Make your own free website on Tripod.com

WAKATI TANZANIA INAKIMBIA IBADA ZA SHETANI.....

Nchini Kenya ibada za mashetani zashamiri mashuleni

lwanafunzi toka familia tajiri huwahonga maskini wajiunge na dini hiyo

lLoleza Sekondari wamecharaza shetani viboko

lMwanafunzi mmoja aandikiwa barua kumtaka amtoe kaka na dada yake kafara

Na mwandishi wetu

WAKATI wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Loleza iliyoko mkoani Mbeya hivi majuzi waliamua kumtimua shetani shuleni kwao kwa kumcharaza viboko nchi ya jirani ya Kenya mambo ni tofauti ambapo shetani amefanikiwa kuwaingia wanafunzi mioyoni na kuishi ndani yao.

kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Raisi Daniel Arap Moi Toroitich iliyo kuwa ikizunguka mikoa yote ya Kenya kuchunguza ibada za shetani, kama ufa hautazibwa sasa kudhibiti kasi ya wanafunzi wa Kenya kujihusisha na shughuli za Kishetani basi ukuta utajengwa.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa wakala kadhaa wa shetani hivi sasa wanazunguka katika mashule na vyuo vya elimu ya juu nchini Kenya wakidai kuwa wao ni maafisa wa Jumuiya ya Kikristo ya Wanafunzi "Kenya Students Christian Fellowship" lakini kinyume na hayo wakiwasajili wanafunzi kuwa watenda kazi wa shetani.

Ripoti hiyo imewashutumu walimu wa Kenya kwa kutokuwa waangalifu kiasi cha kuruhusu wageni kuingia hovyo kwenye mipaka ya shule ambapo imebainika kuwa baadhi ya wageni hao huwaletea wanafunzi madawa ya kulevya na zawadi ghali za kuwashauri wajiunge na ibada na kazi za shetani.

Ripoti ya Tume ya Rais Moi imetoa wito na tahadhari ikijulikana wazi kuwa vijana ndio tegemeo la Taifa kwa kusukuma gurudumu la maendeleo na kwamba upo umuhimu wa serikali kuchukua tahadhari kupambana na shetani kabla hajaipokonya vijana wake wanaopotoka kwa kasi.

Akielezea jinsi alivyoponea chupuchupu kuopolewa na shetani mwanafunzi mmoja wa kidato cha pili nchini Kenya ambaye sasa ameacha shule ameeleza kuwa aliingizwa kwenye ibada za shetani kwa mara ya kwanza katika maisha yake baada ya mama wa kambo, kumpa fedha nyingi sana kiasi cha kumpelekea ajihoji ni nini maana yake.

Mwanafunzi huyo ameieleza Tume ya Rais Moi ya kuchunguza ibada za shetani kuwa mama yake huyo pia alimpa saa ya mkononi ya thamani ambayo kila alipokuwa akiivaa ilikuwa ikimnyonya sana damu yake.

Katika tukio la kushangaza mwanafunzi huyo ameeleza kuwa siku moja akitoka shuleni alikutana na mwanamke mmoja mrembo sana akiwa na mwanaume ndani ya gari jeusi aina ya "mercedes Benz." Walipomkaribia walifunga breki na kumuita, watu hao wawili mwanamke na mwanaume walijitambulisha kwake ndipo walipomwomba aongozane nao mpaka kwenya hoteli moja ya kifahari ya jijini Nairobi.

Walipofika hotelini kwa mujibu wa ripoti ya tume hiyo watu hao waliagiza vyakula na vinywaji kisha wote watatu wakuendelea kisha wakamshawishi kwa lugha laini wakimbembeleza ajiunge na ibada za shetani.

Watu hao hawakuishia hapo tu bali walimwambia mwanafunzi huyo baba yake mzazi aliyefariki kwenye ajali ya gari mnamo mwaka 1992 alitolewa kafara kwa shetani na mamaye wa kambo yule aliyemuingiza kwenye ibada za shetani.

Baada ya watu wale kumshawishi kwa bidii alikubali kujiunga nao ambapo ana elezea kuwa wakimpa nguvu za kishetani za kuweza kubadili umbo lake la kibinadamu kuwa nyoka aina ya Cobra ,

Pia kwa nguvu za roho chafu za shetani aliweza kusafiri kimiujiza mpaka nchi mbalimbali duniani ikiwemo Marekani na Ulaya pia walimpa nguvu za kuweza kupelekea ajali barabarani.

Mwanafunzi huyo anaelezea kuwa aliamua kubwaga manyanga na kuacha dini ya shetani siku alipopokea barua iliyoandikwa kwa kutumia damu tupu ikimtaka awatoe kafara kaka yake na dada yake ambao ni mapacha .

Anasema haikuwa lelemama kuhama kutoka kwa shetani kurejea maisha ya kawaida. Ilibidi Chama cha Wanafunzi Wakristo shuleni kwake wamfanyie maombi ya pekee ambapo baadaye walimu "alikata shauri kumuachisha masomo akapumzike nyumbani mpaka atakapoachana na shetani kabisa.

Naye mwanafunzi mmoja wa kike toka kidato cha kwanza katika shule moja ya sekondari mkoani Rift Valley huko Kenya ameelezea kuwa yeye aliingizwa kwenye ibada za shetani kwa kupewa zawadi kidogo kidogo na wasichana wenzake wa kidato cha nne waliokuwa ni wakala awa shetani shuleni hapo.

Amesema kuwa vitu alivyokuwa akipewa na wasichana hao ni pamoja na juisi za matunda na vinywaji vinginevyo, mkate, nyanya za kupona vyakula vingine vilivyosindikwa Wasichana hao pia kila mara walikuwa na mazoea ya kumpa fedha za matumizi kiasi cha shilingi 5000/- za Kenya

Lakini msichana huyo alishikwa na butwaa siku wasichana hao walipomfuata na kumtaka ajiunge na dhehebu lao la shetani kama hatua ya kulipia vitu ambavyo wamekuwa wakimpatia lijaribu kila awezavyo kuwaeleza kuwa kanisa lake linapinga ibada za shetani, hivyo alikuwa tayari kuwalipa zawadi zao lakini asijiunge nao.

Wasichana wale walikataa kata kata kurejeshewa zawadi zao. Ndipo msichana yule anaelezea kuwa kimiujiza alikuta tayari yeye ni mmoja wa waabudu shetani wazuri.

Toka Tume ya Rais Moi ilipotoa ripoti yake baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kwamba yale yaliyosimuliwa na viongozi wa tume hiyo siyo ya kweli.

Akithibithisha kiasi gani mambo hayo yana ukweli Mwenyekiti wa tume hiyo Rev, Bernard Muindi aliiambia gazeti la "Daily Nation kuwa

"people questining the report on devil worship have no basisi to do so , the report is reality , we have live evidence in our report, such as in "shimo la Tewa and Maragua,where we witnessed young men strip naked before getting down to worship" yaani Mombasa.

"Watu wanahoji kuhusu ukweli wa ripoti ya tume ya kuchunguza ibada za shetani, wanapaswa kuacha kufanya hivyo. Ripoti hii ni kweli na mengine hatujaelezwa bali tumeshuhudia kwa macho yetu huko "Shimo la Tewa Mombasa na Margua vijana wakijipanga kwenye mstari wakiwa uchi kama walivyozaliwa na kumuabudu shetani". Akielezea kuhusu matukio hayo Rev Muindi amesema kuwa huko Maragua walimbamba mwanafunzi mmoja mnamo majira ya saa 9 mchana akiabudu uchi wakati ambapo katika shule ya sekondari ya shimo la Tewa huko Mombasa walishuhudiwa na wanafunzi wakiwachinja kuku na kunywa damu zao.

Naye kiongozi wa chama cha kisiasa cha NDP Bw Raila Odinga ameitaka serikali ya Kenya kutopuuza taarifa za ripoti ya Tume ya Rais Moi sababu watakaoathirika na ibada za kishetani ni wananchi.

Mwenyeketi wa Baraza la Maimamu wa Kiislamu nchini Kenya Bw Juma Ngao amesema kuwa serikali ya nchi hiyo ni lazima ihakikishe inafanyia kazi, maoni yote yaliyotolewa na wananchi kwenye ripoti hiyo.

Naye kiongozi mmoja wa kanisa la Wasabato nchini Kenya Bw. Alex Ayub amesema kwa muda mrefu waabudu shetani wamekuwa wakiiba vitu kanisani mwao na kuvitumia kutengenezea alama zao.

Alama hizo za waabudu shetani zimetajwa kuwa ni pamoja na misalaba yenye nyoka , nyota yenye pembe saluti yeye pembe na namba 666

Maajenti (mawakala) wa shetani waliotajwa kuwa wamekuwa wakishawishi wanafunzi kujiunga na madhehebu ya shetani ni pamoja na wanafunzi wanaosoma vidato vya juu kuanzia kidato cha tatu mpaka cha nne hasa wanafunzi toka familia zenye uwezo mkubwa kifedha.

Wengine ni wasichana warembo sana vijana wa kiume wenye sura za kuvutia wafanyakazi wa "Matatu"hususani toka Nairobi ambao hutumia pesa na muziki uliofunguliwa kwa sauti kuvutia wanafunzi.

Matajiri kadhaa wanaoabudu shetani wamekuwa wakigawa zawadi kwa wanafunzi wanao kubali kujiunga na ibada zao na wengine ni wahubiri wa kujitegemea wanaoendesha mikutano ya Injili iliyojaa miujiza

 

Baada ya pesa kukosa thamani...

Msanii atumia noti kutengeneza ndege za kuchezea watoto

lAonyesha sanaa zake hadharani kwenye kipindi cha Televisheni

lBenki Kuu yamuonya vikali

Na Mwandishi Wetu

PESA hukosa thamani lakini heshima yake hulindwa na kubakia palepale. Pesa zinapokosa thamani kiasi cha noti kutumika kuchambia chooni na kutengeneza ndege za kuchezea watoto basi hapo tena ni makubwa.

Watu wote walioketi karibu na televisheni zao jijini Brasilia mji mkuu wa Brazil hawakuamini macho yao kuona msanii aliyebobea kwa kuonesha michezo ya watoto akitumia noti za pesa ya nchi yao "Cruzeiro"kutengeneza ndege za kuchezea watoto kisha kuzionesha kwenye kipindi cha televisheni ya taifa .

Tukio hilo la aina yake siyo kuwa liliwaacha hoi wananchi wa Brazil peke yao, bali hata Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo alichukuwa hatua za kuwasiliana na msanii huyo kwa njia ya simu papo hapo.

Silvio Santos ni msanii anayeheshimika sana nchini Brazil na aliyejizolea sifa kemkem, amelitangaza jina la Brazil hata nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Kwa mantiki hiyo, hakuna aliyetarajia kuwa Santos angelifedhehesha nchi yake kiasi hicho. Kwa kuheshimu mchango wa Santos katika sanaa nchini humo, Gavana wa fedha alimwambia aache mara moja utovu wake wa nidhamu vinginevyo wangelimchukulia hatua kali mara moja.

Lakini Mac. Margolis mwandishi anayeandikia jarida mashuhuri Brazil la "Veja Journal", anasema kuwa ‘watu hawa wanamuonea Santos tu’

Mwandishi huyo anasema kuwa uchunguzi alioufanya kwenye mitaa mbalimbali ya Brasilia hususan maeneo ya madogo, wananchi walijawa na ghadhabu kufuatia kushuka sana kwa thamani ya pesa yao na sasa hawaithamini tena pesa hiyo inayoitwa "Cruseiro"

alishuhudia walevi kwenye vilabu vya usiku vichochoroni wakitumia pesa hiyo kwa kuchambia chooni; akina mama wanaouza bidhaa walitumia noti hizo kuwafungia wateja wao bidhaa walizonunua na hata watu wengine wakizitumia kufuta vumbi kwenye madirisha ya nyumba zao na mbaya zaidi ni wauzaji wa madawa ya kulevya aina ya "Cocaine" ambao wanatumia pesa hiyo ya Brazil kufunga madawa hayo ya kulevya.

Je, ni kwa nini "Cruzeiro" idharaulike kiasi hicho? Wachunguzi wa mambo kwa karibu huko Brazil wanasema thamani ya pesa ya nchi hiyo imeshuka kiasi kwamba ilifika wakati mmoja ambapo pesa ya Brazil ingeliweza kushindanishwa thamani yake na pesa ya Jamuhuri ya Kidemorasia ya Congo Kinshasa na pesa ya Bosnia peke yake. kiwango cha kushuka kwa pesa ya Congo Kinshasa inajulikana kwani katika nchi hiyo baada ya kifo cha Hayati Joseph Mobutu Seseseko Kuku wa Zabanga wakazi wa kijiji anachotokea cha Gbadolite wamekataa kutumia pesa mpya ya serikali ya sasa badala yake wanatumia ile ile ya wakati wa Mobutu.

Kwenye mtaa mmoja wa mji mkuu wa Brazil wa Brasilia, mwanamke muuzaji wa bidhaa ametandaza makaratasi lukuki na sarafu zisizo idadi hakika huwezi kutofautisha ipi ni pesa na ipi ni bidhaa.

Kwani noti za "Cruzeiro"zimelaliana kiasi cha kuwekwa katika mafungu mafungu mithili ya nyanya.

Nako vichochoroni unakopita penye mitaa ya miji mikubwa ya Brazil kama Rio-de-janeiro na Salam siyo jambo la ajabu kwa wakazi wa huko kukutana na noti za "Cruzeiro"zilizotupwa mithili ya takataka.

Bei za bidhaa ikiwemo vyakula hupanda maradufu karibia kila mwezi nchini humo. Wapo wafanyabiashara ambao sasa wameacha kutumia "Cruzeiro"na badala yake wanatumia Dola za Kimarekani na Paundi ya Uingereza peke yake.

Mtu anayeenda kununua shati moja dukani huko Brasilia, hana budi kubeba kikapu kizima cha noti.

Ni katika hali hiyo ndiyo msanii Silvio Santos; liwalo na liwe akaamua kuithibitishia serikali yake kuwa ni kwa kiasi gani pesa yao ni feki.

Naye akaona yafaa kutengeneza ndege za watoto tu.

 

Wakati kipigo cha rungu kilipokuwa badala ya ganzi

lKabla wagonjwa waligongwa kwa nguvu kichwani ili wazirai kabla ya kufanyiwa operesheni

NaMwandishi Wetu

HAPO zamani kabla dawa ya kutuliza maumivu wakati wa kumfanyia mgonjwa upasuaji haijavumbuliwa wagonjwa walihisi maumivu makali kwani walifanyiwa huduma hiyo pasipo kuchomwa dawa yoyote; wakilia na kupiga mayowe yaliyojaza chumba kizima cha upasuaji michirizi ya damu iliwarukia madaktari waliotoa huduma hiyo na hata kusambaa chumbani kutokana na kujirusha rusha kwa mgonjwa.

Kulingana na kitabu cha historia kiitwacho "Who did it first" kilichoandikwa na Prof. G. C. Thornley mwenye shahada ya juu ya Phd. katika historia vijana wenye nguvu walihitimiza juu ya meza anapofanyiwa upasuaji.

Cha kushangaza na kuogofya zaidi ni kuwa wagonjwa walioneshwa kuwa waoga na wasumbufu waligongwa na kitu sehemu maalum kichwani ili wazirai halafu daktari akawafanyia upasuaji kwa haraka kabla hawajazinduka pindi walipozinduka kabla ya operesheni haijaisha walijikuta wako kwenye maumivu makali kiasi cha kuwapelekea kulaani ni kwa nini walizaliwa duniani wawe hai kuhisi maumivu hayo.

Profesa Thornley anasema kuwa watu wa kwanza kugundua dawa ya kutuliza maumivu wakati wa upasuaji walikuwa ni Wachina .

Dawa hizi za kienyeji zilizodhaifu na zisingeliweza kumtulizia mgonjwa maumivu inavyotakiwa pia zilikuwa na madhara yake kwani kama ulitumia nyingi kwa makusudi ili mgonjwa asiumie, zilimzidi nguvu na kumuua pia kama ulituma kidogo hazikufaa kitu na mgonjwa alihisi maumvu maradufu.

Baada ya mwaka 1970 Joseph Priestley, kwa mara ya kwanza alivumbua gesi iliyofikiriwa ingelifaa kutumiwa kwa kazi hii. Gesi hiyo ndiyo ile ambayo leo yaitwa "Laughing gas" kwa zaidi ya miaka 30 toka Priestley aivumbue hakuna mtu aliyeitilia maanani.

Lakini mwaka 1800, Sir. Humphry Davy aliweza kuthibitisha faida zake hata akaipa jina ambalo imedumu kuitwa hivyo hata leo "Nitrous Oxide" Sir. Humpherey alipendekeza kuwa gesi hiyo ingefaa kutuliza maumivu wakati wa upasuaji lakini miaka ikazidi kuyoyoma huku kukiwa hakuna daktari aliyechukua hatua za kuitumia kwenye upasuaji.

Lakini kunako mwaka 1824, Daktari mmoja aitwaye Hichman alisoma kwa makini vitabu vya Sir. Humphery ndipo akaamua kuijaribisha gesi hii kwa mbwa na wanyama wengineo.

Akaibuka na matokeo mazuri sana lakini Hichman akafa angali kijana katika umri wa miaka 29 tu.

Baada ya hapo gesi hii iliyojulikana kama "Laughing gas" au "Gesi ya vicheko" ilianza kutumiwa kwenye kumbi za dansi huko Marekani; waliipuliza wakati wa kucheza muziki, ikawalewesha na kuwapelekea kucheka hovyo na kufurahi sana.

Lakini mtu mmoja aitwaye Horace Wells alienda katika ukumbi mmoja wapo wa dansi akawachunguza vijana wale kwa makini na kugundua kuwa walipokuwa wakicheka walikuwa pia hawahisi maumivu hata wakijigonga kwenye vitu.

Horace Wells aliamua kuifanyia gesi hiyo majaribio mwilini mwake. Yeye mwenyewe alijipulizia gesi hiyo ikamlewesha kisha akamwambia rafiki yake amng’oe jino lake moja na huyo rafikie akafanikiwa kumfanyia Horace huduma hiyo pasipo kuhisi maumivu yoyote.

Horace Wells alianza kujivunia ugunduzi wake kote katika Marekani lakini alisahau kitu kimoja kuwa hakuwa na hakika ni kipimo kiasi gani kilihitajika cha gesi ili mtu asisikie maumivu anapong’olewa jino.

Alienda katika shule moja na kauwafanyia wanafunzi majaribio ya kuwang’oa meno kwa kutumia gesi hiyo lakini kila mwanafunzi aliyemfanyia jaribio hilo alilalamika kuwa anahisi maumivu makali .

Well aliamua kurudia jaribio lake kwa mwanafunzi mmoja akidhani kuwa safari ya kwanza labda aliwapa dozi ndogo ya gesi.

Lakini safari hii alijisahau akampulizia gesi kupita kiasi mwanafunzi huyo akafa palepale wakati akimfanyia majaribio.

Tukio hilo lilimchanganya akili Bw. Horace Well aliyependa kusifiwa.

Hivyo Well akapagawa na akachukua hatua ya kujiua mwenyewe kufuatia jaribio lake kushindwa.

Baada ya kifo cha Well daktari mmoja bingwa wa majaribio ya kisayansi aliyeitwa J.Y. Simpson aliona upo umuhimu wa kuiendeleza dawa ya gesi, iliyowashinda wataalam wengi kukamilisha na ni yeye ndiye aliyekuja kufanikiwa kutengeneza dawa ya kwanza ya kupunguza maumivu wakati wa upasuaji.

Simposon alizaliwa katika familia ya wazazi maskini sana lakini mama yake mzazi alitaka kuona mwanaye anakuwa na maisha mazuri siku za usoni.

Walimpeleka katika Chuo Kikuu cha Edinbugh ambako aliweza kusomea shahada zote za juu kabla ya kuamua kujitosa kwenye fani ya Udaktari.

Wakati huo daktari mmoja aitwaye Robert Liston alifanikiwa kumfanyia mgonjwa operesheni ya kukata mguu jijini London kwa kutumia dawa yake iitwayo "Either" Dk Liston alitumia dakika 26 kumkata kabisa mgonjwa huyo mguu naye hakuhisi maumivu hata kidogo.

Simpson alisikia habari za operesheni hiyo hivyo akafunga safari kutoka Edinburgh mpaka London kwenda kuchukua "Either’ aje aifanyie majaribio yeye mwenyewe alifanikiwa kuipata na akarejea nayo jijini Edinburgh ambako yeye na marafiki zake wawili; Duncan na Keih walitumia kwa kuifanyia majaribio gesi hiyo.

Mwanzoni Simpson alitaka kuutumia mwili wake yeye mwenyewe kujaribu gesi hiyo lakini, rafiki zake wakamshauri aijaribishie kwa wanyama kwanza. Hivyo alimjaribishia mbwa naye akazidiwa na kufa.

Baada ya kuifanyia utafiti kwa karibu mwaka mzima Simposon na marafiki zake wawili walijaribisha dawa ya Simposon aliyoiita "Chloroform"na ikamlewesha Simpson mwenyewe kiasi kwamba akajikuta amedondoka uvunguni mwa meza.

Halafu Simposon akarudiwa na fahamu akamuona mwenzake Dk. Duncan akiwa uvunguni mwa kiti akiwa hoi amepoteza fahamu na kuacha mdomo wazi baada ya kuzidiwa na "Chloroform".

Dk. Keith naye pia alikuwa akijikokota baada ya kurudiwa na fahamu.

Hapo ndipo Simpson akajikuta amegundua dawa ya kutuliza maumivu wakati wa upasuaji dawa hii ya "Chloroform"aliyoigundua Simpson ndiyo inayomudu kutumika mahospitalini wakati wa upasuaji hata leo. Haikuwa lelemama hivyo kufikia uvumbuzi huo.

 

Margarita; Mtakatifu mwenye kipaji maalum katika sala

lAliishi kwa shida toka kwa mama yake wa kambo

lKabla hawajaoana kimanda wake aliuawa porini

Na Josephs Sabinus

Mbwa wake akamuongoza akilia hadi ilipokuwa maiti

MBWA huyo alirudi nyumbani peke yake akilia kilio cha kusikitisha kilicho watia majonzi watu waliomuona na kuwafanya wamhurumie. Alikuwa akilia, anaondoka na kisha anamrudia tena Margarita.

Margarita akahisi jambo baya kumtokea yeye au mume wake ambaye tangu alivyoondoka nyumbani kwenda kuwinda na mbwa huyo zimepita siku mbili nzima hajarudi toka huko porini na badala yake anarudi mbwa huyo peke yake akilia kwa hali ya kuhuzunisha namna ile. Akahisi damu kumchemka na mwili kumsisimka kwa hofu akapiga moyo konde na kumfuata mbwa yule aliyekuwa akilia na kumuongoza kwa staili ya kukimbia mbele na kisha kurudi kumfuata huku wakiendelea na safari yao ya kwenda msituni.

Walipofika huko msituni kando ya mti ule mkubwa, Margarita aliyezaliwa Liviano karibu na Kartona nchini Italia mwaka 1249 akiwa mtoto wa mkulima maskini akauona mwili wa mume wake. Mtakatifu Margarita aliuona ukiwa na majeraha mengi yaliyoonyesha kuwa kijana huyo wa familia tajiri na nadhifu aliyempenda Margarita na hata kumchukua nyumbani kwake na kuishi naye kwa muda wa miaka tisa sasa kama mke na mume ingawa haijulikani kama walipanga kuoana. Aliuawa kikatili na maadui.

Labda uzuri wa mwili wake Margarita ndio uliomponza na kumfanya mama yake mzazi kufariki na kumacha akiwa na umri wa miaka saba tu; hali iliyomfanya baba yake amuoe mwanamke mwingine aliyeonekana kumchukia sana Margarita na ndiyo sababu iliyomfanya Margarita atoroke na kuondoka kisirisiri toka nyumbani kwa baba yake kwenda kuishi katika maisha ya kujitegemea mwenyewe akiwa na miaka 18 tu; ndipo akakutana na kijana huyo waliyependana.

Katika kuishi kwao Margarita aliishi maisha ya raha, starehe na hata kupenda anasa sana akawa anajipamba sana. Mungu akawaogezea furaha yao kwa kuwapa mtoto mmoja hadi siku hiyo ambayo maisha hayo yalimponyoka na hata kutoweka kabisa ni siku hiyo ambayo kadri ya mapokeo mumewe aliondoka kwenda kuwinda msituni na mbwa wake.

Siku mbili baadaye; baada ya kwenda kuwinda msituni na Margarita kuongozwa na mbwa, Margarita aliukuta.

Unatoa harufu na kuugeuza mawindo yao; wadudu hao walikuwa wameutoboa toboa na kujazana kwenye majeraha na sehemu mbalimbali

Margarita ambaye hukumbukwa pamoja na watakatifu wengine wa Afrika kama Abilus, Viktorinus, Eusirus, Paulus, Donatus na Fortunatus kila ifikapo February 22 alishituka sana moyo wake ghafla ukajawa na sononeko alianza kufikiria hali yake itakuaje iwapo atakufa katika dhambi zake,kabla ya kutubu .

Akazidi kusikitika sana na kisha akakimbia hadi nyumbani kwa baba yake ili kuomba radhi akakata nywele zake na kujifunga kamba shingoni mithili ya mtu aliyestahili kunyongwa.

Margarita aliyefariki dunia Februari 22, 1297 na Papa kumuandikia katika kitabu cha orodha ya watakatifu mwaka 1728 akawaonyesha wakristo wote kwamba anastahili kunyongwa na kwamba anajutia dhambi na mwenendo wake wa uasherati.

Ndivyo alivyojawa na vita vya rohoni mwake kwa kuvishinda vishawishi vya shetani aliyemsumbua mno ili amrudishe katika maisha yake ya awali kwa kufunga na kusali sana, Mungu akampa neema zake mwaka 1276 akakubaliwa kupewa vazi la Ndugu wa toba wa Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Fransico pamoja na mtoto wake Mtakatifu Margarita akahamia katika nyumba ya utawani huko Kortaona ambako alianza kuwasaidia akina mama wajawazito na kisha kuazisha hospitali. Hata hivyo mara nyingi Mtakatifu huyu alikwenda kukaa katika upweke wa sasa kwa muda fulani.

Mwisho mnamo mwaka 1288 alihamia kabisa katika nyumba ya upweke mlimani mwaka kumi ya mwisho ya maisha yake aliishi pale kama mtawa akawa MTAKATIFU MWENYE KIPAJI MAALUM KATIKA SALA

 

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

WICCA: Dhehebu la wapagani wanaodai wamezaliwa upya

Mwanzilishi wake ni Mmarekani aitwaye Terry aliyeasi toka Kanisa la Wanazarini

Na Ignatio Obuombe, JR.

MJI wa Jonesboro upo katika jimbo la Arkansas huko Marekani. Hapo ndipo yalipo makao makuu ya dhehebu jipya lililoanzishwa la Wicca.Dhehebu hili la kipagani limeanzishwa na Mmarekani aitwaye Terry mwenye umri wa miaka 38 akiwa ni mkazi aliyezaliwa na kukulia katika mji huo wa Jonesboro.

Imani ya kipagani ya "Wicca" inaaimini juu ya mambo ya asili ikiwa ni pamoja na uganga wa jadi, uchawi, ramli na nguvu za kimizimu zenye kutenda miujiza.

Hata hivyo jambo la kushangaza ni kuwa "Wicca"ambao pia hujiita "Born Again Pagans" yaani "wapagani waliozaliwa mara ya pili"wanadai kuwa wao ni Wakristo sawa na wengine isipokuwa wanaamini tu juu ya vitu vya asili.

Terry mwenyewe kabla ya kuasi mwaka 1993 na kuanzisha dhehebu hili la kipagani alikuwa ni muumini hodari wa dhehebu la kikristo linalojulikana kama "Nazarene Church"

Terry anadai kuwa aliamua kuachana na dhehebu la "Nazarene"na kuanzisha dini hii ya "Wapagani Waliozaliwa Upya"baada ya kupata maono ya miujiza kwa miaka 5 mfululizo.

Mji wa Jonesboro jimboni Arkansas Marekani umekuwa ni chimbuko la madhehebu mapya ya ajabu ajabu yapatayo 75. Kufuatia hali hiyo ya dini mpya kuzuka katika mji huo kila kukicha watu wameamua kuubatiza mji huo kwa jina la "Fort God" wakimaanisha ng’ome ya Mungu.

Muumini wa dhehebu hili la kipagani la ‘Wicca" linaloongozwa na Terry anapaswa kuwa na vifaa mbalimbali vya kichawi na kimizimu vinavyotumiwa na dhehebu hili wakati wa ibada.Vifaa hivyo vimekuwa ni pamoja na mifupa, vibuyu,rangi,chupa, vitabu maalum,ngoma, mishumaa, ubani, udi na uvumba.

Ili kuwarahisishia waumini wake upatikanaji wa vifaa hivyo, Terry amefungua duka kubwa la kuviuza jijini Jonesboro.

Lakini la kushangaza ni kuwa hivi karibuni duka hilo liliponea chupuchupu kufungwa baada ya mwenye nyumba kumjia juu Terry akimdai kodi.

Steven Griffin, anayemiliki nyumba ambamo Terry amefungua duka hilo alifoka kuwa "mimi siogopi miungu yako na ikifika kesho hujanilipa kodi yangu nitatupa bidhaa zako na kufunga nyumba yangu"

Kauli hiyo ya Griffin iliwapelekea Wamarekani kujihoji ikiwa kweli mizimu ya dhehebu hilo la wapagani waliozaliwa upya inayo nguvu kama kiongozi wao Terry anavyodai.

Terry, yeye kwa upande wake alidai kuwa Grriffin amehongwa na Kanisa la Nazarene alikokuwa akisali hapo awali kabla ya kuasi kusudi apate kutibua ustawi wa dhehebu la Wicca katika jiji la Jonesboro.

Lakini viongozi wa madhehebu kadhaa ya Kikristo huko Marekani wamelipinga dhehebu la "Wicca"vikali na kuliita kuwa la kishetani. Mmoja wa viongozi hao ni Mch. Gary Taylor wa Kanisa la United Christian ambaye anasema "Those kinds of things do not belong in a Christian community. I just don’t believe this is a religion" akimaanisha "Vitu vya aina hiyo havipo katika Ukristo. Kwa kifupi mimi siamini kama hii ni dini"

Dhehebu la Wicca kwa mujibu wa jarida la ‘Times" limepata kuhusishwa na mauaji ya kikatili ya wavulana 3 yaliyotokea huko West Memphis jimboni Arkansas. Wavulana hao maiti zao ziliokotwa sehemu zao za siri zikiwe zimenyofolewa.

Katika maandamano yaliyofanywa hivi karibuni na wafuasi wa "Wicca" wapatao 75 wakipinga 'kukashifiwa' umati wa wakazi wa Jonesboro wapatao 2000 waliwazomea wakipiga makelele ya;"You’ll burn in hell!’ "Mtaunguzwa Jehanamu"

Maandamano hayo ya wapagani waliozaliwa upya hatimaye yalidhibitiwa na polisi wa Marekani wapatao 80

Profesa Robi Anderson, ni profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha Arkansas State Univerisity, kilichoko jijini Jonesboro. Yeye anayo haya ya kusema kuhusu dhehebu hili;"People believe that if its not Christianity its Satanic" yaani

"Watu wanaamini kuwa kama siyo Ukristo basi ni Ushetani bila ya shaka"

Kwa mujibu wa gazeti la Christian Monitor Science linalochapishwa nchini Marekani, dhehebu la "Wicca" sasa linasambaa kwa kasi na limeanza kujipenyeza Afrika Magharibi na Mashariki ambapo Kenya ni moja ya nchi zilizotajwa kuwa nalo, na hakuna ajuaye huenda wapo Tanzania pia.