MAHAKAMA DAR YAAMBIWA

Naingiliwa kinyume cha maumbile kimazingara

Na Getruder Madembwe

MARIA Maru (26) ameitaka mahakama kumwagiza mpenzi wake wa zamani aache kumwingilia kimazingira kwa kuwa tayari ametengana naye.

Mwanamke huyo licha ya kumuomba hakimu msaada huo, alisikika akilia wakati akiondoka kuwa mwanamume huyo humwingilia kinyume na kimaumbile.

"Mwanamume huyu mbona kero, mtu tulikwisha tengana naye iweje basi ananifuatafuata usiku na hali mimi nimekataa" alikuwa akiongea huku analia wakati anatoka mahakamani.

Awali ya hapo Maria Maru ambaye alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kutoa lugha ya matusi kwa PT. Gibson akijitetea mbele ya Hakimu Msensemi alisema kwamba yeye hajawahi kumtukana ila yeye (mlalamikaji -Gibson) ndiye anayemfuata usiku kimazingira na kumfanyia vitendo viovu kinyume na maumbile.

"Hakimu naomba unisaidie ili huyu bwana anipumzishe walau siku mbili tu. Mimi nina mume wangu halafu nalala chumba kingine ili kumkimbia lakini wapi ananifuata ,nitafanya nini? Aniachie siku mbili tu ili nilale na mume wangu namuomba tena sana." Alilalamika Maria Maru.

Naye Neema Dawson anaripoti kuwa mama mmoja mkazi wa Kisarawe Mkoani Pwani amemfikisha mume wake mahakamani akimdai talaka kutokana na kushindwa kukidhi tendo la ndoa kwa mumewe

Shauri hilo ambalo lipo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama ya mwanzo Temeke Asia Dege mwanamke huyo ameiomba mahakama hiyo imuamuru mumewe ampe talaka yake baada ya kushindwa kumudu masharti ya ndoa.

Hakimu huyo alipopata nafasi ya kumuuliza Bw. Hassani Hashim mbaye ni mdaiwa katika kesi hiyo kama yuko tayari kumpa mkewe talaka, mdaiwa huyo aligoma kata kata mbele ya hakimu huyo na kudai kuwa hayuko tayari kutoa talaka kwa mkewe kwani bado anampenda.

Mbali na mgomo huo ,mdaiwa huyo alieleza mbele ya hakimu huyo kuwa tangu walivyooana na mkewe ambaye ni mdai wameishi naye kwa muda wa miezi mitatu tu, lakini mkewe amekuwa mkorofi hasa wakati wa tendo la ndoa na kudai kuwa imekuwa kero na kufukuzana kutupu hali ambayo inamfanya yeye kukasirika na kumpiga.

 

Kizimbani kwa kumuweka mke wa mjomba kimada

Na Leocardia Moswery

LEKWA Mgenga (46) amefikishwa kizimbani wiki hii akikabiliwa na shitaka la kumtwaa mke wa rafiki yake na kumweka kimada.

Katika shauri hilo ambalo lipo mbele ya Hakimu Maimuna Nangwalanya , katika mahakama ya Kariakoo, mshitakiwa, mkazi wa Kariakoo, ambaye aliwasili mahakamani akiwa "chicha" amekanusha madai hayo.

Mgenga anadaiwa kumweka kimanda mke huyo wa rafiki wa mjomba wake aliyefahamika kwa jina Mama Sefu kwa muda wa siku 14.

Katika kikao hicho cha mahakama mlalamikaji akitoa ushahidi alidai kuwa Mgenga alidai kuwa ameshawahi kumtorosha mwanamke huyo mara kadha.

"Alisimamia harusi yangu na pia ameshawahi tena kumtorosha wakati mimi nikiwa safarini morogoro. Na kuongeza kuwa huyu bwana ni mchezo wake na ni kipenzi sana na mjomba".alisema mlalamikaji Alipohojiwa zaidi katika ushahidi mlalamikaji alifafanua kwamba siku ya kuwafumania wakiwa wamelewa mwanamke alikimbia.

Mlalamikaji Moto mkazi wamtaa wa Kilomo karibu na hospital ya TMS alisema kuwa hakutegemea mshitakiwa kwa jinsi walivyiokuwa wakiheshimiana na mjomba wake anaweza kumfanyia kitendo hicho.

Akitoa maelezo yake hapo mahakamani mwendesha mashitaka Konstebo Gilbert alisema mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Bi. Maimuna kuwa mnamo Novemba 6 mwaka huu majira ya 3.00 usiku huko mtaa wa Kilomo mshitakiwa pamoja na mke wa mtu walikutwa wamelewa pombe na mlalamikaji na baada ya kukutwa mlalamikaji alishikwa na mwanamke huyo kukimbia.

Naye mshtakiwa alipohojiwa na hakimu alisema kuwa mlalamikaji anamsingizia na anaonekana kuwa na wazimu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi hapo Desemba, 22 mwaka huu mshitakiwa yupo nje kwa dhamana.

Mwanamke afanya fujo mahakamani

Na Gloria Tesha

MWANAMKE mmoja Fatuma Mohamed amefanya fujo na kuwatukana matusi ya nguoni mahakimu na maaskari wa mahakama ya mwanzo Temeke baada ya kutakiwa kueleza utaratibu aliouchukua kuuza nyumba ya kesi ya mirathi wakati yeye si msimamizi.

Katika kesi hiyo No. 130 ya marehemu Hamad Abdala Ngawezi inayosikilizwa mahakama kuu ya Wilaya Temeke inadaiwa kuwa Bi. Fatuma alishiriki kuuza nyumba ya Abdala Ngawezi kwa thamani ya sh. 5.5 milioni kwa Afisa Magereza Keko.

Nyumba hiyo Namba A/91 iliyopo keko Magurumbasi ambayo ilijengwa mwaka 1953 na Marehemu Abdala Ngawezi (mwenye nyumba) ilikuwa chini ya usimamizi wa Hassan wa Hassan A. Nawezi mtoto wa marehemu aliyeteuliwa na wanandugu katika mahakama kuu ya wilaya mbele ya hakimu Kayombo kusimamia shauri hilo namba 262 ya mirathi hayo.

Inadaiwa na ndugu hao kuwa hakimu Kayombo alitengua kesi hiyo na kuamuru ikasikilizwe upya katika mahakama ya mwanzo Temeke mbele ya hakimu mheshimiwa Matenyange ikiwa ni amri ya mahakama .

Ilitajwa kuwa tarehe 14 mwezi wa 12 wana ndugu wote walitakiwa wafike mahakamani hapo tayari tayari kusikilizwa upya kwa kesi hiyo ya mirathi lakini Bi Fatuma Mohamedi mke wa mmoja wa watoto wa marehemu Abdalah Ngawezi hawakufika .

Hata hivyo habari kutoka kwa mtoto mmoja wa marehemu Hasan Ngawezi zinasema kwamba badala ya Bi Fatuma kufika alimtuma bwana wake anayeishi naye kwa sasa ili aulize yeye anahusika na nini katika mirathi hiyo angali akijua kuwa nyumba yenyewe imekwisha kuuzwa kinyume cha sheria

Mke wa marehemu Abdalah Ngawezi Bi.Asha Seif Majumba (67) ameliambia Gazeti hili kwamba nyumba hiyo ambayo ni mali ya mumewe ni haki ya wanawe na yeye na si mali ya mkwe ambaye aliolewa akaikuta.

"Naomba niondoke hapa mahakamani, hakuna cha maana mnanipotezea muda wangu bure nyumba nimekwisha iuza na hamna la kunifanya na hata hivyo siongei na watu uchwara kama nyie mi naongea na majaji na ninaye jaji wangu:, alidai huku akiondoka kuelekea nje ya mahakama.

"Kama mna njaa semeni mimi naweza kuwalipa mshahara wa miezi mitatu kila mmoja na hivyo visenti vyenu kwangu ni uchafu, mnanionea wivu kwa kuwa napendeza", alizidi kuropoka mama huyo huku akijifunua na kuamuru waandishi wampige picha na kupeleka kokote.

Hata hivyo kwa kitendo hicho cha kuwavuruga maaskari na kuwachania mashati W.P. wawili amefunguliwa kesi ya kuivunjia heshima mahakama huku mashahidi wakiwa ni mahakimu wa mahakama hiyo.

Adaiwa kutishia kumuua mama yake

DAR ES SALAAM:Mohamedi Sakwa Akida (22) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya DMI amefikishwa kortini kwa kosa la kutishia kumuua mama yake mzazi.

Akisomewa hati ya mashitaka na mwendesha mashitaka wa polisi PC Mtanga kwamba mnano tarehe 12 Desemba mwaka huu alimtishia kumuua mama yake mzazi majira ya saa moja usiku.

Akijitetea Mohamedi alisema kwamba si kweli alimtishia kumuua bali alimuomba vyeti vyake vya shule ila mama yake hakumpatia. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 23 mwaka huu na shitaka hilo lipo mbele ya hakimu Jafari Msensemi.

Wakati huo huo Musa Yusuphu (18) na Hassani Malipula wanashitakiwa kwa makosa ya kuvunja nyumba na kuiba Simtank 1 pamoja na mbao vyote vikiwa ni mali ya Recho Mchomi.

Wakisomewa makosa yao na PC Mtanga mbele ya hakimu Jafari Msensemi kuwa mnamo tarehe 7 Desemba makira ya saa 11 alfajiri walivunja nyumba ya Recho na kuiba Simtank 1, beseni, misumeno pamoja na mbao. Walikana shitaka hilo na wamerudhishwa rumande hadi Desemba 28 mwaka huu.

 

Adaiwa kuiba ng'ombe

DAR ES SALAAM:Mchunga ng'ombe Kassimu Omary (21) amefikishwa katika mahakama ya mwanzo ya Kawe kwa kosa la wizi.

Akisomewa hati ya mashitaka na Mwendesha mashitaka PC. Mtanga mbele ya hakimu Jafari Msensemi kuwa mnamo Desemba 8 mwaka huu majira ya saa 8.00 usiku aliiba pesa shs. 22,000, mkanda wa video na redio ndogo vikiwa na thamani ya shs. 20,000, amekubali kosa, na kesi yake itatajwa tena Desemba 18 mwaka huu.

Wakati huo huo Judical Ezekieli (19) amefikishwa mbele ya mahakama ya mwanzo Kawe kwa shitaka la wizi wa kreti za bia zenye thamani ya shs. 60,000.

Akisomewa shitaka hilo mbele ya hakimu Msensemi, mwendesha mashitaka wa polisi PC.Mtanga kuwa mnamo Desemba 1 mwaka huu aliiba kreti nyumbani kwa Recho Mchoni.

Amekana shitaka na amerudhishwa rumande kwa kukosa mdhamini hadi Desemba 23 mwaka huu kesi yake itakapotajwa tena.

 

Akana kuiba mali

DAR ES SALAAM:Amosi Raymondi (23) na Patric Stephano (28) wamefikishwa kortini kwa kosa la kuvunja na kuiba mali na vitu vyenye thamani ya sh. 500,00 mali ya Cathline Adolf.

Wakisomewa mashitaka yao na PC. Mtanga mbele ya hakimu wa mahakama ya mwanzo Kawe Jafari Msensemi kuwa mnamo Novemba 28 mwaka huu, majira ya saa tano usiku walivunja nyumba na kuiba TV moja na deki yake na Music System vikiwa na thamani ya sh. 500,00. Wamekana shitaka lao na kesi yao itatajwa tena Desemba 23 mwaka huu