Mahakamani kwa ufupi

Na Dalphina Rubyema

Akana kuiba ng'ombe

DAR ES SALAAM: SAIDI Komba (38) ambaye ni mkazi wa Ipuli Mkoani Tabora,hivi karibuni alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Ilala kujibu shitaka la wizi wa ngo'ombe 11 wenye thamani ya shilingi 1,320,000.

Mbele ya hakimu wa Wilaya Angela Ngasoma,Mwendesha mashta wa mahakama hiyo Inspekta wa polisi Frances Nyange alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa aliiba ngombe hao mali ya Justice Kiteta Septemba 23 mwaka huu muda usiojulikana katika eneo la Kintiku Wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida.

Mshitakiwa amekana kuhusika na shitaka hilo na yupo nje kwa dhamana hadi Oktoba 22 kesi hiyo itakapotajwa tena.

Aiambia mahakama baba yake hampendi

DAR ES SALAAM:MKAZI mmoja wa Tegeta,Yusufu Kileo hivi karibuni aliiambia Mahakama ya Mwanzo Kawe kuwa Baba yake hampendi kwa vile anapata na kufuata maneno ya uongo kutoka kwa mama yake wa kambo.

Yusufu ambaye ni miongoni mwa washitakiwa wanne waliofikishwa Mahakamani hapo kwa kosa la kufanya fujo,alitoa maelezo hayo mbele ya hakimu Janeth Mnyuwa ambapo washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Julius Milwa(26),Dickson Salakan(23) na Yahya Husein (29).

Akisoma hati ya mashitaka,msoma mashitaka wa mahakama hiyo Konstebo wa Polisi Bakari Bakari alidai kuwa washitakiwa walimpiga ngumi Anthony Tarimo na walifanya kosa hilo Agosti 11 mwaka huu saa 12,00 asubuhi.

Washtakiwa walikana kosa hilo na wapo nje kwa dhamana hadi Oktoba 22 mwaka huu kesi yao itakapoanza kusikilizwa.

Kizimbani kwa kutotunza watoto

DAR ES SALAAM:GAUDENSIA Paulo hivi karibuni alimfikisha mme wake kizimbani kwa tuhuma za kutompatia matunzo.

Mbele ya hakimu Mwanadamizi Stella Kihengu,Msoma mashtaka wa mahakama hiyo Kosntebo wa polisi Khamisi Juju alidai kuwa Hassan Said ambaye ni mme wa mshitakiwa aliacha kutotoa matunzo kwa familia yake yenye mke na watoto wanne tangu mwaka 1994.

Mshtakiwa alikana kuhusika na tuhuma hizo na yupo nje kwa dhamana hadi Oktoba 23 kesi hiyo itakapotajwa tena.

Ashindwa kulipa bia alizokunywa

DAR ES SALAAM:MKAZI mmoja wa Kariakoo Anzan David (29) hivi karibuni alifikishwa katika mahakama ya Mwanzo Magomeni kujibu shtaka la kushindwa kulipa deni la chupa 16 za bia zenye thamani ya shilingi 12,000.

Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Bibi Marry Matoi,Msoma mashtaka Mussa Ruchahe alidai kuwa mshtakiwa alikunywa bia hizo na baada ya kumaliza kunywa alikataa kulipa gharama yake na ni mali ya Ngowi Peter .Mshtakiwa alikana shtaka na yupo nje kwa dhamana.