St. Marian: Shule iliyonuia kuinua kiwango cha elimu Bagamoyo

Awali ilibezwa kuwa ni ya watumwa

MIKOA ya Pwani ni miongoni mwa maeneo ambayo yapo nyuma kielimu nchini na katika makala haya Waandishi DALPHINA RUBYEMA NA GETRUDE MADEMBWE wanabainisha mikakati ya Kanisa Katoliki ya kutokomeza dhana hiyo.

HUKU akionekana kuwa na shughuli nyingi, Mkuu wa shule ya sekondari ya bweni ya St. Marian iliyopo wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Bw. Saleh Mgaza, saa 6:30 anajivuta kutoka nje ya ofisi yake baada ya kengele kugongwa.

Amesimama mbele ya kundi la wanafunzi wasichana wapatao 135 wanaosoma shuleni hapo ambao kulingana na ratiba ya shule hiyo ni saa ya kujipatia mlo wa mchana.

Wanafunzi hao wanawasalimia walimu na wageni wengine waliopo mbele yao na baada ya muda kama askari waliopo mbele ya mkuu wao wanafungua na kufunga miguu kabla hawajageuka na kuondoka.

Huo ni utaratibu wa kila siku wa shule hiyo ambayo imefufuliwa upya mapema mwaka 1994 na paroko mpya wa kanisa la kwanza katika Afrika Mashariki la Mtakatifu Elizabeth lililopo kilometa moja kutoka mjini humo, Padri Valentano Bayo.

Padri Bayo anasema amelazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kuwa shule inakuwepo eneo hilo kutokana na ukweli kuwa kanisa lilikufa sambamba na elimu mjini humo mwaka.

Anasema utaratibu wa elimu na shughuli zingine zilikuwepo tangu miaka ya 1800 lakini muitikio wake kwa wakazi ndio jambo ambalo liliwatatiza hata wale ambao walikusudia kuwaelimisha wananchi.

"Unajua huku Uislamu ndio kilikuwa kitu cha mwanzo kuingia katika mji huu"anasema na kuongeza kuwa waanzilishi wa Kanisa Katoliki waliingia mjini humo mwaka 1868.

"Wamisionari wa Kifaransa waliotokea visiwa vya Re Union na kupitia Zanzibar ndio walioanzisha kanisa hapa na lengo lilikuwa kuinua pia kiwango cha elimu kwa wakazi" anasema.

Kutokana na vikwazo vilivyolipata kanisa, mwaka 1969 wamisionari hao walisambaa hadi Morogoro na huko walifanikiwa kuanzisha seminari kadhaa ambazo zilistawi vema kutokana na mwitikio wa wenyeji.

Anasema kuwa walipoingia wamisionari hao walianzisha shule ya seminari ya Mtakatifu Petro ambayo ni ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki lakini wenyeji hawakutaka kamwe kujiunga nayo.

Padri Bayo, anasema kuwa wenyeji waliwakebehi hata waliokuwa wanasoma shuleni hapo kuwa wanasoma shule ya watumwa.

Jambo hilo anasema lilichangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha lengo lililokusudiwa, hali ambayo ilipelekea shule hiyo kuhamishiwa mjini Morogoro.

Anasema Padri Bayo kuwa alianza kufufua upya elimu sambamba na kuliimarisha kanisa alipofika hapo mwanzoni mwa miaka ya tisini.

Shule ya awali (Chekechea) ilianzishwa mwaka 1992 na baadaye darasa la shule ya ufundi ambalo lilikuwa chini ya mwembe lilianzishwa wanafunzi wa kwanza wakiwa vijana waliokuwa wakizurura katika eneo hilo.

Ufundi uliokuwa unafundishwa hapo kwa kuanzia ni pamoja na useremala na ujenzi na alifanikiwa kwa kiasi fulani kuwakusanya vijana ambao aliwakuta wamejiingiza katika mambo yasiyofaa.

Anasema kuwa vijana hao kutokana na kukosa ushauri na njia sahihi ya mambo ya kufanya, baadhi yao walijikuta wakiwa wakabaji, watumiaji wa madawa ya kulevya na vitendo vingine vya ajabu ajabu.

"Hapa kulikuwa na msitu ambao ulitumiwa na vibaka kama maficho na sio siri wakati huo nilikuwa nikilala na bastola mchagoni" anasema Padri Bayo na kuongeza kuwa chumba cha kufulia nguo kiligeuzwa kuwa karakana.

Anafafanua kuwa wanafunzi hao walibadili hali ya eneo hilo kwa kiasi fulani ikiwa ni mwaka mmoja tangu afike katika parokia hiyo ambayo haikuwa na mtumishi yeyote kwa mwaka mzima.

Banda la mbwa lililokuwa katika eneo hilo la kanisa likatumika kuwa ofisi ya walimu na wazo la kuanzisha shule ya ufundi kwa wasichana likamuingia akilini.

Anasema padri huyo kuwa alijaribu kwa kutumia rasilimali chache zilizokuwepo na ilianzishwa lakini walishindwa kuiendesha na matokeo yake yalikuwa si mazuri.

Anasema wengi walikuwa hawamalizi shule kutokana na ujauzito na sababu zingine ambazo ndizo zinazokwamisha upatikanaji wa elimu kwa wenyeji wa mikoa ya Pwani.

"Matokeo yalikuwa mabaya sana kwani wasichana wengi walipata mimba na kuolewa hivyo kushindwa kuendelea na masomo" anafafanua.

Pamoja na yote hayo Padri Bayo hakukata tamaa.

Kipindi hicho pia wazo la kuwa na sekondari ya bweni kwa wasichana liligonga kichwani kwa padri huyo na alilitekeleza kwa vitendo mwaka mmoja baadaye.

Lengo la kuwa na shule ya bweni ni kuwasaidia wanafunzi wa kike kupata elimu ambayo itaweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye licha ya mazingira magumu ambayo wanaishi, ndivyo asemavyo padri Bayo.

Ukumbi wa mikutano wa kanisa uligeuzwa kuwa bweni ya wanafunzi hao na mafundi wakawa wale wahitimu wa shule ya ufundi iliyoanzishwa na kanisa hilo ambao hata sasa ndio wanaofanya kazi za ukarabati na ujenzi katika majengo ya kanisa hilo.

Mwaka 1993 shule hiyo ilianzishwa na mpaka sasa ina mkondo mmoja kwa kila darasa na jumla ya wanafunzi ni 120. Mbali ya masomo ya kawaida wanafunzi wa shule hii wanafundishwa pia matumizi ya kompyuta na ufundi wa kushona nguo.

Mkuu wa shule hiyo Bw. Mgaza, anasema kuwa kuna jumla ya vyerehani 145, kompyuta 28 na mashine 145 za kuchapa (Typewriters) kwa wastani wa chereheni moja na mashine moja ya chapa kwa kila mwanafunzi shuleni hapo wakati Kompyuta zinawatosheleza wanafunzi wa kidato cha tatu ambao mwakani wanaingia kidato cha nne na hilo ndilo litakuwa tunda la kwanza la shule hiyo.

Walimu ni 10 na kati yao saba ni wanawake na waliobakia ni wanaume na mbali ya hilo wahisani wa Kitengo cha Huduma ya Elimu kilichopo chini ya Kanisa Katoliki (CSSC) wamejitolea kujenga nyumba za walimu wa masomo ya sayansi.

Pengine unaweza kuwazia juu ya kuwepo ubaguzi wa kidini kwa vile shule hiyo inamilikiwa na kanisa, lakini mkuu wa Shule ambaye yeye mwenye ni Muislamu anasema mfumo wa kuwapata wanafunzi hauna ubaguzi wa itikadi za kidini, rangi wala kabila na kinachozingatiwa ni uwezo wa mwanafunzi kitaaluma.

Mwalimu Mgaza, anasema wazazi wanachotakiwa kufanya ni kuchukua fomu za kuomba kujiunga na shule ambazo hupatikana shuleni hapo na Kituo cha Msimbazi kilichopo Jijini.

Anasema kuwa wanafunzi wote hufanya usaili ambao huhusisha masomo mawili na kwa kawaida huwa ni karibu sawa na marudio ya mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi.

"Ni masomo ya hisabati, kiingereza na maarifa," anasema na kuongeza kuwa baada ya hapo majina hupangwa kulingana na alama walizopata.

Mkuu huyo anafafanua kuwa idadi ya wanafunzi huhesabiwa na mstari huchorwa chini ya idadi iliyokusudiwa na matokeo hayo hubandikwa katika ubao wa matangazo.

Anasema lengo la mfumo huo ni kuondoa malalamiko ya wazazi ambayo yanaweza kutokea na amesema mpango huo lengo lake ni kuinua kiwango cha elimu katika mji huo.

Anasema mji huo una shule tatu tu za sekondari ikiwa ni pamoja shule hiyo ni ya kanisa ambayo inatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa kielimu mkoani Pwani katika mchepuo wa Biashara.

 

Kutana na magwiji wa kuoa na kuzaa barani Afrika

Mmoja wao anao wake 36 na watoto wapatao 203,na alipata kuwa mchungaji wa kanisa

MILA ya kuoa wake wengi haijaanza leo. Historia inawataja mabingwa wa kuoa wake wengi kama akina Nabii Suleiman na wafalme wengi wa kale waliomudu kuoa idadi kubwa ya wanawake.Lakini hao walikuwa ni watu wa zama hizo. Je, vipi zama zetu hizi ni akina nani wanaowika kwa kuoa idadi kubwa ya wanawake na kuzaa watoto wengi? IGNATIO OBUOMBE JR, anafanya mapitio ya wachache kati ya wengi.

Mzee Ancentues Akuku Ogwela, ambaye anajulikana sana kwa jina la "Akuku Danger" siyo mgeni kwa watu nchini Kenya na nchi za nje kama Marekani na Uingereza ambako magazeti kadhaa yameandika habari zake.

Mzee Akuku "Danger"ambaye amepewa jina hilo "Hatari" kutokana na machachari yake katika kuoa na kuzaa katika maisha yake, ameoa wake wapatao 42. Sita kati yao wamefariki na sasa amebakia na 36 kwenye maboma yake katika jimbo dogo la Ndhiwa, mkoa wa Nyanza kusini nchini Kenya.

Akuku "Danger"ambaye alizaliwa mwaka 1918 huko Kanyamwa wilayani Homa Bay amezeeka lakini bado ana nguvu nyingi kumshinda hata kijana mwenye umri wa miaka 20, makala katika gazeti moja la Kenya ilieleza hivi karibuni .

Mzee huyo alisoma hadi kufikia darasa la nne, ambapo pamoja na kufanya vizuri kwenye mtihani wa CCE,(Common Entrance Examination) hakuendelea na masomo kufuatia kukosa karo. Baada ya hapo alijiunga na kozi ya ushonaji, hivyo akawa fundi cherehani na mchungaji wa kanisa moja lililoko eneo la Aora Chuodho (Mto wa matope) huko Ndhiwa.

Aliamuoa mke wa kwanza mwaka 1940, na toka hapo akawa kama amewekewa gia ya kuchochea kasi yake ya kuoa na kuzaa kwani miaka minne tu iliyofuata yaani mwaka 1944 tayari ameongeza wanawake 4 mfulilozo.

Kufikiaa mwaka 1950 alikuwa tayari ameoa wake 20. Kana kwamba hapo alikuwa akitania tu, kufikia mwaka 1960 Akuku Danger akawa na wake 40 na zaidi ya watoto 100.

Mwaka 1970 akaongeza wake wengine kiasi cha kuwapelekea kufikia 42.

Mke wa mwisho wa mzee huyo machachari mwenye historia ndefu aliolewa mnamo mwaka 1996 na mashabiki wa mzee Akuku wamempachika jina la "Mama Ngina" ambaye alikuwa ni mke wa rais wa kwanza wa Kenya hayati Mzee Jomo Kenyata. Mpaka sasa unaposoma makala hii Akuku Danger anao jumla ya watoto 203 wasichana wakiwa 108 na wavulana 95.

Ajabu ni kuwa baba yake "Akuku Danger" aitwaye mzee Ongwela, alikuwa na mke mmoja tu na watoto wanne huku Akuku Danger mwenyewe akiwa ndiye mtoto wake wa pekee wa kiume.

Tayari mipango iko mbioni kumtoa "Akuku Danger" kwenye kitabu cha kumbukumbu za dunia "Guiness" Book of Records.

Lakini kumbukumbu zinaonyesha kuwa mzee Akuku Danger siyo peke yake aliyevunja rekodi kwa kuzaa watoto kupindukia barani Afrika.

Hadi anafariki, mwanamuziki nyota wa Nigeria Fela Ranson Anikulapo Kuti"aliyekiri kupenda mno wanawake alikuwa na wake wapatao 25 na watoto 80.

Fela aliyekuwa tajiri kupindukia alikuwa amewageuza wacheza shoo ama wanenguaji wake wapatao 15 kuwa Wake zake. Kwa Fela starehe ilikuwa ni mwanamke wake wote hao wa Fela alikuwa akiishi nao kwenye makazi yake yaliyojengwa nje ya jiji la "Lagos"yakijutikana kwa jina la "Jamuhuri ya Kalikuta"

Jean Bedel Bokassa, aliyekuwa wakati mmoja mtawala wa Afrika ya Kati aliweka rekodi ya kuoa na kuzaa pale alipomudu kuoa wake 27 na kuzaa nao watoto 70. Alipopinduliwa na kukimbilia Ufaransa kutafuta hifadhi, aliyekuwa kiongozi wa Ufaransa wakati huo Francois Mitterand, alishindwa ni wapi angelimweka Mfalme Bokasa na familia yake kubwa kiasi hicho .

Ilimlazimu Rais wa Ufaransa ampe Bokassa kasri moja la kale la kifalme lililojengwa toka mwaka 1775 likiwa nje kabisa ya jiji la Paris. Hata hivyo kulingana na sheria za Ufaransa, Bokassa aliruhusiwa kuishi ndani ya kasri hilo la kifalme na wake 5 na watoto 25 tu.

Siku Bokassa alipotua na familia yake nzima uwanja wa ndege wa "Charles De Gaulle" jijini Paris kilikuwa ni kiroja cha mwaka na kichekesho.

Mwanamuziki Luambo Luanzo Makiadi aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Franco, yeye mpaka anafariki mwaka 1988 katika Hospitali ya "Nakamura" mjini Kinshasa aliacha wake 7 na watoto 17, huku mmoja tu ndiye akiwa na watoto wa kiume 16 wote wakiwa wasichana.

Funga kazi ni mfanyabiashara mashuhuri wa Nigeria Emmanuel Odumosu au "Yesu wa Nigeria" kama alivyojiita wakati wa uhai wake. Yeye aliyejenga makazi yake eneo la ‘Surulere"jijini Lagos na kuyaita "Yerusalemu mpya" Humo aliruhusu mtu awaye yoyote aingie na mkewe kuishi lakini kila aliyefanya hivyo alimpora mkewe na kuzaa watoto 100. Baadhi ya wanawake walioshindwa maisha walijipeleka "Yerusalemu Mpya" na kuzaa naye. Odumosu alidai yeye ndiye Yesu na Yesu hatakuja tena.

Aliyekuwa rais wa kwanza wa Kenya, mzee Jomo Kenyatta naye alijitahidi kuzaa watoto wanaovuka 15 lakini komesha na kufunga kazi ni Mzee Aluoch Osogo wa huko Sakwa Awendo Kenya, ambaye yeye amezaa watoto wengi wanaokaribia 300 kiasi cha Wizara ya Elimu kumpa kibali kuanzisha shule yake ya msingi ya kusomea watoto hao. Kiroja ni kuwa wakeze hawawezi kumudu kupika chai ya kuwatosha wototo hao asubuhi, hivyo mzee Osago amejitwisha mzigo yeye mwenyewe wa kuamka mapema Alfajiri na kuwapikia watoto wake chai kisha wanapanga foleni na yeye Mzee Osogo ndiye huwachotea chai kwa kikombe kikubwa na kuhakikisha kila mmoja ameshiba.

"Nataka nihakikise kila toto imesiba" Mzee Osogo alisema wakati mmoja alipohojiwa na jarida la "Weekly Review"la Kenya.

 

Majibu ya Kikatoliki kwa vikundi vya Kilokole (6)

ILI kuwaelimisha Wakristo Wakatoliki juu ya tofauti ndogondogo zilizopo kati ya Mafundisho ya Kanisa lao na yale ya Kilokole, tumeamua kukichapisha kijitabu hiki kiitwacho" Majibu ya Kikatoliki kwa Vikundi vya Kilokole" ambacho tunaamini kitaleta mwanga wa kutosha kwa wale watakaokisoma. Hii ni kwa sababu si wengi wawezao kukipata kijitabu hiki na kukisoma. Endelea na sehemu ya sita...

inatoka toleo lililopita

c) Mungu anatupenda na anatusamehe.

Mungu anatualika kwenye toba na anatusamehe:

"Hakutenda sawasawa na hatia zetu wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu....

Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao kwa maana yeye anatujua umbo letu, na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi"(Zab.103) Mungu anapenda unyofu wetu; anatuita; "Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi " (Am.5:40) Yesu alitufundhisha kwamba Mungu anasamehe kama baba aliye mwema. Yesu mwenyewe aliwasamehe kila mmoja aliyetubu: kwa mfano mtu aliyepooza, mwanamke mkosefu, mwanamke mzinifu, Zakayo mtoza ushuru, mwizi aliyetubu. Aliwakaribisha wadhambi na kula nao.

D) Yesu alilipatia kanisa lake kazi ya kusamehe dhambi.

Yesu aliwapa mitume uwezo wa "kufunga" na "kufungua" (Mt. 16:19; 18:18). Jioni ya siku ya ufufuko wake aliwatokea wanafunzi wake ghafla wakiwa katika chumba (ghorofani); alipowashushia Roho Mtakatifu wafuasi wake na kuwaambia: "pokeeni Roho mtakatifu wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa (Yoh.20:22)

Kanisa linaendeleza kazi hii ya kusamehe dhambi hasa katika sakramenti ya kitubio(Upatanisho),

e)Matendo ya msingi kwa kuadhimisha Sakramenti ya Upatanisho

I) Utafiti wa Dhambi

Hii ina maana ya kukumbuka dhambi amabazo mtu amezitenda, au kukiri dhambi alizozitenda. Baada ya kujitafiti hakuna haja ya kuchelewa katika hatua hii

i)Majuto.

Hii ina maana ya kukiri makosa (dhambi) mmoja aliyoyatenda na kupatwa na uchungu kwa kumkosea mungu. Toba juju ya (Kuhusu hasara au tatizo lililosababishwa na dhambi zetu) haitoshi kinachotubu hasa ni unyoofu wa "kumrudia" Mungu Majuto (au uchungu kwa sababu dhambi) ni jambo muhimu sana katika sakramenti hii. Hakika mara baada ya kufanya toba ya kweli tunakuwa tayari tumepatanishwa na Mungu. Upatanisho huu tunafurahia baada ya kupokea Sakramenti hii.

Hii ni hatua ya kumweleza mwunganishaji dhambi zetu. Wakati fulani Sakramenti hii kwa ujumla iliitwa; "Muungano" Lakini kumbe kuungana ni sehemu tu ya Sakramenti yenyewe na si sehemu iliyo ya muhimu sana kwa upande wa dhambi za mauti, hata hivyo toba ni ya lazima isipokuwa katika masuala magumu zaidi. Ni kawaida , kila anayetubu dhambi zake atapenda kumweleza mtu mwingine. Hii inaonyesha kwamba atapenda mumweleza mtu mwingine.

Hii inaonyesha kwamba mtu anachukia dhambi.

Zaidi ya hayo kama mwungamishiji anataka kumwondelea mtu dhambi katika jinala Mungu na la Kanisa, atahitaji kujua kuhusu dhambi na majuto yake.

IV)Toba

Hii ina maana ya kukusudia kuacha dhambi. Toba ina lengo la kusafisha masalia ya dhambi (maelekeo mabaya) ambayo yameachwa na dhambi ndani yetu na kurudisha hasara waliyotendwa watu wengine.

V) Maendeleo ya Dhambi

Hii ni alama ya kielelezo cha msamaha wa Mungu na wa Kanisa Mwungamishi anayataja maondoleo hayo kwa maneno na ishara . Mwungamishaji kwa kumwelekezea mikono juu ya kichwa cha yule anayeungama anamwondolea dhambi zote "kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu."

 

Uchumi unaojali(10)

MAKALA hii ni sehemu ya nane ya mfululizo wa makala ambazo tumekuwa tukizichapa kutoka katika kitabu cha 'Uchumi Unaojali' kilichoandikwa na Tume ya Haki na Amani ya Kanisa Katoliki nchini ambacho kinaelezea kwa kina matatizo ya uchumi yaliyopo hapa nchini, chanzo chake na nini kifanyike ili tuwe na uchumi utakaomnufaisha kila Mtanzania.

Hii inahitaji tabaka la wanataaluma wenye kuwajibika katika kuhudumia umma na ambao wanapewa tuzo wanazostaili kadiri ya utendaji wao. Watu wa kawaida nao waatakuwa tayari kutoa tuzo hizo ali mradi tu wataona kuna faida kwao katika kufanya hivyo.

Hapo ndipo tutakuwa tumeweka ushirikano wa kijumuiya ambamo maslahi ya wote na faida ya wote huainishwa na kuruhusu maslahi binafsi kutekelezwa kwa namana ambayo fikra za pamoja katika kutekeleza yaliyo mazuri kwa wengine ni sawa na mahitaji binafsi.

D) namna ya Kuifanya Dira itekelezeke.

Dira na mkakati unaopendekezwa ni kitu ambacho sisi kama jumuiya ya Wakristu, tunaweza kutekeleza kwa urahisi, kwani kama kanisa tayari tunayo miundo ya kijumuiya na daima tunajitahidi kuufanya mfumo wa jumuiya utekelezeke.

Tunaweza kusema kanisa lina nguvu katika jumuiya ndogondogo.

Hivyo kama tunaweza kuunganisha vizuri zaidi, ngazi hizo za chini na zile ngazi za juu, na kuweka uhusiano imara kati ya ngazi hizo, tunaweza kutoa mchango mkubwa kulingana na dira yetu ya uchumi unaojali, na kuzingatia mkakati wa ushirikiano wa kijumuiya.

Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya utaratibu unaoweza kufuatwa katika kutoa huduma kwa mfumo wa jumuiya. Kimsingi ina maana kuwa jumiya ya kikristu katika ngazi ya kijiji, parokia au jimbo, zinaweza kutumika kuwahamasisha watu kuwakusanya pamoja, na kuwauganisha katika mfumo ambao utafuatwa washughulikie kikamilifu matatizo yao. Ngazi hizi zinaweza kuanzisha na kushinikiza serikali za mitaa na taasisi nyingine za huduma za mahali zifanye kazi kwa nguvu na kwa ufanisi zaidi na kuzifanya ziwajibike kadri ya wajibu na malengo yake na vivyo hivyo kuhamsisha ngazi nyingine za serikali na utoaji huduma zinazofuata.

Ili kufafanua fikra zetu hapa tunatoa mifano michache kwa baadhi ya shughuli ambazo Kanisa limepata uzeoefu fulani kwa miaka mingi.

Huduama za Afya.

A) Zahanati za Kijumuiya:

Viwango na mahitaji muhumu mara zote hupangwa na wizara. Malipo ya mshahara, dawa na gharama nyingine pengine hulipwa na jumuiya ya mahali husika.

Tawala za mkoa zinaweza kusaidia baadhi ya mambo kwa kuhakikisha kuwa Bohari za Madawa za Mikoa zinajiendesha kwa kununua na kuuza dawa. Au, vinginevyo zinaweza kusimamia upangaji wa bei katika bohari binafsi za madawa.

Jumuiya huendesha zahanati hizi kwa kutumia Bodi maalaum za Zahanati ili kuhakikisha kuwa zahanati hiyo haitumiki kama chombo cha kisiasa.

B) Hospitali ya Kijumuiya:

Wizara inaweza kutoa kiasi fulani cha ruzuku katika ngazi ya mkoa ambayo fedha yake hukusanywa kutokana na kodi maalumu ya afya katika ngazi ya Mkoa.

Jumuhiya inayo hudumiwa na hospitali hiyo inaweza inaweza kuchunguza gharama zisizo za kawaida na hatimaye kuanzisha ukusanyaji wa fedha kwa kuweka mkakati maalumu utakaopangwa na mamlaka ya wilaya au kanisa.

Gharamaza kawaida za huduma za hospitali zitaweza kulipwa na watumiaji wenyewe.Viwango vya ubora na taratibu za usimamizi zinaweza kupangwa kitaifa.

C)Bima ya Jumuiya ya Kinga ya Afya:

Jumuiya ya hiari inaweza kuanzishwa ambapo kila mwezi watu hulipa mchango wa gharama za matibabu katika ngazi ya zahanati kwa ajili ya huduma za kawaida za kiafya. Ridhaa ya wananchi huonekana katika kuchanga, kuandikisha na kuweka akiba, ili kukimu gharama za msingi au za zahanati. Hii inaweza kufanywa na wanajumuiya ya wa parokia.

D) boharia za madawa za kijumuiya:

Mfumo huu unaweza kuendeshwa kwenye parokia, vyama vya ushirika na vyama vya hiari vinavyoendeshwa kwa misingi isiyotafuta faida kubwa.

Huduma ya Elimu:

a)Shule za Msingi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Jumuiya ya mahali.

Jumuiya ya wazazi itahusika na sera nzima ya uendeshaji wa shule.

Walimu wataajiriwa na kulipwa kutokana na mapato ya mfuko unaochangiwa kutokana na kodi maalum ya maendeleo ya elimu inayosimamiwa na tawala za wilaya.

Vitabu na vifaa vya kufundishia vinaweza kupatikana kwa bei nafuu kwa Serikali kutoa ruzuku.

Viwango vya ubora na kanuni zitaandaliwa na kuratibiwa kitaifa.

Mitihani huandaliwa na shule zenyewe kufuatana na kwa kuzingatia viwango na uthibiti wa mara kwa mara utakaokuwa ukifanywa na serikali.

B)Shule za Sekondari Kimkoa:

Mkoa hukusanya kodi zinazohitajika kwa uendeshaji wa shule gharama za kawaida zinaweza kulipwa kutokana na fungu hilo lililokusanywa kimkoa.

Kamati ya wazazi pamoja na watumishi wa elimu wa serikali katika eneo wanakuwa chombo cha usimamizi.

Serikali kuu inaweka viwango na inauza vifaa kwa bei nafuu.

Mitihani inaandaliwa kimkoa.

Vitega uchumi vya ziada vinagharamiwa kutokana na kodi maalum ya kimkoa kwa upande wa shule za serikali.

B)Shule za Sekondari Kimkoa.

Mkoa hukusanya kodi zinazohitajika kwa uendeshaji wa shule. Gharama za kwaida zinaweza kulipwa kutokana na fungu hilo lililokusanywa kimkoa.

Kamati ya wazazi pamoja na watumishi wa elimu wa serikali katika eneo wanakuwa chombo cha usimamizi.

Serikali kuu inaweka viwango na inauza vifaa kwa bei nafuu.

Mitihani inandaliwa kimkoa.

Vitega uchumi vya ziada vinagharamiwa kutokana na kodi maalumu ya kimkoa kwa ipande wa shule za serikali.

Shule binafsi za sekondari zinaweza kuwa za mifuo miwili kama ifuatavyo:-

1. Shule binafsi zinazoendeshwa kutokana na makusanyo ya ada;

2. Shule zinazopata ruzuku ya serikali na zenye utaratibu maalumu unaozifanya kuwa nusu-binafsi.

Maktaba za kijumuiya na kampeni za Elimu ya watu wazima:

zinasaidiwa na Serikali kupata vifaa vitakavyouzwa kwa bei nafuu, zikiongozwa na jumuiya za parokia za mahali.

Sekta ya Kilimo:

a) Huduma ya Ushauri kwa wakulima wilayani:

parokia zinaweza kuwa mahali ambapo mahitaji ya watu yanashughulikiwa na huduma hizi zikifanywa kwa mzunguko kutoka parokia hadi parokia.

B) Utaratibu maalum wa utoaji kwa riba nafuu:

Utaraibu unaweza kuanzishwa wa kutoa mikopo nafuu kwa wakulima vijana na kwa masharti ya muda mrefu yatolewayo na benki za mahali zinazosimamiwa na mkoa. Benki hizi zinaweza kutumia parokia kama vituo vya kukusanyia akiba na kutoa mzunguko wa mikopo.

C)Parokia zinaweza kuanzisha mifuko midogo ya kuweka na kukopa.

D)parokia inaweza kuwa na uhusiano wa karibuni na duka la ushirika la pembejeo za kilimo.

Sababu kubwa ya kutoa mifano hii ni kutaka kuonyesha kuwa utaraibu wa kijumuiya unawezekana. Kwamba tayari ipo miundo katika ngazi ya vyama vya kidini au vyama vya ushirika inayotekeleza utaratibu huu kwa vitendo.

Ili kutumia vizuri fursa hii tunahitaji kurekebisha muundo wetu wa tawala za wilaya na mikoa, kwa kuweka uhusiano mzuri katia ya uongozi wa kisiasa na wa kiserikali na kuviwezesha vyama hivi vya hiari kuviwezesha vyama hivi vya hiari kuviwezesha kuwa washiriki wanaosaidiana katika maendeleo ya mahali.

Majukumu ya kiwizara na tawala za mikoa lazima yawe na mtazamo wa kusaidia watendaji wakuu, yaani jumuiya za mahali. Utaratibu huu, kwa nchi kama Tanzania ambako asilimia isiyopungua 50 ya watu wake hawana uwezo binafsi wa kukimu mahitaji yao ya msingi,ungewawezesha na kuwapa uwezo kupitia mfumo wa kijumuiya,unaungwa mkono na utawala wa juu na kupewa huduma za kiwizara.

Mfumo wa soko huria unaorekebishwa kijamii unamaanisha kuwasaidia na kuwapa uwezo wale wasiojiweza kushiriki kikamilifu katika mfumo wa soko huria waweze kushiriki.

Mfuko wa soko huria unaorekebishwa katu si huru;ni mbinu za medani za msituni,ambapo wenye uwezo mkubwa wa kiuchumi wanatunga kanuni zote na wanajichomeka katika sehemu zote za mamlaka.Wale wasioweza kushiriki daima wanaachwa nyuma.

Hii si dira ambayo sisi Wakristo tumeirithi kutoka kwa Kiongozi wetu Yesu Kristu,aliyetufundisha kuwa binadamu wote ni watoto wa Baba mmoja,Mungu wa Upendo na Huruma.

Ni familia ile tu inayojali ndiyo inayoweza kujenga na kutumikia Mfumo wa Uchumi Unaojali.

BARAZA LA MAASKOFU TANZANIA

TUME YA HAKI NA AMANI

 

Mtakatifu Scholastika

Alijitengenezea kaburi lake mwenyewe.

Aliomba mvua ikamzuia Benedicto kutoka

Na Josephs Sabinus

Roho yake iliruka Mbinguni katika sura ya njiwa mweupe ambayo Mt. Benedicto aliiona siku ya tatu baada ya kurudi kwake Monte Kasino

. SCHOLASTIKA ni Mtakatifu aliyeheshimiwa mahali pengi kuliko wanawake wengine watakatifu wa karne yake. Jina hilo lenye maana ya mwanafunzi au mwanachuo au mfuasi hakulipata wakati wa ubatizo wake, bali kwa kuwa alikuwa mwanafunzi katika shule ya Utumishi wa Bwana ya Mtakatifu Benedicto kama alivyoita maisha ya kitawa.

Katika shule hii, Scholastika ambaye alikuwa dada pacha wa Mtakatifu Benedicto, alifaidiwa sana akaendelea vizuri hata akajaliwa kuwa mtakatifu kwa kufuata kanuni ya kaka yake na kwa kukaa chini ya uongozi wake.

Watoto hawa pekee kwa wazazi wao;baba yake aliyeitwa Anisio Eutropia na mama yao Abundasia waliokuwa wenye cheo kwa sababu ya fadhila zao za Kikristo walianzisha na kuongoza shirika la masista huko Plombario katika Italia, umbali wa maili tano toka Monte Kasino ilipojengwa Monasteri ya Benedicto Mtakatifu.

Wazazi hao hawakuwazuia hao watoto wao, bali walipanda mioyoni mwao roho ya kujitolea sadaka ambayo nao waliionyesha na hivyo kuwafanya wazidi kujitolea zaidi kwa Mungu.

Hakuna maandiko ya zamani wala magofu ya utawala yaliyobaki ili kushuhudia eneo halisi aliloishi kama ni nyumbani au la..Hata hivyo masista wote Wabenedikto wa siku hizo humtazama na kumheshimu Mt. Scholastika kama mama yao na mwanzilishi wa shirika lao kwa mapendo ya kimwana.

Katika kitabu cha "Mazungumzo"Mt. Gregori mkubwa anasimulia kuwa alianza kujitoa tangu utoto wake na katika kitabu cha "Benedicto na nyakati zake"Kardinali Ildefonso Schuster OSB anasema Scholastika alikuwa ameanza kujitolea kwa Bwana kupokea shela ya Ubikira Mtakatifu.Alimvuta kaka yake kwa mfano wake kuacha Roma na kutafuta upweke katika sehemu za Subiako. Kardinali huyu aliamini kuwa utawa wa Scholastika Mtakatifu ulikuwa wa namna ya makao ya wakaao pekee, namna yenye watawa wachache.

Labda ulikuwa chini ya Monte Kasino lilipo kanisa la zamani sana lilitolewa kwa heshima yake alipokuwa utawani. Scholastika aliendelea kwa mbio katika njia ya utakatifu na fadhila zote za Kikristo zilichanua rohoni pake; zikaipamba mithili ya bustani ya maua.

Ilikuwa ni desturi ya Mt. Scholstika kukutana na kaka yake; Mt Benedikto mara moja kila mwaka mahali fulani kati ya monasteri ya Monte Kasino na utawa wa Mt Scholastika.

Kila mmoja aliondoka kwake akisindikizwa na watawa wachache kituoni walishinda pamoja kwa sala na mazungumzo ya kiroho. Kama kaka na dada walizungumza juu ya maisha ya kitawa na furaha ya mbinguni na hata kujadili njia za kutokuwa na mashaka juu ya maisha ya kitawa. Katika mkutano wao wa mwisho waliisha kula mlo wa jioni na saa ya kuagana ikiwa imekaribia, Scholastika alitamani kuendeleza mazungumzo haya ya kimbingu na kakake. Labda alikwisha fahamishwa na Bwana kuwa maisha yake duniani yamekaribia kikomoni.

Alimuomba kaka yake (Mt.Benedikto)asirudi Monasterini mpaka asubuhi. Kwa kuwa Benedicto alikuwa ni Mmonaki Mtakatifu hakupenda kusikiliza shauri hilo kwani haikuwezekana kwake kukaa nje ya utawa usiku.

Scholastika alifunga mikono yake na kuiweka mezani akainamisha kichwa na kuficha uso mikononi akamlilia Mungu. Alipoinuka ghafla, radi zikamulika na ngurumo zilizoambatana na mvua kubwa zikatawala anga lile lililokuwa jeupe.

Benedicto akashindwa kurudi nyumbani na kukaa, wakakesha wakizungumzia Muujiza huu wa mvua ulidhihirishwa namna Scholastika alivyokuwa. Mt. Scholastika alifariki dunia Februari 10,547. Sikukuu yake huadhimishwa tarehe hiyo kila mwaka.

Roho yake iliruka mbinguni katika sura ya njiwa mweupe ambayo Mt.Benedicto aliiona siku ya tatu baada ya kurudi kwake Monte Kasino. Usiku aliposimama kwenye dirisha alimuona njiwa huyo na kumjua kuwa ni roho ya dada yake.

Alijua kuwa dada yake amefariki, akawapasha habari watawa wake kwa kuwa dada yake ameingia furaha ya milele. Akawaambia watawa wa dada yake na Wamonaki wake "Msilie; Yesu amemchukua ili awe msaada kwetu;atukinge na adui zetu"

Akawatuma wakachukue maiti ya dada yake ili ikazikwe katika kaburi lake alilolitengeneza kwa ajili yake mwenyewe.

ZIJUE IMANI ZA WENGINE

Waafrika waliamini kwamba Mungu aliwatoroka watu kwa sababu ya dhambi

Na Steve Moyo

Bila shaka wengi wetu tunafahamu kuwa katika makabila mengi ya Kiafrika, kulingana na mila ya asili, watu walizoea kutambika mizimu.

Walianza kufanya hivyo katika ile imani ya kuwakumbuka roho za mababa na mababu zao waliokufa katika ukoo wao, baada ya Mungu wao kuondoka karibu nao na kwenda mbali zaidi.

Simulizi za baadhi ya makabila ya Waafrika katika imani ya kiroho zimesema kwamba zamani Mungu aliishi karibu sana na watu, lakini kwa sababu ya makosa fulani ya watu waliondoka kukaa mbali.

Makabila mengi ya Waafrika yaliamini kuwa Mungu anafanana na mtawala Mkuu, ambaye hawezi kukaribiwa na kila mtu na kila siku, na hivyo wakaanza kufanya matambiko.

Katika matambiko ya mizimu ambayo yalianza kukataliwa baada ya kuingia kwa kanisa la Kristo Barani Afrika, watu wanaofanya tambiko hizo waliwatolea vipawa mababa na mababu zao kama pombe na nyama.

Wakati mwingine katika tambiko hizo pia ngoma hupigwa na sala pamoja na maombi nayo hutolewa kwao.

Kulingana na imani hiyo huzaniwa kwamba wale wazee waliofariki huendelea kuwa na mahusiano na kizazi cha ukoo wao hata baada ya kufa kwao.

Inaaminika kwamba marehemu hao wana nguvu zaidi, na wanaweza kuwabariki watoto na wajukuu wao pamoja na watu wengine katika jamii yao au kuwadhuru na kuwaadhibu wakitenda mabaya, hasa wakiwasahau marehemu wao.

Hata hivyo, inaonekana kwamba imani ya Mungu ilikuwepo miongoni mwa makabila fulani ya Waafrika, hasa katika maeneo ya Afrika ya Magharibi ambako huko kuna jamii zilizoamini miungu wengi.

Katika jamii hizo labda Miungu hawa kwanza walikuwa wafalme tu na wale wazazi wa kwanza wa kabila, ambapo mmoja kati yao aliheshikiwa kama Mungu Mkuu.

Lakini makabila mengi katika Afrika ya Mashariki yenywewe yalikuwa yakimwamini Mungu mmoja.

Katika makabila ya eneo hili, Miungi wao walijulikana kwa majina mbalimbali kama vile Muumba, Chapanga, Mahoka na mengineyo.

Mahali pengine watu walikuwa hawataji jina la Mungu, lakini walikuwa na imani yake, ni kutokana na heshima na hofu ya kumwogopa, hivyo hawamtaji.

Katika imani hiyo ya kutambika mizimu ambayo bado inafuatwa na baadhi ya makabila, hudhihirisha imani kwamba roho za marehemu huenelea kuwa na uzima baada ya kufa. Aidha, wazee waliokufa huchukuliwa kama washenga ambapo walipoishi duniani waliwapa wana wa ukoo wao uzima ule unaotoka kwa Mungu, na sasa wakiwa marehemu shukrani na heshima ya wana lazima iwafikie, kwani sasa wanazidi kuwa karibu zaidi na Mungu.

Katika imani hii, hapo pia huonekana vilevile kuwa ushirka wa ukoo na kabila unaendelea kuwa na nguvu na maana hata baada ya kufa.

Kwa kawaida sadaka hazitolewi kwa Mungu, ila watu hutambika mizimu tu, na hizo roho za marehemu huchukuliwa kama washenga wao, ambao kwa njia yao watu wanatoa maombi yao.

Katika shida zao watu wanawaendea waganga (wala si Mungu), nao waganga pengine wanawaambia waende kutambika mizimu ambao waliwasahau mno.

Wakati mwingine katika shida kubwa sana ya njaa au maradhi makabila mengine yanamtolea Mungu mwenyewe sadaka fulani.