Mwelekeo wa Watanzania kijamii umegubikwa na giza - Mtaalamu

Na Josephs Sabinus

MKUFUNZI wa Idara ya Sayansi ya Siasa ya Kijamii na Uongozi katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salam Padre Dk.Cosmas Mogella amesema mwingiliano wa tamaduni na mapinduzi ya kijamii na kiuchumi yanayoikumba dunia hivi sasa yameisababisha jamii ya Watanzania ikose mwelekeo na isijue iendako.

Mtaalamu huyo ambaye alikuwa akiongea katika sherehe za mahafali ya kuwaaga wanachama wa Chama cha Wanafunzi Wakatoliki nchini (TYCS) wanaohitimu kozi ya FTC katika Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) wiki iliyopita alisema mwingiliano huo umeigawa jamii ya Kitanzania katika matabaka matatu.

Aliyataja matabaka hayo kuwa ni lilela "jamii iliyokata tamaa" ambayo wengi wao ni maskini na wenye kipato cha chini. Hao, kwa mujibu wa Mtaalamu huyo ni watu hohe hahe ambao hawakidhi mahitaji na matarajio ya watoto na vijana wao kwa hiyo wamekata tamaa.

Alizibainisha athari nyingine zilizoikumba jamii hiyo ya waliokata tamaa kuwa ni kushindwa kuwadhibiti watoto na vijana wao na hivyo kusababisha kushamiri kwa watoto wa mitaani, ajira ya watoto na vijana kufanya ujambazi wa kila aina.

Tabaka la pili ni lile la "jamii isiyojali na haina muda" ambayo aliitaja kuwa ni jamii ya watu wenye uwezo mkubwa kifedha lakini zimevutiwa sana na tamaduni za kigeni, pamoja na shughuli za kujiongezea mapato.

"Jamii hizi hazina muda kwa familia zao, au katika kuhakikisha kwamba vijana wao wanapatiwa malezi yenye maadili mema," alisema.

Padre Mogella, alisema kutokana na hali hiyo, jamii hiyo imekuwa ikitetea uhuru usio na mipaka kwa watoto na vijana wao, wako tayari kulipia elimu ya watoto wao bila kujali maendeleo ya elimu hiyo.

Alisema watu wa tabaka hilo husomesha watoto wao tuition hata wakiwa shule za chekechea hadi sekondari.Fedha hutumika kuwaridhisha watoto wao; kwa mfano kwenda na gari shuleni, pesa za matumizi ya shuleni kuanzia sh. 500 hadi zaidi ya sh. 1,000 kwa siku, ruksa kwa kijana kurudi nyumbani saa anayotaka, kushiriki mashindano yaitwayo ya "urembo", ruksa ya kuwa na marafiki wa kike au kiume na kadhalika.

"Tabaka lingine ni la jamii yenye kujali linaloundwa na watu wanaotetea maadili ya msingi yanayohitaji mshikamano na malezi ya kimaadili pamoja na kutimiza wajibu na madaraka kwa watoto na vijana," alisema.

Akiongelea kumomonyoka kwa maadili katika jamii nchini alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa vitendo vingi vya uhalifu kama utoaji mimba, kati ya 60-70% hufanywa na vijana kati ya miaka 15-21, utumiaji na usambazaji wa madawa ya kulevya, utupaji wa watoto wachanga, ubakaji, vitendo vya kujiua pamoja na vingine, hufanywa na vijana na akawataka wahitimu hao wawe mfano bora katika kuvipinga.

Alisema vijana wengi wa Kitanzania wameonesha dalili za kukosa mwelekeo na malengo katika maisha kutokana na baadhi ya mambo aliyoyataja kuwa ni pamoja na matarajio makubwa ya vijana yasiyoweza kukidhiwa na wao wenyewe, wazazi au walezi wao pamoja na jamii, ari ya kutaka utajiri wa haraka, ukosefu wa misingi imara ya dini tangia sekondari, kusujudu starehe na anasa licha ya kuwa bado wako masomoni pamoja na ukosefu wa ajira.

Wakati huohuo:Mlezi wa TYCS tawini DIT Mwalimu Frowin Sapura, amewataka wahitimu hao kutumia teknolojiawaliyopata katika masomo yao ili kujadili mikataba, kujiunga katika vikundi na kujiajiri chini ya maongozi ya Mungu.

 

Pengo alindwa na polisi dhidi ya Wanamaombi

Na Mwandishi Wetu

ULINZI mkali kukidhibiti kikundi cha wanamaombi wasihudhurie ibada ya jumapili uliwekwa wiki iliyopita katika kanisa Katoliki parokia ya Magomeni jijini.

Kuimarishwa kwa ulinzi huo kulifuatia tetesi kwamba kikundi kimoja cha wanamaombi kilikusudia kuhudhuria ibada hiyo na kisha kupiga magoti mbele ya Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo wakati wa kukomunika.

Viongozi kadhaa wa parokia hiyo walitanda ndani na nje ya kanisa wakishirikishana na polisi watatu waliovalia sare kutoka kituo cha Magomeni wakati wa ibada ya kupewa sakaramenti ya Kipaimara watoto wapatao 70 kanisani hapo.

Ibada hiyo ya Jumapili ilikuwa ikiongozwa na Askofu Pengo ambaye ni mkuu wa kanisa Katoliki nchini kwa kushirikiana na Maparoko wawili wa Magomeni Merchior Gutambi na Venance Mwekibindu.

Ulinzi uliimarishwa zaidi katika milango miwili mikubwa ya uzio wa kanisa na wale ambao walikuwa wakishukiwa labda ni wanamaombi walisimamishwa kuhojiwa kabla ya kuruhusiwa kuingia kanisani.

Awali Ijumaa jioni wakati wa semina ya wasimamizi wa watoto waliokuwa wakijiandaa kupokea sakramenti hiyo ya Kipaimara paroko wa kanisa hilo padre Gutambi alitoa onyo akimtaka mwanamaombi yeyote ambaye ameteuliwa na familia yake kusimamia mtoto wao katika kupokea sakramenti hiyo aondoke.

Hata hivyo katika mazoezi yote mawili yaliyofanyka Ijumaa na Jumapili hakukuwa na mwanamaombi yeyote aliyekamatwa kanisni hapo.

Aidha katika ibada hiyo ya Jumapili waumini wa parokia hiyo ya Magomeni kupitia kwa paroko wao Padre Gutambi walimkabidhi zawadi ya pesa taslimu shilingi 174,500 Askofu Pengo ikiwa ni zawadi yao kwake wakishukuru kuweza kuhudhuria na kuongoza ibada hiyo ya kuwapatia Sakramenti ya Kipaimara watoto wao.

Akizungumza mara baada ya kupokea zawadi hiyo askofu Pengo aliwaasa waumini wa Kanisa Katoliki kuwa wenye upendo wavumilivu na wanaoheshimu maamuzi yanayotolewa na viongozi wa kanisa lao ili kuijenga imani yao ya kikristu.

Akitoa mfano Askofu Pengo alisema kuwa wakristu wa Ulaya wakati mmoja waliwahi kupoteza imani yao na kuingia katika vurugu kutokana na kuwafuata watu waliopora madaraka ya kanisa na kisha kujifanya kuwa viongozi bila kufuata utaratibu kwa vile tu walipata mafanikio katika kazi ya kuliongoza kanisa.

Alisema kuwa kazi ya kuliongeza kanisa inahitaji daraja za Sakramenti kama vile upadrisho na wala si matumizi ya njia za kijanjajanja au njia za utapeli.

 

BAADA YA MJAMZITO KUFIA HOSPITALINI TARIME KWA KUKOSA PESA

Mganga wa Mkoa asema aliyezembea atakiona

Na Mwandishi Wetu

MGANGA Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mara Dk.Mniko amesema anafuatilia ili ajue hali iliyosababisha kifo cha mjamzito Mariamu Nyangarya (20) kilichotokea katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya kukosa pesa na kisha mwili wa marehemu kuondolewa hospitalini hapo usiku na kwamba atakayebainika kuhusika na uzembe kuhusiana na kifo hicho atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Musoma katikati ya wiki, Dk. Mniko alisema ameshitushwa na kuhuzunishwa na habari hizo. "Sijaliona hilo gazeti, habari hizi za kufedhehesha nimezipata jana (Jumatatu) toka kwa mwandishi mmoja wa habari aliyekwenda huko Tarime. Taarifa kamili toka kwa Mganga wa Wilaya (Tarime) sijazipata; sikuwepo nilikuwa vijijini na yeye hivi sasa yupo safarini"alisema Dk. Mniko.

Alipoulizwa ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya uzembe utakaobainika kuwa ulifanyika toka kwa watumishi wa hospitali hiyo uliosababisha au kuchangia kifo hicho ili kukomesha hali hiyo isijirudie tena, Mganga Mkuu huyo wa Mkoa alisema;

"Nimeanza kulifuatilia suala hili na kwa sasa sitasema lolote mpaka nipate taarifa kamili ya DMO. Hata hivyo aliyefanya uzembe katika eneo lake la kazi lazima achukuliwe hatua kali za kisheria. Haiwezekani abainike aliyezembea halafu asichukuliwe hatua. Kitakuwa kitu cha ajabu. Nitakupa taarifa kamili hili siyo suala la kuficha; ni kitu kilichowazi."alisema Dr. Mniko.

Mnamo Julai 31, mjamzito Mariamu Nyangarya (20) mkazi wa eneo la Sabasaba mjini Tarime alifariki dunia katika hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Tarime baada ya kukosa pesa ili afanyiwe upasuaji wa mimba.

Mume wa Marehemu Bw. Boniface Kemore(24) alisema awali walitakiwa kulipa sh. 11,000/= ili mgonjwa wao aongezwe chupa mbili za damu walizozitoa yeye na mmoja wa ndugu zake aliyemtaja kwa jina la Moris .

Alisema kati ya kiasi hicho, alipata sh.3000/= hivyo kulazimika kuweka redio yake rehani kwa dhamana ya shilingi 8,000 kwa nesi aliyetajwa jina moja la Sara.

Baada ya kuonekana haja ya mjamzito huyo kufanyiwa upasuaji, Bw. Kemore na wenzake walitakiwa kulipa tena sh.12,000/= kwa ajili yashughuli hiyo.

Baada ya kukosa fedha hiyo saa 2:00, mganga wa zamu hospitalini aliwaandikia barua kuwahamishia hospitali binafsi ya Dk. Winani ambapo walikopeshwa vifaa vya upasuaji baada ya kuweka rehani kamera yake kutokana na kushindwa gharama za hapo sh. 15,000/= na hivyo kurudi tena hospitali ya serikali usiku huo.

Marehemu alifariki dunia katika hospitali ya wilaya majira ya saa tano usiku na mwili wake kuondolewa usiku huo huo hali iliyomfanya mganga mmoja wa hospitali hiyo kufanya upasuaji nyumbani kwa marehemu saa 7 mchana Agosti 2 mwaka huu ili kumtenganisha marehemu na mtoto.

Wakati huohuo: Kufuatia tukio hilo, baadhi ya wakazi kadhaa wa jiji la Dar Es Salaam kwa nyakati tofauti wamesema ni wakati muafaka kwa serikali kuonesha namna inavyowajali wananchi wake kwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya atakayebainika kuchangia kutokea kwa kifo hicho.

"Serikali ijiulize; alipokuwa mgonjwa akihitaji operesheni, vifaa havikupatikana, lakini baada ya kufa vikapatikana na marehemu akapasuliwa nyumbani kwake. Vifaa vilitoka wapi na maadili ya fani ya uuguzi yakoje?" alihoji mmoja wa wananchi hao.

Papa kufungua lango la kanisa mkesha wa Jubilei

lMsalaba wa Jubilei kutembezwa majimbo yote

Na Leocardia Moswery, DSJ

BABA Mtakatifu Papa John Paul wa Pili atazindua Jubilei Kuu kwa kufungua Lango Takatifu la Basilika la Mt. Petro kule Roma usiku wa mkesha wa sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo, imefahamika.

Akitoa mada katika semina ya siku moja juu ya kujiandaa na Jubilei iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Msimbazi Centre na kuwahusisha Mapadre, Watawa, Makatesta na Walei, Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturgia wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania {TEC} Padre Julian Kangalawe, alisema makanisa mahalia yatazindua Jubilei Kuu kwa Misa ya kuzaliwa Yesu Kristo Desemba 25 itakayoongozwa na Askofu wa Jimbo katika Kanisa la Katedrali.

Alisema kuwa Tume Kuu ya Jubilei ya Roma imeahidi kuwa itapeleka miongozo itayotumika katika makanisa kwa kipindi cha majilio ya Ibada ya kufungua Lango Takatifu na sala za mkesha wa kuingia mwaka 2000.

Padre Kangalawe alifafanua juu ya Jubilei kwa upande wetu pamoja na kutumia miongozo itakayotoka Roma kwa Kanisa la Tanzania.

Alisema kuwa kila jimbo litajipatia msalaba mkubwa wa jubilei utaobarikiwa na Askofu wakati wa ufunguzi wa Jubilei Kuu na msalaba huo utachukuliwa kwa maandamano na kuingia kanisa kuu la jimbo kupitia mlango mkubwa.

Katibu huyo mtendaji wa Idara ya Liturgia Padre Kangalawe alidai kuwa msalaba utazunguka parokia zote jimboni na hatimaye utarundishwa kanisa kuu kwa kufunga jubilei Januari 5, mwaka 2001.

Alisema kuwa kila parokia itateuwa kikundi cha watu au kamati kusimamia utaratibu wa kupokea, kubeba, na kukabidhi masalaba, kikishirikiana na paroko, kitakwenda kuchukua msalaba kutoka parokia jirani na kuleta kwao kwa siku iliyopangwa.

Watakiwa kuotesha vitalu vya miche kwenye shule zao

Na Dalphina Rubyema

WALIMU wanaofundisha somo la Sayansi Kilimo kwenye shule za msingi zilizopo wilayani Temeke katika mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kuotesha vitalu vya miche ya aina mbalimbali katika shule zao.

Wito huo uliotolewa hivi karibuni na Afisa Elimu wa wilaya hiyo Bw. Ramadhani Mfugale wakati akifungua semina ya siku moja iliyohusu uoteshaji vitalu kwenye shule za msingi zilizopo wilayani humo iliyofanyika kwenye ukumbi wa shule ya Msingi Wailes.

Bw. Mfugale, alisema kuwa lengo la uoteshaji wa vitalu hivyo ni kuboresha zoezi la upandaji miti wilayani humo ambapo aliongeza kuwa hadi kufikia Juni, mwaka kesho anatarajia kupanda vitalu kwenye mashule hayo vyenye na jumla ya miche ipatayo milioni moja.

Katika kusisitiza suala hilo, Afisa huyo aliwaeleza wajumbe wa semina hiyo ambao ni walimu wa somo la sayansi kilimo kuwa shule zote zinatakiwa kuotesha kitalu chenye kuwa na miche isiyopungua 1,000 isipokuwa shule ya jeshi la wokovu yenye wanafunzi wenye ulemavu wa viungo.

Hata hivyo baadhi ya walimu walieleza dukuduku lao kuwa wanakabiliwa na uhaba wa maji hivyo hawataweza kuitunza inavyotakiwa miche yote hiyo kitu ambacho Bw. Mfugale alipinga.

"Kama ni suala la maji msiwe na wasiwasi tatizo hilo litashughulikiwa na tutahakikisha kuwa maji kwa kila shule yanapopatikana eneo la karibu.

Hivyo nasisitiza tena kuwa shule zote zinatakiwa kuwa na kitalu chenye miche 1000 kwenda juu isipokuwa shule ya Jeshi la Wokovu ambayo itaotesha kitalu chenye miche 300 na hii ni kwa vile wanafunzi wake wana ulemavu wa viungo" alisema Bw. Mfugale.

Zoezi hili la uoteshaji wa vitalu limetakiwa lianze mara moja na ukaguzi wa maendeleo ya vitalu utakuwa unafanyika mara kwa mara katika shule zote.

 

AGEH yahitaji wataalamu wenye maadili ya Kikristo

Na Josephs Sabinus

SHIRIKA la Kikristo la Kijerumani linalozisaidia nchi za Afrika kwa kuwatuma wataalamu wake mbalimbali (AGEH) limeshauriwa kuwatuma barani hapa wataalamu wenye ujuzi na mahusiano mema ya kikristo na kijamii ili wasaidie kueneza utaalamu zaidi na kudumisha mahusiano bora kati ya nchi za Afrika na Mataifa ya Ulaya.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na wajumbe wa mkutano wa tatu wa AGEH kutathimini shughuli mbalimbali zinazofanywa na wataalamu wake barani hapa uliofanyika mjini Cape-Town Afrika Kusini wakati wa kusherekea miaka 40 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1959.

Akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya kurejea toka Afrika ya Kusini alikohudhuria kikao hicho kilicho hudhuriwa na wajumbe 10 toka nchi za Afrika zikiwemo Afrika Kusini Tanazania, Malawi, Namibia, Zambia na Zimbabwe tangu Agosti 16 hadi 18 mwaka huu, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padre Method Kilaini alisema ujuzi wa kutosha na mahusiano mema ya wataalamu toka kwa wageni hauna budi kuzingatiwa ili kuwawezesha wataalamu wazalendo walio bora kurithi utaalamu toka kwa wageni ili nchi za Afrika zijiendeleze kitaalamu katika fani mbalimbali zikiwemo za Kilimo ufundi na Udaktari.

Alisema hali hii ikisaidiwa na wazalendo wenyewe barani Afrika kuutambua umuhimu wa kujitayarisha vema kufanyakazi na wageni kwa lengo pia la kujifunza na kupata uzoefu toka kwao kwa kipindi cha uwepo wao katika kazi mbalimbali hapa nchini, itaziwezesha nchi hizi baadaye kuwa na wataalamu wake wazalendo walio bora kuliko kutegemea tu, kuwaagiza toka nje ya nchi.

"Ilionekana ipo haja kwa Watanzania kukamilisha maandalizi ya miradi mapema ili wataalamu wa kigeni wafikapo nchini, wawe wanajua na wakute kinachotakiwa kufanyika kikiwa katika maandalizi yaliyokamilika na hii itasaidia kutowakatisha tamaa" alisema Padre Kilaini.

Aliongeza kuwa ingawa ipo haja kwa AGEH na mashirika mengine kama Misereor, Missio na Cartas kuwasaidia watanzania ili kuwalipa vizuri wataalamu wazalendo na hivyo kuondokana na tatizo la Wataalamu walio bora kukimbilia nchi za nje kama Botswana na Afrika ya Kusini Watanzania pia hawana budi kujiimarisha na kujitegemea kiuchumi ili kuwalipa vizuri wataalamu hao wazalendo na hivyo kuondokana na tatizo hilo.

 

Askofu asema Tanzania yahitaji viongozi wasio wabinafsi

Na Sr. Gaspara Shirima, Morogoro

MHASHAMU Askofu Telosphor Mkude wa Jimbo la Morogoro amesema Jamii ya Watanzania inahitaji viongozi watakaowahudumia na kuwaongoza bila kutaka faida yao binafsi wakati tunapoingia mwaka 2000.

Mhashamu Mkude alisema hayo hivi karibuni kwa nyakati tofauti katikaIbada ya Misa ya Upadrisho wa Mashemasi Liston Lukoo wa Parokia ya Mzumbe na Silvester Mwerondo wa Parokia ya Mhando, Tarafa ya Turiani, Morogoro Vijijini.

Askofu Mkude alisema kuwa viongozi hawana budi katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia, kuwaelekeza watu hususani katika masuala ya ustawi wa jamii, siasa, utamaduni na uchumi.

Mkuu huyo ametoa wito kwa viongozi wa aina zote kutoa ukweli, akisema "haifai kwa kiongozi kutoa ripoti nusu nusu ili kuepa kupatwa na madhara makubwa. Kiongozi anahitajika awe wa ukweli, kujiamini na kuaminika na watu".

Kwa mantiki hiyo Askofu alishukuru kwa kuwa Sakramenti ya upadre ambao wanalisaidia Kanisa kulinda na kugawa mafumbo matakatifu kwa watu.

Mhashamu Mkude aliwataka waumini wawasaidie mapadre katika kazi zao ya kuongoza watu kwa kuwaombea.

Alisema kusema kuwa ni vizuri wanapowaona katika kasoro za kibinadamu wawasahihishe kwa upendo.

 

Wazazi watakiwa kutambua sauti ya Mungu

Na Getruder Madembwe

ASKOFU wa Jimbo la Dodoma Mhashamu Mathias Isuja, amewataka wazazi kusikiliza sauti kutoka kwa Mungu pindi watoto wao wanapotaka kuwa mapadri.

Askofu Isuja alisema hayo alipokuwa akitoa nasaha zake katika daraja la Upadri kwa mashemasi tisa hivi karibuni katika kanisa Katoliki la Dodoma .

Alisema ni wajibu kwa mlezi au mzazi kuwaruhusu na kuwasaidia hadi kufikia daraja takatifu la upadri kwani sauti hiyo hutoka kwake Mungu mwenyewe.

Vile vile Askofu Isuja aliwaasa mashemasi hao kuwapa watu sakramenti na wasiwanyime na pia kuwaongoza kwa imani na maadili mema kwani ndiyo kazi yao muhimu.

"Ninyi mashemasi ambao leo hii mnapata daraja hili la upadri msiwanyime waamini wenu sakramenti bali mtakiwa kuwaongoza kwa imani na maadili mema kwani hiyo ndiyo kazi muhimu kwenu"alisisitiza Askofu Isuja.

Wakati huo huo Katibu Mtendaji Idara ya Utume wa Walei Baraza la Maaskofu (TEC) Padri Nicholaus Segeja amewataka Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kutumia vizuri mikopo wanayoipata kutoka kwa wahisani.

Padri Segeja aliyasema hayo katika ufunguzi wa semina ya tathimini ya miradi iliyofanyika Kituo cha Kiroho cha Mbagala na kuhudhuriwa na viongozi wa wanawake kutoka majimboni.

Alisema katika hali halisi tunavutwa zaidi kutafuta misaada na mikopo lakini hatujibidishi vya kutosha kwamba tunachokipata hakigubikwi na hamu kubwa ya kustarehe,kustawi na kuwa huru bila nidhamu ya kujiwekea utaratibu.

 

Kampuni ya bia kutoa tuzo kwa vijana wa kanisa

Na Pelagia Gasper

VIJANA wote wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wametakiwa wajitokeze kwa wingi ili waweze kujiunga katika mashindano ya kumtafuta mshindi wa makala za kanisa, uigizaji wa mateso ya Bwana Yesu, na Uimbaji.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake hivi karibuni Afisa Uhusiano wa Kampuni inayozalisha bia aina ya Kibo, Bw. Focus Mmari, alisema kuwa mashindano hayo ni ya kumtafuta mshindi wa tuzo ya Guiness yatayozinduliwa Septemba 23 mwaka huu kutoka kwa vijana Wakatoliki.

Alisema kuwa vijana wote kutoka katika vikundi vya VIWAWA, VILAFRA, YOUTH LIVE, na vingine vingi ikiwa ni pamoja na vijana wengine ambao hawapo kwenye vikundi.

Alipoulizwa kuwa ni kitu gani kilichopelekea wao kujiingiza katika masuala ya dini, alidai kuwa wameamua kufanya hivyo kwa kuwa vijana hao wana moyo wa kujituma wawapo katika vikundi vyao, jambo ambalo wao wamependezwa nalo na kuamua kuwasaidia kuendeleza fani zao.

 

Majambazi tisa wapora kituo cha Biblia Dodoma

lWajeruhi walinzi na kumpora Mmisionari Mzungu sh. laki moja

lMtambo wa Redio call wa Kanisa Katoliki Dodoma nao waibiwa

Na Masha Otieno, JR

MAJAMBAZI wapatao tisa wenye silaha wamevamia Shule ya Biblia Emmaus, eneo la Ipagala mjini Dodoma ambapo wamemtishia Mkuu wa kituo hicho Helmut Graef (64) na kufanya uporaji.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa uchapishaji wa "Kanisa la Biblia Publishers" inayomiliki kituo hicho Bi, Ing’e Danzeisen, wezi hao walikivamia kituo hicho kunako majira ya saa tisa usiku wa kuamkia juzi ambapo walifyatua risasi mbili kisha wakamtishia mke wa mmisionari huyo Bi. Brunhilde Graef, ambapo baada ya kumpora zaidi ya shilingi 100,000/= walikimbia kabla ya polisi kufika.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Dodoma, Rashidi Hemedi amekiri kuwepo tukio hilo na amesema polisi wanaendelea na uchunguzi.

Bi. Ing’e Danzeisen amesema tukio hilo ni la pili katika kituo hicho.

Amesema kwa mara ya kwanza Agosti 5, mwaka huu, majambazi wapatao 6 walifika kituoni hapo na kubomoa mlango kwa kutumia jiwe kubwa la fatuma na kuwajeruhi walinzi .

Alisema katika tukio hilo majambazi hao waliingia kwenye jengo la usambazaji, maandiko na kutoweka na Radio Call, Powerstation, Video deck na Screen, Computer Redio kaseti na mabegi mawili ya nguo na kufanikiwa kutokomea na vitu hivyo kabla ya kufika polisi na kwamba Mch. Graef aliyevamiwa na wezi hao ni mwenyeji wa Ujerumani aliyetafsiri vitabu vingi kwa kiswahili pamoja na kamusi ya Biblia.

Mtoto Fikiri anatafutwa na mzazi wake mjini Dar

Na Mwandishi Wetu

MVULANA Meclaud Kahimba (Fikiri 18) muuza nazi mjini Mbeya eneo la Air Port Mbeya anatafutwa na mama yake Bi.Anastazia Komba wa Keko Machungwa Jijini na kwamba popote alipo anaombwa ajitokeze na aliyemuona atoe taarifa kituo cha karibu cha polisi.

Bi. Komba amesema kijana huyo Mngoni alitoweka nyumbani Mbeya Julai 22 baada ya mvurugano kidogo na baba yake mdogo Bw. Dominicus Kahimba na kwamba juhudi zake za kumtafuta hazijazaa matunda.