MAHAKAMANI

 

Aomba kuachiwa huru kwa sababu anaharisha

Na Dalphina Rubyema

 DAR ES SALAAM:SELEMAN Bwera (25) ambaye ni mshitakiwa katika kesi ya kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu,hivi karibuni aliiambia Mahakama ya Mwanzo Magomeni kuwa mahakama hiyo imwachie huru kwa vile anaharisha .

Mshitakiwa huyo ambaye amekaa mahabusu kwa muda wa miezi mitano,alitoa maelezo hayo kama ombi mbele ya hakimu anayesikiliza kesi hiyo Bibi Asia Mpunga.

Akitoa maelezo zaidi,mshitakiwa alidai kuwa ni muda mrefu tangu apelekwe Segerea kama mahabusu na hivyo ameathirika afya yake ambapo aliongeza kuwa hapati chakula na kwa hivi sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa kuharisha lakini kutokana na kwamba tumboni hakuna kitu (chakula) kunamfanya aharishe utumbo.

"Hakimu nionee huruma mamangu,mimi afya yangu siyo nzuri,naharisha utumbo pia ngozi yangu imeharibika sana mama si unaiona,hatupati maji ya kuoga nadhani hata wewe unanisikia ninavyo toa harufu mbaya"alidai mshtakiwa huyo huku akimwaonyesha hakimu Punga makovu ya vipele yalioenea kwenye ngozi ya mwili wake.

Mshtakiwa aliendelea kumwomba hakimu kuwa kama kumwachia huru kutashindikana basi amuruhusu ajidhamini mwenyewe kwani huku mjini hana ndugu wa kumtolea dhamana.

Hata hivyo hakimu hakukubali kumwachia huru au kumpa nafasi ya kujidhamini mwenyewe kwa vile mlalamikaji wake anafika mahakamani kila mara kesi hiyo inapotajwa ambapo alimpa moyo mshtakiwa huyo kuwa atataja kesi yake kwa mara ya mwisho na baada ya hapo atamruhusu ajidhamini mwenyewe.

Awali ilidaiwa na Msoma mashtaka wa mahakama hiyo Konstebo wa Polisi Daniele Kisiri mbele ya hakimu Asia Mpunga kuwa Agosti 25 mwaka jana saa 3.00 asubuhi katika eneo la Tandale Sokoni Wilayani Kinondoni,mshtakiwa alijipatia gunia 6 za mahindi yenye thamani ya sh.108,000 kutoka kwa Jamila Ayubu

Atuhumiwa wizi wa maungoni

DAR ES SALAAM:MKAZI mmoja wa Magomeni Mzumbe ,Hamad Said (23) hivi karibuni alipandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Mwanzo Magomeni kujibu mashitaka matatu ya wizi wa kutoka maungoni ambapo walalamikaji ni watu watatu tofauti na tarehe aliyofanya makosa hayo inatofautiana.

Mbele ya hakimu Asia Mpunga,Msoma mashitaka wa mahakama hiyo Konstebo Anselemo Thobias

Aliadai kuwa shitaka la kwanza lianalomkabili mshitakiwa huyo ni kupora baiskeli aina ya phonex yenye thamani ya sh.40,000 mali ya Abdalah Muhando na litenda kosa hilo Januari 5 mwaka huu saa 6.00 mchana katika eneo la Magomeni.

Shitaka la pili linalo mkabili mshtakiwa huyo ni la uporaji wa sh.35,000 kutoka kwa Amad Ahtuman na mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 8 mwaka huu saa za mchana katika eneo la Magomeni Mtaa wa Idrisa na shtaka la tatu mshtakiwa alipora viatu,saa na pasi vitu vyote kwa pamoja vikiwa na thamanai ya sh.47,00 mali ya Omary Said ambapo mshtakiwa alifanya kosa hilo Januari 9 mwaka huu saa 5.usiku katika eneo la Magomeni Mikumi.

 Mganga wa jadi mbaroni

DAR ES SALAAM:DANIEL Moses (21) ambaye ni mganga wa jadi hivi karibuni alifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni kujibu shItaka la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kama ilivyodaiwa na msoma mashItaka Hassan Lubuva mbele ya hakimu Asia Mpunga.

Lubuva alidai kuwa Desemba 12 mwaka huu saa 5.00 usiku katika eneo la Kariakoo mshtakiwa kwa kujiita mganga alijipatia suruali moja, paspoti,fulana moja vitu vyote vikiwa na thamani ya sh.89,000 kutoka kwa Bwai Alli kwa madai kuwa mganga huyo angempa dawa mlalamikaji ya kuweza kusafiri nchini za nje.Mshtakiwa alikana shtaka na alirudishwa rumande kwa kukosa dhamana.

 Wakana shitaka la kujeruhi kwa bakora

DAR ES SALAAM:WAKAZI wawili wa Tandale Vilabuni hivi karibuni walipandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Mwanzo Magomeni kujibu shitaka la shambulia la kudhuru mwili ambapo walimpiga bakora Hassan Jongo ambaye ni mlalamikaji katika kesi hii.

Mbele ya hakimu Asia Mpunga,Msoma mashitaka wa mahakama hiyo Konstebo Hassan Lubuva aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Kishamba Minja(22) na Jafari Masawe (20) wote wakazi wa Tandale Vilabuni ambao kwa kushirikiana walimpiga makora mlalamikaji huyo na kumjeruhi karibu na jicho.Walikana shitaka na kurudishwa rumande.

 

Mshitakiwa adai polisi wamembadilishia shtaka

DAR ES SALAAM: SIAMIN Peter (19) mkazi wa Tandale katika wilaya ya Kinondoni mkoa wa Dar-Es-Salaam ambaye anakabiliwa na shitaka la wizi kutoka nguoni ,hivi karibuni aliiambia Mahakama ya Mwanzo Magomeni kuwa shitaka lake siyo hilo bali kituo kikubwa cha polisi Magomeni wamembadilishia shitaka lake.

"Mheshimiwa hakimu mimi shitaka linalonikabili na tofauti kabisa na hilo la wizi wa kutoka nguni naona kituo kikubwa cha polisi Magomeni wamelibadilisha shtaka langu"alisema mshtakiwa huyo bila kutaja shtaka halisi linalomkabili.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya hakimu Asia Mpunga,Msoma mashitaka wa mahakama hiyo Konstebo wa Polisi Anselemo Thobias alidai kuwa Januari 7 mwaka huu saa 11.jioni katika eneo la Tandale Magharibi Siamin Peter na mwenzake Ilali Peter (20) wawalipora pesa taslimu sh.135,000 na baiskeli aina ya phonex mali ya Bakari Omary.Washtakiwa wote kwa pamoja wapo nje kwa dhamana.