Je kuna nabii aliyepaa kwenda mbinguni?

Ndugu Ibrahim hili swali lako si dogo kwa sababu ya misamiati miwili.Kwanza neno NABII na pili neno KUPAA.

Nabii ikitafasiriwa kama mmoja aliyewaeleza watu mapenzi ya Mungu. Idadi ya manabii inakuwa kubwa sana. Wanakuwepo kwenye orodha Adamu, Henoko, Abrahamu, Musa, Haruni, Elia, Elisha, Yohana Mbatazaji, Yesu na hata Maria mama yake.

Neno kupaa likiwa na maana ya kutwaliwa mbinguni na Mungu tunalazimika kusema katika historia manabii wanne walipaa mbinguni.

Yaani Henoko (soma Ebrania 11: 5-6). Elia alichukuliwa kwa kisulisuli (2Wafalme 2:11), Yesu na Maria kwa kadiri ya ripoti ya mapokeo.

Lakini idadi hii tuichekeche sasa. Henoko na Elia, Yesu na Maria wote tuwaite manabii? Hilo litategemea makubaliano yetu. Jambo lingine hapo hapo ni udhati na uhalisi wa tendo la kupaa kwenyewe. Mintarafu Henoko imeandikwa katika Waraka kwa (Waebrania 11:5-6) ; hivi kwa imani Henoko alihamishwa asije akaona mauti wala hakuonekana kwa sababu Mungu alimhamisha na kabla ya kuhamiswa Mungu alikuwa ameshuhudia kwamba amempendeza Mungu.

Kwa maneno haya, Henoko haonekani kama amepaa isipokuwa alitwaliwa na Mungu na kutoweka kwake duniani kulikuwa ni kama fumbo na watu hawakuweza kulishududia vema.

Na mitarafu Elia mambo ni karibu hayo hayo. (2 Wafalme 2:11) "Ikawa walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea; tazama kutokea gari la moto na farasi wa moto ikawatenga wale wawili na Elia zikapaa mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Kwa maneno haya ndugu Ibrahimu; Elia hakupaa bali kunyakuliwa kwa namna ya ajabu na kutoweka duniani kwa namna ya ajabu sana.

Na hicho ndicho kisa watoto wake yaani manabii wafuasi wake wakaanza kumtafuta huku na huko wakitumaini kwamba aliangukia mahali fulani mle nchini kwao Ni kusema kuwa Elia hakupaa kwa maana halisi ya neno.

Kadhalika na mapokeo juu ya Maria hayasemi bila simile kwamba Maria alipaa mbinguni isipokuwa tu alichukuliwa kwa mwili wake na Roho kutoweka kwa mtindo wa fumbo.

Basi ndugu Ibrahimu baada ya kuwatoa katika orodha Henoko, Elia na Maria, kupaa kunabaki kwa Yesu peke yake yaani kama tutamtambua Yesu kama nabii hapo turejee Yohana 4: yeye Yesu asipande mbinguni kwa maana halisi sana kitabu cha Luka 24:50-53, na Matendo 1:2, 9-10, na Yohane 2:.

Mintarafu Yesu alikuwa shauri la kutoka duniani kwa namna ya ajabu kwa namna ya fumbo isipokuwa kwenda mbinguni kama alivyokwenda kukaa kwa Baba na kuendelea kutuombea hadi atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu.

Ndugu Ibrahimu maandiko matakatifu yenyewe yanajibu swali lako kifupi jinsi hii; Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni ila yeye aliyeshuka toka mbinguni, yaani mwana wa Adamu, yaani Yesu Kristo Bwana wetu.

Swali jingine la ndugu Ibrahimu Juma linasema Bikira Maria alikuwa na watoto wangapi baada ya Yesu Kristo?

Ndugu Ibrahimu swali lako limezaa majadiliano katika historia ya kanisa. Majadiliano hayo yamezuka kutokana na msamiati uliotumika kwenye sehemu zifuatazo; Mathayo 13:55, Marko 6:3, Yohane 7:3, Matendo 1:14 na1Wakorintho 9:5.

Kwa ajili ya kuwataja ndugu wa Yesu maneno yasiyotumika ni kwa Kigiriki, Adelfe (Dada) wingi wake Adelfai, na kinyume chake Adelfosi (yaani kaka) wingi wake Adelfois.

Katika Mathayo 13:55 na Marko 6:3 watajwa akina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda kama kaka au ndugu wa Yesu.

Ndugu Ibrahimu, majadiliano ni je hao ni ndugu wa Yesu kwa damu ya kuzaliwa kwa mama mmoja au uhusiano wao ni wa namna gani?

Mjadala huu hadi sasa hivi una matawi matatu yaliyo misimamo ya makundi matatu ya watu, kundi la kwanza ndugu Ibrahimu ni la wana mjadala wanaosema kwamba hao waliotajwa kweli ni ndugu wa damu, watoto wengine wa Maria na Yusufu.

Hao hufuata Injili ya Luka 2:7 inaposema kwamba Yesu asikuwa mtoto wa kwanza wa Maria, na hiyo ningemaanisha kwamba alikuwa huyo Maria na watoto wengine waliomfuatia huyo Yesu. Lakini msimamo huu ndugu Ibrahimu unagongana vibaya sana na maoni kwamba Maria alibaki Bikira kabla, wakati na baada ya kumzaa Yesu.

Kundi la pili ni la wanamjadala wanaosema kwamba hao ndugu wa Yesu walikuwa ni watoto wa mzee Yosefu kutoka ndoa yake ya kwanza kabla ya kumwoa Maria.

Huu ni msimamo unaoyakinika.Hata hivyo Agano Jipya halisemi lolote juu ya Yosefu kuwa na ndoa mbili.

Kundi la tatu ni la wanamjadala wanaosimama kwenye utata wa maneno,Adelfai-ndugu wa kike ama dada na Adelfois-ndugu wa kiume au kaka.

Maneno hayo ndugu Ibrahimu yanatafasirika kwa ujamaa mpana zaidi ya ndugu dada au kaka,maana yake pia ni binamu.

Utata wa maneno hayo ndugu ni sawa na ule unao unaosababishwa na neno maarufu sana NDUGU katika kiswahili.

Mmoja akisema anatoka kazini anakwenda kwao kwa likizo ili akawaone ndugu zake atakuwa na maana gani?

Bila shaka atakuwa na maana pana, pamoja na ndugu zake wa tumbo moja, neno ndugu litakuwa linasema juu ya binamu, wapwa, wajomba, shangazi nakadhalika.

Haya, huu ni mfano tu; bahati mbaya neno ndugu ni pana zaidi. Basi msimamo wa wanamjadala wa kundi hili la tatu ni huu kwamba hao wanaotajwa kama ndugu wa Yesu, walikuwa ni binamu wa Yesu, yaani watoto wa Maria kwa Wakleofasi.

Je, sasa tuhitimisheje majadiliano haya; msimamo wa Kanisa Katoliki ni huu ndugu Ibahimu, Maria alibaki Bikira kabla, wakati na baada ya kumzaa Yesu.

Maana yake Yesu alikuwa ni mtoto wa pekee wa Maria na zaidi ya hayo maneno Adelfai na Adelfois yaliyotumika yaani ndugu wa Yesu ni maneno tata yenye kumaanisha binamu pia.

Zaidi ya hayo tukisoma Mathayo 28:10 neno kaka hapo kweli linaonyesha kutumika kwa ujamaa mpana zaidi ya matumizi ya undugu wa kifamilia tu na hoja nyingine inayotolewa na watu siku zote ni hii kwamba laiti Yesu, aliyekuwa na ndugu kama hao, ndugu wa familia moja, basi lingekuwa jambo la Busara kwake kumwacha Maria kwa ndugu zake kuliko kumkabidhi Maria kwa Yohana pale msalabani, kama tunavyosoma katika Injili ya Yohana.

Swali la Mwisho la Ndugu Ibrahimu Juma linasema kuwa kuna sala kuu ngapi?

Swali lako ndugu Ibrahimu linahusika zaidi na Lugha kuliko taaluma ya Biblia. Kitu gani kiitwe kikuu kwa kipengele hiki sala gani iitwe kuu na kwa sababu zipi.

Kiswahili chasema kitu kikuu ni kile chenye umuhimu mkubwa zaidi au cheo ama mamlaka makubwa zaidi na kitu chenye heshima zaidi chenye hadhi au uzuri mkubwa zaidi.

Kwa sababu ya upana wa maeneo ya neno hili kuu, bila shaka utagundua kwamba siyo rahisi watu kukubiliana bila mabishano.

Mmoja atakaposema sala hii ndiyo kuu kutokana na umuhimu wake, mwingine ataonyesha nyingine na kudai ni kuu pia.

Aidha biblia haiwezi kuamua ugomvi huu wa Lugha za binadamu maana yenyewe haisemi popote pale kinaganaga kwamba sala fulani ni kuu. Kutokana na hilo lazima kuogelea kwenye uwanja wa Litrugia na tujaribu kuokoa jambo moja au mambo mawili yatufae.

Ndugu Ibrahimu naomba nikutajie sala ambazo katika historia zimepata kuitwa sala kuu kutokana na umaarufu wake na umuhimu wake.

Mosi ni sala ya msalaba ,sala wanayoitumia wakristo kujichora alama ya ukombozi wao yaani msalaba.Ni sala fupi lakini muhimu sana,hata shetani anaogopa.

Pili ni sala ya Baba yetu, hii ni sala ya mfano aliyotufundisha Bwana Yesu Kristo mwenyewe.Imo katika biblia soma Mathayo 6:9-13 au Luka 11:2-4 ni sala ya msingi ( Baba Yetu) yenye sehemu tatu ambazo ni maingilio,sehemu kuu ya waombi sita na hatima yake.

Tatu ni sala ya Salaam Maria. N isala iliyo na baadhi ya maneno ya Kibiblia mwanzoni mwa ile sala na sehemu nyingine ni maneno yaliyotokana na uchaji wa watu.

Nne sala ya Atukuzwe baba, sala fupi lakini yenye kumsifu Mungu mzima katika nafsi zake zote tatu, yaani Baba, Mwana ndiye Yesu Kristo na Roho Mtakatifu aliye nguvu yetu.

Tano sala ya Imani ndiyo Nasadiki, Kanuni ya Imani, ambayo ni muhtasari wa yote tunayopaswa kuyasadiki katika dini ya Kikristo.

Sita ni sala ya Malaika wa Bwana ambayo wakati wa Pasaka huwa ni Malkia wa mbingu.

Hii au hizo ndizo sala zinazoleta kimuhtasari historia ya wokovu wetu.

Sala hizo kwa kawaida husaliwa asubuhi, mchana na jioni na mara nyingi husaliwa kwa kuambatana na mlio wa Kengele kubwa za kanisa kila mahali.

Saba, sala za vipindi ndizo sala za kutakatikuza siku. Ndiyo breriale ambayo husaliwa alfajiri, asubuhi, mchana, jioni na usiku kama wajibu wa Maaskofu, Mapadre na Mashemasi. Watawa husali pia na leo hii na walei kadhalika.

Mabishano katika kanisa yalikuwa makali kuhusu ukuu wa sala za vipindi, polepole ukuu wake ukapunguzwa mbele ya sala ya Misa.

Basi nane ni sala ya Misa, kwa madhehebu ya Kikristo yenye Misa, Misa ni sala kuu kwa vile ni marudio ya sadaka ya wokovu wetu, sadaka ya Kalvari.

Hata hivyo ndani ya Misa sehemu inayojulikana sala kuu ni hasa kuanzia sala ya utangulizi, Prefasyo na kuendelea sehemu ya mageuzo na sala za EKARISTI ambazo ziko nne za tangu awali na leo hii zimeonyeshwa kufikia zaidi ya saba.

Sala hizo za ekaristi, hufungwa daima na hitimisho kwa kumsifia Mungu (Oksolojia) ambayo hufuatiwa mara na sala ya bwana ndiyo hiyo Baba Yetu.

Tisa ndugu Ibrahim ni sala iliyosaliwa na Yesu kuwaombea wafuasi wake ambayo tunaisoma katika Injili ya Yohane 17.

Yote hapo Kristo anasali kuwaombea wanafunzi wake wabaki katika umoja na mapendo na walindwe hivyo na Mungu mwenyewe.

Swali kubwa sasa ni kwamba Sala Kuu zipo ngapi? Hilo ndilo swali lako.

Ndugu Ibrahimu jinsi nilivyotalii liturujia ya Kikristo namna hiyo unaweza kupata picha ya upana wa majadiliano yaliyopo juu ya sala kuu.

Tatizo ni lugha. Sala ipi iitwe Kuu na kwa sababu ipi. Hata hivyo ukijumlisha majadiliano yanapunguka sana sala kuu ni tatu, Baba Yetu, Sala ya Misa, na sala ya Yesu kuwaombea wanafunzi wake.

Lakini sala zote hizo nilizokutajia si ndogo kwa umuhimu wake.

Maazimio ya warsha ya kukabiliana na maafa yasiwekwe kapuni

Na Neville Meena, TSJ

Warsha ya mafunzo ya njia bora za kukabiliana na maafa iliyomalizika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki mjini Dar es Salaam, iliweka maazimio kadhaa ambayo ni msingi wa kuboresha huduma ya utoaji wa msaada kwa wanaopatwa na maafa, pia njia bora za kukabiliana na maafa hayo.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki (CARITAS) pia iliazimia kuweka mikakati ya kudumu ya kutokomeza visababishi vya baa la njaa nchini, ambavyo vimekuwa sugu katika maeneo mengi kwa muda mrefu hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wengi.

Napenda kuwapongeza sana CARITAS kwa kufanikisha warsha hiyo ambayo inaweza kuwa mhimili muhimu si kwa CARITAS pekee, bali kwa manufaa ya wananchi wa Taifa hili wanaoathirika kwa maafa hivyo kushindwa kutekeleza majukumu mengine katika familia, jamii na Taifa zima kwa ujumla.

Pamoja na pongezi hizo mimi kama mmoja wa waliopata nafasi ya kushiriki napenda kutoa changamoto kwa washiriki wote wa warsha hiyo kusimamia kikamilifu maazimio ya warsha pia kubuni mbinu mbali mbali za kukuza na kuboresha huduma kwa wanaoathiriwa na maafa.

Katika siku nne za warsha hiyo mambo mbali mbali yalijitokeza na kujadiliwa kwa kina. Moja ya mambo yaliyojitokeza ni ushirikiano mdogo kati ya wagawaji wa -caritas-mikoani, serikali kuu, mashirika ya kimataifa na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali (NGOs).

Kwa mujibu wa washiriki wa warsha hii kumekuwepo na kutotambuana miongoni mwa vyombo vinavyotoa huduma kwa wanaoathiriwa na maafa ya njaa, jambo ambalo limekuwa likizorotesha zoezi zima la utoaji wa misaada na wakati mwingine kazi hiyo kukwama kabisa.

Tatizo jingine ambalo lilijitokeza ni uwezo mdogo wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kukabiliana na maafa, jambo ambalo husababisha jamii kupoteza raia wengi hasa maafa hayo yanapotokea ghafla. Tatizo lililochomoza hapa ni vifaa duni kwa ajili ya uokoaji katika sehemu ambazo hupatwa na mafuriko na huduma duni za afya kwa watu hawa.

Mbali na hilo, jingine lililoonekana kuwa tatizo ni kamati za maafa zilizoko mikoani kutofanya kazi zake kama zinavyotakiwa, hivyo kukutana kwa haraka pale tu yanapotokea maafa au wanapotakiwa kugawa chakula.

Hili liliambatana na wajumbe wa kamati hizo kujihusisha na shughuli nyingine kama vile kujihusisha na semina, warsha, safari na shughuli za kibiashara hivyo kuitenga kabisa shughuli ya kukabiliana na maafa na kuwaacha mamia ya raia wakiteseka kwa matatizo ya njaa.

Pamoja na hayo wanawarsha hao waliona kwamba upo umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii itakayosaida kujenga msingi wa kujitegemea kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa ili kuziwezesha familia kuzalisha chakula cha kutosha na ziada kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Ili kufanikisha azimio hilo walipendekeza kuanzishwa kilimo cha umwagiliaji kitakachotumia mbolea za asili katika maeneo yenye ukame na maeneo mengine, pia kujenga utamaduni wa kuhifadhi chakula kwa ajili ya kupambana na maafa ya njaa hasa yatokeapo mafuriko na ukame katika maeneo husika.

Ilitamkwa wazi katika warsha hiyo kwamba asilimia themanini ya watanzania sawa watu milioni 24, wanaishi katika vijiji vipatavyo milioni nne vilivyosambaa nchini kote ambako ndiko kunakotokea matatizo makubwa ya njaa.

Pia ilielezwa kwamba, pamoja na idadi kubwa ya watu wanaoishi vijijini, ni hekta milioni sita tu kati ya hekta milioni 40 zenye rutuba ambazo zinatumiwa na watu hawa kwa ajili ya kilimo.

Pamoja na hayo yapo mambo mengi sana ambayo yalijitokeza kuwa matatizo na njia za kuyapatia ufumbuzi zilipendekezwa ili kuondokana na kabisa na tatizo la maafa ya njaa katika jamii ya watanzania.

Ninaamini kwamba hii haikuwa mara ya kwanza kufanyika kwa warsha kama hii ya kujadili njia bora za utoaji wa huduma kwa watu wanaokabiliwa na maafa ya njaa.

Kuna uwezekano mkubwa sana wa kutotekelezwa kwa baadhi ya maazimio yaliyofikiwa katika warsha zilizotangulia na ndiyo sababu iliyopelekea kuwepo kwa mapungufu mengi katika zoezi zima la utoaji wa

huduma kwa wanaokumbwa na maafa.

Hivyo ni washiriki wa warsha hii wanao wajibu mkubwa wa kuridisha imani kwa wananchi kwa kutekeleza maazimio yaliyowekwa ili kuboresha na kuinua kiwango cha utoaji na ugawaji wa misaada kwa watu waliopatwa na maafa ya njaa hapa nchini.

Pete ya Harusi

lIlianza kuvaliwa miaka ya 1600

lYadaiwa ni nuksi kuinunua Ijumaa

Na Steve Moyo

SIKU zote tumekuwa tukishuhudia watu mbalimbali wakivaa pete katika vidole vyao, lakini bila kuthubutu kujua wapi na lini utamaduni huo ulikoanzia na unahusiana na nini.

<GFIRST 11.35>Hata hivyo kwa miaka mingi sasa utamaduni wa kuvaa pete umekuwa ukihusishwa na sherehe za harusi ingawa katika nchi nyingi imekuwa ni tabia ya kuigwa.

Haijaweza kufahamika wazi ni wapi utamaduni huu wa kuvaa pete ulikoanzia, lakini utafiti unaonyesha kuwa tabia hiyo ilikuwepo tangu katikati ya miaka ya 1600, na Wagiriki ndio watu ambao walionekana kupendelea sana kuvaa pete.

Inasemekana kwamba Wagiriki wataki huo nchi yao ikijulikana kama Uyunani walikuwa na tabia ya kuvaa pete, lakini kwa mtazamo wa mapambano tu na wakati mwingine kwa imani za jadi walizokuwa wakipewa na waganga wao wa kienyeji.

Kasumba ya kuvaa pete katika nchi nyingi, pete huvaliwa kwenye kidole cha nne cha mkono wa kushoto kuanzia kwenye gumba na kubakia kuwa alama ya kuoa ama kuolewa.

Kwa desturi pete hiyo huwa ya dhahabu ama fedha isiyokuwa na urembo wowote, na huelezwa kuwa alama za mapenzi ya kudumu baina ya maharusi yaani bibi na bwana.

Hata hivyo katika baadhi ya nchi, pete ya harusi huambatana na miiko mbalimbali namna ya kuinunua, kuitumia na hata kuitunza.

Kwa mfano katika nchi nyingine inaelezwa kwamba ni mwiko kununua pete ya harusi siku ya Ijumaa na pia kwa mtu mwingine kuijaribu isipokuwa mvaaji mwenyewe tu, na endapo mtu ambaye hajaoa ama kuolewa ataijaribu inaaminika kwamba huenda asioe ama kuolewa maishani mwake.

Aidha kuna imani nyingine kwamba ni nuksi kubwa kwa maharusi kudondosha pete zao kwani inadaiwa kuwa kwa yeyote atakayefanya hivyo huwa ndiye wa kwanza kufariki dunia.

Katika nchi nyingi duniani kabla ya harusi mpambe wa bwana harusi (Bestman) huwa ndiye anayehifadhi pete za harusi, lakini huko Marekani pete huhifadhiwa na kijana mdogo tu kutoka upande mmoja wa familia ya maharusi hao. Hata hivyo licha ya kwamba utamaduni wa kuvaa pete za harusi umekuwa ukitumika katika nchi nyingi duniani, hadi sasa matumizi ya pete za harusi yanatofautiana katika maeneo mbalimbali.

Katika nchi kama Urusi watu huvaa pete kwenye mkono wa kulia hali ambayo ni tofauti na desturi za hapa kwetu Tanzania na Afrika Mashariki ambapo ukivaa hivyo unamaanisha kwamba hujaolewa ama kujachumbiwa ama ni pete ya mapambo tu.

Kwa desturi za Warusi mwanamke anayechumbiwa ama aliyeolewa, huvaa pete yake mkono wa kulia tofauti Afrika Mashariki ambapo kwa kawaida mwanamke aliyechumbiwa ama kuolewa huvaa pete yake mkono wa kushoto.

Hali kadhalika mwanaume aliyeoa huko Urusi huvaa pete yake huvalia pete yake mkono wa kulia, wakati huko Ulaya Mashariki mambo ni tofauti kabisa, kwani kwao mtu kuvaa pete ufahari mkubwa sana.

Mtu wa Ulaya Mashariki huendelea kuvaa pete kwa kuiona kwamba ni mali yake, kitu ambacho amekigharamia kwa hiyo hakuna haja ya kukitupa au kikiacha na wala hawaoni maana kuiweka pete hiyo nyumbani bali kuivaa kama pambo ingawa ni katika mkono wa kushoto.

Kinyume chake huku kwetu iwapo utaoa ama kuolewa na kisha kuachwa au kuacha mtu huvua pete hiyo na kusahau kabisa na wengine huamua kuuza kwa imani za kufuta na kusahau majonzi yake.

 

Kufanana kwa maisha na vifo vya marais Lincoln na Kennedy wa Marekani

Duniani ni jambo la kawaida kutokea kwa watu wanaofanana kimaumbile kama vile sura au sauti, lakini ni mara chache kutokea kwa watu kufanana kimaisha mpaka mauti yao.

Hali isiyo ya kawaida ya kufanana kwa maisha mpaka mauti imetokea huko Marekani kwa watu wawili waliowahi kuwa viongozi wa juu wa taifa hilo.

Watu hao waliotokea kulingana kwa hali ya maisha na mauti yao, si wengine bali ni waliokuwa marais wa taifa la Marekani ambao kwa sasa ni marehemu, Abraham Lincholn na John F Kennedy.

Baada ya kuuawa Rais Kennedy mnamo Novemba 1963, wanahistoria walianza kufanya utafiti juu ya mtiririko wa mambo yasiyo ya kawaida yenye kufanana kwa maisha yake na Rais mwingine wa Marekani aliyeuawa, Abraham Lincoln, karibu miaka 100 iliyopita.

Utafiti huo wa kihistoria wa Marekani juu ya maisha ya marais hao ulionyesha mambo yasiyo ya kawaida yaliyofanana kama ifuatavyo.

Wote wawili Lincoln na Kennedy waliuwawa kwa risasi siku ya Ijumaa, tena wakiwa mbele ya wake zao.

Wakati Lincoln aliuawa katika jumba la mikutano na matu waliokuwa wamejificha juu ya paa, Kennedy aliuwawa kwa risasi zilizomiminwa na mtu aliyekuwa juu ya ghorofa wakati akiwa katika harakati za mkutano.

Katibu Muhtasi wa ofisi ya Lincoln alikuwa akiitwa Kennedy, ambaye alimsihi (Lincoln) asiende katika mkutano, naye Katibu Muhtasi wa Kennedy alikuwa akiitwa Lincoln ambaye pia alimshauri (Kennedy) asiende mkutanoni.

Muuaji wa Lincoln, John Wilkes Booth na muuaji wa Kennedy aliyeitwa Harvey Oswald wanatokea majimbo ya kusini mwa Marekani yaliyokuwa yakipinga serikali ya shirikisho, na wote walikuwa na umri wa miaka ishirini kila mmoja.

Wauaji hao wa Lincoln na Kennedy wote waliuawa kabla ya kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Booth aliyemuua Lincoln alizaliwa mwaka 1839, naye Oswald aliyemuua Kennedy alizaliwa mwaka 1939.

Lincoln na Kennedy baada ya kuuwawa wote nafasi zao za urais zilirithiwa na watu waliokuwa na ubini wa majina ya Johnson.

Andrew Johnson alimrithi Lincoln baada ya kuuawa, wakati Lyndon Johnson alimrithi Kennedy baada ya kuuawa.

Lincoln alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani mwaka 1860, ambapo Kennedy naye alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani mwaka 1960.

Andrew Johnson mtu aliyerithi kiti cha urais cha Lincoln alizaliwa mwaka 1808, naye Lyndon Johnson aliyerithi kiti cha urais cha Kennedy alizaliwa mwaka 1908.

Lincoln wa chama cha Republican alikuwa mzungu wa kwanza mpiga utumwa kuchaguliwa kuwa rais wa 16 wa Marekani, wakati Kennedy wa chama cha Decocratic alikuwa mzungu wa kwanza mpinga ubaguzi wa rangi na Mkatoliki wa kwanza kuchaguliwa kuwa rais wa 35 wa Marekani.

 Watakatifu William wa Sicily na Aybert wa Tournai

lWote walizaliwa na kuishi Italia

IFIKAPO mwezi Apili 7 kila mwaka,wakristo wa Kanisa Katoliki Duniani kote huwakumbuka watakatifu Aybert na William.

Mbali na watakatifu hao wapo watakatifu wengine ambao hukumbukwa kila mwaka katika tarehe hiyo hiyo

Watakatifu wengine ni Hegesippus, Aphraatesn, George The Younger, Celsus au Ceallach, Herman Joseph, Ursulina, Alexander Rawlins, Henry Walpole, Edward Oldcorne na Ralph Ashley.

Mtakatifu William Cufitella alikuwa ni Mfrasiska ambaye alikulia katika kitongoji kimoja jirani na Scicli, Sicily huko Italia, na katika muda wake wa miaka saba alitumia kujifunza mambo ya dini na kuabudu.

Pia wakati wake mwingine aliutimia katika shughuli za kilimo ambapo alikuwa akiendesha kilimo cha mbogamboga katika bustani ndogo ambazo sehemu ya mapato yake aliyatumia katika kuwasaidia masikini, na wagonjwa.

Watu wengi wa eneo hilo la Sicily walimjua na mara kwa mara walipenda kumtembelea na kujifunza kutoka kwake juu ya maisha ya kiroho.

Rafiki wa karibu wa Mtakatifu William alikuwa ni Bruda Conrad wa Piacenza, ambaye yeye mara kwa mara alikuwa akisafiri kutoka mbali kwenye mji wa Pizzoni kwenda kumtembelea mtakatifu huyo.

Mtakatifu William alikufa akiwa na umri upatao wa miaka 25 tu, na siku ya kifo chake mamia ya watu wa Sicily walijitokeza kumzika ambapo kengele za mji wote zilipigwa kuashiria kwamba kuna msiba mkubwa.

Baada ya kifo chake wakazi wa mji huo kwa heshima waliamua kwamba Mtakatifu William awe msimamizi na mlinzi wa mji huo wa Sicily.

Ama kuhusu maisha ya Mtakatifu Aybert au Aibert ,alizaliwa mwaka 1060 katika kijiji cha Espain kwenye dayosisi ya Tournai, na katika maisha yake alijitolea kufanya kazi za Mungu.

Alipokuwa mdogo wakati wa usiku Mtakatifu Aybert alikuwa akitoka kimyakimya akiacha usingizi na wazazi wake kwenda kusali, na alipofikia umri wa ujana aliwataka wazazi wake wampeleke kanisani kusali.

Kipawa cha utakatifu kwa Mtakatifu Aybert kilianza kuonekana hasa kwa wageni waliokuwa wakimtembela ambapo alikuwa akiwasaidia na kuwahubiria mambo ya kiroho pia kufundisha kwamba kila mmoja anapaswa kumjua mwenzake kwa mema.

Hakuna habari ndefu zaidi inayomzungumzia Mtakatifu huyu, lakini moja ya mambo yanayokumbukwa ni ule uwezo wake wa kusali sana rozari, kwani wakati mmoja aliwahi kusali rozari mara hamsini kwa siku moja.

Nini utamaduni wa kifo

Sifa kuu katika utamaduni wa kifo ni kuwa binadamu anakuwa amekufa kidhamiri na hivyo kukosa uwezo wa kutambua, kupenda na kuteteaa uhai na utu wa binadamu. Utamaduni wa kifo hufurahia matendo maovu badala ya matendo mema. Katika utamaduni wa kifo UONGO hutukuzwa na UKWELI huogopwa na kupigwa vita. Uongozi katika utamaduni wa kifo huonekana katika kutoa takwimu zisizo sahihi na kuzitetea katika kuficha kwa makusudi madhara au matokeo ya matendo fulani na matokeo ya nguvu za kimabavu kupitia vyombo mbalimbali vya habari na hata taasisi za fedha na viongozi wasio waangalifu wa nchi.Utamaduni wa kifo huenea kwa kasi kwa kutumia mabavu ya kifedha.Mabilioni ya fedha hutumika katika kutangaza matumizi ya nyenzo za umalaya, kama kondomu,vitanzi, vipandikizi,vidonge, sindano na njia nyingine za kupanga uzazi.

MWANZO WA UTAMADUNI WA KIFO.

Msingi wa utamaduni wa kifo ni ubinafsi, wivu na tamaa.Mawazo mabaya juu ya ‘uhuru binafsi’ndicho kitu kinachojenga msingi katika kisa cha Kaini na Abeli Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu Hapa tunaonyeshwa wazi jinsi roho ya binadamu inavyoweza kugeuka na kuwa mbaya katika "kutamani" mafanikio hata ikasababisha kifo.

Utamaduni wa kifo umeasisiwa, kulindwa, kulelewa na kuendelezwa na taifa la Marekani tangu enzi za Magreth Sanger hadi leo. Nyuma ya programu za kifo Wamarekani wanataka utawala wa kisiasa, kiuchumi, kijeshi na hata kiutamaduni.

Lengo kuu ni kudhibiti kasi ya ongezeko la watu duniani kwa maslahi ya wachache.Mpango wa uzazi unaotumia nguvu ili watu waukubali kwa lazima una chanzo chake katika mabavu ya kisisasa yaliyobuniwa na Marekani Desemba 1974, wakati kitengo cha usalama kilipokamilisha utafiti wake juu ya athari za ongezeko la watu duniani kwa maslahi na usalama wa Wamarekani.Kwa kifupi mpango huu ulijulikana kama ‘NSSM 200’.Mpango huu uliidhinishwa na Dk.Henry Kissinger, Mshauri wa usalama wa Rais Nixon wakati huo.

Mpango huo wa utafiti uliweka shinikizo kwa serikali ya Marekani ili ichukue hatua za kudhibiti ongezeko la watu, kwa "kuwanunua" viongozi mashuhuri wa nchi zinazoendelea wakubali mipango ya kudhibiti ongezeko la watu katika nchi zao. Mpango wa NSSM 200 Ulieleza wasiwasi mkubwa juu ya madhara ya ongezeko kubwa la idadi ya watu katika nchi hizo. Ilionekana kuwa ni tishio kwa usalama wa watu wa Marekani na hasa kama watu hao wanaozidi kuongezeka wangedai mgawo ulio sawa kutokana na pato la dunia. . Pia ilihofiwa kuwa itakuwapo idadi kubwa ya vijana katika nchi zinazoendelea nao wataanzisha upinzani mkubwa dhidi ya ukandamizwaji wa nchi zao ambao unafanywa na nchi zilizoendelea na mashirika ya kimataifa .

Hata hivyo Henry Kissinger na waasisi wenzake wa mpango wa NSSM 200 walichukua tahadhari kubwa ili kuhakikisha kuwa mipango hiyo haijulikani na hivyo kuzuia uwezekano wa mlipuko wa upinzani wa nchi zinazoendelea. Waliahidi kutoa misaada mingi lakini kwa masharti ya kuwa kwanza haki ya mtu binafsi kuamua kwa uhuru wake bila kuingiliwa juu ya idadi ya watoto na namna ya kupanga kizazi ipigiwe debe.Pili nchi zinazopokea misaada ya kimaendeleo, kijamii, na kiuchumi zikubali kwanza sera za kudhibiti ukuaji wa idadi ya watu nchini mwao

MBINU ZA UTEKELEZAJI

Waasisi wa NSSM 200 walitambua kuwa Serikali ya Marekani inaweza kulalamikiwa kutokana na ukweli kuwa misaada katika sekta ya afya imekuwa ikipunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa nchi maskini, wakati misaada kwa programu za idadi ya watu imekuwa ikiongezeka sana . kwa hiyo wakapendekeza kuoanisha programu za idadi ya watu na programu za afya ili matumizi katika sekta hizi mbili yaweze kuchanganywa chini ya kivuli kimoja cha AFYA YA MAMA NA MTOTO

Kutumia mashirika ya kati

Katika ripoti ya mwaka 1977 juu ya utekelezaji wa mpango wa NSSM 200 ilisisitizwa kuwa mashirika ya kati yatumike katika kutekeleza mpango huu kwa vile mashirika hayo yanaweza kufika hadi vijijini. . Mashirika hayo ni pamoja na shirika linaloshughulikia masuala ya idadi ya watu duniani ( United Nations Fund for Population Activities- UNFPA) na Shirika la kimataifa la Mpango wa Uzazi ( International Planned Parenthhood Federation - IPPF). Mashirika hayo mawili yamepatiwa fedha nyingi sana kwa ajili ya shughuli zake; kwa mfano shirika la misaada ya kimaendeleo la Marekani , (United States of Argency for International Development_USAID) mwaka 1989 lilipatiwa dola za kimarekani bilioni 3 kwa shughuli za kudhibiti kasi ya ongezeko la watu katika nchi zinazoendelea. Vilevile Shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) hujishughulisha sana na programu za kudhibiti idadi ya watu duniani.

Mashirika haya ya kimataifa yameshinikiza uanzishwaji wa mashirika ‘shoga’ katika nchi zile ambazo mipango hii inatekelezwa. . Katika hayo yapo mashirika yaliyoanzishwa huko Ulaya na kwingineko lakini hufanyia shughuli zake katika nchi zinazoendelea. Baadhi ya mashirika hayo ni Shirika la Afrika la Utafiti wa madawa (African Medical Research Foundation - AMREF) na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Ujerumani, (GTZ).

Pia Mashirika ya kimataifa ya Fedha, yaani Benki ya Dunia (World Bank) na mfuko wa fedha wa kimataifa, (International Monetary Fund- IMF) ndiyo mashirika mama yanayotoa shinikizo kwa nchi changa kukubali masharti ya mipango ya kizazi kwa njia za kisasa. Uongo unaotumika ni kuwa HATUWEZI KUENDELEA KWA VILE IDADI YETU NI KUBWA MNO. Kwa hiyo tunaamriwa kuwa tusipokubali kujiua hatutapatiwa misaada ya kijamii na kimaendeleo.

Dhana inayoibuliwa hapa ni kuwa misaada tunayopewa hulengwa kwa watu wachache tu; kwa hiyo wingi ni BALAA.

Kujihusisha kwa nchi

Jumuiya ya nchi za Ulaya zilitenga fedha mara dufu kuliko miaka ya nyuma kwa ajili ya kudhibiti kasi kasi ya ongezeko la watu kati ya mwaka 1995 na 1999. Nchi zitakazonufaika na mfuko huo ni zile za Mediterranean,Afrika,Asia,Caribbean na Pacific. Iliamuliwa kuwa misaada yote ya kimaendeleo itakayotolewa kwa nchi hizo kutokana na mfuko huo itakuwa na masharti ya kupokea maelekezo juu ya mipango ya uzazi kwa njia za kisasa. Serikali ya Japan ilitenga dola za Kimarekani 71 milioni kwa shughuli hizo kwa mwaka 1995.

Pia Rais Bill Clinton alipendekeza kwa Bunge lake lipitishe bajeti ya dola za Kimarekani 635 milioni kwa ajili ya kudhibiti ongezeko la watu duniani.

Mikutano na makongamano:

Mkutano wa kimataifa juu ya maendeleo ya jamii uliofanyika huko Copenhagen,Dernmark, Machi 1995 ulihitimisha kwa kusisitiza kuwa suala la utoaji mimba na vitendea kazi vyake vipewe msukumo kwa kwa wasichana na watu wazima kwa kisingizio cha programu za "Afya ya mama" katika nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea.

Hapo mwaka 1994 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani alidhamiria kuandaa muswada wa kuonyesha kuwa ongezeko la watu duniani ni tishio kubwa kwa mazingira. .Maana ya pendekezo hili ni kuwa mazingira ni muhimu zaidi kuliko binadamu. . Katika mkutano uliohudhuriwa na wajumbe kutoka katika nchi 20 za Afrika huko Mauritius,Machi 1994,wajumbe waliofadhiliwa na IPPF waliazimia kupiga vita jitihada za mashirika yanayotetea uhai na kupinga vikwazo vinavyowazuia wanawake kutoa mimba. Kwa wajumbe hao haki ya kutoa mimba ilionekana kuwa ni kitu cha lazima kwa kila binadamu anayependa maendeleo.

Mikutano mitatu muhimu ya maendeleo ya binadamu imefanyika kwa nyakati tofauti na sehemu tofauti. Mkutano wa mazingira uliofanyika Reo de Jeneiro mwaka 1992 pamoja na mambo mengine, ulimwona binadamu kama tishio kwa mazingira.

Kwa hiyo ilikubaliwa kuwa ukuaji wa idadi ya watu uzingatie mazingira. Mkutano wa maendeleo wa idadi ya watu uliofanyika huko Cairo, Misri (1994) ulihitimishwa kwa kusema kuwa ukuajiwa idadi ya watu uende sambamba na maendeleo. Mkutano wa maendeleo wa wanawake uliofanyika Beijing, China 1995 ulishinikiza haja ya kutambua haki na uhuru wa wanawake katika kupanga kizazi.

Maana ya mahitimisho yote hayo ni kuwa mazingira na maendeleo ni muhimu zaidi kuliko binadamu, yaani ikiwezekena binadamu wapunguzwe ili kuleta maendeleo na kulinda mazingira. Pili, wanawake wanadai haki kutoa mimba, uhuru wa kuoana wao kwa wao, na haki ya kuvunja ndoa na kutokuwa na familia.

Huduma katikaa vituo vya kutolea mimba

Huko Ulaya na Marekani vituo vya kutolea mimba (Abortion clinics) vilianzishwa hasa katika maeneo ya shule ili kuwawezesha wanafunzi kutoa mimba kirahisi. Huko Uingereza, kwa mfano imefahamika kuwa serikali inatarajia kuanzisha kliniki nchini kote za kutoa ushauri kwa watoto wa shule katika masuala ya kuzuia mimba na kutoa mimba.

Kupanga uzazi kwa njia za kisasa

Utamaduni wa kifo unawaona baadhi ya binadamu kama kitu hatari sana kwa hiyo lazima azuiwe asizaliwe na kama imetokea bahati mbaya mimba ikatungwa ‘pasipo hiari’ basi lazima auawe. Siyo hayo tu, hata hawa wanaoweza kuzaa waangaliwe ipasavyo.

Basi njia za kisasa za kupanga uzazi zinawaathiri wote, watuamiaji na wale waotarajiwa kupatikana yaani watoto wakiwa bado matumboni mwa mama zao. Njia mbalimbali za kupanga uzazi ni pamoja na vidonge, vitanzi , chanjo, vipandikizi, chanjo, povu, kondomu, na kadhalika. Mbinu hizo zikishindwa basi mauaji kwa njia ya kutoa mimba hufanyika. Masharti ya baadhi ya misaada tunayopwa kutoka nje ni kuwa lazima nchi zetu zikubali kupanga kizazi chao kwa kutumia mbinu/njia hizi za kisasa. Kwa bahati mbaya sana zote hizi zinaleta madhara makubwa sana kwa watumiaji tofauti na zile za kupanga uzazi kwa njia za asili.

Utamaduni wa kifo hapa Tanzania

Hapa kwetu Tanzania utamaduni wa kifo unaojitokeza hasa katika vita halisi dhidi ya uhai wa binadamu umekuwepo kwa chini chini tangu miaka ya 1970, lakini hivi karibuni umejitokeza bayana zaidi hasa baada ya kuanzisha programu za kufuafua uchumi kulingana na maelekezo ya wafadhili wetu.

Katika misaada mingi inayotolewa kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kunakuwepo na masharti ya "mpango wa uzazi kwa njia za kisasa"

Ingawaje utekelezaji wake unaanza tangu miaka ya 1970 , lakini msukumo umekuwa mkubwa zaidi baada ya nchi yetu kukubali kupitisha sera ya Idadi ya Watu mnamo Februari 1992. Sera ya Idadi ya Watu kimsingi hudai mipango ya maendeleo ya nchi ioanishwe na ukuaji wa idadi ya watu. Baada ya kupitishwa sera hiyo Mashirika ya Kimataifa yanayotoa misaada yalielekeza nguvu katika nchi yetu. Kupitishwa kwa sera hiyo kulifungua milango ya kuendesha programu za uzazi wa mpango kwa njia za kisasa.

Ndipo programu za vidonge, sindano, vesektomi, vipandikizi, chanjo na utoaji mimba zilipowewa nafasi kubwa zaidi.

Inaendelea toleo lijalo