Make your own free website on Tripod.com

MAARIFA na Uncle Trevor

 

Tabia : Mapatano yanayotakiwa kwa Maisha ya Ndoa

TALAKA zimeongezeka sana katika familia zetu.Si talaka tu ambazo zinakimbizana kama vile mashindano ya marathoni bali nyumba nyingi zimejikuta zikiwa katika msukosuko mkubwa.

Msukosuko huu mara nyingi huishia katika talaka.Pamoja na juhudi kubwa ya kanisa kutoa mafunzo kwa waumini wake, hali bado inatisha.

Ni nia ya gazeti hili kuimarisha kaya za waumini na wasiowaumini kwa hiyo katika kurasa huu tutakuwa tunawaletea maelezo mbalimbali kuhusu ndoa , maisha na mambo kadha wa kadha yanayopasa kuangaliwa kwa makini katika familia zetu.

Ingawa hakuna jibu wala swali la ziada lenye majibu ya mkato nia ya eneo hili ni kuboresha mahusiano ya kifamilia.

Ukiwa na swali kuhusiana na makala zenyewe au swali ambalo linakukera tuandikie:

Ushauri wa ndoa na maisha,

Mhariri Kiongozi,

P.o Box 9400 Dar es salaam

Na tunakuhakikishia majibu kutoka kwa wataalamu wa masuala ya jamii na wachungaji wako

Utangulizi: Ijapokuwa mvulana na msichana wanaofikiri wataweza kuwa bwana na bibi wa ndoa, wanaanza kufahamiana kwa kuzungumza na kupeana mawazo juu ya mambo mbali mbali - watabaki wageni kwa muda mrefu. Kufahamiana kimoyo na kitabia huhitaji muda mrefu wa kukaa pamoja.

Inayoonekana wazi ni wavulana na wasichana wengi hawachukui muda mrefu kwa kazi hiyo inayotakiwa kwa kutayarisha msingi bora kwa ndoa - wanachumbia na kufunga ndoa haraka, na ndoa zao huanza gizani kabisa. Afadhali wachumbie kwa muda, wakipelelezana zaidi na kuleta mwanga, walau kidogo, katika urafiki wao na kuona jinsi watakavyoweza kupatanisha tofauti katika tabia na kuepa matatizo ya baadaye.

Mantiki yake

1. Kusikilizana: Kabla ya ndoa wavulana wa wasichana hawakabiliwi na kazi hiyo kati yao kwa kuwa kila mmoja anaishi kwake. Maisha ya pamoja ni mazungumzo tu - yaani ni ya nje tu. Katika ndoa, watakabiliwa na mengi zaidi: kujenga pamoja, kulima pamoja, kutunza watoto pamoja, n.k. Na kila anayofanya mmoja huhusika kikamilifu na mwenzake. Ukweli huo husahaulika mara nyingi.

Kusikilizana huhitaji kila mtu awe tayari kutoa mawazo yake, kusikiliza ya mwenzake - na hapo tu kuufikia kwa pamoja utekelezaji unaofaa: kupima mazao kwa chakula na mauzo, kupima matumizi ya fedha, juu ya malezi bora ya watoto, n.k. Umuhimu mkubwa ni kuwa tayari kusikiliza maoni ya mwingine na kuyafikiria.

2. Kupokea kauli: Zaidi ya kusikiliza kauli za mwingine, kila mwenye ndoa huhitaji kipaji cha kupokea kauli moyoni hata zikiwa tofauti sana na zake mwenyewe. Si rahisi!

Maelekeo yetu ya kibinadamu ni kumwona mwingine na kauli tofauti kama adui. Lakini sivyo; ni matokeo ya tofauti za asili, tabia, maoni na mazingara.

Kupeana kauli ni njia bora ya kufahamu zaidi mazingara badala ya kuona upande mmoja tu. Tena, kupokea kauli kweli huhitaji muda wa kufikiria; kwa hiyo, kama nafasi ipo, maazimio yasikatwe haraka, bali muda uwepo na mapatano na utekelezaji utakuwa na thamani kubwa.

3. Saburi/uvumilivu: Ijapokuwa mafanano yapo, tofauti zipo pia na huenda tofauti hizo zinaweza kuchokoza na kukasirisha (hasa wakati wa uchovu, masukosuko, n.k.).

Pengine itakuwa vigumu kupatanisha kauli tofauti na njia ya pekee ya mbele ni saburi na kuvumilia: tofauti za kazi, mazoea ya vyakula vingine, desturi ndogo ndogo. Kila mmoja akimbuke kwamba mwenzake hupaswa kuyavumilia yake.

4. Kusameheana: Tofauti huweza kuvumiliwa pengine kwa muda, na kisha hapo, au wakati wa uchovu na masukosuko, twafikia kiasi kinachotulipusha na hasira. Kwa kiasi, si kitu - hasa tukiwa na uradhi wa kusameheana. Ikumbukwe ya kuwa ni afahali sana kusawazisha malipuko hayo nyumbani kuliko kwenda nje. Afadhali unyenyekevu nyumbani kuliko aibu nje!

5. Matazamio yasiyotimizwa: Kila wa ndoa anamtegemea mwenzake kiasi fulani, hasa mwanzoni mwa maisha ya pamoja - hasa zaidi ikiwa muda wa uchumba ulikuwa mfupi bila kupelelezana sana. Mmoja akipita matazamio ya mwenzake humfurahisha; akishindwa kutimiza matazamio ya mwenzake, humsikitisha. Ni hivyo pade zote mbili. Ndiyo maisha.

Inafaa kuchunguza moyoni kama matazamio tuliyoyatazamia yalikuwa ya haki au siyo. Tuwe tayari, hata hivyo, kupokea masikitiko kwa moyo radhi, kwa upendo na msamaha na kuona kwamba ni sehemu moja tu katika maisha. Licha ya hayo, masikikito yasitunzwe moyoni, kwa kuwa yataota vibaya na kuchafua moyo na hali ya ndoa.

Nini maana ya yote hapo Juu

Kufahamiana ni kazi ya maisha mazima na msingi wake ni tabia radhi. Hakuna mwalimu anayeweza kufundisha kazi hiyo, sisi sote ni wanafunzi.

Kabla ya ndoa, wachumba huangaliana kwa mbali na kukosa kuona mengi; lakini katika ndoa, hukaribiana na kuangaliana kwa karibu - mema na mabaya.

Kufahamiana huhusika na utu uzima: mawazo, kauli, imani, mwili, roho, akili, mazoeo, hofu, matumaini, vipaji, elimu, matazamio, asili, ujuzi, marafiki ...Ni bahari kweli.

Kwa hiyo, wachumba wapelelezane kweli, wasiwe na haraka ya kufunga ndoa. Watumie muda wa kufahamiana, na hivyo wajifahamu zaidi.

Safari ijayo tutaizungumzia kwanza sheria ya ndoa kwa kupata angalau dodoso ndoa zenyewe kisheria zikoje.

 

Upelelezi katika Bahari Kuu ya Pacific

UTAFUTAJI wa biashara Mashariki kuliwafanya Wareno na Waispania wawe wa kwanza kusafiri katika Bahari Kuu ya Pacific.

Lakini katika karne zingine mbeleni, kama 500 A.D., Bahari Kuu ya Pacific ilipelelezwa na Wapolenesia waliokwenda huko katika mitumbwi kutoka nchi kavu ya Asia na kufanya makao yao katika visiwa.

Watu wengine kutoka Amerika ya kusini walisafiri kuja kufanya makao yao pia katika visiwa vya Bahari hii ya Pacific. Wanamaji wa kale wa Kichina na wa Java walikwisha ipeleleza sehemu ya magharibi ya bahari hii ya Pacifici.

Katika karne ya 16 wanamaji wa Ulaya waliingia bahari hii.

Wareno walikuwa wa kwanza: waliingia upande wa mwisho wa magharibi, wakasafiri wakifuata pwani mpaka Uchina na Japan.

Waspania walifuata: mwaka 1521 merikebi za Magellan zilisafiri kuivuka bahari toka mashariki hadi magharibi, na mwaka 1606, Torres alisafiri toka Amerika ya Kusini mpaka New Guinea. Francis Drake, yule Mwingereza mashuhuri, aliivuka bahari kwa kupitia kaskazini zaidi katika mwaka 1579.

Katika karne ya 17, mabaharia wa Kiholanzi waliingia katika Bahari Kuu ya Pacific wakitafuta biashara. Hawa waliendelea kusafiri mpaka upande wa kusini wa bahari hii wakitafuta nchi mpya.

Mtu mmoja maarufu aliyeitwa Tasman alikivumbua kisiwa katika mwaka 1642 ambacho sasa hujulikana kwa jina la Tasmania; halafu akavumbua New Zealand na halaiki ya visiwa kwa upande wa kaskazini. Katika safari yake ya pili Tasman alisafiri kuambaa pwani ambayo ilielekea kwamba ni ya nchi mpya tena kubwa; hiyo ilikuwa ni Australia ingawa ukubwa wake na umbo lake vilikuwa bado kujulikana.

Katika karne ya 18 Waingereza walipeleka msafara wa wataalam wa sayansi kwenye Bahari Kuu ya Pacific chini ya uongozi wa Nahodha James Cook.

Cook pamoja na wasaidizi wake hawakusafiri kwa biashara bali kujifunza jiografia, ustadi wa kusafiri baharini, maarifa ya nyota na mimea. Katika safari hizi mbili kubwa alizozifanya Cook katika Bahari Kuu ya Pacific (toka mwaka 1786 mpaka 1771, na 1776 hadi 1780) aliipeleleza bahari toka mashariki hadi magharibi, na kusini mpaka kaskazini.

Alisafiri akiambaa pwani ya visiwa vile viwili vya New Zealand na pwani ya mashariki ya nchi ya Australia, kisha akaenda kusini kuelekea antarctic hatimaye akaenda kaskazini kupitia mlango Bahari wa Bering.

Safari hii kubwa ya Cook iliwawezesha binadamu kufahamu mengi mno juu ya Bahari Kuu ya Pacific na pia habari ya bara jipya, yaani Australia.