Je, katika dini yupo mwenye haki ya kuitwa Baba duniani?

KATIKA Mathayo 23.8-12 Bwana Yesu anawaambia wafuasi wake: Bali ninyimsiitwe Rabi maana mwalimu wenu ni mmoja. Nanyi nyote ni ndugu: wala msimuite mtu baba duniani kwa maana baba yenu ni mmoja aliye wa Mbinguni. Wala msiitwe viongozi maana kiongozi wenu ni mmoja; naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu; na yeyote atakayejikweza; atadhiliwa. Na yeyote atakayejidhili, atakwezwa. Sasa iweje basi baadhi ya viongozi wa kanisa wanaitwa Baba? Hilo ni swali la Ndugu Elias Joseph wa S.L.P. 304, Songea anajibiwa kama ifuatavyo na PADRE TITUS AMIGU wa chuo cha Teolojia Peramiho.

Baba alikuwa alama rejeo katika utendaji na maisha yote ya kiyahudi

Baba inayoelezwa na Yesu hapa ni jina linalorejea kwa wazee fulani fulani wa Israeli.

Wazee kama Ibrahimu na Isaka walikuwa wanajulikana kama mababa (Ayubu na kadhalika). Baba alikuwa na alama-rejeo katika utendaji wa maisha yote ya Kiyahudi.

Mathalani ; Marabi walikuwa wakigombea watu wajenge majumba yenye nafasi kubwa na milango minne.

Kisa ilikuwa kwamba Ayubu aliyekuwa baba alikuwa na nyumba ya namna hiyo kwani marabi walieleza. Ayubu alikuwa mkarimu na mwema sana. Alijenga nyumba yake na kuweka milango minne. Mmoja Kaskazini, mwingine Kusini ; na mwingine Mashariki na mwingine magharibi ili awakirimu fukara na maskini..Na kubwa ni kwamba Ayubu hakutaka kuwapa taabu fukara waliokuwa wakimiminika nyumbani kwake.Basi alipokuja fukara kutokea Kaskazini ilikuwa rahisi kwani aliingia kwenye nyumba ya Ayubu bila kuzunguka kwa upande ule wa Kusini na kadhalika.

Basi; marabi wakampambanisha Ayubu na Abrahamu ambaye alikuwa baba mwingine katika suala hilo la wema wakisema Abrahamu alikuwa zaidi ya Ayubu kwa kuwa yeye hakufanya kama Ayubu alivyofanya, akakaa na kungojea fukara wamjie isipokuwa yeye Abrahamu alikwenda mwenyewe mitaani na mkewe Sarah kuwakusanya fukara na kisha kuja nao nyumbani.

Yule asiyejua nyama katika maisha yake, alipewa nyama ale. Na yule asiyejua maziwa ni nini katika maisha yake alipewa maziwa akanywa.

Na hata yule asiyejua divai ni nini katika maisha yake alipewa divai anywe. Na kana kwamba hilo halikutosha, Abrahamu alihama na kujenga nyumba yake njiani kati ya Abelishi na Yerusalemu; na pale akajenga nyumba ya wazi ambayo wapita njia waliingia na kuvikuta vile walivyohitaji wakala, kunywa na kusaza bila malipo ya aina yoyote.

Hiyo ndiyo maana ya misingi ya baba , hadhi ya Abrahamu au Ayubu, au Isaka; na Yakobo na kadhalika. Baba si baba koko; ni baba hasa. Na mitarafu, Isaka yeye walimpambanisha na Ishmael-baba wa Waarabu.

Mpambanisho huo ndio ilozaa uadui kati ya Waislaeli na Waarabu tangu wakati ule mpaka leo hii.

Walikuwepo walimu, au viongozi wakubwa wakubwa; kwa mfano Gamalieli ni mmojawapo. Na baada ya kuvunja hekalu walitokea Marabi, Walimu Wakuu; ambao mafundisho yao yalikuwa yanayumbisha watu. Watu walikuwa wanajigawa kufuatana na walimu hao.

Kwa mfano; akina Hileli na Shamahi walimu, ndio waliokuwa miamba ya mafundisho.Na hata wao walikuwa kama mahakimu wakuu kwa sababu hakuna hukumu yoyote ambayo haikuendana na torati na ni haohao walimu tu waliojua torati.

Kwa hiyo ndio wao walioulizwa na kushauriwa kutawala mambo yote; na neno lao ndilo lililokuwa uamuzi wa mwisho. Nafasi ya hao viongozi na walimu haikuwa ndogo. Iliwapasa watu kuwaheshimu walimu kuliko baba mzazi.

Kama Rabi au Mwalimu aliumwa wakati baba yako mzazi vilevile anaumwa , ilibidi kwanza kumshughulikia mwalimu wako kabla ya baba yako mzazi. Aidha kama ni suala la kumtolea mmoja wapo dhamana, basi mwalimu au kwa tafsiri nyingine kiongozi, ndiye aliyekuwa na haki ya kuanza kutolewa dhamana kuliko baba yako mzazi.

Hoja ilikuwa kuwa mtu akufundishaye au mtu akuongozaye katika mambo ya sheria au torati, huyo anakupa uzima wa milele. Na uzima wa milele ni bora kuliko uzima wa damu na nyama ambao baba na mama yako wamekupa.

Basi, kwa kufuatana na viwango hivyo vya juu sana, vya Rabi, Baba na Viongozi, ndipo Yesu anapopiga marufuku majina hayo.Yesu anasema "Mmezidi mno;kumbukeni hao marabi au hao viongozi wenu si lolote; wamepewa ualimu kwa kuaminiwa tu. Mwalimu wa kweli ni mimi."

(Hasemi moja kwa moja jambo hili ila tunamuongezea sasa ). Mwalimu wa kweli ni Yesu Kristo kwa sababu Yesu Kristo ni alama ya wazi ya Mungu asiyeonekana.Yesu Kristo ndiye mfano wa ufunuo maana tunajua hapo kale Mungu alijifunua kwa njia ya manabii na kumbe wakati ule alipofika Yesu, Mungu alikuwa amejifunua kwa kilele kabisa katika yule mtoto.

Hayo ni mashitaka kwa marabi. Yaani kwamba hawajifunui kwa Mungu bali wanajifunua kwao wenyewe.

Yaani wale wanaokitumia cheo cha baba kwa misingi ya Abrahamu, Ayubu, Isaka na kadhalika. Hao hawamfunui Mungu baba bali wanajifunua wenyewe.

Mungu haonekani tena kwa sababu ya hao watu, na kwa sababu hiyo ni marufuku kuwa na cheo cha urabi, ualimu au uongozi kwa misingi hiyo.

Yesu anasema watu wale Wayahudi walikuwa ni ndugu waliopaswa kuheshimiana; yaani mmoja asijidai zaidi ya mwingine maana baba yao wa kweli alikuwa ni mmoja na mwalimu wao wa kweli alikuwa ni mmoja ambaye ni Yesu Kristo.

Yaani alitaka kuzuia majisifu na sifa ambazo walipata binadamu na kumfukia Mungu. Mungu ndiye baba na ndiye mwema wa kweli ; anafanya kama Abrahamu na Ayubu. Lakini yeye anawakaribisha watu wote, si kwa milango minne ya nyumba, ila yeye anafanya mambo yote kwa ujumla.

Abrahamu aliwakaribisha watu maziwa, nyama na divai. Ayubu aliwakaribisha watu katika nyumba yake. Kumbe Mungu aliye wa kweli anawatendea wema watu wote wema kwa wabaya; anawaangazia jua watu wote, wema kwa wabaya- wa hapa na walio mbali.

Na kadhalika anawanyeshea mvua yake watu wote. Huyu Mungu ndiye baba na asili ya wababa wote. Na hivyo Kristo anataka kusema hapa "Muachieni basi jina la baba huyo Mungu, msijiite ninyi"

Na juu ya walimu hivyo hivyo, Kristo anachukua nafasi ya walimu wote, maana ndiye anayemshuhuduia kwa dhati baba kwa maana ndiye aliyemwona baba akitenda na ndiye aliyemsikia baba yale anayosema.

Kwa maana hakuna aliyemwona baba ila Kristo peke yake. Kwa maneno haya Kristo anasema baba ni mmoja-Mungu, na Mwalimu ni mmoja-Kristo.

Sasa ndugu Elias leo hii katika familia wapo akina baba. Mashuleni wapo walimu, Serikalini wapo viongozi.

Huko tuache tubaki kanisani ambapo wapo wanaoitwa Baba au Viongozi au Walimu au Wachungaji. Majina hayo ndugu Elias yanatumika kwa niaba tu. Baba inatumika kwa niaba ya Mungu Baba. Mwalimu inatumika kwa niaba ya Mwalimu Mkuu- Yesu Kristo, na Viongozi kadhalika na Wachungaji kadhalika. Yaani inatumika kwa niaba tu ya Mchungaji Mkuu yaani Kristo Bwana wetu au Mungu mwenyewe ambaye ni Mchungaji Mkuu, kadri ya Agano la Kale. Yaani ndugu Elias, Ualimu wa watu wa kanisa ni taswira ya ualimu wa kweli wa Kristo, na ubaba wa watu wa kanisa ni taswira tu ya ubaba wa Mungu mwenyewe. Isipoeleweka hivyo ndugu Elias hatustahili kuitana Baba, Viongozi au Walimu.

Na kumbe kama tukielewa kuwa majina hayo yanatumika kama kwa niaba tu, basi kuna kila uhalali kuendelea kuyatumia. Yaani tunapenda iwe hivi; hukumuona mtu anayeitwa Mwalimu katika kanisa uone kwamba anamwakilisha Mungu aliye baba wa kweli, na hivyo hivyo kiongozi uone kwamba anamwakilisha Mungu aliye kiongozi wa kweli kwa mambo ya kiroho.

 Ujenzi wa mfereji wa Suez

lNi njia muhimu ya maji iliyojengwa na binadamu

lUlichukua muda wa miaka kumi

Wanadamu katika siku za awali waliweza kuvuka mito na kusafiri katika maziwa na bahari kuu wakitumia magogo ya miti.

Baadae walijua kuyachimba magogo hayo katikati ili waweze kukaa ndani yake ambapo kwanza waliyaita mitumbwi na hata leo mitumbwi ya namna hiyo bado inatumiwa sehemu nyingi duniani.

Lakini watu walioishi katika nchi na miji mikubwa iliyo kando ya kingo za mito mikubwa iliyo kando ya kingo za mito mikubwa wao walianza kuunda mashua zilizopo bora za kusafiria na waliweza kusafiri huku na huko.

Katika safari zao hizo waliweza kuchukua bidhaa kwa kufanya biashara na pia waliweza kuvua hata samaki kwa kutumia mashua hizo zilizovutwa na makasia.

Baadaye kidogo kidogo binadamu walianza kusafiri kwenye milango ya mito kuelekea baharini na hatimaye kusafiri kandokando ya bahari kwenda katika nchi nyingine wakisafirisha bidhaa zao.

Hatimaye waljifunza kuunda merikebu kubwa ili waweze kusafiri salama baharini, merikebu ambazo ziliweza kusafiri pwani kutoka nchi hadi nchi.

Kufuatia maendeleo ya kiuchumi, kibiashara na kisayansi wanadamu walitafuta njia rahisi ya mkato ili kuweza kupitisha maji ya meli kupita kuunganisha mabara yote ya dunia.

Kwa mfano hapo kabla, safari ya maji kuweza kufika bara la Asia kutoka Ulaya ililazimika kupita kusini mwa Afrika; njia ambayo ni ndefu iliyowachukua miezi na majuma kadhaa kufika huko.

Lakini kutokana na kutafuta maendeleo ya haraka binadamu wakaamua kuchimba mfereji mkubwa wa Suez katika eneo la shingo la bara la Afrika na nchi za Mashariki ya Kati ili kuweza kurahisisha safari za Ulaya na Asia.

Mfereji huo wa Suez ukawa ndio njia ya kwanza kubwa ya maji duniani iliyotengenezwa na binadamu ambayo inaunganisha bahari ya Mediteranean na Bahari ya Sham.

Mfereji huo una urefu wa kilomita 169 na ndio njia fupi ya maji ya bahari baina ya Bahari ya Hindi na bara Ulaya.

Kazi ya kuuchimba mfereji huo ilianza Aprili 1859 na ilifanywa na kampuni moja ya Kifaransa ambayo iliundwa kwa makubaliano ya Misri na Ufaransa.

Mfereji huo ambao ni kiungo muhimu cha Ulaya na Asia ulianza kufanya kazi Novemba 17, mwaka 1869 na unapunguza urefu wa safari ya bahari baina ya Ulaya na India kwa kilomita 8,000.

Kufunguliwa kwa mfereji huo kulifanya njia fupi na mpya baina ya Ulaya na Afrika Mashariki pamoja na Asia Kusini na Mashariki.

Ulipofunguliwa; shughuli za Suez ziliendeshwa baina ya Ufaransa pamoja na Uingereza , lakini hali hii ilibadilika mnamo mwaka 1956 wakati serikali ya Misri ilipoutaifisha mfereji huo.

Lakini tangu wakati huo hadi sasa mfereji huo unaendeshwa na Mamlaka ya Mfereji wa Suez, ambayo ni kampuni iliyoundwa na Serikali ya Misri.

Mpaka sasa Mfereji wa Suez ni moja ya njia muhimu inayoiingizia serikali ya Misri kiasi kikubwa cha fedha kwani serikali hiyo inapata karibu dola milioni 2,000 za Marekani kila mwaka .

Hivi sasa ni zaidi ya mika 126 tangu mfereji huo wa Suez uanze kufanya kazi.

Pamoja na kuwa unaiingizia Misri fedha nyingi lakini mtumizi yake yanapungua kwa kiasi fulani kutokana na kukua kwa teknolojia duniani.

Hilo linadhihirishwa na jinsi shughuli za mfereji huo zinavyozidi kupungua mwaka hadi mwaka.

Awali mapipa milioni 2.3 yalikuwa yanapita katika mfereji huo kila siku kutoka bahari ya Sham hadi Mediteranean, lakini sasa kiasi hicho cha mafuta kinapitishwa kupitia mabomba ya mafuta.

Juni mwaka 1967 wakati wa vita vya Mashariki ya Kati baina ya Israeli na mataifa ya kiarabu kwa makusudi Misri iliufunga mfereji huo na kuzamisha baadhi ya meli zilizokuwa hapo.

Mfereji huo ulifunguliwa tena miezi minne baadaye , lakini tayari athari zilikuwa zimeshatokea kwani makampuni ya meli yalianza kutumia meli kubwa sana ambazo haziwezi kupita katika mfereji.

Ingawa sasa mfereji huo umepanuliwa , lakini bado meli nyingi zinatumia njia ndefu ya kupita kusini mwa Afrika njia ambayo ndio iliyokuwa ikitumiwa hapo zamani.

Hivi sasa mamalaka ya mfereji huo wa Suez inafanya juhudi ya kuweka vivutio kwa meli kubwa kama vile kupunguza ushuru na kuzidi kupanua mfereji wenyewe na kuboresha huduma .

Mwaka juzi mamalaka hiyo ilipunguza ushuru kwa asilimia 20 kwa meli zinazosafirisha mafuta , na asilimia 30 kwa meli zinazopakia gesi kutoka Qatar kwenda Ulaya lakini bado hali haijawa nzuri.

 

Mfungwa anayehusudu na kusifia ladha ya nyama ya mtu

lVyombo vya habari vinaruhusiwa kumhoji

lAnadai alikuwa anapewa na polisi

"Nilikuwa ninakula sehemu zenye minofu peke yake,"anajieleza huku akiinua mikono yake iliyofungwa kwa minyororo na kuongeza, "Mapaja ndiyo niliyoyapendelea. Lakini, nilikuwa situpi ulimi na macho kwani ndiyo yaliyokuwa yakinisaidia kuifanya supu kuwa nzito, yenye nguvu na iliyochangamka."anaeleza Bw. Derangel Vergas

Hasiti kueleza bayana namna alivyokuwa akiipendelea nyama hiyo ya wanadamu wenzake jambo ambalo licha ya waandishi wa habari kuwa na uzoefu wa kukutana na mikasa mbalimbali ya namna hiyo, linawafanya wajikute wanatweta kwa hofu wakijawa na nyuso zao zilizoanza kupauka kwa mshangao na kupigwa na mduwao kadri wanavyozidi kuhojiana nae.

Huku akitabasamu alipohojiwa hivi karibuni kama kwamba alilolifanya ni la kawaida, Derangel Vergas ambaye ni miongoni mwa wafungwa wanaosota katika gereza lililoko katika jiji la San Cristabal huko Venezuela mpakani mwa Columbia,anasema ,

"Umaskini ndio ulionilazimisha na kunifanya nile nyama za watu maana sikuwa na njia wala pesa za kunitosheleza kupata mahitaji yangu ya lazima kama chakula. Lakini nilipojaribu, niligundua kuwa zilikuwa nzuri na ninajijutia kwani nilifanya kosa la kuchelewa kuanza kuila.

Waandishi walipomhoji endapo anajisikia mkosaji kutokana na tabia hiyo, Vargas anasema, "Jamani; nimewambia ninajisikia furaha sana na nilikula nyama nyingi za watu kadri nilivyoweza kupata na hata ninajuta kuchelewa kuanza. Hata hivyo kila mtu anaweza kula nyama ya mtu hata nyie. Lakini ukumbuke kuwa unatakiwa uioshe na kuiandaa vyema ili kuepuka magonjwa."Anasisitiza katika majibu yake yanayowashangaza wengi.

Hata hivyo jamaa huyu ambaye aliwekwa katika gereza hilo pasipo kufunguliwa mashitaka ya mauaji kwa kutuhumiwa kuua na kula nyama za watu wapatao 15 hatua ambayo popote pale duniani ni makosa makubwa, anadai hakuwahi kula nyama ya mwanamke kwa madai kuwa wanawake hawana matata na watu na anadai kuwa sababu kubwa ya kupendelea kula nyama za wanaume, ni kwamba uchunguzi wake wa awali uligundua kuwa nyama ya mwanaume ni yenye ladha tamu zaidi.

Vergas anaendelea kueleza kuwa katika sehemu na viungo vya mwili, hakuwa anapendelea kula miguu, mikono na sehemu za siri na anaonong’oneza kuwa "Nilikuwa ninapendelea nyama ya vijana na wazee vikongwe maana nyama ya watu wanene ina aina fulani ya ukinai wa haraka mno kuliko ya wazee na vijana ambayo ni tamu kwelikweli."

Tofauti kubwa iliyopo kwa Vergas na wafungwa wengine ingawa hajafunguliwa mashitaka ni kwamba polisi wanaviruhusu vyombo vya habari kufanya mahojiano naye kwa kadri wanavyopenda.

Hata hivyo suala la kudai kwake kuwa anapendelea ladha na nyama ya binadamu linaonyesha kuwa na mashaka fulani akili yake.

Anakanusha kuwa hakuwa akiwateka na kuwakamata wanao randaranda na wale wanaofanya kazi za kujitolea na kwenda kuwaua kwa kuwapiga nondo, bali yeye mwenyewe anadai alikuwa anapewa miili hiyo na watu mbalimbali wakiwemo polisi.

Polisi wao wanaeleza kuwa inasadikiwa kuwa Vergas alikuwa akiwawinda watu usiku akiwaponda hadi kufa akitumia nyundo na nondo;na kisha kuipeleka miili hiyo nyumbani kwake chini ya daraja lililofichwa na majani ambako alikuwa akiwa katakata kwa kutumia shoka lake kali mithili ya wembe mpya.

"Lakini huenda mtu huyu alikuwa akitumiwa na watu waliokuwa na shida ya viungo vya binadamu kwa ajili ya biashara"Ndivyo wanavyosema baaadhi ya watu waliohojiwa na vyombo mbalimbali vya habari huku polisi wakikariri kuwa bado wanaendesha uchunguzi kuona kama mtu huyu aliwahi kutiwa mbaroni miaka minne iliyopita kwa madai hayo. Hata hivyo madaktari waliompima akili kufuatana na tuhuma hiyo walimwachilia huru kwa madai kuwa hakuwa na taswira wala mwelekeo wa kuwa hatari kwa jamii.

Mtu huyu alikamatwa nyumbani kwake eneo la milima ya kijiji cha Tariba; baada ya majirani kugundua mikono miwili na miguu uwanjani kwake na ndilo likawa chimbuko la kujionea kwao maajabu aliyokuwa akiyafanya mtu huyu ndani ya banda lake la kuogofya hadi sasa.

 

Askofu Balina aelezea chanzo cha mauaji ya kishirikina Mwanza, Shinyanga

Itakuwa si mara ya kwanza kwa Mtanzania yeyote kusikia juu ya mauaji ya kikatili yanayofanywa na baadhi ya watu dhidi ya wazee katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga kwa madai ya kuwa wazee hao ni wachawi.

Mara nyingi wazee wanaokumbwa na balaa hili ni wale wenye macho mekundu, kigezo ambacho hutumiwa na wauaji hawa kwa ajili ya kutekeleza mauaji yao ambayo yamekuwa ni gumzo kubwa katika jamii ya watanzania siku za hivi karibuni.

Kutokana na mauaji hayo ya kutisha, tayari serikali, mashirika ya kutetea haki za binadamu na mashirika ya kidini yametoa wito wa kutokomezwa vitendo hivyo vya kinyama ambavyo ni kinyume na haki za binadamu.

Ni vigumu kuelewa na nini chanzo cha mauaji haya ya kikatili ambayo yalikuwa hayajazoeleka katika jamii ya Watanzania waliozoea amani na utulivu.

Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Shinyanga Aloysius Balina amesema vitendo hivyo vya kutisha ni matokeo ya elimu duni miongoni mwa wakazi wa mikoa hiyo ya kanda ya ziwa hasa mkoani Shinyanga.

Askofu Balina ambaye pia ni msimamizi wa kipapa wa Jimbo Katoliki la Geita mkoani Mwanza anasema kwamba wakazi wengi wa mkoa wa Shinyanga hawana elimu ya kutosha, hali ambayo huwafanya kuwa na imani za kishirikina katika kila tatizo linalolipata.

Anaeleza kwamba msukuma asiye na elimu hatambui kama mtoto anaweza kuugua au kupatwa ugonjwa bila kulogwa jambo ambalo huwapelekea kuishia kwa kutegemea waganga wa kienyeji ili kupata huduma za matibabu.

Anawataja waganga wa kienyeji kama chachu ya mauaji hayo kwani katika upigaji wa ramli huwadanganya wateja wao kwa kuwapa taarifa zisizo sahihi kwamba huwa wamelogwa na wazee wenye macho mekundu.

Anayataja magonjwa kama vile utapiamlo, kwashakoo na Siko Seli kuwa kichocheo kikubwa katika kukuza mauaji hayo kwani hupelekea watoto wengi kuwa na hali zisizo za kawaida kama vile miili yao kudhoofu, kuvimba tumbo na kukosasa nguvu katika miili yao.

Askofu Balina anafafanua kwamba wengi wa wanaokumbwa na matizo haya hawana mawazo ya kuwapeleka watoto wao hosipitali kutokana na ufinyu wa elimu juu ya afya za jamii.

"Mwanamke hawezi kabisa kutunza familia kama hana elimu inayomuwezesha kufanya hivyo na wanawake wengi wa usukumani hawana elimu ya kutosha kwani huacha masomo na kukimbilia kuolewa", anasisitiza Askofu huyo.

Aidha askofu huyo anaeleza kwamba ki-mila urithi wa wasukuma ni ng'ombe na si elimu, na kwamba hiyo ndiyo sababu kubwa ambayo huwapelekea kutotilia mkazo juu ya upatikanaji wa elimu katika jamii hiyo.

Mbali na elimu duni katika mkoa wa Shinyanga Askofu Balina amelitaja tatizo jingine kuwa huduma duni za afya ambapo alisema kuwa mkoa huo hauna hosipitali za kutosha kuwahudumia wanachi.

Kutokana na hali hiyo amesema kwamba ni vigumu sana kwa jamii kuelewa umuhimu wa huduma za afya hali huduma hizo hazipatikani kwa urahisi katika maeneo yao.

Anaeleza kuwa hiyo ndiyo sababu kubwa ambayo hupelekea waganga wa kienyeji kuwa tegemeo pekee la wakazi wa Shinyanga jambo ambalo linahatarisha afya na maisha yao kwa ujumla pia kuleteleza kuwepo kwa mauaji ambayo yamekuwa yakitokea.

Ili kukabiliana na matatizo Askofu Balina anaelezea mikakati ya Jimbo lake ya kujenga shule mbili za bweni kwa ajili ya wasichana mkoani Shinyanga zitakazohakikisha kuwa wanafunzi wote watakaojiunga na shule hizo wanahitimu ili kujenga jamii yenye uwezo wa kielimu.

Askofu huyo anaeleza kuwa mbali na mkakati huo Kanisa Katoliki lina mpango wa kujenga hosipitali moja kwa ajili ya kutoa huduma za afya pia kuanzisha mpango wa elimu ya afya kwa wananchi wa Shinyanga ili waweze kufahamu umuhimu wa kwenda hosipitali kila wanapopata matatizo.

Kama Kanisa la Mungu askofu Balina anasema kuwa wanahubiri na kuwaonya waumini wao kuwa kuua ni dhambi na kwamba ni kinyume na amri na mapenzi ya Mungu.

Hata hivyo Askofu huyo anawashawishi wazaliwa wa mkoa wa Shinyanga waliobahatika kupata elimu ambao wanaishi jijini Dar es salaam na kwingineko mikoani, kujenga tabia ya kuupenda mkoa wao kwa kutoa changamoto kwa wakazi wanaoishi katika vijijini ikiwa ni pamoja na kutoa michango ya kimaendeleo kama vile ujenzi wa shule na hosipitali.

Anaeleza kwamba pamoja na mapungufu makubwa yanayoukabili mkoa wa Shinyanga, mkoa huo unaweza kubadilika tu kama wazaliwa wake walioelimika watakuwa na ari ya kuinua kiwango cha elimu katika mkoa wao.

Anaonya kwamba kama wataendeleza tabia ya kuishi mijini na kusahau jukumu la kuuendeleza mkoa wao, basi kuna hatari kiwango cha ujinga kikaendelea kuongezeka hivyo kuleta athari kubwa zaidi katika jamii yao.

Akizungumzia kushuka kwa maadili katika jamii na Taifa kwa ujumla Askofu Balina anasema kuwa ni jamii yenyewe inayopaswa kulaumiwa kwa kutotoa mwelekeo kwa vizazi vinavyozaliwa.

Anaeleza kwamba mara baada ya uhuru na Azimio la Arusha yalianza kujitokeza mambo kadha wa kadha ambayo yalikuwa kinyume kabisa na maadili ya kiafrika hivyo kuwa chanzo cha uozo uliopo hadi sasa.

"Tulikuwa na shule zetu za misheni ambazo zilikuwa zikiendeshwa kwa misingi ya kiMungu na watoto wetu walikuwa wanakua wakiwa na maadili mema, lakini baada ya kutaifishwa kukawa hakuna tena mkazo katika nidhamu na maadili mema", anabainisha askofu huyo.

Anafafanua kwamba baada ya kutaifishwa kwa shule hizo hakukuwa na njia mbadala ya kudhibiti nidhamu za wanafunzi kama ilivyokuwa katika shule za misheni, hivyo kila mwanafunzi kufanya kama alivyokuwa akitaka.

Anaeleza kuwa vitendo viovu na vya ajabu kama vile ubakaji, uvutaji wa madawa ya kulevya, ulevi wa pombe uliokithiri na mengine mengi ni matokeo ya kudidimia kwa maadili katika jamii na kwamba ni jamii yenyewe inayoathirika kutokana na hali hizi.

Askofu huyo wa Shinyanga anasema kwamba imekuwa ni vigumu kutokomeza maovu haya kwa haraka kwa sababu tatizo kama biashara haramu ya madawa ya kulevya inapata msukumo kutoka kwa baadhi ya watu wenye nyadhifa kubwa katika jamii yetu.

Mbali na kuendelea kuhubiri makanisani, Askofu Balina anaeleza hatua nyingine za kukabilia na hali hiyo kuwa ni kuanzisha shule zinazomilikiwa na makanisa ili kujenga upya jamii yenye maadili mema kama ilivyokuwa awali.

Aidha Askofu Balina anatoa changamoto kwa jamii, mashirika yasiyo ya kiserikali, serikali yenyewe na makanisa kwa ujumla kuungana katika kujenga upya jamii yenye maadili mema na kuongeza kwamba kazi hiyo si ya muda mfupi na kwamba inahitaji ushirikiano, moyo wa kujituma na kujitoa.

Mtakatifu Plato wa Ugiriki

lAliuza mashamba yake na utajiri wake wote akawagawia masikini

Wazazi wa Mtakatifu Plato walifariki katika mji wa Constantinople ambao sasa unaitwa Instanbul huko Ugiriki wakati huo akiwa ni mwenye miaka 13 tu.

Kutokana na kifo hicho cha wazazi wake, mjomba wake aliyekuwa mweka hazina wa utawala wa kifalme alimchukua kumlea na kumpatia elimu na ambapo baadae alimfanya kuwa msaidizi katika kazi yake.

Lakini akiwa na umri wa miaka 24, kijana huyo alianza kuonyesha kipawa chake katika maisha ya kidini, na kuachana na mambo ya ulimwengu.

Aliuza shamba lake la urithi, na kisha hapo alizigawa mali zote alizopata kwa dada zake wawili na masikini, baadaye akafanya safari kwenda kuishi Birthynia kwenye nyumba ya watawa katika mlima Olympus.

Baada ya kufuata mwenyewe mafundisho ya dini, Plato akiwa katika nyumba hiyo ya watawa alijifunza kazi mbalimbali ikiwemo kufanya kazi za kuandika vitabu akiwa pamoja na mapadre.

Baada ya kifo cha Theoctistus katika mwaka 770, Plato aliteuliwa kumrithi nafasi yake wakati huo akiwa na umri wa miaka 36 tu.

Wakati huo ilikuwa ni kile kipindi cha hatari kwa watawa wa Kikristo wa madhehebu ya Orthodox ambapo watawa hao walikuwa wakikamatwa na kufungwa chini ya utawala wa mfalme Constantine Copronymus.

Katika mwaka 775 Mtakatifu Plato alitembelea Constantinople ambako alipata mapokezi na heshima kubwa sambamba na kutunukiwa heshima mbalimbali ikiwemo kupatiwa nyumba ya kitawa ili awe Askofu wa Nicomedia, lakini yote hayo aliyakataa kwa sababu alikuwa bado hajasimikwa rasmi kuwa mkuu wa mafundisho ya dini.

Baada ya hapo aliamua kwenda kuishi Symboleon kuwa mkuu wa Sakkudion, kigango kilichoanzishwa jirani na Constantinople na watoto wa dada yake Theoctista.

Mtakatifu Plato alikiongoza kigango hiki kwa muda wa miaka kumi na mbili hadi alipojiuzulu na kumwachia mpwa wake Mtakatifu Theodore Studites.

Wakati huo ilikuwa ni kile kipindi ambacho mfalme Constantine Porphyrogenitus alitengana na mkewe Maria na kumuoa Theodota.

Mjomba na mpwa wakawa ni viongozi wa jumuiya ya kitawa ambayo baadae ililegalega

baada ya Mtakatifu Plato kukamatwa na kuwekwa kizuizini na utawala wa kifalme.

Alipofunguliwa kutoka kizuizini alikwenda kuishi tena kwa ulinzi wa hali ya juu katika

nyumba ya watawa ya Studius akiwa pamoja na mpwa wake. Baadae aliamua kuishi hapo na kuendeleza kazi za kitawa kwa muda wake mwingi akitoa mafundisho ya dini na kazi mbalimbali za mikono, lakini akiendelea kupinga vitendo viovu walivyofanyiwa watu na utawala wa mfalme Nicephorus na mwishowe alihamishwa na kwenda kuwekwa katika kisiwa cha Bosphorus licha ya kwamba alikuwa mzee na mgonjwa.

Kwa zaidi ya miaka minne aliendelea kufanya kazi zake akiwa kisiwani humo akihama hapa na pale. Mwishowe katika mwaka 811 mfalme Michael wa kwanza alitoa amri Mtakatifu Plato aachiwe huru.

Alipotoka uhamishoni akarejea Constantinople ambako alipokea heshima nyingi baada ya kustaafu shughuli zake za kitawa. Akiwa huko miongoni mwa watu waliofika kumtembelea na kumuombea alikuwa Mtakatifu Nicephorus ambaye awali alikuwa akipinga mafundisho yake ya kuwa mtawa. Hatimaye baada kipindi kirefu cha maisha ya utawa Mtakatifu Plato alifariki dunia mnamo Aprili 4, 814, na Mtakatifu Theodore aliongoza ibada ya mazishi yake.

 

Sheria hulindwa na adhabu

Ni jambo la kawaida kwamba kila ilipo jumuiya yo yote ile ya binadamu kunakuwa na sheria zenye kuilinda hiyo jumuiya. Sheria tungeweza kusema ni vifungu vya maneno vilivyokubalika kikatiba katika jumuiya iwayo yote ile. Ili sheria hizo ziweze kushikwa, basi hapo huwa kuna wakubwa au wenye mamlaka ambao kazi yao ni kuangalia kama hizo sheria au taratibu zinashindwa na hivyo wahusika waweze kuishi na kutenda kwa amani na utulivu. Kwa hiyo basi lengo la sheria po pote pale ni kudumisha amani na utaratibu.

Sisi binadamu tunazo jumuiya nyingi sana hapa ulimwenguni. Kuna ile jumuiya ya msingi na ya kwanza, nayo ni jumuiya ya familia. Katika familia kuna sheria zake, kuna taratibu zake za kufuata hata kama hazikuandikwa katika vitabu basi huwa kama vile zimeandikwa katika mioyo ya wanafamilia. Licha ya hiyo jumuiya ya familia kuna vile vile hasa siku hizi zile jumuiya za shule. Kila shule kwa kawaida ina sheria zake ambazo wanafunzi wanapaswa kuzishiriki.

Huko majeshini nako kuna sheria zao za kijeshi na hao wanajeshi hulazimika kuzishika ili mambo yaweze kwenda vizuri na kwa utaratibu. Licha ya hayo majeshi kuna pia jumuiya za kidini. Kila dini au kila dhehebu la kidini lina sheria zake na ambazo wafuasi wake wanapaswa kushika.

Watu huwa wanaanzisha vikundi mbalimbali vya michezo au vya biashara. Mambo hayawezi kwenda vizuri ikiwa kama hakuna katiba au sheria za kufuata.

La sivyo mambo yatakwenda kombo na hivyo kutofikia malengo yake. Hiyo ni mifano michache tu, lakini tunalotaka hasa kuonyesha ni kwamba sheria ni za lazima kabisa katika kila jumuiya.

Lakini haitoshi kabisa kuwa na sheria bila kuwepo adhabu kwa wale ambao wanavunja sheria.

Kwa hiyo sheria sharti ziende pamoja na adhabu kwa kila mvunja sheria. Daima sheria inapotungwa lazima isemwe ni adhabu gani itampasa yule mwenye kuvunja sheria iwe ni kwa makusudi au kwa bahati mbaya.

Mara nyingi sana hutokea kwamba watu wananung'unika kwa sababu wale wenye kuvunja sheria hawaadhibiwi ipasavyo. Manung'uniko hayo yameenea sana katika nchi yetu ni hivyo kumekuwa na swala la rushwa. Wahalifu wengi hawakuadhibiwa vya kutosha au hata kutokuadhibiwa licha ya uthibitisho wa makosa yao katika jamii. Hivyo mara nyingi watu husema kwamba haki haikutendeka, yaani mhalifu hakuadhibiwa kisheria.

Mambo huwa mabaya zaidi hasa wakati inapotokea kuwa mhalifu hatari kama vile jambazi ameachiwa licha ya kuonekana wazi kuwa ni mhalifu.

Hapo wananchi hujichukulia sheria mkononi {jambo ambalo si vizuri} na kumwadhibu yule mhalifu bila kutumia vifungu vya ssheria. Kwa hiyo wale wenye kusimamia sheria wanaweza kuleta hali mbaya katika jamii ikiwa kama haki haitendeki. Mhalifu huadhibiwa bila kipimo cha sheria kwa mfano mtu ambaye amekamatwa akitaka kuiba kuku, hupigwa hadi kifo. Tunasema hao wahusika wamejichukulia sheria mkononi, lakini tukirudi nyuma tunaona kwamba waliosababisha hayo ni wale ambao wana dhamana ya sheria na hawakutimiza wajibu wao wa kuwaadhibu wahalifu ipasavyo.

Adhabu kama adhabu inatakiwa imfunze mhalifu, na hata ikiwezekana imbadilishe tabia yake. Kwa hiyo adhabu zile wapewazo wanafunzi shuleni tunatumaini kwamba huwasaidia katika kubadilisha tabia zao. Hatutarajii kwamba adhabu kwa mwanafunzi itakuwa ni kitendo cha kumwonea, bali ni kwa ajili ya kumrekebisha tabia yake.Kwa sababu hiyo mwalimu au mlezi atamwadhibu mwanafunzi siyo kutoka na chuki bali ni kutokana hasa na upendo alio nao kwa huyo mwanafunzi. Hapo huwa ni jambo la kushangaza tunaposikia kuwa mwalimu fulani kamwadhibu mwanafunzi hata akauharibu mwili wake kwa majerani na hata kumtia kilema. Hayo tunasema si malezi na wala haiwezi kamwe kumjenga tabia huyo mwanafunzi.

Mlezi au baba ye yote yule hawezi kumwadhibu mwanae hadi kujenga uadui kati yao. Mvunja sheria kama tulivyosema hapo juu ni sharti aadhibiwe kisheria. Ni kweli kuwa haiwezekani kuandika sheria zote na katiba zote, lakini zinapaswa kufahamika na wahusika na hapo zipovunjwa mhalifu asishtuke anapoadhibiwa.

Ni lazima mhalifu atambue kuwa baada ya kuvunja sheria katika jamii adhabu hufuata, lakini pengine hutolewa msamaha kwa kuwa labda yule mhalifu kafanya kosa hilo kwa mara ya kwanza au pengine alikuwa katika mazingira magumu.

Hata hivyo ni lazima akiri kosa lake na ikiwezekana aahidi kwamba hatarudia kulifanya kosa hilo tena. Tunapenda kumalizia Hoja hii kwa kusema kwamba sheria ni lazima ziweko katika kila jumuia na ushirika.

Hizo sheria ni sharti ziende pamoja na adhabu na ikiwezekana na tuzo pia kwa wale ambao wameshika vizuri sheria hizo.

Wahalifu wanapaswa kupewa adhabu yenye kulingana na kosa walilolifanya.

Adhabu isizidi uzito wa kosa, na hivyo si vizuri kwa mtu kujichukulia sheria mkononi mwake.

Unyanyasaji wa kikemikali dhidi ya wanawake na watoto

SUALA la unyanyasaji limekuwa likizungumzwa na hata kupingwa na watu wengi kwa msisitizo tofauti . Ni bayana kuwa watu wengi wanaozungumzia suala hili huzungumzia katika mtazamo wa kijinsia ambapo mwanamke huonekana kunyanyaswa na mwanaume kwa kupigwa kulawitiwa, kubakwa na hata kulazimishwa kuolewa. Unyanyasaji wa aina hii hutumia nguvu au mabavu. Katika makala hii Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Uhai nchini (Pro-Life Tanzania) Bw. EMIL HAGAMU anaelezea aina nyingine ya unyanyasaji iliyo mbaya lakini isiyofahamika sana.

Sheria mbalimbali zimetungwa ili kulinda makundi manyonge katika jamii kutokana na unyanyasaji wa akina mama kupigwa, kubaguliwa, kubakwa na kadhalika. Mfano halisi ni Sheria ya Kujamiiana ya mwaka 1998 ambayo inamhukumu anayepatikana na hatia apate kifungo cha muda mrefu au hata cha maisha. Lakini jamii haijui kama upo unyanyasaji mwingine ambao hauzungumziwi na ambao huendeshwa kwa kampeni kubwa za kitaifa na kimataifa. Watu wameghilibiwa akili na hivyo kuufanya unyanyasaji huu ukubalike na kutokuonekana kama unyanyasaji.

Unyanyasaji wenyewe ni ule wa kikemikali unaofanywa na mashirika ya kimataifa kwa kushirikiana na makampuni yanayotengeneza kemikali za sumu dhidi ya wanawake na watoto ambao unakingwa chini ya kivuli cha UZAZI WA MPANGO KWA MAENDELEO YA NCHI NA AFYA YA MAMA NA MTOTO.

Unyanyasaji huu umepenya katika damu na akili za binadamu kiasi kwamba umehalalishwa na kuhimizwa katika nchi zote duniani ambapo wakuu wa nchi kupitia wizara za afya na baadhi mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’S) huutekeleza wakiamini kuwa wanawasalimisha watu wao.

UZAZI WA MPANGO KWA NJIA ZA KISASA

Asili ya nadharia ya mpango wa uzazi kwa njia za kisasa ni katika misingi mitatu ambayo ni;

-Hofu kuwa idadi ya watu inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko uwezo wa uchumi wa kuhudumia watu.

-Kwamba binadamu wameumbwa kwa ajili ya kufurahia tendo la kujamiiana.

-Ubeberu wa kiuchumi unaoendeshwa na mataifa makubwa. Ili kufanikishwa azma yao, mkakati wa kumfanya binadamu atumie mbinu zozote zile kudhibiti ongezeko la watu na wakati huo huo afurahie tendo la kujamiiana ambalo wanadai halipaswi kuwekewa mipaka hutekelezwa.

Utekelezaji

Sera za idadi ya watu hupitishwa na kutekelezwa kwa nguvu zote. Hapa kwetu Tanzania sera ya idadi ya watu ilipitishwa mwaka 1992 na nguvu za kimabavu zinatumika siku hizi kwa kutumia mamilioni ya fedha za wafadhili katika kuwalazimisha wananchi wazikubali na kuzitumia njia za kisasa za kupanga uzazi zinatokana na nadharia hizo, licha ya kuwa na idadi ya Watanzania ni ndogo sana ukilinganisha na ukubwa wa eneo na mali iliyopo ambayo bado haijavunwa vya kutosha kwa faida ya watu au inafujwa tu na baadhi ya makundi ya watu .

Watetezi wa kupanga uzazi kwa njia za kisasa wanajua fika kuwa lengo lao la ndani ya kabisa sio kuimarisha afya ya mama na mtoto bali ni kupunguza idadi ya watu kwa njia ya mwanamke na mtoto.

Ili malengo yao yafanikiwe wanafanya mambo yafuatayo;

Wanasema uongo, yaani wanawadanganya wananchi juu ya madhara ya matumizi ya vidonge, sindano , vipandikizi, vitanzi na madawa mengine yanayowekwa ukeni na mwilini. Kwa hiyo uongo ndio kinga na ngao yao kubwa.

Wanatumia kampeni na fedha nyingi ili kufanya mambo yao yakubalike. Kundi la kwanza linaloaminishwa ni viongozi wa serikali na wa dini. Kundi la pili ni la wanasiasa na kundi la tatu ni wataalamu katika fani ya afya.

Njia zitumikazo katika kuwaaminisha ni mbili. Mosi kupitia mashirika ya kimataifa na pili kupitia Wizara ya Afya. Kwa vile kwa kufanya hivyo mpango wa uzazi kwa njia za kisasa unakuwa wa kiserikali, basi hutumika vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali na hata vinavyomilikiwa na watu binafsi katika kuhamasisha wananchi.

Miundo ya utawala ya serikali hutumiwa sana na waenezi wa propaganda hizi chafu.

Mipango hii ikishakubalika kwa njia ya sera ya idadi ya watu , yeyote anayediriki kusema madhara yake anaonekana adui na jitihada hufanywa ili kumnyamazisha. Misemo "kama huyu ni mzushi, mjinga , mpinga maendeleo, mpinzani wa maadili ya taifa na mipango ya serikali" hutumika sana na ikibidi sheria hutumika kumnyamazisha mpinzani, hata kiuonevu.

Wanawake na watoto hunyanyaswa kikemikali kwa namna nne.

KWANZA: Kemikali zitolewazo na madawa ya kupanga uzazi hudhuru afya zao, kila mmoja kwa kiwango chake kwa kuharibu mwenendo wa kawaida na maumbile.

PILI: Wanawake hujengewa mtazamo hasi dhidi ya uja- uzito.

TATU: Mwanamke anajiweka katika hali ya utayari wa tendo la zinaa wakati wowote ule.

NNE: Mama hulazimika kuua watoto wachanga bila wao wenyewe kujua.

LENGO LA UNYANYASAJI HUO NI KUWAFANYA WANAWAKE WAWE TASA.

Kwa hiyo kemikali zitokanazo na madawa ya njia za kisasa za kupanga uzazi badala ya kuimarisha afya huzorotesha afya na kuwafanya wanawake wawe wanyonge daima. Hubadilisha tabia ya watumiaji, huvunja ndoa na huvunja uhusiano katika jamii. Unyanyasaji wa aina hii pia huonekana kwa macho kwani wanawake wanaumwa kweli na hata kudhoofika kweli.

Unyanyasaji wa aina ya pili hauonekani kwa macho. Madawa ya kupanga uzazi hutumia hormoni bandia za estrogeni na progestorene ili kumfanya mwanamke asipate mimba au mimba iliyotungwa iharibike. Hormoni bandia ya estrogeni huzuia yaani kukomaa na hivyo kuzuia uwezekano wa mimba kutungwa.

Hormoni ya projestorene huharibu ngozi laini ya tumbo la uzazi na hivyo kumfanya mtoto aliyekwisha tungwa afe kwa kukosa hifadhi na lishe.

MATOKEO YAKE: Kutokana na kampeni kubwa ya program za kupanga kwa njia za kisasa yaonekana kuwa asilimia kati ya 60 na 80 ya wanawake wanazijua njia hizo, na asilimia kati ya 30 na 60 ya wanawake hapa Tanzania hutumia njia hizo.

Hii ni kusema kuwa ifikapo mwaka 2025 kati ya asilimia 70 na 90 ya wale wanaotumia njia za kisasa watakuwa wameathirika kiafya kiasi kwamba hawataweza kuzaa tena na wastani wa kizazi cha Watanzania kitakuwa kimeshuka kutoka watoto 5.9 ( 1997) kila familia hadi 2.1 kila familia na kuongezeka idadi ya watu kitapungua kutoka asilimia 2.5 (1997) hadi 1.5.

Takwimu hizi zitatusaidia kuonyesha kuwa kinyume cha matarajio ya wengi idadi ya Watanzania itazidi kupungua kwa kadri tunavyoelekea milenia ya tatu.

Unyanyasaji wa kikemikali kwa wanawake na watoto upo wa aina tano.

Mosi unyanyasaji unaotokana na kuwafanya wanawake wawe wagonjwa kwa sababu ya sumu wanazoziingiza na kudumu mwilini.

Piliunyanyasaji kidhalili unaofanywa wanawake waingize / waweke miilini mwao vitu visivyotakiwa ( vidonge, sindano, Vitanzi) mara zote waamuapo kuvitumia.

Tatuunyanyasaji wa kisaikolojia unaowajengea hofu ya ugonjwa ambao kwa hakika haupo.Mantiki ya madawa haya ni kuwa mtoto/ mimba au uzazi ni ugonjwa, yaani umama ni laana!

Nnewanawake wanaweka katika hali ya ukatili kwa kuwaua watoto wao [pasipo wenyewe kujua au hiari yao ( baadhi wanaua kwa hiari).

Tano unyanyasaji wa kibiashara na kisayansi wa kuwafanya wanawake waendeleze biashara ya madawa hayo. Na majaribio ya madawa hayo hufanywa hasa kwa wanawake wa nchi zinazoendelea.

Ili kuwaepusha wanawake kutokana na adha hii ya unyanyasaji tunatakiwa sote kwa pamoja tuwaelimishe wananchi juu ya madhara yatokanayo na njia za kisasa za kupanga uzazi . Wanawake wengi wa Kiafrika wakielimishwa wataondokana na njia za kisasa za kupanga uzazi. Hilo ndilo jukumu kuu la Pro- Life TANZANIA yaani kuwajengea wanawake heshima, utu, na nidhamu katika maisha yao.