Ole zinazotajwa katika Ufunuo 9 zitakuja lini? (2)

Katika toleo lililopita lilijibiwa swali la Ndugu Elias Joseph ambalo linapatikana katika kitabu cha Ufunuo 9:12, ambapo tunasoma; Ole wa kwanza umekwishapita, tazama bado ziko ole mbili zinakuja baadaye. Na ndugu Eliasi, anauliza; kutokana na sehemu hiyo ya maandiko Matakatifu, je ole hiyo imepita au bado? Katika sehemu hii ya pili PADRI TITUS AMIGU anajibu.

Ndugu Elias unakorofishwa sana na lugha ya KIAPOKALIPTIKO inayotumiwa na mwandishi wa kitabu cha Ufunuo. Yachane niliyokujibu katika jibu la swali lako lililopita. Ili tupate kujua kama "Ole" hizo zimepita ama la, ni awali ya yote nilazima uzijue Ole zenyewe. Pili ujue tabia za kitabu cha Ufunuo na hivyo namna ya kukitafakari. Basi tuanze kwa kuzifahamu ole zenyewe.

Tarumbeta la kwanza la Ole ni kuanguka kwa dola ya Wasaraseni, Turumbeta ya pili ya Ole ni kuanguka kwa dola ya Waturuki na kishapo mamlaka ya Papa ndio yule nyoka na yule mwanamke kahaba. nk.

Halafu kila siku kwa kadri ya kundi hili, kila siku inayotajwa kitabuni ni sawa na mwaka 1 na hivi kwa mfano siku mia moja ni miaka 100 au siku 1260 ni sawa na miaka 1260. Mtindo wa nne wa kutafsiri ni mtindo wa kisasa, wa kukamilisha yote na kuyahamisha kutoka hapa tulipo na kuyapeleka katika enzi ya mbali, enzi na hali zilizo mbali na hizi ambazo sisi tunazo sasa

Na hivi ni kusema kuja kwa Kristo kusidhaniwe kwa namna yeyote kuwa ni karibu, ila kuko mbali na enzi na hali yetu sisi. Mtindo wa tano ni mtindo mwingine wa kisasa ambao umejengwa juu ya fikira kwamba NERO NI lazima arudi, na Nero huyo ndiye atakayekuwa mpinga KRISTO. Kabla ya mpinga Kristo huyo ambaye atuwa ni Nero hakuna litakalotokea mtindo wa sita, ni mtindo wa kutafsiri KIAPOKALIPTIKO kwa misingi ya Kiyahudi.

Na saba ni mtindo wa ngano za Bab. Mitindo hii # niliyokutajia sasa hivi sitalifafanua bali tu, ningelipenda nijibu swali lako maana nimeyazungumza mengi. Kwa namna yoyote ndugu Elias, sisi hatupaswi kamwe kutafsiri kwa papara za jazba neno kwa neno, picha kwa picha, bila kutafuta kwa utulivu wa rohoni mambo yaliyojificha katika kitabu hiki.

Tukifanya tafsiri yetu kwa jazba, tutajifunga wenyewe macho, na kusubiri tuyaone yaliyomo kwenye kitabu yakitimia moja baada ya jingine na hivyo kuwatisha na kuwadanganya watoto wa Mungu bure. Hakika ninakwambia tukifanya hivyo hatutakosa adhabu yetu. Je sasa ole zilizotajwa katika sura ya 9:12 zimepita au bado? hilo swali lako ndugu Eliasi. Kutilia maanani aya ya 1 ya sura ya 1 ambapo imesemwa wazi kamba mambo yaliyoandikwa katika kitabu cha ufunuo yalikuwa yatukie katika wakati wa karibu wa maisha ya mtunzi. ndugu Elias ni halali kabisa kutafsiri kitabu cha ufunuo kwa mchanganyiko wa mtindo wa kutumia wakati ulipita, pamoja na mtindo wa kutafsiri kihistoria. Hata hivyo ndugu Eliasi mtindo wa kutafsiri kihistoria ikichanganyika na jazba ni hatari na watu wengi wameaibika tayari hasa walipochukua tafsiri ya siku moja mwama mmoja. Mfano Bwana Charles Tagerusero ambaye baada ya kumsadiki William Milla aloposoma kitabu chake cha KIAPOKALIPTIKO, kile cha Nabii Danieli 8:14 baada ya asubuhi na alasiri 2300 nyakati za jioni na asubuhi 2300 ndipo mahali patakatifu patakapotakaswa.

Huyo alipiga hesabu akianzia mwaka 457 kabla ya Kristo akasema mwaka 1843 Kristo anagalikuja, na mwaka 1843 Kristo hakuonekana. RUSEL akasema mnamo mwaka 1876 kwamba Kristo eti alikwishapita miaka miwili iliyopita ila alikuja kiroho tu, yeye Rusel akajipa kazi kuandaa watu kama nabii mmojawapo kati ya manabii saba wanaopaswa kuandaa watu kwa utawala wa miaka 1000 ya Kristo.

Yeye Rusel alidhani alikuwa akiongozwa na Roho Mtakatifu wakati alipokuwa akiagua hayo na aliagua kadri yake kwamba utawala ule wa miaka 1000 ya Kristo ungalidumu tangu mwaka 1914-2914 mambo hayo hayakutokea. Kumbe kilichoanza tangu mwaka 1914 kilikuwa ni vita ya kwanza ya Dunia; na hapo hata babu zetu walikwenda kupigana sehemu mbali mbali kupigania utawala wa Kijerumani. Na mpaka leo hii ndugu Elias, huo ufalme wa miaka 1000 haujaja, ni miaka sasa karibu 83 tangu pale ulipoaguliwa kwamba ungelianza, uwongo ukawa umesemwa na Rusel akawa anaaibika.

Akafanya nini, basi ukawa mwisho wa dunia unaaguliwa na kusogezwa mbele daima na daima. Miaka ambayo ilitabiriwa kuwa mwisho wa dunia ni mingi ambayo ni pamoja na hii ifutayo: mwaka 1914, mwaka 1920, mwaka 1967, ambao ulitabiriwa na JIMM YONES huko Marekani na kadhalika. Hakuna kati ya watabiri hao aliyefahamu kwamba ijapokuwa kuna siku ya mwisho wa dunia tarehe hakuna anayejua; hata Yesu Kristo katika ubinadamu wake hakuijua. Soma Mathayo 24:36. Basi tafsiri ya kweli ya kitabu cha Ufunuo ni ile inayofanywa kwa wakati uliopita katika muunganiko wake na mtindo wa kihistoria.

Sasa Ndugu Elias hizo Ole kwa kujali sura ya kwanza kama nilivyoanza pale kwanza, zimekwishapita tayari. Tungoje mwisho wa dunia kama ulivyo wajibu wetu, lakini tusitumaini kuzishuhudia ole zile tatu kwanza.

Ole haziambatani kabisa na Injili ambamo Bwana wetu amesemwa kwamba aliongelea mambo ya mwisho wa dunia. Soma kitabu cha Marko 13 na hata Injili ya Mathayo 25: Hivi Ole hizi ni matukio ya kihistoria yaliyokwishakupita, mengine hata kabla sisi hatujazaliwa . Sasa nitakufafanulia mifano mbali mbali mistari michache katika hizo ole. Kuanguka kwa nyota ni mfano wa kuanguka kwa mmojawapo wa Malaika walioasi, wale walioanguka, na hii ni kusema ni kuanguka kwa Shetani mwenyewe ambako Yesu Bwana wetu alikuzungumzia. Pia kwenye Injili ya Luka 10:18 Bwana alisema nimemuona Shetani akianguka kutoka mbinguni, maana yake aliuona utawala wa Shetani ukivunjikavunjika. Halafu shimo kubwa linalotajwa katika sura hii ya 9 ya kitabu cha Ufunuo linazungumzia au linamaanisha jeneza ambako ndiko malaika waasi walikofungwa mpaka siku ya hukumu ya mwisho.

Abadon au Apolion maana yake ni uharibifu au mbomoko ambao limewekwa kama mtu, hiyo ni tamathali ya semi na ni mojawapo ya ufundi wa kueleza mambo, ambao mwandishi wa kitabu cha Ufunuo anao, na kwamba lilipopigwa tarumbeta la sita, Yohana muona maono wetu alisikia sauti moja ikitokea kwenye kona za Altare, maana yake ni kwamba adhabu ya wasio amini ilifuatia vilio na sala za wafia dini ambazo zimeelezwa kwenye sura ya 6 mistari ya 9-10.

Juu ya Askari waliokuja kuharibu theluthi ya watu ni wale askari wa Kipathia maana Mto Frati ulikuwa ni mpaka wa mashariki wa dola ya Kirumi na huko walikaa Wapathia ambao walikuwa ni maadui wa kutisha sana kwa dola ya watawala wa Kirumi.

Hivi aya ya 19 ya sura ya 9 inapoelezea juu ya farasi wa vita ambao nguvu zao zilikuwa vinywani mwao na mikiani mwao inarejea kwa wapanda farasi wa Kipathia ambapo baada ya mashambulizi yao, walirudi nyuma kwa mbinu ya kijeshi na baadaye wakarusha mashuti ya Kipathia yaani Salvo ambayo yalikuwa yamewekwa kwenye mikia ya farasi wao. Basi ndugu Eliasi kwa vile mambo haya yamekwisha kupita na yamejengwa tayari juu ya historia, tusitazamie kuyaona huko mbele, labda kwa miujiza. Yamekwisha kupita na sasa kazi ni kwetu sisi tuutafute Ufalme wa Mungu kutekeleza amri kuu ya mapendo na siyo kusubiri ishara za KIAPKALIPTIKO. Wakati wetu ni huu, kifo kinatuwinda, wewe na mimi, tusingoje kuambiwa na Bwana wetu, "kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara". Soma Injili ya Mathayo 16:4.

Ndege ya Concord

lInasafiri maili 1,336 kwa saa

lWanawake wengi uogopa kuipanda

Wanadamu kwa miaka mingi sasa wameweza kusafiri huku na huko duniani kwa kutumia vyombo mbalimbali vya usafiri likiwemo anga, ardhi na maji.

Kwa kutumia uwezo wao wa akili wameweza kuifanya dunia ionekane kuwa ndogo tu kutokana na kutumia vyombo hivyo hasa magari, ndege na meli.

Miongoni mwa vyombo muhimu sana duniani vya usafiri vilivyoifanya dunia ionekane kuwa ndogo ni vile vinavyosafiri angani ambavyo ni ndege.

Katika usafiri wa nchi kavu wanadamu wameweza kuifanya dunia kuwa ndogo kutokana na kutumia magari, pikipiki, baiskeli na treni, ambapo kwa upande wa majini wamekuwa wakitumia meli mitumbwi na majahazi.

Usafiri mwingine ulio muhimu na ambao kidogo tunaweza kuuita wa kisasa ni ule wa kutumia vyombo vya angani kusafirisha abiria na mizigo yao, yaani ndege.

Usafiri huo wa ndege tunaweza kusema ni mgeni au wa kisasa kwa vile ndio usafiri wa miaka ya karibuni kabisa kutumiwa na binadamu kusafiri huko na kule.

Binadamu aliweza kusafiri duniani kutoka nchi moja hadi nyingine kwa masafa ya mbali kabisa kwa kutumia meli ambazo wakati huo zilikuwa zikiwachukua muda mrefu sana katika safari zao.

Usafiri wa magari na treni kwa wanadamu ulikuwa ukitumika kwa ajili ya safari fupifupi tu za nchi kavu.

Hivi sasa watu wanaweza kusafiri kote duniani kwa muda mfupi sana tena bila uchovu kwa kutumia ndege. Mathalani mtu anaweza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa muda wa saa moja tu kwa ndege, wakati akitumia treni atachukua siku tatu na kwa gari siku mbili.

Ndege husafiri angani, na kutokana na mazingira yake zinaweza kusafiri kwa mwendo wa haraka sana kutoka mahali pamoja hadi kwingine.

Katika usafiri huo wa ndege zipo ndege za aina mbalimbali ambazo kila moja ina sifa yake binafsi na inaweza kusafiri kwa umbali wake kulingana na jinsi ilivyoundwa.

Ndege aina ya Concord ndiyo inayoweza kwenda kwa kasi zaidi katika ndege za abiria duniani ikiwa na spidi kati ya maili 1,336 kwa saa.

Ndege hii ya Concord ina injili nne zenje jumla ya nguvu zilizo sawa na injini 300 za magari madogo ya kawaida kama vile Toyota Carina, Peugeot ama Mercedes Benz.

Ufaransa ilikuwa ndiyo nchi ya kwanza duniani kuunda na kurusha angani ndege aina ya Concord namba 001 mwaka 1969, na majuma matano baadaye Uingereza nayo ikarusha angani ndege yake ya kwanza ya aina hii.

Lakini hata hivyo ilichukua miaka 14 tangu kuundwa kwa ndege hizi kwa serikali kufanya safari za kibiashara hapo mwaka 1976. Asilimia 80 ya abiria wanaosafiri na Concord hadi sasa ni wanaume na kati yao asilimia 43 ni wakurugenzi watendaji, wenyeviti watendaji na mameneja wa makampuni makubwa ya kibiashara duniani.

Utafiti huo unaonyesha kuwa wanawake na watoto ni wachache sana waosafiri na ndege hiyo, labda kutokana na jinsi inavyokwenda kasi na kusafiri katika anga la juu sana, na hivyo kuwaogofya.

Ndege aina ya Concord huruka juu sana umbali wa futi 60,000 kutoka usawa wa bahari ikiwa ndio upeo wa juu zaidi wa anga.

Kwa kuruka urefu huo ambao ni mara mbili ya urefu unaoruka ndege aina ya Jumbo, ndege za Concord huwa ziko umbali wa maili 300 tu kutoka mwisho wa upeo wa macho wa mbingu.

Mpaka sasa ni ndege 20 za aina ya Concord zilizoundwa, nusu zikiwa zimeundwa Uingereza na nyingine zilizobaki zimeundwa huko Ufaransa.

Kutokana na ukubwa wa injini yake, ndege aina ya Concord imekuwa na mngurumo mkubwa sana na ndiyo sababu imekuwa ikiruka anga za juu na pia viwanja vyake vingi vipo mbali na miji.

 Kipofu ajishona majeraha kichwani

lNi mzee mwenye umri wa miaka 83

KIPOFU mmoja mzee wa miaka 83 huko Uingereza, hivi karibuni ajilishona majeraha yake yaliyoko kichwani, na hivyo tukio hilo lisilo la kawaida kuingia katika safu hii ya 'Yasiyo ya Kawaida'.

Akionekana mchangamfu na muongeaji anayechekesha mzee huyo Charle Tomlinson ameonekana ni mtu mwenye bahati ya pekee hapa duniani.

Hivi sasa mzee huyo kipofu amekuwa maarufu sana Uingereza kutokana na kuandikwa na kuzungumziwa sana katika vyombo vya habari vya huko kutokana na tukio hilo alilolifanya, kama ilivyoripotiwa na jarida la "Character".

Akiwa ni mzee kipofu, na mtu asiyejiweza kiuchumi, Tomlinson alikuwa ni mtu anayeishi kwa kutegemea misaada ya ndugu, jamaa na marafiki pamoja na kuutimia ujuzi wake kwa kuongea na kuchekesha ili kujipatia mkate wake wa kila siku.

Pamoja na kujipatia riziki yake kwa njia hiyo, bado mzee Tomlinson ni miongoni mwa wazee wanaofaidika na mpango wa nchi ya Uingiereza wa kuwahifadhi wazee wenye umri mkubwa kama huo.

Tomlinson akiwa katika umri huo wa miaka 83 bado ana uwezo wa kutembea, kufanya mazoezi magumu na mambo mengine mengi ambayo si rahisi kwa wazee wenye umri kama wake kufanya.

Mzee huyo aliweza kufanya kila ambacho kinaonekana ni jambo lisilo la kawaida pale alipoweza kujishona majeraha nane ya mipasuko kichwani huku akiwa kipofu bila msaada wa mtu yeyote, na jambo la kushangaza ni kwamba kazi hiyo aliifanya usiku.

Tomlinson alikumbana na mkasa huo siku moja usiku wakati akitokea katika matembezi yake ya kawaida alikuwa akirudi nyumbani kwake kwa ajili ya mapumziko.

Siku hiyo ilikuwa siku mbaya kwake kwani katika kutembea kwa bahati mbaya alikutana na genge la vijana wahuni ambao walikuwa wamekwisha vuta bangi na hivyo kumshambulia mzee Tomlinson.

Vijana hao wahuni waliokuwa tisa walimkamata mzee huyo wakampiga sana kwa kutumia nondo na kisha wakamfunga kamba na kuanza kumpekua wakifikiri alikuwa na fedha nyingi, lakini alikuwa ni tofauti na mitazamo yao kwani waliambualia pauni 1 na senti 89 (sawa na shilingi 2,000) mifukoni mwake.

Baada ya vijana hao kukosa kile walichotarajia kwa mzee huyo, waliamua kumalizia hasira zao kwa kumpiga hadi kupoteza fahamu ndipo nao wakaondoka wakimuacha mzee huyo mahututi.

Muda mufupi baada ya vijana hao kuondoka, Tomlinson alipata fahamu kutokana na kupigwa na baridi kali. Akiwa abado anauja damu alijikokota hadi nyumbani kwake ambako alijiosha damu iliyokuwa imeganda na baada ya hapo alijinyoa kwa kutumia wembe sehemu zilizokuwa zimejeruhiwa.

Mzee huyo akiwa anatetemeka kwa baridi kali aifanikiwa kuchukua sindano ya kushonea ngozi na kujishona majereha yote kwa ujuzi mkubwa bila hata ya msaada wa mtu mwingine.

Baada ya kumaliza kujishona mzee huyo jasiri aliyafunga majereha hayo kwa vitambaa laini na kujipumzisha usiku huo kabla ya kwenda hospitalini siku iliyofuata.

Tomlinson alipofika hospitalini na kuonekana katika hali ile, wauguzi waliompokea kwanza walianza kulia kwa sauti ya juu kana kwamba ni baba yao mzazi jambo lililowafanya wagonjwa wengine nao washangae na wengine kutoa machozi.

Alipelekwa kwa amadaktari ambao nao walishikwa mshangao kwa kumuona akiwa katika hali hiyo na wakastaajabishwa sana na jinsi alivyoweza kujishona majeraha tena na kichwani huku akiwa ni kipofu na akaweza kuishi masaa 48 baada ya kufanya kitendo hicho.

Wakihofia kwamba huenda maisha yake yanaweza kuwa hatarini, madaktari walimfanyia uchunguz wa kina katika kichwa chake na kushangazwa zaidi pale walipoona kwamba hakuna chochote kilichokuwa kimeathirika katika ubongo wake.

Madaktari hao wakitumia utaalamu wao walimfumua nyuzi zote alizokuwa amesitumia kujishona na kumshona upya kwa utaalamu mkubwa na kuruhusu kurudi nyumbani kwake. Jambo lililofuatia baada ya mzee huyo kipofu kupona ni kuwasaka wabaya wake waliomfanyia uhuni. Walipatikana sita, na watatu hadi sasa bado wanatafutwa na polisi.

Askofu aeleza namna kanisa linavyowasaidia Wakimbizi

KUTOKANA na hali ya mapigano yanayoendelea nchi ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo ,Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi mbalimbali kutoka katika nchi hizo mbili ambapo wanahifadhiwa katika makambi mbalimbali ya wakimbizi yaliyopo mkoani Kigoma,mkoa ambao upo mpakani mwa nchi hizo. Kutokana na hali hiyo Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma limekuwa likijishirikisha kikamilifu katika kuhifadhi na kutoa huduma mbalimbali kwa wakimbizi hao kama Askofu wa Jimbo hilo,PAUL RUZOKA na Mjumbe wa Kamati ya Huduma kwa Wakimbizi iliyo chini ya Kanisa Katoliki Steven Menshi, walivyomueleza Mwandishi Wetu DALPHINA RUBYEMA hivi karibuni katika mazungumzo maalum jijini.

"Mkoa wa Kigoma umekuwa ukipokea wakimbizi kati ya 300-400 kwa siku kutoka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo na wale wa kutoka nchini Burundi ni kati ya watu 100-200 kwa siku"anabainisha Askofu Ruzoka.

Anasema kuwa Jimbo lake limekuwa likiishi na wakimbizi kutoka nchini Burundi tangu mwaka 1993 na hadi hivi sasa jimbo hilo kama Kanisa limehifadhi jumla ya wakimbizi 300,000 kutoka katika nchi zote mbili yaani Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Congo.

Askofu Ruzoka anaongeza kuwa mbali na kuhifadhi wakimbizi hao, kanisa pia kwa kupitia idara yake ya CARITAS tawi la Kigoma limekuwa likishirikiana na kitengo cha kuhudumia wakimbizi cha Umoja wa Mataifa (UNHCR) na Kamati ya Kimataifa ya Kuhudumia Wakimbizi (IRC) katika kutoa huduma mbalimbali ikiwemo ya chakula na mavazi.

Alisema kuwa CARITAS hutoa huduma za awali kwa wakimbizi ambao bado wanakuwa hawajapangiwa kambi za kukaa na huduma hii hutolewa katika vijiji wanapoingilia wakimbizi hao ambavyo alivitaja kuwa ni Yelushingo, Kigadia, Itaba, Nganzo, Msanga na Nyakimono.

"Kanisa pia linatoa huduma ya usafiri kwa kuwapeleka wakimbizi wasiojiweza kwenye kambi wanazokuwa wamepangiwa." anasema Askofu Ruzoka na kuongeza,"Magari ya kanisa yanatumika kuwabeba wakimbizi wale wanaokuwa hawana nguvu za kutembea hadi kufika kwenye kambi wanayokuwa wamepangiwa. Kwa wale wenye nguvu zao wanatembea wenyewe kwa miguu" .

Kwa upande wa huduma za kiroho, Askofu Ruzoka anasema, "Kanisa haliwaachi ndugu zetu wakimbizi waangamie kiimani bali pia liko mstari wa mbele katika kuwahudumia kiroho. Linajihusisha sana maana mapadri,watawa na walei huwafuata wakimbizi makambini kwao na kuwapa huduma huko huko."

Ruzoka anazidi kufafanua kwa mfano kuwa katika kambi ya Kenembwa iliyopo Wilayani Kibondo kuna mapadri wanaotoa huduma za kiroho pamoja na Kambi za Matendeli, Manduta na Mkubwa. Kwa upande wa Wilaya ya Kasulu , Mapadri wa Shirika la Moyo Mtakatifu wanatoa huduma ya kiroho katika makambi ya Namtabila A, Mirosa na Namtabila B.

"Pia kuna Padri mmoja ambaye ni Mratibu wa shughuli za huduma za kiroho kwa wakimbizi anayetoa huduma hiyo kwenye kambi ya Rugufi, kambi inayohifadhi wakimbizi wanaotoka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo"alisema Askofu Ruzoka.

Aliongeza kusema kuwa mapadri wakimbizi wanaohifadhiwa kwenye kambi ya Nyarugusu nao pia wanashirikiana na parokia ya Makele ambayo ipo jirani na kambi hiyo,kutoa hudhuma za kiroho.

Pamoja na yote hayo, Askofu Ruzoka anasema kanisa linajishughulisha kutoa huduma ya mazishi kwa wakimbizi ambao wanamaliza muda wao kuishi duniani ambapo miili yao hupumzishwa kwenye mashamba yaliyotengwa rasmi kwa ajili ya shughuli hiyo.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Kanisa inayotoa huduma kwa wakimbizi, Bw.Steven Menshi anasema kuwa hivi sasa baadhi ya wakimbizi wanaoingia mkoani humo ni majeruhi au walemavu kutokana kukanyaga mabomu ya ardhini wengi wakiwa wamekatika miguu na mikono.

Bw. Menshi ambaye ni Mzaliwa wa Kijiji cha Kagunga Wilayani Kigoma Vijijini, anasema kuwa kijiji hicho chini ya Kanisa Katoliki kimeunda kamati ya kutoa huduma kwa wakimbizi wanaoingia mkoani humo.

Kamati hiyo iliyoundwa mwaka 1996, ina wajumbe 13 wanaofanya kazi ya kujitolea kwa muda wa masaa 24 ambapo yeye ni miongoni mwa wanakamati hao.

Akielezea jinsi kamati hiyo inavyofanya kazi, Bw.Steven anasema kuwa wakimbizi kutoka pande zote mbili wakishaingia mkoani humo kabla hawajapangiwa kambi, kamati inawajibika kutoa taarifa kwa Kitengo cha Umoja wa Mataifa cha Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR) kupitia kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji.

Menshi anasema, "Baada ya hapo UNHCR inatumia boti inayoitwa KU 458 ya Parokia ya Kagunga kwa ajili ya kubebea wakimbizi hao ambao wengi wao ni akina mama na watoto."

Anazidi kufafanua kuwa parokia hiyo imepewa zabuni ya kusafirisha wakimbizi na kuwapeleka kwenye kambi wanazokuwa wamepangiwa na imepewa "tenda" hiyo tangu Aprili Mosi mwaka jana.

Bw. Steven anabainisha kuwa wakimbizi kutoka nchi ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo ambao idadi yao ni kati ya 300-400 kwa siku wanaingia mkoani Kigoma kwa kupitia vijiji vilivyopo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Alivitaja baadhi ya vijiji hivyo kuwa ni pamoja na Karago,Sunuka, Kilando,Mkuyu, Sigunga, Elembe, Muhingu, Kalia, Mtanga, Mwamgongo, Zasha na Kagunga

.Anaongeza kusema kuwa baada ya wakimbizi hao kupangiwa kambi za kukaa ambazo ni Rugufu na Mtembeli ,kamati hiyo huchangisha pesa kwa Wakristo na watu wenye mapenzi mema ,pesa ambayo hutumika kuwanunulia wakimbizi hao chakula pamoja na huduma nyingine ikiwemo nishati na matibabu na wanatoa wito kwa vikundi mbaalimbali vya dini na watu wengine kujitoa zaidi ili kuchangia huduma za ndugu zetu hao wakimbizi.

Mtakatifu Catherine wa Ujerumani

lAlitoroka nyumbani kwao Uyahudini na kwenda kuomba ubatizo kwa Mkristo

MTAKATIFU Catherine wa Parc - aux - Dames alikuwa ni mwanamke toka familia ya wazazi Wayahudi waliokuwa wakiishi katika mji wa Louvain, Ujerumani.

Wakati wa maisha yake miongoni mwa watu mashuhuri waliokuwa wakimtembelea mara kwa mara nyumbani kwake ni Gavana wa Brabant na Rayner Mkuu wa ambao walitumia muda wa ziara zao hizo kujifunza mambo ya dini.

Catherine kama Mtakatifu hukumbukwa na kuheshimiwa na Wakristo wa madhehebu mbalimbali duniani yakiwemo yale ya Kikatoliki, Kianglikana na Kiorthodox.

Wakatoliki humkumbuka Mtakatifu huyu kila mwaka ifikapo Mei 4, pamoja na watakatifu wengine kama Monica wa Tunisia, Judas Quiriacus, Helena wa Ugiriki, Florian wa Austria, Venerius wa Italia, Godehard wa Ujerumani na Michael wa Lithuania.

Mtakatifu Catherine ambaye habari za maisha yake zinaeleza kwamba alikuwa bikira, alizaliwa mwanzoni mwa karne ya kumi na tatu.

Alipokuwa mdogo wa umri wa miaka mitano Catherine alikuwa akiitwa Rachel jina ambalo baadae aliliacha kufuatia ubatizo wake.

Rachel alipokuwa na umri wa miaka mitano siku moja Rayner Mkuu alipomtembelea aliwahi kumuuliza, "Rachel unapendelea kuwa Mkristo?", naye alijibu "Ndiyo - iwapo utanieleza ni vipi niwe hivyo".

Kuanzia hapo Rayner alianza kumpa Rachel mafundisho na maelezo mbalimbali juu ya mafundisho ya Ukristo.

Lakini wazazi wa Rachel hawakupendezewa na mafundisho hayo yaliiyoanza kumbadili imani yao ya Uyahudi binti wao, hivyo Rachel alipotimiza umri wa miaka saba wazazi hao walimpeleka mbali na eneo hilo katika mji mmoja ng'ambo ya mto Rhine.

Hata hivyo katika wakati huo tayari Rachel alikuwa ameanza kuingiwa vya kutosha na kuikubali imani ya Kikristo, na inasemekana usiku mmoja alitokewa na Bikira Maria ambaye alimuangazia na kumuonyesha njia ya kuelekea mahala pa ubatizo.

Kufuatia tukio hilo mara moja binti huyo alikatisha usingizi, akatoka nje ya nyumba kuelekea katika nyumba kuu ya watawa ya Parc - aux - Dames umbali wa maili moja na nusu kutoka mji wa Louvain.

Alipofika hapo binti huyo alibatizwa na kuvikwa mavazi ya kitawa na kupewa jina la Catherine, badala ya jina lake la awali Rachel.

Wazazi wake waliposikia habari hizo kwamba binti wao amebatizwa, walikasirika na kuwasilisha malalamiko yao kwa Askofu Mkuu wa Louvain, kwa Gavana wa Brabant na baadaye kwa Papa Honorius kwamba binti wao kisheria hastahili kuishi maisha ya nje ya familia yao hadi atakapotimiza umri wa miaka kumi na miwili.

Askofu Mkuu na Gavana waliyasikiliza malalamiko hayo, lakini yakapingwa na Engelbert aliyekuwa Askofu wa Cologne, na William aliyekuwa mkuu wa watawa wa Clairvaux.

Hivyo kuanzia hapo Catherine aliendelea kuishi kama Mtawa katika nyumba ya watawa huko Parc - aux - Dames hadi kifo chake,na alikuwa mashuhuri sana kutokana na mafundisho na kipawa chake cha ajabu.

Uwepo ukaguzi wa mara kwa mara shule za chekechea

VITUO vya kulelea watoto na shule za awali katika maandalizi ya kuanza shule za msingi ni muhimu na vinahimizwa vianzishwe, lakini vinapaswa kufuata utaratibu, sheria, na mazingira yanayofaa. JUSTIN MWEREKE anaeleza zaidi katika makala hii kuhusu mwelekeo wa vituo hivyo sasa

Vituo vya Chekechea na shule za awali za kuwaandaa watoto wadogo kuanza shule za msingi vikianzishwa na kuendeshwa holela kama miradi tu ya kujikimu kutokana na ugumu wa maisha, upo uwezekano mkubwa wa kupotosha maana, malengo na madhumuni yake kwa manufaa ya watoto na taifa.

Hivi sasa vimeibuka vituo vingi vya Chekechea na shule za awali katika karibu kila pembe ya mtaa hapa jijini Dar es Salaam.

Pamoja na nia yao nzuri, wamiliki wa vituo hivyo hawafuati sheria, taratibu, mazingira au masharti yanayotakiwa.

Utafiti uliofanywa na Chama cha Wazazi cha Kuendeleza Wanafunzi nchini (PASO) katika vituo hivyo wilayani Temeke, Jijini Dar es Salaam ulionyesha kuwa vituo vingi havijasajiliwa, havina wasimamizi au walimu wenye taaluma zinazohusika na vinaendeshwa kwenye mazingira yasiyofaa kama vile kwenye baa, nyumba za kuishi na chini ya miti.

Baadhi ya vituo vya kulelea watoto, havifundishi mambo kwa namna na kwa utaratibu unaofaa watoto hao kulingana na uwezo wao wa akili.

Watoto wadogo chini ya miaka mitano kuwafundisha hisabati badala ya michezo ni kuwapa mzigo usiolingana na uwezo wao wa akili. Mwenyekiti wa Chama hicho chenye makao yake makuu Jijini, Dar es Salaam Bw. Malkiadi Wityenyi alisema PASO ilibaini hali hiyo na kuona umuhimu wa kuwaelimisha wamiliki na wasimamizi wa vituo hivyo kwa njia ya semina ili waweze kuviendesha kwa njia inayoweza kukubalika.

Alisema vituo na shule hizo ni mahali pa kumwandaa na kumpa mtoto malezi bora na maadili mema ambayo atapaswa akue nayo hadi kufikia utu uzima,hivyo ni lazima vimjenge mtoto ili aweze kumudu vema masomo hapo anapoanza shule ya msingi.

"Lakini kama vituo hivyo vikiendeshwa kama miradi tu ya kujipatia fedha, malengo yake hayatafikiwa", Bw. Wityenyi alisema.

Wakichangia mada juu ya "Wajibu wa wamiliki wa vituo vya kulelea watoto" kwenye semina ya wamiliki na wasimamizi wa vituo hivyo iliyofanyika katika Kituo cha Walimu cha Wailes, Temeke wanasemina walishutumu kuwa watendaji katika Idara ya Ustawi wa Jamii ndio wanaokwamisha usajili wa vituo vyao kwa sababu ya urasimu.

Walidai kuwa wanapenda na wanatambua umuhimu wa kusajili vituo hivyo, lakini wanapoenda Idara ya Ustawi wa Jamii husumbuliwa kwa lugha ya "njoo kesho, njoo kesho" jambo ambalo walidai linawakatisha tamaa. Mmiliki wa kituo cha Upendo Day Care Centre kilichoko kwenye viwanja vya Maonyesho ya Kimataifa (Saba-Saba) Jijini, Bibi Joyce Malilae alidai kuwa amefuatilia kwa karibu zaidi usajili wa kituo chake tangu mwaka 1996 hadi sasa lakini bila mafanikio. Wanasemina pia waliomba kipengele au sifa ya kuwa na hati miliki ya mahali panapoendeshwa kituo wakati wa usajili isitiliwe maanani sana kutokana na ugumu wa kupata hati miliki haraka kutoka Wizara ya Ardhi. Afisa Msaidizi wa Ustawi wa jamii wa Wilaya ya Temeke, Bw. David Mganga alisema katika mada hiyo kuwa kituo chochote cha kulelea watoto sharti kiwe na sifa zinazotakiwa ambapo ni mahali, majengo mazuri, mazingira mazuri, hati miliki na hati ya usajili.

Pia mmiliki au msimamizi anapaswa awe na taaluma ya malezi, mtu mzima na mwenye akili timamu, na uwezo wa fedha kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa watoto. Bwana Mganga alikiri kuwepo kwa urasimu mkubwa katika Idara ya Ustawi wa jamii, lakini, aliwataka wamilikaji kutokukata tamaa kufuatilia hadi kupata usajili hadi hapo tatizo hilo litakapoondolewa.

Hata hivyo, kimsingi kuna matatizo mengi katika vituo vya kulelea watoto (Chekechea) na njia pekee ni Serikali kuchukua hatua za kuvichuja vituo hivyo sambamba na kuondoa urasimu uliopo katika usajili wa vituo hivyo. Kadhalika hapana budi ufanyike ukaguzi kuhakikisha kwamba walimu wenye uwezo na fani zinazohusiana na malezi ndio wanaoruhusiwa kufundisha katika vituo hivyo.

Jenga utamaduni wa uhai (2)

KATIKA matoleo yetu ya April 25 na Mei 2 tuliwaletea makala kuhusu "UTAMADUNI WA KIFO". Humo ilielezwa kwamba Utamaduni wa kifo ni tabia ya watu wanaoamini kuwa wanadamu kadhaa wanaweza kunyimwa haki yao ya kuishi ili wachache waweze kufurahia maisha peke yao. Vitendo kama utoaji mimba na mambo mengine yanayoharibu au kupunguza uhai pia yalitajwa. Katika toleo lililopita , ili kuleta mlinganyo EMIL HAGAMU wa Chama Kutetea Uhai (Pro-Life Tanzania akaelezea juu ya "Utamaduni wa Uhai" Endelea na sehemu ya pili ya makala hiyo.

Mtumiaji wa kondomu hujengewa ulofa wa kinga bandia. Matumizi makubwa ya kondomu hueleza kiwango cha kuporomoka kwa maadili ya taifa. Taifa linalohimiza matumizi makubwa ya kondomu ni taifa lililofilisika kidhamiri.

12. MAENDELEO

Utamaduni wa uhai huamini kuwa binadamu ndiye chanzo na lengo la maendeleo. Maendeleo ni nyenzo anayotumia binadamu kwa ajili ya kujiletea manufaa katika maisha yake. Serikali za kimataifa zijenge mazingira mazuri kwa watu kujiletea maendeleo. Licha ya mali nyingi tulizo nazo hapa Tanzania, watu wake bado ni maskini; huduma za afya ni duni, huduma katika utoaji elimu ni mbaya, maji watumiayo wananchi wengi sio salama, barabara zetu nyingi ni mbovu. Umaskini wetu unaelezeka katika vigezo hivyo. Utamaduni wa uhai unaamini kuwa ufumbuzi wa matatizo hayo sio kuwapa watu madawa ya uzazi wa mpango, au kondomu, au kujenga vituo vya kutolea mimba, bali kuwajengea wananchi mazingira bora ya kupata huduma hizo. Wanachohitaji wanafunzi mashuleni ni mazingira ya upatikanaji wa elimu bora sio huduma za afya ya uzazi wala uamuzi binafsi juu ya maisha ya vijana wetu.

Wanachohitaji wakina mama waja-wazito ni huduma za kiafya kabla ya kuzaa na baada ya kuzaa sio, vidonge vya majira, sindano ya depo, vipandikizi au vitanzi. Maendeleo ya kweli humheshimu binadamu sio kumdhalilisha.

13. HITIMISHO:

Utamaduni wa uhai ni hali ya kupenda, kuthamini, kulinda, kutetea na kuendeleza uhai wa binadamu, afya ya binadamu, utu wake na heshima yake. Utamaduni wa uhai humwona na kumjali kila binadamu kama ndugu. Utamaduni huheshimu na kuzilinda ndoa na familia na kuzijengea mazingira mazuri ya kuwepo kwake. Maelekeo yoyote yale, au hali yoyote ilie inayolenga katika kulinda maadili mema ya vijana wetu, huyo ni mtu wa utamaduni wa uhai. Ndoa katika mtazamo wa utamaduni wa uhai ni kitu kitakatifu na watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Watu wa utamaduni wa uhai husali ili kuliombea taifa lienende katika njia sahihi.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

Dini za jadi

Kabla ya kutapaa kwa Ukristo, Uislamu na dini nyingi tulizo nazo leo hii, watu waliamini mambo mbali mbali na kuyawekea tumaini lao la kiroho na kuamini baadhi ya vitu vikiwemo milima, mito na kadhalika kama miungu yao.

Katika kufanya hivyo baadhi ya watu pia walikumbuka au hukumbuka roho za baba na babu zao waliokufa katika ukoo wao. Hao hutolewa sadaka kama vile pombe au wanyama

Wakati mwingine katika tambiko hizo za kimiungu , pengine ngoma hupigwa pamoja na maombi kutolewa kwa miungu hiyo. Makala ya leo inagusia kidogo juu ya baadhi ya imani za jadi.

Katika imani hizo za jadi huaminiwa kwamba wale wazee waliokufa huendelea kuishi huko ahera na mahusiano baina yao na wazazi vya ukoo wao huendelea kama kawaida.

Hata baada ya kufa kwao hudhaniwa kwamba wana nguvu zaidi na wanaweza kuwabariki watu wao duniani au kuwadhuru na kuwaadhibu wakitenda mabaya , hasa wakiwasahau marehemu wao.

Katika imani ya zamani ya dini ya Mizimu huaminiwa kama waaminivyo Wakristo wengi kuwa roho za marehemu huendelea kuwa na uzima hata baada ya kufa miili.

Aidha, katika imani hizo pia wazee waliokufa wanakuwa ni washenga ambao walipoishi duniani waliwapa wana wa ukoo wao uzima ule unaotoka kwa Mungu, na sasa wakiwa marehemnu shukrani na heshima ya wana lazima iwafikie , kwani sasa wanazidi kuwa walinzi au wawakilishi wao kwa Mungu.

Hapo pia huonekana vilevile kuwa ushirika wa ukoo na kabila kuwa na nguvu na maana hata baada ya kufa babu zao.

Hata hivyo katika imani hizo za kijadi au koo nyingi za Afrika zilikuwa zikiamini Mungu mmoja , lakini akijulikana kwa njia na majina mbalimbali.

Baadhi ya Wafuasi wa dini za mizimu waliamini kwamba kuna Mungu Muumba Mtoa uzima , Mleta Mvua , Aliye tangu Mwanzo, Asiyeshindwa, Mwenye Hekima , Baba wa watoto wachanga.

Kwa mfano huko Rumi miaka mingi iliyopita watu walikuwa na utamaduni wa kutupa sarafu za pesa kwenye mto wakiamini kwamba kwa kufanya hivyo walikuwa wanavuta bahati njema.

Wageni wengi walienda kuhiji huko katika chemchemi ya Trevi (Trevi Fountain) iliyoko Rumi. Huko Shiraz, Iran kwa upande mwingine Waajemi walikuwa na utamaduni wa namna hiyo. Sababu ya watu kutupa sarafu katika mito inatoka mbali sana ambapo watu walisadiki kuwa roho ziliishi katika vilindi vya maji ya chemchemi. Hivyo basi sehemu zote zenye chemchemi za maji ziliheshabiwa kuwa za kiungu na takatifu.

Watu waliamini kuwa kama wasingetoa sadaka zao katika chemchemi hizo za maji basi roho ziishizo humo zingewapatiliza kwa adhabu za kukumbwa na mikosi na kila bahati mbaya.

Wakati mwingine baadhi ya waumini wa dini hizo za kimizimu wenye itikadi kali walifikia mahali pa kutoa vitu walivyovipenda kuliko vyote ambapo walifikia hata kuitoa nyama za miili yao wenyewe au damu zao.

Kuwatoa kafara watu wazimawazima pia ni moja ya sadaka "bora" zaidi zilizotolewa. Hili linatihibitishwa na kisa kimoja cha kuhuzunisha kilichotokana na uvumbuzi katika uitwao "Mto wa kafara" huko Chichen Itza, nchini Mexico. Wasichana wadogo wa kabila la Mayan walikuwa wakitolewa sadaka kwa kutupwa mtoni kwa hiyari yao wenyewe ili kuziletea familia zao bahati njema. Cha kushangaza ni kwamba hatua hiyo badala ya kulaaniwa na wasichana hao, wenyewe waliichukulia kuwa ni bahati ya kipekee. Walifurahi wakiamini kuwa huko katika kilindi cha maji ya kisima mungu aliyeishi humo ambaye aliaminiwa kuwa ni mungu wa mvua katika kutambua ujasiri wao wa kujitoa sadaka angewaoa na wangeishi kwa raha mustarehe huko kilindini wakiwa malkia wa mungu huyo.

Kutoka huko ndipo ustaarabu ukaongezeka hadi kufikia hapo ambapo watu hutoa fedha za sarafu kwa nia ya kununua bahati njema kwa kuzitupa kwenye chemchemi za maji.

Kule Upareni katika maeneo ya Ugweno wilayani Mwanga wahenga walipotaka kuomba mvua walisanyana wazee kadhaa, wakamchukua mbuzi na kumtupa ndani ya Bwawa la Chunguli baada ya matambiko ambayo pia uhusisha pombe aina ya dengelua na inaelezwa kuwa kama mbuzi huyo angezama moja kwa moja basi, miungu imekataa sadaka hivyo mvua haitakuwepo na watu watakumbwa na njaa. Lakini iwapo mbuzi huyo angeibuka baada ya kuzama na kujikung'uta maji yakaruka kutoka mwilini mwake, basi huo ulikuwa ushahidi tosha wa kupokelewa kwa sadaka na neema kubwa ya mvua na chakula kingi ingefuata.