Wahenga wetu hutuambia kuwa huwezi kufukuza sungura wengi kwa mara moja. Hivyo pia hatuwezi kuwa na miradi mingi kwa mara moja au kwa wakati mmoja.

KUMEKUWA na kukwama kwa miradi mingi katika taifa letu kutokana na ukosefu wa mipango.

KUNA miradi ya watu binafsi ya mashirika na hata ya serikali ambayo imekwama kutokana na huo ukosefu wa mipango. Tunashuhudia nyumba nyingi ambazo zimejengwa nusu nusu tu. Ni kutokana na ukosefu wa mipango ya fedha na matumizi. Katika kufanya mipango huwa pia kunafanyika makadirio.

PENGINE watu huamua kuwa na miradi inayowazidi nguvu zao. Lakini kama wataketi chini na kufanya makadirio kulingana na uwezo wao, mambo yatakwenda vizuri zaidi.

TUNAPOZUNGUMZIA mambo ya maendeleo iinatupasa kutilia mkazo idara zetu za mipango na pia makadirio hupaswa kuwa imara.

IDARA ya mipango ni kama vile usukani katika shughuli zetu za maendeleo. Tunavyofahamu gari bila usukani haliwezi kwenda mbele wala kurudi nyuma.

HIVYO shughuli za maendeleo haziwezi kufanikiwa bila kuwa na idara ya Mipango.

TUNAHITAJI idara hiyo katika maendeleo yetu binafsi na yale ya taifa. tukumbuke kuwa mtu binafsi anapofanya shughuli ya maendeleo na kufanikiwa huliletea maendeleo hayo taifa zima.

KWA hiyo kila jitihada tufanyayo katika maisha yetu huwa ni mchango wa namna fulani kwa taifa. Lakini pia kinyume chake kila namna ya kushindwa kufanikiwa katika utendaji wetu pia ni hasara kwa taifa.

MAENDELEO ya kweli hupatikana kutokana na kuchangiana utendaji na juhudi. Utendaji huwa bora ikiwa kuna mipango ya kueleweka.

KUFANYA mipango katika utendaji wetu ni sawa kama kutenda kwa kutumia akili. Mtu yule mwenye kutumia akili katika utendaji tunaweza kumwita ni mwenye busara.

WATAALAMU wanatuambia kuwa kabla ya kutenda chochote kile inatupasa tuwe tumefanya utafiti. Utafiti ukisha kamilika hapo tunaweza kufanya mipango ya utekelezaji wa lile jambo tunalotaka kulifanya.

TUNAAMINI kuwa kila anaeshughulikia mipango katika jamii sherti ajihusishe na wale wenye kufanya utafiti wa kina katika jambo ambalo anataka kulifanya.

TUNAPENDA kuwasihi Wananchi na serikali kwa ujumla kuzingatia sera ya mipango katika utendaji. Tusivamie miradi bila kuwa na maandalizi iliyo katika utafiti na mipango thabiti.

TUNAAMINI kuwa wakati umefika ambapo hatustahili kupoteza tena nguvu zetu bure pamoja na vifaa mbali mbali kwa sababu ya kutokuwa na mipango au kutokufanya utafiti wa kina.

KADIRI tunavyozidi kukaribia mwaka 2000 na kuingia karne ya 21 tunapaswa kubadilisha namna ya utendaji wetu tukiwa hasa watendaji wenye mipango.

 

Ili kuondoa Uhalifu; nani aadilishwe?

Na Joseph Sabinus

KATIKA vyombo vya habari hapa nchini hususani karibu kila toleo la gazeti; halikosi habari inayohusu aina fulani ya uhalifu kama vile wizi, uvutaji bangi, ubadhirifu wa mali ya umma, ujambazi, rushwa, ubakaji na hata unajisi wa watoto wadogo ambao hivi sasa umekithiri.

Kila iana ya uovu imepewa kisingizio chake ili kuubariki uovu huo ndani ya jamii. Ujambazi sasa ndio unachukuliwa kama ajira miongoni mwa vijana, utoaji mimba sasa unachukuliwa kama njia ya kudhibiti kasi ya ongezeko la watu, mauaji yanachukuliwa kama fagio la magugu watu.

Rushwa imechukuliwa kama motisha au asante kabla hata huduma haijatolewa, ubakaji na unajisi wa watoto wadogo umechukuliwa kama zoezi la zinaa pasipo kujali athari zake kiafya na kijamii.Imesahaulika kabisa kuwa ubakaji, ulawiti na unajisi wa watoto wadogo ni aibu isiyomithilika wala kuvumilika; inayompa mnyama heshima ya kuwa binadamu na binadamu kupewa hadhi ya mnyama, mdudu au hata chini ya hapo.

Kwa mujibu wa barua ya Chama cha Wafanyakazi wakristo Tanzania ya Agosti 5, 1997 iliyosainiwa na Mwenyekti wa CWM, Mathias Kimira ikiwaalika watu katika kongamano (mkutano wa wazi) juu ya mada ya Unajisi wa Watoto wadogo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii wanawake na Watoto, Idara ya Sheria, idara ya Polisi, Kanisa na Msikiti walishiriki.

Inasema utafiti ulifanywa na Umoja wa Mataifa mwaka 1990 unaonyesha kuwa serikali za nchi zilizoendelea hutumia asilimia 2-3 ya bajeti zao kila mwaka kupambana na uhalifu; wakati serikali za nchi zinazoendela zinatumia asilimia 9-14 za bajeti zao kupambana na uhalifu kwa kupanua jeshi la Polisi, kupanu ana kuongeza Magereza, kununua magari na vifaa vya kisasa; lakini matokeo yake si kwamba hayaridhishi tu, bali yanazidi kuwa duni.

Matukio mbali mbali ya ujambazi yanayotendeka nchini hapa yatuonyesha dhahiri namna Watanzania tulivyo katikati ya janga hili la kuathirika kutokana na aina hizo za uhalifu; iwe kazini, shambani, nyumbani katika majumba ya starehe, misikitini na hata makanisani.

Watu wengi dunaini wanaamini kuwa serikali za nchi zao zenyewe ni sehemu kubwa ya mchango wa tatizo la ongezeko la uhalifu kwani watuhumiwa wengi huachiliwa bila hata ya uchunguzi wa kina kufanyika; hivyo kuwawezesha watuhumiwa wengine kuendesha uhalifu zaidi sambamba na kuendesha ulipizaji visasi kwa waliohusika na kukamatwa kwao. Endapo wameadhibiwa hautashangaa kuona kuwa adhabu wanayopewa ni ndogo sana ukilinganisha na ukubwa wa kosa husika.

Hii ni sababu tosha iliyopelekea wananchi kuamua kuwaua kwa vipigo au moto watu wanaoutuhumiwa kwa kuhusika na uhalifu wa namna moja ama nyingine inayowakera zaidi hususani wezi, wabakaji na wanaonajisi.

Rushwa kutoka ngazi za juu serikalini imekithiri katika nchi nyingi duniani ikiwemo hii ya Tanzania watu wanajiuliza kuwa ni vipi wakuu wa serikali na vyombo vya dola wanaweza kupambana na uhalifu wakati hao wenyewe wana sura na mikono yenye matope ya uhalifu hasa huu wa rushwa? Serikali zinaundwa na kuvunjwa lakini uhalifu bado upo palepale; Je, nani ataweza kuuondoa uhalifu ndani ya jamii yetu? Kwa kila mwenye timamu ya akili; hatasika kusema kuwa hali inatisha.

Hapa Tanzania serikali imeunda tume nyingi ikiwemo hii ya kudhibiti kero ya rushwa inayoongozwa na Mh. Joseph Sinde Waryoba, waliokumbwa na mtego huo; walikumbwa; tuwape pole zetu lakini Wakome, na wenye bahati washukuru na kumuomba Mungu awazidishie mwaka wa kukwepa na kuruka viunzi hivyo lakini wajue siku za mwizi ni arobaini.

Lakini, wasiwasi wangu ni kwamba tume ya Mheshimiwa labda iliwatupia macho vigogo wanaokula mlungula wa mamilioni ya fedha; tena kwa kupitia akaunti za benki. Ndiyo maana sina shaka kuwa wote mtakubaliana nami kwamba labda kila wala rushwa kumi; labda kama bidii ilifanyika sana, walikamatwa wawili.

Sidhani kama kweli tume ya Mheshimiwa ilituma makachero wake katika anga za walala hoi na wanyonge wanaoshindia uji wa muhogo usio na chachu; tena wa kubahatisha. Wanaodaiwa hata shilingi mia moja tu; ambayo wangenunua dagaa halafu wasikate vichwa kwa ajili ya watoto wao wanaotambaa, si rushwa ni rushwa tu; iwe ya shilingi moja au bilioni moja?

Ninasema hivyo kwani licha ya kuwepo kwa tume hiyo ya kudhibiti mapato ya 'giza' bado sehemu nyeti zinazowagusa wananchi kwa karibu zaidi na kwa kila siku, ndizo maduka ya kuuzia haki kwa 'mwenye nyingi;. Ni kwa uchungu huo ninaishauri serikali na tume hiyo ya Mheshimiwa Waryoba iwatume kisisiri wajumbe wake katika mahakama za ngazi zote. Hata mahakama za mwanzo na hospitali.

Tena makachero waende 'kichovu' bila taarifa yoyote; ila wawe makini ili wasijekuambukizwa ugonjwa huo wanaokwenda kuutibu. Ndiyo! waende. Waende waone namna majalida ya kesi yanavyozunguka vyumba bila sababu eti yanatafuta kalamu, waende waone namna wanavyonyang'anywa pesa ili kuwadhamini ndugu zao.

Wasiishie huko, waende hadi kwenye vituo vya polisi waone namna askari hao wanavyopata mishahara mitatu kwa kazi moja. Mlalamikaji hudaiwa 'chochote' eti huita posho ya kumkamata mhalifu. Nae mlalamikiwa lazima ndugu zake watoe 'kitu kidogo' ili apate dhamana na ndipo, humalizia kwa mshahara ule wa mwisho wa mwezi. Kama hali ni hiyo, nani ataondoa maovu wakati hata ukitoa taarifa ya polisi kudai rushwa; wewe ndiye utatupwa 'lupango' kama gunia la ndizi? Au basi nani asiyejua zile staili za mahakimu?

Makachero wa Waryoba hebu vaeni kienyeji muende hospitali huku mmejiunguza walau kichwa muone.

Sasa niungane na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA). Nizungumzie suala la unyanyasaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia ambao ni pamoja na watoto na wanawake kulazimishwa kwa hali na mali kufanya ukahaba , kunajisiwa, kulawitiwa hali ambayo imewakumba sana watoto wadogo kati ya miezi mitatu hadi kumi na minne; jambo ambalo hivi sasa limezoeleka masikioni.

Cha kujiuliza hapa ni kuwa ni nani anayefanya uhalifu huo na ni nani mwenye jukumu la kuuondoa ndani ya jamii yetu? Hebu Watanzania tuwe makini; tusifanye ujanja wa Popo kumnyea Mungu kumbe anajinyea mwenyewe.

Ninachotaka kuelezea hapa ni masikitiko yangu kwani ni ukweli usiofichika kuwa karibu kila idara muhimu inayotegemewa katika kuiadilisha jamii, imekwisha kumbwa na kashfa hii. Sasa Watanzania wenzangu kama sisi hao ndio washiriki wakuu wa kubomoa maadili toka shina hadi kilele; mani atauondoa uhalifu ndani ya jamii kama sio mimi na wewe?

Kama watu wanaotegemewa na jamii kuwa viongozi bora wa kuigwa; ndio hao wanaokuwa mstari wa mbele, watoto wetu wajifunze nini kutoka kwetu, nani abadilishwe kati yetu na watoto; nini Tanzania ye kesho? Jamani taifa linakwenda pabaya; tumwe macho na tuache mzaha.

Kwa nini nisiyaseme hayo hali imefika hatua hata baba anaamua 'kula faida', mwane na hata mjukuu wake; tena eti kwa kubara? Walimu ambao jukumu lao ni kubwa katika kuelimisha na kuadilisha jamii nao sasa wamekuwa mstari wa mbele kufanya unyama huo kuliko hata wanyama wenyewe.

Tanzama hata wale viongozi wa dini wanaoimba kila siku kuwa wametumwa na Mungu kuhubiri habari njema za wokovu; ndio hao sasa kila siku hutakosa kuwasikia kuhusika na uvunjaji wa 'amri ya Sita ya Mungu; Usizini.

Imefika hatua hatua wagonjwa wanafia majumbani kwa kuogopa kwenda hospital au hata kwa waganga wa kienyeji wakihofia kubakwa.Sasa je ili kuondoa uovu nani aadilishwe;mtoto au mtu mzima?

Vyombo vya sheria vitambue haki kama haki na siyo biashara.Vijue kuwa kukidhiri kwa rushwa katika mahakama na polisi ni sawa na kuvilinganisha vyombo hivyo muhimu na kiumbe ambaye hakuzaliwa kabisa au kabisa niseme marehemu.Watu hawa kabla hawaja- adilishwa kisheria,wajiadilishe wenyewe kibinadamu.