Je, katika dini yupo mwenye haki ya kuitwa Baba duniani?

KATIKA Mathayo 23.8-12 Bwana Yesu anawaambia wafuasi wake; Bali ninyi msiitwe Rabi maana mwalimu wenu ni mmoja. Nanyi nyote ni ndugu; wala msimuite mtu baba duniani kwa maana baba yenu ni mmoja aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi maana kiongozi wenu ni mmoja; naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu; na yeyote atakayejikweza; atadhiliwa. Na yeyote atakayejidhili, atakwezwa.Hilo ni swali la Ndugu Elias Joseph wa S.L.B 304, Songea na anajibiwa kama ifuatavyo na Padre TITUS AMIGU wa Chuo cha Teolojia Peramiho.

Maandiko hayo yanasema.

Je, baba, Rabi na viongozi anaowazungumzia Yesu ni akina nani? Ndugu Eliasi, tukumbuke sura ya 23 ya Mathayo kwamba ni sura maarufu sana kwa maneno makali dhidi ya Mafarisayo na Waandishi wao. Ndugu Eliasi, anayoyasema Yesu hatuwezi kuyaelewa vema bila kuingia ndani ya Injili yenyewe.

Yaani hatuwezi kuyaelewa au kuyaeleza vyama nje ya uwanja wa wasikilizaji wenyewe au wasikilizaji wa kwanza.

Kwa wasiklizaji wale waandishi wa Mafarisayo, mabingwa wa Teolojia wakati ule wa Yesu, majina Rabi, baba na mwalimu au tafsiri nyingine kiongozi yalikuwa na maana maalumu kwao; maana rasmi kabisa.

Rabi maana yake BWANA WANGU au Mkubwa wangu. Lilikuwa jina la hadhi kubwa sana. Mtu alijipatia hadhi hiyo baada ya kipindi kirefu cha kisomo na taabu nyingi.

(I) Alipaswa kumfuata mwalimu wake popote alipokwenda akimtazama afanyayo na kuyasikiliza asemayo. Aidha alipaswa kumheshimu mwalimu huyo zaidi ya baba yake mzazi. Uanafunzi huo uliomsulubu mtu kwa kweli ulidumu muda mrefu. Pengine ulidumu hadi mtu alipokaribia umri wa miaka 40.

Na kwa kipindi chote hicho ndugu Eliasi mwanafunzi kwa kawaida alitakiwa kukaa mseja bila kuoa.

Taabu za kupata cheo cha Rabi zilikuwa nyingi; lakini kama wasemavyo watu, mwisho wa uwanja ndio mwanzo wa nje. Alipomaliza mwanafunzi kujifunza Urabi na alipofaulu, alifaidi bila mipaka.

Watu wote walishuhudia jinsi Rabi alivyofaidi na hasa wajane walidhulumiwa zaidi ya marabi.

Rabi alipanua hirizi zake yaani zile hirizi zilizoandikwa "shemaa" yaani Amri ya kumpenda Mungu kwa moyo wote, kwa nguvu zote, kwa akili zote na pia kuwafundisha watu na watoto mambo hayo na kuyaandika mlangoni na kadhalika.

Hizo hirizi zilipanuliwa; na huyo Rabi aliketishwa kwenye viti vya mbele katika karamu na aliketi mbele katika Masinagogi ambako kwa kweli hawakuwa na kazi yoyote ya kuifanya.

Na hao marabi walijipitisha pitisha masokoni ili wapate kuhangaikiwa na watu kwa kusalimiwa na kusikia jina la cheo chao wakiitwa Rabi! Rabi! Rabi!. Hayo ndugu Eliasi ndiyo mambo yanayotangulia Injili yetu katika sura hiyo ya 23 aya za 5 na 7.

Cheo cha Rabi kilipomfikia mtu, ndio ulikuwa mwanzo wa kuwanyenyekesha walala hoi na hii ndiyo maana ya neno rabi ambayo Kristo anaikataza.

Jina "Baba" nalo lilikuwa na hadhi maalumu kabisa.

Baba inayoongelewa na Yesu hapa; ni jina lililorejea kwa wazee fulani fulani wa Israeli; wazee kama Ibrahim na Isaka walikuwa wanajulikana kama Mababa, Ayubu kadhalika.

Baba alikuwa ni alama rejeo katika utendaji na maisha yote ya kiyahudi

Itaendelea toleo lijalo

 

Je, Biblia husema nini kuhusiana na pombe?

..Inatoka toleo lililopita

Ndugu Eliasi umeuliza ni kwa nini Wakristo tunaona kunywa pombe ni halali?

Swali la kinyume kwa swali lako lingekuwa hili: Kwa nini tunakataza watu kunywa pombe hata kidogo? kwa sababu gani

sisi sote tunaomfuata Kristo hatuna budi kufuata mafundisho yake pia ambayo tunayachota kwenye Biblia?.

Wakristo Wakatoliki wameongeza kuyachota mafundisho hayo katika chemichemi nyingine ya mapokeo yaliyofikia watu wa kanisa kutoka kwa wale waliomsikia na kumfuata Kristo kabla yao.

Katika chemichemi hizo mbili yaani Biblia na mapokeo, hakuna mahali popote ambapo divai imekatazwa kwamba isiguswe. Hadi kitabu cha mwisho cha Ufunuo ukianzia kitabu cha kwanza, hilo ndilo limejulikana kwamba divai haikukatazwa kuguswa katika Biblia nzima.

Zaidi ya hayo, kutokukatazwa kwa pombe msingi wake umo katika somo maarufu sana la Injili ya Marko 7:14-23.

Mkisoma katika toleo la zamani sana la Kiswahili kilichotumika huko Zanzibar tangu 1937, sehemu hiyo ya Injili inasomeka hivi: Ikaliita tena lile kundi na kuliambia; visikilizeni vyote mjue maana hakuna kitu kichoponje ya mtu kinachoweza kumtia uchafu. Kikiingia ndani yake; ila yanyomtoka mtu ndiyo yanayomtia mtu uchafu.

Kama yupo mtu mwenye masikio; na asikie. Kisha alipondoka penye watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake wakamuuliza mfano ule; akawaambia, "Kumbe nanyi hamjaelevuka hata leo? Hamjui kila kitu kilicho nje ya mtu kikimwingia hakiwezi kumtia uchafu kwa kuwa hakimwingii moyoni; ila tumboni kisha kikatoka chooni?

Ndivyo alivyotengua miiko yote ya chakula, akasema linalomtoka mtu ndilo linalomtia uchafu.

Kwani ndani; mioyoni mwa mtu hutoka mawazo mabaya, ugomvi, wizi, uuaji, choyo, unyang'anyi, ubaya, uasherati, kijicho, matusi, majivuno na upuuzi. Mabaya haya yote hutoka ndani na ndiyo yanayomtia mtu uchafu.

Je, ndugu Eliasi, unaelewa hayo?

Tupo wengi sana ambao mpaka sasa Bwana Yesu angeweza kutuambia "kumbe nanyi hamjaelevuka; hamjui pombe na kitu chochote kilichoko nje kikimwingia mtu hakiwezi kumtia uchafu?

Kwa vyovyote katika somo hilo la Injili Yesu anatilia maanani neno KIASI maana twajua wote kwamba japokuwa nyama imehalalishwa, ikiliwa kupita kiasi ni ULAFI na ulafi ni dhambi na dhambi inaweza kumdhuru mtu akafa.

Twajua sote kwamba kitu safi kama ugali na wali kikiliwa kupita kiasi ni ulafi. Sasa je, ndugu Eliasi vyakula hivyo vipigwe marufuku kwa vile vinaweza kuhatarisha afya vinapoliwa kwa ngazi ya ulafi?. Na pombe kadhalika ndivyo.

Ndugu Eliasi, kunywa kidogo hakuleti madhara na ni baraka kwa Mungu. Hayo ndiyo yanayosikika katika Zaburi 104:15

La pili, kunywa kupita kiasi ni ulafi, na ulafi wa pombe au kinywaji kuna jina la pekee yaani Ulevi, na ulevi ni dhambi maana unaweza kumdhuru mtu kiafya na kiakili. Je, ni kwa mamlaka gani twaweza kubagua ulafi kati ya ulafi mwingine?

Yale mambo ambayo Yesu anasema yanamchafua mtu kweli kweli yanasabishwa na vitu au watu tunaowaheshimu. Mambo ya uzinzi, ugomvi, uchoyo, uuaji, majivuno, kijicho, matusi, na upuuzi, tunaweza kujifunza toka kwa wazazi wetu, rafiki zetu, shule tunazosoma, miji na hata vijiji tunakoishi.

Je, ndugu Eliasi tusizaane kwa kuwa kuna hatari ya wazazi na watoto kufunzana mabaya? Au tusisome shuleni kwa sababu kuna uwezekano wa kufnzana mabaya? Au tuhame vijiji na miji ili tukaishi peke yetu vichakani kwa sababu kuna uwezekano wa kufunzana mabaya na vijijini?

Huoni Bw. Eliasi swali lako linavyopanuka na hata kuchekesha.

Basi naomba nifunge jibu langu juu ya uhalali wa pombe kwa maneno haya" Angalisho la tangu enzi zile limekuwa moja tu; Kiasi katika yote.

Kiasi katika unywaji ni jambo la maana na jema na hivyo kinywaji kinakuwa baraka ya Mungu; huo ni ushuhuda wa Zaburi 104:15; na kupita kiasi ni ubaya; tuseme kwa uwazi kabisa: Ni dhambi.

Hata hivyo taabu itakuwa ni moja tu, tena taabu ya kale; nayo ni kujua kiasi ni kiasi gani? Watu kadhaa wa kadhaa wamekuwa wakijidanganya kuwa wamelewa na waliolewa wamesemwa kwenye Biblia kwamba walishindwa kumudu mambo na busara zao zilitawanyika.

Mtume Paulo anawashauri akina Timotheo na Tito kwamba watu wasiojua kiasi ni kipi, wasichanguliwe kuwa viongozi wa Kanisa; wala si maaskofu, wala si mashemasi. Kutokunywa au kutoishughulikia divai au pombe ni pendekezo na ushauri tu unaotolewa na Biblia katika sehemu zifuatazo: Mathayo 16: 24-25, anaposema Yesu kwamba anayetaka kumfuata ajitwike msalaba wake maana atakayedhani anaipoteza roho yake, ndiye huyo atakuwa anaiokoa; na yule atakayekuwa anaisalimisha, atakuwa anaiangamiza.

Na Injili ya Marko 49:42-43 ambapo Yesu anasema kuwa kiungo chochote katika mwili wako kikikukwaza kikate; kwani ni aheri kuingia mbinguni ungali kilema, kuliko kuingia motoni ungali na viungo vyako vyote. Na mapendekezo kama hayo; yanapatikana katika barua kwa Warumi 14:13-21 na barua ya kwanza kwa Wakorintho 8:8-13 na barua kwa Waefeso 3:18.

Sehemu hizi ndugu Elias ninarudia, "zimetoa ushauri tu", siyo amri kwa watu wote hata wale wenye uwezo wa kujua kiasi ni nini; kutojishughulisha na pombe au divai.

Kusema divai au pombe isinywewe hata kama ni kwa kiasi tu, si jambo la Kibiblia. Hayo yametokana na utalii wa Biblia niliofanya.

Biblia isisingiziwe. Kama tunataka wasijishughulishe na pombe kwa namna yoyote ile hata bila kujali kiasi kwa vile watu wengi wameshindwa kuitawala pombe na badala yake wanatawaliwa nayo, mimi sina mamlaka ya Kibiblia, itafutwe chemichemi nyingine na Biblia isiwemo ndani.

 

Mashine ya kukata majani

lYa kwanza ilivumbuliwa na Bw. Budding mwaka 1930

KWA kawaida majani ni moja ya mapambo mazuri katika nyumba na pia ni kihifadhi kizuri cha mazingira hasa katika kuzuia mmomonyoko wa ardhi na pia kutoa hewa nzuri kwa binadamu.

Lakini majani hayo yakiachwa kuwa marefu na mengi huwa ni uchafu na hata wakati mwingine kuhatarisha usalama wa watu na viumbe wengine katika nyumba kwani huweza kuhifadhi wadudu hatari kama vile nyoka wenye sumu kali.

Hata hivyo majani mazuri (sio maua) ambayo yanapendeza na kuvutia kupandwa katika nyumba au bustani ni yale ya aina ya nyasi zinazotambaa ardhini.

Nyasi hizo zikipandwa na kutunzwa vema mbali na kuvutia pia husaidia katika kuzuia mmonyoko wa ardhi katika mahala zilipopandwa.

Miaka mingi iliyopita inasemekana kwamba binadamu alipoanza kuishi katika nyumba badala ya mapangoni alijua umuhimu wa kuwepo kwa majani katika mazingira ya nyumba yake.

Moja ya mambo ambayo binadamu wa kale aliona faida kubwa ya kutunza majani katika nyumba yake inaaminika kwamba ni kuyatumia kwa ajili ya chakula chake na pia kwa mifugo yake aliyokuwa akiifuga.

Hata hivyo baadaye miaka iliposonga mbele na kutokea mabadiliko makubwa katika maendeleo, binadamu aliyatumia pia majani hayo kama pambo na kihifadhi cha mazingira badala ya chakula kama ilivyokuwa awali.

Katika kuyaweka vema majani hayo ili yaonekane kuwa pambo zuri la nyumba baadaye kulihitajika vifaa kwa ajili ya kuyakata na kuyatunza vema, katika mpangilio unaovutia.

Baadhi ya vifaa vya mwanzoni kabisa vilivyokuwa vikitumika kwa ajili ya kuyakata na kuyaweka katika sura nzuri majani hayo ni mapanga, mundu na visu vikali.

Lakini baadaye kutokana na utafiti mkubwa uliokuwa ukifanywa na binadamu mashine ya kukatia majani hayo na kuyaweka katika hali nzuri na yenye mvuto ikavumbululiwa.

Mashine ya kwanza kabisa ya kukata majani katika hali ya usawa ilivumbuliwa Uingereza mwaka 1830 na Bw.Edwin Budding aliyekuwa Mhandisi katika kiwanda cha Gloucestershire.

Bw.Budding alivumbua mashine hiyo ya kukatia majani kutokana na mashine yake aliyoitegeneza awali ya kukatia nguo.

Kwanza kabisa inaelezwa kuwa Bw. Budding alihofu kuitwa ama kudhaniwa kuwa ni mwendawazimu kiasi kwamba alikuwa akiijaribu mashine hiyo ya kukata majani wakati wa usiku tu ili asipate kuonekana na mtu yeyote yule.

Akitoa taarifa yake juu ya mashine hiyo mwaka 1830, Bw.Budding alisema, "Wananchi wenzangu watakaoitumia mashine hii huenda wakaiona ni ya manufaa na ya kufurahisha".

Bw.Budding alitoa taarifa hiyo kwa vile mashine yake hiyo ya mwanzoni ilikuwa nzito sana na yenye kelele nyingi, hivyo akidhani kwamba huenda wananchi wasingeikubali.

Miaka miwili baadaye mabwana Ransomes, Sims na Jeffries wa kiwanda cha utengenezaji mashine cha kule mjini Ipswich, nao walitengeneza mashine za kukata majani kuigiza muundo wa Bw. Budding ambaye aliwapa idhini yake (copyright).

Hata hivyo mashine hizo zilirekebishwa baada ya miaka michache na ilipofikia mwaka 1852 wakawa wameuza zaidi ya mashine 1,500 huko Uingereza.

Kama ilivyo desturi ya Waingereza ya kupenda sana bustani pamoja na michezo kama vile soka, kriketi na gofu, basi wakawa tayari kudhamini soko kwa chochote kile ambacho hukata majani chini na kwa usawa katika viwanja hivyo.

Kutokana na 'mtaji' huo wa Bw. Budding baadaye mashine za kukata majani zenye kutumia 'horse power' zilivumbuliwa mwaka 1870 ili kufanikisha kazi katika viwanja vikubwa zaidi.

Hadi ilipofika mwishoni mwa miaka hiyo ya 1800, viwanja zaidi ya mia moja vya mchezo wa gofu nchini Uingereza vikawa vinajivunia majani mazuri yaliyokatwa kwa mashine za Ransomes.

Katika mwaka 1900, Bw.Ransomes alitengeneza mashine ya kwanza ya kukata majani inayotumia petroli ambayo mtu anaweza kukaa juu yake na kuiendesha ama kuisukuma.

Hadi ilipofika mwaka 1939, Bw. Ransomes na washirika wake waliweza kutengeneza zaidi ya mashine 80 kwa mwaka kiasi ambacho wakati huo kilikuwa kikubwa, na nyingi ya mashine hizo ziliuzwa nje ya Uingereza.

Hii leo kampuni hiyo ya Ransomes inauza nje ya Uingereza karibu nusu ya mashine zake inazotengeneza. Moja ya mashine za kwanza kabisa za Bw.Budding ilifukuliwa chini ya ardhi huko Australia na hii ikawa ni uthibitisho kwamba Uingereza ilikuwa inauza nje mashine hizo kuanzia katikati ya miaka ya 1800.

 

Nondo yamtoboa kichwani sentimita sita na kupona

lMadaktari wadai ilikuwa operesheni ngumu kwao

MFANYAKAZI mmoja wa ujenzi, Bhekumuzi Zwane wa Afrika Kusini kutoka eneo maarufu la Kwazulu Natal amenusurika kufa kwa kinachoonekana kama miujiza baada ya kutobolewa na nondo kichwani kwa sentimita 6.

Akiwa ameshafanya kazi katika eneo hilo la Secunda kwa wiki mbili, Bhekumuzi alipatwa na kisanga kisichokuwa cha kawaida baada ya nondo iliyokuwa katika mkunjo wa 'U' kudondoka kutoka umbali wa mita 40 na kutoboa kofia yake ya usalama iliyokuwa kichwani na kupenya hadi kwenye fuvu lake kwa urefu wa sentimita sita.

Akijieleza katika kuonyesha kwamba alikuwa mtu wa kuhangaikia sana maisha, mtu huyo mwenye umri wa miaka 33 sasa, alidai baada ya miaka miwili akitafuta kazi ili kuisaidia familia yake iliyoko kijijini KwaZulu Natal ndipo alipata kazi eneo hilo la ujenzi.

Pamoja na ugumu wake, anasema alijitahidi na ndipo akiwa chini akisaidiana na wenzake kupandisha jukwaa kwenye lifti alishtukia kitu kimetua juu ya kichwa chake hadi kusimamisha nyimbo za wafanyakazi wenzake kama ilivyo kawaida katika kuongeza mori wa kazi nzito.

"Kulikuwa na sauti ya ajabu ikipekesha kichwani mwangu. Nilifikiri sasa nakufa. Baada ya hapo niliona giza, sikujua kilichoendelea baada ya hapo," alijieleza Bhekumuzi.

Dk.Piet Slabbert ambaye ni mtaalamu wa upasuaji wa ubongo aliyekuwa zamu katika hospitali ya Pretoria Mashariki wakati mfanyakazi huyo akifikishwa mahututi alieleza kwamba alifika akiwa amepoteza fahamu.

"Ilibidi tufanye kazi haraka. Nondo ilikuwa imepenya ndani sentimita 6 katika ubongo wake. Ilikuwa ajali mbaya sana," alieleza Dk. Slabbert. Daktari huyo alieleza kwamba operesheni yake iliwachukua saa 2.30. Kofia yake ya usalama ilikatwa kwa kutumia mikasi ya upasuaji, baadaye kichwa chake kilishikishwa mahala na kumnyoa nywele na ndipo juhudi za kuitoa nondo hiyo iliyokuwa na urefu wa sentimita 25 zilipoanza kwa uangalifu mkubwa.

Dk. Slabbert alieleza kwamba hata hivyo kazi hiyo ilikuwa ngumu, kwani kipande cha nondo kilichokuwa ndani ya ubongo wake kisingelichomolewa kiurahisi. Operesheni ikawa ya aina yake.

"Ilibidi tukitoe taratibu, tukihofia kuharibu njia za damu kuelekea kwenye ubongo. Tulipofaulu, tuligundua kulikuwa na vipande kadhaa vya mabaki ya kofia na mifupa ikiwakama sufu katika jeraha lake." alieleza Dk. Slabbert. "ilikuwa miujiza kwake kupona." alishangaa.

Baadaye Bhekumuzi alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi ambako aliunganishwa kwenye chombo cha kupumulia kwa siku 10, ili asipatikane na madhara mengine yakiwamo ya kuvimba ama kutanuka kwa ubongo wake ambako daktari huyo alieleza kwamba kungesababisha ugonjwa mwingine.

Hata hivyo, madaktari walikuwa wakihofia kuwa jicho lake la kulia litaathirika, kutokana na nondo hiyo kupenya katika eneo la ubongo linalosaidia kuona, lakini walishangaa jinsi alivyoanza kupata ahueni.

Bhekumuzi mwenyewe akiwa ameshatimiza mwezi mzima (Desemba mwaka jana), alijieleza kwamba hakuamini macho yake kwamba kweli amepewa kutokana na jinsi alivyoziangalia picha za X-ray zikionyesha jinsi nondo hiyo ilivyokuwa imepenya kwenye kichwa chake.

"Mpaka sasa sijui ni vipi nilinusurika na ajali hii ya kutisha," alisema huku akiwa tayari kurejea tena kazini, baada ya madaktari wake kuthibitisha alikuwa amepona, lakini wakiamini amepona kimiujiza.

Madaktari wanadai ni mtu mwenye bahati ya pekee, mzima na anayeweza kurejea kazini kama kawaida.

 

Mtakatifu Patrick wa Ireland atakumbukwa milele

lAlipokuwa mdogo alitekwa nyara na kuuzwa utumwani

lAliwaangamiza nyoka wote waliokuwepo Ireland

Mtakatifu Patrick ni msimamizi wa taifa la Ireland, na kila ifikapo Machi 17 huwa ni sikukuu yake ambayo huadhimishwa kitaifa na Wairish.

Kila mahala katika Ireland, na miongoni mwa Wairish katika pande zote wanazokuwepo duniani, jina la Mtakatifu Patrick kwao ni alama ya kuheshimiwa mno.

Mtakatifu huyu alizaliwa Dumbarton kule Scotland na baadaye wazazi wake na familia yao kwa ujumla ilihamia katika eneo moja lijulikanalo kama Solway Firth jirani kabisa na Ireland.

Usiku mmoja wakati Patrick akiwa na umri wa miaka 16, mashua kadhaa zilitia nanga katika pwani ya Solway, ghafla bila ya taarifa.

Kutoka katika mashua hizo walikuwepo askari ambao mara baada ya kuteremka waliteketeza makazi ya watu na kuanza kuwaua watu waliokuwepo hapo.

Baadhi ya watu walitoroka kukimbia mauaji hayo, lakini wengine walioshindwa walitekwa nyara akiwemo Patrick, ambao walitiwa mashuani na kupelekwa utumwani Ireland.

Katika safari yao ya kurejea baada ya vurumai hiyo, wateka nyara hao wa Kiairish walimuuza Patrick kwa Milchu aliyekuwa mkuu wa jamii moja yenye kupenda vita.

Milchu alimchukua kijana huyo na kumpa kazi ya kuwa mlinzi na mchungaji wa nguruwe wake katika makonde ya malisho.

Wakati mwingine alikuwa akipewa kazi ya kuchunga kondoo katika malisho ya majabali, hali ambayo mara nyingi ilimfanya Patrick kuwaza na kukumbuka kwao alikotoka.

Kwa miaka sita Patrick alikuwa katika maisha hayo magumu, lakini siku zote alimtii bwana wake na kumtumikia vile alivyotaka.

Usiku mmoja alipokuwa amelala kandoni mwa kilima, alisikia sauti ikimwambia, "Sala na maombi yako yamepokelewa, meli inakuja."

Alipoamka alifikiri kwamba muda si mrefu ataondoka katika utumwa, na mara moja alielekea ufukweni mwa bahari

Kwa karibu maili mia mbili, Patrick alitembea kwa miguu kishujaa na kupambana na yote yaliyomsibu njiani hadi alipofika pwani ya bahari jirani na ulipo sasa mji wa Sligo.

Alipofika hapo furaha yake kubwa ilikuwa ni kuiona meli moja kubwa iliyokuwa ikijiandaa kwa safari ya kuelekea Ufaransa.

Patrick alikwenda hadi kwa nahodha wa meli hiyo na kumwambia "Napendelea kwenda na wewe hadi Ufaransa."

"Unazo pesa au mzigo wowote unaoweza kulipia nauli?" aliulizwa na nahodha. "Hapana sina kitu. Nitafanya kazi yoyote katika meli yako kwa ajili ya malipo yako," alijibu Patrick.

"Kwa hilo huwezi kusafiri nasi. Ondoka hapa!" alisema kwa ukali nahodha wa meli hiyo.

Patrick alisogea pembeni kidogo, na baadaye akawafuata mabaharia wa meli hiyo waliokuwa wakijaribu kuwakamata na kuwapakia melini mbweha waliokuwepo hapo.

Mbwa wa mabaharia hao walikuwa wakiogopa mbweha na wengine walijaribu kutoroka, lakini Patrick aliweza kuwasimamisha na kuwaita kwa upole.

Mbwa hao walisimama na kurejea na kufuata kule alikowaelekeza kwa mkono wake. Jambo hilo liliwashangaza manahodha wa meli hiyo. "Njoo hapa," alimwita. "Nahodha anahitaji kuzungumza na wewe."

Patrick aliporejea, nahodha alimwambia., "Nimebadili mawazo yangu. Unaweza kusafiri nasi na utakuwa mwangalizi wa hawa mbwa tukiwa safarini."

Patrick alimshukuru na kukwea kwa furaha ndani ya meli. Safari yao iliwachukua siku tatu hadi kufika Ufaransa na walipowasili, Patrick alikwenda kuishi na mjomba wake aliyekuwa Askofu mashuhuri wakati huo. Na alipofika hapo naye akawa mtumishi wa mambo ya kidini.

Usiku mmoja, akiwa kijana wakati amelala, malaika alimtokea na kumpatia ujumbe wa barua. Patrick aliisoma barua hiyo iliyokuwa na maneno: "Sauti ya Wairish" na baadae kidogo akasikia sauti ya watoto ikimwita "Njoo na twende pamoja nasi tena."

Patrick alipoamka alitambua kwamba ni lazima siku moja arejee kwao Ireland na kuanzia hapo alitumia muda wake mwingi kujifunza mambo mengi yahusuyo dini ya Kikristo na utoaji mafundisho yake.

Mara moja ilipofika mwaka 432 Baada ya Kristo, Patrick alifanya safari ya kurejea Ireland, lakini wakati huu akiwa sio mtumwa tena, bali akiwa Askofu.

Yeye na rafiki zake walipowasili Ireland, mwanzoni hawakupokewa vizuri, na wakati mwingine walikuwa na kazi ngumu ya kuwapa watu mafundisho kuhusu dini ya Kristo, kwani ni wachache waliokuwa wakiwasikiliza.

Taratibu, Patrick na wenzie waliendelea kupata mafanikio na waliweza kusafiri mahala hadi mahala kueneza mafundisho ya dini. Katika moja ya hadithi zake, tunaambiwa kwamba akiwa safarini katika kueneza Neno la Mungu aliwahi kupiga ngoma iliyowaangusha nyoka wote kutoka mitini na vichakani na kuwachukua hadi kuwatosa baharini, na tangu wakati huo hadi leo hakuna hata nyoka waoonekanao huko Ireland.

 Tuchague:Kuwasaidia watoto wa mitaani au kupanua magereza

"Wanatia huruma mno; huwezi kuamini kuwa ni watoto wa Watanzania. Mambo wanayofanyiwa na vibaka na wahuni, kama wasingekuwa wanachuo ambao mara nyingi huwasaidia wanapokuwa wanazunguka kupumzisha akili kabla ya kuanza vipindi vyao vya usiku, hakika watoto hao wangekuwa na hali mbaya zaidi ya hii waliyonayo sasa" Bwana Augostino Joseph; mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Taasisi ya Teknolojia ya Dar Es Salaam anasema Na Joseph Sabinius

Jioni hiyo ninapita kuelekea katika taasisi hiyo na ninapofika yalipo makutano ya barabara ya Morogoro na ile ya Bibi Titi Mohamed, upepo mkali unaoashiria mvua kunyesha unavuma huku radi zikigonga na kutoa sauti za kutisha.Kama ilivyo kawaida ya watu wa mjini, wanavuka barabara kukimbilia yalipo maduka na majumba mbalimbali ili kujikinga na mvua hiyo bila hata kujali usalama wao wakati wanavuka barabara.

Mimi ninabaki nimeduwaa kwani ninashindwa na ninataka kujua watoto wale wanne ambao mkubwa wao anaonekana kuwa na miaka takribani mitano hivi. wanakimbia kwenda wapi na hali hiyo inanilazimisha kusimama huku mvua ya manyunyu ikianza kunidondokea .

Wanakwenda moja kwa moja na kuingia uvunguni mwa roli upande ule lilipo jengo lililokuwa linatumiwa na gazeti la Mwananchi. Ninapoangalia kwa makini zaidi ninaguna mara ninamuona mama mmoja akiwa na mtoto mdogo ambaye hatazidi mwaka na nusu na wengine wakijivuta na kubanana miguuni kwake, wote wanabanana ndani ya uvungu huo na waume zao na mara mvua inaponizidia zaidi ninakimbia

Ni majira ya saa 12:45 hivi jioni hiyo ninapotoka chuoni hapo. Nataka nindelee na safari zangu.Ninapovuka geti lile kutoka hapo chuoni nilipokuwa nimejikinga mvua, ninatupa tena jicho na kuwaona sasa watoto wale wakitetemeka na wengine wakiwa pamoja na mama zao wakikamua nguo zao zilizolowa kwa maji ya mvua iliyowakumba humo uvunguni mwa gari bila kimbilio lingine

Usiku huo ninautumia muda mwingi kutafakari mambo mengi na hata kujiuliza sababu zinazopelekea hali hiyo. Akilini mwangu ninaanza kuzichambua sababu na ndipo ninakuja kugundua kuwa hayo ni matokeo ya tofauti za kimaisha zilizopo ndani ya jamii. hali ambazo matokeo yake ndiyo hayo ni matokeo ya hali ambazo mimi mwenyewe ninashindwa kuzitamka wazi; lakini ninapoamua kutafuta maoni ya wakazi wa jiji,

Bi Wandigi Mtatiro (23) aliyeko safarini Musoma anasema "Kule Musoma wanawake wengi wanakimbilia kwenye miji mikubwa; wengine hata wanakwenda Kenya baada ya kuvurugana na waume zao kwa kuwa ndoa nyingi kule ni za kulazimishana . Si unaona Nyambura Rusiko alipoolewa na mzee Nyandika mtu mwenye miaka zaidi ya 67; wewe ulitegemea wataishi mpaka mwisho ? Si unaona alishakimbilia Migori Kenya ; wewe uadhani akizaa huko , watoto wataishia wapi kama sio hao wanaokuwa watoto wa mitaani waliotapakaa namna hii?"

Richard Wiliamu ambaye ni dereva wa daladala mkazi wa wilayani Temeke anasema "Wapo watu wengi wanaojipatia riziki zao kivulini na wengine juani.. Maisha ni maisha, lakini ya watoto wa mitaani yanatisha"

Bila shaka hakosei, kwani moja kati ya makundi ya watu ambayo hulazimika kujitafutia riziki katika mazingira magumu ni hili la watoto wa mitaani;ambalo ongezeko lake si kwamba limeyakumba majiji ya nchi za Afrika pekee bali pia Asia, Ulaya na Marekani . Hali hiyo imefanya vituo vingi vya kulelea watoto hao vianzishwe ili walau kuwasaidia watoto hao ambao baadhi yao ni yatima waliotokana na janga la UKIMWI"

Si kwamba hali ya kuwa na watoto wengi wa mitaani katika barabara za jijini hutia aibu tu, kwa ndugu wa watoto hao au Watanzania wote kwa ujumla, bali pia huchangia kwa kiwango kikubwa wimbi la ongezeko la vitendo viovu kama uvutaji bangi, wizi, ujambazi, ubakaji, na hata matumizi ya mihadarati.na kuwepo uwezekano mkubwa wa kuenea kwaugonjwa waUKIMWI.

Zipo sababu nyingi zinazochangia ongezeko la watoto wa mitaani, lakini UKIMWI na mifarakano katika ndoa ndizo sababu zinazoongoza, anasema mtaalamu mmoja wa Sayansi ya Jamii.

Vitendo vya ufuska na ukahaba vimesababisha wazazi wengi kupoteza maisha yao na hivyo kuwaacha yatima ambao baadhi yao wamefikia mahali pa kupoteza matumaini ya kuwepo katika uso wa dunia kwa siku zijazo.

Uasherati na wasichana wadogo au vijana wadogo kuvamia vitendo vya ngono kabla ya wakati wao wao nalo ni eneo jingine ambalo mchango wake katika ongezeko la watoto wa mitaani si haba.

Wapo watoto wengine ambao kutokana na uasherati walinusurika kufa wakiwa kwenye mifuko ya rambo, ,na baada ya kubahatika kuendelea na maisha bado wamekulia katika mazingira magumu na ya kutisha. Lakini wapo watoto wa mitaani ambao wamezaliwa mitaani na wazazi wa mitaani ambao ni omba omba. Hawa nao wanakabiliwa na tatizo lisilotofautiana sana na wale waso na wazazi huko mitaani waliko. Tofauti ni ndogo tu kwamba kundi moja linapata upendo wa wazazi wao, japo katika mazingira magumu sana. lakini adha za kubakwa na wahuni, kulawitiwa na kukosa masomo wanatoka sare.

Maria Juma mwenye umri wa miaka 11 ni mmoja wa watoto wa mitaani ambaye nilikutana naye. Huku akitabasamu na hali akiendelea kula karanga zilizokuwa kwenye kifuko kidogo cha nailoni ananieleza sababu ya yeye na mama yake mwenye watoto watatu ambao wote anao hapa jijini wakifanya kazi hii ya kuomba omba .

Huko kwao Dodoma katika kijiji chaBahi walishambuliwa na njaa na baba yake akawa anampiga mama yake ili eti akatafute chakula. "Mama akienda kuomba msaada katika vijiji vingine na kukosa chochote akirudi baba anampiga eti alikuwa amekwenda kutembea.Ndipo pamoja na njaa ambayo tulikuwa nayo , mama akasema tuje huku ambako wengine wa pale kijini wapo."anasema Maria akimlaumu baba yake Mzee Ndoli wa kijiji cha Bahi.

Baada ya mazungumzo kadhaa huku akieleza namna wanavyolala kwenye bustani za Tume ya Jiji na kusumbuliwa na wahuni ambao mara kwa mara huwanyemelea kwa nia ama ya kuwaibia au kuwabaka "Mvua ikinyesha tukienda kwenye maduka watu wanatufukuza na lile gari (ananionyesha gari moja bovu kwa kidole)usiku linakuwa limejaa. Hata hivyo wengine wamelikatalia eti ni lao," anasema mtoto Maria .

Alipoulizwa kama waliwahi kukamatwa na polisi, anasema tangu aje jijini yapata miezi miwili iliyopita huwa wanakaa chonjo japo wenzao mara kwa mara wamekuwa wanakamatwa.

Alipotakiwa kuzungumzia namna wanavyoweza kuendesha shughuli zao za kuombaomba, Maria alisema mapato yao yanategemea bahati ya siku hiyo na ushapu wa mtu "Ushapu wa mtu bwana hata ukitaka..."kabla hajakamilisha akakimbia,huku akicheka na wala asitake tena kuendelea kuzungunza huku akisema "Ninakujua ni mwandishi wa magazeti."

John Igoti; mfanyakazi katika kampuni moja ya kigeni inayofanya kazi za kupokea na kusafirisha mizigo nje ya nchi hapa jijini ambaye alikuwapo jirani amesimama huku kumbe anayasikiliza mazungumzo hayo anasema, "Kinachosikitisha hapa zaidi ni ukweli kwamba hata wazazi, waumini mbalimbali wa vikundi vya dini wamekuwa wakipita ndani ya magari na kuwatumbulia macho tu pasipo kutoa mbinu za kuwaokoa watoto hao kutoka katika janga hilo linalowasibu"

Jamii inapaswa kujua kuwa watoto wale ambao hushinda juani wakiombaomba, ndio madaktari, wabunge, walimu, waandishi wa habari,na viongozi wa misikiti na makanisa mbalimbali wa kesho; na ndio hao ambao maisha yao yako hatarini namna hiyo kutokana na kuwepo uwezekano wa kukumbwa na magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu,kuhara pamoja na ajali za barabarani, achilia mbali UKIMWI.

Hali hii ya kutapakaa kwa watoto wa mitaani ;imesababisha baadhi ya watoto kuapa kutokuwa tayari kurudi majumbani kwao kutokana na kuzoea na hata kuridhika na maisha ya kuombaomba na kuokota mabaki ya chakula kwenye majalala licha ya karaha wazipatazo..

Watoto hao wamekosa huduma muhimu za kijamii kama vile kukosa elimu, malazi, chakula na huduma za afya na lishe. Ukosefu wa huduma hizo muhimu umekuwa ni kichocheo cha watoto hao kutorokea mijini ili kwenda kubahatisha maisha katika sehemu nyingine.

Kibaya zaidi ni pale nijuapo kuwa serikali ambayo ndiyo yenye jukumu la jumla la kuona kuwa maisha ya watu wake yanaboreshwa siku hata siku, ndiyo hiyo mara kwa mara inatumia maelfu ya maelfu ya pesa kuzidi kuwataabisha watoto hao na wazazi wao.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Luteni Yusufu Makamba aliiagizaTume ya Jiji kuwaondoa ombaomba wote jijini na kuwarudisha vijijini kwao.Hali hiyo ndiyo inayosababisha hata siku hizi mara kwa mara utawaona askari polisi wamewaweka chini ya ulinzi ombaomba katika maeneo mengi ya jijini kama vile Mnazi Mmoja, maeneo ya Faya, Stesheni na kwingineko. Makamba aliongeza kusema kuwa yeyote atakayebainika kuwapa fedha au msaada; atafikishwa katika vyombo vya dola kwa madai kwamba anayetaka kuwasaidia,atoe msaada huo kupitia vikundi mbalimbali kama vya dini au Ustawi wa Jamii.

Mkuu huyo wa mkoa alisahauri kuwa mashirika mengi, makampuni, na hata viwanda vingi zaidi hapa nchini vimejifia vyenyewe si kwa kuwa vinakabiliwa na ukosefu wa fedha wa asili, bali ule unaosababishwa na ufujaji na ubadhilifu.

Isitoshe mara kadhaa imekuwa ikisikika kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwa kiasi fulani cha misaada iliyotolewa kwa ajili ya watu waliokumbwa na maafa, imeishia mikononi mwa watu wengine ambao si walengwa.

Hivi mkuu huyo anaihakishia vipi jamii kwamba misaada hiyo itawafikia walengwa na kwamba historia haitajirudia? Hivi Serikali imeshindwa kuweka mkakati madhubuti wa kuwasaidia watoto wa mitaani na omba omba?

Ni utamaduni ambao Watanzania tumejijengea na kuridhika nayo kuwa wote tu kitu kimoja ndani ya nchi yetu moja ya Tanzania.

Kila Mtanzania anayo haki na uhuru wa kuishi mahali popote ndani ya nchi yake bila kuvunja sheria.

Hatuna ubaguzi wa rangi , dini wala kabila.

Hivi Makamba hakuona kuwa agizo lake linalenga kuwanyima haki na uhuru wa kuishi sehemu nyingine ndani ya nchi yao; na hivyo kuukaribisha ukabila ambao hatuna haja wala kiu nao?

Hivi ni mwanadamu gani mwenye upendo kwa watu wengine ambaye ndugu yake akikumbwa na janga na kukimbilia kwake; badala ya yeye kutoka na silaha nyingi ili amgawie nduguye; washirikane kwa pamoja kumtambua na kumuondoa adui huyo,yeye hutoka na "jeshi" lake na kumtimua ili aende kudhurika zaidi ?

"Taarifa ya Jeshi la Polisi nchini iliyotolewa Desemba 31, mwaka jana na kusainiwa na msemaji wa jeshi hilo Adeni Mwamunyange; kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Omari Mahita ilisema vitendo vya uhalifu nchini vimeongezeka sababu mojawapo ikiwa ongezeko la watoto wa mitaani.

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa makosa ya kujamiina yanazidi kuongezeka kwani toka mwaka juzi hadi mwaka jana yaliongezeka kati ya asilimia 15 na 35.

Taarifa hiyo ilionesha kuwa mwaka jana kulikuwa na matukio 1542 ya kubaka ukilinganisha na mwaka juzi ambapo kulikuwa na matukio 1181na hivyo kulifanya ongezeko la vitendo hivyo kuwa sawa na asilimia 30.48.

Zinaonesha kuwa matukio ya kunajisi watoto yalikuwa 602 mwaka jana ikilinganishwa na matukio 445 ya mwaka juzi ambayo yanafanya ongezeko la matukio 157 sawa na asilimia 35.28kati ya mwaka juzi na mwaka jana.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa matukio ya kulawiti yalikuwa 309 mwaka jana na hali mwaka juzi yalikuwa 267 na hivyo kufanya ongezeko la matukio 42 sawa na asilimia 15.73.

Badala ya kupoteza pesa hizo bure na kuzidisha taabu na mateso kwa Watanzania hao na wanadamu wenzetu wanaohitaji msaada na upendo wa jamii,wafunguliwe kambi ambazo pamoja na mambo mengine, zitawapa watoto hao mafunzo mbalimbali yakiwemo ya elimu ya msingi,ufundi wa fani mbalimbali pamoja na kilimo na ufugaji bora wa kisasa.

Hali hiyo itawajengea siku njema za usoni na hivyo kuboresha maisha yao na kuwa manufaa kwa taifa.

Bila kuwa makini na kulipa uzito jukumu la kuwasaidia watoto wa mitaani ni la jamii nzima; watoto hao watazidi kuongezeka toka kizazi kimoja hadi kingine hali ambayo itapelekea taifa kulazimika kupata gharama za kuongeza idadi na ukubwa wa magereza badala ya kuboresha elimu,huduma za afya pamoja na mawasiliano.

Hebu tutumie moyo wa wajibu,haki na pia tutumie imani za dini zetu kuwahurumia na kuwasaidia watu hawa. Kama Mcha Mungu wa dini yoyote; unayo furaha gani kumuona mwenzio anaishi maisha ya taabu namna hiyo, nawe ukifurahia?Makanisa na misikiti ya kesho itaongozwa na nani?