LICHA YA WEMA WOTE.....

Mkwe alimuua Binti yangu kwa kumchoma kisu mbavuni

lMama yake alimfungia ndani binti yangu akimtoreshea kijana wake

lHeri achinjwe kuliko kutoa ushahidi"

MKATOLIKI mmoja mkazi wa Buhemba wilayani Tarime Mwalimu Morris Mathias wa shule ya msingi Rebu hivi karibuni alitangaza na kuchoma hadharani nyaraka zote za kesi na madai juu ya mme wa binti wake aliyemuua bintiye kwa kumchoma kisu.

Katika mazungumzo na mwandishi wetu Josephs Sabinus wilayani Tarime hivi karibuni mwalimu huyo anaeleza namna vijana hao walivyooana kwa mizengwe ;hata kuhitimisha kwa mauaji baina yao.

Binti wangu Paulina aliyezaliwa 1976 alikuwa anaendelea kusubiri matokeo ya mtihani wa kumaliza shule ya msingi na ule wa private

7/12/1990 mama wa kijana Protas Wambura Marko akatumia nafasi ya "rirandi" (ngoma ya Kikurya hutengenezwa kwa buyu kubwa) iliyokuwa inapita karibu na nyumbani kwao kijijini Nyamongo.

Mama huyo (Teresia Wambura) akawaita wenye rirandi ili watumbuize nyumbani kwake kwa muda ili kuburudisha familia. Nilipomuhoji binti wangu Paulina baada ya mikasa kuanza alisema: "Watu wote tulienda pale kucheza rirandi.

Akaja mdogo wake Marko anaitwa Baby eti akaniambia mama yake ananiita. Tukaenda; mimi nikamfuata hadi kwenye chumba cha kaka yake; nilikuwa sijui wanachoniitia . Nikashitukia mama yake anatufungia nje kwa kufuri mpaka usiku kama saa 6 alipokuja Protasi maana tangia asubuhi hakuwepo. Nikasikia anamwambia Protas aingie halafu atufungie tena nje mimi nikazidi kulia tu; tukakaa humo mpaka asubuhi"

Nilipomuuliza Paulina alichukua hatua gani sasa akasema; "Nilikuwa nalia tu si walinichukua bila hata kuzungumza wala Protasi hakuwa amenizungimzia kuhusu kunichumbia na wala hakuwahi kunisimamisha njiani kwanza Protas hatukuwa na mazoea nae.

Kesho yake niliposema nije nyumbani Protas akaniambia eti hautuamini eti ni kweli walinifungia bila mimi kupenda. Akasema eti anavyofahamu utaniua kwa kuwa ulikuwa unataka unitafutie masomo ndipo na mimi nikaogopa. Tukaenda Mugumu 8/12/90"

Tukaanza uchunguzi mpaka nyumbani kwa wahusika; wakasema hawajui lolote ndipo tukaenda kuripoti polisi Nyamwaga na baada ya siku mbili tukatulia nyumbani.

28/3/91 Paroko wa Nyamwaga Padre Cleophas Adeki akatuambia binti yupo kwa Mzee Marko Wambura amefichwa nje ya nyumba lakini naye hajui alipofichwa.

Sasa; wakawa wanamtumia padre huyo kama mpatanishi wao maana walijua mimi ni Mkatoliki na hivyo ni lazima nitamheshimu Padre wangu. Tukamtuma padre ili binti arudi nyumbani. Paulina akamwambia eti ni mjamzito na hivyo hawezi kuja na mimba nyumbani. Nilitaka arudi hata kama ana hiyo mimba si kitu, aje azae, aache mtoto aende masomoni maana matokeo alikuwa amechaguliwa kuingia kidato cha kwanza Tarime sekondari na hata ule mtihani wa KOWAK sekondari alikuwa ameshinda.

Bado akagoma eti kwa Wakurya ni mwiko binti kutoroshwa, kupata mimba na kisha kurudi nyumbani bila kuolewa.

Padre akatushauri, "Kama mnataka kuleta madhara, endeleeni kumlazimisha arudi." Ndipo mipango ya kuoana ikaanza 5/4/1991 Baba yake Protas akataka tuzungumzie mahari nyumbai kwake; akaogopa kuja kwangu eti ninaweza kumdhuru kutokana na hasira nilizokuwa nazo. Tukavutana mpaka mwezi wa 9 mwaka huo huo ikashindikana kuja kwangu au mimi kwenda kwake hadi ikibidi mazungumzo hayo yafanyike nyumbani kwa rafiki yake katika kijiji jirani cha Nyangoto mwanzoni mwa Decemba 1991 ili kujadili masuala ya mahari,Mzee yule akaomba radhi nikamsamehe.

Mzee yule alinitaka niseme kiwango cha mahari nilichotaka nikamwambia hatumuuzi na wala hatakuwa na mpango wa kumuuoza binti wetu hivyo nikawataka wenyewe waseme kiasi walicho nacho kilicho wachochoea kutafuta mchumba akasema wana ng’ombe 10 kaka yangu Mambaga Kerigi akaghafirika na kumrushia rungu kwani aliona kiasi kile ni kama dharau.

Mambaga alitaka ng,ombe 15 mzee yule akakubali lakini msimamo wangu ukabakia kuwa uleule atoe ng’ombe 10 zilizochukuliwa tarehe 25 mwezi wa 12 mwaka 91.

Ndoa ikafungwa kigangoni Nyamongo katika parokia ya Nyamwanga wakati huo. Ili kuwapunguzia ukali wa maisha nikamtafutia Paulina kozi ya ualimu ili baadaye aitumie kutafuta ajira mmewe akakubali kwa masharti kwamba asihusike na gharama zozote za kozi hiyo na watoto akaniletea nikae nao nilikubali kwa maana nilijua anaweka vikwazo ili mke wake asisome walikuwa watoto wa miaka 3 na 4.

Binti akasoma na kufaulu wakiwa wanaishi Nyamongo nikawaita waje niwaanzishie miradi iwasaidie wakati wanatafuta kazi.

Wakaja Buhemba mwezi wa 10 mwaka 97. Nikawalipia chumba na kuwanunulia mahitaji mengine. Nikampa Paulina mtaji wa kufuma na kuuza vitambaa; mmewe nikamtafutia ufumdi seremala ajiunge na kujifunza; pale kwa Chomete; ni hapa Buhemba.

Muda kidogo ukapita minong’ono ikazidi; Protas akatawaliwa na wivu usio na msingi. Hakutaka Paulina atoke na ilifikia akawa anapanda juu ya miti kumchunguza wakati anaenda kisimani nadhani wivu huo pia ulidumaza maendeleo yao aliweza hata kumpangia muda wa kutoka na kurudi kila alipokweda mahala.

Aliporudi muda kinyume na matashi ya mmewe akapambana na vipigo; kuna kipindi alimpiga na ubapa wa panga na kumchania nguo zote alizonunua kutokana na mradi akamlaza chini eti amchinje huku akiwa amefunga mlango hadi alipookolewa na marehemu Mwalimu Damian Hezron alipobomoa mlango na kisha Paulina kupata nafasi ya kukimbia na kuna siku alimpiga mateke hadi akaanza kublidi ndipo tukampeleka kituo cha afya cha Muriba baada ya kupata PF. 3.Siku hiyo binti alikimbilia nyumbani akiwa na panga lililotaka kumchija na mavazi nusu na mara nyingi nilikuwa namzuia abaki nyumbani anakataa.

Nikaamua auze nafaka palepale Buhemba lakini bado hiyo haikuwa dawa. Mmewe akawa anamuadhibu eti kwa kuongea na watu pale kwenye biashara. Aliponusurika kuchinjwa kwa mara ya mwisho, Paulina akatoroka kwenda kwa shangazi yake Kahama mwezi mei mwaka 97.

Nikamtuma mdogo wake anaitwa Breini ili amfuate maana huko anaweza kukutana na magonjwa, ajali na hata labda mmewe mwenyewe angeweza kumvizia na kumdhuru.

Wakaja Tarime mwezi wa 6 mwaka 98 nikamuita mmewe niwasuluhishe; akagoma nikawarudisha ustawi wa jamii na kabla ya siku ya kuandikiana kutengana, Protas akamtuma Padri Evarist Shayo amuombe radhi lakini safari hii tulikataa tuliona amejenga mazoea ya kufanya kosa na kisha kuomba radhi makusudi.

25/6/98 kabla haijafika 30/6/98 ili wakapeane maandishi ya kutengana na Paulina akiwa nyumbani kwangu, akaenda soko kuu kununua samaki wabichi na mafuta ili awakaange kwa biashara maana mradi huo ndio sasa ulikuwa nguzo yake ya kulelea watoto.

Wakati anarudi miendo ya saa 8 eneo la uwanja wa shule ya mazoezi Buhemba, ghafla Protas akajitokeza tokea njia nyingine. Kwa mujibu wa Paulina kabla ya kifo chake, mmewe akamuita akitaka wasimame ili waongee vema. Binti akasema,Tuzungumze huku tunatembea samaki wasizidi kuharibika pia niwahi biashara. Nikatangulia bila kujua nia yake. Wakati tunaongea nae, nikasikia kitu kinanichoma katikati ya kiuno na mbavu; nikapata maumivu makali na damu ikawa inatoka sana. Protas akanishika taratibu tena kwa upendo akanilaza chini. Akakimbia huku ninalia nikamuona anaenda bila kunisaidia".

Akalia na kelele zikawaita watu ndipo majirani wengine wakatuletea taarifa ni kama mita 100 hivi toka pale. Mama yake akaangua kilio na tulifika na kumkuta amelala chini hajitambui; kisu cha urefu wa inchi 9 kimepotelea mwilini kwenye mbavu.

Nikatumia uzoefu wangu wa kutatua matatizo kwa msaada wa Rozari. Nikamuomba Bikira Maria anirahisishie masumbuko kwa maombezi. Tukampeleka hospitali ya serikali ya wilaya baada ya kupewa PF3 toka kituo kikuu cha polisi akafanyiwa operesheni kutoa kisu kile kilichokuwa kimeharibu ini.

Hali ilipozidi kuwa mbaya tukampeleka Bugando Mwanza huo ilikuwa mwezi wa 9 mwaka jana huko nako akapewa rufaa kwenda Muhimbili ingawa tulishindwa kumpeleka . kabla ya mauti yake 7/11/97 kutokana na hali mbaya ya kifedha.

Hata hivyo kabla ya kifo chake kila data zote muhimu kwa ajili ya kuendeshea kesi ya mauaji na madai tulikuwa nazo ingawa tulishapata taarifa kuwa amekimbilia Kenya sehemu za Mabera kwa binamu yake alipo hadi sasa.

Hatukutaka kufanya haraka ya kumkamata maana angeweza kukimbia zaidi; tukaona ngoja asahau iwe rahisi kumtia mbaroni.

Kilichonikera mno hadi kifo chake ni ndugu wa Protas kutojihusisha kwa lolote hali wanajua mtoto wao ndiye amemuua mtoto wangu. Tangu hospitalini jeneza na hata sanda tukagharamia wenyewe; wao wakafuata mwili tu, kwenda kuzika huko Nyamongo. Hii ni kutokana na mila. Inaonesha bado kulikuwa na kinyongo.

Wakati tunaendelea kukamilisha mipango ya kumkamata muuaji nchi hapo Kenya jirani na tukisubiri ajisahau, Juni 14, 99 siku ya mwisho ya mahubiri ya hadhara ya kikatoliki yaliyofanyika eneo la parokiani Tarime kwa ajili ya Udekano wa Tarime yakiongozwa na Padre Joseph K. Bill wa mbagala kule Dar. mahubiri yakanigusa.

Padre akazungumzia kusameheana; msamaha unaotufanya tusamehe na kusamehewa na Mungu; akasema, "Usitegemee kusamehewa mbinguni kama umekufa kabla ya kumsamehe aliyekukosea; lazima usamehe kabisa uondoe kinyongo ambacho ni kikwazo kikubwa mbele ya Mungu.

Ni muhimu kusameheana na ndiyo maana ya upendo tuwapende na kuwasamehe maadui zetu ili tupewe baraka za Mungu tusiyemuona za kimwili na kiroho" maneno hayo yakaigusa imani yangu ya kikatoliki nikapanda jukwaani kutoa ushuhuda wangu upendo wa Kristo; Kichwa cha Kanisa ukanijaza ushujaa nikautangazia umati ule kuwa muuaji wa binti wangu nimemsamehe tangu siku hiyo na sina kinyongo nae; wala ndugu zake.

Hata vielelezo vyote vya kuendeshea mashitaka nikavichoma palepale mbele ya umati hata baadhi ya ndugu zake walikuwapo. nilichoma hati zote za mashitaka kuoneesha kuwa moyo wangu umechoma na kufuta kinyongo na kesi hiyo kabisa.

Wapo ndugu waliochukizwa sana na uamuzi wangu. Lakini kwa kuwa ninatimiza mapenzi ya Mungu sina hofu najua ni Mungu huyo atakayenisaidia zaidi na kwamba hata wao ipo siku wataondoa vinyongo juu yangu wanisamehe na kuniombea.

Hata kama vyombo vya dola au jamhuri watataka kumkamata na kumshitaki, heri nami niuawe lakini siwezi kutoa ushahidi wowote maana nilishaahidi kwa Mungu na hivyo siwezi kuvunja ahadi yangu kwa Mungu mimi ni Mkatoliki.

 

Wizi wa watoto kwa njia ya simu washamiri nchini Marekani

lMama mmoja akata simu nyumbani kwake kukwepa bintiye asiibiwe

Na Mwandishi Wetu

KATIKA hali inayodhihirisha kuwa Dunia sasa inaelekea kupasuka kwa vituko; huko Marekani kumeibuka wizi wa aina yake wa karne ambapo watoto wadogo huibiwa kwa njia ya simu na kisha kutoweka kutoka kwa wazazi wao katika mazingira ya kutatanisha sana.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kituo cha kushughulikia watoto waliotoweka na wanaonyongwa kwa kutumiwa kwa shughuli mbalimbali zisizolingana na umri wao NCMEC National Centre for Missing and exploited children, idadi kubwa ya watoto wameripotiwa kuibiwa kwa njia hiyo, majimbo ya Marekani ya Calofornia, Texas, Florida, Wyoming, Utah na Arizona.

Rais wa taasisi hiyo ya NCMEC Bw. Ernie Allen anasema kuwa watoto wanaoibiwa kati ya miaka 8 mpaka 15.

Danniel Montgomery mvulana mwenye umri wa miaka 15 mkazi wa Maple Valley, Washington DC ni mojawapo kati ya watoto ambao mpaka sasa wametoweka baada ya kuibiwa na wahuni kwa njia ya simu.

Montgomery alikuwa na tabia ya kupiga simu kwa watu ambao wazazi wake kamwe hawakuwafaamu.

Mama yake mzazi alipojaribu kumchunguza kuwa ni wapi alikuwa akipiga simu hizo lakini alikataa katakata kumueleza . Nyakati zingine Montgomery akiwa shuleni watu hao walipiga simu nyumbani kwao na wakisikia ni sauti ya mama yake amepokea walikata simu mara moja.

Montgomery aliendelea na tabia ya kuwasiliana na watu hao wasiojulikana mpaka alipokuja kutoweka kabisa kutoka nyumbani kwao mapema mwezi Mei mwaka huu wa 1999.

Baada ya kutoweka kwake rafiki yake waliyekuwa wakisoma naye aitwaye Twain aliwaelezea wazazi wake kuwa yapata siku mbili kabla Montgomery hajatoweka alienda kwenye sanduku lake la posta ambamo alikuta amemtumiwa tiketi ya basi na cheki ya pesa ndipo alipoondoka kwao na kuelekea kusikojulikana .

Siku moja tu baada ya Montgomery kutoweka toka kwao mtu mmoja aliyekuwa akiongea kwa sauti nzito aliwapigia simu wazazi wake . mtu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Dammien Starr aligombana kuwa ni yeye ndiye aliyekuwa amemuiba Montgomery na alikuwa naye nyumbani kwake hata hivyo alikataa kuwaeleza wazazi wa mtoto huyo kuwa walikuwa naye upande gani wa Marekani.

Kitu cha kushangaza ni kuwa watu hao wanaoiba watoto huko Marekani wanaripotiwa kuwa na chama chao na wanafanya mashindano ya kuiba ambapo mhuni anayefanikiwa kuiba idadi kubwa ya watoto ndiye hutanagazwa mshindi kwenye chama chao na kutuzwa zawadi.

"He who dies with the most kids—wins"

"Anayefanikiwa kupata watoto wengi huwa mshindi".

Anasema Ernie Allen rais wa taasisi ya kusidia kupatikana watoto walioibwa.

Baada ya wazazi wa Montgomery kutoa taarifa kwenye taasisi hiyo ya NCMEC hatimaye walipewa taarifa kuwa mtoto wao ameonekana akiwa na mtu mmoja jijini San Fransisco huko California kwenye vilabu vya usiku vya wanaume mashoga na wanawake wasagaji.

Baada ya juma moja mtu aitwaye Damien Starr aliyejigamba kumuiba Montgomery aliwapigia tena wazazi wake simu na kuwataarifu kuwa alikuwa ameelezwa na matoto huyo kuwa yeye hawapendi wazazi wake na angependa kuishi huko Califonia milele.

Lisa Noblle mwanamama wa Kimarekani mkazi wa mji wa St. Mathews, Ky ni mojawapo wa wazazi waliopoteza watoto wao kupitia wizi huu unaoendeshwa kwa njia ya simu.

Binti yake mwenye umri wa miaka 13 aitwaye Tara alianza kupigiana simu za mapenzi na jibaba lenye umri wa miaka zaidi ya 40.

Baada ya mwezi mmoja tu Tara, msichana mdogo mrembo alitoweka nyumbani kwao na hadi leo wazazi wake hawajamuona tena. Kupigiana simu kati ya Tara na jibaba hilo kulimpelekea mama yake kuamua kukata simu nyumbani kwake lakini yote hayo hayakusaidia kitu.

Baada ya wiki mbili Tara aliwaandikia barua wazazi wake kuwa wasijihangaishe kumtafuta yeye yuko mikononi mwa mtu ampendaye.

Wapo pia akina mama wenye umri mkubwa wanaoishi Marekani na kuwaficha majumbani mwao ili wawatumie kwa manufaa ya mapenzi.

Kunako Juni 5 mwaka huu afisa wa polisi aitwaye Pam McGraw alimuokota Montgomery aliyeibiwa na Durncien Starr akiwa ametelekezwa kwenye uwanja wa ndege wa San Fransisco.

Ernie Allen wa taasisi ya NCMEC anasema kuwa mpaka sasa maelfu ya wazazi walioibiwa watoto wao wameripoti kwenye kituo chake na anafanya kazi bega kwa bega na polisi wa Marekani kudhibiti wizi huu wa aina yake wa karne ulioibuka.

Nani aligundua Eropleni?

Watu walipoteza maisha yao katika jaribio la kubuni ndege

NaMwandishi Wetu

LEO usafiri kwa njia ya anga unaunganisha pande mbalimbali za dunia Madege makubwa ya mashirika tofauti huruka kutoka mji mmoja hadi mwingine. Kote duniani na mtu aweza kusafiri kwa muda mfupi tu kutoka Afrika mpaka Ulaya. Je ni nani aliyegundua ndege?

Binadamu alianza kufikiria kuruka angani yapata zaidi ya miaka 200 iliyopita Hili lathibitishwa na simulizi ya kale toka Ugiriki.

Huko Ugiriki inasimuliwa kuwa mtu mmoja mzee aitwaye Daedalus na mwanaye mdogo aitwaye Icarus walifungwa gerezani katika kisiwa cha Crete.

Daedalus alitaka atoroke na mwanaye toka kifungoni lakini asiweze sababu walizungukwa na bahari pande zote.

Ndipo alipofikia uamuzi wa kujitengenezea mabawa yeye na mwanaye Icarus. Waliamua wavae mabawa hayo kisha wajaribu bahati yao kwa kuruka kutoka kisiwa cha Crete mpaka kisiwa cha Sicily kilichoko huko Italia. Katika jaribio hilo mwanaye Daedalus aitwaye Icarus alidondoka baharini na kufa papo hapo. Lakini Daedalus yeye akafanikiwa kutumia mabawa aliyojitengenezea kufika Sicily salama. Hivyo yaaminiwa Daedalus ndiye binadamu wa kwanza kufanya jaribio la kuruka angani ingawa habari zake ziko katika hadithi tu za Wagiriki.

Jaribo la kwanza la kuruka kwa kutumia chombo cha angani lilifanywa kwa kutumia,maputo makubwa (Balloons) katika mwaka wa 1783 mtu mmoja aitwaye Joseph Montgolfier aliona kuwa mifuko ya karatasi iliyoinamishwa juu ya moto iliweza kupeperuka na kuruka juu angani.

Ndipo yeye na ndugu yake anayeitwa Etienne wakaamua kufanya jaribio la kuruka kwa kutumia "Balloon" kubwa ya kufanyia jaribio lao.

lakini kabla hawajatekeleza azma yao wakazi wa jiji la Paris huko Ufaransa walimshawishi mwanasayansi wao aliyeitwa Charles awajengee "Balloon"ambapo alitumia kanuni ile ile ya akina Montgolfier.

Kwa kweli mpaka mwaka huo Wafaransa hawakujua ni kitu gani kilichopelekea"Balloon’za Montgolfier kupaa lakini walihisi zilikuwa na hewa fulani nyepesi ndani yake.

Ndipo mwaka 1766 mwanasayansi mahiri wa kiingereza aitwaye Cavendish akagundua kuwa gesi ya Hydrogen ilikuwa ni nyepesi kuliko hewa.

Hivyo mwanasayansi wa Ufaransa Charles akawaza kuwa lazima itakuwa ni gesi hiyo ya Hydrogen ndiyo Montgolfier alitumia kuwezesha Balloons zake kupaa.

Hivyo ilipofikia Agosti 26 mwaka 1783 wakazi wa jiji la Paris walikusanyika kushuhudia Charles akifanya jaribio la kurusha puto lake kubwa kwa mara ya kwanza.

Jaribio lake lilifanikiwa na puto lake likaruka umbali wa maili zipatazo 15 juu ya uso wa nchi kisha "Ballon" hilo kubwa likatua katika kijiji kimoja huko mashambani. Lilipotua gesi ya Hydrogen iliyokuwemo ndani yake ilikuwa imeungua vya kutosha kiasi cha kutoa harufu mbaya sana . Wanakijiji washamba walibana pua kwa harufu waliyohisi kwa vile hawakujua dude hilo linalotoa harufu ni kitu gani walilishambulia kwa mapanga na marungu na majembe wakaliharibu lote.

Lakini mwaka huo huo wa 1783 Mfalme Louis wa kumi na sita wa Ufaransa akatoa amri jaribio la kwanza lifanyike la kurusha Ballon likiwa na watu ndani yake hivyo akaagiza wafungwa wawili waliokuwa wamehukumiwa kifo watumike katika jaribio hilo lakini ofisa mmoja katika baraza la mawaziri la Mflame Louis alikuwa na wazo tofauti na Mfalme.

Mtu huyo aliyeitwa Pilatre de Rozier alimshauri mfalme Louis kuwa hapakuwa na haja ya kuwapa wafungwa heshima kubwa hiyo ya kushiriki jaribio la kuruka angani hivyo akamuomba Mfalme aidhinishe yeye "De Rozier" pamoja na rafiki yake mwingine wafanye jaribio hilo. Mfalme alikubaliana naye.

Hivyo ilipofika Novemba 21 mwaka 1783 De Rozier na rafiki yake wakitumia "Ballons" iliyojazwa gesi ya Hydrogen walifanya jaribio la kwanza kwa Ballon kurushwa ikiwa na binadamu ndani yake walimudu kusafiri umbali wa maili 5 kisha wakafanikiwa kutua wakiwa salama .Dunia ikaamini upo uwezekano wa binadamu kuruka angani na kutua salama.

Kutoka hapo majaribio mengine lukuki ya kuruka kwa kutumia Ballons yakafanyika mtu mmoja akamudu kuruka kwa Balloon umbali zaidi ya maili 1000 kutoka Ufaransa mpaka Urusi.

Mwaka 1852 jaribio la kwanza la kutumia chombo chenye Injini kuruka angani likafanywa na Henri Giffard wakati huo huo Kaskazini mwa Ujerumani ndugu wawili OttoLilienthal na Gustar Lilienthal wakajitengenezea vifaa vya kufanyia majaribio ya kuruka "Gliders"na wakaviita vifaa vyao hivyo "ndege zisizo na Injini"walijenga kilima kidogo cha mawe karibu na kwao ambapo kila siku majirani walikusanyika kuwatazama wanavyoruka.

Agosti 1896 Otto Lilienthal alipata ajali mbaya alipokuwa akifanya jaribio la kuruka na akafa papo hapo.

Kifo cha Otto kilifungua njia huko Marekani kwa Wavulana wawili waliojulikana kama "Wright Brothers" wao walikuwa wakiishi Calfornia.

Wakitumia kanuni ya Otto Lilienthal walitengeneza ndege ya kwanza ndogo yenye injini Mnamo December 17,1903 mmoja wa wavulana hao aliyekuwa akiitwa Orville Wright alifanya jaribio la kwanza la kuruka na ndege ndogo yenye Injini angani akiwa na kaka yake. Tukio lao lilipelekea mwezi December kuwa muhimu mno katika sayansi ya kuruka angani na mwaka 1908 mmoja wa ndugu hao Wilbur Wright aliruka angani salama na ndege yake akitumia masaa mawili na dakika Ishirini.

Mwaka 1909 tajiri mmoja anayemiliki magazeti huko Uingereza aliyeitwa Northcliffe alitoa paundi 1000 kwa mtu ambaye angelifanikiwa kuvuka mlango wa bahari wa "English Channel"kwa kutumia ndege.

July 25,1909 Mfaransa mmoja aitwaye Louis Bleriot alijaribu bahati Ufaransa kuja Dover Uingereza lakini ndege yake ikafanikiwa kufika salama Uingereza ikiongozwa na meli iitwayo "Escopette"

Wakati Bleriot anafanikisha jaribio hilo ilipata mtu mmoja aitwaye Hurbert Latham alishajaribu kuvuka mlango huo wa bahari kwa kutumia ndege lakini akaishia kutumbukia baharini.

Mtakatifu Polikarpo:Askofu wa Smirna

lAliburutwa chini na gari akaumia vibaya sana

Alishindikana kuuawa na moto; akachomwa upanga kifuani

Na Josephs Sabinus

"Una shida gani bwana? Hakuna shida wala dhambi kumuita Kaisari wangu Mungu.

Je, ni dhambi gani kutoa sadaka kwa miungu ili kujiokoa?"

Alipoona Askofu Polikarpo hajibu neno, Jemedari Herodi akazidi kumchokoza. Hata hivyo ilifikia hatua Polikarpo akamjibu.

"Sikia bwana; hakuna neno liwezalo kunigeuza. Siogopi pingu wala upanga, mkuki, moto, maji wala teso liwalo lolote liwe. Kamwe siwezi kumfukiza ubani binadamu; sembuse shetani." Majibu hayo ya Askofu Plikarpo yakamkasirisha Jemadari; akamsukuma na kumuangusha chini ya gari lake. Askofu yule mzee akamburuta njiani na kuumia vibaya mguuni.

Hatua hii inatokana na maswali aliyoulizwa na Jemadari Herodi aliyekuwa akija kumkamata alipompandisha kwenye gari lake na kuazna kumuuliza kwa upole; akijaribu kuyageuza mawazo ya Polikarpo.

Unajua; wakati ule Smirna alikuwa chini ya Serikali ya Roma na katika zamani hizo, Kaisari Marko Aurelio alitoa amri iliyowakataza Wakristo waliokuwa katika miliki ya Waroma wasifuate dini yao.

Wakristo waliokataa kuabudu sanamu za miungu wa uongo walikamatwa na kuuawa. Polikarpo nae alichongewa ndiyo maana walianza kumtafuta.

Siku moja alikutwa juu ghorofani katika nyumba ya mkulima karibu na Smirna. Polikarpo angeweza kutoroka, kukimbia na hata kutokomea kabisa na wala asikamatwe. Lakini alikataa; akajisemea, Ni amari ya Mungu." Yeye mwenyewe akashuka na kuwafuata: Akawasalimu bila hofu yoyote moyoni mwake.

Nao walishangaa walipomuona ni askofu mzee. Tena mzee mwenye mvi. Yote kwa yote; ni mtu asiye na uoga wala chuki maana yeye aliwatazama kwa wema tu.

Maaskari wale waliyaona hayo; lakini kutokana na amri waliyopewa wangefanya nini? Walimkamata na kumpeleka mahakamani. Polikarpo aliwaomba ruhusa ili apate fursa ya kusali kidogo hali akiwa amemwambia mpishi wake awaandalie watu hao chakula.

Akawaacha wakila. Akajitenga kidogo na kusali kwa muda wa masaa mawili hivi. Matandiko yalipokuwa tayari, akapanda punda na kufuatana na askari wale na ndipo njiani wakakutana na jemadari Herodi na kuanza kumshawishi kwa Upole na hila ili amgeuze.

Msimamo wa Polikarpo ulipozidi kuonekana thabiti, usioteteleka huku akitoa majibu yaliyowaondolea matumaini ya kumgeuza Jemadari Herodi ambaye alikuwa amembeba kwenye gari lake akakasirika sana na hata akamsukuma na kumuangusha chini ya gari hilo. Gari likamburuta Askofu Polikarpo na kumfanya aumie vibaya sana mguuni.

Wakampeleka katika uwanja wa michezo ili kuhojiwa na Liwali. "Ndiwe Polikarpo?" Akamjibu, "Naam". Liwali akamwamuru amwapize Kristo; lakini Polikarpo akasema.

"Sasa ni miaka 36 nikimtumikia Kristo na wala hakunidhuru bali tu; amenijalia mema. Nitawezaje kumwapiza aliyenitendea mema matupu; akanisaidia; akanisimamia na kunitegemeza?"

Liwali nae akachukia na kuzidi kumtishia. "Usipoabudu ninavyokuamuru, utatupwa mbele ya wanyama wakali wakurarue. Polikarpo aliyefundishwa dini na mitume katika ujana wake na kubatizwa akasema.

"Walete hao wanyama wakali. najua siwezi kijigeuza niwe mbaya zaidi. Lakini bora niteswe ili mateso yangu yanitakase na kunifikisha uwinguni."

Kwa ghadhabu, Liwali akaendelea, "Huogopi wanyama? Basi kama hugeuki, sasa hivi utaokwa. Tofauti na wengi wetu ambao vitisho vidogo vinatubadili imani, Mtakatifu Polikarpo yeye hakujali vitisho ili aisaliti imani yake kwa Kristo; akasema.

"Unanitishia moto? Ndio utakaozimika mwishoni. Kwani haujui kuwa moto ule uwakao milele ndio utawaunguza wapagani; nitese upendavyo."

Liwali akaagiza kuni zikusanywe na zilipokuwa tayari kutiwa moto, Polikarpo mwenyewe alivua kanzu lake; akakataa kufungwa mikono kwenye nguzo akisema, "Niache hivi hivi; mwenye kunipa moyo wa kuvumilia moto, atanijalia nisimame thabiti bila kukazwa na vifungo vyenu.

Alifungwa mikono kwa nyuma pasipo kufungwa kwenye nguzo iliyosimikwa kati ya lundo la kuni. Akapanda juu ya lundo hilo; akainua macho juu na kunena, "Mungu Mwenyezi; nashukuru kwani umenijalia siku na saa hii; niwe katika hesabu ya mashahidi wako; nami nionje bilauri ya Kristo nipate kuufikia uzima wa milele.

Naomba nipokewe leo kati yao mbele yako kama sadaka ya harufu nzuri. Ndivyo ulivyotaka, ulivyoamua na ndivyo ulivyotimiza. Ninashukuru , kukutukuza kwa ulimi wa kuhani wa milele aliyekaa nawe mbinguni. Ndiye mwenye kustahili sifa zote pamoja na Roho Mtakatifu; sasa na milele; Amina."

Alipokwisha tamka AMINA; moto uliwashwa lakini palitokea muujiza mkuu kwani ndimi za moto hazikumteketeza badala yake zilimuambaa na kumzunguka mithili ya taa.

Wapagani waliokuja kumuangalia walipoona hawakufaulu kumuangamiza, wakajawa na ghadhabu, wakamchoma kwa upanga kifuani na kumfanya avuje damu kwa wingi na hata kumwagika katika ndimi za moto ule mkali na kuuzima.

Hata hivyo, nae hakuendelea kuishi, akafariki akiwa shahidi namna hii Februari 23, 155 saa nane.

Mtakatifu Polikarpo aliyekuwa rafiki wa Mt. Inyasi wa Intiokia wote wakiwa wafuasi wa Mtume Yohani aliyemfanya Polikarpo kuwa askofu wa Smirna (Uturuki) alipokuwa mzee alisafiri kwenda Roma Italia kuzugumza zaidi na Papa juu ya maisha yake.

Wakristo wa Smirna waliandika barua juu ya kifo chake kwa Wakristo wa Kanisa la Filomelium (Uturuki). Barua hiyo imetunzwa hadi leo. Kwa njia hiyo, tulipata habari kamili za matukio yake.

Mtakatifu Polikarpo askofu na mfiadini anakumbukwa na baadhi ya Watakatifu wengine kila mwaka ifikapo Februari 24.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

OMIER: Nyoka aliyeabudiwa na Wajaluo kandoni mwa ziwa Victoria

lAlizusha kasheshe kwenye makazi ya watu akimsaka mke wake

Na Ignatio Obuombe, JR.

KANUNI ya demokrasia kuhusu mtu kuamini na kuabudu imani yoyote anayotaka ili mradi tu asivunje sheria imewapelekea wanadamu kuabudu hata vitu visivyostahili kuabudiwa hebu soma mkasa huu

Nchi ya Kenya ni mojawapo kati ya mataifa barani Afrika ambako watu wamechanganywa na imani tofauti za kidini zinazozuka kila kukicha.

Katika Mkoa wa South Nyanza"eneo la Karachunyo penye ufukwe wa ziwa Victoria Wajaluo wanaoishi katika eneo hilo wamekuwa na jadi ya kuwaabudu nyoka wawili Bibi na Bwana waliokuwa na makazi yao penye ufukwe wa ziwa hilo.

Kwa mujibu wa profesa Onyango Aluoch wa Kitivo cha Elimu ya udaktari katika chuo Kikuu cha Nairobi ambaye amepata kumfanyia nyoka huyo matibabu ikani hii ya kumuabudu nyoka huyo mkubwa sana Omier wakazi wa Karachuonyo wamekuwa nayo tokea zama za mababu. Omier nyoka jike ambaye amekuwa akiishi na mwenzake dume anayeaminiwa kuwa ni mumewe anaheshimika sana miongoni mwa wakazi wa Karachunyo kiasi kwamba penye vichaka vya ufukwe wa ziwa alikofanyia maskani yake hakuna anayeruhusiwa kufyeka.

Mkazi yeyote wa maeneo hayo anapotokea kukumbana na Omier njiani inambidi asiondoke pahala hapo. Bali anatuma watu wawaite wazee wa kitongoji wanaojulikana kama "Jodong Gweng" wakishakuja kinachofuata hapo ni kafara kutolewa ambapo mbuzi, kondoo au ng’ombe huchinjwa ndipo "Omier"huwa huru kumruhusu mtu huyo aende baada ya kafara.

"Wazee hao waitwao "Todong gweng"pia huhakilisha kuwa msimu wa kutayarisha mashamba kwa ajili ya kilimo unapofika; watu wanachoma vichaka na magugu hawawashi moto penye eneo ambako Omier anapendelea kuvinjari.

Hata hivyo kunako mwaka 1987 baadhi ya wavuvi wakorofi huko "Karachuonyo’walifanya jaribio la kuchoma moto vichaka vilivyoko kwenye ufukwe ambao ilikuwa ikiaminiwa kuwa ‘Omier na mwandani wake walikuwa wakiishi; kwa bahati mbaya moto huo uliwaka kiasi cha kuyafikia makazi ya Omier na ukamjeruhi kiasi majeraha aliyoyapata Omier yaliwapelekea wazee wale waitwao "Jodong Gweng" kuja juu ambapo walifanya kafara na kuwaombea dua mbaya wale wote walioshiriki kuwasha kwa makusudi moto uliomchoma Omier. Mei 1987 Omier (nyoka)alichukuliwa na kupelekwa Nairobi kwa ajili ya matibabu chini ya usimamizi wa Profesa Onyango Aluoch ambaye naye pia ni mzaliwa wa huko Karachuono.

Matibabu ya Omier yalishindikana Nairobi na akasafirishwa mpaka London Uingereza akafanyiwe uchunguzi na wataalamu wa nyoka.

Huku nyuma Karachunyo Omier akiwa Ulaya kasheshe ya aina yake ilizuka wakati joka moja kubwa dume lililoaminiwa kuwa mumewe lilivamia nyumba za watu wa Karachuonyo huku ikitishia usalama wa watu.

"Jodong Gweng"walidai kuwa alifanya hivyo kwa sababu alikuwa akimhitaji mkewe (Omier) Penye nyumba alizovamia watu walikimbia mji na kumuachia ama walimtupia kuku kisha akimmeza alitambaa na kuondoka kwa amani pasipo kumdhuru mtu.

Wazee wa Karachuonyo walifunga safari mpaka Nairobi na kumwambia Profesa Aluoch awarejeshee nyoka wao wa vile wazee walikuja juu "Omier"ilibidi akatishe matibabu Ulaya hata hivyo aliporejeshwa alichukua siku tano tu na akafariki Juni 15,1987.