Make your own free website on Tripod.com

Afikishwa kizimbani kwa kumtukana baba yake

Na Dalphina Rubyema

DAR ES SALAAM: SIKUDHANI Mohamed ambaye ni mkazi wa Magomeni Kagera Wilayani Kinondoni katika mkoa wa Dar-es-salaam hivi karibuni alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni kujibu shitaka la kumtolea lugha ya matusi baba yake.

Mbele ya hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Bibi Matrona Luanda,Msoma mashitaka wa Mahakama hiyo Konstebo Joyce Edson alidai kuwa mshtakiwa alimtukana matusi ya nguoni baba yake aliyetajwa kwa jina la Abdalah Tanda.

Mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 28 mwaka huu saa 4.30usiku na kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo Julai 29 mwaka huu ambapo kwa hivi sasa ushahidi kutoka kwa mlalamikaji umeanza kusikilizwa na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Novemba 23 mwaka huu.

Aachiwa huru baada ya mashahidi kushindwa kufika mahakamani

DAR ES SALAAM: KUTOFIKA Mahakamani kwa mashahidi,kumeifanya Mahakama ya wilaya Kinondoni imwachie huru Selemani Yasini (20) ambaye alikuwa ni mshtakiwa katika kesi ya kujaribu kubaka.

Kulingana na kifungu 225 cha sheria ya makosa ya jinai,Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo Muhidini Matitu alisema kuwa kwa vile mashahidi wameshindwa kufika mahakamani hapo kwa muda mrefu, mahakama kwa kauli moja haikuwa na sababu ya kuendelea kumweka mshitakiwa huyo mahabusu na badala yake ilimwachia huru.