Wakatoliki huabudu sanamu?

Katika Amri Kumi za Mungu, BWANA Mungu wetu ametuonya tusichonge sanamu na kuzifananisha na chochote kilicho mbinguni, wala duniani. Je, mbona Wakatoliki hupenda sana sanamu. Sio kuziabudu?

Elias Joseph wa SLP 304, Songea: Anauliza!

Swali la kwanza limeulizwa kutokana na kifungu cha kitabu cha Kutoka 20:1-17, Ili tuweze kulielewa vema swali hilo ni vyema tusome sehemu hiyo ya maandiko hayo Matakatifu: "Mungu akanena maneno hayo yote akasema mimi ni Bwana Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri katika nyumba ya utumwa, usiwe na miungi ila mimi, usijifanyie sanamu ya kuchonga wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

Usivisujudie wala kuvitumikia kwa kuwa mimi Bwana Mungu wako maovu ya Baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao. Nami nawarehemu maelefu, elfu wanipendao na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako maana Bwana hatamuhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure, ukumbuke siku ya Sabato uitakase, siku sita fanya kazi utende mambo yako yote lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyte, wewe wala mwana wako wala binti yako, wala mtumwa wako wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, maana kwa siku sita Bwana lifanya mbingu na nchi na habari na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba. Kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya sabato, akaitakasa. Waheshimu baba yako na mama yako siku zako zipate kuwa nyngi katika nchi upewayo na Bwana, usiuwe, usizini, usiibe, usimshuhudie jirani yako uwongo.

Usiitamanai nyumba ya jirani yako, usimtamani uke wa jirani yako. Wala utumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake wala chochote alichonacho jirani yako.

Kutokana na sehemu hiyo ya maandiko matakatifu ndugu Elias Joseph anauliza; baada ya kifungu hicho mbona amri kumi zimetimizwa na katika kutufundisha haifanani. Ni kuwa sababu gani? Ndugu Elias umepigwa na mshangao, kwa kweli mshangao wako ni nusu mshangao, laiti ungelisoma tena orodha ya amri hizo iliyomo kwenye kitabu cha kumbukumbu la torati 5: 6-12, na halafu ungesoma orodha anayotoa Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya Marko 10: 19-20 pale alipomwuliza yule tajiri kama anazijua amri ungelishangaa kwa mshango kamili mtarafu tofauti wa mpangilio wa amri kumi za Mungu. msigano wa mpangilio wa amri za Mungu Ndugu Elias, unasababishwa na jambo moja kubwa, kwamba Biblia yenyewe haikupatia amri hizo katika mpangilio wa namna moja, mbili, tatu, nne, tano, sita, saba, nane, tisa na kumi. Hat Musa hakuzipa hizo namba mpaka hiyo namba kumi tuliyo nayo sisi.

Mpangilio wa kinambari halikuwa swala kati ya wayahudi wenyewe, ndiyo kisa Musa mwenyewe analiita amri hizo kumi kwa mtindo mwingine kwenye hotuba yake inayosomeka katika Kitabu cha Kumbukumbu la torati 5:6-21. Jambo kubwa kwa Wayahudi wakati huo lilikuwa ni kuzielewa na kuzishika" Ya kwanza kati ya hizo kumi au ya mwisho ni ipi halikuwa jambo la kupotezea usingizi kama sisi tusumbukavyo na kupoteza usingizi wetu. Jambo kuu ninarudia, lilikuwa ni kuzielewa na kuzishika. Kwa sababu ya kutotilia sana maanani mpangilio wa kinambari hata yesu katika Injili ya Marko 10: 19-20 anazitaja kwa mpangilio wa aina yake. Aya hiyo inasema, Wazijua amri, usiuwe, usizini, usiibe, usishuhudie uwongo, usidanganya, waheshimu baba yako na mama yako, ndugu Elias unaona mpangilio wa ajabu, ubali na kitabu cha kutoka 20: 1-17? Sasa ndugu Eliasi, sisi binadmau tuliozipokea amri na hasa sisi tunaoishi miaka mingi mbali na akina Mussa na Yesu, sisi tunaoishi katika karne hii, ndio tulioshikwa na hari ya kutaka kuzishika amri hizo kinambari, ili tupate pia kuwafundisha wenzetu, basi ndio chanzo cha utoaji wa namba kwa amri za Mungu. Yaani tumetaka kuzipanga kimuhtasari zipate kushikika kirahisi, Ndugu Eliasi harakati hizo zote za kupanga kinambari na kuweka muhtasari zilitegemea jinsi binadamu walivyozielewa wenyewe. Ndipo ilipozuka mipangilio mbali mbali. Shida ya awali ilihusu ipi ni amri ya kwanza na shida ya mwisho ilikuwa ni ipi ni amri ya kumi na upana wake inakomea wapi. Juu ya amri ya kwanza wakatokea baadhi ya watu walioona kwamba ni msitari wa kwanza hadi msitari wa sita sura hiyo ya 20 ya kitabu cha kutoka, ni utangulizi tu wa amri hizo za Mungu, hivyo bas mistari yote hiyo iwe ni amri moja tu, kwa muhtasari usiwe na miungu mingine. Ila mimi au usiabudu miungu wengine ila mimi. Hao ndio waliokwenda kwenye mstari wa saba kwa ajili amri ya pili ndiyo usilitaje bure jina la Mungu wako.

Huo ulikuwa msimamo mmoja. Msimamo mwingine ulikuwa mintaarafu amri hiyo ya mwanzoni ni ya wale walioona kwamba haya ya 3 inaweza kuwa amri ya pekee yaani usiwe au siabudu Miungu mingine na mstari au haya ya nne inaweza kuwa amri nyingine ndiyo ya pili kwao yaani usijifanyie sanamu ya kuchonga. Na baada ya hapo haya ya saba ikawa kwao amri ya tatu, usilitaje bure jina la Mungu wako, hivyo amri ya kushika sabato ndiyo kushika kitakatifu ikawa kwa watu wa kundi hili la pili amri ya nne.

Na amri ya kuwaheshimu Baba na Mama ama wazazi ikawa kwa watu hawa wa kundi la pili hili amri ya tano, na kuendelea. Nadhani umeelewa mkasa huu. Sasa tuhamie kwenye mkasa wa wapi amri zikomee, hapo hapo kumetokea misimamo miwili, wapo wanaovunja maswala yote ya kutamani, wakawa na amri ya tisa yaani dhidi ya kutamani mke asiye wako na amri ya kumi ikawa dhidi ya kutamani vitu vinginevyo alivyonacho mtu, mwingine licha ya mke wake, huo ni msimamo nambari moja.

msimamo mwingine wa pili ni wa wale wanaoona kwamba mambo yote hayo ya kutamani yawekwe kwenye amri moja tu, nayo ndiyo ya kumi yaani usitamani mke, wala nyumba ya mtu, wala kitu kingine chochote kisicho chako. Ndugu Elias hayo yote yalihusu shida ya mpangilio wa kinambari. Kwa vile Biblia yenyewe haipangi amri kinambari, basi binadamu waliojaribu kuzipanga kinambari kwa bahati mbaya wanatofautiana namna ya kuzihesabu hasa amri ya kwanza na ile amri ya mwisho, (ya tisa au ya kumi).

Sasa, juu ya kutimizwa, ni ukweli wa kibiblia kwamba amri kama amri zinatolewa kwa uweleo rahisi zilikuwa zikieleweka bila matatizo kwa Wayahudi, lakini amri hizo kabla hazijaingizwa katika maandishi ya Biblia, hapo zamani zilielezwa kwa mazungumzo na mdomo tu. Na wakati huo zilikuwa zikipata maelezo fulani fulani kukailiana na wale waliokuwa wakitafuta mianaya ya kuzivunja.

Chukua mfano wa amri ile ya kushuka siku ya kupumzika yaani siku ya ?Sabato: Nyongeza zilizopatikana ni pamoja na hiyo ya kuwataja ni akina nani wapumzike. Yaani wapo Wayahudi waliotaka kuivunja amri hiyo kiujanja: Walijisemea kuwa "tumekatazwa kutenda kazi sisi", Wayahudi basi bila shaka watumwa wanaeza kufanya kazi siku ya Sabato.

Basi hilo likasababisha nyongeza, usifanye kazi, wewe wala mtumwa aliyeko kwako. Na Nyongeza nyingine ikawa hata hao watumwa usibague jinsia siyo wa kike wala wa kiume, wote wapumzike siku ya sabato. na kisha hapo mwanya ukatafutwa, labda kwa kuwatumikisha wageni ama wanyama; na hiyo ikasababisha nyongeza nyingine kwa kutoa ufafanuzi kwamba hata wageni na wanyama wasifanyizwe kazi siku ya Sabato. Hivi ndugu Elias Biblia yenyewe inatuletea kwanza nyongeza hizo na hizo nyongeza huitwa Wigo wa amri.

Hivi basi kwa kuwa amri hizi zimetujia na wigo wake, inatumia kazi kubwa zaidi sisi tunaojaribu kuzipanga amri hizo kinambari halafu kujaribu pia kupata muhtasari kabambe wenye kushikika na waumini wote. Ninamalizia kwa kusema ugumu wa kuzipanga amri za Mungu, uliosababishwa na binadamu tulioishi baada ya Musa na Yesu, si rahisi kuutibu na wala hali ya kutimizwa kwa amri za Mungu kulikosababishwa na kutofautiana kuzielewa hizo amri na wigo zake nako siyo rahisi kufutika.

Lakini tukumbuke hapo mwanzo wa bistoria ndugu Elias wakati wa Musa mwenyewe na hata wakati wa Yesu, ambaye ni Bwana wetu mpangilio wa nambari za amri, halikuwa jambo la kukosea usingizi na kutokea machozi moyoni. Jambo la muhimu lilikuwa ni kuzielewa hizo amri na kuzishika na kila aliyezishika hakuwa mbali na ufalme wa Mungu. Sasa Ndugu Elias ni wakati wetu wa kurudi kwenye mambo hayo muhimu yaani kuzielewa na kuzishika amri hizo, bila kukosea usignizi, ipi ni ya kwanza au ipi ni ya pili au ipi ni ya mwisho.

Kudadisi sana mambo ya umbali si mbali sana na alama ya kutaka kutegea na kujaribu kushika zaidi baadhi ya amri na kuzikanyaga nyignine kimoyomoyo zile zitakazodhaniwa siyo za msingi. Ndugu tuzishike amri za Mungu kikamlifu, siyo kwa kuzitegea kijanjakijanja.

 Wimbo wa Mungu Ibariki

lSasa umetimiza karne moja

lAwali ulikuwa wimbo wa kanisani

lNi wimbo wa taifa wa Tanzania, Zambia, Afrika Kusini

" Mungu Ibariki Afrika" ni moja ya nyimbo mashuhuri na maarufu sana barani Afrika na duniani, ambao hivi sasa unatumiwa kama wimbo wa Taifa na mataifa mengi ya Afrika ikiwemo nchi yetu Tanzania.

Lakini watu wengi hujiuliza ni nani aliyeutunga wimbo huu wa "Mungu Ibariki", na inakuwaje wimbo huo umekuwa pia maarufu katika mataifa mengine ya Afrika kiasi cha kuutumia kama wimbo wa Taifa?

Wimbo huo chimbuko lake ni katika nchi ya Afrika Kusini ambako wenyewe huko kwa lugha ya Kizulu huuta "Nosi Sikelela I’ Afrika" na ambao kwa Kiswahili hapa kwetu Tanzania humaanisha "Mungu Ibariki Afrika".

Katika bara la Afrika wimbo huo bado hutumiwa kama wimbo wa taifa na nchi za Tanzania, Zambia na Afrika Kusini yenyewe, na wakati mmoja huko nyuma uliwahi pia kutumiwa kuwa wimbo wa taifa katika nchi za Ghana, Zimbabwe na Namibia mara zilipopata uhuru, lakini hivi sasa zimeacha kuutumia.

Mtunzi wa wimbo huo ni Enock Sentongo wa Afrika Kusini ambaye hivi sasa ni marehemu, na ambaye pia alikuwa mtunzi maarufu wa nyimbo nyingi za Kanisani.

Hata hivyo jambo ambalo hakujua mwenyewe wakati huo ni kwamba wimbo wake huo alioutunga akiwa kanisani ulioitwa "Nkosi Sikelela I’ Afrika" siku moja ungekuwa wimbowa kimataifa ambao ungepigwa na kuimbwa katika nchi nyingi duniani karne moja baadae.

Enock alitunga kifungu cha kwanza cha wimbo huo mwaka 1897 na baadae kidogo baada ya hapo mwaka 1902 mtunzi mwingine aliongezea vifungu kadhaa vya wimbo huo.

Wimbo huo unamuomba Mungu aibariki Afrika, viongozi, watu wake na heshima yake ijulikane ulimwenguni na pia ikimtaka Roho mtakatifu wa Mungu awashukie watoto wa Bara la Afrika.

Awali katika wimbo huo Enock alikuwa akimtaka Mungu awabariki watu na watoto wa Afrika kwa nia ya kwamba waweze kuvumilia mateso waliyokuwa wanayapata kutoka kwa Wazungu wakati wa utawala wa kikoloni.

Enock mwenyewe alikuwa ni Mkristo mcha Mungu na mwalimu wa shule kutoka kabila la Wakhusa ambalo pia anatokea Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Nelson Lohlahla Mandela.

Huko Afrika Kusini wimbo huo unajumuisha lugha za makabila matatu yakiwemo matatu ya Kiafrika yaani Kizulu, Kikhosa na Kisotho pamoja na kiingereza na Kiafrikana.

Jambo la kuzingatia ni kwamba wimbo huo ulikuwa ukiimbwa na wapinganaji wa chama cha African National Congress (ANC) kama wimbo wao wa taifa hata kabla chama hicho kuingia madarakani.

Wapiganaji hao wa ANC walikuwa wakiuimba wimbo huo wakati wa hekaheka za mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi ikiwa njia mojawapo ya kuwaimarisha na kuwahamasisha Waafrika.

Hata hivyo jambo la muhimu zaidi ni kwamba nchi nyingi za Kiafrika mare zilipopata uhuru kutoka kwa wakoloni nazo ziliuchukua wimbo huo na kuufanya kuwa wimbo wao wa taifa.

Nchi kama Tanzania na Zambia ambazo bado zinaendelea kuutumia wimbo huo tangu zilipopata uhuru, ziliyachukua hata maneno yaleyale na hata sauti za wimbo huo.

Enock ambaye aliutunga wimbo huo kwa vile alikuwa Mwafrika hana historia ndefu iliyoandikwa juu ya maisha yake licha ya kwamba alikuwa mwalimu na mtunzi wa nyimbo za kanisani.

Hii inatokana na zile siasa za kibaguzi zilizokuwepo huko Afrika Kusini.

Ni mwaka juzi tu ilipoamriwa na serikali ya Rais Mandela kwamba kaburi lake lisakwe na mnara wa kumbukumbu ujengwe mahali alipozikwa, ili iwe kama kumbukumbu kwa mtu ambaye katika miaka mia moja iliyopita alikuwa na ndoto ya kuiunganisha Afrika.

Baada ya muda mrefu wa kulitafuta hatimaye kaburi lake lilionekana, alikuwa amezikwa miongoni mwa makaburi ya Waafrika katika kitongoji cha Bromfontein mjini Johannesburg.

Kaburi lake lilikuwa limeandikwa "Kafir" neno ambalo lilikuwa likitumiwa na Wazungu kuwadharau Waafrika, pamoja na jina lake la kwanza tu Enock, na wala hapakuwa na dalili zozote kuonyesha kwamba aliyekuwa amelala hapo alikuwa mtunzi Enock Sentonga wa wimbo maarufu wa "Mungu Ibariki Afrika".

Mali na kujengwa mnara wa kumbukumbu katika kaburi lake, pia makaburi yote ya Blomfontein ambayo ni makubwa na yenye kuwatenganisha Wazungu kwa upande mmoja na Waafrika kwa upande mwingine, sasa yapewe jina la Enock Sentonga.

Jina la barabara moja kuu inayopita upande mmoja wa makaburi hayo nayo sasa inaitwa Enock Sentonga kwa kumbukumbu na heshima yake mtunzi huyo.

Enock alikuwa akiwa mtu wa kawaida tu, lakini atashangaa sana iwapo leo hii ataamka kutoka kaburini baada ya miaka mia moja na kuona jinsi wimbo wake ulivyotanda katika eneo kubwa kiasi hicho na heshima kubwa inayotolewa wakati wimbo huo aliotunga unavyopigwa duniani kote.

 Watoto wenye sura za kizee

Wote wanatoka katika familia moja

Duniani kuna mambo mengi yasiyo ya kawaida ambayo kama mtu mwenye tabia ya kudadisi kila kitu anaweza akaandika zaidi ya vitabu 1000 vinavyoelezea mambo hayo yasiyo ya kawaida.

Moja ya mambo ambayo yameonekana kuwa siyo ya kawaida na kuingia katika safu hii ni ule ugojwa wa "Cutis Laxa" ambao unamfanya mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja au miwili anapougua kuwa kama mzee wa miaka hamsini au zaidi.

Ugonjwa huo kulingana na gazeti la "The People" la Uingereza hivi sasa uko kule Brazil ambako umeikumba familia moja ya mjane masikini Bi Maria Jose Dos Santos na kumfanya awe kivutio yeye pamoja na wanawe ambao wameathirika na ugonjwa huo.

"Cutis Laxa" kama uanvyojulikana kitaalam unamfanya mtoto mdogo anapougua kuwa kama mzee kimaumbile, lakini akili na uwezo wake wa kufahamu mambo vikiwa vimebaki salama.

Viungo vyote vya mwili vinaendana na umri wa mtoto anayehusika, mawazo, michezo na mambo mengine yote ya kitoto yanafanyika kama wafanyavyo watoto wengine, na tatizo siyo wanaonekana vipi, bali jinsi wanavyojisikia katika hali hiyo.

Bi Maria (33), ameshapewa msaada wa kufanyiwa operesheni ya kubadilishwa sura yeye na watoto wake, lakini alikataa msaada huo

"Mungu alichoumba hakuna binadamu yeyote anayeruhusiwa kukibadilisha" allisema mama huyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari za redio, televusheni na magazeti nyumbani kwake Paraiba, Brazil.

Bi Maria anasema kuwa wanahuzunika sana yeye na familia yake pale wanapotembelewa na watu ili kuangaliwa, lakini akadai kuwa hayo yote ni mapenzi ya Mungu na wataishi hivyo na wanahisi wamebarikiwa.

"Hii ni nchi masikini lakini watu wanatusaidia chakula, fedha na misaada mingine kutokana na jinsi tunavyoonekana," anasema Bi Maria na kuongeza.

Sijisikii tofauti na mwanamke yeyote mwenye umri kama wangu wa miaka 33 natembea kama kawaida ingawa naonekana mzee, lakini najiona bado ni damu changa ya mwanamke" alisema.

Mwanamke huyo wa Kibrazil ndiye alikuwa wa kwanza kuathirika na ugonjwa huo katika familia yao ingawa wazazi wake, kaka zake na dada zake hawakuwa nao.

Baada ya Bi Maria kuanza kuzaa, kila mtoto aliyemzaa alirithi ugonjwa huo. Watoto hao watatu ni Flaviano (1), Adriano (11), na Luciano (13) ambao wanaonekana wazee kutokana na ugonjwa huo.

Kutokana na hali hiyo waliyo nayo Maria na watoto wake, baba mzazi wa watoto hao Jose Santos amewakimbia na kuwatelekeza na mama yao.

Mtaalamu mmoja wa magonjwa ya ngozi Dk. Michael Palton wa Hospitali ya Mtakatifu George ya London, Uingereza alieleza kuwa ugonjwa huo unafahamika nchini humo na husababishwa na kutokuwepo kwa mpangilio mzurichembechembe katika utengenezaji wa ngozi kwa mgonjwa.

Ugonjwa huo uligundulika nchini Brazil pale Bi Maria alipokwenda kuwapeleka hospitalini ili kupimwa watoto wake Adriano na Luciano mwaka 1985.

Pamoja na ugonjwa huo wa kusikitisha kwa familia hiyo ya Jose Dos Santos wa Brazil, lakini familia hiyo inaishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine ingawa ni mara chache Maria anadai kuwa watu wageni wamekuwa wakiwasalimia watoto wake kama watu wazima.

Kituo cha maadili kwa jamii chaanzishwa

Siku za hivi karibuni kumekuwepo malalamiko juu ya kushuka kwa maadili katika jamii, hali inayodaiwa kuwa chanzo kikubwa cha vitendo viovu na vya kutisha kuliko ilivyokuwa siku zilizopita. Hili limeiingiza jamii, vyama vya hiari, makanisa na Taifa zima kwa ujumla kwenye mjadala mkubwa, kuangalia jinsi wanavyoweza kurejesha heshima iliyokuwepo awali. Ili kupambana na hali ya kushuka kwa maadili katika Taifa letu la Tanzania kimeanzishwa kituo cha maadili kwa jamii kama mwandishi NEVILLE MEENA wa TSJ alivyoojiana na Katibu Mtendaji wa kituo hicho Bwana Senya Florentine.

Swali: Kituo hiki kilianzishwa lini?

Jibu: Kituo cha maadili kwa jamii kilianzishwa mwezi October 1997 kwa ushirikiano wa watu 12, wakiwa ni wanawake wanne na wanaume wanane na kimepeta usajili rasmi kama shirika lisilo la kiserikali Februali 11 mwaka huu.

Swali: Unaweza ikaeleza mazingira yaliyopelekea wewe na wenzako kuanzisha kituo hiki?

Jibu: Tulipata wazo hili baada ya sisi wenyewe kufanya utafiti wa kina kwa kufanya ziara katika mikoa kadhaa hapa nchini na kujionea kwa macho yetu jinsi maadili mema yanavyotoweka. Katika ziara hiyo iliyoihusisha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma, tuliweza kujionea jinsi maadili yanavyokiukwa na kushuhudia watu mbalimbali wakiendesha shughuli zao kinyume kabisa na mila pia desturi za Kiafrika. Hili lilipelekea sisi wote kuona umuhimu wa kuanzisha kituo kama hiki ambacho makao yake Makuu yatakuwa jijini Dar es Salaam.

Swali: Ni sababu gani zilizowafanya ninyi kuamua kuweka makao makuu katika jiji la Dar es Salaam?

Jibu: Kwa kuwa baadhi ya majukumu ya kituo hiki ni kuandaa vipindi mbalimbali vya kuifunza na kuhamasisha jamii kwa kutumia vyombo vya habari kama vile televisheni na radio, tuliona ni vyema makao yake makuu yawe Dar es Salaam ambako vyombo hivi vinapatikana kwa urahisi zaidi. Pia katika utafiti wetu tuligundua kuwa jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa ukiukaji maadili katika jamii kutokana na mchanganyiko wa makabila mbalimbali pia wageni wengi wanaongia kutoka nchi za nje wakiwa na tamaduni zao ambazo hazikubaliki katika nchi yetu. Hii ilitudhihirishia kwamba jiji la Dar es Salaam linahitaji huduma hii kuliko maeneo mengine ya hapa nchini.

Swala jingine ni kwamba kituo cha maadili kwa jamii ni taasisi changa ambayo inahitaji kushirkiana na taasisi nyingine kwa ajili ya kuimarisha na kujenga uwezo wa kutoa huduma bora kwa jamii na nyingi ya taasisi hizo ziko Dar es Salaam. Si hilo tu bali ni rahisi kuwasiliana na mikoa mingine kwani njia za mawasiliano ni nzuri na rahisi kupatikana.

Swali: Ni nini madhumuni ya kituo cha maadili kwa jamii?

Jibu: Madhumuni ya kituo hiki ni kusisitiza na kuhimiza uadilifu wa maisha katika jamii kuanzia kwa watoto, vijana hadi watu wazima. Uadilifu tunaouzungumzia ni pamoja na matumizi ya lugha nzuri, mavazi ya heshima yanayo, kubalika katika jamii nakadhalika.

Ili kufanikisha malengo haya kituo kinasisitiza usawa na haki kwa watu wa jinsia zote. Usawa tunaousema si katika misingi ya mali ijapokuwa nalo linaweza kusaidia misingi tunayoizungumzia ila usawa wa kijinsia ni muhimu na kituo chetu kinaamini kwamba maadili mema ni pamoja na kuheshimiana na kuthaminiana.

Pia tunawaelimisha watu wawatambue yatima, walemavu na vikongwe ili waonekane kama sehemu ya jamii kwa kusaidiwa na kushirikishwa katika mambo ambayo wanaweza kushiriki, pasipo kujali hali zao kwa kuwapa nafasi za kujiendeleza kimasomo kwa walioko tayari. Kwa kufanya hivyo tutapunguza wimbi la watoto walioko mitaani ambao ni chanzo cha maovu yanayotendeka katika jamii.

Kuna mambo mengine ambayo yanaweza kutishia amani katika jamii kama vile matumizi ya lugha chafu jambo ambalo limekuwa la kawaida. Wanaotumia usafiri wa mabasi watakubaliana na mimi kwamba haiwezekani kupanda basi na ukafika mwisho wa safari bila kusikia matusi aidha kwa waliomo ndani ya basi au nje ya basi.Hivyo tutaadaa fulana na mabango ambayo yatakuwa na ujumbe wa kuielimisha jamii athari zinazotokana na matumizi ya lugha chafu.

Pamoja na hilo jambo jingine mavazi hasa kwa upande wa dada zetu. Hivi majuzi nilishuhudia dada mmoja akizomewa na kurushiwa mawe jambo ambalo lilipelekea mpita njia asiye na hatia kuumizwa pia mfanyabiashara aliyekuwepo katika eneo hilo la Mwananyamala naye kuumizwa na kuporwa baadhi ya bidhaa zake. Matukio kama haya yanahatarisha amani katika jasmii yetu.

Swali: Ni maeneo yapi ambayo kituo kitayatumia ili kujenga upya jamii yenyer maadili mema?

Jibu: Baada ya kufanya uchunguzi tumegundua kwamba mmomonyoko wa maadili unaanzia katika shule za msingi na sekondari kutokana na ukweli kwamba elimu ya dini haifundishwi kabisa na kama inafundishwa basi basi haipewi umuhimu wa kutosha. Kituo kinaamini kwamba mchango wa elimu ya dini katika kukuza tabia njema ni mkubwa na mwanafunzi anayefundishwa vizuri elimu hiyo hawezi kuwa na tabia zisizofaa. Hivyo tutashirikiana na vyombo vinavyohusika kuhakikisha elimu ya Dini inafundishwa na ikiwezekana itungiwe mithani ya ndani na ya kitaifa ili wanafunzi watilie maanani somo hilo.

Kwa upande mwingine tunataraji kuanzisha shule za awali kwa ajili ya watoto wadogo, shule za msingi na hata sekondari hapo baadaye ambazo zitatoa elimu ya kawaida ila msisitizo mkubwa kwa wanfunzi utakuwa ni kuwa na tabia njema ili ziwe mfano bora kwa shule nyingine hapa nchini. Hii pia itasaidia kujenga jamii yetu katika misingi ya uadilifu.

Tunao wajibu wa kutoa ushauri nasaha kwa familia mbalimbali namna wanavyoweza kuepuka migogoro katika maisha ya kila siku kwani inaonekana kwamba kuvunjika kwa ndoa nyingi nako kunachangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa maadili hasa watoto wanapokosa malezi ya mmoja wa wazazi wao.

Swali: Uanachama katika kituo cha maadili kwa jamii ukoje?

Jibu: Kituo cha maadili kinatoa uanachama kwa mtu yeyote bila kujali rangi, kabila, itkadi wala jinsia. Mtu anayehitaji kuwa mwanachama anatakiwa kujaza fomu maalum za maombi na fomu hizo kupitiwa na kamati maalum ya usajili. Baada ya kukubaliwa kuwa mwanachama atashiriki shughuli zote za kituo kama atakavyoelekezwa ikiwa ni pamoja na kulipa ada ya mwaka. Ila si lazima mtu akubaliwe kuwa mwanachama kwani kamati inao uwezo wa kukataa kutoa uanachama kutokana na sababu za msingi.

Swali: Kituo kinapata wapi fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zake?

Jibu: Kwa sasa hivi kituo kinaendesha shughuli zake kwa kutegemea ada na michango ya wanachama pia michango ya wahisani wa humu nchini. Ila baadaye tuna mpango wa kuanzisha miradi midogomodogo kama vile mgahawa, duka la stationary na vibanda vya biashara ili kituo kiweze kujitegemea kwa kiasi kikubwa.

Pia tunataraji kuwa na gazeti, kuandaa matembezi ya hiari na bahati na sibu ili malengo yetu ya kufikisha ujumbe kwa walengwa yaweze kufanikiwa. Kwa kuwa lengo letu ni kujiimarisha ili tuweze kujitegemea, faida zote zitakazotokana na akaunti zilizoko Benki zitatumika kuendesha shughuli za kituo chetu. Pia tunafanya mipango ya kupata mikopo kutoka Benki na taasisi nyingine za fedha ndani na nje ya nchi.

 Mtakatifu Paulo wa Israel

lAwali aliupinga Ukristo, lakini hatimaye aliukubali na kuutangaza kwa nguvu zote

Mtakatifu Paulo (Mtume) wa Israel ndiye yule suala ambaye awali alikuwa akiupiga vita Ukristo, lakini baadaye akakubali na kuutangaza kwa nguvu zake kama alivyoweza katika Ulaya ya kale.

Katika kumuenzi Wakristo hasa wa Kanisa Katoliki kote duniani huadhimisha siku ya kumbukumbu yake ifikapo Juni 29 kila mwaka.

Paulo alikuwa ni mmisionari mashuhuri sana katika wakati ule ambapo dola kama vile ya Ugiriki, Uyahudi (Israel) na ile dola ya Kirumi zilikuwa zikiitawala Ulaya ya kale.

Ujumbe wa Paulo katika wakati wake inaaminika kuwa uliweza kuibadili Ulaya kuondoka katika 'zama za giza' na hatimaye kuwa Bara la watu wenye kumcha Mungu, kwa njia ya Kristo.

Kutokana na uwezo wake Paulo hivi leo maelfu ya wamisionari duniani kote wamekuwa wakiiendeleza kazi yake ya kueneza neno la Mungu na kazi waliyoachiwa na Yesu Kristo.

Jina la Paulo katika Ukristo ni kubwa na ambalo linaonekana kuchukua nafasi yake kwa heshima yake, na ndio maana hata Papa wa sasa anayeongoza Kanisa Katoliki alichagua jina lake la Paulo na kuliweka kuwa jina la pili.

Alipokuwa mdogo Paulo alikuwa akiitwa Sauli ambapo alikuwa akifuata maisha, utamaduni, sheria na dini ya jadi ya Kiyahudi ambazo zote zilikuwa na misingi ya kuupinga Ukristo na wafuasi wake.

Wakati mmoja akiwa askari na mtumishi wa serikali ya Uyahudi, Sauli alitumwa kwenda kuwakamata Wakristo wa Dameski kule Syria na kisha kuwapeleka Yerusalemu, Israel kuadhibiwa kutokana na imani yao.

Alipokuwa njiani kutoka Yerusalem kwenda Dameski kuwakamata Wakristo, ghafla Sauli alipigwa na mwanga mkali usoni na kuanguka chini kutoka juu ya farasi wake.

Kundi la washirika wake walipomuinua waligundua kwamba amekuwa kipofu, ambapo walimbeba na kisha kumpeleka mjini Dameski kwa matibabu, lakini hakuweza kupona.

Baadae mkristo mmoja kwa jina Anania ambaye alikuwa akiishi Dameski aliagizwa na BWANA kwenda kumuona Sauli na kumuombea. Baada ya kumuombea na kumuwekea mkono usoni kwake, Sauli aliweza kuona tena na akabatizwa.

Kuanzia hapo Sauli ambaye alikuwa Myahudi na mtumishi mzuri wa serikali ya Kiyahudi, aliamini kwamba kweli Yesu ni mwana wa Mungu, na akaanza kuhubiri na kueneza kwa nguvu habari za Ufalme wa Mungu katika masinagogi ya Uyahudi.

Paulo ni jina la Kigiriki lenye maana ya "ndogo" au "mdogo". Mtakatifu Paulo kabla ya kubatizwa jina lake la awali lilikuwa Sauli ambalo kwa Kiebrania ni lenye maana ya "aliyechaguliwa" au "mteule".

Mtakatifu Paulo alizaliwa katika mji wa Tarso. Wazazi wake walikuwa ni Wayahudi matajiri na akiwa mdogo walimpeleka katika mji wa Yerusalem kupata elimu, ambapo akiwa huko alijifunza mambo ya biashara.

Sehemu zinazokumbukwa kwamba alifika na kwuahubiria watu ni pamoja na visiwa vya Cyprus, Ugiriki, Uturuki, Macedonia, Palestina na sehemu za Asia ya Kati hadi Italia ambako kote huko alipata mafanikio.

Hata hivyo katika safari zake hizo akiwa pamoja na mshirika wake Sila, Mtakatifu Paulo alipatwa na misukosuko mingi ikiwemo wakati mmoja kukamatwa na kufungwa gerezani.

Maisha ya Mtakatifu Paulo inaaminiwa yalifikia kikomo mnamo mwaka 53 baada ya Kristo ambapo alisafiri kukatisha bahari ya Aegea na kufika kwa Waefeso ambako hapo aliishi kwa muda mfupi na kisha kusafiri Kaisaria hadi Antiokia alikomalizia safari yake ya kimisionari na kifo kumchukua.

Nini utamaduni wa kifo?(2)

UTAMADUNI wa kifo ni matendo na maelekeo ya binadamu katika kuendeleza na kutetea hali zile zinazosababisha binadamu apoteze uhai wake, adhuru mwili wake, adhalilishe utu wake au kuufanya mwili wake kuwa bidhaa inayeweza kununuliwa, kuuzwa na kuchezewa. Chochote kile kinachopingana na uhai kama vile mauaji, utoaji wa mimba na vitendo vinavyoharakisha kifo. Hali hiyo huitwa utamaduni wa kifo kwa vile mwanadamu mwenyewe kwa makusudi anafurahia hali ya kujidhuru na kuizoea. Katika sehemu ya pili ya makala hii, EMIL HAGAMU wa Chama Kutetea Uhai (Pro-Life Tanzania anaeleza kwa kina juu ya "Utamaduni wa kifo"

 Sera potofu za uzazi wa mpango

Mpango kabambe wa kupanga uzazi kwa njia za kisasa ni mpango wa kulaaniwa kwa nguvu zetu zote, ni mpango wa mauaji. Hapo awali nimezitaja njia zitumikazo katika kupanga uzazi. Madhara yake kwa watumiaji ni mengi na makubwa. Mataifa yaliyotumia njia hizi kwa miaka mingi ya nyuma, leo hii yanajuta na yanafanya mikakati ya kuona kuwa idadi ya watu inarudia katika hali yake ya zamani.

Ufaransa imetangaza rasmi kuwa idadi ya watu wake iko chini; hivi kwamba imeanzisha mpango wa vivutio kwa vijana na watu wenye familia kubwa huduma bora za nyumba, mikopo yenye riba nafuu kwa familia changa, na uhakika wa posho ya likizo ya uzazi.

Serikali ya Uswisi pia imetangaza sera ya kinga ya kiuchumi na kijamii hasa kwa familia na watoto, kwa mfano posho kwa wanafamilia, bima ya uzazi na likizo yenye malipo.

Mwaka 1984 Serikali ya Ujerumani ilitengeneza sera ya kuhakikisha kuwa watoto 200,000 wanazaliwa kila mwaka. Wazazi walipewa nafuu ya kodi, na kila mama mwenye mtoto mchanga alilipwa Dola za Kimarekani.200 (karibu Sh.140,000) kama posho yake kila mwezi hadi mtoto wake anapotimiza umri wa mwaka mmoja. Pia wazazi walipewa likizo sambamba na posho hiyo ya uzazi.

Huko Ugiriki, sheria ya kuzuia wanawake wasifukuzwe kazini wakiwa wajawazito imetungwa. Likizo ya uzazi ya majuma 14 na posho ya uangalizi wa watoto vimetolewa kwa watu wenye familia kubwa.

Ndipo tunajiuliza, iwapo Watanzania tutajiua sisi wenyewe kwa kutumia njia za kisasa za kupanga uzazi je, tutakuwa na uwezo wa kuweka sera za kurudisha tena idadi ya watu kama wenzetu wanavyofanya sasa hivi?

Na kwa kweli kweli utafiti uliofanywa na Waingereza na kuchapishwa katika gazeti la ‘Nature’ unaonyesha kuwa UKIMWI unaweza kabisa kumaliza idadi ya watu wa Afrika na katika miaka michache ijayo tutaanza kuona upungufu wa watu badala ya ongezeko la watu. Na Shirika la Afya Duniani linatabiri kuwa huenda baadhi ya nchi zikawa tupu katika miaka 10 au 20 ijayo kutokana na balaa la UKIMWI.

Na hapa kwetu Tanzania, idadi ya watu wanaokufa kutokana na UKIMWI inaongezeka mwaka hata mwaka. Katika hotuba yake kwenye siku ya UKIMWI duniani, Desemba mosi mwaka 1997, Waziri wa Afya alikiri kuwa idadi ya wagonjwa wa UKIMWI imeongezeka na watu walioathirika na virusi vya UKIMWI wamefikia milioni moja na laki mbili.

Mashirika na idara

UMATI

Watanzania wengi tunawafahamu UMATI, na wengi wetu tunajihusisha shirika hili na ‘uzazi wa mpango kwa njia za kisasa’.

Na kwa kweli ndizo shughuli zake. Shirika hili limefanya kazi hapa nchini kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Pamoja na muda huo kuwa mrefu, bado Shirika hili linalalamika kuwa ukubalifu wa huduma zake bado uko chini. Shirika hili linataja baadhi ya sababu kuwa ni pamoja na hofu ya wazazi kwa vifo vya watoto, kutozijua huduma hizo na woga. Pengine Shirika hili linashindwa kukubali ukweli kuwa watu wasio wajinga, wanakataa kuzitumia kwa sababu zinawaua.

MARIE STOPES

Bila shaka wengi mnazijua kliniki za Marie Stopes. Kliniki hizi zimeanza kuenea mikoa yote hapa nchini. Hapa jijini Dar es Salaam kliniki hizi zimetapakaa pande zote. Lengo la kliniki hizi, kama zilivyoasisiwa na mwanzilishi wake, Marie Stopes wa Uingereza ni kupunguza idadi ya watu kwa njia ya kutoa ushauri nasaha kwa wanawake wenye matatizo ya uzazi.

Hata hivyo Shirika hili linajishughulisha pia na kampeni ya VASEKTOMI kwa wanaume. Jijini Dar es Salaam, tunaambiwa kuwa hadi sasa ni wanaume wachache tu wamejitokeza kupatiwa huduma hii.

PROGRAMU YA NYOTA YA KIJANI

Hii ni programu inayoendeshwa na Wizara ya Afya inayowahamasisha wananchi kutumia njia za kisasa za kupanga uzazi. Mkakati kabambe unaotumia vyombo vya habari hasa Redio Tanzania Dar es Salaam, umebuniwa na kuratibiwa. Nguvu ya programu hii inalala katika nyanja mbili. Mosi, semina zinazoendeshwa nchi nzima kwa kisingizio cha AFYA YA MAMA NA MTOTO kupitia huduma za afya mijini na vijijini. Pili, michezo ya kuigiza kupitia redio, na sasa hata Televisheni.

VITA DHIDI YA UTAMADUNI WA UHAI

Nchi na mashirika yanayotetea utamaduni wa kifo yanaendesha kampeni ili nafasi ya kudumu ya Baba Mtakatifu iondolewe kutoka Umoja wa Mataifa!

Vilevile wanavipiga vita vikundi na mashirika yanayotetea uhai wa binadamu duniani kote. Kejeli inayojengwa ni kuwa Vatikani ni ya kikale na mashirika yanayotetea uhai wa binadamu hayana huruma au yana msimamo potofu wa kidiniau kiimani.

Lengo la hatua hizi ni kuondoa uwezekano wa mashirika yanayotetea uhai kupata nafasi katika Umoja wa Mataifa na hivyo kufifishwa nguvu zake katika ngazi ya kimataifa.

Jitihada zilifanywa kuhakikisha kuwa ujumbe wa Vatikani na Mashirika yanayotetea uhai wa binadamu hayapati nafasi ya kushiriki mikutano ya kimataifa ya Cairo, Beijing na Copenhagen ili maamuzi ya kishetani yaweze kupitishwa.

KUPINGA JITIHADA ZA VYAMA VYA KUTETEA UHAIWatetezi wa Utamaduni wa Kifo hutumia hujuma dhidi ya vikundi na vyama vianvyotetea uhai. Mbinu moja kuu ni kuwalaghai viongozi wa serikali wavichukie vyama hivi na hivyo kuchukua hatua za kisheria dhidi yao. Fedha nyingi hutumika katika kuwarubuni viongozi wa serikali na wanasiasa.

Mfano huko Canada, watetezi wa utamaduni wa kifo walifanikiwa kuwashawishi viongozi wa serikali na siasa ili wakifute chama cha HUMAN LIFE INTERNATIONAL - CANADA.

Hilo lilifanikiwa na chama hicho kimezuiwa kufanya kazi nchini humo. Pia hapa Tanzania Pro-Life TANZANIA ilitishiwa kufutwa kama haitaacha vita vyake dhidi ya "wapenda kifo". Katika hali hii vyama au mashirika yanayotetea uhai na utu wa binadamu vinatukanwa, kubezwa na kudharauliwa. Viongozi wa serikali na siasa huungana na watetezi wa kifo katika kuendeleza utamaduni wa kifo.

HITIMISHO

Utamaduni wa kifo umeizingira jamii ya kimataifa na ya kitaifa. Utamaduni wa kifo ni mtindo wa maisha wa kufurahia maovu, udhalimu, mauaji, na hata uasherati ili kukidhi haja ya mwovu. Lengo lake kuu ni kumwangamiza binadamu mwenyewe. Katika utamaduni wa kifo, binadamu ni bidhaa tu, ni kiumbe dhaifu kuliko mazingira na maendeleo. Fedha nyingi zinatumika katika kulinda wanyama na ndege wasiangamie. Fedha nyingi zinatumika ili kumtokomeza binadamu.

Utamaduni wa kifo unalelewa na binadamu yeyote mwenye mabavu dhidi ya binadamu mnyonge.

Unyonge unaweza kuwa wa kiuchumi, kisiasa, kijinsia, kiumri au hata kiutamaduni. Watoto wadogo, wazee, walemavu, wagonjwa, na maskini ndio wanaostahili kuondolewa na kuwapisha watu wenye nguvu waendelee kuishi. Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?. Utamaduni wa kifo huuona uhai kama laana na uhai mpya kama balaa.

Utamaduni wa kifo hulenga kuiangamiza familia; yaani baba mama na mtoto. Lengo kuu la utamaduni wa kifo ni mwanamke ambaye ana uwezo wa kuzaa na kulea.

Ili kumtengua nguvu mwanamke, anapewa madawa mbalimbali kwa kisingizio cha kuzuia mimba ili adhoofike kiafya na hivyo kuufanya mwili wake kuwa mnyonge na usio na uwezo wa kufanya kazi.

Anaambiwa aue mtoto mchanga ndani ya tumbo lake (kutoa mimba) kwa vile mtoto huyo atakuwa kikwazo kwa maendeleo ya mama yake. Lengo la pili la utamaduni wa kifo ni kuua mtoto au uhai mpya. Huyu hatakiwi kabisa, ndiyo maana vifaa na zana zinabuniwa ili kumwua akingali tumboni mwa mama yake.

Lengo la tatu ni mwanamume. Huyu ndiye mpangaji mipango katika familia. Ili kudhoofisha utu wake anaambiwa ahasi ili asiwe tena na uwezo wake wa kiume. Kwa hiyo utamaduni wa kifo hushambulia UBABA, UMAMA, na UTOTO.

Je, katika hali ya namna hii tufanyeje?

Ili kukabiliana na utamaduni wa kifo, lazima tujenge utamaduni wa uhai kwa njia zifuatazo:Kuwa watu wa uhai; Sisi sote tutambue kuwa tumeumbwa kwa mapenzi ya Mungu.

Hakuna hata mmoja kati yetu alichagua kuzaliwa na kuwa hivyo alivyo. Kumbe uhai tulionao ni zawadi tu kutoka kwa Mungu. Mungu ametupatia na Mungu atauchukua. Hakuna mwenye uwezo wa kuingilia kati uwezo huu wa Mungu.

Kwa hiyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuulinda, kuutetea na kuuendeleza. Uhai huja mara tu na ukiondoka haurudi tena. Kila mmoja wetu apinge mbinu zote zinazohatarisha uhai wa binadamu.

Sala: Kila mmoja asali kwa ajili yake na kwa ajili ya uhai wa watu wengine. Tusali daima bila kuchoka. Tuwaombee viongozi wetu wa serikali, siasa, na dini wasiingizwe katika mitego ya yule mwovu na wasitutelekeze kwa manufaa yao.

Vyama vya kutetea uhai: Tujiunge na vyama vinavyotetea uhai, vya ndani na nje ya nchi yetu. Tukiwa katika vyama hivi ni lazima tuseme kwa sauti kubwa ili kwamba ukweli na ushuhuda wetu upate kuonekana na kusikiwa na watu.

Kubadili dhamiri: Jitihada za pekee zifanyike katika kubadilisha mioyo ya watu ili wajengeke katika dhamiri safi. Hili linahitaji elimu ya daima na uhamasishaji.

Vyombo vya habari: Vyombo hivi vina nafasi kubwa katika jamii. Kwa kuvitumia kwa lengo la kujenga utamaduni wa uhai, waandishi wa habari na vyombo vya habari vitakuwa vimetimiza wajibu wake wa kulinda, kutetea, na kuendeleza uhai wa binadamu.