Mtu aliyemtembelea Mfalme wa Uingereza kifua wazi bila shati

lWalinzi wa Ikulu "Buckigham Palace" nusura wamtie mbaroni

lPamoja na kuwa msomi aliyebobea alipokufa hakuacha chochote zaidi ya miwani, kanda mbili mkeka na saraka la vitabu

Na Mwandishi Wetu

Kila mtu jijini London alikuwa akisubiri kwa hamu kubwaa kumuona mgeni kutoka India ambaye angelitembelea Uingereza majira hayo ya kiangazi.

Mitaa ya jiji la London alipambwa hasa siku ambayo mgeni huyo mheshimiwa angelifika Ikulu ya "Buckigham Palace" kuonana na mfalme George kwa ajili ya mazungumzo na pia kunywa naye chai ya jioni. Kwa hakika ilikuwa furaha tele jijini London.

Hata magari ya kukokotwa na farasi yalipambwa vilivyo. Hali hii iliwadhihirishia wakazi wa London kuwa mgeni aliyekuwa akutaraji wa kuwazuru hakuwa mtu wa hivi hivi.

Lakini watu wote hao waliokuwa na furaha ya kumngojea mgeni huyo, akiwemo King, George mwenyewe ambaye angelikuwa mwenyeji wake hakuna aliyejua kuwa mgeni huyo wa heshima angezusha kiroja huko kwenye kasri ya mfalme. Kiroja cha kihistoria ambacho kingelisimuliwa mwaka nenda rudi kadri ambavyo sayari ya dunia ingeliendelea kudumu kuwapo.

Akiwa amewatia homa wakoloni wa Kiingereza huko kwao India, mnamo mwaka 1943, Mahtma Ghandhi alipewa mwaliko maalum na mfalme George apate kutembelea jiji la London Waingereza wapate fursa ya kumuona uso kwa uso.

Vipo vitu vingi vilivyopelekea Mfalme George kumheshimu Mahatma. Kwanza pamoja na kuwa alikuwa ni msomi wa hali ya juu aliyebobea mara tu baada ya kuhitimu shahada yake ya juu katika fani ya sheria kwenye chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza, serikali ya kikoloni ilikuwa tayari kumpa cheo kikubwa akirejea kwa India. Lakini Mahatma alikataa kuajiriwa popote na zaidi ya yote akakataa kuvaa mavazi ya watu wa magharibi.

Alivaliwa ''rubega'' la Kihindi, kandambili na miwani ya bei ya chini hali iliyofanya Waingereza wamuogope. Alipoulizwa kwa nini anafanya hivyo Mahatma alijibu.

"Wapo Wahindi wenzangu wenye taabu na dhiki nataka niwe sawa nao thamani ya mtu haipo katika mavazi".

Jambo lingine ni kuwa Mahtma alipambana na Waingereza kutaka India ipewe Uhuru akitumia mtindo wa kupigania haki unaoujulikana kama "Satyagratha" mtindo huu, ni wa mtu kupigania haki pasipo kufanya fujo na kumwaga damu.

Mara kadhaa alinusurika kuuliwa, katika njama zilizopangwa na wakoloni wa Kiingereza nchini India. Hivyo alipotembelea Uingereza mwaka 1943 ilikuwa ni baada ya mfalme Geogre kumnyanyulia mikono na kumpa heshima kwa jinsi alivyo shujaa.

Sasa nikurejeshe jijini London ambako mgeni alikuwa akingojewa. Hatimaye saa ikawadia. Vingora vikasikika penye kasri ya Mfalme kuashiria kuwa mgeni ndiye huyo anaingia. Askari waliokuwa wakilinda kasri ya mfalme waliangaza macho yao huko na kule wasimuone mgeni mwenyewe.

Mara kelele zikasikika, askari aliyekuwa doria akapuliza kipenga cha hatari tangazo likakikika.

Tumemkamata mtu hatari sana penye lango la kasri ya Mfalme".

Naye mtu mwenyewe alikuwa kavalia kinguo mithili ya nepi ya kumfunga mtoto mchanga, huku akiwa yuko kifua wazi bila shati. Machoni alivalia miwani ya bei nafuu huku akikamilisha miguuni kwa kuvalia malapa (kandambli).

Kwa sura alionekana kweli ni Muhindi kutoka India haswa. Lakini amefikaje pale kasri ya "Buckingham Palace" akiwa na hali kama ile? Tena ikiwa ni siku maalum ya kupokea mgeni wa heshima anayesubiriwa kwa hamu?

Basi walinzi wa Kasri ya mfalme jijini London, wakamtia mbaroni mtu yule na wasijue kuwa huyo ndiye Mahtma Ghandhi mwenyewe waliyekuwa wakimngojea kwa hamu anywe chai ya saa kumi na Mfalme wao. Basi nini kilifuata?

Askari wakampigia simu mfalme George, kumuelezea taarifa za kukamatwa kwa mtu anayetembea kifua wazi bila shati penye kasri ya mfalme. Mfalme akawauliza yukoje? Nao wakaelezea ndipo akaamuru mtu huyo wa ajabu aruhusiwe kuonana naye.

Basi askari wa kamchukua mtu yule chini ya ulinzi mkali mpaka mbele ya mfalme. Naye mfalme George alipokutana uso kwa uso na mtu huyo akasema.

"Mahtma Ghandhi karibu, nimekusubiri kwa hamu sana".

Basi askari wa Kiingereza wakipigwa na butwaa baada ya kugundua kuwa mgeni yule asiye na shati waliyemkamata ndiye Mahtma Ghandhi mwenyewe aliyekuwa akisubiriwa kutembelea mfalme penye kasri yake.

Pamoja na jitihada zake za kupigania uhuru Mahatma Ghandhi hakuweza kudumu kuwa hai kushududia India ikipata uhuru wake Agosti, 7, 1947. Miaka miwili tu kabla ya India kupata uhuru Mahatma aliuwawa kwa kupigwa risasi na kijana wa Kiingereza aliyejifanya kuwa ni mwandishi wa habari aliyetaka kumhoji.

Mnara wa kumbukumbu ya mtu huyu wa ajabu umejengwa jijini Cape Town, Afrika Kusini alikopata kuishi kama mkimbizi.

Mauti ilipomfika hakuna fedha wala mali aliyoacha zaidi ya miwani, kandambili, mkeka wa kulalia na saraka la vitabu.

 

Miji ya London, Lisbon, Moscow, Nairobi, Cairo na Paris

 

lChimbuko lake ilikuwa vituo vya biashara kanda ya mito mikubwa

SAA zinaelekea kuwa Magharibi katika mji wa Moscow. Umati Mkubwa wa watu wanavinjari huku na kule wakipunga upepo kandokano ya mto. Ukiwa umepambwa na mandhari nzuri ya mto Moskva, Moscow ndio mji mkuu wa Jamhuri ya Russia.

Mji huu wa sifika licha ya kupata kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki pia umekuwa ni kitovu cha elimu na kiunganishi cha safari za ndege na miji mingine mikubwa duniani.

Mto Moskva ama kwa hakika ndiyo chimbuko la mji wa Moscow. Ni mto huu pia ndio uliopelekea mji huu kuitwa Moscow.

Tangu mwaka 1320, mababu za Warusi ambao waliitwa Waslv, tayari walishaanza kufanya biashara kupitia mto Moskva. Waslav mbali ya kuwa hodari kwa biashara pia walikuwa ni wafugaji na wavuvi wazuri, kitu kilichowavutia kwenda kuishi kando ya mto Moskva.

Mji wa Moscow ulianza kama kijiji cha uvuvi kando ya mto Moskva lakini taratibu miaka ilivyoenda wafanyabiashara toka sehemu zingine za Russia walivutiwa kuweka vituo vyao hapo na ukaanza kukua kwa kasi. Leo Moscow siyo kijiji cha uvuvi tena kama iliyvokuwa zama za Waslav wa kale.

Mji huu ulioanza kando ya mto leo una vitutio vingi vya kutazama ikiwa ni pamoja na mandhari nzuri ya mto Moskva, Ikulu ya Kremlin, sanamu ya mwanashairi Alexander Pushkin, jengo la Utamaduni la Bolshoy Theatre na uwanja mkubwa wa mpira wa ‘Lemin Central Stadium’.

Hoteli kubwa ya Rosiya iliyoko mjini Moscow ni mojawapo kati ya mahoteli yaliyoingizwa kwenye kitabu cha "Guinness Book of Records" kwa kuongoza kwa kupika idadi kubwa ya vikombe vya chai.

London mji mkuu wa Uingereza, viwanja vyake vitatu vya ndege vya Heathrouw Gatwick na Stansted hupokea idadi kubwa ya wageni wanaoutembelea kila siku toka mataifa mbalimbali.

Mji huu hali kadhalika mithili ya Moscow chimbuko lake ni Mto mkubwa wa "Thames" unaotiririka kati yake. Mto huu kando ya kuwa chimbuko la London pia umeiongezea hadhi na mandhari nzuri ya kuvutia.

Thames umedumu toka zama za "Anglo Sacons" za mababu za Waingereza. Mwaka 1440 wakati biashara kandoni mwa mito iliposhamiri huko Uingereza, Mto Thames ulikuwa tayari upo.

Leo London siyo kijiji tena kando ya mto bali ni jiji kubwa lenye mandhari ya kuvutia kando ya mto. Daraja la "Tower Bridge" lililoko kwenye mto Thames ni mojawapo ya vivutio katika jiji la London. Sehemu zingine za kuvutia za London ni pamoja na "Trafalgar square" ikulu ya "Buckingham palace" na bustani lukuki za kutunzia wanyama.

Mpaka leo hii Wareno wanaamini kuwa unapoutaja mji wao mkuu wa Lisbon basi unamaanisha mto mkubwa wa "Tagus".

Ukiwa ni mto mkubwa wenye mandhari ya kuvutia Tagus unatiririka katikati ya jiji kubwa la Lisbon.

Lisbon mithili ya London na Moscow, nao pia ulianza kama kituo cha kibiashara na mawasiliano kando ya mto. Wareno wanasifika kwa uvuvi.

Mwaka 1520 kulingana na kitabu cha "Portgualinees of History" kilichochapishwa kwa lugha ya Kireno na Chuo kikuu cha Lisbon, mji huu ulianza kama kijiji kidogo tu cha uvuvi kando ya mto Tagus.

Leo mto mkubwa wa Tagus ndiyo fahari ya jiji la Lisbon. Wakati wa likizo idadi kubwa ya watalii hutembelea Lisbon kusudi wapate kufurahia mandhari nzuri ya mto Tagus. Kwa hakika mto huo wa kale mdogo ndio chimbuko la Lisbon ya leo.

Nako katikati ya jiji kubwa la Paris mto mkuwa wa Seine unatiririka. Pamoja na kuwa mnara mkubwa wa Eifel umejizolea sifa ya kuwa alama ya jiji la Paris, kama mji huo ungelikuwa ni supu basi mto Seine ungelikuwa ni chumvi yake. Ndiyo kusema bila Seine jiji la Paris lisingekuwa Paris.

Historia yathibitisha mto Seine ulianza kuwavutia Wafaransa toka zamani sana. Mfano hai ni katika miaka ya 1320 ambapo msafiri mmoja wa Kijerumani alifka Ufaransa na kugundua kuwa jamii za Wafaransa zilikuwa na hija maalum ya kuuzuru mto Seine kila mwaka.

Pahala walipozoea kupazuru kando ya mto Seine leo ndio jiji kubwa la Paris.

Mji wa Paris kando ya kuwa kituo maalum cha kibiashara pia ni kitovu cha sanaa.

Mji wa Paris haujawavutia wazungu pake yao, bali hata Waafrika. Mtaa wake wa Rue St. Denis leo umegeuka kuwa makazi ya wahamiaji wa Kiafrika.

Uwanja wake wa ndege "Charles De Gaule Int" ni kituo cha mawasiliano na miji mingine mikubwa na mashuhuri duniani. Uwanja huo umepewa jina hilo kama kumbukumbu ya Jenerali Charles de Gaule" aliyepata kuwa rais wa Ufaransa.

Nako nchini Kenya, Mto mdogo wa "Nyorobi" kwa hakika ndio ulioupa mji mkuu wa Kenya jina lake la Nairobi. Wazungu walowezi wa awali kufika Kenya walivutiwa na ardhi zenye rutuba katika maeneo ya nyanda za juu yaliyokaliwa na Wakikuyu na hata kuyaita "Whites Highlands".

Hata hivyo walivutiwa pia na hali ya hewa kando ya kijito kidogo kilichoitwa "Nyorobi".

Wakaweka kituo cha kibiashara hapo. Miaka ilipozidi kusogea kituo hiki kikikua kikabadilishwa jina na kuitwa Nairobi kufuatia Mto huo wa "Nyorobi"

 

Mtakatifu Klara wa Asizi mtawa mwanzilishi wa shirika la Waklara

lNi Wakrala fukara

lAlimuingiza utawani ;dada yake aliyetaka kumbadili yeye imani yake.

Na Josephs Sabinus

Hawakula nyama hawakulala kitandani wala kuvaa viatu

INGAWA kwa wakati huo Mtakatifu Klara alikuwa mgonjwa sana, siku hiyo alijikongoja huku akisali kwa unyenyekevu mkubwa mbele za Mungu. Akatoka kitandani na kuifuata njia ile iliyokwenda kanisani akatwaa chombo cha Hostia Takatifu akapiga magoti na kusali;akasema "Mungu! Usitoe roho zetu sisi tunaokutumainia kwa watu hawa wakali. Uwalinde watumishi wako uliowakomboa mwenyewe kwa damu yako"

Siku hiyo makundi mengi ya Waislamu yalikuwa yameshambulia mjini wa Asizi na kuuteka kabisa wakaingia kila mahala na kufanya madhara makubwa; walitaka hata kuingia katika monasteri ya Mtakatifu Klara.

Lakini;baada ya Klara kujua hali ilivyokuwa na kumnyenyekea Mungu akimlilia kwa sala hiyo, ghafla bila kujua Waislamu hao wakashikwa na hofu tele na wote wakaanza kutetemeka ovyo tena wakakimbia kwa fujo isiyomithlika na kutokomea wenyewe.

Mtakatifu Klara aliyezaliwa mwaka 1194 huko Asizi zamani za Mtakatifu Fransisco, tangia maisha yake ya utoto alitamani sana na mara nyingi alipenda kukaa katika hali ya upweke huku akisali kwa mafungo na maombi makali. Klara alipochunguza kwa makini aliuona na kuutambua mwenendo wa Mtakatifu wa Fransisco akamfuata na kumwambia.

"Nataka kuiacha dunia na badala yake nimtumikie Mungu kwa faragha"

Mtakatifu Fransico alifurahi sana juu ya habari hizo;akaamua kumjaribu kwanza; akamtuma kwenda kuomba chakula chake kwa watu kama mtu maskini.

Akiwa na umri wa miaka kumi na minane Mtakatifu Klara anayekumbukwa kila ifikapo Agosti 11 alitoka kisirisiri nyumbani kwao;kwa baba na mama yake. Hatua hiyo ilikuwa baada ya kukataa kuolewa mara mbili huku akikataa kata kata kuchumbiwa ingawa wazazi wake walitaka aposwe na kijana mmoja tajiri.

Siku hiyo ya sikukuu ya Matawi alienda katika Kanisa la Porsiunkula akayavua mavazi yote ya urembo na umaridadi;akamuomba Mtakatifu Fransisco amkate nywele zake.akamkata na kisha kumvika shela ya masista.

Wazazi wake walichukizwa sana na hatua hiyo wakataka wamrudishe nyumbani kwao kwa nguvu lakini Mtakatifu huyu akawambia na kusema simtaki mchumba mwingine isipokuwa Yesu Kristu pekee niliyenaye hadi sasa" Klara akasema kwa ushujaa. Na huku akionekana kuwa maudhi kwa wazazi hao na nduguze.

Wazazi hao wakajadili na kuamua kutumia mtu. Ndipo punde kidogo dada yake Klara aliyeitwa Anyesi alikuja kumtazama kwa lengo hasa la kumsemea na hata kumbadili Klara nia yake ya kuendelea kuishi utawani.

Lakini mambo yakageuka; Klara akaanza yeye kwa kumshawishi huyo dada yake amfuate na kujiunga nae katika utawa ikawa hivyo Anyesi mwenyewe akabadili nia badala ya kumbadili Klara yeye ndiye aliyebadilika akajiunga na kuingia utawani. Klara akafurahia hatua hiyo ya maana alijua kazi, uwezo na mapenzi ya Mungu vimejidhihirisha kwake maana alishajua lengo la dada yake.

Haikupita miaka mingi hata baba yao alipofariki na kumuacha mama yao,pia aliingia utawani na huo ndio ulikuwa mwanzo wa shirika la WAKLARA FUKARA. Watawa hawa wa familia moja waliishi maisha magumu sana tena yanayotia huruma tena yaliyokuwa chini ya msaada mkubwa na ulinzi wa Mungu.

Kwa mujibu wa kanuni na taratibu za watawa hao hawakuvaa viatu bali walitembea miguu mitupu wala hawakutakiwa kulala kitandani bali walilala chini zaidi na zaidi hawakula nyama katika maisha yao yote na hata kule kuzungumza tu hawakuzungumza na mtu hadi pale ilipolazimu kwa kulazimishwa kufanya hivyo au hadi pale ilipokuwa kwamba wamesemeshwa.

Klara aliyetangazwa rasmi kuwa mtakatifu mwaka 1255 miaka mitatu tu baada ya kufariki alikuwa na busara kubwa ya kuwatunza masista kwa hivi alimwandikia mama mkuu wa Konveti nyingine asiongeze mambo magumu zaidi alisema ".......Sababu miili yetu siyo ya chuma "

Akawa Mkuu wa shirika lake kwa muda miaka 40 hata alipofariki mwaka 1253.

 

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

MUNGIKI:Dini ya jadi ya Wakikuyu inayoendelea hadi leo

lWanaamini mashujaa wa vita vya Mau-Mau kuwa ni mitume wao

Na Ignatio Obuombe, JR.

Nywele zao husokotwa katika mitindo wa rasta. Ukikutana nao kwa mara ya kwanza katika maisha yako watazielekeza hisia zako Jamaika, nchi iliyo moja ya visiwa vinavyounda "Carribean". Kwa nini?

Mitindo ya Rasta ya nywele za waumini wa Mungiki haijatofautiana hata kidogo na ile ya nywele za aliyekuwa kigogo wa muziki ya "Reggae"duniani hayati Robert Nesta Bob Marley aliyekuwa mzaliwa wa Jamaika.

Ikiwa ni dini ya jadi ya jamii ya Wakikuyu wanaoishi nchini Kenya Mungiki inazidi kukua kwa kasi ya aina yake, huku likihatarisha usalama nchini Kenya kwa kuendesha malumbano baina yake na Serikali.

Dini ya Mungiki haijaanza leo.Ni ya tangu zama za kale ambapo Wakikuyu walikuwa wakiabudu katika mlima Kenya ambao walikuwa wakiamini ni mlima wa Mungu "Engai". Jina la nchi ya Kenya lenyewe kwa lugha ya Kikuyu ni "Jogoo" na waliuita mlima huo Jogoo kufuatia maumbile yaliyoko juu ya kilele chake.

Dini ya Mungiki viongozi wake ni wazee wa jadi wa jamii ya Wakikuyu na yasadikiwa hata muasisi wa taifa la Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta alikuwa ni mfuasi hodari wa dini hii ya Mungiki.

Ili mtu ajiunge na dini ya Mungiki kama ni mwanamke, sharti la kwanza ni lazima atahiriwe na kama ni mwanaume pia sharti atahiriwe na ashiriki uvamizi wa kuiba na kuteka mifugo ama mali za jamii nyingine.

Ni katika kipengele hiki cha kutahiri wanawake ndiko unapozukia ugomvi katika ya dini ya Mungiki na Serikali ya Kenya ambayo siku hizi inapinga tohara kwa wanawake.

Kwa vile asilimia kubwa ya wapigania Uhuru walikuwa ni watu wa jamii ya Wakikuyu mara tu baada ya vita vya "Maumau"kunako mwaka 1953 na mara baada ya Uhuru wa Kenya mwaka 1963, waumini wa dini ya Mungiki walidai kuwa ni wao wenye haki ya kuitawala Kenya kwa sababu mashujaa wote wa vita vya Uhuru waliotoka kwenye jamii ya Wakikuyu walikuwa waumini waaminifu wa "Mungiki"waliokula kiapo.

Wapiganaji wa Kikuyu walioshiriki kwenye vita vya "Maumau" (Mzungu Arudi Ulaya Mwafrika Apate Uhuru) wote wanahesabika ni mitume watakatifu wa "Mungiki"na mizimu yao huabudiwa na waumini wa"Mungiki"hata leo .

Baadhi ya nchi mashujaa wa vita vya 'Maumau' wanaohesabika hata leo kuwa ni watakatifu wa dini ya "Mungiki" ni pamoja na Field Marshal Dedan Kimathi, Jenerali China na wengineo wengi.

Mugo wa Kibiro ambaye hapo kale alikuwa nabii wa Kikuyu aliyetabiri kuhusu kuja kwa walowezi Wazungu kuteka ardhi ya Wakenya, hususan maeneo yenye rutuba ya Wakikuyu naye pia anahesabika kama nabii wa dini ya Mungiki na anaabudiwa.

Mpaka sasa dini ya Mungiki ipo kwenye mgogoro na Serikali ya Kenya kwani imani waumini wa Mungiki walivyojiwekea ni kuwa siku moja kupitia kwa mizimu ya mitume wao kama Field Marshall Dedan Kamathi, Jenerali China na Mugo wa Kibiro watafanikiwa kutwaa madaraka kuongoza serikali.

Kila muumini wa Mungiki ni sharti aning’inize picha ya mmoja wa mashujaa wa vita vya "Maumau" ukutani ndani ya nyumba yake.

Kitabu cha Rais wa kwanza wa Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta kinachoitwa "Facing Mount Kenya" yaani "Kutazama Mlima Kenya" kinayo mengi ya kuelezea kuhusu utamaduni wao na imani yao kwa "Engai,"mungu waliyeamini anaishi juu ya kilele cha mlima Kenya.

Mungiki wamejiimarisha zaidi katika mkoa wa Kenya wa Rift Valey, Mkoa wa Kati na Mkoa wa Nairobi hususani wilaya ya jirani nao kama Kiambu na Thika. . Maeneo ya Murang'a na Nyeri, pia ni maskani ya waumini wa Mungiki. Mitume wa Mungiki kama Dedan Kimathi aliuwawa na Wazungu wakoloni na Jenerali China naye pia alinyongwa na wakoloni.