Atuhumiwa kuua

DAR ES SALAAM:ALBERT Peter (260 ambaye ni Mkazi wa Keko Matangini katika wilaya ya Temeke Mkoani Dar-Es-Salaam hivi karibuni alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni kujibu shtaka la mauaji.

Akisoma hati ya mashitaka mbele hakimu wa mahakama hiyo Nisseta Wambura,Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo Inspekta Msaidizi wa Polisi Dunstan Sagoda alidai kuwa Januari 20 mwaka huu saa 1.00 kamili jioni katika eneo Keko Matangini,mshtakiwa alimuua Peter Tryphone.

Hata hivyo Inspekta hakutaja ni vipi mshitakiwa alimuua marehemu na mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote kuhusu shitaka hilo na alirudishwa rumande kwa kukosa wadhamini.

 

Akana kuiba gari

DAR ES SALAAM:MKAZI mmoja wa Mtoni kwa Azizi Ally,Alphonce John (22) amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni kujibu shitaka la kujaribu kuiba gari aina ya Toyota Corona lenye namba za Usajili TZM 7894 thamani yake ikiwa ni shilingi 4,000,000 mali ya Rashid Seleman.

Mbele ya hakimu Nisseta wambura,Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo Inspekta Msaidizi wa Polisi Dunstan Saguda alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 17 mwaka huu katika eneo la Mtoni kwa Kidande.Mshitakiwa alikana shtaka na alirudishwa rumande hadi febriari 9 mwaka huu kesi yake itakapotajwa tena.

 

Mshitakiwa akana kugushi

DAR ES SALAAM:VENANCE Shirima (54) ambaye ni mkazi wa Magomeni Ifunda alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni kujibu shitaka la kugushi kwa nia ya kujipatia nyumba kutoka kwa Notibu Ndugumbi ambaye ni kipofu.

Mbele ya hakimu Khamisa Karombola,Msoma mashitaka wa mahakama hiyo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Lenihadi Lisapita alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa aligushi barua inayoonyesha kukabidhiwa nyumba na kipofu huyo,nyumba iliyopo eneo la Magomeni Ifunda jijini.Mshitakiwa alikana shitaka na yupo nje kwa dhamana.

 

Akana kujipatia mali kiudanganyifu

DAR ES SALAAM:MIRAMBO Khamis (37) ambaye ni mkazi wa Kongowe Wilayani Temeke Mkoa wa Dar -Es-Saalam,hivi karibuni alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni kujibu shitaka la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu ambapo alichukuwa magunia 117 ya viazi mbatata thamani yake ikiwa ni sh.1,369,628 mali ya Mohamed Anoel (37).

Mbele ya hakimu Khamisa Karombola ,Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo,Mrakibu Mwandamiazi wa Polisi Leniahadi Lisapita alidai kuwa mshtakiwa alijipati mali hiyo Aprili 7 mwaka jana katika eneo la Ubungo Sokoni ambapo alikubaliana na Mohamedi ambaye ni mlalamikaji katika kesi hii kuwa angempa pesa hiyo baada ya mauzo.

Mshitakiwa alikana shtaka hilo na yupo nje kwa dhamana hadi Machi 3 mwaka huu kesi yake iatakapo nedelea kusikilizwa.

 

Ashtakiwa kwa kuwatukana mahakimu kuwa ni walanguzi

Na Neema Dawson

 

MKAZI mmoja wa Mtoni Mtongani jijini, Fatuma Mtupa (37) amepandishwa kizimbani katika mahakama ya mwanzo ya Temeke akikabiliwa na mashtaka mawili ya kuwatukana maaskari polisi na mahakimu wa mahakama hiyo .

Mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Bibi.Asia Dege, ambapo Mwendesha mashtaka , Lilian Irira, alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo mnamo Desemba 15 mwaka jana ambapo aliwaambia askari polisi na mahakimu kuwa ni "wasenge"na walanguzi.bila

Upande wa mashtaka uliendelea kudai kuwa mshtakiwa huyo baada ya kutoa matusi hayo, pia alifanya vurugu mahakamani hapo ,hali ambayo ilisabababisha kutokuwepo na amani pia kusimama kwa shughuli za mahakama .

Habari za kimahakama zimedai kuwa mshtakiwa huyo siku hiyo alifika mahakamani hapo akiwa na ndugu zake kwa lengo la kusikiliza kesi yao ya mirathi namba 262 iliyokuwa mbele ya hakimu,Modesti Matenyange na kwamba baada ya kumalizika kwa kesi hiyo,ndipo alipotoka nje na kuanza kutoa kashfa hiyo kwa wahusika wa vyombo vya dola.