Haki ya mwanamke kutoa mimba na madhara yake

Je mwanamke ana haki ya kutoa mimba? Kama sivyo hiki ni nini? Wapo wale wanaosema mwanamke anayo haki ya kuudhibiti na kuumiliki mwili wake mwenyewe na hivyo kudai wana haki ya kutoa mimba.Haki ya Mwanamke kutoa mimba? Hili ni suala linalozua mjadala mkali kila linapozungumziwa kutoka makundi yenye imani tofauti za Dini na Kitamaduni: Hata hivyo bado utoaji mimba unafa-nywa kwa siri katika Nchi ambazo kutoa mimba ni kosa la Jinai na kusaba-bisha vifo vingi. Katika makala haya Mwandishi wa Shihata, Shishee Belela, anaelezea madhara yanayowapata wanawake kwa utoaji mimba na njia za kuzuia mimba zisizo-hitajika.

 

YAPO madai kuwa utoaji mimba ni kitendo ambacho mwanamke anakifanya akiwa hana uhakika na matokeo yake.Lakini kwa wataalamu wa mambo ya kisaikolojia na hata utaalamu wa tiba wanatuambia kwamba huo ambao mara nyingi ndio unakuwa mwanzo wa matatizo ya tumbo la uzazi, kila mtu anajua.

Matatizo ya sasa kwa wanawake wengine kuhusiana na tatizo la kuporomosha au kutopata kabisa mimba huenda yamechimbiwa na vitendo vyao vya zamani vya utoaji mimba ambavyo mara nyingi huleta mushkeri mkubwa katika tumbo la uzazi.

Hivyo mhusika mara nyingine hushindwa kupata mtoto maishani mwake au anaweza kupoteza maisha kabisa.

Ingawa katika mkutano uliozungumzia ongezeko la watu duniani uliofanyika Cairo, Misri mwaka 1994 kati ya moja ya maazimio yaliyopitishwa ni nchi ambazo haziruhusu utoaji mimba ziruhusu mwanamke awe na uhuru wa kutoa mimba na pia kuhakikisha kuwa wanawake wanapata elimu juu ya uzazi wa mpango.Hali halisi ni kinyume na matarajia ya akili ya binadamu na haki ya kusihi ambayo ni ya kila kiumbe chenye uhai hata kama hakiwezi kujitetea.

Kwani miaka minne sasa toka Mkutano wa Cairo ufanyike, nchi nyingi bado hazijatekeleza maazimio yaliyopitishwa Cairo kama ilivyo kwa maazimio mengine yanayopitishwa na Jumuiya za Kimataifa kutokana na sababu mbali mbali .Moja ya sababu sawia ni misimamo ya kidini na kitamaduni dhidi ya zana nzima ya uhuru wa mauaji ambao huitwa haki ya mwanamke kwa mujibu wa mkutano wa Cairo.

Hata hivyo kila mwaka mamilioni ya wanawake duniani wanahatarisha maisha yao kwa kutaka kutoa mimba ambazo hawazihitaji. shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kila siku mimba 55,000 zinatolewa kwa njia zisizo salama kati ya hizo, asilimia 95 ni kutoka katika nchi zinazoendelea.

Katika taarifa maalumu ya kuadhimisha siku ya Afya Duniani Aprili 7, mwaka huu, WHO inakadiria wanawake 75,600 duniani wanakufa kila mwaka kutokana na utoaji mimba usio salama sawa na zaidi ya vifo 200 kwa siku.

Ingawa idadi hiyo inaonekana kubwa, lakini shirika hilo la Afya lnasema bado haionyeshi hali halisi ya tatizo lenyewe ikizingatiwa kuwa wanawake wengi wanaathirika wanatoka katika nchi zinazoendelea ambapo ni vigumu kufanya utafiti kutokana na matatizo ya fedha.

Ukiondoa nchi ya Japani, Nchi za Asia zinaongoza kwa tatizo hilo ambapo wanawake 37,600 wanapoteza maisha yao kila mwaka na katika nchi za Afrika wanawake 33,000 wanapoteza maisha yao kwa kutoa mimba.

Kwa upande wa Tanzania, inakuwa vigumu kupata takwimu halisi ya idadi ya wanawake wanaokufa kutokana na kutoa mimba kwa kuwa kutoa mimba ni kosa la jinai, hivyo mimba nyingi zinatolewa kwa siri, mara nyingi zinatolewa na watu wasiokuwa na utaalamu.

Vyombo vya habari mara nyingi vimeripoti juu ya vifo vya wasichana wadogo vilivyosadikiwa kusababishwa na kutoa mimba.

Mwanzoni mwa mwaka jana msichana Silvia Haule, alikufa muda mfupi baada ya kufika Hospitali ya Temeke na baada ya uchunguzi iligundulika kuwa kifo chake kilisababishwa na utoaji mimba.

Dk. Kalista Simbakalia kutoka Waizra ya afya kitengo cha Huduma ya Afya na Mama na Mtoto (MCH) anaeleza kuwa kuna Idadi kubwa ya wanawake wanaokwenda Hospitali wakiwa na matatizo ya tumbo yanayotokana na vitendo vya kutoa mimba.

Hata hivyo, Dk. Simbakalia anasema kwamba idadi kamili ya wagonjwa hao, haijulikani kwani Wizara ya Afya haijafanya utafiti kuhusu suala hilo.

Kwa mujibu wa WHO, utafiti uliofanywa katika Hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam unaonyesha kuwa asilimia 34 mpaka 57 ya wagonjwa waliolazwa katika Hospitali hizo kwa matatizo ya tumbo walikuwa na matatizo yanayotokana na utoaji mimba usio salama.

Aidha WHO katika taarifa yake ya mwaka huu kuhusu uzazi salama, inasema kuwa wanawake wengi wanaotoa mimba wameolewa au wanaishi na wanaume kama mke na mume na tayari wana watoto.

Taarifa hiyo imefafanua kwamba lengo la wanaotoa mimba hizo ni kutaka kudhibiti idadi ya watoto, wala siyo kuchelewesha uzazi wa kwanza.

Wanawake wengi wanajikuta na uja uzito wasioutarajia kutokana na sababu mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutotumia huduma ya uzazi wa mpango au matumizi mabaya ya njia hizo.

Kati ya mimba milioni nane (8) na milioni 30 kila mwaka, zinatokana na wanawake kushindwa kutumia njia za uzazi wa mpango au matumizi mabaya ya njia hizo.

Sababu nyingine zinazomfanya mwanamke apate mimba asiyoitarajia ni pamoja na kubakwa, hali mbaya ya maisha inayomfanya msichana mdogo kuhangaika kutafuta riziki kwa kutumia mwili wake.

Ingawa tatizo la utoaji mimba liko kwa wanawake wa umri wote, lakini ni kubwa zaidi kwa wasichana wadogo, ambao uwezo wao wa kupata elimu juu ya huduma ya uzazi wa mpango ni mdogo na pia ni vigumu kwao kupata fedha kwa ajili ya kutoa mimba kwa wataalamu.

Kutokana na wasichana wenye umri mdogo kujihusisha na vitendo vya ngono, mara nyingi wanakuwa hawana ushauri, hivyo pindi wanapokuwa wajawazito wanakuwa waoga kuwaeleza wazazi wao.

Hali hiyo inachangia wasichana hao kutegemea kupata ushauri kutoka kwa wenzao, ambao mara nyingi maamuzi yao yanahatarisha maisha yao.

WHO inasema katika nchi za Afrika asilimia 70 ya wanawake wanaolazwa kwenye Hospitali mbali mbali kwa matatizo ya utoaji mimba wana umri wa chini ya miaka 20.

Ili kuondokana na tatizo hilo, vyombo vinavyohusika havina budi kuhakikisha kwamba huduma ya uzazi wa mpango inatolewa kwa watu wote hasa wakina mama na wasichana pamoja na kuwaelimisha njia mbali mbali za kuepuka mimba zisizohitajika, izkizingatiwa mafunzo ya dini na kitamaduni kuhusu mazingira ya kujamiiana katika jamii.

Dk. Anatoli Rukonge, mratibu wa Huduma ya Uzazi wa Mpango wa Chama cha Uzazi na Malezi bora Tanzania (UMATI) anasema kuwa ni wanawake 50,000 tu ndio waliojiunga na huduma za uzazi wa mpango.

Dk. Rukonge anabainisha kuwa ingawa wanawake wengi wangependa kujiunga na huduma za uzazi wa mpango lakini wanakabiliwa na vikwazo kutoka kwa waume zao na wengine wanashindwa kutumia njia mbali mbali za uzazi wa mpango kwa sababu inapingana na imani ya dini zao.

Aidha vyombo vinavyohusika vihakikishe wanaume wanaelimishwa kuhusiana na mpango wa uzazi madhara yake na kupewa jukumu la wao wenyewe kuchagua njia salama na bora ya kuwawezesha kuwakubalia wake zao kuzaa kwa mpango hivyo kuzuia uwezekano wa kupata mimba zisizohitajika.

"Kama jamii itaelimishwa na kuelewa juu ya faida ya kujiunga na huduma ya uzazi wa mpango, basi lengo la kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na mimba kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2000 litafanikiwa," Amesisitiza Dk. Rukonge.

Chama cha Uzazi na malezi Bora nchini (UMATI) kwa kushirikiana na Waizara ya Afya imeanzisha Kilniki zinazotoa elimu ya uzazi na magonjwa ya zinaa kwa lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya suala hili muhimu.

Kliniki hizo (Community based Distributing Agents) zilizoanzishwa katika mikoa ya Ruvuma, Tanga, Mtwara, Dodoma, Arusha pamoja na Dar es Salaam zisambazwe mikoa yote ili kupeleka huduma hiyo karibu zaidi kwa wananchi.

Serikali kupitia Wizara mama ya Afya, haina budi kuongeza juhudi katika kuwapatia elimu wazazi ambao nao wataelimisha vijana wao wa kike na kiume juu ya athari za kuzingatia uzazi salama, ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha madhara yatokanayo na utoaji mimba ili iweze kufikia lengo lake la kupunguza vifo vitokanavyo na mimba za uzazi.

 

MUHIMU:Makala haya ni ya Shihata hayana mahusiano yoyote na msimamo wa kanisa kuhusu uzazi wa mpango ambapo inasisitizwa kutumia njia ya asili.Kwa Kanisa utoaji mimba ni mauaji tunakaribisha mawazo zaidi kutoka kwa wasomaji wengine kuhusiana na sakata hili la haki ya mwanamke kutoa mimba. MHARIRI

 

Nionavyo kuhusu Sheria

Na Zakie Chattanda

Wanaoingia mikataba ni lazima waridhiane

1. MKATABA ni makubaliano ya hiari ya pande mbili yenye lengo la kibiashara au masuala yoyote, kutegemeana na mazingira ambayo wenye mikataba wanatarajia kuingia.

2. Mbali na dhana hiyo, mkataba ili ukamilike na kukubaliwa kisheria ni lazima utimize masharti yaliyowekwa.

3. Masharti hayo yametajwa wazi wazi kuwa ni lazima wanaoingia mkataba wakubaliane wenyewe bila kulazimishwa wala kushinikizwa. Wanaoingia mkataba ni lazima kuwepo na pande mbili.

4. Kadhalika ili mkataba uheshimiwe na kukubalika lazima uwe na sifa zilizo wazi na zinazokubalika kisheria.

5. Baadhi ya sifa hizo ni kwamba mkataba lazima usomeke na mtekelezaji wa mkataba huo lazima utoe malipo na kupangiwa muda kulingana na mkataba wao unavyosema.

6. Sifa zingine, mkataba au wanaoingia mkataba wawe na mawasialiano ya mara kwa mara ili kuweza kueleweshana na kukumbushana majukumu ambayo yapo kwenye mkataba kwa nia ya kuwekeana msimamo ili yaendelee kutekelezwa kama inavyokusudiwa, bila kukikwa.

7. Sifa nyingine ya mkataba ni kwamba kuwepo na taarifa ya awali, kutoka upande ambao unataka kuingia mkataba na upande mwingine, taarifa hiyo iwe ya kumshawishi mtu/upande ambao unataka kuingia nao mkataba na upande huo urudishe taarifa kuwa umekubali.

9.Kwa mantiki hiyo mkataba unaotambulika ni ule ambao pande zote mbili zimeridhiana awali kabla ya kuingia mkataba, baada ya upande mmoja kutuma taarifa (offer) na upande mwingine kuonyesha kuwa umekubali.

10. Kwa mujibu wa vifungu vya sheria kuhusu mikataba ni katika kitabu cha kanuni ya adhabu sura ya 433, sura hiyo inafafanua wazi kuwa mkataba lazima uwe wa hiari na kama sio wa hiari basi sio mkataba.

11. Hata hivyo kifungu cha 15, kinaanisha kuwa pande zinazoingia mkataba lazima zikubaliane na kuwekeana saini katika mkataba kwa hiari na kama kutokuwepo kulazimishwa kuweka saini basi huo mkataba utakuwa Batili.

12. Kifungu kingine ni cha 17 ambacho nacho kinaeleza wazi kuwa kama utakuwepo udanganyifu na wanaoingia mkataba kusaini bila kujua halafu wakaja kujua baadaye basi wana haki kisheria kuukataa mkataba.

13. Mfano ambao upo wazi ni katika kesi ya Holwel Securities Ltd, v. Hughes (1974) l Wlr 155 ambapo wahusika katika kesi hii waliigia mkataba lakini upande mmoja haukujibu kama umekubali kuingia au la licha ya kutumiwa taarifa.

14 Upande uliotia saini kwa ajili ya kushawishi upande mwingine ulianza kutuwa mizigo kwa lengo la kufanya biashara wakati upande mwingine haujakubalil icha ya kupokea taarifa (offer).

15. Kisheria katika mazingira hayo hapakuwepo na mkataba wowote unaotambulikana na kama mtuma bidhaa, bidhaa zake ziliharibika au kupotea basi hasara itabidi aigharamie mwenyewe.

16. Katika kesi hiyo mahakama ilitamka wazi kuwa hasara zote alizoingia mtumajiwa bidhaa atalazimika kugharamia mwenyewe kama kuna hasara imetokea na kuongeza kuwa upande wa pili haukuonyesha kukubali kuingia mkataba kwa njia ya maandishi.

18. Hata hivyo sheria ya kuingia mkataba inaelezea wazi kuwa kama utakuwa na udanganyifu huo sio mkataba, na kama kutakuwepo kulazimishana nao sio mkataba na kuongeza kuwa kama mkataba utakiukwa au kuvunjwa masharti yake, basi utabatilishwa na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa muhusika aliyevunja mkataba.

ZINGATIA: (Tafsiri kutoka lugha ya Kiingereza kuja kiswahili ni ya mwandishi)