Make your own free website on Tripod.com

Aliyefiwa na mke wake Hospitalini Tarime asema:

Wangemtibu kwanza, mke wangu Hangekufa kama mbwa; angekufa kama mtu

"Japo niliweka rehani redio yangu na ile kamera kwa manesi ili atibiwe, tuliporudi tena usiku walikataa kumpokea; akafia pale mlangoni kwenye kitanda tlichombebea pembeni ya mlango na laiti wangemtibu kwanza, hangekufa kama mbwa; angekufa kama wengine."

"Ningefanya nini hali kati ya jumla ya sh. 26,000/= zilizohitajika tangu asubuhi ile ya saa nne asubuhi hadi saa tano usiku(saa ya mauti yake) nilipata sh. 3000/= tu? Ni kweli kama tungekuwa na hela, marehemu asingekufa katika hali ya kupuuzwa namna ile maana walivyogundua hatuna chochote hakuna aliyekuwa na muda na sisi."

Boniface Kemore (24) mkazi wa mtaa wa Starehe eneo la Sabasaba mjini Tarime anaeleza hali aliyomkumbana mkewe Mariamu Nyangarya aliyekuwa mjamzito alipofikishwa katika Hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Tarime akisumbuliwa na tatizo la mimba na hatimaye kufariki na kisha mwili wa marehemu kuondolewa hospitalini hapo usiku huohuo bila kufanyiwa upasuaji kuondoa mimba hali inayoisema nikupuuzwa kutokana na ukosefu wa pesa uliomkumba tangu alipomfikisha hospitalini hapo kama alivyomsimulia mwandishi wetu Josephs Sabinus aliyekuwa mjini Tarime hivi karibuni.

"Nilizidi kuzunguka zunguka huku na huko nikitafuta mtu wa kunisaidia ili nimhangaikie mgonjwa

Nilikuwa na wasiwasi Matinde (Mariamu) akifa akiwa mikononi mwangu; nitafanya nini kwa kuwa ninakae nae kama mke wangu kimada hii ikiwa ni mimba yangu ya pili. Ile ya kwanza alijifungua vyema japo baadae mtoto alifariki dunia na hata hatujaoana kihalali; Nimekaa naetu , sikuwa nimemlipia chochote.Wakurya ; Wakira wa Sirari, ninvyoajua nitawaambia nini ?

Nilipoona amekata roho nilichanganyikiwa maana kile nilichoomba kisinitokee, tayari kimefika chenyewe Nitafanya nini na ndugu zake nitawaambia nini wanielewe!!

Bw. Kemore akaanza mwanzo: "Jumamosi tarehe 31 mwezi wa saba niliondoka nyumbani saa12:00 asubuhi kuelekea kibaruani nikamuacha akiwa mzima kabisa. Ilipofika saa 2:00 asubuhi, mtoto wa dada yangu; aitwaye Godfrey pale kibaruani aakaniambia eti mjomba nenda nyumbani Matinde amesema uende kumpeleka hospitali sijui anataka kuzaa. Nikashituka; nikasema mmh mimba ya miezi saba na nusu anataka kuzaa?

Lakini nikaona sio vizuri kupuuza na kuchelewa kuitikia wito ni kutafuta mengine makubwa.Nikasema ngoja nikaone kuna tatizo gani pengine kuna mgeni muhimu. nikaondoka.

Hata sijafika nikakutana nae akichechemea huku ameinama; ameilalia mikono yake huku anatembea akivuta miguu.

Tukatembea kwa miguu kwenda Bomani (Hospitali ya Serikali ya Wilaya) Ningefanyaje na huku sina hela yoyote walau ya kukodi hivi vigari! na kadri muda ulivyopita, ndivyo alivyozidi kutoa kilio cha maumivu ya tumbo

Mapokezi nikalipa shilingi 500/= ili niandikiwe cheti baada ya kulipa ili mke wangu atibiwe, akapelekwa wadi ya wazazi na kisha kupimwa. Tukaambiwa Mariamu amepasua chupa ya uzazi na hata hivyo licha ya damu ile iliyozidi kumvuja, kile kiumbe kilichokuwa tumboni kilikuwa kimekufa na inabidi apasuliwe kle kiumbe kisiende na mama yake.

Manesi wakasema zinatakiwa sh.11,000/=kwa ajili ya upimaji na utoaji wa damu toka kwa watu wawili. Sasa nikashangaa, maana damu yote tumetoa wenyewe; mimi na yule ndugu yangu Moris Sasa nikaona watu tunauguliwa tena nikae kuuliza uliza gharama mwishowe watuachie kumtibu wenyewe, hawa watu wa mahospitali sio wa kuchokoza wanaweza kukufanyia wanavyotaka; nilichokitaka ni uzima wa mke wangu; vitu vinapatikana na kupotea. Nikashindwa nifanyeje maana mimi hapa mjini ni mgeni; Mnyamongo toka kijiji cha Nyangoto; ni nani angenisaidia hata kwa mkopo na hali ya siku hizi ilivyo ngumu? Mfukoni nilikuwa na sh. 3,000/= tu na hospitali wanataka sh. 11,000/= Nikashindwa sasa nitoe wapi hizo 8000/= zinazopungua ili zitimie 11,000/= wanazotaka ili Mariamu aongezwe damu

Nilikimbia hadi nyumbani pale mjini nikaichukua ile redio yangi nikaja nikawaomba manesi wanisaidie kwa kiasi hela niliyokuwa nayo wakakataa kabisa eti wanachokitaka ni pesa.nikawabembeleza wazipokee hizo elfu tatu;wamsaidie Mariam ili wakati anatibiwa, niweke redio kaseti yangu rehani ili nikatafute hela inayopungua nije kuikomboa .

Nesi mmoja aliyekuwepo maabara anaitwa Sara akazipokea na redio hiyo kwa dhamana ya sh 8000/= akawekewa chupa mbili za damu tangu saa 8 mchana japo sikuona cheti chochote cha malipo hayo nilinyamaza manesi na wahudumu wengi walikuwa wananifokea ovyo

Wakati wa upasuaji, nikaombwa tena sh. 12,000/= Nilipowaambia sina hizo hela wakaniandikia karatasi eti nikanunue vifaa mahali ninapojua (anaonyesha karatasi ile ilikuwa na orodha ya vitu).

Sikuwa na hela wala tumaini la kuzipata nikamfuata rafiki yangu Januari Burule aliyeniazima kamera aina ya Yashica ili nayo niiweke rehani ili Mariam afanyiwe upasuaji huo.hata hivyo hilo halikuingia masikioni mwao ;wote wakakataa wakasema wanachotaka ni hela; mambo ya kamera hawayajui.

Nesi mmoja akatamka wazi "nini kamera ya nini?; sasa kamera tufanyie nini shauri zenu kama hamna hela"

"Kama hamna pesa msaada tunaoweza kuwapa ni gari na barua mwende mkajaribu kwa .Winani"(hospitali ya kibinafsi) Dr.Kululetala akatuandikia barua kwenda kwa Winani saa mbili na nusu usiku.(gazeti hili lilipata nakala ya barua hiyo) tukapanda kwenye lile gari la hospitali walilotupatia .

Tulipofika kwa Winani tukawa kama kituko. wakasema eti wao watatufanyaje kama tumekoswa msaad serikalini . Wakasema: Mrudisheni Bomani akashughulikiwe .Ndivyo tulivyoambiwa na mke wa Winani mwenyewe

"Motaka atana nkolo "(maneno ya Kikurya yenye maana maskini hana hasira) nikambembeleza mke wa Winani akakubali kupokea kamera rehani na kutupatia vifaa vya upasuaji baada ya kukataa kumpasua kwa kuwa tulikoswa sh.15,000/= nadhani aliogopa uhamisho ule.

Tulijua tumepata vifaa, hivyo basi atatibiwa Dereva aliyetupeleka usiku huo alipotaka kuondoka mama yule alimkimbilia na kusema "Aa-aa mchukueni mgonjwa wenu mwende nae;sasa mnapomwacha atatoa wapi usafiri mwingine usiku huu!"

Tukarudi tena usiku huo hadi Bomani .Kilichonitia uchungu mno usiku huo ni kuwa marehemu Mariamu hakupokelewa badala yake aliwekwa mlangoni mpaka hali yake ilipokuwa mbaya zaidi na hatimaye kukata roho.

Sijui tulikuwa tumewachosha maana hakuna aliyekuwa na taimu na sisi. Marehemu Mariamu ambaye aliutamani uzima wa mbinguni na hata kuomba aitiwe padri ili ambatize siku hiyo majira ya jioni alikuwa akisomea mafundisho ya sakramenti ya ubatizo katika Parokia ya Tarime Mungu alisikia maombi yake na kupata sakramenti hiyo siku hiyo.

Alifia sakafuni mlangoni huku wakinamama wajawazito na wagonjwa wa wadi ile wakimtazama. Mariamu alikufa huku akilia na kuomba msaada akisema;

Manesi njooni mnisaidie jamani; nisaidie ndugu zangu mie ni mwanamke mwenzenu hata kama maishani kwangu sitawasaidia basi mtasaidiwa na wengine Jamani mwanamke mwenzenu naumia; naumia jamani mimba inaniua jamani. Basi naombeni hata uji; njaa nayo inaniuma aaa-aaa jamani. Basi kama mmeshindwa kabisa kunisaidia kwa herini; tutaonana mbinguni Akakata roho.

Usiku huo tukaambiwa tuuchukue mwili wa marehemu na kuondoka. Ilikuwa inaelekea saa 6.00 usiku. Licha ya juhudi zetu kujaribu kumsubiri mganga yule tuliyekwenda kumuita nyumbani peke yetu, hakutokea wala kuonekana.

Usiku huo tukashirikiana na ndugu wengine wapatao watano tuliokuwa nao katika mahangaiko hayo. Tukambeba marehemu wetu akiwa na kiumbe chake tumboni bila hata kufanyiwa upasuaji kukitoa kiumbe hicho na hivyo kuwezesha mazishi kufanyika kwa mujibu wataratibu.

Kesho yake akashindia ndani ni kiumbe wake tumboni hadi huku tukijadiliana kila mtu akisema lake Jumapili hiyo hakuna tuliloambulia la msingi

Jumapili tukiwa na marehemu nyumbani na kila mmoja akiwa na mtindo wake wa kulia dada Anna akaniita na kusema, "Kemore mdogo wangu ! Unaona yaliyotupata; tufanye nini ili hicho kiumbe kitolewe kwa ajili ya taratibu za mazishi? Tumekoswa hela;Mariam amekufa; tufanye nini ndugu yangu ili tumzike kwa taratibu sahihi?!

Tukaombe serikali itusaidie la kufanya ili kukitoa kiumbe hiki tumboni mwa marehemu ili tuzike.

Jumatatu tukaamkia kwa OCD tukamwelezea;akapiga simu hospitali kisha akatuambia twende ofisini kwa Dokta Mkuu Bw. Kemore alizidi kusimulia kwa uchungu akafuta machozi kwa kutumia upande wa shati lake.

Tulipofika tukaambiwa Mganga Mkuu haonani na watu siku za Jumatatu. Tukawasihi wahudumu wake waturuhusu;wakakataa, hadi tulipowaambia kuwa tulikuwa kwa OCD na ndiye aliyetutuma kwake

(Bw.Kemore akanukuu mazungumzo kati yao na Mganga Mkuu wa wilaya)

Mganga Mkuu:Niwasaidie nini?

Wafiwa: Tulikuwa kwa OCD amesema amekupigia simu na akatuambia tuje tukuone utusaidie.

Mganga Mkuu:Mna tatizo gani?

Wafiwa: Juzi usiku tulifiwa na mjamzito na tukaambiwa tuondoke na marehemu usiku huo bila hata kupasuliwa, na sasa ombi letu ni msaada wa kumpasua ili kutoa kiumbe tumboni twende kuzika.

Mganga Mkuu: Hilo pekee ndilo lililowapeleka kwa OCD; Kwanini hamkuja hapa moja kwa moja?

Wafiwa: Kwa sababu marehemu alifia hapa na tuliambiwa tumchukue toka hapa hapa hospitalini hali ikijulikana kuwa ana kiumbe tumboni.

Mganga Mkuu:Wewe ndiye mume wa marehemu?

Bw. Kemore: Ndiyo ni mimi.

Mganga Mkuu:Kwanini hukutaka kuja kwa wakubwa zaidi ya wale waliowaruhusu kutoa maiti usiku huo?

Bw. Kemore:Hatukujua kuwa kuna wakubwa zaidi ya wale tulioonana nao.

Mganga Mkuu: Shida yenu hasa mnahitaji kusaidiwa nini?

Bw. Kemore: Kumpasua ili kutoa mtoto tumboni kwa ajili ya mazishi; si ameisha kufa hakuna ujanja na hata polisi hatukwenda ili kushitaki bali kupewa ufumbuzi wa suala hili.(Akaendelea kusimulia kisa hicho cha kusikitisha.)

Kilichotushangaza ni kuwa Dokta akamuita yule nesi na kumwamuru kuturudishia ile redio yetu na alipomtaka Dk. Kululetela, alete faili la marehemu eti likakosekana.

Gazeti hili lilipowasiliana na wifi wa marehemu Bi. Annastazia Ghati Kemore (33) alisema, "Serikalini ikae ikijua hali ilivyo hapa ni heri kutokuwa na hospitali kabisa; wanaotibiwa na kupona ni wenye fedha, walala hoi tunakufa kama kuku."

"Maana mpaka tulipokwenda polisi ndipo upasuaji ulifanyikia nyumbani kama saa 7:00 bila malipo yoyote hali mganga aliyefanya kazi hiyo alitoka Hospitali ya Wilaya; ndipo tukafanya mazishi katika makaburi ya Kikristo maeneo ya Ronsoti saa 9:00 alasiri baada ya masaa 36?"

Baba wa marehemu Mzee Nyangarya Motegha Mkazi wa Sirari alikataa madai ya kuwa Kemore alipe sh. laki sita kama mahari ya kumuoa marehemu baada ya kifo na badala yake alipe sh. 50,000/= alizotamka mwenyewe.

Sakata la wanawake kunyonyesha vyura sasa lahamia Zimbabwe

Mmoja ajitupa chini kutoka garini kukwepa asinyonyeshe

Bulawayo, Zimbabwe

KATIKA mazingira yanayoonyesha kuwa waafrika wanazidi kukubuhu katika sayansi na teknoloja ya jadi, kile kizaizai kilichousibu mji wa Mbabame, Swaziland cha wanawake kutekwa nyara na kulazimishwa kunyonyesha chura sasa kimehamia nchini Zimbwabwe kwa kasi ya umeme.

Wakazi wa miji mikubwa ya Zimbabwe ukiwemo Harare Bulawayo,Gweru,Victoria falls na Queque sasa kwa tahadhari kubwa hukwepa wasikumbwe na mikasa hiyo huku wanawake wakiwa ndio walengwa wakubwa.

Kamanda wa Polisi wa jiji la Harare Inspecta Jenerali Gilbert Mpofu amethibitisha kuwepo matukio hayo, kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya habari ya kimataifa wiki hii.

Huku kesi ya Meya Chidarikira wa mji mmoja wa kaskazini mwa Zimbabwe ya kukutwa na kichwa cha binadamu ndani ya gari lake ikiwa inatokota, polisi wa Zimbabwe wamethibitisha kuwa wanaume wanaoteka wanawake na kuwalazimisha kunyonyesha vyura wamelata hofu kubwa kwa wanawake nchini humo.

Bwana Mpofu amesema kuwa watu hao wanaolazimisha wanawake nchini Zimbabwe kunyonyesha vyura mithili ya wale walioripotiwa kuwepo nchi jirani ya Swaziland wanafanya hivyo kwa imani za kishirikina za kuletea biashara zao au kuwa wenye bahati katika maisha.

Waganga wa kienyeji walio wengi hususan wa sehemu za mashambani huko Zimbabwe ndio wanaodaiwa kuwapatia wateja wao wenye tamaa ya utajiri vyura ili wawanyonyeshe wanawake kwa nia ya kujipatia utajiri kirahisi.

Mwandishi mmoja wa BBC, Bw. Portbart Chibunga alikaririwa wiki iliyopita akisema kuwa kuwa katika tukio moja la kushangaza lililotokea hivi karibuni jijini Bulawayo, mfanyabiashara mmoja aliyevalia nadhifu kabisa alifika penye klabu moja ya usiku ya jijini Bulawayo

na kuegesha gari lake la kifahari aina ya "Mercedeces Benz penye maegesho ya klabu hiyo. Alijitoma humo ndani ambapo alifanikiwa kumshawishi mwanamke mmoja kuondoka naye kwenda kustarehe baada ya kumnunulia viywaji .

Hata hivyo "Benz"ikiwa njiani kuelekea nyumbani kwa mwanaume aliyemuopoa yule bibi, mwanamama yule alijikuta starehe ikimtumbukia nyongo pale mwanaume yule alipofungua "Brief case" kubwa aliyokuwa nayo ndani ya gari na pandikizi la chura likajitokeza huku likiwa limemkodelea macho mwanamama yule.

Mwanamke yule alipiga mayowe kisha akaruka na kujitupa nje ya gari lile ambapo alijeruhiwa na kuchubuka vibaya.

Wasamaria wema walimchukua na kumfikisha hospitalini ambapo pamoja na polisi wa Bulawayo kupewa taarifa na kulisaka hilo gari jiji zima hawakuweza kulipata.

Jimbo la Florida huko Marekani lilipata wapi jina lake

Kwenye ufukwe wa bahari ya Atlantic katika mji wa kitalii wa West Palm Beach idadi kubwa ya watu wamelala chini ya miamvuli yenye rangi nzuri wakifurahia likizo ya majira ya joto.

Wengine wanaogelea, wengine wanajipatia kinywaji baridi hali wengine pia wanacheza michezo inayochezwa ufukweni mwa bahari.

Ukiwa ni mji mdogo katika jimbo la kusini mwa Marekani la Florida, West Palm Beach ni mojawapo kati ya miji inayovutia idadi kubwa ya watalii kuitembelea kila mwaka.Idadi ya watalii wanaotembelea karibia inataka kulingana na ya wale wanaotembelea Mji mkubwa wa jirani yake Miami.

Likiwa ni jimbo mashuhuri kwa biashara ya utalii huko Marekani Florida pia ni jimbo linalositawi kwa kilimo hususani cha miwa mboga na matunda.Mji wake wa Tampani kituo kikubwa sana cha safari za ndege za kimataifa.Je nini asili ya jimbo hili? Ilanza anzaje?.

Kunako mwaka 1442 Mvumbuzi mmoja wa Kihispania aitwaye Ponce de Leon aliyekuwa akiishi huko saville kusini mwa nhi hiyo alisikia habari za simulizi kuhusu chemichemi ya ujana "fountain of youth"

Mfanyabiashara mmoja aliyekuwa amesafiri pande mbalimbali za Dunia alimsimulia De Leon kuhusu nchi moja nzuri sana nayoitwa "Bumini" kulikokuwa na chemichemi ya ujana ambao ingeliweza kumbadili mzee kurudia ujana wake iwapo angelijitumbukiza ndani yake na kuogelea.

Habari hizo zilimvuia sana pia malkia Isabella wa uhispania hata akatamani naye pia a yapate maji ya chemichemi ya ujana aoge apate kurejelea ujana wake. Lakini angeyapataje?

Hakukuwa na mwingine ambaye angeliweza kusafiri na kufikia yaliko maji hayo na kuyaleta isipokuwa mvumbuzi kijana "Ponce de Leon"

Baada ya maelewano na malkia wa Uhispania Ponce de Leon aliondoka Uhispania na majahazi makubwa matano yaliyojaza wasaidizi wake tayari kwa kuitafuta ilipo "chemichemi"ya ujana.

Safari yao iliwachukua miezi mingi sana baharini huku wakiwa hawafahamu n wapi wanaelekea hasa ukichukulia zama hizo sehemu zilizo nyingi za dunia zilikuwa bado hazijavumbuliwa.

Baada ya kusafiri kwa kipindi kirefu sana pasipo kuona nchi kavu, makundi ya wasaidizi walioandamana na Ponce de Leon walianza kunun’gunika.

Wapo waliopendekeza ni bora warejee Uhispania walikotokea pia wapo waliosema nchi kavu yoyote watakayoifikia kwa mara ya kwanza watie nanga hapo hapo na kumfanya De Leon kuwa mfalme wao.

Makundi kadhaa ya watu katika msafara wake nao pia walisema kuwa Ponce de Leon ni mtu anayestahili kuhukumiwa kwa kuwaleta katikati ya bahari wafe kabla ya muhula wao .

Asubuhi moja ya mwezi Agosti mwaka 1443 mbinja vigelegele na vifijo vilisikika ndani ya Merikebu zile tano zilizokuwa zimewachukua wafuasi wa Ponce De Leon walikuwa wameona ardhi ya nchi kavu. Sehemu waliyokuwa wamefikia ilikuwa ni ile ya ufukwe wa pwani yya mashariki mwa Marekani.

Waliweka kambi yao kwa muda lakini wakati wa kung’oa nanga kuendelea na safari ulipofika merikebu mbili watu wake waliasi na kuamua kusalia hapo. Hivyo "Ponce de Leon"akaendelea na safari yake pande za kusini mwa marekani akiwa na wafuasi wachache watiifu waliosalia ndani ya merikebu mbili tu.

Wakati wakisafiri kuambaa ambaa kwenye ufukwe wa pwani ya Amerika kuelekea pande za kusini walipishana na wahindi wekundu wakazi asilia wa marekani ambao Ponce De Leon alijaribu kuwauliza

"where is Bumini"?

"Ni wapi ilipo Bumini"?

Jamii ya wahindi wekundu ambao hawakuweza kuzungumza lugha ya kihispania wala Kiingereza waliishia kumuonesha kwa vidole tu kuwa azidi kusafiri kuelekea pande za kusini zaidi mwa Marekani.

Baada ya safari ya takribani miezi mitatu waliwasili kwenye nchi nzuri sana naiita nzuri kwa sababu ilikuwa imejaa maua mazuri ya kila namana kwa wastani uoto wa asili wa nchi hiyo ilikuwa ni maua.

Basi Ponce de Leon na wafuasi wake wakaamini kuwa wamefika Bumini nchi nzuri yenye chemichemi yenye uwezo wa kumbdili mzee kurejealea ujana wake.

Walishuka na kuanza kuvinari kwenye hiyo nchi iliyojaa maua na wasiione chemichemi ya ujana yenyewe Ponce de Leon akapaita pahala hapo"Florida"akimaanisha nchi nzuri sana iliyojaa maua ya kila namna ya kuvutia macho unapoyatazama.

Ponce de Leon na wafuasi wake wakafunga safari kurejea uhispania wakiwa na huzuni nyingi sana kwa sababu hawakuitimiza azma yao ya kuipata chemichemi ya ujana "Fountain of Youth"hawakujua watajitetea vipi mbele ya malkia wa Uhispania pindi wakirejea huko.

Lakini walikuwa wamefanya jambo moja muhimu katika historia ya Dunia Ponce de Leon alikuwa amelipatia jimbo hilo la kusini mwa Marekani jina lake la kudumu kwani hata leo jimbo hilo linadumu kuitwa florida hivyo ndivyo jina la Florida lilivyoanza.

 

Mtakatifu Ita; Bikira wa Ireland

lAlisali mpaka kichwa cha shemeji yake kilichokuwa kimekatwa kikarudi kupitia angani na kuungana tena na kiwiliwili chake.

lHakuwa anakula kwa siku tatu mpaka nne.

Na Josephs Sabinus

Miongoni mwa wanawake watakatifu wanaojulikana na hata kukumbukwa kutokana na imani zao thabiti zilizopelekea miujiza kutendeka huko Ireland ingawa maisha yake yalikumbwa na misukosuko mingi ni Mtakatifu Ita.

Mtakatifu huyo hujulikana pia kwa majina mengine kama vile Ida, Mida, pamoja na majina mengine mengi ambayo tofauti baina yake na hayo majina mengine yaliyotajwa ni baadhi ya herufi tu.

Huyu ni Mtakatifu ambaye amechukua umaarufu mkubwa badala ya Mtakatifu Brigid.

Katika maisha ya usichana ya Mtakatifu huyu, alijitokeza kijana wa familia maarufu aliyemchumbia huku akimsihi baba yake Ita ili amkubalie na hivyo amuoe binti wake.

Lakini kutokana na sala zake zilizoambatana na mafungo makali aliyoyafanya kwa siku tatu mfululizo na kwa msaada wa malaika, alifanikiwa kuishinda nia ya baba yake ya kutaka kukubaliana na ombi la kumuoza na hivyo baba yake mwenyewe akamkubalia na kumruhusu; aishi maisha ya ubikira. Akampa mwanya binti wake kuishi kadri anavyotaka. Hali hiyo ikamfanya sasa Mtakatifu Ita ahamie Hy Canaill; upande wa Magharibi wa Limeric ya sasa. Akiwa huko eneo la Killeedy, alikutana na wasichana wenzake. Wakashirikiana kwa pamoja na kuendesha shule ya watoto wadogo.

Mmoja wa watoto waliofundishwa na Ita, alikuwa ni Mtakatifu Brendan ambaye Askofu Mtakatifu Erc alimpa jukumu Mtakatifu Ita ili amfundishe.

Ita alifanya hivyo kwa muda wa miaka mitano na baadaye Brendan akawa Abate na Mmisionari maarufu sana.

Tunaambiwa kwamba mwanzoni Mtakatifu (Ita) alitembelea maeneo kadhaa kwa siku tatu hata nne; bila kula chochote. Malaika alipoona hali hiyo ikielekea kumzidia Ita; alimtokea na kumsemea maneno ya kumsihi; akimtaka ajilinde zaidi na afya yake kwa lishe ya mwili.

Mtakatifu huyo alipoonekana kusita, malaika alizidi kumsisitiza kwa ajili ya mapenzi na huruma aliokuwa nao akimsisitiza na kumwambia kuwa kwa siku za mbeleni, Mungu angempa mahitaji yake yote.

Tangu siku hiyo Mtakatifu Mida (Ita au Ida) alianza kuishi kwa kula chakula alichokuwa akipata bila kujua kimetoka wapi. Mwanzoni hata yeye hakuwa anajua chakula hicho kilitoka mbinguni mpaka siku moja alipoulizwa na msichana mmoja;"Ni kwa nini hata Mungu anakupenda namna hiyo? Unalishwa nae kimaajabu, unaponywa dhidi ya maradhi, unahubiri yaliyopita na hata licha ya hayo, malaika wanazungumza nawe kila siku; na kamwe huachi kuyafanya mawazo yangu yawe juu ya Mungu!".

Pia alitokea siku moja mvulana Brendan akamtafuta Mtakatifu Ita na kuanza kumuuliza maswali. Alitaka amueleze mambo matatu yamependezayo Mungu kwa kiwango kikubwa zaidi.

Mtakatifu Ita akamjibu, "Imani yaani uaminifu wa kweli na kuwa msafi wa moyo, maisha ya kawaida na roho ya kumcha Mungu. Na la tatu, ni ukarimu utokanao na upendo wa kweli. Hivi ndivyo vitu vitatu vinavyompendeza Mungu".

Alipotulia kidogo, Brendan alizidi kumuuliza. "Je ni vipi vitu vitatu vinavyomchukiza Mungu zaidi?" "Uso", Mtakatifu Ida akajibu haraka haraka na kuendelea, "Uso unaoleta picha mbaya kwa jamii ya watu; kwa matendo ya ukatili na yenye kuweka matumaini makubwa katika fedha na mambo ya dunia". Wote wakatulia kubaki kutazamana wakimuomba Mungu awaongoze katika mapito yao.

Ilikuwapo miujiza mingi iliyomhusu Mtakatifu Ita tena miujiza iliyokuwa ya kipekee.

Mfano mmojawapo wa miujiza iliyotendwa na Mtakatifu huyu ni ule unaosimuliwa kutokana na hadithi ile ya msanii aliyetunzwa na kuhudumiwa naye, na ambaye Ita alimpa dada yake ili awe mkewe.

Ita akamuahidi kuwa msanii huyo aliyekuwa mchongaji na mbunifu, angekuja kuwa baba wa mtu mashuhuri na tena kijana mtakatifu.

Yalipotokea mapigano dhidi ya wavamizi, kwa bahati mbaya msanii yule aliangukia mikononi mwa wavamizi hao.

Wavamizi wakamtesa na hatimaye wakamkata kichwa chake na kuondoka nacho. Katika juhudi za kumtafuta jamaa na watu wake wakaambulia kuokota kiwiliwili pekee kisicho na kichwa.

Kwa kuwa mtakatifu huyu alikwisha ahidi na hata sasa bado ahadi yake haikuwa imetimilika, alizidi kujawa na huzuni.

Akafanya maombezi makali yenye sala na imani thabiti akimlilia Mungu.

Matunda ya sala zake zenye unyenyekevu yalionekana dhahiri pale kichwa cha msanii yule kwa nguvu na mapenzi ya Mungu kilipopaa na kupeperuka angani, kikamrudia na kujiunga chenyewe katika kiwiliwili chake baada ya saa nzima ya maombezi, kisha wote kwa pamoja wakarudi kwenye monasteri yao.

Baada ya muda kadhaa, msanii huyu alimpata kijana aliyejulikana kama Mtakatifu Mochoemog.

Kijana huyo wa msanii ndiye baadaye alikuwa Mkuu wa Monasteri ya Liath Mor au Leagh katika Tipperary. Mtakatifu Ida alimpa jina hilo akimaanisha "Mdogo wangu Mrembo" na ndiye huyo pia aliyemtunza na kumlea. Wakati mwingine jina hilo liliitwa kwa Kilatini; Percherius.

Maneno yaliyotajwa katika historia hii fupi ya Ida aliyefariki mwaka 570 baada ya kufanya kazi za Mungu na majirani akikumbukwa kila ifikapo Januari 15, juu ya mambo yampendezayo na kumchukiza Mungu, yanatuonesha njia ya namna ya kuuona ufalme wa Mungu.

Imani thabiti aliyokuwa nayo aliposali na kumuomba Mungu kwa bidii, inatufundisha kusali tukiwa tumeikunjua na kutakasa mioyo yetu tukiamini kabisa kuwa Mungu wetu ni mwenye huruma na huyasikia maombi yetu.

 

Wavamizi wakamtesa na hatimaye wakamkata kichwa chake na kuondoka nacho

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

MORMONS: Kanisa linalodai kila muumini wake ni Mtakatifu

lKwao kuoa wake wengi ni Ruksa

lKiongozi wao alioa wake zaidi ya 50,linakua siku hadi siku hapa Tanzania

Na Iganito Obuombe.

DINI zilizo nyingi za kikristo zinapiga vita ndoa za wake wengi lakini hivyo sivyo ilivyo kwa Mormon "Church of latter days Saints" ambalo linadai kuwa waumini wake wote ni watakatifu wa siku za mwisho je ni kweli?

Mwaka 1820 Josephs Smiths aliyekaa Marekani ,mkoa wa New York alidai kuwa amepata maono. kwenye maono hayo Smith ambaye kulingana na kitabu cha "History of Mormonism"alipata kuoa wake zaidi ya 50 alidai kuwa aliwaona Mungu Baba na Yesu Kristo kama watu wanaofanana na walimwagiza aanzishe kanisa ambalo ndilo leo linaitwa Mormons .

Miaka 7 baadaye Smith alipata vibao vya dhahabu vyenye maandishi. Anadai kuwa malaika aitwaye Moroni alimwambia atafsiri vibao hivi kwa kiingereza . Baada ya Smith kumaliza kutafsiri kitabu hicho alikuta"kitabu cha Mormon"ambapo leo wafuai wa kanisa hilo wanadai kuwa kitabu hicho hakina makosa lakini Biblia ina makosa ndiyo maana kwao kitabu hicho ni muhimu kupita Biblia.

Mwanzoni Smith na wafuasi wake waliishi Kirtland huko Ohio Marekani. Lakini kufuatia jamii kutotaka kuwaona na kumchukua Smith mwenyewe walihamia kaskazini mwa jimbo la Missouri na baadaye Nauvoo.

Safari hii ya kuhamahama ilipelekea wanaume wengi kufa kwa baridi, jambo ambalo lililozusha zinaa miungoni mwa wafuasi wa Smith pale mwanaume mmoja ilipombidi aoe mwanamke zaidi ya mmoja kufuatia uhaba wa wanaume.

Kunako mwaka 1890 walituma wamisionari wao wa kwanza kwenda Uingereza na nchi za Skandinavia ambapo waliongolewa huko na kujiunga na dini ya Mormons waliletwa Marekani.

Katika jimbo la Utah waumini wa dini ya Mormons kati ya mwaka 1862 na 1882 walipigana vita na jeshi la Serikali ya Marekani baada ya kugoma kutii amri ya Serikali ya Congress katika jimbo hilo ilivyowataka kuacha desturi yao mbaya ya kuoa wake wengi.

Siku zote za uhai wake mwanzilishi wa dhehebu la Mormons Joseph Smiths alisimama kidete kutetea ndoa ya wake wengi huku yeye binafsi akionyesha mfano kwa kuoa hovyo wanawake zaidi ya 50 mpaka mauti ilipofurika katika gereza la Carthage ambako alinawa na wahuni ambao hawakufurahia sera zake Smith aliuawa Juni 27,1844.

Leo dini ya Mormon's inasambaa kwa kasi sana katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania .jijini Dar es Salaam peke yake tayari huko Kinondoni, Chang'ombe, na Ubungo.

Mormons wa hapa Tanzania wana mfungamano na "Mormons" wa Nairobi Kenya ambao hivi karibuni serikali ya nchi hiyo iliwatuhumu kuwa wanajihushisha na ibada za shetani. Dhehebu la Mormons hapa Tanzania ni tawi tu makao makuu kwa Afrika Mashariki yako Nairobi huku makao yao mkuu bara zima la Afrika yakiwa Johnesburg Afrika Kusini.

Katika kile kinachoonyesha kuwa waumini wa Mormons tukielekea karne ya Sayansi na Teknolojia bado wamo kwa kuoa wake wengi gazeti la Guardian London,; la April 4,1999 lilichapisha habari za Daniel Kingstone mmoja viongozi wa kanisa hilo huko Marekani mwenye wake wengi na aliyefikishwa mahakamani kwa kumbaka mpwa wake wa kike aitwaye Mary mwenye umri wa miaka 15 tu.

Mpaka Daniel alipofikishwa mahakamani jijini Salt Lake City, alikuwa tayari amemdhalilisha binti huyo vya kutosha na kumgeuza mkewe halali wa ndoa

Mapambano ya Mormons na Serikali ya Marekani katika jimbo la Utah wakipigania kuoa wake wengi kati ya 1862 na 1882 yalitungiwa kitabu kwa jinsi yalivyovuma kitabu hicho kilichapishwa kama "Utah war" ikimaaanisha "vita vya Utah"