Wakatoliki na  Urais wa Marekani

l                 Alianza Al Smith, Kennedy na sasa John Kerry

WAKATI taifa kubwa kama Marekani linaaminiwa na walimwengu kwa kuwa na demokrasi ya hali ya juu. Kuna ubaguzi wa kidini katika kuchagua marais. Moja ya madhehebu ya dini ambayo yalibaguliwa kwa muda mrefu ni Wakatoliki. Ili kujua mtazamo wa Wamarekani juu ya rais Mkatoliki fuatilia makala haya kama ilivyoandikwa na Erick Samba.

Wakati Seneta John F. Kennedy wa Massachusetts alipogombea urais mwaka 1960, alikabiliana na mashambulizi ya maswali kutoka kwa Waprotestanti, maswali kama, “Tunajuaje kwamba unaweza kutenganisha imani yako ya Kikatoliki na wajibu wako wa kisiasa?”

Lakini mgombea wa sasa, Seneta John F. Kerry pia wa Massachusetts mambo hayatakuwa hivyo; ila yeye maswali yake yatatoka kwa Wakatoliki wenzake na huenda yakawa kama: “Ni jambo gani linalokufanya udhani kwamba unaweza kutenganisha imani yako ya Kikatoliki na majukumu yako ya kisiasa unapofika wakati wa kupigia kura utoaji mimba?”

Mambo mengi kuhusu maseneta hao wawili wa Massachusetts yanaweza kuwa sawa, ila hali ya hewa ya kisiasa na kidini ya Kerry inafanana kidogo sana na ile aliyokabiliana nayo Kennedy.

Kati ya zama za Kennedy na Kerry kulitokea hukumu ya Mahakama Kuu kuhusu utoaji mimba na kuongezeka kwa uangalizi wa baadhi ya watu katika kanisa kuhusu kura za wanasiasa Wakatoliki bungeni.

Kerry kama mgombea urais wa pili kutoka chama kikubwa akiwa Mkatoliki katika historia, alichokabiliana nacho Kennedy kabla ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ulikuwa ni umma wa Wamarekani ambao ulitaka kuhakikishiwa iwapo Baba Mtakatifu asingekuwa anaongoza serikali ya Marekani.

Lakini Kerry, kwa upande mwingine, ni Mkatoliki ambaye atatakiwa kutetea msimamo wake kwa nini huwa hajali mafundisho ya Kanisa pale anapopiga kura katika bunge la Seneti, hasa kuhusiana na kuunga kwake mkono utoaji mimba kuendelea kuwa halali kisheria, wakati mafundisho ya kanisa yanapinga vikali.

Kabla ya Kennedy kuwa mgombea urais wa Marekani na kushinda, kulikuwa na mgombea mmoja tu Mkatoliki aliyekuwa amewahi kugombea kiti hicho. Huyo sio mwingine bali ni Gavana wa New York wakati huo, Al Smith ambaye hata hivyo alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 1928.

Katika hotuba yake kwenye bunge la Seneti hapo Januari 1928, Seneta Thomas Heflin wa Alabama, alionya kwamba, Wakatoliki walikuwa wanajaribu kukiteka chama cha Democratic ili kupinga “Ku Klux Klan” au utaratibu wa Kiprotestanti na kwamba walikuwa wanajaribu kudhibiti magazeti ya kusini mwa Marekani ili kumwimarisha mgombea wao wa urais, Gavana Smith.

Alisema, “azimio la Kikatoliki limetolewa katika makala ya siri kwamba ‘Al Smith atafanywa rais. Wataweka mkono mzito wa dola ya Kikatoliki juu yenu na kufutilia mbali maisha yaliyotokana na Uprotestanti katika Marekani.”

Hali hiyo ya wasiwasi na hofu juu ya Wakatoliki, iliibuka tena miaka 32 baadae, wakati Seneta John Fitzgerald Kennedy wa Massachusetts alipoanza mbio za kuelekea Ikulu ya Marekani mwaka 1960.

Kwa mfano Kanisa la Kibaptisti la Kusini mwa Amerika, lilipitisha azimio la pamoja kuelezea hofu yake iwapo Kennedy au Mkatoliki anapaswa kuwa rais wa Marekani.

Tamko jingine lililosainiwa na wachungaji pamoja na walei 150 wa Kiprotestanti wakiongozwa na Mchungaji Norman Vincent Peale, lilisema kwamba, rais Mkatoliki angekuwa chini ya ushawishi mkubwa wa hairakia ya kanisa lake na kuoanisha sera ya mambo ya nje ya Marekani na ile ya Vatican.

Hata hivyo, Rais Harry Truman alilaani hali ya kutovumiliana kidini, ingawa mwanzoni alikuwa amepinga uteuzi wa Kennedy kwa sababu ya kutoelewana na baba yake, Joseph P. Kennedy aliyekuwa amewahi kuwa balozi nchini Uingereza.

Truman alisema, “Siko kinyume na Baba Mtakatifu. Niko kinyume na Pap,” akimaanisha Kennedy mkubwa.

Hata hivyo, John F. Kennedy alitatua suala la Ukatoliki katika hotuba yake kwa njia ya televisheni, Septemba 1960, aliposema ukomunisti, umaskini, elimu na sayansi ya anga za juu, yalikuwa ndiyo mambo muhimu sana ya kujadili katika uchaguzi lakini yalikuwa yamefunikwa na mjadala juu ya Ukatoliki.

Alieleza imani yake katika Marekani, ambamo utengano kati  ya kanisa na dola ni mkubwa. Hakuna askofu Mkatoliki anayeweza kumwambia rais (iwapo ni Mkatoliki) namna ya kutenda na hakuna mchungaji wa Kiprotestanti angeweza kuwaambia waamini wake ni nani wa kumpigia kura.

Kennedy aliwataka wapiga kura kumhukumu kwa kufuata rekodi yake ya kisiasa, na sio kufuata nukuu zilizochaguliwa kwa uangalifu kutoka kwenye kauli na taarifa za viongozi wa kanisa.

Hata hivyo, alikubali tamko la maaskofu Wakatoliki wa Marekani la 1948 ambalo lilisisitiza utengano kati ya kanisa na dola.”

Alisema kuwa yeye hakuwa mgombea urais kwa tiketi ya Wakatoliki. “Mimi ni mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Democrat, ambaye pia nimetokea kuwa Mkatoliki. Siongei kwa niaba ya kanisa langu katika masuala ya umma, na kanisa haliongei kwa niaba yangu.”

Maneno haya yalimsaidia Kennedy kushinda kwa tofauti ndogo. Majivuno ya Wakatoliki kwa kuwa na rais ambaye alikuwa mmoja wao yaliashiria mwisho wa muda ambao walijihisi kutengwa kisiasa.

Hakuna wakati wowote ambao tungeweza kumwona mtu akisema, “Baba Mtakatifu atakuwa akiongoza nchi,” alisema Clyde Wilcox profesa wa Chuo Kikuu cha Georgestown.

Hata hivyo, jitihada za Kennedy kutenganisha dini yake na wajibu wake hazikujulikana kwa Wakatoliki. Wala viongozi wa kanisa hawakuwa wakifurahishwa na upinzani wake wa ajenda ya maaskofu, kama kumrudisha balozi wa Marekani katika Vatican.

Baada ya Kennedy kuvunja mwiko, hatua ya kuwajumuisha Wakatoliki kama wagombea wa umakamu wa rais lilikuwa jambo la mara nyingi japo halikufanikiwa, lilikuwa ni mkakati wa vyama vyote viwili katika uchaguzi tangu mwaka 1964 mpaka 1972.

Kwa upya, “suala la Ukatoliki” lililipuka upya mwaka 1984 juu ya wanachama wawili wa Democrat kutoka New York, mwakilishi Geraldine Ferraro na Gavana Mario Cuomo.

Tangu siku yake ya kwanza ya kampeni kwa ajili ya nafasi ya makamu wa rais, kama mgombea mwenza wa Walter Mondale wa Minnesota, Ferraro aliulizwa kwamba anawezaje kuwa  Mkatoliki safi na huku anapiga kura kama alivyokuwa amefanya awali kuunga mkono uhalalishaji wa utoaji mimba.

Askofu Mkuu wa New York, Mhashamu John J. O’Connor, ambaye baadae alikuwa kardinali, alikwaruzana waziwazi na msimamo huo kuunga mkono serikali kufadhili utoaji mimba, kwa maelezo yake kwamba anatenganisha mafundisho ya kanisa na wajibu wake kwa umma.

Tangu wakati huo wanasiasa Wakatoliki wamekuwa wakiegemea hoja kwamba: “Mimi binafsi napinga utoaji mimba, lakini simaanishi kwamba ninapaswa kutunga sheria ya imani yangu ili kufanya utoaji mimba kuwa halali katika nchi hii.”

Mwaka 1990, Kardinali O’Connor alisema kuwa, hoja za namna hiyo zitawafanya wanasiasa Wakatoliki kutengwa, ingawa alisema yeye na maaskofu kama kundi, wanasisitiza ushawishi kwa wanasiasa ili wabadili msimamo badala ya kuwatenga.

Muda mfupi kabla ya kutajwa kama mkuu wa jimbo kuu la St. Louis Desemba iliyopita, Askofu Mkuu Raymond L. Burke aliwaambia mapadre katika jimbo la La Crosse, Wisconsin, kuwanyima Ekaristi wanasiasa Wakatoliki ambao hawafuati mafundisho ya kanisa juu ya utoaji mimba na euthanasia (kifo cha huruma).

Askofu Mkuu wa Boston, Mhashamu Sean P. O’Malley alisema kwamba wanasiasa Wakatoliki wanaounga mkono utoaji mimba, wanapaswa kuacha kupokea komunyo kwa hiari, ingawa alisema kanisa halinyimi sakramenti hiyo kwa watu wanaoijongea altare, kwa kuamini kwamba wanafanya hivyo, “kwa imani safi.”

Mwaka 2003, nyaraka mbili zilizotolewa na Vatican ziliwataka wanasiasa Wakatoliki kuwa na jukumu kubwa na wazi la kupinga sheria ambazo zinakiuka mafundisho ya kanisa kuhusu haki ya uhai au ndoa za jinsia moja.

Kwa wakati huu ambapo John Kerry anatarajiwa kuwa mgombea urais wa kwanza Mkatoliki katika miaka 44, baadhi ya makundi ya kutetea uhai yanamshinikiza Askofu Mkuu O’Malley na maaskofu wengine kumzuia kupokea komunyo takatifu kwa sababu hafuati mwongozo wa kanisa juu ya utoaji mimba.

Katika kitabu chake cha mwaka 2003, “Mwito kwenye Huduma,” Kerry alijieleza kama “Mkatoliki anayeamini na kuishi imani yake.” Yeye pamoja na mkewe, Teresa Heinz Kerry, mara nyingi huhudhuria misa Jumapili.

Kerry ambaye aliachana na mkewe wa kwanza mwaka 1988, baadae alisema kwamba alikuwa akitafuta ubatilisho wa ndoa yake. Lakini mpaka sasa haikujulikana kama ubatilisho huo ulifikiwa na majimbo ya Kikatoliki huwa hayatangazi masuala hayo hadharani.

Mke wake wa sasa alibaki mjane baada ya kufiwa na mumewe Seneta John Heinz wa Pennsylvania (Republican), alikufa katika ajali ya ndege mwaka 1991.

Katika kura za hivi karibuni kwenye bunge la Seneti, Kerry alipinga miswada ya kupiga marufuku utoaji mimba, akaunga mkono uondoaji wa marufuku ya utoaji mimba katika maeneo ya jeshi la Marekani, nchi za nje na kuunga mkono azimio na kudhibitisha kwamba hukumu ya kuhalalisha utoaji mimba. Misimamo yote hiyo ni kinyume na ule wa kanisa lake.

Kuhusu masuala mengine, misimamo ya Kerry karibu inafanana na misimamo inashawishiwa na kanisa. Kwa mfano, huwa anapinga adhabu ya kifo isipokuwa kwa magaidi.

Mafundisho ya kanisa ya hivi karibuni yanasisitiza kwamba, katika jamii ya kisasa hakuna mazingira ambamo adhabu ya kifo ni lazima.

Majibu ya Kerry juu ya shutuma dhidi yake kutokana na kupuuza mafundisho ya Kikatoliki kuhusu utoaji mimba, yatajengeka katika mwenendo wa kampeni zake. Ingawa kauli moja aliyoitoa mwaka jana inarudia kile alichosema Kennedy miongo kadhaa wakati akijibu shutuma tofauti kabisa, lakini zenye msingi wa kidini.

Shirika la habari la Associated Press lilimnukuu Kerry hapo Agosti mwaka jana akitoa maoni yake kuhusiana na waraka uliotolewa na Vatican ambao uliwataka wabunge Wakatoliki kupinga ndoa za jinsia moja.

“Ninaamini katika kanisa na ninalijali sana. Ila nafikiri kwamba ni muhimu kanisa kutowaelekeza wanasiasa nini cha kufanya. Huko ni kuvuka mpaka ambako sio sawa nchini Marekani.”

Sababu kumi za kuzaa mtoto

BAADHI ya watu wamekuwa wakiwaona watu wengine hasa watoto wadogo na watoto ambao hawajazaliwa kama “magugu watu” wanaokwaza ustawi wa watu wengine duniani hivyo, wanastahili kuondolewa kabisa au kuzuiliwa wasizaliwe.

Watoto wanaowekwa katika janga hilo, wanauawa ama wakiwa wamekwishazaliwa, au hawajazaliwa kwa njia ya utoaji mimba. Watu wengine wanatumia juhudi kubwa kuhakikisha kuwa, hawazai mtoto hata mmoja., ili wafaidi maisha. Lakini je, wanajua vyema faida za kupata watoto? Ungana na MWANDISHI WETU katika makala hii ujue sababu kumi za kupata mtoto. Wakati hayo yakiendelea, Makala hii inazitaja sababu kumi,  za kuzaa watoto. Huku makala ikisisitizwa na Kanisa na jamii kuwa uzazi bora ni ule unaozingatia idadi ya watoto ambao wazazi watamudu kuwalea na kuwapa huduma muhimu za Kijamii hadi wanapojitegemea

 

Biblia Takatifu inatuambia kuwa watoto ni baraka kutoka kwa Mungu na ndivyo walivyo.

Lakini, tunaishi katika ulimwengu unaochukia uzao. Utetezi wa kifo umekengeusha thawabu ya uzazi wa mtoto na kuuona uzao kuwa ni chukizo la mlipuko wa watu. Wazazi wa Kikristo mara kadhaa huhitaji kuhamasishwa ili wakubali thawabu za ziada.

“Tazama wana ndio urithi wa Bwana Uzao wa tumbo ni thawabu” (Zab 127: 3).

 

Sababu ya Kwanza

 

Pata mtoto  ili uungane na Mungu katika kuumba.

 

Zaeni mkaongezeke

Wazazi wamepewa jukumu maalum na Mungu la kusaidia kuumba roho isiyokufa. hata malaika hawajapatiwa neema hiyo.

Mtu mashuhuri duniani ni mama. Hawezi kujivuna kuwa amejenga Kanisa Kuu pekee. Lazima awe amejenga kitu kingine cha fahari zaidi kuliko Kanisa Kuu (Katedrali); makazi ya roho isiyokufa, mwili mkamilifu wa mtoto wake.

Hata malaika hawajapatiwa neema hii. “Ni nini lililo tukufu zaidi ya hili kuwa mama?”

 

Sababu ya pili

 

Hakuna furaha iliyo kubwa zaidi  kama kumkaribisha mtoto mwingine katika maisha yako.

Utashangazwa na jinsi mtoto wako alivyoumbika kwa ukamilifu na jinsi utakavyompenda. Utafurahiwa na kila sehemu ya mwili wa mtoto wako.

Rangi ya nywele zake umbile la pua yake na tabasamu lake lisilo kifani na utaongea juu ya upande wako au wa mumeo.

Katika hali ya shukrani, kuzaliwa kwa mtoto kutakufunga zaidi kwa Mungu kuliko ilivyokuwa kwanza. “Ulikuwa muujiza wa ajabu uliowahi kutokea katika maisha yangu,” aliwahi kuandika Whittaker Chambers kuhusu binti yake  katika kitabu cha Witness na katika maisha ya wengi wetu.

“Nilifikiri kuwa siku moja nitakuwa msanii na kutengeneza kazi maarufu sana, badala yake, Mungu amenifanya kuwa mama na watoto wangu; ndio zao lake bora. Maumbo ya maisha yao yatadumu baada ya kifo changu. Kilichopangwa mioyoni mwao kitadumu milele.” (mtu aliyeyasema haya, hajulikani).

 

Sababu ya tatu

 

Pata mtoto  ukue katika utakatifu na thawabu.

Kwa wale wanaoamini na kuwa na familia, Mungu huwapatia watoto kama njia ya kuwakuza katika utakatifu na thawabu.

Watoto huwafundisha wazazi wao uvumilivu, subira, upendo na unyenyekevu. Wanawapatia wazazi wao nafasi ya kutekeleza kwa matendo  huruma ya kimwili na kiroho.

Watoto huzaliwa uchi nasi tunawavika, wenye njaa nasi tunawalisha, wenye kiu nasi tunawapa maji ya kunywa. Matendo haya yote tunapaswa kuyatenda kwa Mungu wa hawa “ndugu zetu wadogo” tunatenda kwanza kwa watoto wetu.

 Mtakatifu Katarina wa Sienna alipata maono. Mungu alimwingiza kwenye chumba kilichojaa misalaba na kumwambia achague mmoja.

Mtakatifu Katarina alichagua msalaba mkubwa na mzito zaidi, lakini Mungu alimwambia huo haukuwa wake”; huo ulitengwa kwa ajili ya wazazi wenye familia kubwa. 

 

Sababu ya nne

 

Pata mtoto usaidie kumaliza janga la utoaji mimba.

Mama Teresia wa Calcutta aliwahi kuulizwa juu ya njia bora ya kuendelea na shughuli za utetezi wa uhai, alijibu kwa uhakika wote, “Kuwa na familia kubwa na utii ndiyo njia bora ya kumaliza janga la utoaji mimba.” Sio vigumu kuelewa kanuni hii inavyofanya kazi.

Kwa kadiri tunavyokabiliana na uhaba wa watoto kutokana na matumizi ya vidhibiti mimba, kufunga kizazi na utoaji mimba, ndivyo jamii ya watu inavyopoteza viungo vya furaha na matumaini ambayo huletwa na watoto tu. Katika hali ya namna hii, vidhibiti mimba na utoaji mimba, vinajilisha vyenyewe kwa kadiri hao wachache wanavyozidi kupunguzwa. Kwa kuwa na mtoto unaonesha tena kuwa, mtoto ni zawadi kuu ya Mungu.

“Watoto hujenga maisha ya familia na jamii” kama ambayo Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, “Mtoto anakuwa zawadi kwa kaka na dada zake, wazazi wake na familia yote.”

Uhai wake wote huwa ni zawadi kwa watu wote ambao walikuwa watoaji wa uhai na ambao walilazimika kuonja uwepo wake, ushiriki wake katika maisha yao na mchango wake katika mambo mema na kwa jumuiya ya wanafamilia.”

Kwa kadiri jamii hii inavyokuwa ya watu wengi, ndivyo  hivyo jamii hii inavyokuwa ya watu watetea uhai, na ndiyo itakavyokuwa rahisi kupigana vita dhidi ya maovu na utoaji mimba.

 “Nazishuhudia mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana basi chagua uzima ili uwe hai wewe na uzao wako(Kumb 30:19)

 

Sababu ya tano

 Pata mtoto  ili watoto wako wa kiume na wa kike wapate wadogo zao.

Watoto wenye wadogo zao wanajifunza kushirikiana mapema katika maisha yao. Wanajifunza kutenda kwa zamu na kujali mahitaji ya wengine kabla yao wenyewe.

Undugu unaojengwa kati ya ndugu hawa ambao ni kaka na dada, ni wa kudumu, wa maisha na ni imara kulinganisha na ule wa marafiki “Tazama jinsi ilivyo vema na kupendeza ndugu wakae pamoja, kwa umoja.”

“Ni kama mafuta mazuri kichwani yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake” (Zab 133:1-2). Wavulana wenye dada zao wanajifunza kuwatendea wasichana na wanawake kwa heshima kama ambavyo wangependa dada kutendewa.

Wasichana wenye kaka wanajifunza kutambua ukamilisho wa wanaume na wanawake wote wakiwa wameumbwa kwa mfano wa Mungu.

 

Sababu ya sita

 

Pata mtoto  ili wewe na wazazi msibaki wapweke uzeeni

Watu wenye watoto hawahitaji kuwategemea watu wasiowajua katika uzee wao. Watoto pia watakuwa wazazi wa wajukuu wako. Wajukuu huleta furaha uchangamfu na kicheko wakati huo huo, wanakupatia nafasi ya usingizi mzuri. “Wana wa wana ndio taji ya wazee, na utukufu wa watoto ni baba zao” (Mith 17:6).

 

Sababu ya saba

 

Pata mtoto kwa vile watu ndio rasilimali kuu.

Binadamu wamejaliwa zawadi ya akili na utashi. Binadamu anao uwezo wa kupata majibu kwa matatizo mbalimbali yanayotokea. Watu wasiokuwa na watoto lazima wakumbuke kuwa daktari aliyetokana na wazazi wengine, ndiye atakayeweza kusalimisha maisha yao wanapohitaji matibabu.

Ni wazazi wa watoto wengi ndio watakaoweza kuzima moto nyumba yao inapoungua. Mhandisi wa reli atatoka katika familia ya watoto wengi.

 

Sababu ya nane

 

Pata mtoto  achangie uchumi.

Familia zenye watoto ni kama mafuta kwa uchumi, ununuzi wa nyumba, magari na wanachuo wa vyuo mbalimbali. Bila vijana kuingia katika ajira, mifumo ya usalama na huduma za jamii huanguka.

Bila watoto wa kusoma, walimu hawana kazi, viwanda vingi hutegemea watu kuviendesha. Bila watu, hatimaye uchumi huanguka. “Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao nyumbani mwa nyumba yako, wanao kama miche ya mizeituni wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo yule amchaye Bwana” Zab 128:3-4.

 

Sababu ya tisa

 

Pata mtoto  ili kukabiliana na ukame wa watu duniani

Yeyote aliyesafiri kutoka Pwani hadi Pwani ya Marekani na kuona mapori yasiyokuwa watu atagundua kuwa nchi hiyo haina mrundikano wa watu. Na kwa kweli watu wote wa dunia wangeweza kuishi katika Jimbo la Texas, katika vyumba vya familia ya wastani, wakawa na sehemu za mapumziko mbele na nyuma ya nyumba…viwango vya vizazi vinaporomoka kote duniani watu wa dunia hawataweza tena kujizalisha kwa mara mbili.

 Kama viwango vya kizazi vitabaki vilivyo, idadi ya watu itafikia kilele katikati ya mwaka karne hii na kisha, kuanza kupunguka bila uwezekano wa kuzuia. Tatizo letu la muda mrefu sio watu wengi, bali watoto wachache. Kuwa na mtoto mwingine kutasaidia kuondaa tatizo la uhaba wa watu.

 

Sababu ya kumi.

 

Pata mtoto  usaidie kuwa na watakatifu wengi mbinguni.

 

Mtoto ambaye wewe na mwenzi wako mmempokea kwa mikono miwili kutoka kwa Mungu, ameumbwa ili arudi kwake Mungu baada ya maisha ya hapa duniani, aishi milele mbinguni na Mungu.

Bwana wetu alisema, zipo nafasi tele kwa roho zetu huko mbinguni. Hakuna tatizo la msongamano wa watu huko mbinguni.

Kaka na dada zake, wazazi wake na familia yote. Uhai wake wote huwa zawadi kwa watu wote ambao watoaji wa uhai na ambao wanalazimika kuonja uwepo wake, ushiriki wake katika maisha yao na mchango wake katika mema na kwa jumuiya ya wanafamilia’.

Kwa kadiri jamii inavyokuwa na watoto wengi, ndivyo hivyo jamii hii inavyokuwa ya watu wateteao uhai na ndivyo itakavyokuwa rahisi kupiga vita dhidi ya uovu wa utoaji mimba.

*Makala hii imetafsiriwa kutoka kipeperushi cha POPURATION RESEARCH ISTITUTE (PRI)

 

Shirika hili, PRI lilianzishwa mwaka 1989 na Steven Mosher, akateuliwa kuwa Rais wake mwaka 1995.

Malengo makuu ya kuanzisha shirika hili yalikuwa ni pamoja na kupigania watu, kukanusha nadharia kuwa, idadi ya watu inakwenda kasi kuliko uwezo wa kiuchumi na kufichua ukiukwaji wa haki za binadamu katika programu za uzazi wa mpango.

Mengine ni kudumisha mitazamo ya utetezi wa watoto na familia kimataifa, kulinda familia na kuongea juu ya haki za watoto katika nafasi yoyote ipatikanayo pamoja na kuziua ueneaji wa utoaji mimba, vidhibiti mimba na kufunga kizazi kunakofanywa na Serikali kwa dhana ya udhibiti wa idadi ya watu, badala yake, kusemea programu zinazofanya wanyonge wawe vichocheo vya maendeleo yao.

 

 

 

 

 

 

 

 

Kanisa Katoliki lapania kuleta maendeleo Zanzibar

Lilian Timbuka na Peter Dominic

 

PAMOJA na ugumu uliopo katika mustakabari na mchakato mzima wa Uinjilishaji wa Kanisa Katoliki visiwani Zazibar bila kujali itikadi, juhudi na mikakati ya kanisa hilo inaashiria nyota njema ya ukombozi wa maisha ya kiroho na kijamii kwa wananchi wa visiwani humo.

Kanisa hilo hilo ambalo limekuwa shabaha ya hujuma zinazofanywa na watu wanaotaka kutekeleza matakwa yao kiimani na kisiasa, limekuwa na uhusiano mzuri kwa watu wote.

Pamoja na hujuma hizo, kanisa linasimamia na kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na afya, elimu na malezi ya jamii, ambayo inawalenga watu wote bila kujali itikadi ya mtu.

“Walio mbali na Zanzibar, wanajua sisi tuna hali mbaya sana kimahusiano na kiusalama. Ukweli ni kwamba si watu wote wana  nia mbaya na Kanisa, kuna watu wachache ambao wanatufanyia hujuma, hawa wanaendesha mihadhara na kukashfu ukristo. Lakini kwa ujumla wazanzibar ni watu wazuri mno,” anasema Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar Mhashamu Agustino Shao.

Miradi ya kijamii inayoendeshwa na kanisa, ni kielelezo tosha cha dhamira ya kanisa kuwasaidia na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.

Moja ya huduma za kijamii zitolewazo na Kanisa visiwani humo, ni kituo cha wazee wasiojiweza kilichopo eneo la Welezo, ambacho kinaendeshwa na Masista wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kituo hicho chenye majengo manane, kinapambwa na wazee ambao huketi barazani wakibadilishana mawazo, wakati vikongwe wenye nguvu bado hukaa wakisuka mikeka ingawa wenye umri mkubwa zaidi husikika wakikohoa wakiwa vyumbani mwao.

Wazee hao hususani wasio na ndugu wa kuwahudumia, wanapata mahitaji muhimu ya kumalizia kipindi kilichosalia cha uwapo wao hapa duniani kabla ya kuitwa na Mwenyezi Mungu, wakiwa salama na matumaini.

Kwa Mujibu wa msimamizi Mkuu wa Kituo cha Welezo Sista Mary Theresina Ndoro (C.R.S) wa Shirika la Masista wa Damu Takatifu ya Yesu, anasema  kituo hicho chenye idadi ya wazee 66 ambapo wanaume wako 49 na wanawake 17, kinaendeshwa kwa ushirikiano wa Shirika lake na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Sisita Theresina anasema, wamekuwa wakitunza wazee wenye umri mkubwa, ambapo alisema, mzee ambaye ana umri mkubwa zaidi ana miaka 112, na mwenye umri mdogo ni yule aliye na umri wa miaka 70 hivi sasa.

kihistoria kituo hicho kilianzishwa na Kanisa Katoliki Mwaka 1911 na Wamisonari wa Shirika la White Fathers, kikikusudia kuwahudumia watu waliokuwa na ugonjwa wa ukoma.

Hata hivyo kituo hicho kilitaifishwa na Serikali mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar kutokea, na kuwafanya wamisionari waliokuwa wakikisimamia kuondoka na kukiacha mikononi mwa serikali.  Mwaka 1982 serikali ilikiteua kuwa kituo cha kulelea wazee wasiojiweza.

Sisita Theresina anasema kuwa, serikali ya mapinduzi iliendelea kuwahudumia wazee wasiojiweza kupitia kitengo cha Ustawi wa Jamii. Hata hivyo anasema tofauti na hali ilivyokuwa awali, serikali haikuweza kumudu mazingira ya kuwahudumia wazee hao hali iliyochangia kuwaweka wazee  katika hali mbaya.

Anasema hali hiyo ilichangiwa na kuchakaa kwa majengo, kukosekana kwa wafanyakazi wa kutosha baada ya serikali kushindwa kuwalipa mishahara, ukosefu huduma muhimu ikiwa ni pamoja na maji, umeme na vifaa vya kutosha kuwahudumia hali iliyowafanya wazee wasioge kwa muda mrefu.

Serikali iliamua kurejesha kituo hicho kwa Kanisa Katoliki katika miaka ya 1990 ili kuboresha huduma za kituo. Shirika la Damu  Takatifu ya Yesu lilianza utaratibu wa  kukarabati na kuboresha huduma kwa makubaliano maalum ya mkataba wa miaka miwili miwili.

 “Kila baada ya miaka miwili  tulitiliana saini ya kuanza mkataba mpya na serikali, kwa vile tulihofia kushindwa kutokana na gharama kubwa za uendeshaji,” alibainisha Sista Theresina.

Sista Theresina anabainisha kuwa, makubaliano yaliyopo kati ya Kanisa Katoliki Zanzibar na serikali kwa hivi sasa, ni kwa serikali  kuendelea kulipa mishahara ya wafanyakazi ambao idadi yao inafikia 66, walinzi 14 na wahudumu wa kawaida pamoja na Muuguzi mmoja ambaye huwahudumia wazee kwa matibabu kwa kushirikiana na Sista Theresina ambaye   pia kitaaluma ni muunguzi.

Anasema kuwa, Daktari mmoja kutoka serikalini hufika na kuwahudumia wagonjwa na wale wanaoshindikana hupelekwa katika hospitali ya Rufaa ya serikali ya Mnazi Mmoja.  Akielezea namna kituo hicho kinavyopokea wazee, alifafanua kuwa, serikali ya Zanzibar  huwatumia Masheha kuwakusanya wazee wasiojiweza katika maeneo yao wakizingatia wasio na ndugu kisha huwaleta kituoni hapo.

Akizungumzia gharama za uendeshaji, anasema kuwa awali serikali ilikuwa ikitoa posho kwa wazee ikiwa ni jumla ya shilingi 500,000  kwa mwezi, ingawa baadaye ilionekana isingeweza kukidhi mahitaji ya kila mzee.

Hata hivyo anasema, kulingana na kupanda kwa gharama za mahitaji, hivi sasa serikali inatoa kiasi cha shilingi Milioni 2 kwa mwezi ingawa bado kiwango hicho ni kidogo.

Kuwepo kwa masista wa shirika hilo, imeonekana ni faraja kwa wazee hao kama wanavyobainisha. “Najisikia faraja kuwepo hapa, tunafurahia huduma zinazotolewa na masisita najisikia nipo na ndugu zangu,” alisema Mzee Omari Mtiro (70). Naye Mzee Juma Bakari ambaye hakukumbuka umri wake, alisema, “mwili ulikuwa ukitetemeka, sasa najisikia afadhari, tatizo langu macho, lakini ninaimani hawa ndugu zangu watanisaidia tu, wana moyo sana Mungu awabariki sana.”

Mzee Raphael Daima (70) na Mzee Musa Almas (87) wameshukuru huduma zinazotolewa na kituo hicho tangu kuwepo kwa uongozi wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu. Sisita Theresina alisema kuwa, umri walionao wazee kama hao, wanahitaji kuhudumiwa kama watoto wadogo.

Sisita Theresina alisema pamoja na wingi huo wa wazee hakuna tishio la vifo ambapo wastani unaonesha kwamba vinaweza kutokea vifo 12 kwa mwaka.

Akiongelea suala la Elimu na Mikakati ya Jimbo Katoliki la Zanzibar Mhashamu Shao aliwaambia Waandishi wa makala haya kuwa, hivi sasa Kanisa linamkakati wa kueneza elimu bora zaidi kwa jamii.

Alisema tayari kanisa limekwisha jenga shule za msingi na sekondari ambazo kwa hivi sasa zinachukua wanafunzi kama kawaida.

Shule ya msingi ambayo hivi sasa inaonekana kuwa ni shule ya kisasa zaidi kuliko shule zingine mjini Unguja, ni ile ya Mtakatifu Fransis Maria Libermann iliyo katika Kitongoji cha Tomondo, inayochukua wanafunzi toka wale wa darasa la awali, mpaka darasa la saba, shule hiyo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 kwa sasa.

Katika uchunguzi uliofanywa na waandishi, imebainika kuwa karibu asilimia 80 ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo, ni wa dini ya kiislamu, hali ambayo inaonesha wazi kuwa Kanisa limedhamiria kutoa huduma za jamii kwa watu bila kubagua.

Shule hiyo ya Mtakatifu Fransis Maria Libermann, ilianzishwa mnamo mwaka 1997, ikiwa ni   shule ya chekechea, ambapo watoto walikuwa wakisomea chini ya Mwembe na kukalia vipande vya magogo ya minazi kama madawati. Shule  ilianzishwa kwa msaada wa Askofu Mstaafu wa Jimbo la Zanzibar wakati huo, Mhashamu Bernard Nganviliyao.

Majengo yaliyopo hivi sasa, yamejengwa chini ya Uongozi wa Mhashamu Agustino Shao, kwa kushirikiana na wafadhiri mbalimbali wa nje na ndani, akiwamo Askofu Donald Wuerl.

Shule hiyo ambayo ni ya kutwa na bweni, tayari ina wanafunzi 24 wa bweni. Shule inauwezo wa kulaza wanafunzi 50 hivi sasa.

Akijibu swali juu ya shule kuwa na wanafunzi wengi wa Kiislamu kuliko Wakristo Mhashamu Shao alisema;

“Lengo la Kanisa ni kutoa huduma kwa watu na si kwa kuangalia huyu ni muamini wa dini ipi, au mkazi wa wapi. Kazi yetu kubwa ni kueneza Injili kimwili na kiroho, na ikiwa ni pamoja na kutoa huduma muhimu kwa jamii kama hii ya Elimu.”

Pia Mhashamu Shao alibainisha kuwa, Wakristo wengi waishio visiwani humo wamekuwa wakishindwa kuwapeleka watoto wao shule, kwa kuwa na matumaini ya kurudi Tanzania Bara muda wowote.

“Hapa visiwani Waamini wengi wa Kikristo ni wale ambao wamekuja kutoka bara, kwa hiyo ukimwambia mpeleke mtoto shule, atakwambia mimi sikai sana hapa, nimekuja kutafuta maisha kwa muda tu, nikifanikiwa narudi kwetu Shinyanga au Tabora” alifafanua Mhashamu Shao.

Hata hivyo Mhashamu Shao alibainisha pia kipato kidogo walichonacho Wakristo kinachangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kusomesha watoto, kutokana na kukosa ada.

Pamoja na machungu ya kupigwa mabomu kwa mali za Kanisa na watu wasiotaka maendeleo visiwani humo, ikiwa ni pamoja na kulipuliwa kwa basi la Shule la Mtakatifu Fransis Maria Libermann na Kanisa, kulikofanyika hivi karibuni, bado Kanisa Katoliki halijakata tamaa ya kutafuta maendeleo ya wananchi wake visiwani humo.

Jimbo la Zanzibar hivi sasa linaendelea na ujenzi wa shule ya Sekondari katika kijiji cha Cheju kilicho  nje kidogo ya mji wa Zanzibar, ambayo inatarajia kuanza kufundisha masomo kamili ya sekondari katika siku chache zijazo.

Shule hiyo ambayo ilianzishwa rasmi mnamo April 1999, kwa sasa inajulikana kwa jina la Cheju Wisdom Centre, ikiwa ni kituo cha malezi ya Vijana shule hiyo imekamilisha baadhi ya majengo, na inachukua wanafunzi wanaojiandaa kwa masomo ya sekondari wa kike na wa kiume.

Akizungumza shuleni hapo, Mkuu wa Shule hiyo, Padre Damas  Mrina alisema kuwa, shule hiyo ambayo ina jumla ya wanafunzi 46, wasichana 32 na wakiume 14, hivi sasa inawaandaa vijana kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kuwatawanya katika shule za sekondari zilizoko Tanzania Bara, zikiwamo zile za Kiraeni, Kifungiro, Marangu, Kibosho,  Sila na shule ya Mtakatifu Fansis ya Mbeya.

“Shule yetu mpaka hivi sasa iko katika ule mtindo wa chuo cha malezi, vyuo ambavyo hata wenzetu waislamu wanavyo,” alisema Padre Mrina.

Hivyo aliainisha kuwa, kwa sasa shule inawafundisha wanafunzi masomo ya Kiingereza na Hisabati ambayo wameyafanya kama masomo ya msingi. “Tunafundisha pia masomo mengine ikiwemo Jiografia, Elimu ya Biblia, Siasa, sayansi na Afya,” alisema Padre Mrina.

Alisema masomo yote hayo hufundishwa kwa kutumia lugha ya kiingereza na Kiswahili. Aliongeza kuwa, lengo kuu la shule hiyo hivi sasa ni kuwajengea uwezo wanafunzi wa kuweza kuyamudu masomo ya sekondari ambayo huyasoma baada ya kutoka hapo.

Shule hiyo ambayo iko umbali wa kilomita 30 toka katikati ya Mji wa Zanzibar, huchukua wanafunzi kutoka Tanzania Bara na Visiwani. Na  hivi sasa iko katika kampeni ya kutaka kuiwezesha kuwa sekondari kamili ya bweni. Na maandalizi ya ujenzi wa mabweni unaendelea.

Mbali ya masomo ya darasani, shule hiyo pia inafundisha elimu ya kujitegemea. Tayari shuleni hapo kuna miradi ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi, na nguruwe wapatao 63.

Padre Mrina alisema mradi wa nguruwe huingiza kiasi cha shilingi Laki 5 kwa mwaka, na nguruwe hao huwauza katika Hoteli za kitalii zilizomo visiwani humo.

“Hawa nguruwe wanatuingizia kipato, hasa katika sikukuu za mwaka, kama zile za Pasaka na Krismasi,” alisema Padre Mrina.

Shule hiyo pia inamiliki shule ya awali, iliyopo ndani ya majengo ya shule.

Kanisa katoliki visiwani linajishughulisha pia na utoaji wa elimu ya UKIMWI kwa kuanzia ngazi ya vitongoji mpaka mkoa.

Akizungumzia utoaji wa elimu hiyo, Mhashamu Shao alisema Zanzibar hivi sasa hakuna NGO yoyote inayotoa elimu ya UKIMWI kwa kina kama Kanisa Katoliki.

Alisema Kanisa hivi sasa limekuwa mstari wa mbele na tayari wafadhiri wa mfuko wa Global Fund, wamelitambua hilo.

Mhashamu Shao anasema tayari Jimbo lake limekwisha jenga vituo kadhaa vya Afya, vinavyoendelea kutoa huduma ya afya kwa hivi sasa, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wagonjwa walioathirika na virusi vya ukimwi.

Alisema kisiwani Pemba jimbo limejenga zahanati Tatu, na Hospitali moja ambayo hutoa huduma ya ukunga kwa wanawake wajawazito.

“Cheju tayari tumejenga Zahanati, lakini bado haijaanza kufanya kazi kutokana na ukosefu wa wafanyakazi wenye sifa,” Mhashamu Shao alisema.

Alisema lengo la Kanisa ni kutoa huduma zenye ubora na si za kubahatisha, japoakuwa  walipoanza kujenga zahanati hizo, walipata kipindi kigumu toka kwa waamini wenye itikadi tofauti na ya wakristo, kwa madai ya kuwa kamwe wasingeweza kutibiwa katika zahanati hizo ambazo walidai sindano zitumikazo zina nguruwe.

“Lakini taratibu sasa wameelewa, sasa hivi ukitaka kufanya sensa ya wagonjwa wanotibiwa katika zahanati zetu kwa asilimia kubwa ni wale waliokuwa wanatupiga vita hapo awali,” alibainisha Mhashamu Shao.

Akizungumza na KIONGOZI katika Zahanati ya Mtakatifu Camillius Mission, iliyo katika Kitongoji cha Tomondo Zanzibar, Muuguzi Mkuu  Sista Imelda Nafun N.O wa Shirika la Evangelising Sister’s, alisema kuwa, kituo hicho kinapokea wagonjwa wa aina mbalimbali ambao hupata huduma kila siku.

Sista Imelda aliongeza kuwa, zahanati hiyo inawatibu pia watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kutoka kundi la (ZAFA+), ambapo aliainisha kuwa wagonjwa hao hupatiwa dawa na gharama za matibabu hulipwa na ofisi ya Askofu wa Jimbo la Zanzibar.

Aliongeza kuwa, kwa hivi sasa zahanati yake haina vipimo vya maradhi ya UKIMWI, bali vipimo vyote hufanyika katika Hospitali ya Serikali ya Mnazi Mmoja.

Zahanati hiyo ambayo iko ndani ya eneo la shule ya Mtakatifu Fransis Maria Libermann, mbali ya kuwahudumia waathirika,  pia imekuwa ikitoa huduma za vipimo vya maabara, kliniki kwa akina mama wajawazito na watoto, na hutibu maradhi ya kawaida kwa jamii ya eneo hilo, na wanafunzi wa shule ya Mtakatifu Fransis, kwa gharama za shule.

Tofauti na Tanzania Bara, waathirika wa ugonjwa wa ukimwi, wamekuwa wakitengwa na kubaguliwa na jamaa zao. Huduma zinazotolewa na kanisa zimekuwa faraja kwa waathirika hao ambao sasa wanaishi kwa matumaini.

Pamoja na misukosuko inayoendelea kuliandama Kanisa Visiwani humo hivi sasa kwa kuharibiwa mali zake ambazo ziko kwa faida ya jamii ya watu wa visiwani, Mhashamu Shao alisema kamwe hawatakata tamaa katika kutafuta maendeleo.

“Pamoja na kuwa wanatutukana lakini wanapoona kuwa kuna dini nyingine pia  ambayo inafanya mambo mazuri, basi wanaelewa maendeleo ni nini,” alisema.

Alisema suala la baadhi ya watu wanaodai  wakristo waondoke Zanzibar, eti hawana kazi, wanakosea, alisema “Wakristo wana kazi kubwa na moja wapo ni kama hii ya kutafuta maendeleo ya visiwa hivi.”

Hata hivyo katika kutafuta maendeleo ya kweli ya visiwa hivyo, jumuiya ya Zanzibar kwa hivi sasa, haina budi kuonesha hali ya mshikamano, upendo na umoja, ili kujenga na kuendeleza amani kwa maendeleo ya wananchi wake, badala ya kurudi nyuma kwa kufanya uharibifu kwa kile kilichotengenezwa kwa faida ya kizazi kijacho.

Vita dhidi ya mila potofu ihusishe jamii za wahamiaji

Na Edna Ndejembi

MIAKA zaidi ya 10 iliyopita, nilishuhudia kioja kwenye Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Dodoma ambapo, mama mmoja mjamzito alishindwa kujifungua kwa vile sehemu yake za siri zilikuwa zimeshonwa.

Muuguzi Mkuu kwa wakati huo, Ruth Kalanje, alilazimika kuwasihi mama na ndugu wa mjamzito huyo, kumfumua mara moja mgonjwa wao ili aweze kujifungua salama lakini, hawakumsikiliza.

Tulielezwa kuwa, mjamzito huyo mwenye asili ya Kisomali alikuwa amefanyiwa ukeketaji na kisha, kuzibwa sehemu za siri, (INFIBULATION).

Aina hii ya ukeketaji inayosababisha maumivu makali, ni maarufu sana katika nchi za Sudan, Somalia na Djibouti

Mama yake ambaye hatimaye alimfumua binti yake baada ya kutishwa kuwa angepelekwa polisi, alitueleza kuwa binti yake huyo alikeketwa alipokuwa na umri wa miaka minane na kuzibwa kwa kushonwa sehemu zake za siri.

Anasema, alipofikisha miaka 16, aliolewa na hivyo kufumuliwa ili kumwezesha mumewe kumwingilia.

Hata hivyo, msichana huyo alilazimika kushonwa tena kwa vile mumewe aliyekuwa dereva wa magari makubwa, alikuwa anasafiri kwa muda mrefu na kwamba, hadi muda huo hakuwa amepata ujauzito.

Njia hiyo inadaiwa kuwa, ilikuwa inasaidia kumfanya mwanamke aliyeolewa asiweze kutoka nje ya ndoa yake, hali inayoweza kumsababisha kupata ujauzito

Mama huyo anasema, kilichomfanya akatae kumfumua tena binti yake, ni woga aliokuwa nao kwa vile angeshindwa kumjibu mkwewe ni kwa jinsi gani mwanae kapata ujauzito, wakati ameshonwa.

Akadai kwamba, binti huyo licha ya kuzibwa sehemu za siri, ajabu ni kwamba binti yake alitembea na mwanaume mwingine na kwa namna ya ajabu, akapata mimba.

Aina nyingine ya ukeketaji, ni ile inayohusisha ukataji wa sehemu kubwa bila ya kuziba. Hii hufanyika nchini Ethiopia, wakati aina ya tatu inayofanywa kwenye nchi nyingi zaidi ikiwemo Tanzania, inahusisha ukataki wa ncha tu (excision).

Huko Ulaya ambako ukeketaji ulikuwa unaruhusiwa kisheria hadi mwaka 1985 kabla ya kuzuiwa, ulifanyika kwa lengo la kuzuia michezo ya usuguaji hasa miongoni mwa watoto.

Wazazi walikuwa huru kuwapeleka watoto wao hospitalini na kufanyiwa ukeketaji aina ya excision kama tiba dhdi ya usuguaji.

Lakini pamoja na Bara hilo la Ulaya kupiga vita kitendo hicho, hivi majuzi Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, David Blunkett, ametangaza sheria mpya dhidi ya ukeketaji, baada ya vitendo hivyo kushamiri nchini humo.

Amesema sheria hiyo itawawabana wazazi wanaowapeleka watoto wao nje ya Uingereza ili kuwakeketa.

“Kwetu hakuna mila, matibabu au sababu yoyote inatakayoweza kuhalalisha ukeketaji ambao unawasababishia maumivu makali mabinti zetu,” alisema Blunkett na kuongeza kuwa, inakadiriwa kuwa wanawake 74,000 waliohamia Uingereza kutoka Afrika, wamekeketwa.

Jitihada za vita dhidi ya ukeketaji pamoja na mila potofu ambazo ni za unyanyasaji dhidi ya mwanamke, zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali hapa nchini, hazina budi kusambazwa kwenye jamii zote, badala ya kuhusisha tu, wananchi walioko vijijini.

Kama inavyoeleweka, jamii za Kisomali hazikubali kuacha vitendo vya ukeketaji kwa kuwa ni mila inayotukuzwa sana, na ndio maana kwa kuogopa kujulikana wakiwa nchi zilizopitisha sheria kali kama Uingereza, hudiriki kuwapeleka mabinti zao kukeketwa nchi za nje.

Vita dhidi ya ukeketaji na mila nyingine potofu kama ndoa za utotoni katika nchi yoyote ile, haiwezi kufanikiwa endapo jamii zote husika hazitashirikishwa.

Ukeketaji una madhara mengi na kubwa zaidi, ni kumsababishia maumivu na kuvuja damu nyingi endapo kovu litatanuka na kuchanika hasa wakati wa kujifungua, au kusababisha mtoto ashindwe kutoka hadi hapo upasuaji unapofanyika.

Jamii sharti ijue hilo na isiuone ukeketaji kama njia ya kujipatia kipato au basi kwamba, ni ufahari kama asemavyo Mama Shufaa Mahfudh (61); ngariba wa Kisomali ambaye amekuwa akifanya kazi ya ukeketaji kwa miaka mingi.

“Mimi silipwi pesa, wala sitaki kulipwa chochote; jamii yetu imenipa heshima kubwa sana ambayo ninajivunia kwani sio kila mwanamke anaweza kuruhusiwa kufanya kitendo hiki ambacho kinawaweka wasichana kwenye hali inayokubalika,” anasema Bibi Shufaa.

Bibi Mahfudh, mkazi wa eneo la Makola, linalokaliwa na jamii kubwa ya Kisomali Manispaa ya Dodoma anasema kuwa, huwakeketa watoto wa kike wanapofikisha umri wa kuanzia miaka 5 hadi 6 na kwamba, baada ya kuvunja ungo, hushonwa hadi pale watakapoolewa.

Ushonaji huo kwa mujibu wa Bibi Mahfudh, hufanywa ili kuwazuia wasichana kutojamiiana kabla ya kuolewa, na kwa wale walioolewa, huwazuia wasitoke nje ya ndoa pindi waume zao wanapokuwa mbali nao.

Nilipomuuliza kuhusu wasichana au wanawake walioshonwa kubeba mimba, Bibi Mahfudh alisema kuwa, kitendo hicho huweza kutokea iwapo mshonaji hatakuwa ameziba nafasi zote.

Hata hivyo uchunguzi uliofanywa kwenye jamii hiyo umeonesha kuwa, licha ya kushonwa, bado wanawake na wasichana wengi hujihusisha na ngono kama kawaida.

Aidha, ndoa za utotoni ni jambo la kawaida kwenye jamii hiyo na kwamba, watoto huhamishwa kutoka wilaya na hata mkoa mmoja hadi mwingine kwa lengo la kuolewa.

“Watoto watatu wamepelekwa nchi jirani mwaka huu kwenda kuolewa. Hivi sasa wote wanaweza kuwa wamekwishabeba mimba,” Bibi Mahfudh alieleza na kuongeza kuwa, watoto hao ambao hawakuwahi kusoma, walikuwa na umri wa chini miaka 15.

Vita dhidi ya mila potofu inapaswa kuhusisha watu wote waishio ndani ya mipaka ya nchi yetu, bila ya kubagua wala kuogopa jamii wanazotoka, ili mradi wako nchini Tanzania ambapo mikakati na sheria dhidi ya vitendo hivyo zinatekelezwa.

Hivi karibni mtandao dhidi ya mila potofu – AFNET, ulitaarifu kuwa unafanya mpango wa kuwawezesha kiuchumi mangariba mkoani Dodoma waachane na vitendo hivyo, kuangalia njia itakayowafanya mangariba kama Bibi Mahfudh ambao hawafanyi shughuli hiyo kwa malipo kuachana na vitendo hivyo.

 

KONA YA SHERIA

Ijue sheria ya ugaidi

Na Dotto Shashi

Matukio ya ugaidi yamekithiri sana hivi sasa. Ni ukweli usiopingika kuwa amani ya Dunia haipo tena, kwani limekuwa ni jambo la kawaida kila kukicha kusikia matukio ya mauaji ambayo ni ya kujitoa mhanga au hata bila kujitoa muhanga, lakini matukio yote hayo yamekuwa yakiwalenga watu, na mbaya zaidi waathirika wengi ni watu ambao hawana hatia yeyote kwa Mwenyezi Mungu na hata kwa magaidi wenyewe.

Katika mada ya toleo hili, tutaiangalia sheria ya kuzuia ugaidi iliyopitishwa na Bunge la Tanzania mwaka 2002.

kwa kuwa sheria hii ya ugaidi ina mambo mengi sana yaliyowekwa kisheria, na kwamba watu wengi sasa kwa kiasi kikubwa tayari wana upeo wa kutosha wa kuuelewa ugaidi ni nini, toleo hili tutaitazama sheria hii katika eneo linalohusu watu ambao wanatabia ya kuficha magaidi au taarifa zozote, ambazo zinaweza kusaidia kupatikana kwa watuhumiwa wa ugaidi.

Sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya 2002, yaani ‘The prevention of Terrorism Act, 2002’, imeweka vifungu vya sheria vinavyomfanya mtu kuwa na wajibu wa kutoa taarifa inayohusu ugaidi.

Sehemu ya nane ya sheria hiyo, yaani ‘Part Viii’, vimeorodheshwa vifungu ambavyo vinazungumzia suala zima la wajibu wa mtu katika kutoa taarifa ya ugaidi.

Kifungu namba 40 kifungu kidogo cha kwanza (1) kinaeleza kuwa, kila mtu ambaye ana taarifa ambayo inaweza kusaidia; (a) Kuzuia kitendo chochote cha ugaidi ambacho kinaweza kufanywa na mtu au (b) Kusaidia kukamatwa kwa mtu au mashitaka yake chini ya sheria hii.

Atatakiwa mara moja kutoa taarifa hiyo kwa Askari polisi ambaye ana cheo kisicho kuwa chini ya cheo cha Mrakibu msaidizi wa  Polisi, (Assistant Superintendent of Police) au mkuu wa kituo cha Polisi.

Katika kifungu kidogo cha pili (2) imeelezwa kwamba, hakuna kitu chochote katika kifungu kidogo cha kwanza ambacho kinataka utoaji wa habari ambazo zina kinga (Information protected by privilege).

Kifungu kidogo cha tatu (3) kinasema, “mtu yeyote hawezi kushitakiwa aidha kwa kesi ya jinai au kesi ya madai kwa kutoa taarifa yoyote kwa nia nzuri au katika mazingira kama inavyoelezwa katika kifungu kidogo cha kwanza(1).”

Kifungu kidogo cha nne (4) kinasema kuwa, mtu yeyote ambaye itathibitika kushindwa kutekeleza matakwa au wajibu wake kama ilivyoelekezwa katika kifungu kidogo cha kwanza, atakuwa amefanya kosa la jinai, na hivyo akitiwa hatiani atatakiwa kwenda kutumikia kifungo jela cha miaka isiyopungua miwili na au isiyozidi mitano (Tafsiri ya kifungu hiki ni ya mwandishi mwenyewe).

Tunaona katika adhabu iliyotolewa na sheria hii, kuwa kosa la kushindwa kutoa taarifa, halina adhabu ya faini kama ilivyozoeleka kwa wengi katika makosa mengi ya jinai, hivyo mtu akipatikana na hatia katika kosa hili ajue yeye ni mtu wa kifungo.

Baada ya kuona kosa la mtu kushindwa kuwajibika katika kutoa taarifa za ugaidi kama anavyotakiwa katika kifungu namba 40(1).

Tuangalie kifungu kingine ambacho kina mtaka mtu kuwa na wajibu wa kutoa taarifa kwa Polisi inayohusu mali za gaidi au mali zinazomilikiwa kwa niaba ya gaidi au kundi la magaidi ambazo zimetumika kwa kutendea kosa la ugaidi.

Kifungu namba 41 kifungu kidogo cha kwanza (1), kinaeleza kwamba; kila mtu atalazimika kutoa taarifa mbele ya Afisa wa Polisi mara moja ya;

(a) Umiliki wake au kukabidhiwa kwake mali yoyote ambayo kwa ufahamu wake ni mali ambao ni ya gaidi , au inayotunzwa kwa niaba ya kundi la magaidi.

(b) Mipango ya utekelezaji au inayokusudiwa kutekelezwa kuhusiana na mali yoyote kama ilivyoelezwa katika kipengele cha (a) hapo juu.

Neno Afisa wa Polisi kama lilivyotumika katika kifungu cha 41 lina maana, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo na Afisa wa Polisi mwenye cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Polisi, hii ni kwa mujibu wa kifungu namba 3 cha sheria hii ya Ugaidi.

Tukiendelea na kifungu cha 41, tunaona  kuwa katika kifungu kidogo cha pili (2), Taasisi za Fedha nchini zimetakiwa kutoa ripoti kila baada ya miezi mitatu, mbele ya Afisa wa Polisi au mtu yeyote ambaye amepewa mamlaka kisheria ya kusimamia na kurekebisha shughuli za Taasisi hiyo ili kuona endapo Taasisi hiyo;

(a) Haimiliki au kuwa na Amri juu ya mali yeyote ya kundi la magaidi au;

(b) Ina miliki na kuwa na Amri juu ya mali ya magaidi, maelezo kuhusu watu (magaidi), Hesabu za Fedha, na mipangilio inayohusiana na mali hiyo ikiwa ni pamoja na thamani ya jumla ya mali hiyo.

Kifungu kidogo cha tatu (3) kinaeleza kuwa, kwa nyongeza ya matakwa ya kifungu kidogo cha pili hapo juu kila Taasisi ya Fedha italazimika kutoa taarifa mbele ya Afisa wa Polisi ya kila hatua ya shughuli ambazo wana kila sababu ya kuhisi kuwa hatua hizo shughuli zao zina mwelekeo au zinahusiana na magaidi.

Kifungu kidogo cha Nne(4) kinasema kuwa, mtu yeyote hawezi kushitakiwa kwa kosa la jinai au madai kwa kutoa ripoti kwa nia njema, kama inavyotakiwa katika vifungu vidogo vya (1), (2) au (3).

Mwisho katika kifungu kidogo cha tano(5), inatolewa adhabu kwa mtu ambaye atashindwa kutii matakwa ya vifungu vidogo vya (1), (2) na (3).

Na kwamba adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miezi isiyopungua kumi na mbili jela (12).

 

 

Kwa kumalizia mada hii, ni matumiani yangu kuwa sote tumeona umuhimu wa kutii sheria hii ya kuzuia ugaidi (Prevention of Terrorism Act, 2002), kwani bila kufanya hivyo tutakabiliwa na adhabu kali, kama inavyoelezwa katika sheria hii.

 

SHERIA ZA KANISA

SAKRAMENTI YA NDOA: Kan. 1055 – 1165.(17)

Katika Toleo lililopita tuliishia katika kipengele kinachotaja DARAJA TAKATIFU kama moja ya vizuizi vya Sakramenti ya Ndoa. Kabla ya kuendelea na mjadala juu ya kizuizi hiki, hebu kwanza tujikumbushe historia fupi kuhusu sheria ya useja. Endelea

Mafundisho kuhusu useja yanakutwa katika mapokeo ya Kanisa kama vile, maandishi ya Mababa wa Kanisa: Mt Yohana Christostom, Tertulliano, Origen, Jerome, Clement wa Alexandria, Eusebiowa Caesarea, Sirilo wa Yerusalemu, na Gregori wa Nazianzen. Lakini, mafundisho ya kisheria kuhusu useja wa ki-kanisa yanakutwa katika mafundisho ya Kanisa (magisterium) na basa ya Kanisa Katoliki ya Magharibi. Kwa namna ya pekee, hatuwezi kusahau mchango wa mkutano wa Elvira (hispania) wa 306.

Uliwakataza wote waliopokea madaraja makubwa kuendelea na maisha ya ndoa (DZ 119). Ingawa mkutano huo ulikuwa na baadhi ya majimbo ya Hispania, majimbo mengine yalifurahishwa na msimamo huo. Yakaidhinisha maazimio yake, kama vile mkutano wa Arles (314) wa Ancyra (314) wa Roma (386). Hata Mababa Watakatifu Damaso, Siricio na Innocent waliwataka makrelo kuishi hivyo.

Mikutano mingine ya Kanisa iliyofuata iliyoyakubali maamuzi hayo ni pamja na Mkutano wa Karthage- Africa (390), Orange Ufaransa (441) wa Tours-Ufaransa (461), na Turino - Italia (398). Aidha maaskofu katika majimbo yao waliwahimiza watu wao, kuishi maisha ya useja. Hatuwezi kusahau mchango wa Gregori VII aliyeishi karne ya 11 ambapo kulikuwa na uozo wakimaadili na kiroho.

Watawa walikuwa wameacha monasteri na kuoa au kuolewa. Makleri waliacha huduma za Kanisa na kuoa.

Aliandika barua nyingi na kuwatuma wawakilishi sehemu mbalimbali za dunia ili kuhimiza suala la useja wa kiKanisa (Delhaye P., History of Celibacy, katika, New Catholic Encyclopedia, Vol. III, Jack Heraty & Associates, Washington, 1967, uk. 369). Alifanikiwa kiasi kikubwa. Mababa Watakatifu waliofuata walifuata nyayo zake: Urbano II na Callisto II. Mitaguso ya Kanisa iliendeleza utaratibu huo: Laterano I (1123), Laterano II (1139), Trenti karne ya 16, Vatikano I (1869-1870) na Vatikano II (PO, 16; PC, 12; LG, 42; OT, 10).

 Kumbe, ni kutokana na juhudi hizo zote kwamba sheria imeweka kanuni zinazohusu useja wa kiKanisa (kan. 227; 1037; 1042 na 1087).

Wajibu wa kuishi useja unawahusu wale wote wanaoshiriki madaraja matakatifu, yaani, maaskofu na mashemasi-waseja. Wakivunja sheria hiyo na kufunga ndoa, ndoa hiyo ni batili (kan. 1087). Zaidi ya hayo, yeyote atakayefunga ndoa hata kama ni ya kiserikali atavuliwa madaraka yote ya Kanisa (kan. 194) na kusimamishwa kama ilivyo kawaida (kan. 1394).

Lakini kwa sababu kubwa sana Baba Mtakatifu peke yake anaweza kumwondolea mtu wajibu wa kuishi maisha ya useja (kan. 1078, 291) na kuruhusiwa kuoa. Ordinari mahalia hawezi kumwondolea mklero, hasa padre au askofu, wajibu wa useja (kan. 291). Wajibu wa useja wa mapadre au maaskofu au mashemasi unaondolewa na Baba Mtakatifu tu. Kwa maaskofu na mapadre, matayarisho na kesi nzima vinapitia kwa Idara ya Mafundisho ya Imani na yale ya ushemasi yanapitia kwa Idara ya Sakramenti. Wakati wa hatari ya kifo, ordinari mahalia anaweza kumwondolea shemasi wa kudumu wajibu huo.

 

Nadhiri ya usafi wa moyo shirikani:

kan. 1088.

 

Sheria ya Kanisa inasema waziwazi kuwa wale walioweka hadharani nadhiri ya daima ya usafi wa moyo katika shirika la kitawa hufunga ndoa batili (kan. 1088). Ili ndoa iweze kuwa batili lazima masharti manne yatimizwe, yaani: nadhiri iwe ya usafi wa moyo, iwe ya daima, iwekwe hadharani na iwekwe katika shirika la kitawa.

Kizuizi hiki hakiwahusu wale wanaoweka nadhiri ya muda ya usafi wa moyo au nadhiri ya binafsi au wanaoweka ahadi ya kutunza usafi wa moyo katika mashirika mengine ya Kanisa yasiyo ya kitawa. Pamoja na kufunga ndoa batili mtawa anajifukuza mwenyewe kutoka shirikani (kan. 694;1394) na kuacha huduma zote za Kanisa (kan. 194).

        Kizuizi hiki kinaweza kuondolewa na mamlaka halali ya Kanisa. Ikiwa nadhiri imewekwa katika shirika la kitawa la kipapa, mamlaka ya kuondoa kizuizi hiki ni Kiti cha Kitume, yaani, idara inayoshughulikia watawa na mashirika mengine ya Kanisa (kan. 1078). Uongozi wa Jimbo unaweza kuondoa kizuizi hiki wakati wa hatari ya kifo tu.

Iwapo mawasiliano na Uongozi wa Jimbo ni magumu sana na kuna hatari ya kifo, padre yeyote anayeruhusiwa kufungisha ndoa anaweza kuondoa kizuizi hiki. Hii ni pamoja na shemasi anayeruhusiwa kufungisha ndoa (kan. 1079 na 1116). Padre mwungamishi anaweza kuondoa kizuizi hiki wakati wa hatari ya kifo na wakati akiadhimisha Sakramenti ya Upatanisho na ikiwa kizuizi hiki ni cha siri, yaani, hakijulikani kwa watu.

            Kwa mtawa wa shirika la kitawa la kijimbo, ni Uongozi wa Jimbo unaoondoa kizuizi hiki. Inapotokea sababu maalum (kan. 1079 na 1080) na ikiwa mawasiliano na Uongozi wa Jimbo ni magumu, mapadre au mashemasi walioruhusiwa kufungisha ndoa wanaweza kuondoa kizuizi hiki.

 

NIONAVYO MIMI

Adhabu ya kunyonga si suluhisho

Na Charles Misango.

 

TAIFA   hivi karibuni, liliambiwa kuwa watanzania 350 wanasubiri kuuawa kwa kunyongwa, baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya mauaji na uhaini, kati yao 11 wakiwa ni wanawake.

Ingawa takwimu hizi hazikubainisha idadi ya watu wanaosubiriwa kunyongwa kutokana na kosa la uhaini na lini walitenda kosa hilo, dhahiri wengi wao watakuwa wanakabiliwa na makosa ya mauaji.

Takwimu hizi zimedhihirisha kuwepo kwa ongezeko la mauaji hapa nchini. Nalazimika kuamini kuwa wapo wengine walioua  zaidi ya hawa waliotajwa bungeni, kwa sababu kesi zao bado hazijaamuliwa na mahakama.

Katika miaka ya hivi karibuni, taifa limeshuhudia taarifa nyingi za mauaji hasa ya ujambazi. Huko mkoani Mbeya, matukio ya mauaji yanayoandamana na uchunaji ngozi za watu yalivuma sana ndani ya miaka miwili iliyopita.

Sote tunatambua uchungu walionao na ambao wataendelea kuwa nao, wale ambao ndugu zao waliuawa na mmoja wa watu hawa wanaosubiri kuuawa pia.

Waliouawa katika matukio yanayopelekea kunyongwa kwa wahusika hawa walikuwa baba zetu, kaka ama dada zetu ambao walikuwa tegemeo kubwa katika familia zetu.

NIONAVYO MIMI, msingi wa kuwepo kwa sheria hii ya kunyonga, ni kuhakikisha kuwa raia wanalindwa kikamilifu  na hata kuzuia matukio ya mauaji hususani ya kukusudia.

Hata hivyo, sidhani na sikubaliani kabisa kuwa kuwanyonga wafungwa wa makosa ya mauaji ni njia sahihi na bora ya kupunguza ama kukomesha kabisa, matukio ya mauaji nchini.

Ninazo sababu kubwa, na nyingi za msingi kuthibitisha haya nisemayo; Mosi, itakumbukwa kwamba wakati fulani ujambazi ulizuka kwa kiwango kikubwa sana katika Jiji la Dar es Salaam.

Wakazi wake wengi baada ya kuchoshwa na vitendo hivyo na hasa pale ilipodhaniwa kwamba jeshi la polisi lilikuwa limeshindwa kabisa kudhibiti vitendo hivyo, waliamua kuwachoma moto palepale wale wote waliokamatwa wakifanya ujambazi.

Wakazi hawa walifanya hivyo wakitambua kuwa kwa kuwauwa kwa njia hiyo, bila kujali kama jambazi alikuwa amesababisha kifo, wangewatia woga na kuwakomesha kabisa majambazi hao.

Lakini hadi wakati huu unaposoma makala hii, vitendo vya ujambazi havijaisha na ndio kwanza vinaongezeka kwa kasi.

Majambazi na hata vibaka wamekuwa hawasubiri tena giza liingie, bali hufanya uharamia huo, mchana wa jua kali. Kibaya sana, ujambazi sasa unafanyika hata katika nyumba za ibada. Sio tu kwamba sasa watu hawaogopi macho ya watu, bali hata hawaheshimu nyumba za ibada.

Sababu ya pili inayonifanya niamini kuwa adhabu hii haisaidii kukidhi haja yake, ni matukio ya ajali za barabarani. Kwa watu wa vijijini, pengine sababu hii haitawaingia kikamilifu.

Lakini kwa wale tunaoishi mijini tunafahamu na kutambua kikamilifu kwamba, dereva yeyote anayeendesha gari kwa uzembe  na kumgonga mtu, dereva huyo hupigwa hadi kufa na gari lake kuharibiwa vibaya hata kama aliyegongwa atakuwa hajafa.

Kama vile ilivyokuwa katika suala la kuwachoma vibaka, ilitegemewa kuwa ajali za kugonga watu, hasa wale waendao kwa miguu, zingepungua sana. Kinyume chake sasa, ajali zimeongezeka mno tena hata katika sehemu ambazo usingetegemea zitokee.

Wakazi wengi wa mijini, watakubaliana nami jinsi ambavyo watembea kwa miguu wanavyogongwa kila siku wanapovuka barabara kwenye eneo la zebra (alama za pundamilia) ambako ni haki yao.

  Je ile adhabu ya kuwapiga na kuwaua iliyokuwa ikitolewa kwa madereva wa aina hii imesaidia kukomesha vitendo hivyo?

NIONAVYO MIMI, jibu litakalopatikana katika swali hili, ni wazi kuwa litakuwa likisema kuwa bado vitendo hivyo havijasaidia kitu, isipokuwa kasi ya ajali inaongezeka kila kukicha.

NIONAVYO MIMI, mbali na kutosaidia lolote, adhabu ya kuwanyonga wahalifu, haina manufaa kwa waathirika wa ndugu wa kwanza aliyeuawa. Mtu aliyeuawa na jambazi ama yeyote iwe kwa makusudi ama kwa bahati mbaya, huacha nyuma yake familia yenye simanzi na mateso.

Anaacha familia yenye chuki, visasi na uhasama mkubwa baina yake na familia ya aliyeuwa.

Kwa kumnyonga muuaji, familia ya awali haitakuwa imeepuka msiba mzima wa kuondokewa na mzazi ama ndugu yao. Familia haitakuwa imenufaika kifedha ama kwa mali, na wala haitakuwa imesaidia kuondoa chuki baina ya familia hizo mbili, eti tu kwa kuwa adui yao nae kauawa.

NIONAVYO MIMI, kwa kumnyonga mhalifu wa mauaji, serikali na jamii kwa jumla itakuwa imewaadhibu watu wengine zaidi ya yule mhalifu wa mauaji.

Kama familia 350 za wahalifu wa mauaji zimebaki yatima, kwa kuwanyonga wahalifu hao, serikali na jamii itazalisha kiasi kama hicho cha yatima na kufanya jumla kuwa 700!

Je serikali inaweka mpango gani basi, kuhakikisha kwamba adhabu wampayo mtu huyu haitawaathiri kwa kiwango cha kuwaingiza katika matendo mabaya watoto wa mzazi aliyehukumiwa kunyongwa? Inawasaidia kwa jambo gani kuboresha iwe ni maisha ya watoto wa marehemu wa kwanza, achilia mbali yule wa pili?

NIONAVYO MIMI, badala ya kuwanyoga, serikali ingeliwahukumu wafungwa hawa kifungo cha maisha. Huko basi, wangetumika kufanya kazi za uzalishaji mali kama vile uchimbaji wa migodi ya dhahabu, ujenzi na kazi nyingine za uzalishaji mali.

Kwa kufanya hivyo, taifa lingepata faida nyingi kwa sababu gharama za uzalishaji kwa kuwatumia watu wasiostahili mshahara na marupurupu makubwa, zingekuwa ndogo sana.

Aidha, serikali ingeliweza  kuweka utaratibu wa kutoa sehemu kidogo ya faida ipatikanayo kutokana na kazi za uzalishaji mali wa mfungwa huyo, kuisaidia ile familia ya mtu aliyeuawa na mfungwa.

Natambua kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiye pekee mwenye uwezo wa kuamua juu ya hatima ya mfungwa  mwenye hukumu ya kifo, akishauriwa na kamati maalum ijulikanayo kama “Kamati ya Huruma.”

NIONAVYO MIMI, kwa msingi huo, ningeshauri wana kamati, taasisi mbalimbali na vyama vya kutetea uhai wa binadamu, kushauri kwa umakini njia mbadala ya adhabu ya kifo. Kwa kweli haisaidii, sio kwa serikali tu, bali hata kwa jamii nzima.