Mjue kijana Mtanzania aliyeonja chungu ya vita ya Wasomalia

Aliwazika mama, dada yake peke yake; ni baada ya kubakwa na kuuawa mbele yake

Alishindwa kumsaidia mtoto aliyekuwa akinyonya maiti ya mama yake

Abdulah Hamad ni miongoni mwa vijana wa Kizigua ambao mababu zao walichukuliwa utumwani huko Tanga na kupelekwa nchini Somalia; akazaliwa na kukulia huko. Kijana huyu mwenye umri wa miaka 30 anasimulia machungu ya dunia aliyokumbana nayo huko nchini Somalia baada ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe vya makabila ya nchini humo kama anavyosimulia katika makala hii alipozungumza na waandishi wetu Dalphina Rubyema na Josephs Sabinus hivi karibuni eneo la Mbagala jijini akieleza namna alivyotaabika na sasa yupo hapa nchini kwake baada ya kuwapoteza wazazi wake wote.

Kwa mara nyingine moyo ukanilipuka; safari hii sasa machozi hayakuwa na mjadala na mimi. Lakini, ningefanya lipi jema kwa mtoto huyu mchanga maskini; aliyekuwa akijaribu kunyonya matiti ya maiti ya mama yake ambaye alikuwa amelala chini baada ya kuuawa kwa risasi ?

Maskini mtoto wa watu hakuwa anajua kuwa ule ndio ulikuwa mwisho wa kuyapata mapenzi ya mama yake huyo hapa duniani.

Mtoto huyo wa kike aliponiona alianza kunililia hali akinitolea macho yenye ishara ya kuniomba nimsaidie kumwita mama yake ili ampe huduma aliyozoea kuipata toka kwake.

Nilishindwa nimsaidiaje mtoto huyo ambaye tayari alikuwa ametapakaa damu zilizoganda; zilizotokana na majeraha ya risasi yaliyomuua mama yake ambaye yeye alidhani anamkatili kwa makusudi.

Lakini, angefanya nini wakati amekwisha kuwa yatima?"Abdulah alimeza mate kidogo kisha akaendelea . "Roho ilinisuta sana na moyo wa uwajibikaji ukanisukuma nimsaidie kiumbe huyu mchanga ambaye hata wale inzi weusi wakubwa walikuwa wamemkalia huku mdomo wake ukionyesha kuwa mtoto huyo alifikia hatua ya kula damu zile za marehemu mama yake.

Hata ninapokumbuka, roho inaniuma sana lakini ninatumaini Mungu atanisamehe kwa kuwa sikupenda nimuache mtoto yule pasipo usaidizi wowote hali akihitaji msaada wangu.

Ningetoa wapi nguvu na akili za kukimbia naye, hali nami ni dakika chake zilizopita nilipomaliza yangu kazi ya mazishi ya mama yangu mzazi na dada yangu Sophia peke yangu baada ya kubakwa na kuuawa na vijana wa Kisomali kwa risasi mbele yangu!

"Huo ulikuwa ni mwaka 1990 nikiwa dereva wa kampuni moja iliyojulikana kama Hollsmen Sugar Company; ya Somalia. Nilikuwa nikiendesha trekta kazi niliyoifanya kwa miaka saba kabla ya kuteuliwa kuwa Mtunza Stoo wa kampuni hiyo; kazi hiyo niliifanya kwa mwaka mzima"

Kijana huyu wa Kizigua aliyezaliwa katika kijiji cha Kwamofi nchini Somalia alitulia kidogo akapangusa machozi yaliyoanza kumlenga lenga.kisha akaendelea kusimulia zaidi na kusema "Mwaka 1991 katika mji wa Mogadishu ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo, vilizuka vita kati ya makabila ya Majentini,. Wamerehane na Isuka (Abgali). Mji mzima ulienea machafuko ya kutisha na kusababisha mabosi wa kampuni hiyo waliokuwa wazungu wakimbie.

Hivyo wengine tukarudi vijijini kwetu. Siku hiyo iliyoleta mauti ya mama ilikuwa ni majira ya saa tatu hivi asubuhi. Walifika vijana watatu wa Kisomali katika hali ya kutisha. Muonekano wao ulimdhihirishia marehemu mama kuwa ujio wao haukuwa wa heri.

"Abdulah! Kimbia mwanangu; kimbia",Mama aliniambia katika juhudi zake za kunitaka nijisalimishe.Alipoona nasita aliniskumia chooni. Mimi, mama na dada yangu tulikuwa tukikaa katika nyumba yangu ya vyumba saba.Baba alishafariki kwa ugonjwa wa kawaida na nilikuwa na ng'ombe 14 na mbuzi 32.

Si kwamba vijana wale tuliofanya nao kazi walitaka kuondoa uhai wangu pekee katika machafuko hayo ya kikabila, bali pia walijua wazi nafasi yangu na hivyo huenda pia walijua nina kiasi gani cha fedha pale nyumbani. "Pesa za mumeo ziko wapi?" "Toa haraka!" niliwasikia vijana wale wakimuamuru mama ambaye alikuwa kitinda mimba wa bibi Mchiwa huku wakimpiga na kitako cha bunduki juu ya paji lake la uso.

"Mume wangu hayupo;amefariki" mama akajibu huku akiongonzwa kwenda ndani. Mmoja wa vijana wale waliokuwa wafanyakazi wenzangu na ambao sasa ndio wamenigeuka na kunikatili namna hiyo aliyeitwa Ishaq, alikuwa akiendelea kumdhalilisha dada Sophia pale nje; aliyofanyiwa..."

Ninazidi kusema kuwa vitendo alivyofanyiwa dada huku ninashudia kwa macho yangu, na wengine wakimvua nguo na kumvutia zaidi ndani aliko mama yangu, na hao vijana wengine wakizidi kutafuta pesa ni siri yangu; mtajua wenyewe namna ya kuyaandika"anasema Abdulah huku akijitahidi kuwatazama waandishi hawa kwa ushujaa. Kisha anaendelea

"Walibeba redi yangu aina ya Panasonic na kiasi cha Shilingi 300,000 ambazo walimlazimisha mama awape.

Kisha kilichotendeka sikukijua huko ndani kwani nilichokiambulia sasa ni sauti mbili za milio ya bunduki.

Nilipoteza fahamu kwa muda pale chooni nilipokaa tangu saa 3 asubuhi hadi saa kumi na mbili unusu jioni na fahamu ziliponirudia nilichungulia tena nikaona wameondoka huku maiti za mama na dada yangu zikiwa zimelala chini.

Jioni hiyo niliridhika na ukimya uliokuwepo kijijini hapo ambao uliniashiria usalama kidogo.Sasa nilitumia nguvu kubomoa kile kimlango cha choo; nikatoka. . Nilichukua shuka pale chumbani nikarudi nyumanyuma chumbani mle na kuwahifadhi.

Nilichukua jembe na kuchimba mashimo mawili ya kina cha kupita magoti kidogo, bahati nzuri ni eneo lenye udongo wa kichanga ; hivyo Mungu akanisaidia walau nikafanikiwa kulikamilisha jukumu hilo linalonikabili peke yangu bila msaada wa mtu yeyote, nikaivuta miili ya marehemu wangu; mmoja mmoja nikawazika; kila mtu kwa shimo lake. Niyalifukia haraka haraka hata ilipohitimu saa moja kasorobo, bado nyumba zilizoungua zilikuwa zinamalizia ile mioshi ya mwisho ya kuteketea.

Ndipo nami sasa nilipoamua kukimbia kijiji ili kuwatafuta wenzangu. Nilipofikia umbali kidogo njiani ninamkuta mwanamke mmoja jirani yetu, jina lake Mwajuna, naye amekufa kwa risasi na kuacha katoto hako kakilia hapo mlangoni katika nyumba ile iliyopo jirani kabisa na njia hali kakimpekua marehemu mama yake na kujaribu kunyonya, bila mafanikio.

Hapa, ujasiri na huruma wangu vikanishinda; Mungu nisamehe, nilikaacha vinginevyo, kangesababisha mauti kwangu.

Usiku ulikuwa umeingia mno na sikuamini masikio yangu maana niliona ni kama ndoto yangu ya mwisho duniani. Sikujua kuwa vijana wale walioniita walikuwa na nia njema; nikajua sasa Abdulah nimekwisha, sikujua kama labda vijana hao Ally na Hussein walikuwa na masaibu kama yaliyonifika; na kwamba labda walitaka wote twende nchini Kenya, na safari yetu sasa ilikuwa imetufikisha hadi katika msitu wa (Kwa Mnumuli) na ilipotimu saa 7:15 usiku tulipanda na kulala juu ya mti.

Ilipotimia alfajiri ya saa 11:30 hivi asubuhi iliyofuatia baada ya mkesha wetu juu ya kitanda hicho cha aina ya "mti mkubwa" kisicho kuwa na godoro wala neti ya mbu,wala shuka kwa muda wa siku saba za mwanzo wa safari yetu tukila mizizi ya miti tulikuwa na nguvu bado.

Ndani ya msitu ule wa Kwa Mnumuli hatukuwa tukijua uelekeo wowote; ilikuwa bora liende. Hata hivyo nilikumbuka maneno ya marehemu babu yangu. "Wanangu; nyie ni Watanzania mkae mkijua ndiko kwenu, ndiyo maana mnaona hata majina yenu ambayo ni majina ya vijiji vyetu kule Tanzania. Ya Mungu mengi; siku ikitokea mmelazimika kurudi kwetu (Tanzania) bila kupanga japo tangu mmezaliwa hamjafika huko, fuateni mwelekeo wa upande jua linapozamia. Fuateni uelekeo huo tu; na hatimae mtatokea nchini kwenu asilia; Tanzania."

Abdulah ni wa mwisho katika familia yao yenye watoto watano; wa kike wakiwa wawili na wa kiume watatu baada ya dada yao (Sophia) kuuawa katika machafuko hayo huko nyumbani kwao nchini Somalia.

"Tukiwa njiani sasa tunaendelea kusota kupiga kwata ,nasi hali yetu ikizidi kuwa mbaya, kwani hata maji tuliyokuwa tukinywa baada ya safari ndefu yenye hofu na pasipo tumaini lolote yalikuwa hayakuhitaji mjadala wa kama ni masafi ama la.

Siku hiyo yalikuwa majira ya adhuhuri ,tumechafuka na hata kuchoka sana ;tukiwa tunaendelea na safari yetu ;tunashtushwa na mlio wa bunduki eneo jirani na sisi, Nikamwambia Ally tumekwisha ;tumekwenda; tunakufa sasa. Kila mmoja alitafuta uelekeo wake wenye kufaa ,ndani ya msitu huo mnene wa kutisha .Mungu saidia baada ya kukimbia kwa karibu saa moja hivi ndani ya msitu huo kila mtu kivyake, ghafla tunakutana kwenye kichaka kimoja mimi na mwenzangu Ally, laiti wote tulipigwa na butwaa na kama tungelikuwa na silaha ,ladba tungeliuana wenyewe kila mmoja kila mmoja akimdhania mwenzake ni adui .

Hapo tulifurahi na hata kudhani kuwa mila,desturi na tamaduni za kikwetu sambamba na matambiko ndiyo yanayotusaidia namna hii.Tukapeana matumaini na kuendelea na jukumu letu la safari isiyo na kikomo. Ally alinitangulia katika mbio zetu hizo za kichovu na wala hazikuwa zimepita hata dakika kumi za uwepo wetu mpya wa pamoja katika mbio hizo.

Ghafla akapigwa risasi ya mgongoni iliyomtokea kifuani.Kabla akili yangu haijazama kwenye tafakari kamili juu ya jinsi gani nimsaidie Ally, nami nikapigwa risasi mguuni (anawaonesha waandishi sehemu aliyopigwa risasi ikiwa na matundu mawili).Nikatambua kwamba japokuwa wapo mbali kidogo,hii ni rasharasha;masika iko njiani.inakuja.

Ndugu yangu ogopa risasi ;maumivu yake ni makali nashindwa niyafananishe na nini, lakini kuliko kupigwa risasi usife, heri uuawe kabisa. Ally alipokuwa akipumua damu zilitiririka kifuani kwakekama unavyoweza kuona ng'ombe akichinjwa. Kila nilipojaribu kumkokota ili walau akafie mbele, ilishindikana na badala yake alipiga magoti kusali ,akaniomba maji ya kunywa Nikamwambia hakuna maji lakini aliendelea kunidai nimpe maji, hadi nilipoona nitapigwa na mimi risasi nyingine, kwa uchungu nikamwacha nikakimbiana jeraha langu mguuni.

Sikufurahi kumwacha Ally katika mazingira yale lakini ningefanya nini hali nami sasa ni mlemavu anaonyesha kwa kila hali kwamba maisha kwake basi?

Sikuwa na jinsi ; nikamuacha na Mungu wake lakini nikamwambia "Ally! ninapenda nikusaidie, lakini nitakusaidiaje? kama sio kufa wote hapa? Tumuombe Mungu atusaidie." Maneno yalitoka moja kwa moja toka moyoni mwangu.

Nilizidi kukimbia huku nikichechemea na kujificha vichakani kila nilipozidiwa maana nami sasa nilikuwa mmoja wa walemavu. Hata hivyo maumivu niliyokuwa nayo japo niliamini kuwa nitakufa muda si mrefu nikazidi kujikokota taratibu kabla sijakata tamaa.

Uchovu, uchungu, njaa na kiu nilivyokuwa navyo, vilinifanya kupoteza fahamu.

Kijana Abdulah akapitisha mkono machoni kwa siri siri. Kila aliyemuona aliona dhahiri kuwa anapangusa machozi yaliyomlengalenga na hakutaka mtu alijue hilo. Anaendelea kusimulia hali wote waliokuwepo ndani wakiwa kimya .Watoto wadogo wa nyumba yalipofanyikia mazungumzo baina ya Abdulah na waandishi, walikuwa wameketi sakafuni wakimsikiliza kwa huzuni. Akaendelea,

"Sikujua linalofuatia kwangu baada ya muda mfupi; nikaendelea kujipumzisha pale kivulini kwa hali ya kutokuwa na tumaini lolote hapa duniani huku nikijaribu kulifunga lile jeraha langu la risasi kwa shati nililokuwa nalo katika mguu wangu huu wa kulia.

Jeraha hilo japo lilikuwa mali yangu, kwa namna lilivyokuwa limeharibika, niliona yeyote anatakaye taka kuukata mguu ule na kuliondoa, angekuwa amenisaidia sana kwani licha ya maumivu yake, sasa lilitoa harufu ambayo hata mbwa mlafi asingependa kuinusa.

Itaendelea toleo lijalo.

 

Makanisa ya Kiprotestanti na Kikatoliki Uganda

Ilikuwa ni kusakwa chanzo cha Mto Nile?

Na Mwandishi Wetu

Nchi ya Uganda ipo katika eneo la Afrika ya Mashariki pamoja na nchi za Kenya na Tanzania.

Nchi hii iliyopo kaskazini mwa Tanzania, ina heshima kuu mbele ya waumini wa Kikristo,hasa kutokana na ile habari ya vijana wake waliojitoa mhanga wa kuipokea licha ya kupata mateso makubwa na kisha kuuawa.

Tukio hilo linalojulikana kama "Mashahidi wa Uganda" linakumbukwa kila mwaka duniani kote na Wakristo wa madhehebu yote yale ya Kikatoliki na Kianglikana.

Kisa hiki cha kumbukumbu ya Mashahidi wa Uganda kinakwenda sambamba na kuingia kwa Kanisa la Kiprotesestanti na Katoliki katika nchi hiyo.

Uganda kwa mara ya kwanza ilifikiwa na Wazungu mwaka 1862, nao ni Speke na Grant kutoka Uingereza ambao walikuwa wakitafuta chanzo cha mto mrefu uitwao sasa Nile.

Baada ya Wazungu hao wawili, wengine nao walifuata ambao walipelekea habari kwao Ulaya kuwaarifu watu wa huko kwamba kuna haja ya wajumbe wa dini ya Kikristo kufika katika nchi hiyo.

Kabla ya kifika huko Uganda, Speke na Grant walikaa kwanza Tanzania kwa Chifu Rumanyika mpaka waliopata ruhusa ya kuuvuka mto Kagera kuingia Uganda.

Lakini wakati huo Grant alikuwa mgonjwa wa mguu, ikampasa Speke kumwacha kwa Rumanyika na kuendelea peke yake hadi Uganda.

Katika safari hiyo Speke alipewa Mwambata na Rumanyika ambaye alikuwa akiitwa Rozarx ili afuatane naye hadi Uganda na kisha arudi naye Karagwe, Tanzania.

Mtawala wa Uganda ya wakati ule aliyeitwa Kabaka aliwakaribisha na mwaka 1877 Kanisa la Kiprotestanti lilianza rasmi nchini Uganda kufuatia safari hiyo ya Speke.

Miaka miwili baadae, yaani mwaka 1879 wamisionari wa kanisa la Kikatoliki nao wakabisha hodi ndani ya nchi hiyo ambapo walifika na kuanzisha kanisa lao.

Kabaka aliyekuwa mtawala wa himaya ya Uganda alikuwa ni mtu mwema, ambaye alikuwa mkarimu kwa wageni na aliyeupokea vyema Ukristo.

Mtawala huyo alikufa mwaka 1884, na mwanawe aliyeitwa Mwanga akarithi kiti chake cha ufalme kuitawala nchi hiyo ya Uganda.

Lakini baada ya kurithi kiti hicho cha enzi, Mwanga hakuwa mtawala mzuri, kwani aliwachukia wale wote waliokuwa wakifuata dini mpya ya kikristo, na akaanzisha mauaji dhidi yao.

Mwanga na utawala wake aliendesha mauaji hayo bila huruma kwa Waganda wote walioupokea Ukristo kwa miaka mingi kidogo, hata ikawalazimu Waingereza wa Chama Cha Imperial Bristish East Africa Company (IBEA) kuingilia kati.

Waingereza hao waliingilia katika kutuliza mauaji hayo baada ya kushauriwa na Waganda wenyewe ambao walikuwa tayari wameupokea Ukristo.

Aliyefaulu kutuliza mauaji na ghasia alikuwa Mwingereza mmoja Mmisionari aliyeitwa Lugard, ambaye alifika Uganda mwaka 1890, lakini baadae tena matata yakaanza upya.

Matata hayo mapya ya mwaka 1892, yaliwafanya wanachama wa IBEA kulazimika kuikabidhi sehemu hiyo ya Uganda kwa serikali yao ya Uingereza, na hapo ukawa ndio mwanzo wa Uganda kuwa chini ya utawala wa Waingereza hadi ilipohitajika uhuru wake mwaka 1962.

 Kanisa linaloua watu weusi laibuka Marekani

Lengo lao ni kufyeka watu weusi duniani kote

Wanadai mtu mweusi asili yake ni matope

Tayari wameuwa wengi ndani na nje ya Marekani

Na Ignatio Obuombe

Kunako karne ya 18 chuki ya watu Weupe dhidi ya mtu Mweusi kupata haki yake ilidhihirika pale rais wa Marekani wa wakati huo Abraham Lincoln alipopigwa risasi usiku na kuuliwa na Wazungu wenzake. Je ni nini kilichopelekea apigwe risasi? Jibu kubwa ni kwamba alikuwa amewapa uhuru watumwa Weusi waliouzwa Marekani wasiwe chini ya utumwa wa Wazungu. Tena. Jambo hilo liliwakasirisha Wazungu wenzake ambao hawakutaka mtu Mweusi apewe haki na ndipo wakalipiza kisasi kwa kumuua kwa risasi Lincoln aliyejawa na huruma kuona watumwa weusi wananyanyasika .

Lincoln alipigwa risasi usiku akiwa yuko kwenye jumba la kuonesha michezo ya kuigiza ambapo usiku huo mchezo unaoonesha kukoma kwa utumwa wa mtu Mweusi huko Marekani, ungelioneshwa jukwaani. Hata hivyo, badala ya watu hao waliofurika ndani ya ukumbi kuona mchezo wa kuigiza, walishuhudia kilio kikubwa kilichotawala ukumbi na eneo zima.

Kana kwamba hilo halikutosha, mwezi Agosti mwaka 1968, Mpigania haki mashuhuri wa Marekani mwenye asili ya Kiafrika Mmarekani Dk, Martin Luther King, JR alifika mjini Memphis katika jimbo la Tenessee akiwa na lengo la kuandaa maandamano ambayo yangelifanyika kesho yake kupinga ubaguzi dhidi ya mtu Mweusi kwenye magari ya Abiria na vyombo vya usafiri.

Lakini Dr.King, JR hakulala ndani ya Hoteli ya Ambassador aliyofikia hata aongoze maandamano hayo kama alivyotarajia. Jioni hiyo alikuwa amesimama na Kasisi Jesse Jackson penye roshani ya hoteli hiyo. Dr, King alipigwa risasi na kufa papo hapo.

Mtu aliyempiga risasi James Earl Ray ambaye alikuwa ni Mzungu alikamatwa baadaye mjini London, Uingereza na kufungwa maisha hadi alipofia jela mwaka 1998 lakini jamii ya Watu Weusi kote duniani ilikuwa imepoteza kiongozi shupavu ambaye pengo lake halijazibwa hata leo.

Steve Biko, Chris Hani, Samora Machel, Shabbaz Malcolm X wote hao ni Watu Weusi waliouliwa katika mazingira yaliyogubikwa na uhasama wa ubaguzi wa Waafrika.

Na sasa tukiingia katika karne ya Sayansi na Teknolojia, ajabu ni kwamba huko Marekani limeibuka Kanisa moja linaloundwa na Wazungu tu huku mkakati wao mkuu ukiwa ni kuifutilia mbali mbegu nyeusi kutoka kwenye uso wa dunia.

Kanisa hilo linalojiita THE CHURCH OF CREATOR wakimaanisha Kanisa la Muumba linaongozwa na Mzungu Benjamin Nagli Smith ambaye kwa asili anawachukia Watu Weusi kwa kiasi kikubwa.

Msimamo wa Kanisa la Muumba unasema kuwa "Mtu yeyote Mweusi ni wa matope hivyo hana thamani na hastaili kuwepo juu ya uso wa dunia"

Kanisa la Muumba limepania kufutilia mbali rangi ya mtu mweusi kwa kuwaua na kuzidi kuliinua taifa wanalotaka kuliunda na Watu Weupe ambalo kwa madai yao wanasema kuwa ndio wenye haki ya kuikalia dunia.

Kiongozi wa mauaji wa Kanisa hilo la ajabu Smith mwenyewe hivi majuzi alikamatwa na polisi nchini Marekani katika eneo la Salem jijini Chicago jimbo la Illnois akiwa kwenye pilika za kutorekea baada ya kufanya mauaji.

Smith aliyepata kutumika kwenye operesheni nyingi za mauaji ya kikundi hicho siku aliyokamatwa kwenye kiunga cha SALEM, ilikuwa yapata ndiyo ametoka kuwapiga risasi waumini 3 wa Kanisa la Orthodox wenye asili ya Kiyahudi. Pia siku hiyo alikuwa amempiga risasi mwalimu wa zamani wa mpira wa vikapu katika Chuo Kikuu cha Chicago mwalimu huyo aliyempigwa risasi kadhalika alikuwa ni mtu mweusi.

Kabla ya kuua watu hao tayari Smith ameishahusishwa na matukio kadhaa ya mauaji ya Watu Weusi ndani na nje ya Marekani.

Kanisa la Muumba "The Church of Creator’ kama wanavyojiita wameamua kuwa wanataka kuendesha mapambano dunia nzima ya kuhakikisha kuwa mbegu ya Mtu Mweusi ambayo ni ya matope kama wanavyodai inafyekwa na kutoweka yote tukiingia kizazi kipya.

Kiongozi wao mkuu Nacht Feell alipohojiwa na Shirika la Habari la REUTERS kuhusu nini sera, zao alikuwa na haya ya kusema.

"Sera zetu hazijatofautiana sana na za wakoloni wa Kizungu waliotawala huko Afrika, katika kipindi cha miaka iliyopita. Kwetu Mtu Mweusi ni sawa na nyani tu"

Alipotakiwa Kueleza matatizo yao, alisema kuwa matatizo yao ni kumpendelea zaidi Mtu Mweupe kuliko Mtu Mweusi.

Kiongozi wa Kanisa la Muumba amesema kuwa pia wanalaani vikali kumalizika kwa utawala na sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, kwani ambacho Makaburu Weupe walikuwa wakiwatendea Waafrika nchini humo ni kile ambacho Mtu Mweusi alistahiki kabisa.

Hata hivyo wamesema operesheni ya kufyeka mbegu ya matope (mtu mweusi) wataitekeleza kimya kimya ili kukwepa kuzusha vita vikubwa .

"Tunataka kuwamaliza kimya kimya pasipo kuzusha vita"alisema Feill.

Mpaka sasa wamekiri kuwa ni muuaji wao ndie aliyemuua kijana mmoja Mweusi jimboni India tena kwa kumfunga kwa kamba kwenye gari na kisha kumburura bila ya huruma hadi akakata roho. Pia muuaji wao mashuhuri aitwaye Smith ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi amekiri kuwa ni yeye aliyemuua mhamiaji mmoja mwenye asili ya Kiafrika nchini Marekani kwa kumpiga risasi 30.

Genge lao la Mauaji sasa limekuwa tishio kwa Watu Weusi katika miji mikubwa ya Marekani kama New york,Washingon DC, Detroit, Chicago, San Francisco, Los Angeles, na Dallas huko Texas.

Katika kile kinachodhihirisha wazi kuwa kikundi hiki hatari kina mikono yake mpaka Ulaya , jijini London, Uingereza nako pia tayari kipo kikundi kingine mithili ya hicho ambacho kimeibuka na kusema kinataka kuhakikisha watu wote wenye ngozi nyeusi nchini Uingereza wanauawa.

Kikundi hicho cha London tayari kimehusika na mauaji ya kikatili ya msichana mmoja Mweusi mwenye asili ya Carribean ambaye alipigwa risasi ndani ya basi mjini London. Kanisa la Muumba ambalo siyo la kawaida kwa itikadi zake za kuua Weusi limeazimia kuifanya dunia kuwa ya Wazungu pekee.

Majibu ya Kikatoliki kwa vikundi vya Kilokole(5)

ILI kuwaelimisha Wakristo Wakatoliki juu ya tofauti ndogondogo zilizopo kati ya Mafundisho ya Kanisa lao na yale ya Kilokole, tumeamua kukichapisha kijitabu hiki kiitwacho" Majibu ya Kikatoliki kwa Vikundi vya Kilokole" ambacho tunaamini kitaleta mwanga wa kutosha kwa wale watakaokisoma. Hii ni kwa sababu si wengi wawezao kukipata kijitabu hiki na kukisoma. Endelea na sehemu ya tano...

inatoka toleo lililopita

2.MAFUNDISHO YA KIKATOLIKI

a) Kuingizwa katika utu uzima, kuingizwa kaitka ukristu.

Kadiri ya mapokeo ya Kiafrika, vijana wanatakiwa kupitia mfumo mrefu wa malezi ya kuangalia katika utu uzima, ili kufikia mtu kamili na kuwa muumini kamili katika jamii hiyo.

Mtu anayetaka kujiunga na Kanisa anapaswa kupitia hatua ya kuingizwa katika Kanisa hilo, hatua ambazo zinahusiana na mambo matatu.

1. Kuikubali Imani ya Kikristu na kuwa mwanajumuiya hiyo.

2. Kushiriki taratibu mbalimbali za kiliturujia,

3. Kuchagua njia ya maisha inayofaa kwa kuwa Mkristu.

Njia hiyo ya kuingizwa katika ukristu imewekwa kwa ajili ya watu wazima wenye akili na utashi wa kuamua na kuchagua mwenendo wa maisha yao (ili kubatiza watoto wachanga, masharti kadhaa yanahitajika ambayo tutayaona baadaye) Njia hii ya uchaguzi na maandalizi yake inaitwa’ "Ukatekumeni", inaweza kuchukua miaka kadhaa.

Hatimaye tunayo maadhimisho ya Sakramenti tatu za kuingizwa katika Ukristu: Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu. Wakati mwingine Sakramenti hizo huadhimishwa pamoja. Kuhusu watoto wachanga kikawaida Sakramenti za Kipaimara na Ekaristi takatifu huahirishwa.

B) Ubatizo ni mlango wa kuingilia kanisani.

Ubatizo ni Sakramenti ambayo:

1: Inatuunganisha na Kanisa

2.Inatupatia neema (Uzima mpya kama mtoto wa Mungu) papo hapo kufutiwa dhambi ya asili na dhambi nyingine tunazotenda.

3)Inaimarisha Imani, yaani kule kumkubali kwetu Kristu kama mlinzi wa maisha yetu yote.

Ubatizo ni wa muhimu kwa wokovu wetu na pia wa lazima kwa kupokelewa katika kanisa kwani Bwana alituambia "Aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini, atahukumiwa" (Mk. 16:16) lakini ni hakika kwamba licha ta ubatizo inawahusu wale wasiomjua bado Kristo au Kanisa sawa sawa lakini bado ni watu wema, hawa nao pia wanaokolewa.

C)Maji ni alama inayojitosheleza.

Ubatizo maana yake ni kuzamishwa katika maji au kuoshwa. Ni lazima katika Kristu kujazwa na roho wake na anayeishi ndani yake anatakaswa na kufanywa upya naye. Maji hasa kwa sababu ya sifa yake ya kutakasa na kueneza uzima (bila maji kila kitu hukauka na kufa),hakika ni alama inayojitosheleza.

Katika Agano la Kale, maji yanatajwa daima. Muhimu zaidi maji yanatajwa katika tukio ka kuvuka Bahari ya Shamu ambayo kwa Waebrania tukio hilo lina maana ya kuokolewa kutoka utumwani na kuanza maisha mapya kama watu huru.

D) Kristo ni wa Ubatizo.

Yesu:

*alibatizwa na Yohane

*aliongelea juu ya ubatizo mpya.

*Aliuanzisha ubatizo huo mpya.

Kubatizwa kwake Yesu na Yohane kulikuwa ni kielelezo cha ubatizo ambao Yesu mwenyewe alitarajia kuanzisha baadaye wainjilisti wote wanauelezea ukweli huu. Yesu alipobatizwa ; Utatu Mtakatifu ulifunuliwa na Yesu mara akaanza kazi yake hadharani. Daima Yesu alizungumza juu ya maji (Yoh.4:13-14; Yoh. 9) Akizungumza na Nikodemo, Yesu aliwapa wafuasi wake amri ya kuwabatiza: "Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkibatizwa kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu" (Mt. 28:19-20), na jumuiya ya kwanza ya Wakristu ilianza mara moja kazi ya utume.

E) Ubatizo wa watoto wachanga.

Ubatizo unahitaji uamuzi thabiti wa mtu binafsi wa kumfuata Kristu. Kutokana na sababu hiyo, hatuwezi kuwabatiza watoto wachanga isipokuwa kwa sheria kwamba wazazi wao (au angalau mmoja wao) anachukua jukumu la kuwalea katika maisha ya Kikristu. Ili kuwasaidia katika jukumu hili, wasimamizi huchaguliwa. Wasimamizi hawa wanapaswa kuwa Wakristu hodari wa kuweza kuwasaidia watoto hao kwa mfano kwa ushauri, kuishi kadiri ya imani yao. Katika adhimisho la ibada yenyewe wajibu huu kwa wazazi na wasimamizi huelezwa waziwazi.

Sura ya Saba

Sakramenti ya Kitubio (Upatanisho)

1. Mtazamo wa Kilokole

Mungu peke yake anaweza kusamehe dhambi; na msamaha wa Mungu hautegemei Sakramenti yoyote iliyowekwa na kanisa. Agano Jipya liinatuonyesha jinsi Mungu anavyotusamehe, yaani ni kwa njia ya Yesu Kristu.

*Lakini Kanisa Katoliki limejiongezea mfumo wake wa kibinadamu ili kumiliki msamaha wa Mungu. Ni wazi mtindo huo kwa kiasi kikubwa unaongeza nguvu za mapadre na kuzuia nguvu zote za Mungu za kusamehe.

2)Mafundisho ya Kikatoliki.

a) Msamaha wa dhambi katika dini.

Katika kila dini, watu wanajitafutia washenga ili kuomba msamaha wa Mungu. Watu wanatumia sala na sadaka zao kuomba huruma ya Mungu

b) Sisi tu Wakosefu

Katika Agano Jipya utambuzi wa dhambi umekuwa wazi sana. Sisi sote ni wadhambi isipokuwa Kristu, ambaye hakutenda dhambi na "aliyejaa neema" sisi tumemkosea Mungu na "Ulimwengu wote" upo "chini ya hukumu ya Mungu" (Rum.3:19).

Dhambi ni tendo la choyo, ubinafsi kukataa kumpenda Mungu matendo yetu hata hivyo si matukio yaliyotengwa; ni matendo yanayoeleza hali zetu za daima, namna tulivyo au hali halisi kwetu. Hii inaweza au kuimairishwa au kubadilishwa kwa kila tendo tutakalolifanya. Dhambi ni adui mkubwa wa utu wema.

Kwa kutenda dhambi watu wanajidhuru wenyewe na jumuiya wanamoishi, yaani kikundi, kanisa, binadamu (wengine).

c) Mungu anatupenda na anatusamehe.

Mungu anatualika kwenye toba na anatusamehe:

"Hakutenda sawasawa na hatia zetu wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu....

Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao kwa maana yeye anatujia umbo letu, na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi"(Zab.103) Mungu anapenda unyofu wetu; anatuita; "Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi " (Am.5:40) Yesu alitufundhisha kwamba Mungu anasamehe kama baba aliye mwema. Yesu mwenyewe aliwasamehe kila mmoja aliyetubu: kwa mfano mtu aliyepooza, mwanamke mkosefu, mwanamke mzinifu, Zakayo mtoza ushuru, mwizi aliyetubu. Aliwakaribisha wadhambi na kula nao.

D) Yesu alilipatia kanisa lake kazi ya kusamehe dhambi.

Yesu aliwapa mitume uwezo wa "kufunga" na "kufungua" (Mt. 16:19; 18:18). Jioni ya siku ya ufufuko wake aliwatokea wanafunzi wake ghafla wakiwa katika chumba (ghorofani); alipowauliza Roho Mtakatifu wafuasi wake na kuwaambia: "pokeeni Roho mtakatifu wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa (Yoh.20:22)

kanisa linaendeleza kazi hii ya kusamehe dhambi hasa katika sakramenti ya kitubio(Upatanisho),

e)Matendo ya msngi kwa kuandimisha sakramenti ya Upatanisho

I) utafiti wa Dhambi

hii ina maana ya kukumbuka dhambi amabazo mti amezitenda, au kukiri dhambi alizozitenda. Baada ya kujitafiti hakuna haja ya kuchelewa ktika hatua hii

i)Majuto.

Hii ina maana ya kukiri makosa (dhambi) mmoja aliyoyatenda na kupatwa na uchungu kwa kumkosea mungu. Toba ya juju juu (Kuhusu hasara au tatizo lililosababbisha na dhambi zetu) haitoshi kinachotibu hasa ni unyoofu wa "kumrudia" Mungu Majuto (au uchungu kwa sababu dhambi) ni jambo muhumu sana katika sakramenti hii. Hakika mara baada ya dkufanya toba ya kweli tunakuwa tayari tumeatanishwa na Mungu. Upatanaisho huu tunafurahia baada ya kuupokea Sakramenti hii.

Hii ni hatua ya kumweleza mwunganishai dhambi zetu. Wakatia fulani Sakramenti hii kwa ujumla iliitwa; "muungano" Lakini kumbe kuungana ni sehemu tu ya Sakramenti yenyewe na si sehemu iliyo ya muhimu sana akwa upande wa dhambi za mauti, hata hivyo toba ni ya lazima isipokuwa katika masuala magumu zaiodi. Ni kawaida , kila anayetubu dhambi zake atapenda kumweleza mtu mwingine . hii inaonyesha kwamba atapenda mumweleza mtu mwingine. Hii inaonyesha kwamba mtu anachukia dhambi. Zaidi ya hayo kama mwungamishi anataka kumwondelea mtu dhambi katika jinala Mungu na la Kanisa, atahitaji kujua kuhusu dhambi na majuto yake.

Iv)Toba

hii ina dmaana ya kukusudia kuacha dhambi.toba ina lengo la kusafisha masalia ya dhambi (maelekeo mabaya) ambayo yameachwa na dhambi ndani yetu na kurudisha hasara waliyotendwa watu wengine.

V) Maendeleo ya Dhambi

hii ni alama ya kielelezo cha msamaha wa Mungu na wa Kanisa Mwungushi anayataja maondoleo hayo kwa maneneo na ishara . mwunganishi kwa kumwelekezea mikono juu ya kichwa cha dfyule anayeungama anamwondolea dhambi zote "kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu."

 Mtakatifu Maria Goreti Bikira na mfiadini wa Ankona Italia

Alishindikana kubakwa kachomwa visu 18

Madaktari walishangaa kuona hakufa

Na Mwandishi Wetu

ILIKUWA Jumamosi ya Julai 15,1902, Maria Goreti; mtoto wa kwanza kati ya sita wa Aloisi Gorei na Asunta Karlini; aliyezaliwa Oktoba 16,1890 na sasa akiwa na umri wa miaka 12, alikuwa ameketi juu ya ngazi ya nyumba yao akishona nguo.

Aleksanda; kijana aliyeishi katika nyumba aliyokuwa anaishi mtoto (Maria Goreti) ambaye wazazi wake walikuwa wakulima fukara lakini wenye imani isiyotetereka, alimpita na kuingia chumbani. Muda mfupi tu, Aleksanda alirudi na kumnong’oneza kwa sauti ya chini; "Maria njoo humu chumbani" haraka. Maria aliitambua nia mbaya aliyokuwa nayo kijana huyu. Akamjibu;"Nije kufanya nini?" Aleksanda akazidi kusema kwa hasira "njoo humu ndani" Nae Maria Goreti akaendelea kushikilia msimamo wake, "Siji; chumbani humo siingii"

Alipokwisha kusema hayo na kutaka kuondoka Aleksanda alimrukia na kumkamata mkono akimvuta chumbani mtoto huyo aliyebatizwa siku moja baada ya kuzaliwa kwake na kupewa jina la Maria. Kisha Aleksanda akafunga mlango.

Maria Goreti ambaye baba yake alifariki kwa ugonjwa wa malaria na kumuacha angali mdogo chini ya uangalizi wa mama yake aliyemfundisha kusali, Hata alipokuwa na akili alijifunza Katekisimu, alimshuhudia rafiki yake Teresia Chimarei yaliyotokea humo chumbani akasema;

"Alipotaka tutende jambo baya, nilimkatalia; nikasema siji; sitaki kabisa. Aleksanda; ukifanya hayo utatupwa motoni mwa milele. Lakini yeye hakunisikia basi akanichoma kisu na kunitia majeraha mwili mzima" Hata baadaye Aleksanda mwenyewe alikiri na kusema, " Nilipokusudia uovu huo nilijua dhahiri ninatenda jambo linalokatazwa na Mungu. Nilitaka Maria akubali kutenda dhambi nami,ikabidi nimuue kwa sababu alinikatalia"

Madaktari waliomtibu mtoto huyo ambaye kutokana na ufukara wa wazazi wake hakubahatika kujiunga na shule kama watoto wengine, walibainisha majeraha 18 ya kisu mwilini kwake hali 9 yakiwa yameenda ndani sana ya mwili ni wake.

Madaktari hao walistaajabu sana kuwa mtoto Maria Goreti ambaye mifano na matendo ya mama yake yalikuwa shule bora kwake iliyomfanya aishi kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu hakufa palepale nyumbani baada ya kujeruhiwa kwa kisu namna hiyo.

Asubuhi iliyofuata, Maria ambaye katika maisha yake hakutenda mambo ya ajabu bali tu; ya kawaida ila kwa uangalifu mkubwa huku akidumisha hali ya utiifu na kuwa msaidizi hodari wa mama yake, alikuwa amedhoofika sana. Hali yake ikazidi kuwa mbaya na hata ikabidi Padre ampatie Komunyo Takatifu.

Fadhila kuu za moyo wa msichana huyu zilikuwa unyenyekevu, Ukunjufu na Usamehevu. Kinywani kwake kamwe halikutka neno la Uongo.

Alitunza usafi wa mwili na roho yake. Maria kamwe hakuwa na hasira wala kisasi kwa Aleksanda bin Serenali; kijana aliyekuwa na mazoea yasiyo mema na asiyeweza kujishinda hali iliyomfanya shetani wa tamaa mbaya asikawie kuuona udhaifu wake; akamjia na kumpandikiza tamaa ya kutaka kulala na Maria Goreti, hata baada ya kumbembeleza lakini akashindwa na kuamua kutumia nguvu, mama yake pamoja na Padre walimuuliza.

"Maria unamsamehe Aleksanda kwa uovu na ukatili alioutenda?" Maria mwenyewe akajibu; "Ninamsamehe kwa moyo wangu wote na kumuombea atubu"

Jioni hiyo Maria Goreti alikata roho. Mazishi yake yalikuwa kama maandamano ya furaha. Maelfu ya watu walikuja kumpa heshima zao msichana huyo Mtaktifu aliyeshinda dhambi kwa mauti.

Aleksanda alihukumiwa kutumikia kifungo jela kwa miaka 30. Hata hivyo baada ya kutumikia kifungo hicho kwa miaka 27 aliachiliwa huru.

Jambo la kwanza alilojitahidi kufanya kijana huyu ni kwenda kumtembelea mama yake Maria Goreti na kumuomba radhi ili amsamehe.

Wakuu wa Kanisa walichunguza habari za maisha ya Maria Goreti na mnamo Aprili 27,1947 watu walijaa katika kanisa la Makatifu Petro huko Roma wakingoja kuishihudia ibada ya kumtangaza Maria kuwa miongoni mwa Wenyeheri.

Miaka mitatu baadaye yaani mwaka 1950 Papa alimtangaza Maria Goreti kuwa Mtakatifu bikira na mfiadini.Muuaji wake (yaani Aleksanda) alikuwa bado yungali hai wakati Maria Goreti anatangazwa kuwa Mtakatifu.

Wakristo Wakatoliki maisha na uimara wa imani ya Mtakatifu huyu ni mfano kwetu.