Umuhimu wa tabia mafanano na tofauti katika ndoa

TALAKA zimeongezeka sana katika familia zetu.Si talaka tu ambazo zinakimbizana kama vile mashindano ya marathoni bali nyumba nyingi zimejikuta zikiwa katika msukosuko mkubwa.

Msukosuko huu mara nyingi huishia katika talaka.Pamoja na juhudi kubwa ya kanisa kutoa mafunzo kwa waumini wake, hali bado inatisha.

Ni nia ya gazeti hili kuimarisha kaya za waumini na wasiowaumini kwa hiyo katika kurasa huu tutakuwa tunawaletea maelezo mbalimbali kuhusu ndoa , maisha na mambo kadha wa kadha yanayopasa kuangaliwa kwa makini katika familia zetu.

Ingawa hakuna jibu wala swali la ziada lenye majibu ya mkato nia ya eneo hili ni kuboresha mahusiano ya kifamilia.

Ukiwa na swali kuhusiana na makala zenyewe au swali ambalo linakukera tuandikie:

Ushauri wa ndoa na maisha,

Mhariri Kiongozi,

P.o Box 9400 Dar es salaam

Na tunakuhakikishia majibu kutoka kwa wataalamu wa masuala ya jamii na wachungaji wako

Utangulizi

BILA shaka, twaona mara na mara ndoa za watu hutaabika na magomvi na fitina; na kisha hali hiyo kuanza, majirani huingia kuwatuliza au kuwachochea wenye kugombana. Lakini, kwa kawaida, wanawake humpigania mwanamke na wanaume humpigania mwanamume. Sababu gani?

Twakuta mara na mara wanaume hawafahamu tabia ya wanawake wakisema: "hawana akili, kichwa cha kuku..." Vivyo hivyo, wanawake hawafahamu tabia ya wanaume wakidhani: "wakorofi".

Inapashwa iweje: Tumeumbwa wote kwa sura ya Mungu, na kwa hiyo tuko sawa. Twafanana wote na Mungu, na kwa hiyo twafanana sisi kwa sisi. Wote wana akili, wote wana roho zenye kudumu milele; wote wameitwa kuwa watoto wa Mungu na wote wameitikia vile vile- katika hali ya dhambi, hali ya kuokolewa. Hakuna aliye bora zaidi sababu ni mwanaume ama mwanamke.

Mungu alituumba wenye tofauti. Twaweza kuona kwamba miili ina tofauti, mwanamume kwa mwanamke: za nje, za ndani. Lakini si wote wajuao tofauti baina ya tabia moja na nyingine.

Habari yenyewe: Mengine yapo, lakini tuangalie na kulinganisha yanayoweza kusababisha shida katika ndoa.

1. Nguvu kwa kazi: Wanaume wana nguvu kadiri ya mazoezi waliyopewa kwa kuwatayarisha kwa kazi zao: kufyeka, kubeba kuni kubwa, kubeba mizigo mabegani, kujenga, n.k. Katika kazi hizo wanaume huwashinda wanawake kwa wastani.

Wanawake wamezoea kazi nyingine, na nguvu zao zimezoea kuzitenda: Kazi hizo ni kama kutwanga mahindi, kusaga ulezi, kubeba mtoto mgongoni na mizigo kichwani, n.k. Katika kazi hizo, wanawake huwashinda wanaume kwa wastani.

Kumbe, nguvu za kazi siyo sababu ya kuchukiana. Wanaume huwakosea wanawake wakisema hawana nguvu yoyote, na wanawake huwakosea wanaume wakifikiri ni nguvu za kijambazi tu. Mazoezi huwatayarisha kila mtu kwa kazi kusudi kazi za wote husaidina na kukamilishana.

2. Akili na Elimu: Wanaume, kama watoto, walisisimuliwa zaidi kusoma shule na kupata elimu, na wamezoezwa na wazee kufikiria na kujadili makubwa makubwa kama siasa, mipango ya jamaa na kijiji. Wamezoea kusema.Wanawake, kama watoto, wengi walinyimwa elimu kamili shuleni; ama hawakuruhusiwa kwenda ama walitolewa mapema kusaidia katika kazi za nyumbani.

Hii siyo sababu ya kukosa akili, bali fikra za watu hazithamini elimu kuwa muhimu kwa akini mama, kama kwa akina baba. Tena, wamezoezwa na wazee kukaa kimya mbele za akina baba na kufikiria madogo kama utunzaji wa watoto na nyumba.

Kumbe, wanaume huwakosea akina mama wakisema hawana akili- akili wanazo, ila wamenyimwa nafasi ya kuzipanua kwa kupata elimu shuleni - wamezoezwa kunyamaza. Kwa hiyo, hawasemi sana juu ya makubwa. Wote wakumbuke, katika shida zote makubwa na madogo yapo - kwa hiyo, wapeane nafasi ya kusema, na kusikiliza. Akina mama wakikosa kusema huenda mipango itashindwa!

3. Hasira na Ukali: Wanaume wana hasira inayoamka hima kwa wastani, tena na hasira isiyoridhika na maneno, hata matusi. Mara nyingi hawatambui nguvu za maneno yao, na wanaanza kuchemka zaidi na ngumi au silaha, wakitaka kweli kumshinda adui kabisa. Hasira yao hutumia nguvu mara nyingi - lakini hupoa haraka, na hata kesho yake waliopigana wanawake kuwa marafiki tena.

Wanawake wana hasira inayoamka polepole zaidi, kwa wastani - na matamshi yake ni ya maneno tu hasa; mara chache tu labda wanatumia nguvu. Maneno mengi na sauti kuu! Tena , ikiamka, hasira yao hutunzwa muda mrefu kuliko hasira ya wanaume. Usipime saa, pima siku!

-Kumbe, wanaume waangalie hasira yao isifike moto wa kulipuka na matendo ya ukali yanayoharibu zaidi ya maneno, na hata kuleta mashitaka. Wanawake wasitunze hasira moyoni hata, bwana akija kupatana, hawawezi kuona mapatano yoyote. Akina mama waangalie ukali wa akina baba; akina baba waangalie udumifu wa hasira ya akina mama. Wakaribiane na kupatana polepole, lakini wasikatae kupatana kisha ugomvi. Wagombanao wapatanao!

4. Kusikia na Kujihoji: Wanaume si wepesi kwa wastani kwa kujihoji katika dhamira ijapokuwa wanazoea zaidi kufikiria makubwa. Huwa wanaona kukiri makosa, kujipatanisha wazi, ni kama kujiaibisha na kumwaga heshima chini - hasa mbele ya wanawake. Sababu ni kiburi ama haya?

Wanawake - kwa tabia, hutunza mambo zaidi moyoni, tena pengine mno. Zaidi hutafiti dhamiri na wakikiri kosa, hufanya kwa kirefu zaidi na wako tayari zaidi kupokea mashauri kuliko wanaume, wastani.

-Kumbe, kwa kuwa kujipatanisha ni kitu cha lazima katika maisha, na zaidi katika ndoa, ni muhimu kutambua ni hatua inayotakiwa kwa maendeleo ya ndoa. - ijapokuwa ina maumivu yake. Siyo aibu - bali unyenyekevu; sote ni wakosefu na kusameheana na kuungana ni alama za tabia zinazofaa.

5. Tamaa za mwili :Wanaume huwaka vyepesi, pengine bila msisimuo mkubwa na katika tendo la ndoa mielekeo ni kutimiza mapema; kisha hapo, hutulia vyepesi.

Wanawake huwaka polepole zaidi kwa wastani, na pengine kwa msisimuo mkubwa tu. Tena, kisha tendo, hutulia polepole zaidi kuliko wanaume.

Kumbe, kujiangalia na kujikinga na vishawishi, ijapokuwa ni mazoezi yanayotakiwa kwa wote kwa kutunza tabia njema, labda twaweza kusema ni muhimu zaidi kwa wanaume. Baadaye, tutakapozungumzia viungi vya uzazi, utaratibu utasisitizwa na mashauri.

Nini tumejifunza kwa uhakika: Bwana na Bibi waheshimiane, kila mmoja akitambua ndani ya mwenzake sura ya Mungu. Kila mtu anacho kichwa chenye kumwongoza kwa akili na moyo mwenye kuwaka upendo.

Katika ndoa, mume ni kichwa na mke ni moyo - hata tofauti za tabia zao huoenyesha ya kuwa mume hutawaliwa zaidi na kichwa na mke hutawaliwa zaidi na moyo! Watumie tofauti za tabia zao ili kuendesha ndoa yao kikamilifu.

Tena, itakavyosisitizwa baadaye, tutakapozungumzia ulezi wa watoto, watoto huhitaji ulezi wa wazazi wote wawili wapate pia tabia za kikamilifu. Mtoto anarith tabia za wazazi wake na anahitaji matunzo sawa apate kupevuka sawa. Mtoto anayelelewa na mama peke yake atakuwa na kasoro ya tabia, na vivyo hivyo akilelelwa na baba tu hatapevuka inavyotakiwa ki-moyo.

 

MAARIFA

na Uncle

Trevor

 

Wazungu Waipeleleza Pwani ya Afrika

Katika karne ya 15 wafanya biashara wa Ulaya walikuwa wakitafuta njia ya baharini ya kufikia Bara Hindi na Uchina. Shughuli hii ililifanya Bara la Amerika livumbuliwe na kadhalika Bahari Kuu ya Pacific ipelelezwe sana, tena iliwafanya Wazungu kufika kwenye pwani za Afrika.

Wareno ndio walio- tangulia. Mfalme Henry, Baharia mashuhuri (1394-1460), aliwapeleka wanamaji wa Kireno kuipeleleza pwani ya Afrika Magharibi.

Mfalme huyu alipendelea mno biashara na jiografia. Aliketi na ramani zake huko Sagres akiwangojea wanamaji wake.

Mwaka 1434 wanamaji wa Kireno walifika Rasi ya Bojador, na mwaka 1445 walifika Rasi ya Verde, mwaka 1462 walifika Sierra Leone.

Katika mwaka 1469 Gomez aliendesha biashara na nchi ya Guinea na mwaka 1482 Diego Cao alifika kwenye maingilio ya mto Congo.

Njia ya kupitia ncha ya kusini ya Afrika ilivumbuliwa wakati Bartholomew Diaz alipoizunguka Rasi ya Tumaini Jema.

Miaka kumi ilifyofuata Vasco da Gama aliendelea mbele zaidi katika pwani ya Mashariki kuelekea Kaskazini mpaka Mali- ndi kabla ya kuvuka kwenda Bara Hindi. Wengine walimfuata na baada ya mwaka 1600 pwani ya Afrika ilijulikana, na ramani ikachorwa.

Ingawa Wareno walitaka hasa kufanya biashara na nchi za mashariki, walianza kufanya biashara na Waafrika pia, wakinunua pembe za ndovu, dhahabu, viungo na watumwa. Walifanya makao yao katika miji ya biashara ya Waarabu katika Dola ya Zenj huko pwani ya mashariki. Walijenga ngome, kama Elmina katika pwani ya magharibi, na Fort Jesus lililoko Mombasa. Ngome hizi zilikuwa vituo vya biashara; zikawa bandari maarufu kwa meli zote ziendazo na zitokazo Bara Hindi.

Kokote Wareno walikotangulia kwenda, walifuatwa na Waingereza, Waholanzi, Waspania, na Wafaransa. Baada ya mwaka wa 1550, Waingereza walikwenda hasa Guinea na kwenye maingilio ya mto Niger ili kupata pembe za ndovu, dhahabu na watumwa,

Watumwa hawa walisafirishwa kwa marikebu mpaka visiwa vya Magharibi. Kwa kuwa Waholanzi nao walitaka kupata bandari moja ambako merikebu zao ziendazo Visiwa vya Mashariki ziweze kutua, basi walijenga huko Capetown mwaka 1652.

Ngome na makao haya makuu ya pwani baadaye yalitumiwa na wapelelezi wa Ulaya kuwa milango ya kuingilia barani ili kuanzisha makoloni yatakayotawaliwa na dola za Ulaya.