Risala ya watoto yawatoa machozi akinamama Dar

Na Josephs Sabinus

NAIBU Waziri wa Afya Mhe. Tatu Ntimizi ni miongoni mwa akinamama waliolizwa na risala ya watoto wa shule ya chekechea ya Zakhem Mbagala jijini Dar es Salaam waliyoisoma kwa niaba ya watoto wenzao katika siku ya maandamano ya kupinga vitendo vya utoaji mimba yaliyofanyika wiki iliyopita jijini Dar Es Salaam.

Katika risala yao watoto hao walivilaani vitendo vya kikatili vya utoaji mimba wanavyofanyiwa watoto ambao hawajazaliwa wakiwa matumboni mwa mama zao.

"Ingawa mimi sijalia kwa machozi kama akina mama wenzangu, maneno hayo ya watoto yameniliza moyoni" alisema Mheshimiwa Ntimizi kwa huzuni huku akina mama wengine wakizidi kutiririka machozi na kuyafuta kwa kanga zao.

Risala ya watoto hao iliyowaliza akina mama ilikuwa na maneno yafuatayo;

"Sisi watoto wadogo ,tuone hatuna nguvu wala uwezo wa kujitetea mkiamua kutuua mnaweza. Mkiamua kutulinda na kututea tutaendelea kukua.

Tunaelewa kuwa utoto ni hatua ya mwanzo ya kukua kwa binadamu. Kila binadamu mzee alianza akiwa binadamu mtoto.

Wazazi wetu, tuko mikononi mwenu .Tunaishi kwa sababu ya huruma yenu mnapoendelea kuwaua wenzetu ambao bado hawajazaliwa, mnaliua taifa. Je, kuna taifa bila watoto?Je kuna maendeleo bila watu?

Asante wazazi wetu. Lindeni uhai wetu sisi ndio viongozi wa Taifa letu la baadaye?

Msituue ".

Katika maandamano hayo ambayo Mhe. Ntimizi alikuwa mgeni rasmi ,mwenyekiti wa shirika la kutetea uhai (Pro-Life Tanzania) Bw. Emil Hagamu alisema inakadiriwa kuwa watoto wapatao laki tano huuawa nchini kila mwaka kwa utoaji mimba wa kienyeji kwa kumeza idadi kubwa ya vidonge aina ya Chloroquene au kuchemsha majani ya mitishamba ukiwemo "Mwarobaini"

Alisema inakadiriwa kuwa watoto milioni moja na nusu huuawa nchini kila mwaka kwa utoaji mimba wa kitaalamu na kwamba vitendo hivyo havina budi kukomeshwa na akaiomba serikali kuupuuza hoja ya kuhalalisha vitendo hivyo.

Juu ya matumizi ya kondomu Hagamu alisema kati ya 20%-40% ya wanaozitumia kujikinga na maambukizo ya magonjwa ya zinaa, huathirika na kwa mujibu wa utafiti uliofanywa Marekani asilimia 13 ya watumiaji wa kondomu huambukizwa UKIMWI wakati 10.8% wanazitumia kupanga uzazi hupata mimba.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kwa mujibu wa utafiti mwingine uliofanywa Marekani na kuchapishwa katika jarida la Population Report Volume XXVll la April mwaka huu hadi sasa hakuna kondomu zilizotengenezwa kwa ajili ya nchi za joto ikiwemo Tanzania.

Alisema kondom nyingi ni mbovu na zimekwisha muda wake wa matumiz.i Aliongeza kuwa njia za mpango wa uzazi kama kemikali, vidonge vya majira, sindano, vitanzi na nyingine zina madhara kwa watumiaji ikiwa ni pamoja na kuzaa mtoto asiyekomaa kuharibika kwa tumbo la uzazi, uwezekano wa kupata sarakani ya matiti, mimba nje ya tumbo la uzazi na baadaye mimba kutoka zenyewe.

Mhe. Ntimizi alitishia kuwa upo uwezekano wa kuzifungia hospitali, dispensari na vituo vya afya zitakazobainika kujihusisha na utiaji mimba kinyume na maadili ya kazi .

 

KUTANGAZWA KWA MATOKEO YA MITIHANI YA KIDATO CHA SITA NCHINI

Shule za Kanisa Katoliki zaendelea 'kutesa'

Na Josephs Sabinus

Shule za Sekondari za Kikatoliki zimeongoza katika mtihani wa kidato cha sita mwaka huu ambapo kati ya shule 20 bora kitaifa miongoni mwa 138 zilizoshiriki mtihani huo 14 ni za kanisa Katoliki, imefahamika.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana toka kwa Katibu wa Idara ya Elimu ya Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Padri Elias Msemwa, kati ya shule 10 za mwisho kuna shule mbili tu za kanisa.

Taarifa imezitaja shule bora kuwa ni Rubya Seminari ambayo imeshika nafasi ya 2 na wanafunzi wake wote 12 wamefaulu. Katoke Seminari imejinyakulia nafasi ya nne wakati mwaka jana ilikuwa ya 44; wanafunzi wote 9 wamefaulu.

Shule ya sekondari ya St.Mary’s Mazinde iliyokuwa ya 61 mwaka jana, safari hii imekuwa ya 5 wanafunzi wote 17 wamefaulu. Nafasi ya 6 imeshikwa na Nyegezi seminari iliyokuwa ya pili mwaka jana wanafunzi wake wote 21 wamefaulu.

Nyingine ni Kifungilo sekondari iliyokuwa ya 7 na mwaka jana ilikuwa ya 52.kati ya wanafunzi wake 19, hakuna. Seminari ya Maua imeshika nafasi ya 9 na mwaka uliopita ilikuwa ya 98; kati ya watahiniwa wake 22, amefeli mmoja. Nayo Same Seminari imekuwa ya 10 wakati mwaka uliopita ilikuwa ya 93. Seminari ya Salesian imepata nafasi ya 11 baada ya kuwa ya 47 mwaka jana .wanafunzi wote 35 wamefaulu

Taarifa imezitaja shule nyingine bora kati ya hizo 20 kuwa ni.USA Seminari iliyokuwa ya 18 mwaka jana na hivi sas imekuwa ya 13 baada ya wanafunzi wake wote 21 kufaulu. Pamoja na Arusha seminari iliyofaulisha wanafunzi wote14 na kuwa ya 15 baada ya kuwa ya 9 mwaka jana.Likonde sekondari imekuwa ya 17 na mwaka jana ilikuwa ya 7.wanafunzi wote 14 wamefaulu.

Nyingine ni Uru seminari iliyoshika nafasi ya 18 baada ya kuwa ya 5 mwaka jana. Wote 13 wamefaulu. St. James seminari iliyokuwa ya 11 mwaka jana, watahiniwa wake wote 15 safari hii imekuwa ya 19 na ya 20 kwa ubora ni Kasita iliyokuwa ya 16 mwaka jana.

Shule nyingine za sekondari zisizoza kanisa zilizo miongoni mwa 20 bora ni Ilboru iliyopata nafasi ya kwanza kitaifa kati ya shule zote 138 zilizoshiriki mtihani hiyo ya kidato cha sita iliyofanyika mwezi Mei mwaka huu. Mzumbe imekuwa ya tatu na Tabora Boys imekuwa ya nane.

Shule ya sekondari ya Mzizima imeshika nafasi ya 12, Al-Muntazir Islamic imeshika nafasi ya 14 wakati Bwiru sekondari imeshika nafasi ya 16

shule kumi za mwisho kabisa katika mtihani huo ni Kaloleni iliyokuwa ya mwisho (138), ikifuatiwa na Mafinga, Bondeni, Buhangija,Manka sekondari na Al-Hamarain Islamic iliyoshika nafasi ya 133.

Nyingine ni Kigurunyembe iliyokuwa ya 132 wakati mwaka jana ilikuwa ya 121. Wanafunzi wake28 wamefaulu na 17 wamefeli, Highland sekondari imekuwa ya 131, Eukenford sekondari imekuwa ya 130 na nafasi ya 129 imeshikwa na shule ya sekondari ya Iramba iliyokuwa ya 117 mwaka jana na imefaulisha wanafunzi 4 na 2 wamefeli

Katibu huyo padre Msemwa amesema mabadiliko ya kufaulu na kufeli kwa shule hizo hizo kumetokana na sababu mbalimbali katika mashule. hakutaka kuzitaja.

 

Matumaini zaidi yawajia wenye maradhi ya macho Arusha

Na Father Joseph Hando-Arusha

WANANCHI mkoani Arusha wanaokabiliwa nam maradhi ya macho sasa watapata matibabu ya kisasa na bora zaidi kufuatia kozi na msaada wa vifaa vya kuchunguza na kutibu macho vilivyotolewa na taasisi za Ujerumani.

Matumaini hayo mema yanafuatia wahitimu tisa na washiriki wengine wanne wa kozi ya tiba ya macho iliyoendeshwa katika Hospitali ya Mtakatifu Elizabeth, jimboni Arusha kuzawadiwa vifaa mbalimbali vya kisasa vyenye thamani ya dola za kimarekani 6,500 ili kutibu maraddhi ya macho kwa ufanisi zaidi

Kwenye kusheherekea mafahali ya kumi ya kozi ya macho kila mhitimu na mshiriki wa kozi hiyo iliyoendeshwa kwa muda wa miezi miwili alizawadiwa seti moja ya vifaa hivyo vya kisasa vilivyokuwa na thamani ya dola za kimarekani 500 kwa kila seti kutoka shirika la Lions Club lililoko nchini Ujerumani.

Mmoja wa wawakilishi watano katika mashirika ya Lions Clubs na Missereo yote ya nchini Ujerumani Dk.Alexander Schweiker ambaye pia alikuwa miongoni mwa wakufunzi aliwataka wahitimu kuthamini zaidi mafunzo waliyopata na kwenda kufanyia kazi ipasavyo na wala siyo kufurahia zaidi vyeti vyao ambavyo alidai kuwa ni makaratasi matupu.

Mwakilishi mwingine Dk.. Gerald Kuhnhardt alisema kuwa amefurahishwa zaidi kwa mchango na jitihada za dhati za wazawa wenyewe ambazo kwa kujumuisha na ufadhili wa kutoka Messereo uongozi wa hospitali ukaweza kufanikisha mafunzo hayo na hata mahafali kwa ujumla.

"Nimeridhika na matumizi ya msaada wa pesa mlioupata .. nitafikisha ujumbe huo kwa wafadhili nirudipo nyumbani ili kuwahamasisha waendelee kufadhili tena kozi kama hii kwa miaka mingine ijayo,.."ninadhani ingefaa muda uongezwe ili kufikia walau wiki kumi na nne badala ya nane kama ilivyo hivi sasa "amesema Dk. Gerald Kunhurdit.

Naye Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Arusha Padre Fred Karori ambaye alikuwa ndiye alikuwa mgeni rasmi wa sherehe hiyo alisema jimbo zima kwa ujumla limefurahishwa na kushukuru kwa dhati kutokana na ufadhili wa kozi na zawadi kwa ujumla toka mashirika hayo mawili ya Ujerumani.

Awali Daktari Mkuu wa Hospitali hiyo ambayo pia hujulikana zaidi kwa jina la "Hospitali ya kwa Padri Babu’ Dk. Emiretus Chibuga, alisema kuwa uongozi kwa kushirikiana na wafadhili watajitahidi kuongeza idadi ya washiriki kutoka sehemu nyingi zaidi siyo tu mkoani Arusha na Singida kama ilivyokuwa kwa awamu hiyo kwani matatizo ya ugonjwa wa macho yametapakaa karibu nchini kote.

 

Pengo kutoa Sakramenti Maranta

Na Getruder Madembwe

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo mwezi ujao anatarajiwa kubariki na kutoa sakramenti ya Kipaimara katika kigango cha Mtakatifu Dominic kwa Maranta Parokia ya Kunduchi, imefahamika.

Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia ya Kunduchi padri Dominic Alteri alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni.

Alisema kigango hicho kipo sehemu za Mbezi,na siku hiyo wanafunzi wote wa Kipaimara wa Kigango cha Maranta katika Parokia hiyo wanatarajiwa kupewa Sakramenti ya Kipaimara na Mwadhama Pengo.

Mkristo aliyeoa wake watatu azusha balaa

Na Pelagia Gasper

MLALAMIKAJI Godliva Magezi (39) hivi karibuni aliwaacha hoi wasikiliza kesi mbalimbali baada ya kueleza kuwa siku alipofariki marehemu mume wao Bw. Jostinian Valentine Magezi, mke mwenzake Ester Magezi (42) aliamua kuandaa shughuli za matanga kivyake vyake.

"Mheshimiwa, baada ya mume wetu kufa mwenzangu alifanya matanga yake kwa kuyagawa mara mbili na kwenda kufanya nyumbani kwake kivyake vyake na kuniacha mimi nikiwa sielewi kwanini aliamua kufanya hivyo", alisema mlalamikaji.

Mlalamikaji alisema kuwa wakati wa mazishi ya mume wao yeye na mke mwenzake walionana makaburini kwa ajili ya kumaliza maziko,lakini baada ya kumaliza shughuli hiyo kila mtu alishika njia yake na kwenda kuendelea na msiba wake.

Awali alieleza kuwa mume wao ambaye ni marehemu aliwaoa wake watatu ambao ni Ester Magezi, Savera Magezi ambaye ni marehemu na Godliva Magezi ambaye ni mlalamikaji katika mashitaka mawili likiwemo la kutishiwa kuuawa kwa maneno.

Alidai kuwa siku ya tukio yeye alikuwa yuko nyumbani kwake ambapo alifika mshtakiwa (mke mkubwa) pamoja na mwanae Elitruda Magezi ambao wote kwa pamoja walitoa kauli moja ya kumtaka aondoke katika nyumba anayoishi kwa kuwa nyumba hiyo ni mali yao.

Baada ya majibizano ya muda kati ya mlalamikaji na washtakiwa, ndipo walipoamua kumkaba kabali iliyopelekea achunike sehemu ndogo ya shingo.

"Mheshimiwa angalia makovu shingoni na bado hayajafutika... washtakiwa walinikaba shingoni kwa kutaka kuniua kwa ajili ya ugomvi wa nyumba", alidai.

Alidai kuwa baada ya kukabwa shingoni na mke mwenzake (mshtakiwa wa kwanza) akishirikiana na mtoto wake (mshtakiwa wa pili) yeye alipiga kelele za kuomba msaada ambapo walikuja kumsaidia .

Anadai kuwa baada ya kusaidiwa na majirani hao alienda kutoa taarifa ya kutishiwa kuawa na mke mwenzake katika kituo kidogo cha polisi cha Mtoni Mtongani.

Mlalamikaji alidai kuwa katika tukio hilo walioshuhudia na ambao walifika kumsaidia wakati akipiga kelele ni Rukia Leonard na Metrodia Petro ambao ni wapangaji wake.

Hakimu wa wilaya Iddi Mtiginjola, alimuuliza mlalamikaji kama washtakiwa wana uhasama wa siku nyingi, ambapo alikiri kuwepo kwa uhasama huo ambao unatokana na kugombea nyumba ya mirathi ya watoto wao.

Alieleza kuwa ugomvi huo ulitokea baada ya mke mwenzake wa pili ambaye ni marehemu Bi. Savera Magezi kufariki mwaka 1996, akiwa amemuacha mtoto wa kiume Nickson Magezi aliyerithishwa nyumba hiyo baada ya yeye na mke mwenzake kumzalia marehemu watoto wa kike tu.

Alidai kuwa mtoto Nickson ni mtoto pekee wa kiume katika familia ya wake hao watatu kwa marehemu Magezi, na siku hiyo walipofika washtakiwa walianza kumtuhumu kuwa ni kitu gani kilichopelekea anyoe nywele wakati wa msiba wa mke mwenzao.

"Waliniambia kuwa kwa nini nilinyoa nywele wakati mama yake Nickson amekufa, kwanini nisinyoe nywele wakati mume wetu amekufa", alidai.

Awali mlalamikaji huyo aliieleza mahakama kuwa yeye alizaa na marehemu watoto wawili wa kike ambao ni Agnela na Magreth .

Baada ya kumaliza ushahidi wake mlalamikaji alitoa nakala ya wosia wa marehemu kwa watoto wao ambapo ulikataliwa kupokelewa mahakamani hapo.

Hata hivyo Wakili wa washtakiwa, George Mshumba aliiomba mahakama kutopokea wosia huo ambapo ni nakala kwa kutumia kifungu cha sheria 67 (1) a, cha mwaka 1996 cha sheria ya ushahidi.

"Huwezi kuleta kopi ya wosia, mahakama hii inataka ‘original’ ya wosia wa marehemu na sio hiyo...hiyo kaiweke kwa ajili ya faida yako tu na si kwa kuisaidia mahakama kutoa usuluhishi", alisema wakili.

Naye Hakimu alikataa kupokea wosia huo kwa kutumia kifungu hicho hicho cha sheria ya ushahidi.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya mlalamikaji na washtakiwa:

Mshtakiwa 1: Wewe ni mke halali wa marehemu?

Mlalamikaji: Ndiyo.

Mshtakiwa 1: Kama ndiyo, je wewe unaye mtoto wa kiume, na kama huna kwanini unang’ang’ania kukaa katika nyumba hiyo?

Mlalamikaji: Sina mtoto wa kiume, lakini ninamtunza mtoto wa kiume wa marehemu mke mwenzangu ambaye alirithishwa nyumba ninayoishi kwa kuambiwa na mume wangu wakati yuko hai.

Mshtakiwa 2: Unasema mimi na mama tulikushambulia kwa kukukaba shingoni, je mimi nahusika vipi kama wewe unasema nyumba hiyo ilirithishwa kwa mtoto wa kiume wakati wa uhai wake?

Mlalamikaji: Ndiyo mlinikaba shingoni huku mkinitishia kuniua.

Mshtakiwa 2: Je, matanga kila mmoja alifanya kivyake vyake, kweli si kweli?

Mlalamikaji: Ndiyo , ulifanya kivyako na mimi vyangu hadi nilipokuona makaburini.

Awali ilidaiwa na mwendesha mashitaka, Inspekta msaidizi Yusufu Machibya kuwa Juni 24 mwaka huu, majira ya saa 9:00 mchana huko Mtoni Mwembe madafu washtakiwa walimtishia kumuua na kumshambulia kwa kumkaba shingo na kumsababishia maumivu makali mlalamikaji.

Washtakiwa walikana shtaka na wako nje kwa dhamana, hadi Oktoba 6 mwaka huu kesi hiyo itakapoendelea kusikilizwa tena mahakamani hapo.

 

Mlamleni waomba kupigwa msasa

Na Dalphina Rubyema

ILI kuendelea kufufua Ukristo katika kigango cha Mlamleni kilichopo katika Parokia ya Mbagala katika Jimbo Kuu la Dar Es Salaam Viongozi wa kigango hicho ambao wanafanya kazi ya kujitolea umeomba upatiwe elimu zaidi ili uweze kutoa mafundisho sahihi ya dini kwa waamini wake.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni alipotembelea kigango hicho Makatekista wanaotoa huduma ya kiroho kigangoni hapo Bw. Geofrey Nchimbi na Bw Peter Chimagula walisema kuwa wao hawana elimu yoyote ya ukatekista hivyo wanaendesha ibada kwa kutumia vipaji " Sisi hatuna Elimu, hivyo tunaendesha ibada kwa kutumia vipaji ...tunaomba tupatiwe elimu ili tuweze kufufua Ukristo katika kigango chetu ambacho kimezungukwa na dini ya Uislamu,"alisema Bw. Chimagulu.

Viongozi hao walisema kuwa kigango hicho kilijengwa rasmi kwa miti kwa nguvu za waamini na kuezekwa kwa makuti mwaka 1987 na baadaye Parokia iliingilia kati na kukijenga kwa matofali na kuezeka bati.

Walisema kigango kilianza na Wakristo wapatao 20 ambapo zilikuwa kaya tano na kwa hivi sasa zipo kaya 88 zenye waamini 500

Bw. Nchimbi alisema, hivi sasa watu wameanza kupata mwamko wa dini ya Ukatoliki na wale waliokuwa wamepotea kwa kuhamia Uislamu wameanza kurudi katika kundi.

"Hivi sasa watu wengi wamerudi na kubatizwa , nasi tunaendelea kufufua Ukatoliki hivyo tunahitaji kuungwa mkono"alisema Bw . Nchimbi.

Uongozi huo pia umeomba wasamaria wema wajitokeze zaidi katika kumalizia ujenzi wa kigango hicho ambacho hakijamalizika .

Pia uongozi huo umeomba uwezekano wa kuweka shule ya chekechea na na zahanati ili kuboresha huduma za afya katika eneo hilo.

Kigango kimetoa shukrani kwa uongozi wa Legio Maria (Curia) kanda ya Chang’ombe ambao umekuwa ukifika mara kwa mara kigangoni hapo kutoa changamoto ya kujiuga na chama hicho.

Legio Maria kanda ya Chang’ombe inazijumuisha parokia za Mtoni, Yombo, Mbagala na Chang’ombe yenyewe chini ya Mwenyekiti Bw. William Mabula.

 

Kupunguza idadi ya watoto si suluhisho la umaskini-Askofu

Na Neema Dawson

"KUPUNGUZA idadi ya watoto wanaozaliwa si suluhisho dhidi ya Umaskini" amesema Mwenyekiti wa Idara ya Afya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashamu Askofu Aloysius Balina ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Shinyanga alipokuwa akifungua mkutano wa Idara ya Afya uliofanyika katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu (TEC) jijini hivi karibuni.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Katibu Mtendaji wa Idara hiyo Dk.Albani Hokororo pamoja na madaktari kutoka katika hospitali mbalimbali hapa nchini zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki, Askofu Balina alisema suala si Tanzania kuwa na idadi ya kubwa ya watu bali familia kutomudu mahitaji ya lazima kama vile chakula malazi, pamoja na elimu.

Askofu huyo wa Jimbo la Shinyanga alishutumu taasisi za kimataifa zinazopendekeza njia za kisasa za Uzazi wa mpango kama suluhisho kwa matatizo ya nchi zinazoendelea badala ya kusaidia kuzipa uwezo wa kumudu mahitaji ya jamii ya kila siku.

"Rasilimali nyingi zinaelekezwa kupandikiza sera hizo za kupinga uhai

Katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Idara hiyo Mhashamu Askofu Balina alizitaka taasisi za afya za Kanisa Katoliki hapa nchini kuinua zaidi viwango vya huduma ili kukabiliana na changamoto za karne ya 21 ambayo alisema wananchi wanatarajia huduma bora zaidi.

"Tunapokaribia Millenia ya tatu ninaona haja ya kuziangalia upya huduma za afya," alisema na kisha , akawataka waganga na wauguzi wote kutogeuza huduma kwa wagonjwa kama mradi wa kujipatia fedha"

Sambamba na hayo pia akizungumzia matatizo ya afya nchini, Askofu Balina alisema kuwa umaskini umekuwa kichocheo kikubwa cha maradhi ambapo aliyataja maradhi yanayochochewa na umaskini kuwa ni Malaria, Kuhara na Kuhara damu pamoja na UKIMWI.

Alisema kuwa hadi hivi sasa wananchi wanashiriki vizuri katika huduma za afya ambapo wanachangia kati ya asilimia 40-70 ya bajeti za taasisi za afya , kwani alisema kiwango hicho cha juu ukilinganisha na asilimia 10-20 ya bajeti ya miaka ya nyuma iliyokuwa ikichangiwa.

 

TRA yabaini mbinu za wakwepaji kodi ya petroli

Na Dalphina Rubyema

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kugundua mbinu zinazotumiwa na wakwepaji wa kodi katika bidhaa za mafuta ya petroli na wale ambao huingiza mafuta hayo ndani ya nchi wakidanganya kuwa yanapita kwenda nchi nyingine halafu wanayauza hapa hapa nchini..

Taarifa iliyotolewa wiki hii kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu kwa walipa Kodi, Bw.Augustine Mukandara imesema kuwa siri hiyo imefichuka baada ya TRA kupata fununu juu ya mfanyabiashara mmoja anayejihusisha na ukwepaji wa kodi kwa kutumia magari yake kusafirisha mafuta ya Transit na baadaye kuyauza hapa nchini.

Bila kutaja mmiliki wa magari hayo taarifa imesema maafisa wa TRA walifuatilia gari aina ya Scania 112 (tanker) lenye nambari za usajili TZA 1965 na Trela lenye nambari TZJ 5164 lililokuwa katika kituo cha mafuta cha Agip Kimara ambacho nacho kimetajwa kuwa kinatumiwa kwa kuuza mafuta haramu.

Baada ya maafisa hao kufuatilia gari hilo kwa muda wa siku nzima waligundua kwamba gari hilo limebadilisha nambari zake za usajili na likawa limebandikwa nambari zingine ambazo ni ART 819 na nambari za Trela zikawa TZB3271.

Maafisa walilikamata gari hilo na baada ya kufanya upekuzi iligunduliwa kuwa namba za aina moja TZA 1965 nyingi zilikuwa zimefichwa ndani ya kabini ya lori hilo la mafuta ambazo zinaonekana ndizo wanazozitumia mara kwa mara wanapokuwa katika shughuli za uhalifu.

Baada ya hapo TRA ilifanya uchunguzi katika kumbukumbu za msajili wa magari ambapo imegundulika kwamba nambari halali za gari hilo pamoja na trela lake ni ART 819 na TZB 3271. Nambari TZA 1965 ni za Pick-Up aina ya Peogeout 504 ambayo ilikuwa na nambari za SU 13972 na nambari TZJ 5164 ni za Min Bus aina ya Toyota Costa ambapo nambari TZA 9616 ni za pikipiki aina ya Bavo inayomilikiwa na SUMARIA Group.

Taarifa inaeleza kuwa hali hii inaonyesha wazi kwamba gari hilo ni maalum katika kupakia na kuuza mafuta ya transit kwa njia ya magendo.

Mamlaka ya Mapato bado inafanya uchunguzi na baada ya kukamilisha uchunguzi wake hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara huyo kwa mujibu wa sheria ya forodha.

Wakati huo huo Mamlaka ya Mapato inaomba vyombo vya usalama barabarani kushirikiana na TRA pamoja na raia wema ili kuboresha tabia ambayo imezuka ambapo kumekuwa na mtindo wa wenye magari ambayo hayakusajiliwa kutumia nambari za chasisi(fremu)ya magari hayo kama nambari za usajili na kuyatembelea

 

Mbunge akata rufaa kwa madhehebu ya dini

Na Charles Hililla, Shinyanga

Mbunge wa Bariadi Mashariki Mh. Danhi Mkanga (UDP), amewaomba viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kupeleka huduma za kiroho jimboni kwake ili kukabiliana na janga la mauaji ya wazee na vikongwe linalotokea kwa wingi mkoani hapa hususani kutokana na imani za uchawi.

Bw. Makanga alitoa rai hiyo wakati wakichangia mada kwenye semina ya siku tatu ya kupinga mauaji hayo iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Semina hiyo iliandaliwa na chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wapatoa 98 kutoka wilaya zote saba za mkoa wa Shinyanya.

Aidha, Mbunge huyo aliitaja dini kuwa ni kinga na tiba ya kukomesha mauaji hayo, na akatoa mfano kuwa wengi wa wanaofanya au kuhusika na mauaji hayo ni watu ambao hawana dini yeyote.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Shinyanga ACP Wolfungan Gumbu aliutaja mkoa wa Shinyanga kuwa unaongoza kwa kuua watu kwa imani za uchawi.

Akitoa takwimu za mauaji kwenye semina hiyo kamanda Gumbu alisema kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana, jumla ya watu 50 wameuawa kutokana kuhisiwa kuwa ni wachawi.

Idadi hiyo inaongozwa na wilaya ya Shinyanga yenye idadi ya watu waliouawa 19, ikifuatiwa na wilaya ya Bariadi ambayo waliuawa watu 14, wilaya ya Kahama waliuawa watu watatu, wilaya ya Maswa na Bukombe watu 5 kwa kila wilaya, ambapo wilaya ya Meatu waliuawa watu 3.

Takwimu hizo za mauaji ya kutisha zinatisha pia, kwani kwa kipindi cha miaka mitatu 1997 hadi Agosti mwaka huu jumla ya watu 185 waliuawa kutokana na Imani za uchawi.

Katika idadi hiyo wanaume ni 17 tu waliobaki wote ni wanawake.

Idadi ya vifo hivyo inatisha sana ukilinganisha na watu waliokufa kutokana na ajali mbalimbali za barabarani kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kwenye ajili za barabarani watu waliokufa kwa muda kama huo ni 124, hivyo saala kubwa la vifo mkoani hapa ni mauaji yanayosababishwa na imani za uchawi.

Mauaji ya imani za uchawi yamezidi idadi ya vifo vya ajali kwa watu 61.