Mahakamani kwa ufupi

Na Dalphina Rubyema

Apewa kifungo cha nje

DAR ES SALAAM: MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu Mkamba Idd (20) kukaa kifungo cha nje muda wa mwaka mmoja kutokana mauaji aliyoyafanya mwaka 1993 ambapo alimuua bila kukusudia Hamis Magomba.

Mkamba ambaye ni mkazi wa Buguruni amepewa adhabu hiyo ndogo ambayo hailingani na kosa alilotenda kutokana na kutenda kosa hilo akiwa na umri ulio chini ya miaka 18 ambapo kipindi hicho alikuwa na miaka 15 na adhabu imepungua kwa vile alitenda kosa hilo bila kukusudia.

Awali kabla ya kutoa hukumu hiyo,hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ambaye ni hakimu mkuu mkazi wa Mahakama ya Kivukoni,Gabriel Rwakibalila alisema kuwa mshtakiwa alimuua marehemu siku ya mkesha wa krisimas ya mwaka 1993 ambapo ulitokea ugomvi baina ya mshtakiwa na marehemu.

Atuhumiwa kuchoma nyumba

DAR ES SALAAM:WAKAZI wawili wa Chanika Msumbiji Ahamade Mgwami (20) na Omary Adam (26) hivi karibuni walipandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Wilaya Ilala kujibu shitaka la kuchoma nyumba mali ya Mohamed Shirika.

Mbele ya hakimu Bakari Kisensi,Mwendesha Mashitaka wa Mahakama hiyo Inspekta wa Polisi Willy Mlulu alidai kuwa washitakiwa wote kwa pamoja walishirikiana kuchoma nyumba ya mlalalamikaji na vitu vyenye thamani ya shilingi 300,000 viliungua.

Washitakiwa walitenda kosa hilo Novemba 8 mwaka huu saa 12.00 asubuhi katika eneo la Chanika Zogowale.Wote kwa pamoja walikana shtaka hilo na walirudishwa rumande kwa kukosa wadhamini hadi Novemba 25 kesi yao itakapotajwa.

Atuhumiwa kumwibia mjomba wake

DAR ES SALAAM:MKAZI mmoja wa Mabibo Jeshini Fikiri Kombo,hivi karibuni alifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Manzese kujibu shitaka wizi wa ambapo alimwimbia mjomba wake aliyetajwa kwa jina la Kibwana Ramadhani pesa taslimu shilingi 35,000.

Mbele ya hakimu Kwege Mketo,Msoma Mashitaka wa mahakama hiyo Konstebo wa Polisi Leonard Izuya alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Novemba 9 mwaka huu saa 3.00 asubuhi katika eneo la Mabibo.Mshtakiwa alikana kuhusika na shtaka hilo.

Atuhumiwa kutoa matusi ya nguoni

DAR ES SALAAM: AZALI Punja (50) mkazi wa Mtaa wa Uhuru Kariakoo hivi karibuni alikana shitaka la kutoa lugha ya matusi dhidi ya mshitakiwa Nuliath Zuberi.

Katika hati ya mshtaka kama ilivyosomwa na msoma mashtaka wa mahakama hiyo Konstebo wa Polisi Obedi Matoi mbele ya hakimu Moga Staford ilidaiwa kuwa kwa makusudi mashtakiwa alimtukana matusi ya nguoni malalamikaji na alitenda kosa hilo Novemba 6 mwaka huu saa 11.00 jioni katika eneo la Kariakoo.Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.