KORTINI KWA UFUPI

Kizimbani kwa tishio la Kuua

Justino Madimundi (24) amepandishwa kazimbani katika Mahakama ya Mwanzo ya Kawe akikabiliwa na shitaka la kutishia kumuua mpenzi wake baada ya kumnyima unyumba.

Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa Polisi Konstebo Bakari Bakari mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Janeth Mnywwa kuwa mnamo Septemba 26, mwaka jana majira ya saa 5.00 usiku, mshitakiwa alitishia Kumuua mpenzi wake kwa kisu.

Akiielezea mahakama hiyo, mlalamikaji katika kesi hiyo Dina Chacha (31) alidai kuwa siku hiyo mshitakiwa alimlazimisha kufanya kitendo hicho vinginevyo; angemuua kwa kumchoma kisu.

"...Alinilazimisha nifanye naye mapenzi nikamkatalia na kumweleza kuwa nilikuwa naendelea kutumia dozi ya vidonge vya T.B na kwamba nilikua nimezuiliwa kufanya kitendo hicho hadi nitakapo maliza dozi hiyo." Alisema.

Hata hivyo aliongeza kuwa mshitakiwa alimlazimisha na kumtolea kisu ndipo alipopiga kelele kuomba msaada na mshitakiwa akaamua kukimbia.

Dina aliiambia mahakama kuwa aliisha achana na mshitakiwa na tangu Januari 1997,hakuwa na mahusiano naye kabisa ya kimapenzi. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 16 itakpotajwa tena.

Naye Josephs Sabinus; anaripoti kutoka Kisarawe kuwa watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kisarawe kwa tuhuma za wizi wa mifugo kwa kutumia nguvu.

Watu hao Mazengo Mdachi, Legunji Fumbi, Rogasiani Kusaduka na Mazengo Manyungu wanadaiwa kuiba ng’ombe 17 wenye thamani ya jumla ya shilingi milioni tatu mali ya bwana Nestory Tesha mkazi wa eneo la Vibura wilayani hapa.

Ilidaiwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kisarawe Hemedi Mnamby na Mwendesha Mashitaka wa Polisi Inspekta Salumu Kidinda kuwa mnamo Julai 19,mwaka juzi usiku, katika kijiji cha Vibura wilayani hapa ,washitakiwa kwa pamoja walitumia nguvu kuiba ng’ombe 17 mali ya mkazi huyo.

Washitakiwa wote wakalikana shitaka na wawili kati yao wako nje kwa

dhamana hadi Machi 15 mwaka kesi hiyo itakapotolewa hukumu.